Thursday, April 28, 2011

YALE TUYAITAYO MABAYA NDIYO HUTUFUNZA HEKIMA!!!

Hatuwezi kujifunza kupitia mazuri bali tunayoita mabaya, tunayojifunza kwa kusikiliza si kuongea, tunakuwa wema kwa kutoa wema si kutendewa wema. Sisi ni zaidi ya mema na mabaya. Tunatakiwa kuimarisha msuli wa akili si msuli wa Mwili. Na ukweli ni kwamba hakikisha wema wako unashinda uovu.

Ujumbe huu nimetumiwa na Dada Frida Magari wa FAJI. Nami sikutaka nifaidike peke yangu nimeona ni vema niuweke hapa kibarazani ili wengi tufaidike pia kujifunza. Ahsante sana dada Frida.

Wednesday, April 27, 2011

HONGERA KWA SIKU YA KUZALIWA KWAKO DA´MIJA MWANAMKE WA SHOKA!!!


Napenda kukutakia siku yako ya kuzaliwa kheri na baraka tele. Mwenyezi Mungu na akulinde uwe salama pia uwe na afya njema siku zote. Na pia uwe bibi kizee ili uweze kucheza na wajukuu wako pia vijukuu. HONGERA SANA KWA SIKU YAKO HII TUKUFU KWA KUONGEZA LIMWAKA:-) UWE NA SIKU NZURI NA WALA USITHUBUTU KUTUNYIMA HIYO KEKI!!!
Zaidi unaweza kumwona mwanamke huyu wa shoka kwa kubonyeza Da´Mija.

Tuesday, April 26, 2011

KWA NINI IWE NI WANAUME TU WANAONUNUA MKUYATI?

Jamaa akinunua Mkuyati

Kuna wakati wanaume wanaweza kuwa na ugumu wa kujua kwamba wake au wapenzi wao hawaridhiki kimapenzi. Hiyo inatokana na uwelewa mdogo waliokuwa nao wanaume juu ya tofauti kubwa iliyopo kati ya wanawake na wanaume kuhusiana swala zima la hisia za kimapenzi.
Wanawake wana matarajio makubwa sana katika kila eneo linalohusu maisha yao, lakini linapokuja swala la tendo la ndoa mambo ni tofauti sana. Kwa kawaida wanawake wengi ambao hawaridhishwi na tendo la ndoa kwenye uhusiano wao huwa wanafanya siri.

Bila kujali kama tatizo liko kwao au kwa waume zao, wanawake hufanya siri kutoridhika kwao kimapenzi, na huweka siri kwa waume zao na hata kwa madaktari. Na ndio maana sishangai kuona kwamba wateja wa wauza dawa zinazohusiana na kuongeza hamu ya tendo la ndoa yaani Mkuyati ni wanaume.

Nilipokuwa nyumbani Tanzania, jijini Dar Es Salaamu nilishangaa sana kuona katika magazeti maarufu ya Udaku, {Tabloids} matangazo mengi ya biashara yanayotawala katika magazeti hayo ni ya kuuza dawa za kuongeza nguvu za kiume au hamu ya tendo la ndoa kwa wanaume na nyingine zilikuwa ni za kuongeza ukubwa wa maumbile ya kiume, dawa kama Mkuyati, Mzakaru, Super Shaft, Kifaru, Sekwa na nyingine chungu nzima ni maarufu sana jijini Dar Es Salaam.

Sio kwamba wanawake hawana matatizo ya tendo la ndoa, la hasha. Wanawake wanayo matatizo hayo ya tendo la ndoa lakini kwao hiyo siyo agenda, yaani si kitu cha kuwaumiza sana kichwa. Lakini kwa wanaume ni tofauti sana, wanapokuwa na tatizo la kukosa ufanisi katika tendo la ndoa huo utakuwa ni mgogoro mkubwa sana, kwani kwao hili ni jambo linalopewa kipaumbele kuliko mambo yote.

Kwa wanaume kukimbilia hospitalini au kwa mganga wa jadi na kusema “nina tatizo kubwa” ni jambo la kawaida kabisa…. Lakini wanawake hawafanyi hivyo, Badala ya kulifanya tatizo hili ni mgogoro halisi, huwekwa chini kabisa kwenye orodha ya matatizo yao, huwekwa kiporo na litashughulikiwa kwa wakati atakapojisikia kufanya hivyo kwa wakati wake.

Wanawake wanaweza kwenda kuomba ushauri au kuwasimulia mashoga zao, kuhusu matatizo ya ndoa. Lakini ni hadi wachokozwe ndipo wanapoweza kusema kwamba maisha yao ya tendo la ndoa na waume zao hayako sawasawa. Hilo halipewi uzito wa juu au naweza pia kusema hufanywa siri.

Wanawake hawaridhishwi na tendo la ndoa kwa sababu mbali mbali. Lakini bila kujali sababu hizo, kwao ni vigumu sana kusema kuhusu kutoridhishwa kwao. Ukiona mwanamke anatangaza sana kuhusu kutoridhishwa kwake na tendo la ndoa, basi ujue huyo na mumewe wako kwenye uhusiano mbaya sana. Kwani atakuwa anatumia maelezo ya kutoridhika kwake kama adhabu ya kumkomoa mumewe kwa kumuaibisha.

Lakini wale walioko kwenye ndoa imara ni vigumu kuwasikia wakilalamika kwamba hawaridhiki na tendo la ndoa. Inawezekana kutoridhika kwake kunatokana na yeye mwenyewe, yaani labda hana hamu au hafiki kileleni kutokana na matatizo mbali mbali yakiwemo ya kisaikolojia au matumizi ya baadhi ya njia za uzazi wa mpango, lakini bado sehemu kubwa wanaume huchangia. Hata hivyo pamoja na sababu hizo, mwanamke hayuko tayari kusema kuhusu kutoridhika kwake.

Kushindwa huko kunatokana na jinsi jamii ilivyomfunga mwanamke, kutoonesha kuhitaji tendo la ndoa. Akionesha kutoridhika na tendo la ndoa huonekana ni Malaya, kwa hiyo hukaa kimya na kuonesha kutojali.

Lakini bila shaka nadhani umefika muda wa wanawake kuwa huru kuhusu tendo la ndoa na kusema hisia zao wazi wazi bila kuogopa jamii itawaonaje, kwani jamii imekandamiza haki yao ya kuzungumzia tendo la ndoa kwa muda mrefu sasa.

Wanaume nao wanapaswa kujua kwamba wanawake hawapendi au hawawezi kuzungumzia kutoridhishwa kwao na tendo la ndoa, hivyo kutosema kwao kusitafsiriwe kuwa ndio wanawaridhisha, ni vyema kutoa ushirikiano kwa wake au wapenzi wao na kutafuta kujua kama wanawaridhisha. Ni jambo la busara kama mwanaume atadadisi kwa upendo na lugha ya upendo na kuonesha kama yuko tayari kutoa ushirikiano pale ambapo mke au mpenzi ataonesha kutoridhishwa na tendo la ndoa.

Mada hii nilikwisha wahi kuiweka hapa kibaraza , nimevutiwa nayo tena nikaona sio vibaya kuirejea ili kujikumbusha. Kama nisemavyo kila wakati kurudia kusoma kitu ndio kujifunza mengi.

Sunday, April 24, 2011

KHERI KWA SIKUKUU YA PASAKA KWA WOTE!!


BWANA AMEFUFUKA NA WOTE TUFURAHI LEO....KHERI SANA KWA PASAKA!!!

Saturday, April 23, 2011

KUMBUKUMBU:- LEO UMEFIKA MWEZI MMOJA TANGU ASIFIWE WETU ATUTOKE!!

Leo imetimia mwezi mmoja tangu Asifiwe wetu atutoke!


Ilikuwa tarehe 23/3/2011 mpendwa wetu Asifiwe alitutoka ghafla. Leo tarehe 23/4/2011 imetimia mwezi mmoja tangu atutoke. Familia ya Mzee Ngonyani ipo katika harakati za kufanya arobaini(thelathini) ambayo itafanyika Nyumbani Ruhuwiko-Songea 30/4/2011. Mwenyezi Mungu ailaze roho ya mpendwa wetu Asifiwe mahali pema peponi amina.

Hapa china nilitumiwa barua pepa na kaka Raymond Mkandawile ujumbe huu ufuatao. Nami nimeupenda ni ujumbe mzuri na nimeona ni vizuri niuambatanishe hapa. Ahsante sana.Ujumbe wenyewe ni huu :-
Duania tu wapitaji na hakuna ajuaye siku yake ni lini. Hivyo hatuna budi kujiandaa na kuwa tayari kila itwapo leo.Dada yetu Asifiwe pumzika kwa amani na sisi pia tunafuta....bwana alitoa na yeye ametwaa jina lake libarikiwe.
Si vibaya kama tukisikiliza na nyimbo hizi ambazo Asifiwe alikuwa akisikiliza sana....

HALAFU HUU PIA ALIUPENDA PIA....

WOTE TWAJUA UMETUACHA KIMWILI LAKINI KIROHO UPO NASI NA TUTAKUKUMBUKA NA KUKUPENDA DAIMA!!!

Friday, April 22, 2011

IJUMAA KUU HII IWE NJEMA KWA WAUMINI WOTE!!Ni ijumaa ambayo Bwana Yesu Kristu atapata mateso kwa ajili yetu. Sijui kama kuna mtu angeweza kujitoa roho yake kwa ajili ya mwingine kama Bwana wetu Yesu anavyofanya kwa ajili yetu?..Na nawaombeni usisahau leo ni ile siku ambayo ni siku moja tu kwa mwaka ambayo tunaombwa kuacha kula vyakula vya damudamu hasa nyama ....Mwenyezi
ungu na atawala Nyumbani mwenu. Amina. IJUMAA KUU IWE NJEMA KWA WOTE....

Thursday, April 21, 2011

HESHIMA KWA WANAWAKE

Kweli huu uungwana?


Acheni niwape heshima iliyotukuka wanawake woote;
IMAGINE:

ANAKUFUMANIA: Analia, ananyamaza, anasononeka, unambembeleza anakuelewa
anakusamehe halafu anasahau!!!

UNAZAA NJE YA NDOA: Anasononeka na kulia sana. Anakuchukia lakini baadaye
anakusamehe. Halafu analea mtoto uliyemzaa nje kwa upendo. Kama ni
kuchukiwa atachukiwa mtoto, si wewe uliyefanya umalaya!

UNARUDI USIKU WA MANANE UKIWA MTUNGI: Anakukaribisha, anakuandalia
chakula, unagoma kula. Anahifadhi chakula alichokuandalia bila
manung'uniko.

UNAAMKA ASUBUHI NA MAHANGOVER: Anakuandalia staftahi (saa nyingine unagoma
kutumia staftahi yake unakimbilia baa kwenda kunywa Supu na kuzimua. Wala
halalamiki!

CHAKULA CHA USIKU: Ushapiga mtungi wako, unataka huduma. Unamrukia, hamna
maandalizi unamuumiza. Anavumilia ili akuridhishe. Na kesho yake tena
inaweza tokea hii; hana kinyongo!

UNAJIANDAA KWENDA KIBARUANI: Unakuta kashakuandalia viwalo, suruwale
imenyooshwa kama ya askari trafiki, shati limepigwa pasi ya maana! Nguo
ulizovua jana zimeshalowekwa tayari kwa kufanyiwa usafi! Ulichomuudhi jana
kashasahau na kukusamehe!

UNAMPA UJAUZITO: Anauthamini, anautunza anajifungua kwa uchungu, mtoto
anakuachia wewe umpe jina, la kwake halimo kabisa kwenye majina
atakayotumia mtoto! Na pamoja na uchungu wa kuzaa, bado yuko radhi
kukuzalia mtoto mwingine na mwingine tena!

Na mengine meeeeengi sana wanafanyiwa hawa watu lakini WANASAMEHE,
WANAVUMILIA! Ni watu muhimu sana hawa watu maishani mwangu!

HIVI INGEKUWA WANAUME TUNAFANYIWA HIVI INGEKUWAJE?

Nimeipenda habari hii na nimeona niwahabarisha na wenzangu kwani elimu ni kuelimishana. habari hii imetoka Jamii Forum.

Wednesday, April 20, 2011

SASA HAPA SIJUI ITAKUWAJE?Kaaazi kweli kweli, sasa hapa nafasi itapatikanaje?

Kwa nini watu wanapima joto kwenye paji la uso??

Mtoto wa kike na kipimajoto mdomoni


Wakati Mwili unapovamiwa na wadudu (bakterie) au virus, kwa kawaida joto huwa linapanda. Hii ndiyo sababu joto la mwilini linaweza kusaidia kugundua kama mtu ni mgonjwa. Wengi watakapo kumpima mtu joto anapojisikia kuumwa wanaweka mkono kwenye paji la uso. Hii yote ni kwasababu tu paji la uso halivaliwi nguo.(Yaani lipo wazi tu na ni rahisi kupima joto kwa haraka)

Kwa vile joto haliwezi kupimwa sawasawa na mkono, kwa hiyo mbinu hii haitoshi. Hivi karibuni kumeanzishwa aina mpya checha za vipimajoto, ambavyo vitaweza kupima joto katika paji la uso. Katika utafiti inaonyesha kwamba joto la paji la uso linayumba na 1,5 C kutoka joto kamili la Mwili. Kwa maana hii njia hii sio nzuri.

Njia nzuri zaidi ni kupima joto makalioni. Pia sikioni au mdomoni. Lakini upungufu ni sawasawa. Ni muhimu/lazima kuongeza nusu C kwa kupata joto kamili.

Chanzo: Illustrerad Vetenskap nr 6/2011

Monday, April 18, 2011

WANAUME NA KAULI HIZI: 'HUYO SIO WA KUOA, NI WA KUCHEZEA TU'

Bila shaka wewe msomaji unayesoma hapa utakubaliana na mimi kuwa umeshawahi kuzisikia kauli hizi kutoka kwa wanaume pale anapozungumziwa mwanamke mzuri kwa sura na umbo.

Kwa kawaida vipimo vya uzuri wa mwanamke kwa wanaume vimegawanyika. Wanaume wengi hupima uzuri wa mwanamke kwa sura au umbo, lakini linapokuja swala la kuoa, suala la tabia na mwenendo hupewa nafasi kubwa.

Na ndio maana wakati mwingine unaweza kushangaa kukuta mwanaume ambaye ni hodari wa kuchagua wanawake wazuri, lakini ukija kumuona mke aliyemuoa, utakuta ni mbaya kwa sura na umbo, lakini kwa upande mwingine utakuta mke huyo ni mzuri katika maeneo mengine kama vile, tabia nzuri,upendo, wema, na anayemudu malezi ya watoto katika familia.

Sifa nyingine ni zile za kumkubali mwingine kirahisi, kuwa tayari kusaidia yanapojitokeza matatizo katika familia, mpenda amani na kumfanya mume wake aone kuwa hakukosea kumchagua yeye kuwa mke wake. Kwa kifupi wanawake wa aina hii hata kama wangekuwa ni wabaya kwa sura na umbo bado wako kwenye nafasi ya kuonekana kuwa ni wazuri, na huolewa kirahisi zaidi.

Wanawake wazuri kwa sura na umbo ambao tabia na mienendo yao hairidhishi wako kwenye nafasi kubwa ya kuishi bila kuolewa, na kwa bahati mbaya zaidi wanawake wengi wanaohesabika kuwa ni wazuri, tabia na mienendo yao ni ya kutilia mashaka. Wanaume wengi huvutiwa na wanawake hao kujenga uhusiano nao hasa wa kimwili tu na si vinginevyo, na ndio maana wanawake wazuri kwa sura na umbo wanalo soko kubwa sana kwa wanaume, lakini huishia kuchezewa zaidi kuliko kuolewa.

Wanaume nao kwa upande wao wamejenga dhana kwamba wanawake wazuri sana sio wa kuoa na hivyo kuwaogopa. Wanaamini kwamba wanawake wazuri sana ni wasumbufu, kitu ambacho kina ukweli kwa kiasi fulani. Wanaume wanaamini kwamba wanawake wazuri sana kwa sura na umbo huwasababishia waume zao maradhi ya moyo,shinikizo la damu na wakati mwingine hata kuwafanya kupata matatizo fulani ya kiakili, na hiyo inatokana na waume hao kuwa katika mashaka ya wake zao kuchukuliwa na wanaume wengine wakati wowote kutokana na uzuri wao. Hata hivyo wanawake wazuri nao huwaendesha waume zao wakijua kuwa ni wazuri na soko lao liko juu na waume zao nao huwanyenyekea wakihofia kuachwa.

Na ndio maana usishangae kuona kuwa wale wanawake ambao watu wamekuwa wakiamini kuwa ndio wabaya kwa sura au umbo lakini tabia na mienendo yao ni mizuri ndio wanaoolewa na hata ndoa zao zinadumu, tofauti na za wale wanaoonekana kuwa ni wazuri sana kwa sura na umbo na ambao tabia na mienendo yao si mizuri, ndoa zao hazina umri mrefu.

Sunday, April 17, 2011

PASAKA HIYOOO INAPIGA HODIIII:- LEO NI DOMINIKA YA MATAWI!!!

Na blog ya Maisha na Mafanikio inapenda kuwatakieni wote Dominika hii ya matawi upendo,furaha na amani. DOMINIKA NJEMA YA MATAWI KWA WOTE!!!!

Friday, April 15, 2011

IJUMAA YA LEO: HEBU FIKIRIA MILO YETU HII YA ASILI, WANAODHARAU VYAKULA KAMA HIVI HAO WANA HASARA HASWA!!!

Najaribu kufikiria naamka asubuhi. Naingia shambani kuchuma boga, nalichemsha na halafu tayari kwa Chakula cha asubuhi. Yaani boga kwa chai ya rangi. Kwa mimi chai yangu kama kawaida bila sukari hapo nitafaidi na kulamba mikono. Na mchana ni ugali, samaki, mboga majani kidogo, mchuzi, maharagwe kinywaji maji. Mmmm!! yam yam yam!!utamu jamani ...karibuni tujumuike basi.... Jioni naona tubadili mboga, tutakula KISAMVU ..yaani hapa mimate hadi inanidondoka si mchezo ..karibuni sana jamani tufaidi uhondo huu... Picha hizi kutoka kwa kaka Mjengwa . IJUMAA NJEMA WANDUGU!!!

Thursday, April 14, 2011

AJALI YA RESTIELI

Restieli.

Gari lao lililohusika na ajili hiyo.

Mama na baba Restieli.

Kama mnakumbuka niliwahi kuweka ushuhuda wa binti mmoja aitwae Restieli Moses Mbwambo akieleza kisa chake cha kuungua na mafuta akiwa mdogo (ukitaka kujikumbusha waweza kubofya hapa). Juzi nimepata taarifa kuwa familia ya binti huyo akiwemo mwenyewe Restieli, walipata ajali katika maeneo ya Lembeni mkoani Kilimanjaro.Ajali hiyo ilihusisha gari lao dogo aina ya Toyota RAV 4 waliyokuwa akisafiria kutoka Upareni kurejea Moshi hapo mnamo siku ya Jumanne ya tarehe 5/04/2011. Ajali hiyo ilitokea baada ya tairi la mbele la gari hilo kupasuka na hivyo kupinduka mara kadhaa. Habari nilizozipata ni kwamba wote walisalimika katika ajali hiyo isipokuwa walipata majeraha kadhaa mwilini ambapo walitibiwa na kuruhusiwa.Mleta habari amebainisha kwamba kutokana na ajali hiyo gari lao limeharibika vibaya, na ukiliangalia hutaamini kama waliokuwa ndani ya gari hilo wote wamepona.Blog ya Maisha na Mafanikio inapenda kuchukua nafasi hii kuwapa pole wote walionusurika katika ajali hiyo, na ninaamini Mungu ataendelea kuwalinda.

Wednesday, April 13, 2011

Tafakari ya leo:- Umpendaye ndiye?

Moyo wa mtu ni kichaka na watamanianao huonekana wengi bali wapendanao ni wachache na hawajulikani. Hebu fikiria leo Mungu akisema kila moja asimame na ampendaye Je? Wewe utasimama na nani? Na huyu umdhaniaye ukimkuta amesimama na ampendaye utafanyaje? Haaaaaa…..!! Unacheka?

Monday, April 11, 2011

MWENZENU NIMEGUNDUA KUWA!!!!!...............

Inasemekana kuwa kuna tofauti kati ya tembo wa Afrika na tembo wa India(Uhindi) hebu angalia tofauti zao na kufananakwake hapa chini:-


Tembo wa afrika wana masikio makubwa na pembe kubwa.Masikio yao yanafanana na Ramani yetu ya Afrika!!Tembo wa India wana masikio madogo na pembe ndogo.Pia masikio yao yanafanana na Ramani ya India .


Je Uligundua hili wewe pia??Sunday, April 10, 2011

NAPENDA KUWATAKIA WOTE JUMAPILI NJEMA KWA UJUMBE HUU

Macho ya huruma hufurahisha moyo, habari huburudisha mwili. Kuchukiana huendekeza fitina, kupendana husitiri makosa yote. Nilikuwa mgonjwa ukaja kuniona .Nilikuwa na njaa ukanilisha. Kumhudumia mgonjwa ni wito. Jumapili njema jamani:-) ngoja tusikilize wimbo huu kuhusu Afrika yetu

.
Muwe salama wote na kumbukeni wote mnapendwa!!!

Saturday, April 9, 2011

Nimekumbuka enzi zangu? Je? Unaweza kugundua nimesimama wapi?

Natumai wakumbuka enzi hizi lakini waweza kunikumbusha mimi nimesimama wapi katika picha hii manake nilikuwepo teeeeh teeeeehhhh,...kaaazi kwelikweli

Friday, April 8, 2011

MAJINA YETU/LEO TUANGALIE MAJINA YA KISUKUMA!!!

Kuna wakati niliwahi kuandika kuhusu majina/vibongo vya wangoni. Kwa kujikumbusha zaidi au kwa wale waiowai kusoma basi ingia hapa .Utaona hayo majina na pia maoni ya watu. Na sasa leo katika upekuzi wangu nimekutana na majina ya wenzetu Wasukuma ebu angalia hapa napo, majina haya nimeyapata Jamii Foum.
Majina ya Kisukuma
1. Masanja Mawenge 2.N'kwabi N'gwanakilala 3.Rupondije Inuka 4.Mabula Nkwimba 5.Nyeunge Maneno 6.Budodi Nzobhe ya Siketi JidulamabambasiN'gwanangwa Masabhuda, Masumbuko, Wangaluke, Nchimika, Ng'wana Malundi, shindike Bunani Jidalu, Jidiku ikong'oro, Igunani Matanda, Isungangwanda Kidalu, 6: Sawaka Ng'wana gandila, Itendegu Jibinza, Shija, Mabura, Kasase, Nzungu, Midelo, Lufulo Ndama Nyangwaka Ndili, Lisolilo Ligasu, Kaswalala Buyonzi, Nyanzobe Mayunga, Ngw'ana Nh'wani, Jodoki Mpembele, Ngwizukulu jilala, nyanzala ng'wandu, mwanasabuni lushanga, manyilizu shiganga, kabadi madilisha, mashenene masagida, chenge saguda, pula kiheka, tabu lukelesha, ngasa ingombe, masanja malale, malila lushumbu, luhende mwanansale, Ngosha Magonya, Manyanza, Jongh'ela, Nkulukulu, Ngw'alali, Ngh'ungulu, Zanzui, Sanagu, Shushu. TUKUTANE TENA WAKATI MWINGINE!!!!!! IJUMAA NJEMA KWA WOTE!!!!

Thursday, April 7, 2011

Ujumbe toka kwa Nangonyani!!! Aka Kapulya Mdadisi!!

Maisha sio zile siku ambazo zimepita. Isipokuwa ni zile siku uzikumbukazo.
SIKU NJEMA KWA WOTE!!!!!

Tuesday, April 5, 2011

NIMEMKUMBUKA KWELI MDOGO WANGU ASIFIWE LEO

Yasinta na Asifiwe 2009 mwezi wa pili
Leo nimeamka nikimuwaza kweli mdogo wangu Asifiwe nusu nichukue simu na kumpigia ili tuchape hadithi zetu kama tulivyozoea. Nikawa nasikia kama vile ananiita dada, dada, nami nikawa namwita jina lake na mara nikakukumbuka shairi hili aliloandika mtani wangu Fadhy ukitaka kusoma mashairi yake zaidi basi ingia Fadhili ya diwani Shairi lenyewe linasema hivi:-
Pumzika kwa amani, Asifiwe Ngonyani

Asifiwe! Asifiwe! sauti zetu sikia,


Asifiwe! Asifiwe! kweli unatusikia?


Asifiwe! Asifiwe! mbona hujaitikia?


Asifiwe umekwenda, dunia 'meikimbia,


Wajua tulikupenda, ila Mungu kazidia,


Mauti yamekutenda, wewe umetangulia,


Pumzika kwa amani, Asifiwe Ngonyani.


Umetwachia majonzi, hakika twakulilia,


Tumejawa na simanzi, hatuwezi elezea,


Mdogo wetu mpenzi, uchungu 'metuachia,


Pumzika kwa amani, Asifiwe Ngonyani.


Ulijawa na adabu, nao ukarimu pia,


Kwa wako utaratibu, ni nuru imepotea,


Umekwenda kama bubu, kwa heri hukutwambia,


Pumzika kwa amani, Asifiwe Ngonyani.


Wewe mtu mwuungwana, kwa njema yako tabia,


Tulikupenda kwa sana, nd'o maana twaumia,


Mfano wako hakuna, kwa pengo kulizibia,


Pumzika kwa amani, Asifiwe Ngonyani.


Kuondoka kwatuliza, kila tukifikiria,


Twatamani tungeweza, kifo tungekizuia,


Mwaka huu kumaliza, nayo inayof'atia,


Pumzika kwa amani, Asifiwe Ngonyani.


Lakini sisi ni nani, Mungu tukamwamulia?


Tukamwuliza kwa nini, wewe amekuchukua?


Mwamuzi ndiye Manani, aloiumba dunia,


Pumzika kwa amani, Asifiwe Ngonyani.


Pengo halitozibika, wewe ulotuachia,


Daima 'takukumbuka, wema'wo kusimulia,


Tukimwomba Rabuka, mwanga kukuangazia,


Pumzika kwa amani, Asifiwe Ngonyani.


Upumzike salama, kwa Mola twakuombea,


Akupe pahala pema, nuru kukuangazia,


Asifiwe mtu mwema, buriani twakwambia,


Pumzika kwa amani, Asifiwe Ngonyani.


Shairi hili nimeliandika maalumu kwa marehemu Asifiwe Ngonyani, mdogo wa kike wa dada yetu, rafiki yetu na mwanablog mwenzetu Yasinta Ngonyani. Asifiwe alipatwa na mauti Jumatano 23.03.2011. Asifiwe umetuacha kimwili tu, kiroho tungali pamoja nawe. Tunakuombea pumziko salama la milele. Amina. AHSANTE SANA MTANI FADHY KWA SHAIRI HILI!!

Sunday, April 3, 2011

HEBU SIKILIZA HAPA JINSI WALIVYOJUA KUIGIZA...KAAZI KWELIKWELI


Muda mrefu nimekuwa mkimya bila kusikiliza miziki kwa ajiliya machungu yaliyonipata katika upekuzi wangu nimekutana nao hau kwa kweli wamenifanya nitabasamu kiduchu.. sijui nanyi wenzangu mtajiunga nami???

JUMAPILI YA LEO NATAKA KUWAOMBEE MAREHEMU WOTEEE KWA SALA HII!!!

Salam Maria, umejaa neema, Bwana yu nawe, umebarikiwa kuliko wanawake wote, na Yesu mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Maria Mtakatifu mama wa Mungu, utuombee sisi wakosefu sasa na saa ya kufa kwetu. Amina. JUMAPILI NJEMA KWA WOTE !!!!!!! pamoja daima bado najikokota ila nipo....

Friday, April 1, 2011

IJUMAA NA MWISHI WA JUMA MWEMA KWA KIBAO HIKI!!Nawatakieni wote MAPUMZIKO MEMA NA TUTAONANA TENA WAKATI MWINGINE!!!