Friday, July 29, 2016

NAPENDA KUWATAKIENI WOTE MWISHO MWEMA WA JUMA...IJUMMA NJEMA

NI MATUMAINI YANGU UTAKUWA NA MWISHO MZURI WA JUMA HILI PIA MWEZI...TUPENDANE NA TUTAKIANE HALI PALE  TUPATAPO WASAA...SALAMU NI NUSU YA KUONANA.....KAPULYA WENU.

Thursday, July 28, 2016

HILI NI CHAGUO LA BLOG YA MAISHA NA MAFANIKIO...PICHA YA WIKI

SONGEA,RUVUMA
Karibuni kwetu Songea  kuangalia mazingira,...  si unajua wangoni tulivyo wakarimu hutaangalia mazingira tu, tutacheza kitoto/lizombe, kula na kunywa pia. KARIBUNI.

Wednesday, July 27, 2016

Monday, July 25, 2016

NASIKITIKA SANA MWAKA HUU BUSTANI YETU HAISTAWI KAMA MIAKA MINGINE....

 ...Nimejaribu mara zaidi ya mara sita kupanda mbegu za mbogamboga kama nifanyavyo lakini zimenigomea. Nikaona labda nijaribu kupanda kwenye kopo nikafanikiwa ndo hili/ huu mmea wa boga muuonao:-(. Kwanza nilifikiri ardhi  imechoka nikaweka mbolea lakini wapi....

 Viazi mviringo afadhali vimekubali na kama muonavyo nitavuna karibuni maana majani yameanza kukauka pia....
 Nikajaribu na njegere ...aaahhh mama yangu nusu nilie ndo kama muonavyo sijui kama tutakula.   pia kumezuka konokono wanakula mimea yotr walayo binadamu kwa hiyo mie nikipanda ikijitokeza tu wao wanafyeka/kula tu....Inakatisha tamaa
Na mwisho nikaona nijaribu kutumia makopo/ndoo ili kuweza kupanda  na kuona kama itakuwaje matokeo  yake ni haya Nyanya,  pilipili, pilipili hoho na maua  na kuviweka kwenye varanda vimekubali. Lakini sasa nitakulaje viungo tu bila mboga na ugali?:-)
Naomba kwa yeyote mwenye ushauri anishauri la kufanya.... JUMATATU NJEMA!

Saturday, July 23, 2016

UNAKUMBUKA ULIVYOKUWA UKIZUNGUMZA KATI YAKO NA BABU AU BIBI YAKO? EBU JIKUMBUSHE HAPA MAONGEZI KATI YA BABU NA MJUKUU WAKE.....

MJUKUU; Eti Babu mwisho wa dunia tutalia na kusaga meno ? 
BABU; Ndio mjukuu wangu. 
MJUKUU; Sasa mbona wewe huna meno ?

BABU; Kuna malaika ameajiriwa na Mungu kutugawia meno siku ya Mwisho
PAMOJA DAIMA!

Thursday, July 21, 2016

KARIBUNI TUJUMUIKE CHAKULA NI CHAGUO LAKO.....

 Ugali wa mahindi na maharage
 Ugali, samaki wa kuoka na mchicha
au ndizi
Binafsi nachagua chakula hicho cha katikakati si mnajua mimi ni mnyasa/mngoni:-)

Tuesday, July 19, 2016

MSIONE KUSUASUA NIPO.....MNAJUA TENA MSIMU HUU NI LIKIZO KWA HIYO FAMILIA INABANA:-) ILA NIPO

Si mnaona hapa .....msifikiri nimekasirika ni uchovu tu ila muda si mrefu nitakuwa nimeondokana na uchovu. Nawatakieni wote mtakaopita hapa siku njema ....Kapulya wenu.

Friday, July 15, 2016

TUMALIZE WIKI HII KWA KUTEMBEA RUVUMA KWETU...KWA BURUDANI HII ..RUVUMA YETU NZURI


Wimbo una sema Ruvuma yetu ni nzuri karibu tule vyakula vyetu vya asili kama mlivyoona alivyoonyesha....Yaani leo nimeselebuka sana...Ruvuma yitu yabwina...Ruvuma yitu yabwina mwe jasho tu hapa....

Wednesday, July 13, 2016

TENDA WEMA KADRI UWEZAVYO BILA YA KUJALI HALI ULIYONAYO.


Nimetumiwa hii habari na msomaji wa Maisha na Mafanikio...nimeona niiweka hapa ili iwe Elimu kwa  wengi wetu ...Karibu  twende pamoja.....
Daktari aliingia hospitalini kwa haraka sana baada ya kuitwa kwa shughuli ya Upasuaji wa haraka, alipokea simu haraka, na kuvaa nguo za kazi na kuelekea moja kwa moja kwenye chumba cha upasuaji. Wakati akielekea kwenye chumba cha upasuaji alimkuta Baba wa mtoto anazunguka huku na huku karibu na chumba hicho akimsubiria Daktari.
Baada ya kumuona tu, Baba mtoto akapayuka: “ Kwanini umechelewa kuja? Hufahamu kama maisha ya Mtoto wangu yapo hatarini? Hivi unayajua majukumu yako? ”Yule Daktari alitabasamu na kumwambia: “ Samahani sana, Sikuwa Karibu na Hospitali na nimejitahidi kuja kwa haraka sana baada ya kupokea simu kutoka hapa hospitalini….. Na kwakuwa nimeshafika ningekuomba upunguze jazba na hasira ili nifanye shughuli yangu” “Punguza hasira?!
Hivi ingekuwaje kama Mwanao ndiye angekuwa chumba cha upasuaji sasa hivi, ungeweza kupunguza hasira? Kama mwanao ndiye angekuwa anakufa sasa hivi ungefanyaje?” Yule Baba aliongea kwa hasira sana. Yule Daktari alitabasamu tena na kumjibu: “Daktari hawezi kurefusha maisha ya Binadamu” Nenda katulie na umuombee mwanao, sisi tutajitahidi kadri kwa uwezo tulionao kwa Baraka za Mwenyezi Mungu.
“Kutoa Ushauri kwa vitu visivyo wahusu ni rahisi sana” Alinong’ona yule Baba mwenye mtoto. Upasuaji ulifanyika kwa masaa kadhaa mara tu baada ya kumalizika Daktari alitoka akiwa anafuraha, “Asante Mungu! Mtoto wako amepona!” Kama una swali lolote utamuuliza Nurse!!” Bila ya kumsubiri Baba Mwenye mtoto kujibu chochote aliondoka kwa haraka kwenye eneo la upasuaji.
“ Kwa nini ni mkorofi sana huyu Daktari? Yaani hawezi hata kusubiri kidogo nimuulize maendeleo ya mwanangu” Baba wa mtoto alimjadili akiwa na nurse baada ya Daktar kuondoka. Nurse akamjibu, huku akitokwa na machozi:
“Mtoto wake alifariki jana kwenye ajali ya gari, alikuwa katika mazishi ya mtoto wake wakati tunampigia simu aje Hospitali kwa ajili ya upasuaji wa mtoto wako. Amefanikiwa kuyaokoa maisha ya mtoto wako, kwahiyo ameondoka kuwahi mazishi ya mtoto wake.”
HEKIMA:1. “USIMHUKUMU MTU YEYOTE…. SABABU HUYAJUI MAISHA YAKE NA KIPI KILICHOMKUTA KWENYE MAISHA YAKE.
2. “TENDA WEMA KADRI UWEZAVYO BILAYA KUJALI HALI ULIYONAYO.

Tuesday, July 12, 2016

ILE NYUMBA YETU YA MBINGA HUU NDIO MWONEKANO WAKE KWA SASA

 Pole pole ni mwendo...tutafika tu
 ....na pia madanda  yapo maana  tusikusahau mifugo....
.....matunda pia kama tuonavyo ndizi na miembe....mengine yanapandwa ........
kwa leo tuishie hapa.... kukiwa na mabadiliko basi tutajuzane. Tumwombe Mungu atujalie afya.

Monday, July 11, 2016

MAISHA YETU: FAHAMU NJIA SAHIHI YA KUKOSOA ILI MTU ASICHUKIE

KAMA binadamu tulioumbwa na Mwenyezi Mungu kila mmoja wetu amekuwa na upungufu katika eneo fulani, hali inayofanya mtu mwingine kutoa kasoro. Sio mbaya kutoa kasoro hiyo ila kuna njia nzuri ya kumkosoa mtu ili asichukie.
Leo tutaangalia mifano mbalimbali katika maisha yetu tunayoweza kuitumia pale tunapotaka kumkosoa mtu yeyote aliyefanya jambo kwa makusudi au kwa kutokujua bila kumfanya ajisikie vibaya. Kwa kuanzia, tumuangalie mkurugenzi mmoja aliyekuwa na viwanda mbalimbali vya kutengeneza nguo. Lakini siku moja aliamua kufanya ziara ya ghafla katika kiwanda chake kimoja.
Alipofika kiwandani aliwakuta baadhi ya wafanyakazi wake wakivuta sigara karibu kabisa na kibao kinachokataza uvutaji sigara sehemu hiyo. Mkurugenzi huyo akakisogelea kibao hicho na kuwaonesha wafanyakazi hao huku akiwauliza, ‘hamjasoma hapa?’ Wafanyakazi wote wakataharuki, wakashindwa kujieleza. “Vijana ningefurahi kama mngevuta sigara nje ya eneo hili au niseme hata nje ya kiwanda.”
Wafanyakazi hao walielewa kwamba bosi wao anatambua kuwa wamevunja sheria, lakini walimfurahia kwa sababu hakuzungumza nao kwa ukali, bali alizungumza kwa upendo na kuwafanya wajisikie kwamba wao ni wa muhimu katika kiwanda kile. Hilo lilikuwa ni fundisho kubwa kwao, kwani tangu hapo hawakurudia kosa hilo tena. Hivyo unaposhughulika na watu mbalimbali jaribu kuwa na busara katika kuwaeleza jambo.
Mfano mwingine ni kwa ofisa mmoja aliyejulikana kwa jina la Robby. Alikuwa na biashara zake na kila siku alikuwa akitembelea mojawapo ya biashara hizo. Ilifika siku moja akaenda kwenye ghala lake la vinywaji na kumwona mteja amekaa anasubiri huduma, lakini kulikuwa hakuna mtu wa kumhudumia kwa kipindi hicho.
Aligundua kuwa kwa wakati huo, wafanyakazi wake hawakuwa tayari kumsikiliza mteja huyo, bali walikuwa wamekaa kaunta, wakicheka na kuzungumza habari zao zinazowahusu bila kujali kuwa eneo lile ni eneo la kazi. Robby hakuzungumza lolote, taratibu akanyata kando ya kaunta na kumhudumia mteja yule mwenyewe na kukabidhi pesa kwa wauzaji hao wakati alipokuwa anaondoka.
Hapo tunaona kwamba Robby alitumia njia ya busara ya kuishi na wafanyakazi wale. Angeweza kutumia ukali au kuchukua hatua ya kuwafuta kazi mara moja, lakini kwa kuwa alikuwa ni mtu mwenye hekima na busara, aliamua kumhudumia mteja yule aliyemkuta na hilo lilikuwa fundisho kubwa kwa wafanyakazi wake.
Aliwapa somo kwa njia ya vitendo kwamba kazi si mahali pa mchezo, bali panahitaji kuheshimiwa na kumheshimu kila anayehitaji huduma. Vile vile tunaona kwamba viongozi wa umma mara nyingi wamekuwa wakipingwa kutokana na kutokuonekana katika majimbo yao.
Mara zote wanasongwa na kazi, wamekuwa katika hali ya ulinzi muda wote na wasaidizi wao ambao hawapendi watu wawabughudhi mabosi, kwa kuruhusu wageni wazungumze nao.
Lakini kuna mbunge mmoja ambaye mara zote amekuwa akiwaasa wafanyakazi wake kuwaruhusu watu wamuone. Amekuwa akisema kwamba sera zake zipo wazi kwa kila mmoja, lakini wasaidizi wake wamekuwa wagumu kumuelewa, na kuendelea kuwazuia wananchi wasiweze kumuona kwa urahisi ili waeleze matatizo yao yanayowakabili.Baada ya kuona somo hilo halieleweki kwa wasaidizi wake, mbunge huyo mwishoni alipata suluhu kwa kuamua kuondoa mlango wa ofisi yake.
Kitendo hicho kilitoa ujumbe kwa urahisi kwa wasaidizi wake, kwamba mbunge huyo yuko wazi na yuko tayari kumsikiliza kila mmoja. Hapo inamaanisha kwamba si lazima kila mara ukawa unazungumza na watu ambao hawakuelewi, wakati mwingine unaweza kuzungumza kwa vitendo, utaeleweka.
Kwa kawaida unapobadilisha maneno mawili au matatu inaweza kuleta tofauti kati ya kushindwa na mafanikio katika kuwabadilisha watu wasiweze kuwa na uchungu. Unapotumia njia ya busara katika kumrekebisha mtu aliyekosa, inamfanya mtu yule asiyekuwa na uvumilivu katika kuwasahihisha wengine kwa kuwakosoa katika njia ya uwazi, kujifunza kitu.
Mfano mwingine upo kwa familia mmoja, iliyokuwa inakarabati nyumba yao, kwa kutumia mafundi ujenzi, familia hiyo ilifikia mahala ikaamua kuwashawishi mafundi kufanya usafi mara tu wamalizapo kazi yao.
Kwa siku za mwanzoni mwa ujenzi huo, mama mwenye nyumba alipokuwa akirudi nyumbani baada ya kazi, alibaini kuwa eneo la nyumbani kwake lilikuwa chafu, lenye kuonekana vipande vya mbao na uchafu mwingine. Mama huyo hakutaka kuzungumza na mafundi hao, kwa sababu walikuwa wamefanya kazi nzuri.
Kwa hiyo baada ya mafundi hao, kuondoka, yeye na watoto wake waliokota vipande hivyo vya mbao na kusafisha eneo hilo la ujenzi. Siku iliyofuata alimwita kiongozi wa mafundi waliokuwa wakijenga na kumwambia kuwa, “Nimefurahishwa na jinsi mlivyoacha eneo hili jana usiku, lilikuwa zuri na safi, na halikuweza kuleta usumbufu kwa jirani.” Tangu siku ile na kuendelea, wafanyakazi wale baada ya kazi walikuwa wakikusanya takataka zote na kuacha eneo lile safi. Na kiongozi yule alikuwa akihakikisha kama wafanyakazi wake wameacha eneo walilofanyia kazi likiwa safi.
IMEANDIKWA NA LUCY NGOWI IMECHAPISHWA: 25 JUNI 2016

Saturday, July 9, 2016

MAISHA:- KIPAIMARA CHA BINTI YA KAKA YANGU JANETH NGONYANI

Katika maisha ya ukuaji wetu  kuna mambo mengi tunapitia...kwa mfano maisha ya kidini kwa sisi WAKATOLIKI  ni ubatizo, komunio ya kwanza, kipaimara, ndoa,au sakramenti nyingine kama upadre nk...kwa hiyo binti yetu JANETH tarehe 3/7/2016 alipata KIPAIMARA...Nami kama shangazi yako nakupa HONGERA SANA KWA KUPOKEA SAKRAMENTI HII YA KIPAIMARA.
Naupenda sana mtindo ulioanzishwa sasa kwa uvaaji wa nguo za kipaimara...

Friday, July 8, 2016

NYUMBANI NI NYUMBANI.....HODI HODI

Naona nimepatia muda kabisa ila huyo mlinzi hapo mlangoni sijui itakuwaje hapa maana na njaa ndo ninayo....

Thursday, July 7, 2016

LEO NI SIKUKUU YA SABABA/SIKUKUU YA WAKULIMA....

Leo ni sikukuu ya sabasaba...Basi mwenzeni nimekumbuka mwimbo huu tulikuwa tukiimba shuleni Saba saba eeh
Saba saba eeh mama x2
Aaahoiye eeh mama x2
Wakulima eeeh
Wakulima eeeh mama x2
Aaahoiye eeh mama x2
Muendelezo nimesahau ..Je? kuna anayekumbuka anisaidie? Maana hapa kuna kucheza pia sio kuimba tu ....

Wednesday, July 6, 2016

NAPENDA KUWATAKIENI SIKUKUU YA EID AL-FITR IWE NJEMA "EID MUBARAK"

Kwa muda kama mwezi sasa ndugu zetu Waislamu walikuwa katika mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani wakitimiza ibada ya nguzo za uislamu ambayo ni kufunga. KILA LA KHERI.

Sunday, July 3, 2016

UJUME WA JUMAPILI HII YA KWANZA YA MWEZI HUU WA SABA:- JUMAPILI NJEMA!

Kuna jambo linaweza kuja kwako kwa sura mbaya yenye kuumiza, lakini mwisho wake ukawa mzuri wenye utukufu, furaha na ushindi. Usikate tamaa kwa lolote unalopitia hujui mwisho wa hilo kuna nini. JUMAPILI NJEMA KWA YEYOTE ATAYEPITA HAPA!...