Friday, July 31, 2009

NGOJA TUFUNGE MWEZI HUU NA PICHA HII:-JE? WEWE UNAONA NINI HAPA?

Nikiangalia mtu huu naona kama sahani kubwa ya kupakulia ugali. Yaani mpaka raha.

Thursday, July 30, 2009

Salamu wanablog I

Nimelipenda shairi hili na nimepewa idhini toka kwa aliyeandika Kaka Fadhy Mtanga kuwa niliweka hapa kwangu.


Nashika kalamu yangu, salamu nazituma,
Kwenu marafiki zangu, natumai mu wazima,
Nawaombea kwa Mungu, mjaliwe yalo mema,
Salamu wanablog.

Simon Kitururu, huzamia MAWAZONI,
Fikra zake ni huru, pia zina burudani,
Nasi tunamshukuru, hachoki tangu zamani,
Salamu wanablog.

Yupo dadetu Yasinta, yeye hupenda MAISHA,
Kamwe hawezi kusita, mazuri kutuonesha,
Sifa tele azipata, maana huelimisha,
Salamu wanablog.

Christian Bwaya yupo, hutaka tuJIELEWE,
Daima aandikapo, vichwa vyetu tusuguwe,
Ukweli daima upo, muhimu ujadiliwe,
Salamu wanablog.

Mubelwa Bandio pia, MZEE WA CHANGAMOTO,
Haishi kutuambia, mambo yalo motomoto,
Muziki hutupatia, yenye midundo mizito,
Salamu wanablog.

Subi dada yetu sote, wa NUKTA SABA SABA,
Ili mengi tuyapate, blog yake yashiba,
Asichoke asisite, ajaze hata kibaba,
Salamu wanablog.

Chib naye ni rafiki, hutumia HADUBINI,
Kazi yake haichoki, popote ulimwenguni,
Magharibi mashariki, hutujuza kulikoni,
Salamu wanablog.

MWANAMALENGA Kissima, hutuonesha MWANGAZA,
Makala zenye hekima, na mambo kuyachunguza,
Kwa ushairi ni vema, tungo zake zapendeza,
Salamu wanablog.

Serina Serina huyo, ana UPANDE MWINGINE,
Yale ayaandikayo, hupendwa nao wengine,
Kwa mawazo si mchoyo, hufanya tushikamane,
Salamu wanablog.

Koero Mkundi pia, hutuambia VUKANI,
Hachoki kutuletea, yatokeayo nchini,
Daima hukumbushia, tutoke usingizini,
Salamu wanablog.

Ndugu yetu Mumyhery, kabobea kwa MAVAZI,
Vitu vyake ni vizuri, hilo mbona lipo wazi,
Yupo kwenye mstari, hachoki kufanya kazi,
Salamu wanablog.

Kamala tunamjua, wa nyegerage KIJIWENI,
Fikra apambanua, ili tutoke kizani,
Sote tukajitambua, tujijue kina nani,
Salamu wanablog.

Masangu wa Nzunzullima, CHAKULA chake KITAMU,
Hatosahau daima, kutupa yote muhimu,
Ujuzi wake kisima, haisaliti elimu,
Salamu wanablog.

Markus Mpangala, KARIBUNI sana NYASA,
Yeye wala hajalala, mengi ameshayaasa,
Kabobea mijadala, ya jamii na siasa,
Salamu wanablog.

Lumadede mshairi, USHAIRI MAMBOLEO,
Mashairiye mazuri, tena yale ya kileo,
Huukuza ushairi, na kuupa mwelekeo,
Salamu wanablog.

Na MWANASOSHOLOJIA, siachi kumsifia,
Elimu kutugawia, na picha kutuwekea,
Mazuri hutuambia, ndani ya hii dunia,
Salamu wanablog.

Nami MWANANCHI MIMI, wa DIWANI YA FADHILI,
Tungo zangu siwanyimi, nawapenda kiukweli,
Tena mara kumi kumi, tena na kwa kila hali,
Salamu wanablog.

Ambao sijawataja, lipo shairi jingine,
Sote tungali pamoja, kwa mema tuombeane,
Tusichoke zetu hoja, hivyo na tushikamane,
Salamu wanablog.

Wednesday, July 29, 2009

BABA NA MAMA, NI NANI AMBAYE HAKUCHEZA MCHEZO HUU?


Katika ukuaji wetu, naamini wengi wetu tumeshiriki michezo mingi ya utotoni.
Mingi ya michezo tulioshiriki ni huu wa baba na mama ambao kule kwetu Songea tumezoea kuuita Madangi.

Mchezo huu wa baba na mama huchezwa na watoto kwa kuwaiga wazazi wafanyavyo kwa kuigiza mambo ya mapishi na mambo ya mapenzi ya kitoto.

Mchezo wa Mapenzi ya kitoto ndio ambao ningependa kuuzungumzia leo. Naamini karibu wote sisi, hakuna ambaye hajapitia mchezo huu. Inasemekana watu saba kati ya kumi miongoni mwetu, hakuna asiyefahamu mchezo huo.

Hata hivyo takwimu zisizo rasmi zinaonyesha kwamba watoto wa kiume ndio wanaoshiriki zaidi mchezo huu wa mapenzi ya utotoni kwa asilimia 85, ukilinganisha na watoto wa kike ambao wao hushiriki kwa kiwango cha asilimia 75.

Mchezo huu kiukweli hauna madhara yoyote kwa kuwa washiriki wote ni watoto, isipokuwa, adhabu na kauli zinazotolewa na wazazi hugeuka sumu.
Hebu fikiria watoto wanafumaniwa na mzazi wakicheza mchezo huu wa mapenzi ya kitoto, mzazi huyo anatoa adhabu ya viboko kwa watoto hao kisha kuwaita watoto hao kuwa ni wajinga na shetani wakubwa kwa kufanya jambo hilo ambalo wakati huo litabatizwa jina la mchezo mchafu na usiofaa kabisa, na mara nyingi kauli hizi kuelekezwa kwa mtoto wa kike, lakini mtoto wa kiume huachwa tu kwani kwa wazazi wengine huonekana ni shujaa.

Mara nyingi kile tulichoambiwa utotoni ndivyo tunavyokichukulia hata ukubwani, kwa hiyo zile adhabu za kuchapwa bakora na kuambiwa kuwa huo ni mchezo mchafu na wa kishetani, hubaki akilini mwetu hata leo na ndio maana tendo la ndoa miongoni mwetu hasa wanawake linabeba taswira ya kitu cha aibu na kisichofaa. Hii inatokana na zile kauli tulizoambiwa utotoni kuwa mchezo huo ni mbaya na wa kishetani.

Wanawake ndio wahanga wa kauli hizi na ndio maana hata wale walioko kwenye ndoa wanakosa uhuru wa kujieleza kwa wenzi wao kutoridhishwa na tendo la ndoa inakuwa ni vigumu. Atawezaje kujieleza wakati alimbiwa kuwa huo ni mchezo mchafu na wa kishetani usiofaa hata chembe kufanywa na mwanaadamu?

Unaweza kukuta mwanamke ameolewa lakini hawezi kuwa huru kumueleza mwenzi wake hisia zake za kimapenzi kwa sababu ya kauli hizi kukaa kichwani na kuhisi aibu.

Kwa hiyo kwa kutumia sauti za wazazi wetu au walezi wetu na sauti ya jamii tunalitazama tendo la ndoa kama uchafu ili hali tunalihitaji na ni muhimu ili tuendelee kuwepo.

Tuesday, July 28, 2009

UPENDO KWA NCHI YANGU+ NAJIVUNIA

Hapa vipi?


Sijui kama wenzangu mmewahi kujisikia hivi, mwenzenu leo nimeamuaka na kujiona ya kwamba:- Ninaringa kwa kuwa mtanzania nchi yangu yenye sifa zote za ustaarabu.

Ninaringia rangi yangu nyeusi, macho meupe, ngozi yangu nyororo, ninapendeza na nywele zangu nyeusi na kiswahili ni lugha yangu.

Ninajivunia nchi yangu ya Tanzania yenye miji ya kuvutia iliyojengeka. Angalia Dar es salaam, Mwanza nayo Dodoma bila kusahau kwenye marashi mji wetu Zanzibar. Halafu ukienda Arusha, Tanga, Kilimanjaro, Mbeya, Iringa na Songea.

Mnajua kuna vivutio vingi ndani ya Tanzania vinavyotufanya sote tujivunie kwa mfano kuna bahari fahari ya Taifa, Ziwa nyasa, viktoria, Tanganyika pia mlima mkubwa barani afrika Kilimanjaro. Bila kusahau mbuga za wanyama Serengeti, Ngorongoro, Tarangire, Mikumi n.k

Sunday, July 26, 2009

MAJIBU KWA KAKA BWAYA KUHUSU MIMI "YASINTA"

Hapa ni maombi maalau kutoka kwa kaka Bwaya. Anasema:-Dada Yasinta, mie nina maombi maalumu yafuatayo:

1. Tutajie mambo kumi tusiyoyajua kuhusu wewe. Uamuzi wa yapi unaweza kutuambia, unabaki kuwa wako.

2. Ni watu gani watano huwezi kuwasahau katika maisha yako?

3. Mambo yepi mawili yanatumia muda wako mwingi katika masaa ishirini na mane ya siku?

Nami nimejitahidi kujibu kama ifuatavyo:-

1. Tutajie mambo kumi tusiyoyajua kuhusu wewe. Uamuzi wa yapi unaweza kutuambia, unabaki kuwa wako.

=Mpole kiasi
=Mcheshi
=Mwenye upendo kwa watu wote bila kujali rangi, dini, kabila na itikadi
=Anayejali familia
=Anayependa kujitolea kuisaidia jamii, kwa njia mbali mbali
=Asiyependa majungu
=Mdadisi na anayependa kujifunza mamabo mapya
=Anayependa kuwafundisha wengine yale anayoyafahamu
=Anayependa kusikiliza muziki wa aina mbali mbali
=asiyependa kuona jinsia ya kike ikidhalilishwa kwa sababu ya mfumo dume2. Ni watu gani watano huwezi kuwasahau katika maisha yako?
=mama yangu na baba yangu
=Mzee aliyenilea nilipokuwa masomoni chuo cha kupiga chapa
=Rafiki yangu aliyenipeleka hospitali nilipokuwa naumwa na mguu baada ya kuchomwa na mwiba wa samaki
=Mume wangu
=watoto wangu

3. Mambo yepi mawili yanatumia muda wako mwingi katika masaa ishirini na mane ya siku?


=Familia na kublog
=Kazi

JUMAPILI NJEMA KWA WOTE!!!

Friday, July 24, 2009

SALAAM KUTOKA SWEDEN KWENDA MAHENGE - SONGEAKatika maisha kuna wengine maisha yao yote wameishi na baba na mama. Lakini kuna wengine wameishi na watu tofauti tofauti. Kati ya hawa watu walioishi na watu tofauti tafauti ni mimi. Kuanzia mwaka 1989 mpaka 1991 nilikuwa naishi na familia ya mzee Innocent Kapole Nyoni Mahenge Songea.
Kipindi hicho nilikuwa nasoma chuo cha typing pale Songea. Nilipotoka pale ndo nikaenda Sec.School Wilima kuanza kazi. Kwa hiyo huyu mzee ni mtu muhimu sana kwangu. Kwani yeye ndiye aliyenitafutia kazi ile. La sivyo leo nisingekuwa hapa ninablog na kufahamiana na watu wote niliofahamiana nao.
Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa familia nzima. Kwani wao wamekuwa kama familia yangu kabisa. Mungu awe nanyi daima.

Wednesday, July 22, 2009

MAISHA HAYA JAMANI!!!!!!

Alikuwa ni Binti wa nne kuzaliwa hapo mnamo mwaka 1967 kati ya watoto nane katika familia hiyo, akiwa ametanguliwa na kaka zake watatu. Alipofikisha umri wa kwenda shule hapo mnamo mwaka 1974 alipelekwa kusoma shule iliyopo kijiji cha jirani takribani kilomita 4 akiwaacha kaka zake wakisoma shule iliyoko umbali wa mita 200 kutoka nyumbani.

Inasemekana kuwa eti aliandikishwa kusoma katika shule hiyo ya jirani lakini kutokana na shule hiyo kupokea wanafunzi wengi kupita kiasi ndipo walipogawanywa na wengine kupelekwa kijiji cha jirani ambapo kulikuwa na nafasi.

Kulikuwa uwezekano mkubwa wa baba yake kufanya mipango ya kuhakikisha kuwa mwanae huyo hasomi mbali na nyumbani lakini hazikufanyika juhudi zozote kufanikisha jambo hilo na badala yake aliachwa na hivyo aliendelea kusoma katika shule hiyo.

Alilazimika kuamka majira ya saa kumi alfajiri kila siku akiwa na wanafunzi wenzie walitembea kilomita hizo nne kwenda na kurudi na huku wakipigwa na baridi kali na wakati mwingine kunyeshewa na mvua, lakini alivumilia na baada ya miaka saba alimaliza darasa la saba mwaka 1980.Baada ya kumaliza masomo kama ilivyokuwa kwa kaka zake hakubahatika kuendelea na masomo ya sekondari, ingawa baba yake alikuwa na uwezo wa kuwaendeleza na masomo wanae lakini hakuona umuhimu wa kufanya hivyo ingawa yeye alisoma mpaka darasa la nane la mkoloni na kuajiriwa serikalini kama karani katika chama cha ushirika wilayani.

Mnamo mwaka 1981 kaka yake binamu ambaye alilelewa na wazazi wake na ambaye alikuwa ni dereva alimchukua na kumpeleka Moshi kwa madai kwamba amemtafutia chuo cha kujifunza mambo ya Typing.

Alipofika huko alifikia kwa mama mmoja wa kisomali ambaye alikuwa na familia ya watoto nane, watano wa kike na wakiume watatu. Cha kushangaza alijikuta akiamshwa asubuhi na mapema na mama huyo na kukabidhiwa furushi la nguo akafue. Binti wa watu akatahamaki, kulikoni apewe kazi ya kufua wakati alikuwa ameahidiwa kusomeshwa mambo ya Typing? Yule mama kama vile alikuwa akisoma mawazo yake akamwambia kuwa yeye pale ni House Girl, na akapewa ratiba ya siku nzima. Alikuwa akiamka alfajiri saa kumi na kuanza usafi wa nyumba akimaliza apike chai ya watu wote kisha achukue nguo za familia nzima kuzifua, akimaliza anaosha vyombo vilivyotumika kwa chai ya asubuhi, kisha anaenda sokoni na kadhalika na kadhalika ilimradi ilikuwa ni kazi mtindo mmoja.

Alikuwa akitukananwa na kudhalilishwa kama vile hakuwa na wazazi, lakini alivumilai kwa kuwa hakuwa na pa kwenda.

Hakuwahi kumuona yule kaka yake binamu kuja kumjulia hali wala nini alijikuta akiwa ametelekezwa ugenini asijue kwa kukimbilia.

Baada ya miezi mitatu ya mateso bila malipo ndipo siku moja akakutana na mjomba wake ambaye alikuwa ni mfayabiashara maeneo ya sokoni, walisalimiana lakini mjomba wake alimshangaa kutokana na kumuona akiwa amekonda sana, alimuuliza sababu ya kukonda kiasi kile na alitaka kujua anaishi pale Moshi na nani?

Yule binti alisimulia mateso anayoyapata na kutokana jinsi alivyokuwa amekonda mjomba wake hakuvumilia alilia sana na pale pale alikata tiketi ya basi na kusafiria naye hadi kijijini kwao ambapo alimlaumu sana dada yake kwa kitendo chake cha kumtoa mwanae na kumpeleka kufanya kazi za ndani na kuteseka kiasi kile, mama wa yule binti alishangaa sana kwani yule binamu yake aliyemchukua alikuwa kila akipita pale kijjini na gari alikuwa anatoa salamu kutoka kwa huyo binti kuwa ni mzima na anaendelea na masomo vizuri.

Mama wa binti yule alilia sana kwa uchungu, ingawa baba wa binti hakuonekana kujali sana, kwani wakikutana na huyo binamu aliyemchukua huyo binti hununuliwa pombe kwa hiyo hakuonekana kujali wala kumlaumu binamu kwa kitendo chake cha kikatili.

Binamu alipofika moshi aliambiwa kuwa binti ametotoka na ameiba nguo na pesa kiasi cha shilingi elfu ishirini, miaka hiyo ya themanini elfu ishirini ilikuwa ni kiasi kikubwa cha pesa, kumbe ilikuwa ni uongo kwani binti alikuwa ametumwa sokoni na alipewa shilingi hamsini za kununua mahitaji fedha ambazo hata hivyo alizisalimisha kwa mama yake mara alipofika tu.

Siku iliyofuata binamu alifika na kudai kuwa binti ni mwizi na kamfedhehesha sana, mama wa binti alimkata kalima, na kumuuliza sababu ya kumpeleka binti yake kuwa mtumishi wa ndani wakati alimuahidi kuwa atamsomesha Typing?Alimkabidhi ile shilingi hamsini na kumuambia aipeleke kwa msomali wake.

Kumbe huo ndio ulikuwa mwanzo wa mateso ya binti huyu.

Mwishoni mwa 1981 alichukuliwa na mama yake mdogo waliyechangia baba na mama yake na kupelekwa Dar kwa ahadi ya kusomeshwa, alipofika jiji Dar alijikuta akiwa ni muhudumu wa kuku wa mayai, kwani huyo mama yake mdogo alikuwa ni mfugaji wa kuku.

Mnamo August 16,1982, binti huyu alipata pigo la mwaka baada ya kupata taarifa za kufariki kwa mama yake ghafla kwa ugonjwa wa moyo.Ilimlazimu kurudi kijijini haraka ili kuhudhuria mazishi ya mama yake, ingawa hata hivyo alichelewa.

Baada ya mazishi Binti yule alimueleza baba yake kuwa alipokuwa Dar hakuwa akisoma kama alivyoahidiwa, safari hii tena akachukuliwa na mama yake mdogo tumbo moja na mama yake na kupelekwa Arusha alipokuwa akiishi huyo mama yake mdogo ili akasomee hayo mambo ya Typing, na alipofika kule kweli alijiunga na chuo cha kusomea typing, lakini mama yake mdogo alikuwa ni mkorofi kweli kwani ilikuwa kila akichelewa kidogo tu alikuwa akipigwa sana kwa madai kwamba alikuwa kwa wanaume, na pia alikuwa akitumikishwa kufanya kazi za hapo nyumbani kupita kiasi.Yule mama alikuwa na mradi wake wa mambo ya ususi, wakati huo kulikuwa hakuna mambo ya saloon. Kwa hiyo akimaliza kazi za nyumbani alikuwa anamsaidia mama yake huyo kazi zake za ususi.

Mateso yalipozidi ilibidi atoroke na na kurudi kijijini. Baada ya kutoonekana kwa siku mbili mama yake mdogo alisafiri hadi kijijini na kumkuta binti akiwa nyumbani kwao ametulia.

Baada ya mashauriano ikaamuliwa binti abaki pale kijijini.Miezi kadhaa baadae binti akapata mchumba, akalipiwa na mahari, haikuchukua muda hata kabla ya kufunga ndoa binti akapata ujauzito, na hivyo ndoa ikaahirishwa mpaka baadae atakapojifungua.

Baada ya miezi tisa binti alijifungua mtoto wa kiume, jambo ambalo lilifurahiwa na pande zote mbili. Hata hivyo swala la kufungwa kwa ndoa likawa linapigwa danadana hatimaye kijana muoaji akatoa taarifa kuwa haoi tena.Kisa, yalipenyezwa maneno ya fitna na baadhi ya ndugu ili kuvunja ule uchumba, mpaka leo sababu haijulikani.

Mnamo mwaka 1985 binti akalazimika kwenda Dar kwa kaka yake mkubwa ambaye alikuwa ni mtumishi serikalini ili kutafutiwa shughuli ya kufanya.Alipofika akatafutiwa kazi na kaka yake na hivyo kumudu kujitegemea kwa muda mfupi.

Mnamo mwaka 1990 akapata mchumba mwenyeji wa Singida ambaye alikuwa ameachana na mkewe na hivyo kuanza maisha mapya akiwa na mumewe huyo bila ya kufunga ndoa.Maisha hayakuwa mazuri sana kwani bwana huyo alikuwa na wivu sana, kwani alikuwa hataki kumuona akiongea na mwanaume yeyote, na ikitokea amemkuta na mwanaume ni lazima kutatokea ugomvi mkubwa ajabu.

Maisha na bwana yule hayakuwa mazuri sana, kwani kila siku hali ilizidi kuwa mbaya na kibaya zaidi ni pale yule bwana alipoachishwa kazi. Ilibidi binti aanzishe biashara ili kumudu kujikimu, lakini bwana yule wivu ulimzidi, kila akiongea na mteja ni bwana ake.

Binti yakamshinda, mnamo mwaka 1993 mwishoni akaondoka na kurudi kwa kaka yake akiacha vitu vyake vyote kwa yule bwana, kwani yule bwana ndiye aliyehamia kwa binti lakini alizuia vitu vyote kwa madai kuwa ni vya kwake.

Baadae binti akjikuta ni mjamzito, lakini hakutaka kumwambia yule bwana ingawa alikuwa na uhakika kuwa ule ujauzito ni wa yule bwana.Mwanzoni mwa mwaka 1994 binti aliamua kurudi kijijini kwao, wakati huo ujauzito wake ulikuwa na miezi mitano.

Ujauzito ulipofikisha miezi sita binti yule alipotea akawa hajulikani alipo. Ndugu zake walifanya juhudi kumtafuta bila mafanikio, lakini baada ya siku mbili alirudi mwenyewe akiwa amechoka sana, lakini alikuwa kama amechanganyikiwa, alipopelekwa hospitalini hakuonekana kuwa na ugonjwa wowote na mapigo ya moyo ya kiumbe kilichokuwa tumboni yalikuwa yanaenda vizuri.

Ilibidi awekwe chini ya uangalizi wa bibi yake mzaa mama kwani ilihofiwa kuwa angetoroka tena na kupotelea porini.Mwezi mmoja baadae, ujauzito ulipokuwa na miezi saba, binti yule alipata kifafa cha Mimba na hatimaye roho yake ikaachana na mwili, ilikuwa ni May 12, 1994.

Huo ndio ukawa ni mwisho wa binti huyu.

Simulizi hii ni Dedication kwa binti huyu ambaye ni dada wa rafiki yangu.

Monday, July 20, 2009

HISTORIA FUPI YA VANGONI (WANGONI)

Mwenzenu leo nimejikuta kutamani kuandika historia hii ya wangoni kwa kingoni. Naogopa nitasahau lugha yangu ya asili. Haya someni kama mtaambua mawili -matatu nitafurahi.


Vangoni vitama kuSongea-Tanzania. kuZambia na kuMalawi. Kadeni vangoni avo vatamayi kuZululand. Myaka ya 1800 vakawuka kwenuko pamonga na vanduna na vankosi vavi na kuyingila kumulima uwu. Mulugendu lwavi ulo vakapita kutova ngondo nakutola vavanda vamahele na kuvakita vangoni ngita vene, muni vajovayi “mwana wa lihimba nga lihimba mewa”. Pakukomana ngondo, vangoni vanyagayi ngómbi, mene, mamberere, ngúku na kuwuka. Popoha pevatovayi ngondo vavatolayi vandu vavi na kuyonjekesa uvaha wa kabila lawu na kuyendelela kulingolo na kuyingila mavidunda venijovilivo. Vangoni vayingili kuTanzania kwa mabanja gadatu libanja la Vangoni va Zwangendaba, libanja la vangoni va Mputa Maseko na libanja la vangoni va Zulu Gama na Mbonane Tawete. Mabanja aga goha hata ngati galongosini lepi lukumbi lumonga pakuyingila kuTanzania, nambu gapitili mulamula mwe gipitili mabanja gangi na kutola vavanda. Nsava ya naha ukuvavona vangoni vahangasiniki na mahina gavi pamonga na vibongo na mahina vavanda wavi.

Vangoni va Zwengedaba

Zwangendaba au vakumkemela Zongendaba, amanyikini muni na vangoni na vazeyi voha va chingoni. Chibongo cha lukolo lwa Zongendaba chavi Nkosi au Tole. Vibongo voha ivo akavileka na kutola lihina la Jere. Dadi wa Zongedaba na wamkelayi Hlachwayo. Vijova ya kuvya Zongedaba ahumili kuTanzania. Vangoni va Zongendaba vevayingili kuTanzania, vakahamba kuUjiji ya kuTabaora na kutama kuKahama. Kwenuko vimanyikana kwa lihina la Vatuta. Zongendaba afwili kuMapupo (Chipata) –Ufipa mwaka 1858 na wamhilili kukwokwo. Hinu vandu veavayolili Zwangendaba kuyingila kuTanzania nde ava: Waswazi, Wandwandwe, Wathonga, Wakalanga, Wamashona, Wasenga, Wachewa Watumbuka, Wakamanga, Wasukuma.

Vangoni va kwaZulu Gama na va kwa Mbonane Tawete
Lukolo lwa kadeni sana kuyingila kuSongea lwavili lwa mwene Bambu Zulu Gama na Mbonane Tawete. Yiwonekana veneva vavi he pamonga na Zongedaba peayingilayi kuTanzania na kuhamba kuTabora. Zulu Gama na Mbonane vabwelili lukumbi lungi kuhuma kuzululand. Mbonane Tawete avi mwana wa Mshopi, mwana wa Kibovu mwana wa Kisara. Mulugendu lwavi kuhuma kuzululand, Mbonane na dadi waki Mshopi wakakonganeka kunyanja na vangoni wa kwaZulu. Kunyanja kula Zulu Gama na Mbonane wakatemana ukozi. Mbonane akampela Zulu mlumbu waki Ushambazi au wakumkemela Mafunasi (Nasere) kuvya inkosikazi waki. Mbonane Tawete avi mkozi wa Zulu. Pakuhuma kunyanja kula, voha vavili vakayingila pamonga kuTanzania. Ndava ya naha vandu va Zulu na va Zwangendaba vihwanana mahina na cibongo vyavi. Kuhuma kwa kunyanja uko, voha Mbonane na Zulu vakagenda pamonga na kutindila ngita vangoni va Zwangendaba naha, kuhuma kuSwaziland, vakapita kwa vatonga, kwa wakalanga, kwa wasenga na kwa wasukuma, wakavayonjakesa na wachewa. Vangoni va kwaZulu na va kwaMbonane vakonganiki he na vangoni ya Zwangendaba. Ila pevapitayi vazulu na va Mbonane vapilikayi kuvya mulamula apitili Zwangendaba. Zulu na Mbonane vakakupuka mfuleni wa Zambezi kwa mtahu sana ndava mfuleni uwu unyoliki na kutaluka na umemi mang´wina. Pakumala kukupuka, vandu vakam´bongelela na kumyimbila nyimbo Jeru muni avalangisi pahala pabwina pakukupuka. Pakuhuma kwenuku, vakalongolela na kuhika kuMalawi na kuZambia na kuyingila kuMalangali – Tanzania. Njeru dadi wa Zulu na Mshopi dadi wa Zongendaba vene wafwili kuZambia, vayingi he kuTanzania.

Sunday, July 19, 2009

HONGERA KWA SIKU YA KUZALIWA BABA/BABU YETU

Hapa ni wakati wa ujana nadhani ilikuwa miaka ya 1970.
Hapa ni mwaka 2009 na baadhi ya wajukuu wake

Napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumlinda baba yetu mpaka siku hii ya leo, umetimiza miaka 62. Sisi watoto, wajukuu na marafiki tunakutakia maisha mema na tunakupenda sana. Kwani wewe ni mtu muhimu sana katika maisha yetu. Uwe na siku nzuri baba.Thursday, July 16, 2009

UTALII SASA KUVUMA RUVUMA

Nafikiri wote mnajua kuwa mimi ni mtu wa kutoka kijiji cha Litumbandyosi.


WanaMbinga kuonyesha njia

Vivutio vya Kusini kutangazwa


WILAYA ya Mbinga, chini ya usimamizi wa Halmashauri yake, mkoani Ruvuma, imedhamiria kufungua mianya ya kitalii kwa kuanza na uhifadhi wa pori la akiba la wanyama la Liparamba lenye wanyama na ndege wa aina mbalimbali, imefahamika.

Pori hilo la Liparamba ni msitu mnene wenye maji yanayotiririka na linaweza kutajwa kuwa kati ya hifadhi chache zenye vivutio vya kipekee.

Pori hilo litaendelezwa na kutunzwa ili wanyama na ndege wengi waweze kuzaliana na hatimaye vijiji vinavyolizunguka vianze kufaidika na hifadhi hiyo.

Wakati Wilaya hiyo imefanikiwa kuanzisha pori la akiba la wanyama Liparamba, wananchi wa vijiji vya Litumbandyosi, Paradiso, Luhagara, Ruanda, Mtunduwalo na Ndongosi wilayani humo nao kwa kauli moja wameridhia pori la Litumbandyosi linalozunguka vijiji hivyo kuwa hifadhi ya wanyama .

Halimashauri hiyo imependekeza kutenga pori la akiba la Litumbandyosi wilayani humo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 320 kwa ajili ya hifadhi ya wanyama pori baada ya kuwashirikisha wananchi wanaozunguka vijiji vya hifadhi hiyo.

Vijiji hivyo viliridhia mpango huo tangu mwaka 2003, na kisha Serikali iliweka mipaka ya kutenga eneo hilo na maeneo ya wananchi.

Kijiji cha mwisho, cha Kingole, ambacho kilikuwa hakijatoa ridhaa ya kukubali pori hilo kuwa hifadhi, hatimaye nacho kiliridhia nia hiyo Novemba 2008.

Akizungumzia hatua hiyo hivi karibuni, Kamanda wa Kikosi cha kuzuia ujangili Kanda ya Kusini, Metson Mwakanyamale aliwasisitiza wananchi wanaozunguka vijiji hivyo kuwalinda wanyama waliopo katika hifadhi na kuhamasisha utalii katika Mikoa ya Kusini.

Mwakanyamale anasema utalii si kuona wanyamapori pekee bali ni pamoja na shughuli za kiasili na kipekee zinazofanywa katika maeneo yao pamoja na kuweka mazingira ya utalii endelevu.

Anasema kwa kuridhia mchakato wa hifadhi ya pori hilo sasa wananchi wataweza kupata maendeleo ya haraka kama wawekezaji watafika kuwekeza.

“ Sasa mtaingizwa katika uhifadhi shirikishi katika mamlaka zilizoundwa na Serikali za Vijiji za kuhifadhi wanyama, mtapangiwa wanyama wa kuwinda kwa kuwa ni haki yenu na ndiyo moja ya faida ya sekta ya utalii,” alisisitiza .

Aliongeza: “Utalii hauzungumzii jambo moja tu la kuangalia wanyama, bali pia ni pamoja na kusafiri kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine pamoja na kuona shughuli zinazofanywa na watu katika maeneo husika.”

Katika kuhakikisha sekta ya utalii inakuwa endelevu katika kanda ya kusini na hasa mkoani Ruvuma, Kamanda Mwakanyamale anasema amefanya mazungumzo na Ofisa Elimu wa Mkoa wa Ruvuma kuhusu mikakati ya sera ya idara ya wanyamapori kuhusu utalii Kusini mwa Tanzania .

Anasema chini ya sera hiyo kuna utalii wa kuangalia wanyama bure unaofanyika katika hifadhi ndogo ya wanyama ya Luhira iliyopo Manispaa ya Songea.

Kulingana na Mwakanyamale, utalii huo wa bure katika hifadhi hiyo unaanza mwezi huu hadi mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka huu ambapo wameagizwa maofisa elimu katika wilaya zote mkoani Ruvuma kuhakikisha kuwa wanafunzi wanakwenda katika hifadhi hiyo ili kuwaona wanyama bure.

“Licha ya burudani hiyo ya kuwaona wanyama bure pia wanafunzi na watu wengine watakaokwenda kutembelea hifadhi hiyo watapa elimu ya biolojia na ekolojia kuhusu utalii, lengo likiwa ni kuamsha utalii wa ndani kuanzia mtoto wa shule ya awali, msingi na sekondari.” Anasema.

Meneja Mkuu wa mradi wa pori la akiba la wanyama Liparamba, Mbinga, ambaye pia anasimamia hifadhi ya Litumbandyosi, Hashim Sariko anasema ya kuwa eneo hilo linafaa kuwa hifadhi ya wanyama kwa kuwa lina wanyama na ndege wa aina mbalimbali.

Anawataja wanyama waliomo katika pori hilo kuwa ni viboko, nyati, parahala, nyani, nguruwe pori, chui, pofu, swala, tembo, faru na aina mbalimbali za ndege wakiwamo kware, kanga na njiwa.

Sariko anasema kuwa eneo hilo lipo katika ukanda wa uhamiaji wa wanyama kutoka Hifadhi ya wanyama ya Selous ambako kuna wanyama wengi na kwamba wanyama hao wamekuwa wakiingia katika pori la Litumbandyosi kupitia ushoroba uliopo katika maeneo ya Lutukira, Hanga Gumbiro na Ngadinda wilayani Songea.

Anaongeza kuwa hifadhi tarajiwa hiyo pia ilipata kuwa kitalu cha uwindaji ambacho kilimilikiwa na kampuni ya Miombo Safari Hunting ambayo ilianza kuimarisha ulinzi na uendelezaji wa pori hilo ikiwa ni pamoja na kutengeza barabara, madaraja na camp site moja kabla ya kuacha kuendeleza pori hilo baada ya wananchi wanaozunguka hifadhi hiyo kushindwa kutoa ushirikiano na kampuni hiyo na kusababisha wanyama kutoweka.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, malengo makubwa ya Serikali katika sekta ya utalii sasa ni kujaribu kupanua wigo wa utalii Kusini mwa Tanzania kwa kutambua vivutio vya utalii vilivyopo Kusini na kuviuza nje ya nchi ili wananchi waweze kunufaika navyo.

“Pori la wanyama Liparamba tayari limeendelezwa na watu wanaweza kwenda kutembelea na kuangalia madhari ya msitu mnene na namna maji yanavyotiririka kutoka milimani na kuingia katika mto Ruvuma, wanaweza kuangalia ndege na wanyama waliopo katika pori hilo,” anasema na kuongeza:

“Ni sehemu chache sana za hifadhi za wanyama hivi sasa ulimwenguni zinazofanana na uzuri wa pori la Liparamba, vivutio hivyo ndivyo ninavyouzwa sasa nje ya nchi na hapa Litumbandyosi baada ya kukamilisha mipaka ya hifadhi itanibidi nikae chini na kuangalia ni kitu gani kitawavutia wageni katika hifadhi hii na hasa wanyama.

Sariko anasema watalii wanaoingia nchini itabidi waje Kusini baada ya milango ya utalii kufunguliwa badala ya kwenda kaskazini pekee wakati Kusini kuna vivutio vingi vipya vya utalii ambavyo havijatangazwa.

“Lengo ni pamoja na kuboresha maisha ya wananchi wanaozunguka katika vijiji hivyo yawe bora kwa kutumia hifadhi ya wanyama ya Litumbandyosi baada ya mchakato wa kuifanya kuwa hifadhi ya wanyama pori kukamilika,” anasisitiza.

Anabainisha kuwa barabara za lami kutoka Masasi hadi Mbambabay zinatarajiwa kujengwa hivyo ni vema kujiandaa na watalii mbalimbali ambao wataingia Kusini kwa kuvitambua vivutio vya utalii na kuvitangaza sanjari na kusomesha vijana kozi mbalimbali za utalii.

Hii habari nimeipata kutoka raimwema http://www.raiamwema.co.tz


NI MARA CHACHE SANA UTAKUTANA NA MWANAUME AKITOA MACHOZI YA UHAKIKA

Chozi
Wanawake kweli ni viumbe wa thamani ambao wakati mwingine hushangaza; hata hivyo yote ni kwa utukufu wa Mungu aliyetuumba tuwe tofauti ili kukamilishana.

Machozi ni moja ya vitu ambavyo mwanamke huhusika moja kwa moja hata katika malezi wazazi wetu walikuwa wanatuonya watoto wa kiume tusilie tukikutana na jambo kubwa au gumu kwani walisema kulia ni mwanamke na si mwanaume.

Mwanaumke huweza kutoa machozi akifurahi, akihuzunika, akikutana na rafiki au ndugu ambaye walioachana muda mrefu, hata wakati mwingine hutoa machozi ili kupata kitu na wakati mwingine hutoa machozi kwa kupoteza kitu katika miliki yake yaani moyo, na kwenye misiba basi huko usiseme maana ukichanganya na mila inakuwa shughuli nzito.
Kwa maelezo zaidi ya machozi na mwanamke soma hapa

Pia machozi ni moja ya silaha mwanamke hutumia hasa kujilinda kwani anaweza kujieleza kwamba tafadhari “Usiniambie mapungufu yangu la sivyo nitaaza kutoa machozi sasa hivi”
Hata hivyo kazi kubwa ya mwanaume ni kutofautisha machozi ya hisia, msongo wa mawazo na uchoyo, ni kweli mwanamke ni emotional creature ambaye mwanaume lazima uwe makini to handle with care.

Hata hivyo Watafiti wengi wanakubaliana kwamba mwanamke anayetoa machozi ni mzuri sana lipokuja suala la hisia katika maeneo yote ya maisha hii ina maana kwamba mwanamke mwenye kumwaga chozi mara kwa mara ni mtamu chumbani kwa sababu anaweza kujieleza katika lugha ya mapenzi (love making, act of marriage) Na mwanamke mwenye macho makavu maana yake ni mgumu kuji –express wakati wa kuwa mwili mmoja.

Wanawake wenye machozi ni mara chache sana kuwa baridi (frigid) wakati wa kuwa mwili mmoja kwani ukimwandaa ni rahisi kuwa connected kihisia.

picha na maandishi kutoka kwa kaka Lazarus Mbilinyi :- mbilinyi.blogspot.com

Tuesday, July 14, 2009

KUMBUKUMBU+MAISHA

Nakumbuka ilikuwa mwaka 1983 nilikuwa naishi Lundo (Nyasa) wakati huo. Siku moja mchana nilikuwa naosha vyombo. Nilikuwa nasugua sufuria na vyungu hii ilikuwa kazi yangu. Kama mjuavyo Nyasa ni kula samaki sana. Kuna mtu alitupa miiba ya samaki ovyo na kwa mimi kutojua ni sehemu ile ile niliyokuwa nikiosha vyombo. Kwa bahati mbaya nilipiga magoti bila kujua napiga magoti kwenye miiba. Mmh kazi kwelikweli.

Baada ya siku goti lilianza kuvimba, nilichofanya tangu siku ile ya kwanza sikumwambia mtu nini kimenipata. Sababu kubwa ni kwamba ningeambiwa nibaki nyumbani. Sio kwenda shule ni mgonjwa. Na goti lilizidi kuvimba, lakini nilijikakamua na kuvumilia na maumivu yote. Kisa nilikuwa sitaki kubaki nyumbani bila kuhudhuria masomo.

Lakini siku moja wakati nipo shule nilikosa raha sana kwa maumivu. Rafiki yngu mmoja aitwae Claire Mputa aliona goti langu limevimba sana. Akanishauri niende hospitali naye atanisindikiza. Hata hivyo nilikataa kisa ni kile kile kuogopa kukosa masomo yatanipita. Lakini Claire aliweza kunishauri.

Ilichukua muda mrefu kufika hospitali kwani sasa goti lilikuwa limevimba mno na nilikuwa nachechemea na pia lilikuwa linauma sana, kwani kidonda kilianza kutunga usaa (infection). Kwa hiyo tulikuwa tunatembea polepole sana. Na hapo hatukuwa sisi tu kulikuwa na wanafunzi wengine pia waliokuwa wagonjwa wao walitangulia . Baada ya muda, yaani tulikuwa tunakaribia kufika hospitali tukawakuta wale wanafunzi wenzetu waliotangulia wamechepuka maporini ambako kulikuwa na miembe mingi iliyoshonana. Claire akaniambia; Yasinta twende tukaangalie wanafanya nini? Basi tukaenda kuangalia wote mie na Claire, tulipofika, tukawakuta wanafanya ule mchezo unaofanywa na wanandoa (ngono). Tulishangaa sana na kuondoka, kumbe wao walikuwa si wagonjwa walitaka tu kukwepa masomo na kwenda kufanya ule uchafu. Yaani ilikuwa kinyume kabisa na mimi, na sikutarajia kama wanafunzi kwa umri ule tuliokuwa nao wangeweza kufanya yale tuliowakuta wakiyafanya.

Haya, tulipofika hospital kama kawaida kukaa foleni. Mara ikaja zamu yangu Claire Mputa akanishika mkono na kunisindikiza ndani ya chumba ambacho kilikuwa maalum kwa mambo ya vidonda. Nakumbuka yule daktari alikuwa mzee kidogo, aliitwa Kataulaki. Alinitisha alipochukua mkisu mkubwa nilifikiri anataka kuukata mguu wangu. Lakini hakufanya hivyo alinitibu na mimi na Claire Mputa tukarudi tena shuleni.

Kikubwa ninachotaka kusema hapa ni kwamba kama Claire asingenishauri kwenda hospitali basi leo hii nisingekuwa na mguu wa kushoto. Na pia nisingeyaona yale nilioyaona kule miembeni, kwani yalinifunza kwa kiasi fulani. Napenda kuchukuwa nafasi hii kuwashukuru rafiki yangu Claire Mputa na pia yule Daktari Kataulaki
Napenda kuwaambia ahsanteni sana.

Monday, July 13, 2009

JE? UNAJUA HII PICHA UMEPIGWA WAKATI NIPO WAPI AU UNAONA NINI?

FUMBO UFUMBIWA MJINGA

...mtani si yana mwisho haya alijisemeaga Kuli?
Aaah wapi, mwisho wake lini mbona...
A-a-, mtani sikiza nikwambie, kwetu tumezaliwa ndugu kaka na dada, na kwa bahati, mzee wetu alikuwa na shamba lenye mali mingi, mifugo hene hene na ardhi yenye tuvimawe tudogo tudogo na thijakwambia tena tune visima vyenye maji chumvi na maji poa. Asa siku moja kadogo kangu 'Nkiki Iki' katundu sana hako, kakawa kanachimbua vijiwe na kwenda kuchezea mabento na watoto wa jirani zetu. Mzee 'Miiwi Alewode Soni', babake mtoto wa jirani, akaviona vile vijiwe, basi akamwambia Nkiki 'uwe unavichimbua na kuvileta muchezee halafu atakayemmanga mwenzie mi ntambadilishia nimpe gololi'. Ikawa ndo mchezo wao. Sa kumbe Mzee wetu akamstukia Nkiki ndo akamkamata Nkiki na siye wote akatuketisha chini akatwambia 'iwe marufuku kuchimbua vijiwe vile. Wakati wake bado na aliviacha kwa makusudi'. Ndiposa akatupa siri kuwa tule tivijiwe bwana kumbe mzee Miiwi (babake na mtoto wa jirani) alikuwa akivifanyia biashara Ng'ambo. Mzee akatwambia kuwa tule tujiwe tofauti na mazao ya nafaka, huwa hatuozi tule, hivyo hutwo utatufwaa sana kwa biashara tukishakuwa na akili mukichwa na ikiwa shughuli za mifugo ama nafaka itakuwa haikidhi mahataji yetu. Zaidi sana alitaka tujue jinsi ya kushirikishana na wadogo zetu na familia yetu yote ya baba mkubwa, mamdogo na shangazi hadi kijiji kiuzima tuviuze ili wote tuwe angalao na ubora fulani wa maisha. Aliamini hivyo kwa dhati marehemu Mzee wetu.

Mzee alituhenyesha kwenye elimu na akahakikisha tunasoma kweli kweli, yaani hata na wazee wenzie kijijini alihakikisha wanapelekwa shule kwa mwendo wa PUGU (Pata Ujuzi Gawia Umma). Lakini alitusisitizia pia kuwa elimu izingatie kilimo, mifugo, uvuvi na viwanda ghafi kwa sababu bado ni mali sana hivo, na vile vijiwe vibakie tu maana haviozagi hivo.

Kwa bahati nzuri ama mbaya, Mzee wetu aliugua na akafariki katika umri wa KiBiblia kama alivyojikadiria mwenyewe, sasa kumbe kaka zangu na dada zangu walikuwa wanamwonaga Mzee wetu mwanga na kauzibe flani katika mipango yao. Unaambiwa ile Mzee anakata roho tu, kwanza wao wakaanza na kuandaa zinga la sherehe kisha wakasherehekea kivyao kwa siri, alafu ndo wakaandaa bonge la mazishi na kwenye maziko wakihakikisha wanaweka sementi na kofuli kwenye kaburi la Mzee ili asijenyanyuka; si walijua fika kuwa makamuzi waliyopanga kuyafanya yanaweza kumwamsha Mzee kutoka ufuni?

Sasa mtani wewe ikiwa umeshawakalisha kaka zako na ndugu zako chini na ukawaita Wazee ili mzungumze kuhusu dhuluma wanazokufanyieni ninyi ndugu zao wa kuzaliwa damu moja wachilia mbali wale watoto wa shangazi, mjomba na kijijini, na Wazee waliokua na Mzee wetu hawasikiii, eeeh, yaani woooote ninyi mmegeuka kuwa ombaomba na hamjui kesho itakuwaje, eeeh, kaka zako na dada zako baada kusomeshwa na Mzee na kuachiwa urithi wamegeuka kuwa watoto wa mjini yaani siku hizi wao wanavaa kata-k, pullneck wananunua vitu supamarkiti, vekesheni udosini, watoto wao hawasomi tena Kamachumu, ninyi wadogo zao shule hamuioni na kama Mzee aliwaacha ndo mpo Sekondari mjue Chuo Kikuu mtaishia kukisikia tu, na kama mna watoto ndiyo hata haijulikani mliwazaa kwa sababu ipi, we unafikiri we uta...

..kwanza zamani si Mzee alikuwa anasema ni marufuku kufunga milango ya vyumba vyenu kwa kuwa sisi sote ni ndugu siri ya nini? Basi alipoitwa na Mungu tu, kaka zako na dada zako wamevuruga utaratibu siku hizi hata kupita korido ya nyumbani kwenu ni kwa mahesabu maana ukikaribia mlango tu ni kula mbata kwa kwenda mbele. Yaani umewekewa kauzibe huwezi kukaribia hata kizingiti cha chumbani labda uwe na cheti maalum! Cheti maalum cha kumwona kaka yako au dada yako tena kwa ruhusa maalum kutoka kwa Sektretari wake ambaye ni kutoka kijiji cha jirani. Kuingia chumbani kwao tena kama ilivyokuwa zamani kabla Mzee hajafariki ni ndoto tena macho yako uyageuzie kule mbali kila unapopita kuelekea kibarazani.

Sasa mtani, kweli kwa hali hiyo wewe utaendelea kuwa wa kawaida? Uvumilivu huo uwe labda umetunukiwa na Mwenyezi Mungu lakini kama ni mtu wa kawaida kabisa kabisa kama mdogo wangu mwingine 'Ote Kilemie Mnu' aliyefikwa na maji ya shingo, walahi nakuhakikishia akikujia nanihii akakwambia hii ishu ndogo sana kwangu naweza kuwasubiri kaka zako na dada zako siku moja wamekutana pale kwao kama kawaida yao WaChagga kuhiji kila Krismasi basi nasubiri wakitoka Kanisani wameshakula, wakati wanaendelea na mbege zao wakiteremshia na ndafu mi nawatumia salam kupitia vijana wangu, mtani we hapo utawaza mara mbili wewe?

We acha wewe mtani wangu! Mi nlivyowaza kuhusu maswahibu yangu basi ndiyo sababu iliyonifanya niwaze kununua bastola japo sijui kitako na kichwa vinatofautianaje. Ni mengi yamenichosha. We fikiria mtu unaposhindwa kutofautisha kati ya raha na karaha aisee, we unafikiri...

...ebu kwanza subiri kidogo kuna mdundiko unapita hapa sijui mtoto wa nani wanamcheza leo, hizi ni raha ndogo ndogo mtu huwezi kuziacha zipite hivi hivi. Yana mwisho haya! Na pia napenda kusema asante Da Subi kwa mada hii.

Sunday, July 12, 2009

NAPENDA KUMPA HONGERA KWA SIKU YA KUZALIWA KAKA YANGU


Huyo ni kaka yangu mkubwa yaani wa kwanza kunyonya yeye ziwa na kuniachia mimi.Hongera sana kaka kwa siku yako ya kuzaliwa.

SALA YA MUME AKIMWOMBEA MKEWE

Hapa nimejaribu kubadili maneno kutoka kwenye ila sala ya kumwombea mke au niseme ni kama mfano vipi mume anaweza kumwombea mke wake.


Ee Bwana, wakati mwingine namtazama mke wangu Nami nashangazwa.
Inakuwa kama ni kwa bahati tu nilikutana naye.Siku ile ya kwanza,
Tulikutana na kila mmoja alikuwa mgeni kwa mwenzake.Sasa ninamjua sana.
Lakini bado ninashangaa na kujiuliza.Bila yeye ningekuwa mtu wa namna gani?
Ningefanya nini?

Je? Ningekuwa nimefanya mambo mengi hivyo?
Je? Ningekuwa bado nikitafuta?
Nikitafuta anasa mbaya za maisha, nikiondoa upweke na uchungu,
Kwa chupa moja ya bia baridi au kwa kumtembelea rafiki.

Ninajua kwamba nimebadilika, yeye alinibadilisha.
Upendo wake, na upole wake, kunitunza kwake, na subira yake,
Vimenifundisha na kunijenga.Amenifundisha niwe zaidi,
Niwe zaidi mtu yule uliyetaka niwe.Amenisaidia niwe hivyo
Mlifanya kazi pamoja, ulifanya kazi ndani yake
Naye katika wewe

Ninyi -wawili- Bwana,
Mlinipa moyo, mlinipa nguvu,
Mlinipa amani ya kweli, raha na furaha.
Mlinisaidia, nikajiamini.

Na nikakuamini.
Kwani, Ee Yesu mpendwa, ulikuwa mgeni.
Picha kwenye kitabu, Mtu aliye angani mbali nami.
Mpaka nilipokutana naye.

Kwani alinionyesha nafsi yangu mwenyewe. Na alinionyesha wewe.
Alinipa watoto, watoto wako Ee Bwana. Sasa ni watoto wetu

Hali hii tuliyo nayo leo hii, ni dalili ya upendo wako,
Ninakushukuru kwa ajili yake,umbariki na unlinde.
Umweke salama, na unifundishe jinsi ya kumpenda zaidi.


NAPENDA KUWATAKIENI WOTE JUMAPILI NJEMA

Saturday, July 11, 2009

Friday, July 10, 2009

KWA NINI WANAUME/AKINA BABA WENGI WANAFIKIRI WAO NDIO WAAMUZI/WAFALME WA NYUMBA?

Suala hili limekuwa likinikera sana akilini mwangu kwa miaka mingi. Ya kwamba akina baba/wanaume wao wanafikiri kazi yao kubwa katika nyumba ni kuwa MUME/BABA basi. Mara nyingi utasikia wanasema mimi ndio mkubwa wa nyumba. Na kama wanafanya kazi za ofisini basi ndo itakuwa kero mno. Kwani hapa atataka anaporudi toka kazini akute chakula mezani, maji ya kuoga bafuni tena ya moto, nguo zimepigwa pasi n.k. Na kinyume kama hana kazi basi atakuwa anashinda kilabuni(UGIMBI) na akirudi toka huko basi ni kelele tu, hakuna amani wala maelewano

Bado naendelea, kuna wengine wanaona kupika, kulea watoto, kutafuta chakula ni kazi ya wanawake. Yaani hawawezi hata kujipikia chai kwa vile wao ni wanaume au hata kumbadili mtoto nepi, Mtoto amabaye ni wake. Kikubwa wanachofanya ni kukaa kitini/sofani na kuletewa kile wanachotaka. Wanasahau kabisha jambo la USAWA.

Bado wanaishi dunia ya mababu, mababu na mababuzi. Tuache UBINAFSI tuishi kwa kushirikiana/kusaidiana kwani wote ni SAWA. Nasema tena tuishi kwa kusaidiana hapo wote tutafurahia maisha. Tuache mambo ya UTUMWA.

Thursday, July 9, 2009

JE UNATAFUTA FURAHA? SOMA HAPA

Picha na makala kutoka kwa kaka Shaban KaluseNatafuta furaha!


Wengi wetu hatuna furaha kabisa kwenye maisha yetu,
Hakuna kati yetu aneyejua ni kwa nini hatuna furaha. Nasema hakuna kati yetu , sisi ambao hatuna furaha kwa sababau, kama tungekuwa tunajuwa tusingeendea kubaki bila furaha.
Hatuna furaha kwa sababu hatujui kwamba furaha haiko huko nje kwenye vitu tuvionavyo na kuvisikia, bali tunayo wenyewe ndani mwetu. Ni suala la sisi kuamua kuichukuwa furaha hiyo pale tunapoweza na kuitumia.

Binadamu anatakiwa kuwa na furaha wakati wote, kwa sababu anayo mwenyewe furaha hiyo.
Ningependa kukuambia kwamba, kama kweli unapenda furaha, basi usijaribu kuthibiti hali halisi.

Hivi sasa nikiangalia, naona watu wengi wasio na furaha ni wale wanojaribu kushindana na hali halisi. Mawazo yao iwe wanajua au hawajui huwaambia kwamba wanaweza kuthibiti hali halisi.
Ukweli ni kwamba haiwezekani, hakuna anayeweza kudhibiti au kubadili hali halisi.
Kama mazingira yanabadilika na huwezi kuyadhibiti, unachotakiwa kufanya ni kukubaliana nayo, kukubali kusogea nayo pamoja, hiyo ndiyo siri ya kuyamudu, bila ya kujali yako kwenye sura gani.

Kujaribu kudhibiti jambo au kitu ambacho hatukiwezi, ni kujiumiza kiakili , kihisia na kimwili pia, ni kujinyima furaha.
Jambo muhimu zaidi ni mtu kujua kwamba, anachoweza kukidhibiti au kukibadili ni yeye mwenyewe, siyo kingine chochote kilicho nje yake.
Kuna kitu kimoja tu, ambacho mtu anaweza kukidhibiti hapa duniani, nacho ni yeye mwenyewe.
Huwezi kudhibiti hali ya hewa, hivyo kuumia mvua inaponyesha na biashara yako kushindwa kuuzika ni kuzidi kujiumiza bure.

Huwezi kudhibiti watoto, mkeo au mumeo, hivyo kukerwa na mambo yao ni kujiumiza zaidi tu.
Nje ya imani zako, mawazo yako, mitazamo na matendo yako, hakuna kingine unachoweza kukidhibiti.
Jaribu kujifunza namna utakavyoweza kudhibiti imani, mawazo, mitazamo na matendo yako ili visikupe maumivu.

Vile vyote vilivyo nje yako ambavyo huna uwezo wa kuvidhibiti, viache vitokee , visikusumbue. Ukimudu kufanya hivyo, hakika utaanza kuhisi tofauti.
Halafu fanya uamuzi kuhusu kile unachokitaka maishani mwako, kisha ung’ang’anie hapo. Ni vema mtu kuishi akiwa anajua anataka kitu gani hasa, anataka maisha yake yawe vipi hasa, kwani kubahatisha maisha huondoa sana furaha ya mtu. Bila kujua twendako maisha ni vurugu tupu.

Ni vema kuchagua kile ambacho mtu anpenda kukifanya bila kutoka nje.
Kumbuka kwamba mara nyingi hatuna furaha kwa sabau hatujawahi kuwafanya wengine wafurahi.

Tukishwafanya wengine wafurahi ni wazi na sisi tutakuwa kwenye furaha kubwa kuliko wao.
Ukitaka kuwa na furaha unapaswa kuwa na marafiki wenye kutia moyo na kufikiri kwa mkabala mzuri. Watu ambao wanaaminika na wenye hekima na busara wanapokuwa karibu na wewe, hakuna kitu chenye kufurahisha kama hicho.

Kuna mambo kama uimara wa ndoa au uhusiano na mpenzi. Kama unataka kuwa na furaha ya kwelini lazima uhakikishe kwamba umejitahidi na kujenga uhusiano mzuri na mke, mume au mpenzi wako. Juhudi hizi kwa sehemu kubwa ni lazima zitokane na wewe kumkubali mwenzio kama alivyo ili uweze kusaidiana naye karibu kwa kadiri inavowezekana.

Kuna mengi ambayo yanaweza kumsaidia mtu kuwana furaha ya kweli maishani, lakini yote hayo yanategemea mtu anvyojiona mwenyewe na alivyo tayari kukubaliana na yanayomtokea kila sekunde, dakika , saa na maisha yake yote.
Furaha ipo, ni suala la mtu kuichukuwa na kuitumia.

Tuesday, July 7, 2009

SALAMU KUTOKA SWEDEN KWENDA MATETEREKA

Leo napenda kumwiga Mzee wa Changamoto kwa kutoa pongezi kwa watu muhimu walioniwezesha. Miaka 10 iliyopita nilikuwa nimeanza kufanya kazi katika Sec. School ya Wilima iliyoko katika kijiji cha Matetereka tarafa ya Madaba. Nilipokuwa kule nilikuwa naishi katika familia ya mzee Mayemba. Katika picha ni Mzee ("baba") Lukas Mayemba na mkewe mama Emelensiana. Nawashukuruni sana mlinilea kama binti yenu na nimejifunza mengi sana kwenu. Hawa ndio walikuwa baba na mama yangu kipindi naishi Matetereka. Nawatakieni maisha mema.

Monday, July 6, 2009

YEBOYEBO: USAFIRI WA PIKIPIKI ULIOGEUKA KICHAKA CHA UBAKAJI RUVUMA

Ilitoka katika gazeti la mwanchi
Nimeona si vibaya kama wote tukijua yanayotokea mkoani Ruvuma.

Tatizo la wanawake kubakwa mkoani Ruvuma limekuwa likiongezeka siku hadi siku na kuwafanya wanawake wengi kuishi kwa woga.
Watuhumiwa wakubwa wa vitendo hivi ni madereva wa pikipiki ambao wanafahamika kwa jina la Yeboyebo ingawa pia wamo wanaume wengine katika makala haya Mwandishi Wetu Joyce Joliga anaeleza athari za tatizo hilo.
HUDUMA ya usafiri wa pikipiki ambayo inajulikana kama Yeboyebo mkoani Ruvuma umekuwa na msaada mkubwa kwa wakazi wake. Hawalazimiki tena kutumia fedha nyingi au kutembea kwa miguu mwendo mrefu wala kusongamana katika mabasi ambayo hayakuwa na uhakika.
Si hayo tu, vijana wengi ambao walikuwa wakizurura ovyo na wengine kujiingiza katika vitendo vya uhalifu wamebadilika kwani wamepata ajira na hivi sasa wanaendesha maisha yao kutokana na kazi hiyo ya kuendesha pikipiki.
Hata hivyo, kama wahenga wasemavyo, kila masika yana mbu wake, usafiri huu umesababisha madhara kadhaa. Hayo ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya ajali. Wananchi kadhaa wamepoteza maisha na wengine kupata ulemavu wa maisha kutokana na ajali zilizosababishwa na pikipiki hizi.
Chanzo kikubwa cha ajali hizi ni uendeshaji usiozingatia sheria ikiwa ni pamoja na vijana wengi kutokuwa na ujuzi wa kutosha kwani wengi hawakusomea na badala yake wamekuwa wakijifunza kienyeji tu.
Lakini tatizo kubwa jingine ambalo limesababishwa na kuwepo kwa aina hii mpya ya usafiri mkoani Ruvuma ni kuongezeka kwa matukio ya ubakaji ambayo yamechangia pia ongezeko la maambukizo ya ukimwi, magonjwa ya zinaa, mimba zisizotarajiwa na mauaji.
Waathirika wakubwa wa vitendo hivi ni wanawake hasa wale wanaofanya kazi hadi usiku hivyo kuhitaji usafiri huo kuwarejesha makwao au wanaokwenda katika starehe na harusi.
Pamoja na vitendo hivi kutokea mara kwa mara, vinavyoripotiwa ni vichache mno. Ni wanawake wachache ambao wamekuwa wakithubutu kutoa taarifa katika vituo vya polisi wanapofanyiwa ukatili huo sababu ikiwa ni hofu ya kudharauliwa, kuchekwa au kutengwa na jamii.
Kamanda wa Polisi Mkoa Ruvuma, Michael Kamuhanda anasema kuwa idadi ya wanawake waliobakwa na kuripotiwa mwaka jana ni 298 na Wilaya ya Songea ndiyo iliyoongoza kwa kuwa na idadi ya wanawake wengi waliobakwa ikifuatiwa na Mbinga na Namtumbo.
"Tatizo la ubakaji bado ni kubwa mkoani kwetu. Kwa mfano, Januari mwaka huu wanawake 24 walibakwa. Februari wanawake 25 na Machi walikuwa 37 na hadi kufikia April 3, tayari wanawake watano walikuwa wamebakwa hivyo kufanya jumla ya wanawake waliobakwa mkoani wetu tangu Januari hadi Aprili 3, kufikia 91," anasema Kamuhanda.
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Ruvuma, Baptista Mhelela anasema kuwa mwaka 2008, kesi 39 zilifunguliwa na kati ya hizo, 20 zilisikilizwa na watu nane walihukumiwa vifungo baada ya kupatikana na hatia za kutenda kosa hilo na kesi 19 zinaendelea kusikilizwa.
Anasema mwaka huu kesi 14 zimefunguliwa hivyo kufanya kesi zilizopo katika mahakama hadi sasa kufikia 28.
Mbali ya kubakwa, wanawake wengi wamekuwa wakiporwa mali zao kama fedha, simu za mikononi na vitu mbalimbali vya thamani. Pia wamekuwa wakipigwa na hata kutelekezwa porini au njiani kabla ya kufikishwa waendako.
Kutokana na adha hiyo, wapo wanawake walioamua kuyakimbia maeneo waliyokuwa wakiishi kuepuka aibu lakini wapo walioamua kujiua kutokana na msongo wa mawazo.
Wanawake waliohojiwa wanakiri kufanyiwa vitendo hivyo lakini wamekuwa waoga kutoa taarifa hizo katika vyombo vya dola kwani wengi wao ni wachumba au wake za watu hivyo kuhofia kuachwa.
Halima Rashid (26) anasema alibakwa na mmoja wa madereva wa pikipiki hizo hadi kupata ujauzito. Hamjui baba wa mtoto wake hadi leo na anasimulia kwamba mara baada ya kugundua kwamba amepata ujauzito, alifikiri kutoa mimba hiyo lakini aliogopa baada ya kuelezwa kuwa angepoteza maisha... "Nililazimika kulea mimba hiyo kwa shida huku watu wakinicheka na kuninyanyapaa."
Anasema pamoja na adha hiyo ya kuchekwa hakukata tamaa, aliendelea kufanya vibarua vya kusaidia kuuza chakula kwa mamalishe hadi alipojifungua.
Lakini anasema alilazimika kuondoka eneo alilokuwa anaishi awali la Minazini, Namtumbo baada ya kuchoshwa na kebehi za majirani na baadhi ya ndugu zake na kwenda kuishi Songea ambako anaendesha maisha yake kwa kuuza baa na huku akimlea mwanae wa kiume ambaye sasa ana umri wa mika miwili.
“Sikutoa taarifa popote baada ya kubakwa. Mama yangu alitaka nifanye kuwa ni siri, tulikubaliana nisiende kuripoti polisi kwani mtu aliyenibaka nilikuwa simjui ingawa alinibeba kwenye pikipiki.”
"Nilimlipa Sh2,000 lakini bado alinitupa chini na kuniingilia kwa nguvu, niliumia kwani nilichanika vibaya na baada ya mwezi kupita niligundua kuwa nimenasa ujauzito nikamweleza mama akanitahadharisha nitunze kiumbe hicho kwani ningetoa ningeweza kupoteza maisha. Ingawa niliumia sana moyoni nilikubaliana na ushauri wa mama yangu nikakubali kulea tumbo hadi sasa nimefanikiwa kupata mtoto,' anasema Halima
Mhudumu wa Baa ya Mtini Pub, Oliver Lwambano anasema rafiki yake ambaye hata hivyo, hataki kumtaja jina amewahi kubakwa na dereva wa Yeboyebo baada ya kudaiwa kwamba hakulipa nauli.
Anasema licha ya kufanyiwa unyama huo, mwanamke huyo aliogopa kutoa taarifa polisi na kubaki nyumbani akijiuguza baada ya kuambukizwa ugonjwa wa zinaa.
Kamanda Kamuhanda anawatoa hofu wanawake wanaoogopa kutoa taarifa hizo akisema kwamba ofisi yake imeanzisha kitengo maalumu cha polisi wanawake ambacho kinashughulikia matatizo hayo kwa usiri mkubwa.
Anasema kuna viongozi wanawake ambao kazi yao katika kitengo hicho ni kusikiliza siri za wanawake ambao wamebakwa na kuchukua hatua.
Madereva wa pikipiki hizo wanakiri kuwepo kwa vitendo hivyo, Shaban Kassim (39), anasema amewahi kusikia kwamba kuna wenzake ambao wamekuwa wakiwaingilia wateja wao wa kike kwa nguvu. Hata hivyo, anasema wanaofanya hivyo ni wahuni ambao wanajificha katika biashara ya kusafirisha abiria kwa pikipiki.
"Taarifa hizi zinatuumiza sana moyo hasa sisi ambao tunafanya biashara hii kwa lengo la kujipatia kipato cha kuendesha maisha yetu na familia zetu. Wanatuharibia biashara kwani wateja wengi ni wanawake nao wamekuwa wakituogopa na kutuita wabakaji lakini si wote ambao tunafanya vitendo hivyo," anasema Kassim na kushauri:
"Ilikupunguza tatizo hili ni vyema pikipiki zote ziwe na namba za usajili na za utambulisho, tena ziandikwe ubavuni ili kuzitambulisha kama zinavyoandikwa namba za magari, nafikiri hii itatusaidia kuwajua wabakaji ambao wanajificha katika biashara hii."
Anawashauri wateja kujenga tabia ya kukariri namba za pikipiki ikibidi kwa siri ili wanapofanyiwa ubaya wowote wajue jinsi ya kuwanasa wahalifu wao.
Dereva mwingine Zidadu Seleman (32), anasema baada ya kusikia tuhuma hizo zikielekezwa kwao aliwauliza wenzake ambao walikiri kuwepo kwa vitendo hivyo.
Anasema vitendo hivyo vya ubakaji vinatia doa biashara yao na kuwaweka wahusika katika hatari ya kuambukizwa magonjwa ya zinaa ukiwemo ukimwi.
Mwendesha pikipiki mwingine, Binaya Waliya (29) maarufu kwa jina la Suzuki Buzu anasema wanaofanya vitendo hivyo wanajulikana akiongeza kwamba baadhi yao pia ni wezi, na wanawanyanyasa wateja wao hasa kina mama.
Mkuu wa Wilaya ya Songea, Thomas Sabaya anasema tayari wameanza kudhibithi tatizo hilo na kwa kuanzia polisi inafanya doria usiku na mchana. Ili kuhakikisha kuwa ulinzi unaimarika, kila kata imepangiwa polisi wanne.
Sabaya amepanga kukutana na madereva wote wa Yeboyebo waliopo katika Wilaya ya Songea ili kuzungumza nao na kuwabaini wanaofanya vitendo hivyo ili washugulikiwe na vyombo vya dola.
Anawataka wanawake kuacha kutembea usiku wakiwa peke yao na badala yake watumie vyombo vya usafiri ambavyo ni salama kwa maisha yao.
Kwa upande mwingine, anawataka madereva Yeboyebo kuzingatia sheria ili kurudisha imani kwa wananchi kwa kuwafichua wenzao wanaowabaka wanawake ili kupunguza malalamiko kutoka katika jamii.

USAFIRI WA BAISKELI + MAISHA

Kujitegemea ni vizuri

Sunday, July 5, 2009

SALA YA MKE KUMWOMBEA MUMEWE

Nimeona si vibaya kama tukirudia hii sala tena na tena

Ee Bwana , ni ajabu,
Jinsi fikra zangu zinavyomrudia kila mara
Huyu, mume wangu,
Mwenzi anayeshiriki maisha yangu kwa namna ya pekee.
Ninapofagia nyumba na mazingira yake,
Nataka kutengeneza nyumba nzuri kwa ajili yake.
Ninapopika chakula vizuri,Napenda kumfurahisha.
Ninaponunua nguo mpya na kujaribu kuonekana mrembo,
Ni kwa ajili yake tena, Ee Bwana.

Na ninaweza kukuambia kwamba
Ninamwonea fahari,
Anafanya kazi kwa bidii ili kupata riziki yetu;
Ni mtu mwenye haki, mwadilifu,
Naye hujitahidi kutufurahisha.
Kwangu, yeye ni mpole na mwangalifu.
Hunijali na kuonyesha kweli kwamba anajali.
Hunifanya mimi nijiamini mwenyewe,
Anajua jinsi ya kuondoa hofu zangu,
Hunipatia usalama na upendo ambao nahitaji sana.

Ee Bwana, ninakuomba,
Umbariki na umlinde.
Katika safari zake, umfikishe salama.
Kazini mwake, umpe fanaka
Na hapa, nyumbani petu naomba apate amani na heri.

Bwana, unisaidie mimi pia
Niweze kuwa yule mke anayehitaji.
Unifanye niwe mtu anayeweza kumwamini daima,
Mwanamke ambaye anaweza kumfurahia,
Niweze kumsaidia asahau matatizo yake,
Niweze kuondolea mbali hofu zake na kupunguza uchungu wake.

Bwana, Wewe ndiwe uliyenipa mume huyu,
Na katika yeye,Umenipatia sehemu ya nafsi yako mwenyewe.
Ninakusifu kwa ajili yake, Ee Bwana.

Napenda kuwatakieni wote Jumapili Njema.

Saturday, July 4, 2009

TUFANYEJE ILI TURIDHISHANE KIMAPENZI?

Ilibainishwa humu hivi karibuni kuwa utafiti ulionyesha kuwa baadhi ya wanaume wana haraka ya kufanyamapenzi (sex). Habari ile bado inawafanya baadhi yenu kuendelea kunitumia mails zenye michango ya hoja na maswali pia.
Miye si mwalimu katika hili bali nimerejea dondoo za utafiti uliofanywa na wengine. Maana tunajifunza kutokana na uzoefu wetu na uzoefu wa wengine.
Hapa kuna swali; “Tufanyeje ili turidhishane kimapenzi?
Hatuhitaji watafiti ili kufahamu kuwa cha msingi na kikubwa kabisa ni MAWASILIANO kati ya wawili wapendano. Tumeona kuwa kufanya sex si kazi rahisi. Inahitaji muda, mwanamme anaweza akajisikia kuwa haridhiki na partner wake kwa vile partner hawi wa kwanza katika kuonyesha anataka na mengineyo.
Mwananme anaweza akahisi partner wake hampendi. Kama tulivyoona, mwanamke anahitaji muda zaidi ili awe tayari. Kushikana na mabusu yana umuhimu wake, lakini hata kumsaidia partner wako na kazi za nyumbani kunaongeza hamu ya mapenzi kwa patner wako.
Kama ni mwanamme, jaribu siku moja moja kushiriki kazi za nyumbani. Ni wajibu wako pia na inamsaidia mpenzio hata inapofikia wakati wa shughuli yenyewe. Hata kama ni baba nyumbani jitahidi basi kufagia, kuzoa takataka za nyumbani na kwenda kuzitupa pipani, it’s sexy too!
Ikumbukwe, kuridhishana ni kuridhiana. Na kikubwa ni MAWASILIANO. HABARI HII INATOKA http://www.kwanzajamii.com/ Asante kwa habari hii.

Friday, July 3, 2009