Tuesday, March 3, 2009

MWANAUME NA MWANAMKE MAHITAJI YAO.SEHEMU YA II

a) Usalama: Ndiyo hali ya kujisikia kuwa huna hofu yoyote au wasiwasi. Wakati ambapo hakuna kitu cha kutisha au cha kuvuruga akili. Najisikia salama hatari ikiwa mbali, maadui hawapo nami nimeshinda matatizo.
Yapo mambo mengi ambayo yanaweza kutuondolea usalama katika mioyo yetu. Ajali yaweza kutokea, vita, magonjwa yaweza kutupata; watu pia wanaweza kutudhuru, kuiba mali yetu na hata kuhatarisha maisha yetu. Hofu ipo ndani yetu kwa namna nyingi. Hofu ya mambo tusiyoyajua, hasa katika kutafuta kazi, au tukiwa ugenini, tubadilishapo mtindo wa maisha.

Ingawa yote hayo yapo, bado tunajua usalama. Kuna usalama wa mtoto kifuani kwa mama yake. Usalama wa mtoto ashikapo mkono wa baba yake. Usalama wa rafiki ambaye anajua kwamba kwa vyo vyote rafiki yake yuko tayari kumsaidia. Usalama wa mwanamke aliye na hakika juu ya mapendo ya mumewe. Usalama huu ndio msingi wa haja zetu na usalama unatakiwa hasa katika ndoa. Haja hiyo ya usalama ikitoshelezwa, amani kubwa na utulivu wa moyo hupatikana.

b)Kukubalika: Haja yetu ya pili yaitwa kukubalika. Ni haja ambayo wewe na mimi tunaijua sana. Ni ile hali ya kukubalika na watu kama tulivyo, kueleweka nao, kpokewa jinsi tulivyo na tunavyojitahidi kuwa. Kila mmoja wetu anahitaji sana mtu mwingine wa kumsindikiza, kufurahi na kuhuzunika pamoja naye. Mtu ambaye anajua matatizo na matakwa yetu; pia mwenye kuelewa tunayohofia.
Jaribu kufikiri kidogo maisha yangalikuwa ya namna gani kama hatingalikuwa na mtu ye yote wa kumkimbilia wakati wa shida, au mtu wa kutupongeza na kututia moyo.

Katika ndoa mwezi wako Mume/mke, anatazamia kupata hayo kutoka kwako. Mume wako ama mkeo anataka kuhakikishiwa kwamba kwa upande wako hatapata masharti yo yote ya kumkubali; hii ina maana kwamba unamkubali na kumpokea kwa furaha jinsi alivyo nawe unamjulisha jambo hili.

Hii haina maana kwamba huwezi kuona kasoro na udhaifu alio nao mwenzako. Maana yake ni kwamba unakuwa tayari kumwambia: “Najua ya kwamba wewe si mkamilifu, lakini nakupenda jinsi ulivyo, na pia nakubali ujue kuwa wala mimi si mtu mkamilifu. Hata hivyo nina hakika kuwa unanipenda”. Unapokuwepo ukubaliano wa namna hii kila mmoja huwa na imani kubwa na mwnziye na kujiamini pia.

c) Kuthaminika: Ndilo hitaji la tatu ndani mwetu. Je, tulieleweje hitaji hilo? Unaweza kupata mwanga kidogo juu ya jambo hili kama ukikumbuka jinsi unavyojisikia wakati umekwisha fanya kila juhudi na kujisumbua ili upate kumfurahisha mwingine. Halafu mtu huyu unayetaka kumfurahisha hajali wala hatambui kwamba umefanya kitu kwa ajili yake. Katika hali hii utajisikia kama umekosa kitu fulani, na kitu chenyewe ni kuthaminika.

d) Kujikamilisha binafsi: Hiki ndicho kilele cha mahitaji yote ya hisi. Ni ile hali ya kujisikia kitu cha maana. Kujisikia kwamba nimetumia vipaji vyangu vyote kikamilifu. Nimetumia nguvu zangu zote za mwili, akili na moyo, na kweli nimefaulu kuwafurahisha wengine. Kwa kufanya hivi najiona mtu zaidi.
Si lazima kufanya mambo makubwa. Kwa mwanamke yaweza kuwa kazi ya kudarizi au kuremba kwa ushanga, kupamba nyumba kwa namna ya pekee, kutengeneza nguo za watoto zitakazomletea sifa ya wengine. Kwa mwanamume yaweza kuwa kuchukua kozi kwa njia ya posta ili kupata kazi nzuri zaidi au mshahara mkubwa zaidi.

Katika kufanya mambo haya kila mmoja anahitaji mwenzake, mume au mke. Kwa sababu kule kujikamilisha binafsi, mara nyingi, huhitaji msaada wa mwenzio. Mapendo yake yatakudhihirishia vipaji fulani ambavyo hukuvijua kwanza, na mapendo haya haya yatakupa nguvu ya kuviendeleza. Kwa pamoja utaweza kujijenga. Kwa pamoja pia mtayatosheleza mahitaji haya yaliyomo ndani ya moyo wa kila mwanamume na kila mwanamke.

Mahitaji ya kiroho
Aina ya mwisho ya mahitaji ni yale ya kiroho. Je, nina maana gani kusema hivi? Ninataka kusema, kuhitaji kitu kilicho kikubwa zaidi kuliko vile vya kibinadamu. Ni kuhitaji heri iliyo kubwa zaidi ya ile ya kibinadamu, kuhitaji amani iliyo kuu kupita moyo wa binadamu, kuhitaji Mungu Mwenyewe.

3 comments:

Simon Kitururu said...

DUH!


Dada Yasinta umemaliza!


Ila bado mahitaji ya mwanamke na mwanamume hata yakifanana kama ningekuwa najua lugha vizuri ningetofautisha maneno.

Naamini kabisa mwanamke akisema anakupenda na mwanaume akisema anakupenda kunauwezekano wanamaanisha NAKUPENDA zilizo tofauti.

Nafurahi kuwa kwa WAZULU South Afrika hata neno rangi kijani wao wanayo maneno kibao ambayo kwa kiswahili yote ni neno moja, KIJANI.

Kazi kwelikweli!:-(

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

mh. na mahitaji ya watoto wanaojificha vivhankani nk, ninini? wakifanya wao si ni uasherati na uzinzi? sasa sijui wao wanatumia vifaa gabi.

karbu tena ila ni aibu kutokupost kitu ulipokuwa bongo na kutokututafuta baadhi yetu

Yasinta Ngonyani said...

Simon, kweli kazi kweli kweli:-(

Kamala, si kweli inaonekana hukuwa unanitembea kwani kuna vitu nimeposti wakati nipo bongo. Kuhusu kukutafuta SAMAHANI nilishindwa kwani wakati mwingi nilikuwa MGONJWA. ni hayo tu.