
Wiki iliyopita na wiki hii nimekumbuka sana nyumbani, nadhani ni kwa sababu wiki iliyopita tarehe 17 ilikuwa ni tarehe ambao mama yangu alifariki na wiki hii 23/5 imetimia miezi miwili tangu Mdogo wangu alifariki. Kwa kweli nam-miss sana mama yangu pia mdogo wangu.
Nakumbuka ilikuwa kila nikienda likizo, nilikuwa natumia muda mwingi kuwa jikoni na mama yangu nikizungumza naye simulizi za kale za enzi ya utoto wangu.
Ni simulizi ambazo kwa kweli kila nizikumbukapo huwa natamani yale maisha yajirudie kwani kuna mengi ya kufurahisha na ya kuhuzunisha ambayo kwangu mimi nimejifunza mengi kwako.
Lakini lipo jambo moja ambalo nimelikumbuka, ambalo kwa kweli huwa linanifikirisha sana. Jambo lenyewe ni kuhusiana na baadhi ya marafiki zangu kule nyumbani.
Kusema kweli ule ukaribu niliokuwa nao na baadhi ya marafiki zangu umepungua kiasi cha kukatisha tamaa.
Sababu kubwa ni kutokana na kile walichodai kwa nimewatupa kutokana na kutowasaidia kupata wachumba wa Kizungu. Yupo rafiki yangu mmoja mbaye yeye aliwahi kunitamkia wazi kuwa mimi ni mbinafsi kwa kuwa ni mara nyingi ameniomba nimtafutie mchumba wa Kizungu kwa kuwa ninaishi huku ughaibuni lakini nimeshindwa kumtafutia.
Nakumbuka nilimweleza ukweli kuwa siwezi kumsaidia juu ya jambo hilo kwa sababu liko nje ya uwezo wangu, lakini kutokana na labda tuite ufinyu wa kufikiri, nilimpoteza rafiki huyu kwa sababu ya kushindwa kumtafutia mchumba wa kizungu……..yaani kaaaazi kweli kweli.
Hata hivyo nilijiuliza swali moja, kuwa hivi hakuna wanaume huko nyumbani mpaka mtu aamue kutafuta mchumba wa Kizungu? Je ni mapenzi au ni Uzungu unaotafutwa hapo?
Lakini kwa upande mwingine sikumshangaa sana kwa sababu kwa huko nyumbani ipo silka ya baadhi ya watu ambao wanaamini kwamba kuoa au kuolewa na Mzungu ni jambo la kujivunia sana. Huwa nimezoea kauli za baadhi ya watu kule nymbani kila niendapo likizo wakisema, ‘siyo mwenzako yule, kaolewa na Mzungu’ .
Yaani mpaka leo hii bado kuna baadhi ya watu wanaamini kuwa kuoa au kuolewa na mzungu ni jambo la kifahari na la kujivunia. Kinachotafutwa sio mapenzi tena ni huo uzungu..
Kuna baadhi ya watu wamefikia hatua ya kuamini kuwa sisi waafrika ni duni na wenzetu weupe ni bora na waliokamilika.
Lakini nadhani makosa hayo hayakuanza leo, yameanzia mbali sana. Kwani kizazi na kizazi tumekuwa tukiaminishwa kuwa wazungu ni bora zaidi yetu sisi.
Kwa mfano, mtu kufanya mambo yake kwa umakini na anayefuata muda huyo ataitwa ni mzungu, au mtu asiyependa majungu, uzinzi, uasherati na umbeya naye ataitwa kuwa ni mzungu. Nakumbuka wakati nikisoma kule nyumbani, ilikuwa kama kuna mwalimu ambaye ni mwadilifu kwa wanafunzi na anayewajali, utawasikia wanafunzi wakisema, ‘yule mwalimu ni mzungu’
Yaani kipimo cha kufanya mambo kwa uadilifu na kuwajali wengine kimekuwa kikihusishwa na uzungu, mpaka imefikia mahali kila mtu anatamani kuolewa au kuoa mzungu wakiamini kuwa hao wamekamilika.
Hata huko makazini napo watu wanaochapa kazi kwa uadilifu wanafananishwa na wazungu. Wakati mwingine huwa nacheka kwa sababu naamini hao wanaoamini kwamba mtu kuwa mzungu anakuwa amekamilika ni wazi kwamba hawawafahamu watu hao.
Kwamba kuwa mzungu ni kutokuwa na tabia mbaya, kama uvivu, udokozi, kutojali muda, kusengenya, umbeya, wivu, au kijicho, uzinzi, uasherati, ushoga na tabia zote mbaya tunazozijua hapa duniani, nikujidanganya bure.
Nasema kuamini hivyo ni kujidanganya, kwa sababu kwa wale wanaoishi huku ughaibuni au wale wanaofanya kazi na hawa wenzetu huko nyumbani, watakuwa ni mashahidi wangu.
Kama mlikuwa hamjui ni kwamba hawa wenzetu nakubali kuwa wapo waadilifu na wenye tabia nzuri, lakini pia wapo wenye tabia za ajabu kama uvivu, udokozi, kutojali muda, kusengenya, umbeya, wivu, au kijicho, kutojiamini, uzinzi, uasherati, ushoga na tabia zote mbaya tunazozijua hapa duniani.
Ule udhaifu tulio nao pia wenzetu hawa wanao tena wenzetu hawa wamepitiliza. Ila kutokana na kudanganywa na TV na hizo kauli za wazee wetu tumejikuta tukiamini kitu ambacho hakipo.
Mie wakati mwingine huwa nashangaa pale ninapokutana na baaadhi ya Watanzania wenzangu ambao wanaishi au wamewahi kuishi huku ughaibuni wanapozungumza kwa kubana pua kama hawa wenzetu. Wanashindwa kujua kwamba ile ni lafudhi ambayo inatokana na lugha yao. Ni kama pale unapokutana na Mmakonde, Mngoni au Msukuma au Mpare anapoongea Kiswahili kwa lafudhi ya lugha yao.
Mbona wenzetu kwa mfano Wanaijeria au Wakenya wanaongea kwa lafudhi ya lugha zao. Ni rahisi sana kumtambua Mkenya au Mnaijeria kutokana na lafudhi yake pale anapoongea Kiingereza, tofauti na sisi ambapo Tunajitahidi kubana pua mpaka tunajisahau hata pale tunapoongea Kiswahili.
Na ndio maana kuna baadhi ya wanawake huko nyumbani na hata huku ughaibuni wamefikia hatua sasa wanaukataa uafrika na kuanza kujichubua kwa mikorogo ili kuutafuta weupe.
Kuna wakati nilipokuwa huko nyumbani nilishangaa kuwaona baadhi ya wasichana ambao nawajua kabisa rangi zao kuwa ni weusi kama mimi lakini wamekuwa weupe mpaka wanatisha! Tabu yote hiyo ni ya nini?
Tumefikia hatua sasa kila jambo linalofanywa na hawa wezetu tunaiga, na ndio sababu siku hizi tabia kama za ushoga, usagaji na tabia nyingine chafu tunazozishuhudia huku zimetamalaki huko nyumbani.
Sisi kama Watanzania tunazo tabia nzuri ambazo hawa wenzetu wanazitamani sana tofauti na tunavyodhani. Kwa mfano, sisi ni kawaida mtu kuamka na kupita nyumba mbili tatu na kuwajulia majirani zake hali, au kuingia nyumba yoyote na kama akikuta chakula akala bila wasiwasi.
Kwa upande wa Misiba au harusi watu wamekuwa wakichangiana na kusaidiana kwa hali na mali, yaani tumekuwa na ushirikiano wa hali ya juu tofauti na wenzetu hawa.
Kuwa mzungu haimaanishai kuwa mwadilifu wala kuwa na tabia nzuri, bali tabia nzuri inatokana na tabia ya mtu na malezi kwa ujumla wake, hakuna mahusiano yaliyopo kati ya uadilifu, tabia nzuri na uzungu. Nasisitiza kuwa hakuna kitu kama hicho, ni kujidanganya bure.
Inashangaza kuona kwamba, badala ya kujivunia tabia hizi nzuri tulizo nazo ambazo hata hivyo wenzetu wanazitamani, tunatamani za kwao ambazo nyingi ni mbaya na zenye kuumiza.
Tubadilike………………