Saturday, July 23, 2016

UNAKUMBUKA ULIVYOKUWA UKIZUNGUMZA KATI YAKO NA BABU AU BIBI YAKO? EBU JIKUMBUSHE HAPA MAONGEZI KATI YA BABU NA MJUKUU WAKE.....

MJUKUU; Eti Babu mwisho wa dunia tutalia na kusaga meno ? 
BABU; Ndio mjukuu wangu. 
MJUKUU; Sasa mbona wewe huna meno ?

BABU; Kuna malaika ameajiriwa na Mungu kutugawia meno siku ya Mwisho
PAMOJA DAIMA!

Thursday, July 21, 2016

KARIBUNI TUJUMUIKE CHAKULA NI CHAGUO LAKO.....

 Ugali wa mahindi na maharage
 Ugali, samaki wa kuoka na mchicha
au ndizi
Binafsi nachagua chakula hicho cha katikakati si mnajua mimi ni mnyasa/mngoni:-)

Tuesday, July 19, 2016

MSIONE KUSUASUA NIPO.....MNAJUA TENA MSIMU HUU NI LIKIZO KWA HIYO FAMILIA INABANA:-) ILA NIPO

Si mnaona hapa .....msifikiri nimekasirika ni uchovu tu ila muda si mrefu nitakuwa nimeondokana na uchovu. Nawatakieni wote mtakaopita hapa siku njema ....Kapulya wenu.

Friday, July 15, 2016

TUMALIZE WIKI HII KWA KUTEMBEA RUVUMA KWETU...KWA BURUDANI HII ..RUVUMA YETU NZURI


Wimbo una sema Ruvuma yetu ni nzuri karibu tule vyakula vyetu vya asili kama mlivyoona alivyoonyesha....Yaani leo nimeselebuka sana...Ruvuma yitu yabwina...Ruvuma yitu yabwina mwe jasho tu hapa....

Wednesday, July 13, 2016

TENDA WEMA KADRI UWEZAVYO BILA YA KUJALI HALI ULIYONAYO.


Nimetumiwa hii habari na msomaji wa Maisha na Mafanikio...nimeona niiweka hapa ili iwe Elimu kwa  wengi wetu ...Karibu  twende pamoja.....
Daktari aliingia hospitalini kwa haraka sana baada ya kuitwa kwa shughuli ya Upasuaji wa haraka, alipokea simu haraka, na kuvaa nguo za kazi na kuelekea moja kwa moja kwenye chumba cha upasuaji. Wakati akielekea kwenye chumba cha upasuaji alimkuta Baba wa mtoto anazunguka huku na huku karibu na chumba hicho akimsubiria Daktari.
Baada ya kumuona tu, Baba mtoto akapayuka: “ Kwanini umechelewa kuja? Hufahamu kama maisha ya Mtoto wangu yapo hatarini? Hivi unayajua majukumu yako? ”Yule Daktari alitabasamu na kumwambia: “ Samahani sana, Sikuwa Karibu na Hospitali na nimejitahidi kuja kwa haraka sana baada ya kupokea simu kutoka hapa hospitalini….. Na kwakuwa nimeshafika ningekuomba upunguze jazba na hasira ili nifanye shughuli yangu” “Punguza hasira?!
Hivi ingekuwaje kama Mwanao ndiye angekuwa chumba cha upasuaji sasa hivi, ungeweza kupunguza hasira? Kama mwanao ndiye angekuwa anakufa sasa hivi ungefanyaje?” Yule Baba aliongea kwa hasira sana. Yule Daktari alitabasamu tena na kumjibu: “Daktari hawezi kurefusha maisha ya Binadamu” Nenda katulie na umuombee mwanao, sisi tutajitahidi kadri kwa uwezo tulionao kwa Baraka za Mwenyezi Mungu.
“Kutoa Ushauri kwa vitu visivyo wahusu ni rahisi sana” Alinong’ona yule Baba mwenye mtoto. Upasuaji ulifanyika kwa masaa kadhaa mara tu baada ya kumalizika Daktari alitoka akiwa anafuraha, “Asante Mungu! Mtoto wako amepona!” Kama una swali lolote utamuuliza Nurse!!” Bila ya kumsubiri Baba Mwenye mtoto kujibu chochote aliondoka kwa haraka kwenye eneo la upasuaji.
“ Kwa nini ni mkorofi sana huyu Daktari? Yaani hawezi hata kusubiri kidogo nimuulize maendeleo ya mwanangu” Baba wa mtoto alimjadili akiwa na nurse baada ya Daktar kuondoka. Nurse akamjibu, huku akitokwa na machozi:
“Mtoto wake alifariki jana kwenye ajali ya gari, alikuwa katika mazishi ya mtoto wake wakati tunampigia simu aje Hospitali kwa ajili ya upasuaji wa mtoto wako. Amefanikiwa kuyaokoa maisha ya mtoto wako, kwahiyo ameondoka kuwahi mazishi ya mtoto wake.”
HEKIMA:1. “USIMHUKUMU MTU YEYOTE…. SABABU HUYAJUI MAISHA YAKE NA KIPI KILICHOMKUTA KWENYE MAISHA YAKE.
2. “TENDA WEMA KADRI UWEZAVYO BILAYA KUJALI HALI ULIYONAYO.

Tuesday, July 12, 2016

ILE NYUMBA YETU YA MBINGA HUU NDIO MWONEKANO WAKE KWA SASA

 Pole pole ni mwendo...tutafika tu
 ....na pia madanda  yapo maana  tusikusahau mifugo....
.....matunda pia kama tuonavyo ndizi na miembe....mengine yanapandwa ........
kwa leo tuishie hapa.... kukiwa na mabadiliko basi tutajuzane. Tumwombe Mungu atujalie afya.

Monday, July 11, 2016

MAISHA YETU: FAHAMU NJIA SAHIHI YA KUKOSOA ILI MTU ASICHUKIE

KAMA binadamu tulioumbwa na Mwenyezi Mungu kila mmoja wetu amekuwa na upungufu katika eneo fulani, hali inayofanya mtu mwingine kutoa kasoro. Sio mbaya kutoa kasoro hiyo ila kuna njia nzuri ya kumkosoa mtu ili asichukie.
Leo tutaangalia mifano mbalimbali katika maisha yetu tunayoweza kuitumia pale tunapotaka kumkosoa mtu yeyote aliyefanya jambo kwa makusudi au kwa kutokujua bila kumfanya ajisikie vibaya. Kwa kuanzia, tumuangalie mkurugenzi mmoja aliyekuwa na viwanda mbalimbali vya kutengeneza nguo. Lakini siku moja aliamua kufanya ziara ya ghafla katika kiwanda chake kimoja.
Alipofika kiwandani aliwakuta baadhi ya wafanyakazi wake wakivuta sigara karibu kabisa na kibao kinachokataza uvutaji sigara sehemu hiyo. Mkurugenzi huyo akakisogelea kibao hicho na kuwaonesha wafanyakazi hao huku akiwauliza, ‘hamjasoma hapa?’ Wafanyakazi wote wakataharuki, wakashindwa kujieleza. “Vijana ningefurahi kama mngevuta sigara nje ya eneo hili au niseme hata nje ya kiwanda.”
Wafanyakazi hao walielewa kwamba bosi wao anatambua kuwa wamevunja sheria, lakini walimfurahia kwa sababu hakuzungumza nao kwa ukali, bali alizungumza kwa upendo na kuwafanya wajisikie kwamba wao ni wa muhimu katika kiwanda kile. Hilo lilikuwa ni fundisho kubwa kwao, kwani tangu hapo hawakurudia kosa hilo tena. Hivyo unaposhughulika na watu mbalimbali jaribu kuwa na busara katika kuwaeleza jambo.
Mfano mwingine ni kwa ofisa mmoja aliyejulikana kwa jina la Robby. Alikuwa na biashara zake na kila siku alikuwa akitembelea mojawapo ya biashara hizo. Ilifika siku moja akaenda kwenye ghala lake la vinywaji na kumwona mteja amekaa anasubiri huduma, lakini kulikuwa hakuna mtu wa kumhudumia kwa kipindi hicho.
Aligundua kuwa kwa wakati huo, wafanyakazi wake hawakuwa tayari kumsikiliza mteja huyo, bali walikuwa wamekaa kaunta, wakicheka na kuzungumza habari zao zinazowahusu bila kujali kuwa eneo lile ni eneo la kazi. Robby hakuzungumza lolote, taratibu akanyata kando ya kaunta na kumhudumia mteja yule mwenyewe na kukabidhi pesa kwa wauzaji hao wakati alipokuwa anaondoka.
Hapo tunaona kwamba Robby alitumia njia ya busara ya kuishi na wafanyakazi wale. Angeweza kutumia ukali au kuchukua hatua ya kuwafuta kazi mara moja, lakini kwa kuwa alikuwa ni mtu mwenye hekima na busara, aliamua kumhudumia mteja yule aliyemkuta na hilo lilikuwa fundisho kubwa kwa wafanyakazi wake.
Aliwapa somo kwa njia ya vitendo kwamba kazi si mahali pa mchezo, bali panahitaji kuheshimiwa na kumheshimu kila anayehitaji huduma. Vile vile tunaona kwamba viongozi wa umma mara nyingi wamekuwa wakipingwa kutokana na kutokuonekana katika majimbo yao.
Mara zote wanasongwa na kazi, wamekuwa katika hali ya ulinzi muda wote na wasaidizi wao ambao hawapendi watu wawabughudhi mabosi, kwa kuruhusu wageni wazungumze nao.
Lakini kuna mbunge mmoja ambaye mara zote amekuwa akiwaasa wafanyakazi wake kuwaruhusu watu wamuone. Amekuwa akisema kwamba sera zake zipo wazi kwa kila mmoja, lakini wasaidizi wake wamekuwa wagumu kumuelewa, na kuendelea kuwazuia wananchi wasiweze kumuona kwa urahisi ili waeleze matatizo yao yanayowakabili.Baada ya kuona somo hilo halieleweki kwa wasaidizi wake, mbunge huyo mwishoni alipata suluhu kwa kuamua kuondoa mlango wa ofisi yake.
Kitendo hicho kilitoa ujumbe kwa urahisi kwa wasaidizi wake, kwamba mbunge huyo yuko wazi na yuko tayari kumsikiliza kila mmoja. Hapo inamaanisha kwamba si lazima kila mara ukawa unazungumza na watu ambao hawakuelewi, wakati mwingine unaweza kuzungumza kwa vitendo, utaeleweka.
Kwa kawaida unapobadilisha maneno mawili au matatu inaweza kuleta tofauti kati ya kushindwa na mafanikio katika kuwabadilisha watu wasiweze kuwa na uchungu. Unapotumia njia ya busara katika kumrekebisha mtu aliyekosa, inamfanya mtu yule asiyekuwa na uvumilivu katika kuwasahihisha wengine kwa kuwakosoa katika njia ya uwazi, kujifunza kitu.
Mfano mwingine upo kwa familia mmoja, iliyokuwa inakarabati nyumba yao, kwa kutumia mafundi ujenzi, familia hiyo ilifikia mahala ikaamua kuwashawishi mafundi kufanya usafi mara tu wamalizapo kazi yao.
Kwa siku za mwanzoni mwa ujenzi huo, mama mwenye nyumba alipokuwa akirudi nyumbani baada ya kazi, alibaini kuwa eneo la nyumbani kwake lilikuwa chafu, lenye kuonekana vipande vya mbao na uchafu mwingine. Mama huyo hakutaka kuzungumza na mafundi hao, kwa sababu walikuwa wamefanya kazi nzuri.
Kwa hiyo baada ya mafundi hao, kuondoka, yeye na watoto wake waliokota vipande hivyo vya mbao na kusafisha eneo hilo la ujenzi. Siku iliyofuata alimwita kiongozi wa mafundi waliokuwa wakijenga na kumwambia kuwa, “Nimefurahishwa na jinsi mlivyoacha eneo hili jana usiku, lilikuwa zuri na safi, na halikuweza kuleta usumbufu kwa jirani.” Tangu siku ile na kuendelea, wafanyakazi wale baada ya kazi walikuwa wakikusanya takataka zote na kuacha eneo lile safi. Na kiongozi yule alikuwa akihakikisha kama wafanyakazi wake wameacha eneo walilofanyia kazi likiwa safi.
IMEANDIKWA NA LUCY NGOWI IMECHAPISHWA: 25 JUNI 2016

Saturday, July 9, 2016

MAISHA:- KIPAIMARA CHA BINTI YA KAKA YANGU JANETH NGONYANI

Katika maisha ya ukuaji wetu  kuna mambo mengi tunapitia...kwa mfano maisha ya kidini kwa sisi WAKATOLIKI  ni ubatizo, komunio ya kwanza, kipaimara, ndoa,au sakramenti nyingine kama upadre nk...kwa hiyo binti yetu JANETH tarehe 3/7/2016 alipata KIPAIMARA...Nami kama shangazi yako nakupa HONGERA SANA KWA KUPOKEA SAKRAMENTI HII YA KIPAIMARA.
Naupenda sana mtindo ulioanzishwa sasa kwa uvaaji wa nguo za kipaimara...

Friday, July 8, 2016

NYUMBANI NI NYUMBANI.....HODI HODI

Naona nimepatia muda kabisa ila huyo mlinzi hapo mlangoni sijui itakuwaje hapa maana na njaa ndo ninayo....

Thursday, July 7, 2016

LEO NI SIKUKUU YA SABABA/SIKUKUU YA WAKULIMA....

Leo ni sikukuu ya sabasaba...Basi mwenzeni nimekumbuka mwimbo huu tulikuwa tukiimba shuleni Saba saba eeh
Saba saba eeh mama x2
Aaahoiye eeh mama x2
Wakulima eeeh
Wakulima eeeh mama x2
Aaahoiye eeh mama x2
Muendelezo nimesahau ..Je? kuna anayekumbuka anisaidie? Maana hapa kuna kucheza pia sio kuimba tu ....

Wednesday, July 6, 2016

NAPENDA KUWATAKIENI SIKUKUU YA EID AL-FITR IWE NJEMA "EID MUBARAK"

Kwa muda kama mwezi sasa ndugu zetu Waislamu walikuwa katika mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani wakitimiza ibada ya nguzo za uislamu ambayo ni kufunga. KILA LA KHERI.

Sunday, July 3, 2016

UJUME WA JUMAPILI HII YA KWANZA YA MWEZI HUU WA SABA:- JUMAPILI NJEMA!

Kuna jambo linaweza kuja kwako kwa sura mbaya yenye kuumiza, lakini mwisho wake ukawa mzuri wenye utukufu, furaha na ushindi. Usikate tamaa kwa lolote unalopitia hujui mwisho wa hilo kuna nini. JUMAPILI NJEMA KWA YEYOTE ATAYEPITA HAPA!...

Thursday, June 30, 2016

HILI NI CHAGUO LA BLOG YA MAISHA NA MAFANIKIO KUWA PICHA AZIPENDAZO NA ZA MWISHO WA MWEZI HUU WA SITA

 Huwa najisemea  mara nyingi sana hakuna kabila litunzalo mila, tamaduni kama kabila la kiMasai ebu angalia hao akina kaka mavazi yao au tu kwa ujumla jinsi uwaonavyo wanavyothaminimila/utamaduni wao

Na hawa akina dada yaani mavazi yao ni rahisi na wamependeza. Bado watu tunahangaika  na utamaduni wa watu wengine  sijui masuruali.....nk. Kwanini kuiga utamaduni wa wengine wakati wenyewe tuna utamaduni mzuri na wa kuvutia?.....

Wednesday, June 29, 2016

UKOSAPO NENO JEMA, KHERI UJINYAMAZIE.

Nakuasa usikie, usemaji ni karama,
Maneno usirukie, sema mambo kwa kupima,
Utamkapo ujue, neno halirudi nyuma,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Kheri ujinyamazie, ovu huleta khasama,
Majuto yasikujia, “Laiti nisingesema”,
Mtu baa azuae, Motowe utamchoma,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Ni wengi wajiponzao, kwa zao mbovu kalima,
Heshima waitakao, waseme usemi mwema,
Wale waumbukanao, ni kwa ndimi kuparama,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Watazame wakuao, dunia kuwatazama,
Ni wale wapimiao, kabla ya kuyasema,
Na kimya wanyamazao, wakosapo neno jema,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Neno huenda likuwe,lizidi hata vilima,
Mambo mawi liyazue, akili zende mrama,
Au mema yatukie, liwapo neno la wema,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Funzo walitufunzao, wazungupule wa zama
Zama za kale na leo, walokimcha Karima,
Yawe mema tusemao, tusije zusha zahama,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Mola akubarikie, na ambaye akusoma,
Na furaha ututie, uwe ni diwani njema,
Mema utuhadithie, wana kwa watu wazima,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Shairi hili limetungwa na Mshairi maarufu Afrika Mashariki Bwana Amri Abedi, nami nimeona sio vibaya kulirejea ili tujifunze pamoja................. panapo  majaliwa tutaonana tena...

Tuesday, June 28, 2016

KUMBUKUMBU ISIYOSAULIKA...NIMEKUMBUKA MIAKA ILE NILIPOKUWA BINTI MDOGO NA KAZI YA KUTWANGA MIHOGO ILI KUPATA UNGA WA UGALI KULE NYUMBANI LUNDO/NYASA!

Ama kweli tumetoka mbali...nakumbuka shughuli hizi kama vile ilikuwa jana. Ila mama yangu huko aliko asterehe kwa amani. Ahsante mama kwa kunifunza hizi kazi, hata kama ilikuwa kwa mikwala:-) maana nakumbuka nilikuwa nachukua mihogo na vifaa vingine na kwenda kwa rafiki zangu Oliva,,, na huko sasa nikitoka saa nane  nyumbani kurudi saa kumbi na mbili. Kisa kucheza mipira wa kudaka(rede...redesta)...mmmmhhh we acha tu...je nawe unakumbuka shughuli  yoyote ile....

Monday, June 27, 2016

MABALAA HUMUANDAMA MTOTO WA KIKE TANGU AKIWA TUMBONI………!


Tatizo hili hufahamika kama Female Infanticide, yaani mauaji ya kukusudia yanayofanywa kwa mtoto wa kike. Achilia mbali kile kitendo cha mtoto kuuawa muda mfupi tu baada ya kuzaliwa, utelekezwaji wa mtoto wa kike mara tu anapozaliwa na kutoa mimba baada ya ugunduzi kwamba, ni mtoto wa kike, zote ni njia za kumuondoa mtoto wa kike duniani. Tatizo hili liko katika jamii zote zinazomchukulia mtoto wa kike kama balaa na yule wa kiume kama baraka kwa familia.
Kwa hapa nchini mtoto wa kike huuawa kwa njia isiyo ya moja kwa moja. Watoto wa kike hudharauliwa na kuachwa linapokuja swala la elimu katika familia. Ukichunguza hata wewe utabaini kwamba, katika familia nyingi, ambapo watoto wa kiume wamepata elimu bora, watoto wa kike katika familia hizo wamepuuzwa na hata kutopewa kabisa elimu.
Watoto wa kike, hasa wale wanaozaliwa nje ya ndoa wametelekezwa kirahisi, wamekataliwa na baba zao kirahisi, ukilinganisha na watoto wa kiume. Idadi ya watoto wa kike wanaokufa kutokana na kutelekezwa na kukataliwa na baba zao ni kubwa kuliko ya watoto wa kiume. Hata zile kesi nyingi za watoto kukataliwa na baba zao zinahusisha watoto wa kike zaidi.
Ni jambo la kushangaza kwamba ndoa ambayo ina watoto wa kike watupu hutazamwa kwa bezo na dharau ukilinganisha na ile yenye watoto wa kiume watupu. Hata wale wanawake wanaozaa watoto wa kike watupu hujihisi vibaya na kuamini kwamba walistahili kuzaa watoto wa kiume pia.
Kwa maeneo ua vijijini na katika familia masikini, watoto wa kike hutazamwa kama, ‘biashara ya kesho’ambapo watauzwa kwa njia ya mahari. Kwa hiyo thamani yao ni kuolewa, ni ile ya kibidhaa na sio kibinadamu. Na ndio maana mtoto wa kike anaposhindwa kuolewa huanza kuonekana kama mzigo usio na thamani, na hata kuzongwa hutokea.
Ili kujinasua na tatizo hili, msichana huenda kwa mwanaume yeyote kama kwa kujilazimisha. Kila mtu anajua kuhusu wazazi hapa nchini, ambao wamekuwa wakiwalazimisha binti zao kurudi kwenye ndoa za mateso kwa hofu ya kurejesha mahari. Kinachotokea ni binti hao kuuawa na waume zao. Ni wazi hii ni njia ya makusudi ya kuwapunguza wanawake, bila kujali mtu ataieleza vipi……………….
Chanzo........Jamii Forum

Sunday, June 26, 2016

JUMAPILI NJEMA.... LEO TUMETEMBELEA KANISA NDOGO LA SEMENARI YA PERAMIHO

KANISA NDOGO MPYA LA SEMINARI YA PERAMIHO
BARAKA ZA MWENYEZI MUNGU NA UPENDO ZIWE DAIMA KATIKA NYUMBA ZETU.

Friday, June 24, 2016

NAWATAKIENI MWISHO MWEMA WA JUMA ...NYASA HII! CHAKULA AKIPENDACHO KAPULYA

Ugali wa muhogo, Kisamvu, dagaa wabichi na kipande cha samaki tena kichwa...nakwambia hapo ni utamu tu....


Tuesday, June 21, 2016

ZAWADI KUTOKA KWA RAFIKI YANGU HUKO NYUMBANI....NI KISAMVU NA MIHOGO

 Nalipenda zao hili la muhogo sana kwanza unapata mboga, mti wake unaweza kutumika kama kuni...
...muhigo wenyewe unaweza kutafuna, kuchemsha na kula kwa chai asubuhi au chakula cha mchana au jioni pia unaweza kupika kama futari tena wakati huu wa mfungo wa Ramadhani  muhogo una  thamani ana. Maganda ya muhogo ni chakula kizuri sana kam unafuga baadhi ya wanyama pia samaki... hii ilikuwa  habari fupi kuhusu mihogo. Ila hii ni zawadi yangu kutoka kwa rafiki yangu. Najua kuna watu humu mmetamai:-)

Monday, June 20, 2016

SWALI KUTOKA KWA MSOMAJI WA BLOG YA MAISHA NA MAFANIKIO

Habari za leo ndugu zanguni...nimetumiwa huu ujumbe kwa barua pepe yangu..nimeona ni kheri niweke hapa kibarazani ili tusaidiani maana kwenye wengi pana mengi. Karibu tumsaidie huyo dada................................................................

Habari,  mimi ni dada ninayeishi Iringa nina umri wa miaka 18 kwa bahati mbaya mpenzi wangu amenipa mimba na kutokana namna alivyo baba yangu Naamini akifahamu kwamba nina mimba ataniua Kwani mimi ni mwanafunzi.
Nimeongea na mchumba wangu tumekubaliana tukaitoe.
Hata hivyo bado najiuliza kama kutoa mimba  ni kitu sahihi? Na je, nifanyeje Kwani nipo kwenye njia panda.

Sunday, June 19, 2016

JUMAPILI YA LEO TUPO KATIKA KIINI CHANGU NYUMBANI LITUMBANDYOSI...NA HILI NDIYO KANISA LETU

Kanisa hili ndilo alilosali babu, bibi, shangazi baba yangu na karibu wanafamilia wote wa Ngonyani husasani mimi Kapulya na  nimeshawahi kusali katika  kanisa hili na familia yangu....USISAHAU ULIKOTOKA NYUMBANI  KWA BABA YAKO NI NYUMBANI KWAKO.....JUMAPILI NJEMA KWA WOTE!

Friday, June 17, 2016

NI IJUMAA NYINGINE NA NI MWISHO WA WIKI KWA MAPUMZIKO KWA WALIO WENGI BASI UKIPATA WASAA CHUKUA DAKIKA YA KUPUMZIKA KWA MZIKI HUU...KWA AFYA


SIKILIZA NA HAPA PIA

NAWATAKIENI WOTE MWISHO MWEMA WA JUMA! KILA BINADAMU ANAHITAJI KUPUMZIKA/UTULIVU.

Thursday, June 16, 2016

LEO TUANGALIE METHALI ZETU ZA KISWAHILI....

1. Jirani mwema ni bora, kuliko rafiki.
2. Waarabu wa pemba hujuana kwa vilemba.
3. Usifungue duka ili kupenda kucheka.
4 Ukitaka kusaidiwa nawe, saidia mwenzako.
5. Palipo na moshi pana moto.
6. Kizuri kwako, kibaya kwa mwenzako.
7. Kaa na mwenye tabia njema, utashiriki ya heshima.
8. Baba na mtoto mwanaume, mama na mtoto mwanamke.
Kwa leo ni hizi ila nitaendelea kpekua nyingine  na kama nawe msomaji unazo mbili tatu  usisite kuendeleza orodha...WOTE MNAPENDWA!

Wednesday, June 15, 2016

NIMEOTA NDOTO NIPO LUNDO/NYASA NAKULA UGALI KWA SAMAKI NA KISAVU... MLO AUPENDAO KAPULYA...

Nilipoamka kumbe sio...maana hapa nilipo hata unga sina wa kusonga huo ugali sina. Nitabaki kula kwa macho tu......Ngoja nikatafute unga......

Tuesday, June 14, 2016

LEO TUPO KIJIJI FULANI MBAMBA BAY...

Nimeipenda taswira hii..inanikumbusha mbali sana. Hakika tumetoka mbali ...ngoja niache panapo majaliwa tutaonana tena. Kapulya.