Hiki ndiyo kitabu nilichokiota nakisoma!
Wakipanga bidhaa!
---------------------------------------------------------------------------------------------------------
Gulio ni soko la siku moja moja. Katika kijiji cha Katerero, Wilayani Bukoba siku hiyo ni Jumanne. Wakulima hukusanyika kuuza mazao yao, na watu wengi huenda kuyanunua.
Watoto wa katerero hushirikiana na wazazi wao katika kazi za nyumbani. Kila Jumanne wakati wa likizo, Kiiza na wazazi wake huchukua mazao na kupeleka gulioni. Siku moja Kiiza, mama yake na shangazi yake walikwenda gulioni. Kiiza alichukua kikapu cha maharagwe na mama yake alichukua mkungu wa ndizi. Shangazi yake Kiiza alichukua tangawizi na kabichi. Kiiza alifunga kikapi kwenye baiskeli akawa anafuatana nao. Njiani walikutana na watu waliokuwa wanakwenda gulioni. Wengine walikuwa na mayai na kuku, na wengine walichukua nguo na mikeka. Walipofika gulioni walikuta watu wengi sana. Pale gulioni kulikuwa na vitu vingi vilivyoletwa kuuzwa.
Kiiza, mama yake na shangazi yake wakatafuta mahali pazuri pa kukaa, halafu wakapanga vitu vyao waviuze. Kiiza alipanga mafungu ya maharagwe; tangawizi na kabichi. Mama yake alitandaza majani ya mgomba na akauweka mkungu juu yake. Mara akaja kijana mmoja akauliza, "Mama, mkungu huu bei gani?" Mamake Kiiza akajibu, "Shilingi nane na thumuni." Yule kijana akaomba apunguziwe. Akasema, "nitakupa shilingi sita." Yule mama akakataa. Wakabishana bei mapaka yule mama akakubali kumwuzia kijana kwa shilingi saba. Kiiza aliwasikiliza mama na kijana.
Alipoondoka yule kijana, mama akamwambia Kiiza, "Nenda nyumbani ukaulete ule mkungu mwingine nilioukata jana jioni." Kiiza alichukua baiskeli akakimbia nyumbani na kurudi na mkungu. Mara tu alipofika gulioni alikutana na watu waliotaka kununua ndizi. Akawaambia, "ikiwa mnataka nipeni shilingi nane na nitawauzia." kwa vile mkungu ulikuwa na ndizi nzuri wale wanunuzi waliuchukua bila kusita kwa bei waliyoambiwa. Kiiza alipofika gulioni mama akamwuliza, "mkungu uko wapi? Tena basi umechelewa." Kiiza akamjibu mama, "Ule mkungu nimeuuza." Mama yake akamwuliza, "Fedha ziko wapi?" Kiiza akzichukua zile shilingi nane akampa mama. Mama yake alipoelezwa juu ya uuzaji huo alifurahi sana. Alimshukuru mwanae kwa kitendo hicho.
Kiiza, mama yake na shangazi yake wakaendelea kuuza maharagwe, tangawizi na kabichi. Kwa kuwa hawakuwa na mizani, walitumia mkono kupimia maharagwe na tangawizi. Waliuza kopo moja la maharagwe kwa senti hamsini na kopo la tangawizi kwa shilingi moja. Waliuza vitu vyao vyote mpaka vikamalizika.
Wakati huu, Kiiza alianza kuona njaa. Mama yake akamnunulia karanga na maandazi. Kisha wote watatu wakaenda hoteli kunywa chai. Walipokuwa hotelini, Kiiza alimkumbusha mama yake kumnunulia ndara: Mama yake akamwambia, "Tukisha kunywa chai nitakununulia. Tena umenikumbusha kumnunulia baba yako kitasa na kitana cha mti." Walipotoka hotelini waliona kuwa mahali walipokuwa pamepangwa vitu vingine. Kitu kilichomvutia zaidi Kiiza ni embe kubwa. Alimwuliza mama, "Embe hizi hutoka wapi"? Mama akamjibu, "Embe hizi hutoka Tabora." Kiiza alizimezea mate akamwomba mama amnunulie moja aionje. Baada ya kula moja alitaka ya pili, lakini mama alimwambia, "Twende kwanza tukanunue vitu vingine.
Kiiza, mamake na shangazi wakaondoka kwenda kununua vitu hivyo. Mwisho mamake akanunua mafuta ya kupikia. Wakati huo mvua za rasharasha zilianza. Mama yake Kiiza shangazi yake na majirani wote wakapanda basi kurudi nyumbani. Gulio likavunjik. Mvua ilipokatika Kiiza akapanda baiskeli yake na kurudi nyumbani.
Walipofika nyumbani, Kiiza alimweleza baba yake mambo yote aliyoyaona sokoni. Alimweleza pia habari ya mvua iliyonyesha na kulifanya gulio livunjike. Baba yake akamwambia kwamba wazee wamekwisha amua kujenga soko zuri la mawe litakaloezekwa kwa bati, Watashirikiana kukusanya mawe na kuanza kujenga mara tu masika yatakapomalizika.
------------------------------------------------------------------------------------------------------
Na mara nikashtuka na ule ukurasa ukawa umeisha ...halafu la ajabu pia nimeota ndoto hii siku ya JUMANNE!!!
10 comments:
@Yasinta;
Ama kweli ya kale ni dhahabu na vitabu hivi vilitusaidia katika mazoezi ya kusoma na kuwekeza katika dhana ya kuwa wasomaji mahiri makini.Sikiliza watu wa enzi hizo na utasikia usomaji katika mtindo wa maneno.Leo hii usomaji ni mashaka matupu na umepoteza ladha kabisa.Mimi binafsi nakumbuka nikiwa msomaji wa darasa na hadi uwezo wangu wa kusoma hadarani ni mkubwa na wenye ladha maridhawa.
"Usomaji katika mtindo wa kuumba maneno".
UKWELI VITABU HIVI VIRUDISHWE
MAANA HATA KAPULYA MDADISI TULIMWONA NA MPAKA LEO DADA AMEKUWA MAARUFU KWA KUFUATA NYAYO ZA KAPULYA,HII ILIJENGA MTU KUJIAMINI KAMA CHILUNDA APAMBANA NA CHUWI NK
HUO NDIO UKWELI MIMI NAKUMBUKA HATA KWENYE KIMOMBO KULIKUWA NA VITABU NA HADITHI KAMA KANAKAMSUNGU,THE CROCODILE KEEPER,MKISI CROSS LAKE NYASA ,NK HIVI UKIVISOMA UKWELI HUWEZI SAHAU MPAKA LEO, NA ILE YA KARUDI BABA MMOJA TOKA SAFARI YA MBALI, SIZITAKI MBICHI HIZI
CHE JIAH
hahahahah umenikumbusha mbaliiiiiiii hadi raha
Hakika,rafiki ni bora kuliko mwana sesere,kibanga ampiga mkoloni,Damasi na juma,,nk hadithi zilizo tukuka naukizisoma unapata maarifa.mfano ule utenzi /shairi ,karudi baba mmoja toka safi ya mbali.... kwa kweli zamani waliandika.nanyingine nimekumbuka maneno haya',aleya leya kana kansungu umwelu umwelu' nafikiri ilikuwa katika vitabu vya kiingereza. asante kwa kumbukubu.kaka s
We Yacinta! Una nakala ya vitabu hivi? Kama unavyo naomba tupange unitumie lau watoto wangu waliozaliwa huku Amerika wavisome hata kwa lazima. Wakati ule elimu ilikuwa na maana siyo kama sasa watu wanachakachua. Umenikumbusha mbali sana hasa nilivyokuwa nimekariri mashairi yale kiasi cha kutokea kuwa mshairi na mtunzi. Kimsingi nawashukuru waliotunga vitabu hivi pamoja na akina Chinua Achebe maana bila wao nisingefikia nilipofikia kiutunzi.
ndugu zangu wapendwa hakika ya kale ni matamu yaani huwa nikikumbuka tu shule ya msingi basi nachukua vitabu tulivyokuwa tunasoma na kusoma basi ni raha tu. Halafu kama alivyosema Mwl. Hata mimi nawasomea wanangu au wao mara nyingie wananisomea:-) ..Mwl. Mhango.labda tuwasiliane:-)
Nitumie email yako haraka lau niwanusuru wanangu. Maana wanakuwa wakanada kuliko wabongo kusema ule ukweli. Samahani kwa kuchelewa kujibu.
Vinapatikana wapi aisee nimekumbuka mbali sana
Nimeipenda hii đ
Post a Comment