Tuesday, May 31, 2016

HUU NDI UTAMADUNI WETU NA UASILI WETU WANA SONGEA/RUVUMA

NGOMA ZIKIPIGWA TAYARI KWA KUCHEZA ´LIZOMBE
Na hapa ni kikundi cha mchezo wa lizombe tayari wakiwa wamevalia sare zao kwa umaridadi kabisa...tusisahau uasili wetu. Tuwasimulie watoto wetu kama tutakuwa hatuna picha au sauti iimbayo ni muhimu sana nao wajue wapi kiini kilipotoka.

Monday, May 30, 2016

MAMBO YA MSINGI YA KUFANYA KABLA YA KUOLEWA/KUOA

image
Ndoa nyingi zinaingia kwenye migogoro kwa sababu ya mambo ya kukurupuka na kufanya haraka bila wahusika kufahamiana vizuri, hebu tuzingatie yafuatayo ili tusiseme 'NINGEJUA NISINGEOA/NISINGEOLEWA'
1. Chanzo cha uhusiano wenu kiwe ni upendo wa dhati.
2. Chunguza kwa mwenzio juu ya tabia kama:- nidhamu, adabu, hasira, ulevi na uzinzi.
3. Mpeane muda wa kutosha kufahamiana.
4. Mtembee pamoja maeneo tofautitofauti kama michezoni, mgahawani na sehemu  mbalimbali ili muone kila mmoja anapenda nini.
5. Muwe wa imani moja, ila kama mmeendana sana na mwaweza kuvumiliana hata wa imani tofauti ni sawa.
6. Wajue ndugu wa mwenzio ili kupata habari zao zitakazokufahamisha mwenzi wako  yukoje.
7. Pimeni afya zenu bila aibu,  kuna maradhi mengi kama vile  HIV/AIDS na mengine.
8. Kama ni Mkristo au Muislam funga ndoa Kanisani au Msikitini na siyo Bomani.
9.Kwa Wakristo ndoa haina talaka,  huu ni mpango wa Mungu. Kuachana na kuoa mwingine ni dhambi.
N.B: kama mwenzio ana tabia usiyoipenda, usifunge ndoa naye ukitegemea atabadilika/abadilike wakati mkiwa wachumba na siyo kwenye ndoa, labda kama umeshamkubali kama alivyo.
NAWATAKIENI WOTE JUMATATU HII YA MWISHOYA MWEZI HUU WA TANO IWE NJEMA SANA. TUPO PAMOJA DAIMA!

Sunday, May 29, 2016

HILI NI VAZI LANGU LA LEO JUMAPILI HII YA MWISHO YA MWEZI HUU WA TANO NA PIA NI SIKU YA AKINA MAMA/MORSDAG

 Ni vazi langu mpya na nilipendalo hapa bila mkanda
Na hapa nimejaribu kutinga na mkanda kama nipendavyo....sijajua ipi ni safi zaidi :-)....NAWATAKIENI WOTE JUMAPILI NJEMA NA PIA IWE SIKU NJEMA KWA AKINA MAMA WOTE/MORSDAG NANYI AKINA BABA NA AKINA KAKA MUWE NA SIKU NJEMA PAMOJA NA AKINA MAMA, DADA, SHANGAZI, BIBI...NK. Kapulya wenu.

Friday, May 27, 2016

CHAGUA LA BLOG YA MAISHA NA MAFANIKIO KUWA HII IWE PICHA YA MWISHO WA WIKI HII:- MAISHA YETU NA USAFIRI WETU....

Napenda usafiri wa baiskeli, ni usafiri mojawapo mzuri, hauna foleni ni rahisi kufika uendako...Ila hapo duh! dadangu kamaliza 4 kwa 1:-) ....ila tutafika tu!

Thursday, May 26, 2016

NGOJA TUTOKE MOROGORO NA KUELEKEA SONGEA KWETU AMBAKO NI NYUMBANI - KIJIJI CHA LUGAGARA

SHULE YA MSINGI LUGAGARA
Lugagara , ipo katika Kata ya Kilagano , Songea Vijijini  , Mkoa wa Ruvuma  Lugagara ni kijiji ambacho kipo nje ya Songea karibu na Peramiho katika Kata ya Kilagano . Kijiji hiki kina Wakazi wasiozidi 3,700.

Wanafunzi wa shule ya msingi Lugagara wakiwa ndani ya mapozi:-) Nimekumbuka mbali kama vile najiona hapo....


Wednesday, May 25, 2016

LEO TUTEMBELE MOROGORO MJI KASORO BAHARI NA MILIMA YAKE....

Milima ya Uluguru ileeee...
Kilichonipendeza hii picha/taswira ni huu udongo mwenkundu pia shamba la mahindi...nimekumbuka mbali sana

Hapa tunaona milima ya Uluguru na shamba la katani....Najua wengi wetu tunakumbuka historia ya mashamba ya katani...

Tuesday, May 24, 2016

UJUMBE WA LEO KUTOKA KWA BLOG YA MAISHA NA MAFANIKIO KUJA KWA WEWE MSOMAJI WA MAISHA NA MAFANIKIO

"MAISHA NI MAFUPI SANA, UKIAMKA ASUBUHI NA MASIKITIKO HAIFAI. KWAHIYO WAPENDE WATU WANAO KUPENDA, SAHAU WALE AMBAO HAWAKUPENDI."
TUPO PAMOJA...KAPULYA.

Monday, May 23, 2016

KWA NINI WANAWAKE WANATENDEWA MAMBO YA AJABU NA WANAUME?

Siku ya leo nimeamka na mawazo mengi sana katika kichwa changu....Nimewaza na kuwazoa bila kupata jibu nimeona ni bora tuwaze pamoja.  Mawazo yenyewe  ni haya.....
Hivi ni kwa nini wanawake wanatendewa mambo ya ajabu na wanaume?
Ni kwa nini wanawake wanaonekena wanyonge mbele ya wanaume...?
Ni kwa nini wanawake wanakuwa wategemezi kwa wanaume...?
Kuna tofauti gani kati ya mwanamke na mwanamume kiakili, kihisia, kimwili na kiroho?
Ni nini chanzo cha yote haya:- Ni maumbile? Mfumo dume?  Je? ni uvivu tu wa wanawake?  Au ni kushindwa kujitambua kwa mwanamke?

Sunday, May 22, 2016

NAWATAKIENI JUMAPILI NJEMA...UJUMBE- MAVUNO....

ZAO LA MAHINDI
Unapopanda mbegu huwa unategemea kuvuna mazao mengi...Hii picha nimetumiwa na ndugu yangu wa karibu sana. Utavuna ulichopanda. NAWATAKIENI WOTE JUMAPILI NJEMA SANA.
BASI TUMALIZIE NA WIMBO HUU WA MAVUNO WA MIRELLE BASWIRA NA CHRISTINA SHUSHO.........KARIBUNI!

Friday, May 20, 2016

IJUMAA YA LEO TWENDE MPAKA LIULI MKOANI RUVUMA NA NGOMA YA KIODA/CHIHODA


IJUMAA NJEMA KWA WOTE NA NGOMA HII YA KIODA/CHIHODA KUTOKA KWETU LIULI....

Thursday, May 19, 2016

MCHANA WA LEO:- KARIBUNI TUJUMUIKE UGALI NA SAMAKI WA KUKAANGA (VIBUA) PIA MCHUZI

Karibuni ndugu zangu tujumuike kwa chakula akipendacho Kapulya...ugali na samaki. Si mnajua ugali ndio uliotukuza...:-) Kila la kheri wote na mlo mwema....

Wednesday, May 18, 2016

CHEKA TARATIBU NDUGU YANGU...!!!

Mwalimu aliingia katika darasa moja huko Iringa Vijijini na kuuliza wanafunzi wake. "Nani atanipa jibu la wingi wa Chumvi?" Mwanafunzi mmoja kwa kujiamini akasimama na kujibu, "Fyuvi!" Duh, kasheshe  hiyo.....!

Tuesday, May 17, 2016

ZILIPENDWA: HAPA NI POSTA MJINI SONGEA MKOANI RUVUMA 1960

Hivi ndivyo Ofisi ya Posta Mjini Songea, Mkoani Ruvuma ilivyokuwa ikionekana mwaka 1960.

Monday, May 16, 2016

JUMATATU YA LEO TUANZE NA NA KUANGALIA BAADHI YA SIFA ZA MIKOA YA TANZANIA

Nimeamka asubuhi hii na kukuta ujumbe huu katika barua yangu pepe nimecheka sana na nikaona nisiwe mchoyo kama kawaida yangu  liwe jema au baya  ni ELIMU  huwa napenda kuwashirikisha na walio nami. Karibu labda utaona mkoa wako mie nimeshaona:-)


1. DAR ES SALAAM - Utapeli
2. ARUSHA - Starehe
3. MBEYA - Matukio
4. MWANZA - Fujo
5. TANGA - Mapenzi
6.  MOROGORO - Kilimo
7.  DODOMA - Bahati
8.  IRINGA  - Kujinyonga
9.  RUVUMA - Pombe
10. RUKWA  - Uchawi
11. TABORA - Mikosi
12. SHINYANGA - Njaa
13. SINGIDA - Umalaya
14. KAGERA - Misifa
15. LINDI - Waoga
16. KIGOMA - Ubishi
17. PWANI - Uvivu
18. MTWARA - Hasara
19. KILIMANJARO - Utajiri
20. MARA - Hasara
21. MANYARA - Ubahili
22. GEITA - Presha
23. SIMUYU - Maradhi
24. NJOMBE - Haraka
25. KATAVI - Aibu
Je? mwenzangu watokea mkoa gani kati ya hii?  Binafsi kama wote mjuavyo natoka RUVUMA:-)                  

Thursday, May 12, 2016

UPELEKAJI MIHOGOCHINA WAZUA BALAA BUNGENI

Dodoma. Mbunge wa Songea Mjini (CCM), Leonidas Gama amemtaka Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage kufuta kauli ya kusafirisha mihogo ghafi kwenda China.
Mbunge huyo alisema jana kuwa, kauli hiyo inapingana na hotuba ya waziri huyo iliyosheheni mipango ya Serikali ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati kupitia viwanda ifikapo mwaka 2025.
Mbali na mbunge huyo, wabunge wengi waliochangia hotuba hiyo bungeni walionyesha wasiwasi wa Tanzania kuwa nchi ya viwanda kwa vile Serikali haielezi itajenga viwanda vya aina gani.
Gama alimtaka waziri huyo kufuta kauli yake ya kupatikana kwa soko la mihogo China kwani inapingana na mipango aliyoianisha na pia ni kuhamishia ajira nchini humo.
“Mheshimiwa Mwijage aone namna ya kufuta ile kauli. Kuna kauli moja alitoa Aprili 19, alisema anawaomba wananchi wa Lindi wazalishe kwa wingi muhogo umepata soko China,” alisema mbunge huyo.
“Sasa kwa maelezo haya, tukipeleka muhogo China maana yake tunahamisha ajira China. Kama viwanda viko China vya kuchakata muhogo kwa nini visije Tanzania?” alihoji.
Mbunge huyo alisema ni vyema viwanda hivyo vikajengwa Lindi na Songea ili mchakato wa kusindika muhogo ufanyike Tanzania na siyo China na kuwa katika hilo hatamuunga mkono.
Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Annatropia Loikila aliitaka Serikali itumie msemo kuwa “ipo siku moja Tanzania inaweza kuwa na uchumi wa viwanda” badala ya kutoa hakikisho.
“Nimeona ni namna gani tunataka kuwahadaa wananchi kwamba Tanzania itakuwa ya uchumi wa kati ifikapo 2025. Ni bora tuseme iko siku moja tunaweza kwenda kwenye uchumi wa kati,” alisema.
Mbunge wa Bagamoyo (CCM), Dk Shukuru Kawambwa alisema tangu 2008 Serikali ilipofanya tathmini ya fidia, wananchi hawajalipwa ili eneo hilo liwe huru kwa ajili ya ujenzi wa viwanda.
Hata hivyo, Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba alisema Serikali ni lazima iwe na mtazamo unaoeleweka kwamba inataka kujenga viwanda vya aina gani badala ya kutoa kauli ya jumla.
“Waziri ni lazima utuambie unataka kujenga viwanda vya nini. Focus (mkazo) yetu ni nini? Tungeanza na viwanda vya sukari, mafuta ya kula na ngozi ili wakulima wetu wafaidike,”alisema.
Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Hawa Mwaifuga aliitaka Serikali kulinda kwanza viwanda vya ndani kabla ya kufikiria kujenga vipya akisema bidhaa kutoka nje ndizo zinaua viwanda.
CHANZO:-  Daniel Mjema, Mwananchi- Tuesday, May 10, 2016.

Wednesday, May 11, 2016

KATUNI YETU YA WIKI HII...PUNGUZA MWENDO....

Je? wewe ungefanya kama huyo mtoto?....Nawatakieni  siku njema!

Tuesday, May 10, 2016

UTAPENDA MPAKA LINI?

Inasemwa siku zote kwamba, upendo ni kubadilishana, yaani mtu anampenda mwingine na huyo mwingine anampenda yeye. Hii ni kweli. Inapotokea kwamba, mpenzi mmoja anasahau wajibu Wake, yaani kumpenda mwenzake na anasubiri kupendwa tu, tatizo hutokea.
Hali hii inapotokea, anayependa ambaye tunasema ndiye mtoaji pekee, hufikia mahali huingia kwenye hali ya hisia ambayo hufahamika kama resentment flu (Homa ya masikitiko). Hii ni hali ambayo, yule ambaye anatoa tu, yaani anapenda mwenzake, lakini mwenzake hampendi, huihisi anapokuwa amechoka.
Kwa kawaida tunasema, mtu anapopenda asisubiri naye kupendwa, yaani anapotoa aijali kama mwenzake anatoa au hatui. Lakini hufikia mahali kanuni za maumbile humfanya huyu anayetoa kuhisi kama amebeba mzigo mkubwa sana. Kama tunasema kupenda ni mtu kutoa bila kutarajia kupewa, ina maana kwamba, huyu anayeshindwa kutoa, ameshindwa kupenda.
Kama ameshindwa kutoa ina maana kwamba, ameshindwa kutekeleza jukumu lake na hiyo ina maana kwamba, ameshindwa kupenda. Anaposhindwa kupenda anakuwa amevunja kanuni ya kimaumbile inayosimamia kupendana ambayo inasema ili kupendana kukamilike, pande zote ni lazima zitoe na kupokea.
Kumbuka nasema, kupendana, siyo kupenda. Kwenye kupenda tunatakiwa kutoa tu, kwenye kupendana tunatakiwa kutoa na kupokea. Kama tunampenda mtu na mtu huyo hatupendi, yaani hatimizi majukumu na wajibu Wake kwenye kutupenda sisi, hatimaye tunafika mahali tunaingia kwenye hiyo hali niliyoitaja ya homa ya masikitiko.
Kumbuka ninaposema kutoa sina maana ya kutoa fedha, bali kumtendea na kumtolea kauli za wema mwenzako. Kwenye tatizo hili, wanawake wanaonekana kama wanaathirika zaidi.
Kama mwanamke akihisi kuwa yeye anatumikia upendo na mwenzake hajali tena, huumia kuliko ilivyo kwa mwanamume. Labda ni kwa sababu, wanawake huumia kihisia kirahisi zaidi kuliko wanaume na jambo hili linapotokea huumiza zaidi hisia.
Mwanamke huanza kuingia kwenye hali hii polepole, pale anapobaini kwamba, mwenzake anapokea tu, badala ya kupokea na kutoa. Hii ina maana, mwanamume anaposubiri au kufurahia kutendewa mema na kutolewa kauli njema tu, wakati yeye hafanyi hivyo, hajali kuhusu mpenzi Wake. Mwanamke kwa kawaida huonyesha dalili kwamba, yupo kwenye hali hii kwa kuanza kuacha kufanya vile vitu ambavyo kwa kawaida huitwa au kuonekana vidogovidogo kwenye uhusiano.
Kwana mfano, anaweza akaacha kumtayarishia mumewe chakula anachokipenda sana ambacho alikuwa anamtayarishia kwa nyakati fulanifulani, anaweza asiwe anamchagulia tena nguo za kuvaa, anaweza  asiwe anamkagua baada ya kuvaa, anaweza kuchukus hatua mbaya zaidi kama kukataa kushiriki tendo la ndoa. Mwanamume anapoona mke akiwa hivyo, naye huanza kumtendea mkewe kwa njia kama hiyo, yaani kuongea kiwango chake cha kutojali. Anaweza kuanza kuchelewa kurudi nyumbani, anaweza kuacha kukaa pamoja na mkewe hata akiwa nyumbani, anaweza hata kujitoa kabisa kwenye uhusiano, yaani kufanya mambo yake kama vile hana mke.
Inapotokea hali ambapo mwanamke anahisi kuingia kwenye homa hii, inabidi ajiulize haraka ni kwa nini ameingia huko. Ni vizuri kujiuliza kwa sababu, akisubiri zaidi, mume naye ataanza kuwa mkorofi zaidi. Ikifikia hapo, njia ya kusuluhisha tatizo hili ambalo kwa kawaida, linaweza kuondolewa kwa mazungumzo, huwa ngumu zaidi.
Kwa hiyo, hakuna suala la `hitapenda hadi lini,` kwa sababu kupenda hakuumizi. Kunakoumiza ni kushindwa kutoa mapenzi. Ukitoa upendo wako kwa mtu ambaye yeye kazi ni kupokea tu, lakini hajui kutoa upendo, yeye ndiye atakayeumia. Yeye atakufanya uache kuendelea kutoa, hivyo yeye ndiye atakayekosa, sio wewe. Yeye atapata shida kwa sababu, kila mtu akayeamua kuishi naye kama mpenzi, atahisi hali ulioihisi wewe na ataamua kukimbia. Ni hadi ajifunze kutoa, ndipo atakapoanza naye kuingia katika kupendana.
Hebu fikiria kwamba, unamtendea na kumtolea kauli nzuri mkeo au mumeo. Unahakikisha kwamba, unampa kila ambacho nawe ungependa kupewa, bila kujali kama naye anafanya hivyo kwako au hapana. Umemkubali kama alivyo na udhaifu Wake na unazingatia zaidi ubora Wake na siyo udhaifu huo. Hapa tunasema unampenda.
Lakini kwa bahati mbaya, huyo mwenzako ni mkosoaji, asiyejali, mchoyo, mlalamishi na mwenye ghubu. Huyu tunasema, hajui au hataki kupenda. Kwa maana hiyo, anaishi kwenye uhusiano usio na maana kwake. Hauna maana kwake kwa sababu, hana cha kutoa, ameshindwa wajibu wake katika uhusiano ambao ni kupenda. Kwa sababu hiyo, ni wazi hataweza kuendelea  na mahusiano, ni lazima atasababisha uvunjike, kama tulivyoona.
Kama nawe hujui kupenda, utamuiga na utakuwa umeshindwa wajibu wako, kama yeye. Kwa hiyo, kwenye hali kama hiyo, hakuna kinachotolewa wala kupokelewa. Ni wazi uhusiano hauwezi kuwepo katika hali ya namna hiyo. Uzuri wa mmoja kuendelea kutoa bila kujali mwenzake anafanya nini ni kwamba, huyu mwenzake anaweza kungámua tatizo au kasoro yake na kubadilika.
CHANZO: MAPENZI KUCHIPUA NA KUNYAUKA/gazeti la Mshauri wako.

Monday, May 9, 2016

JUMATATU HII TUANZE NA PICHA HII ....RAMANI YA AFRIKA KWA MTINDO HUU....

Ramani ya Afrika kwa kutumia Kahawa...nimependa ubunifu huu...ndani ya ungo sisi wangoni tunasema ungo...lupalu....NAWATAKIENI WOTE JUMATATU NJEMA. PANAPO MAJALIWA TUTAONANA TENA!

Sunday, May 8, 2016

NAPENDA KUWATAKIENI WOTE JIONI HII YA JUMAPILI YA LEO KWA MLO HUU...

UGALI, KACHUMBALI NA SAMAKI WA KOKA
Mwenyezi Mungu na aubaribi mlo huu na watakaokula nao pia washibe na kupata baraka zake. JUMAPILI NJEMA SANA PIA JIONI NJMEA. KAPULA/KADALA

Saturday, May 7, 2016

MAKAMBAKO MWAKA JANA:- PICHA YA MWISHO WA JUMA.....


Inavyoonekana hapo ni kwamba Nguruwe hao kama vile wanataka kuruka yaani hawataki kuwa katika lori hilo ...kuwa kitoweo....Nami nilikuwa naogopa wataturukia ....NACHUKUA NAFASI HII KUWATAKIENI WOTE MWISHO MWEMA WA JUMA...KAPULYA

Thursday, May 5, 2016

ANAOMBA USHAURI AFANYEJE AWEZE KUOKOKA NA HILI JANGA?


Hapa inaonekana alikuwa anakata mti mara simba akatokea akapanda juu ya mti huko kakutana na nyoka, akataka ajirushe majini akaona mambo. Mmmh... hapa sijui bora akapambane na nyoka .... Je? ungekuwa wewe ungefanyaje?...

Monday, May 2, 2016

KILIO CHA MWANAMKE WA KIAFRIKA NI NANI AKISIKIE!?

Kulea kwa shida
Kutafuta maji kilomita kadhaa tena ya kisima
Kutafuta kuni kilomita kadhaa
Kupikia familia zao
Ndugu wasomaji leo jinsi  wanawake walivyokuwa na shughuli za kila siku katika kuhudumia familia zao, nilikutana na wanawake wakitafuta kuni, wako waliokuwa wakitafuta maji tena umbali mrefu. hiyo ilinikumbusha madhila wayapatayo wanawake wa vijijini ambao wanaishi katika mazingira magumu ajabu, halafu tunaambiwa eti kuna usawa, utoke wapi?

Sunday, May 1, 2016

NAWATAKIENI WAOTE JUMAPILI NJEMA PIA SIKU YA WAFANYAKAZI IWE NJEMA/MEI MOSI NJEMA

SISI TUNAFANYA KAZI HAPA!
Leo napenda kuwatakieni wote JUMAPILI NJEMA na pia  SIKU HII YA WAFANYAKAZI IWE NJEMA. BINAFSI NIPO KAZINI LEO...HAPA KAZI TU.