Kama kawaida ni JUMATANO NYINGINE TENA NA NI KILE KIPENGELE CHA MARUDIO YA MATUKIO MBALIMBALI. Na Makala hii nimeshawahi kuiweka hapa. Lakini nimeshindwa kuvumilia kutoiweka hapa tena. Ni ZAWADI AMBAYO SITAWEZA KUISAHAU MILELE.
Yasinta Ngonyani, Picha kwa hisani ya Maisha Blog
Ni binti halisi wa kitanzania, ingawa anaishi ughaibuni lakini hujivunia asili yake na utaifa wake, ni binti pekee aliyejitolea muda wake kuwaelemisha watu wa rika zote bila kujali rangi, kabila, itikadi, taifa wala jinsia.
Binti huyu si mjivuni na hupenda kubadilishana mawazo na watu mbali mbali, na pia hupenda kufuatilia habari za nyumbani kwao alikotoka na haoni tahayari kuongea lugha ya kwao. Daima hujitambulisha kwa jina la asili ya kwao na huona fahari kutumia jina hilo.
Binti huyu hakuona ajizi kuwajuza wanae asili ya kwao japo wamezaliwa ughaibuni, amekuwa msitari wa mbele katika malezi ya wanae ili kuhakikisha wanae hao hawajitengi na asili ya aliotoka yeye.
Si mchoyo wa ushauri na kupitia makala zake aziwekazo kibarazani kwake amekuwa ni msaada kwa wengi, amekuwa mstari wa mbele katika kuilemisha jamii bila kujali rika. Amejitolea kufundisha kile akijuacho juu ya malezi na matatizo mbali mbali yanayowakabili wanandoa na malezi ya watoto.
Kibaraza chake kimekuwa ni kitovu chenye kukutanisha wadau mbali mbali wenye fikra pevu, na kuibua mijadala yenye kuelimisha, kufundisha, kuburudisha na kuhuzunisha pia.
Binafsi napenda kumuita dada na kwangu mimi ni zaidi ya dada, kwani amekuwa ni mwalimu mzuri kwangu nikijifunza mambo mengi kupitia kibaraza chake nimekuwa nikijifunza mengi, na sisiti kukiri kwamba chimbuko la kibaraza cha VUKANI ni kutokana na kile nilichojifuza kwake.
Ni mkweli na muwazi, na hasiti kusema wazi hisia zake, lakini huwa makini sana ili kuepuka kumuumiza mtu mwingine kihisia, na kama kwa kusema huko kutamkera mtu mwingine, ni mwepesi kuweka sawa maelezo yake ili kuondoa msigishano wa mawazo.
Nakumbuka wakati fulani nlipopata msongo wa mawazo kutokana na tofauti zangu na wazazi wangu, alikuwa ni mtu wa kwanza kunitumia email binafsi akijaribu kuniliwaza na kunitaka nisichukue hatua yoyote kujidhuru, naomba nikiri kwamba email ile ilinisaidia sana kurudi katika hali yangu ya kawaida na nilijisikia fahari kuona kwamba kuna mtu ananipenda na kunijali japo sijawahi kuonana naye uso kwa uso.
Huu kwangu ulikuwa kama muujiza, inakuwaje, mtu kusoma mawazo yangu kupitia blog tu halafu awe karibu nami kiasi hiki, ni kitu gani kimemvuta? Kusema kweli tangu siku hiyo niliamni kuwa maandishi yana nguvu sana na kupitia maandishi yawezekana mtu mwingine kukufahamu vizuri sana.
Nimekuwa karibu sana na binti huyu, na amekuwa ni mwema sana kwangu na mshauri wangu pia, na kupitia vibaraza vyetu, tumekuwa tukibadilishana mawazo na kupeana ushauri mbali mbali ili kuboresha ustawi wetu na wa familia zetu.
Huyu ndiye Yasinta Ngonyani, kwa kumsoma zaidi bofya hapa.
-------------------------------------------------------------------------------------------------Makala hii iliandikwa na mdogo wangu wa hiari Koero Mkundi mwaka 2009/08/14 bado nimevutiwa sana na hii makala na nimeona niiweke hapa kwangu pia kama kumbukumbu na pia kujikumbusha yaliyopita kwani si vibaya. Pia nachukua nafasi hii kwa kumshukuru sana mdogo wangu huyu wa hiari Koero Mkundi kwa kazi nzuri anazozifanya kwa kumsoma zaidi kazi zake ingia hapa. Pia nauthamini sana uwepo wake Mwenyezi Mungu na akulinde na akuongoze na yote utendayo yawe mema. Kwani yeye ndiye mwezeshaji wa yote na yeye ndiye ajua anavyotuwazia maana mawazo atuwaziayo ni mema. Ni hayo tu kwa leo...Halafu sijui upo wapo Koero?
TUKUTANE TENA JUMATANO IJAYO AU WAKATI MWINGINE....