
Hali hii inapotokea, anayependa ambaye tunasema ndiye mtoaji pekee, hufikia mahali huingia kwenye hali ya hisia ambayo hufahamika kama resentment flu (Homa ya masikitiko). Hii ni hali ambayo, yule ambaye anatoa tu yaani anampenda mwenzake, lakini mwenzake hampendi, huihisi anapokuwa amechoka.
Kwa kawaida tunasema, mtu anapopenda asisubiri naye kupendwa, yaani anapotoa asijali kama mwenzake anatoa au hatoi. Lakini hufikia mahali kanuni za maumbile humfanya huyu anayetoa kuhisi kama amebeba mzigo mkubwa sana. Kama tunasema kupenda ni mtu kutoa bila kutarajia kupewa, inamaana kwamba, huyu anayeshindwa kutoa ameshindwa kupenda.
Kama ameshindwa kutoa ina maana kwamba, ameshindwa kutekeleza jukumu lake na hiyo ina maana kwamba, ameshindwa kupenda. Anaposhindwa kupenda anakuwa amevunja kanuni ya kimaumbile inayosimamia kupendana ambayo inasema ili kupendana kukamilike, pande zote ni lazima zitoe na kupokea.
Kumbuka nasema, kupendana, siyo kupenda. Kwenye kupenda tunatakiwa kutoa tu, kwenye kupendana tunatakaiwa kutoa na kupokea. Kama tunampenda mtu na mtu huyo hatupendi, yaani hatimizi majukumu na wajibu wake kwenye kutupenda sisi, hatimaye tunafikia mahali tunaingia kwenye hiyo hali niliyoitaja ya homa ya masikitiko.
Kumbuka ninaposema kutoa sina maana ya kutoa fedha, bali kumtendea na kumtolea kauli za wema mwenzako. Kwenye tatizo hili, wanawake wanaonekana kama wanaathirika zaidi.
Kama mwanamke akihisi kuwa yeye anatumikia upendo na mwenzake hajali tena, huumia kuliko ilivyo kwa mwanamume. Labda ni kwa sababu, wanawake huumia kihisia kirahisi zaidi kuliko wanaume na jambo hili linapotokea kuumiza zaidi hisia.
Mwanamke huanza kuingia kwenye hali hii polepole, pale anapobaini kwamba, mwenzake anapokea tu, badala ya kupokea na kutoa. Hii ina maana , mwanamume anaposubiri au kufurahia kutendewa mema na kutolewa kauli njema tu, wakati yeye hafanyi hivyo. hajali kuhusu mpenzi wake.
Mwanamke kwa kawaida huonyesha dalili kwamba, yuko kwenye hali hii kwa kuanza kuacha kufanya vile vitu ambavyo kwa kawaida huitwa au kuonekana vidogovidogo kwenye uhusiano.
Kwa mfano, anaweza akaacha kumtayarishia mumewe chakula anachokipenda sana ambacho alikuwa anamtayarishia kwa nyakati fulanifulani, anaweza asiwe anamchagulia tena nguo za kuvaa, anaweza asiwe anamkagua baada ya kuvaa, anaweza akaacha kumuuliza angependa kula nini na wakati mwingine anaweza kuchukua hatua mbaya zaidi kama kukataa kushiriki tendo la ndoa.
Mwanamume anapoona mke akiwa hivyo, naye huanza kumtendea mkewe kwa njia kama hiyo, yaani kuongeza kiwango chake cha kutojali. Anaweza kuanza kuchelewa kurudi nyumbani, anaweza hata kuscha Kukaa pamoja na mkewe hata akiwa nyumbani, anaweza hata kujitoa kabisa kwenye uhusiano, yaani kufanya mambo yake kama vile hana mke.
Inapotokea hali ambapo mwanamke anahisi kuingia kwenye homa hii, inabidi ajiulize haraka ni kwanini ameingia huko. Ni vizuri kujiuliza kwa sababu, akisubiri zaidi, mume naye ataanza kuwa mkorofi zaidi. Ikifikia hapo, njia ya kusuluhisha tatizo hili ambalo kwa kawaida, linaweza kuondolewa kwa mazungumzo, huwa ngumu zaidi.
Kwa hiyo, hakuna suala la “nitapenda hadi lini,” kwa sababu kupenda hakuumizi. Kunakoumiza ni kushindwa kutoa mapenzi. Ukitoa upendo wako kwa mtu ambaye yeye kazi yake ni kupokea tu, lakini hajui kutoa upendo, yeye ndiye atakayeumia. Yeye atakufanya uache kuendelea kutoa, hivyo yeye ndiye atakayekosa, siyo wewe.
Yeye atapata shida kwa sababu, kila mtu atakayeamua kuishi naye kama mpenzi, atahisi hali uliyoihisi wewe na ataamua kumkimbia. Ni hadi ajifunze kutoa, ndipo atakapoanza naye kuingia katika kupendana.
Hebu fikiria kwamba, unamtendea na kumtolea kauli nzuri mkeo au mumeo. Unahakikisha kwamba, unampa kila ambacho nawe ungependa kupewa, bila kujali kama naye anafanya hivyo kwako au hapana.Umemkubali kama alivyo na udhaifu wake na unazingatia zaidi ubora wake na siyo udhaifu huo. Hapa tunasema unampenda.
Lakini kwa bahati mbaya, huyo mwenzako ni mkosoaji, asiyejali, mchoyo, mlalamishi na mwenye ghubu. Huyu tunasema, hajui au hataki kupenda. Kwa maana hiyo, anaishi kwenye uhusiano usio na maana kwake. Hauna maana kwake kwa sababu, hana cha kutoa, ameshindwa wajibu wake katika uhusiano ambao ni kupenda. Kwa sababu hiyo, ni wazi hataweza kuendelea na uhusiano, ni lazima atasababisha uvunjike, kama tulivyoona.
Kama nawe hujui kupenda, utamuiga na utakuwa umeshindwa wajibu wako, kama yeye. Kwa hiyo, kwenye hali kama hiyo, hakuna kinachotolewa wala kupokelewa. Ni wazi uhusiano hauwezi kuwepo katika hali ya namna hiyo. Uzuri wa mmoja kuendelea kutoa bila kujali mwenzake anafanya nini ni kwamba, huyu mwenzake anaweza kungámua tatizo au kasoro yake na kubadilika.
Kwa hali hiyo, unaweza kuona jinsi upendo ulivyo kutoa na kupokea au njia mbili-kwenda na kurudi kama wengine wanavyosema. Unapokuwa wa kupokea tu bila kutoa au wa njia moja, hauwezi kuendelea kuwepo.
MAKALA HII NIMEISOMA MARA NGAPI SIJUI NA NIMEIPENDA NA NIMEONA SI VIBAYA NIKIWASHIRIKISHA NA WENZANGU ELIMU KUGAWANA …NIMEISOMA KWENYE KITABU CHA MAPENZI KUCHIPUA NA KUCHANUA KILICHOANDIKWA NA MAREHEMU MUNGA TEHENAN…PIA HABARI HII IMEWAHI KUTOKA KWENYE GAZETI LA MSHAURI WAKO.