Tuesday, March 29, 2011

SHUKRANI ZA DHATI TOKA KWA FAMILIA YA MZEE NGONYANI/K​LAESSON!!!


Familia ya mzee Ngonyani 2008-2009 Ruhuwiko-Songea
Kwa niaba ya wanafamilia jamaa na marafiki wote. napenda kutoa shukrani za dhati kwa kuwa nasi bega kwa bega tangu 23/3/2011 siku ya Jumatano mpaka hivi leo. Kwa kweli ninyi ni NDUGU wa kweli kabisa hamkuwa nyuma hata mara moja. Nilipopata tu habari hii nikajikakamua ili kuwahabarisha. Hazikupita sekunde baada ya kuweka tangazo mara nikaona maoni yananza kutiririka. Nikawa mchovu nikaenda kulala, kuamka asubuhi naangalia nakuta Mawazoni nako tangazo lipo. Dakika hazipiti mara naona tangazo jingine kwa mdogo wangu kwa mama mwingine Vukani naye ameweka na pia kashikwa na mshangao wa kutoweka kwa ndugu yetu mpendwa Asifiwe. Mara nasikia simu yangu ya kiganjani inaita napokea nasikia sauti ambayo sijawahi kusikia sio mwingine tena bali ni yeye mwenyewe Mwanamke wa shoka. Dada huyu amekuwa akinipigia simu kila siku kutujulia hali. Na pia bila kusahau tumekuwa tukitumiwa barua pepe nyingi nyingi mno pia ujumbe wa simu ya kiganjani. AHSANTENI wote na mwenyezi mungu awazidishia mara dufu kwa wema wenu. Hakika kwa msaada/ushirikiano wenu wa kueneza habari na wengi wakiwemo wanafamilia kuweza kupata habari kwa njia hii tunawashukuru sana. Watu wengi wameguswa sana na kifo cha ndugu yetu Asifiwe, sina la kusema zaidi ya AHSANTENI SANA. Kuhusu kumuenzi Asifiwe hakukuishia hapo naye Swahili wa Waswahili akaongeza mchango wake. Habari zikazidi kuenea na watu wakawa wanazidi kutufariji. Kwa kweli hapo ndipo nilipojikuta najisemea, kweli kublog si kublog tu bali ni mahali ambapo hukutanisha watu na kuwa NDUGU. Muda ukapita nikaona Kazi yako ni jina lako naye kaweka tangazo nikapiga magoti na kushukuru jinsi habari zinavyoenea kwa haraka. Hapa bado ni siku ya Alhamisi 24/3/2011 mara nikaona Mwananchi mimi kaandika kitu pia wakiwa wawili zaidi yaani kaka Shabani Kaluse na Chacha o`Wambura. Na hapo hapo nikawa napokea simu, watu wakitupa pole kwa msiba nikajikuta kama nipo hapa nyumbani na watu 500 kumbe hapana. Matangazoyakazidi kuongezek na watu kupata habari kona zote kwani naye Nyahbing worriors hakuwa nyuma. Ijumaa tarehe 25/3/2011 Diwani ya fadhili akasema hapana ni lazima niweka kitu, kwa kweli nasema kama mdogo wangu Koero Mkundi alivyosema kuwa msiba huu si wangu tu ni wa wote ni kweli kabisa. Kufumba na kufumbua barua pepe zikawa nazo zinamiminika kutoka sehemu mbalimbali. Wote mliotuma msione kimya tumezipata pole zenu ila ni kutingwa tu. Mwenyezi Mungu na awe nanyi. Kweli aliyeanzisha kublog na apongezwe sana. Habari ya msiba wa Asifiwe haikuishia hapo kwani Mzee wa Lundu Nyasa naye akaibuka kutoka ziwani. Lakini hata hivyo kama waswahili wasemavyo hakuna kuchelewa naye Mzee wa Changamoto akaona naye ni lazima atoe aliyo nayo moyoni. Halafu napenda kumshukuru BOSI wangu kwa kunipa ruhusu ya kuwa nyumbani kwa nyumbani kwa kipindi hiki kigumu. Bila kuwasahau WAFANYAKAZI WENZANGU ambao wamekuwa wakipiga simu na kunipa pole. Kwa kweli zimekuwa siku za machungu, pigo pia tumeachiwa pengo ambalo halitazibika kamwe. Tarehe 26/3/2011 ndio ilikuwa siku ya mazishi niliendelea kupokea simu kutoka sehemu mbalimbali na pia nikiwa nawasiliana na Ruhuwiko. Kwa kifupi mazishi yalifanyika kwa utulivu mkubwa, watu walifurika kama utitiri kiasi kwamba Kanisa la Ruhuwiko likawa ndogo . Kwa niaba ya wanandugu, tunawashukuruni sana wote walioshiriki wakiwa karibu au wakiwa mbali kwa kumsindikiza Asifiwe katika safari yake ya mwisho. AHSANTENI SANA WANABLOG/WASOMAJI WANANDUGU WOTE. TUNASHUKURU KWA USHIRIKIANO WENU WA HALI NA MALI. BILA NINYI SIJUI INGEKUWAJE? PAMOJA DAIMA!!!

Monday, March 28, 2011

Marafiki waliokuja kutufariji siku ya ijumaa!!

Hapa ni marafiki wawaili waliokuja kutufariji siku ya ijumaa wote manjua mimi ni hapo katikati na kulia kwangu ni Dada mkubwa Mariana Kutoka nchini Angalo na kuchoto kwangu ni Dada Asta kutoka Ivory Coast. Hapo walinilazimisha kunywa chai na unywaji wangu wote wa chai hapo nilikuwa hoi kabisa. Wote tunawashukuru kwa kutufariji maana wanaonywsha ushirikiana mzuri. Na jana Jumapili alikuaja Dada mmoja yeye anatokea Njombe ila samahani nilitingwa kuchukua picha yake. Na picha hii hapo juu mpigaji si mwingine tena ni Erik..... nitarudi mtandaoni hivi karibuni nitengamae kwanza. MNAPENDWA WOTE...

Saturday, March 26, 2011

MAZISHI RUHUWIKO: TUUNGANE PAMOJA KWA KUMSINDIKIZA MPENDWA WETU ASIFIWE NGONYANI KATIKA SAFARI YAKE YA MWISHO

Asifiwe Ngonyani
Kuzaliwa 26/11/1989
Kuiacha dunia 23/3/2011
Kuzikwa 26/3/2011

Asifiwe Ustarehe kwa amani peponi Amina

Habari nilizozipata leo kutoka nyumbani Ruhuwiko ni kwamba watu wengi SANA wamemiminika na wanazidi kumiminika.TWAMSHUKURU MUNGU KWA HILI.
Leo tarehe 26/3/2011 siku ya jumamosi saa tatu tukwenda kuchukua mwili wa Asifiwe katika sehemu ya kuhifadhi miili katika Hospitali ya mkoa Songea. Baada ya hapo mwili wa Asifiwe unapelekwa nyumbani Ruhuwiko kwa buruani ambayo itakuwa saa tano. Saa sita mchana maandamano kwenda kanisani Ruhuwiko. Saa saba nusu mchana misa inaanza katika Kanisa la Ruhuwiko. Na baada ya hapo wote tunaandamana ili kumsindikiza mpendwa wetu ASIFIWE NGONYANI KWA SAFARI YAKE YA MWISHO. MWENYEZI MUNGU TWAKUOMBA UIPOKEE ROHO YAKE PEPONI AMINA.

FAMILIA YA MZEE NGONYANI NA FAMILIA YA NGONYANI/KLESSON ITATOA SHUKURANI ZA DHATI KWA USHIRIKIANO WENU KATIKA KIPINDI HIKI KIGUMU!!!!

Friday, March 25, 2011

SHIDA, SHIDA MPAKA SIKU YA MWISHO!!!!!!Habari zaidi za mazishi nitaziweka karibuni ndugu zanguni ila kwa kifupi tu NASEMA AHSANTENI SANA KWA USHIRIKIANO WENU ULIUONYESHA Familia ya Mzee Ngonyani Ruhuwiko-Songea na Familia ya Ngonyani/Klaesson Sweden. Inatoa shukrani za dhati sana. Ahsanteni...

Wednesday, March 23, 2011

MSIBA RUHUWIKO:-FAMILIA YA MZEE NGONYANI INASIKITIKA KUTANGAZA KIFO CHA BINTI, DADA,MDOGO,SHANGAZI, MAMA MDOGO PIA SHEMEJI ASIFIWE NGONYANI!!


Asifiwe Ngonyani 26/11/1989-23/3/2011
Jioni hii muda si mrefu nimepigiwa simu kuwa sina mdogo tena. Mdogo wangu mpendwa na wa pekee ametuacha amekata roho jioni hii kama saa tatu kasorobo ya TZ. Mwenyezi Mungu na aipokee roho yake mahali pema peponi AMINA. HAKIKA NI PIGO KUBWA SANA KWA FAMILIA YETU..Habari zaidi nitawaelezeni.....

SUPER MUHOGO: Unga Safi wa Muhogo !!!!

Katika makuzi yangu chakula changu kikuu kilikuwa ni uji na ugali wa muhogo. Si mnajua tena ukiwa mkazi/mzaliwa wa kando ya ziwa Nyasa hiki ndo chakula kikuu. kutoka U-KACHIKI mpaka kufikia U-MBUYAMUNDU wangu hii ndo ilikuwa lishe yangu kuu. Ugali wa muhogo na majani yake KISAMVU na pia bila kusahau SAMAKI. Nilienda kumsalima Prof. Mbele ili nibadili chakula angalao nipate ugali wa MAHINDI na MAHAREGWE (mandondo). Kumbe naye siku hizi anakula ugali wa MUHOGO . Jamani tule ugali wa muhogo. Ahsanteni sana kwa kuendeleza biashara hii ya unga wa muhogo kila la kheri....Zaidi unaweza kumsoma prof. Mbele kwani naye amesema kitu. Prof.Mbele

Tuesday, March 22, 2011

Tanzania:- Baadhi ya wanamuziki wa Five Stars wafariki ajalini
Nawatakia nafuu na afya njema majeruhi na kuwaombea wapone haraka.
Pole kwa wote waliofikwa na msiba huu.
Roho za marehemu zipumzike pema.

MICHEZO YETU!!


Netiboli....
Leo nimeamka na mawazo yangu yamefika hadi Lundo pia Kingoli wakati nasoma shule ya msingi. Nilikuwa mchezaji mzuri sana wa netiboli tena nilikuwa mfungaji magoli yaani mchezo huu ni raha kweli. Najiuliza sijui bado unachezwa mashuleni bado au?

Monday, March 21, 2011

UJUMBE: AFRIKA /TANZANIA YETU!!!Nimeusikiliza wimbo huu leo zaidi ya mara kumi na mwisho nimeona ni vema nikiuweka hapa ili na wenzangu muusikie....

Wanawake! naona urembo kweli kazi he he !

ukitaka kupendeza inabidi kuvumilia...
SRXA anasema****Si urembo ndo sababu ya kulia...ni kwa sababu kapima afya majibu si mazuri.....Ebu angalia na nywele zilivyokatika.

TI anasema****Kanyimwa hela na bwana, sasa anaona uchungu kutumia zake anazobana kwenye bajeti ya mboga!

HK anasema ***hapo ni anajiangalia kwenye kioo kaona hajapendeza kama alivotegemea ndo akaanza kulia..................

KIL anasema******Mie naona kama amelazimishwa kunyolewa kwa nguvu na mkasi.Labda mume ameona urembo wake wa nywele unamtia hasara.

FK anasema*****Huyu lazima kuna kitu kimemuudhi sana huko nyumbani. Sasa ili kujiliwaza kaona akajirembe huko salon.Lakini katikati ya urembo huo mawazo yanamjia anabubujikwa na machozi. Kwani kina dada/mama hili halijawahi kuwakuta?
Kuna siku niliona mama mmoja yuko sehemu na watoto wake wanakula lunch. Kajipamba sana ila alikuwa amevaa miwani ya jua nikadhani ni urembo tu. Kumbe nyuma ya hiyo miwani mikubwa alikuwa kaiva macho kwa kulia.

Akina baba/kaka mnatupeleka pabaya sana mjue!

Oneni sasa! Huo mchozi siyo wa maumivu ya kurembwa wala siyo wa kulazimishwa kunyoa nywele maana hapo naona si mchezo katika hiyo Salon ni salon ya uhakika na bei yake si chini ya 40,000/=

GFKanasema****Huyu kapigwa biti na bwana akanyoe kwasababu amekuwa akitoka akiulizwa anasema alikuwa saloon
WAKATI SI KWELI.
Habari hii nimeipata Jamii Forum!!!

Friday, March 18, 2011

JAMANI HUU KWELI NI UUNGWANA? KWELI BINADAMU KUFUNGWA KAMBA KAMA MBUZI????


Habari hii imenigusa sana kwa kweli, yaani bado tunaishi miaka ya 1970-1990 sikutegemea kabisa kama mambo haya yatakuwa bado katika ulimwengu huu. Najua ni sehemu nyingi si Afrika tu walikuwa wanaona ni kama laana kupata watoto wenye mtindio wa akili. Nakumbuka nimewahi kushuhudia kwa macho yangu familia moja ilikuwa na mtoto mwenye mtindio wa akili. Walikuwa wakimficha ndani hakuna aliyejua, kama kuna mtoto wa aina hiyo pale nyumbani pao. Siku moja nilipita pale, na nikakutana na mama wa nyumba anampeleka haja kubwa nikamuhoji inakuwaje ndo akanisumulia. Kwa kwa kweli jamii yetu haina ule utu kabisa kwani walikuwa wakiwacheka na mambo mengine mabaya mengi. Lakini kitu kimoja ambacho kimenipa nguvu ni kwamba sio sisi tu. Hata wenzetu nchi zilizoendelea walifanya hivyo walipopata watoto wa mtindio wa akili waliwaacha sehemu maalumu, lakini hata hivyo hawakupata yale maisha ambayo kila binadamu anastahili. Kwa hiyo nachotaka kusema hapa kwa fikra zangu ni kwamba najua kwamba kila binadamu anastahili kupata maisha bora awe mwenye akili timamu au mwenye mtindio wa akili. BINADAMU WOTE NI SAWA. HEBU SOMA HABARI HII HAPA CHINI KUHUSU PICHA HIYO HAPO JUU yenye kichwa cha habari kama ifuatavyo.

HUYU NI MKOROFI NDIO SABUBU ANAISHI KWA KUFUNGWA KAMBA.!!!!?


"... wewe kaka acha tu! huyo ni mkorofi sana hivi ukimfungulia kamba hapa anazunguka mitaa yote ya mji wa Tanga na hapo alipo ana majeraha ya kupigwa na kuchanjwa na nyembe kutokana na ukorofi wake hivi tumeaona njia pekee ni kumfunga kamba na kumchunga kama ng'ombe akiwa malishoni japo na usiku akilala tuna mfunga kamba pale anapolala" alisema mwanamke huyo anayekadiliwa kuwa na miaka kati ya 23 na 25

Hata hivyo anasema mbali ya kufungwa kamba pia kwa upande wa chakula wamekuwa wakimwekea katika sahani yake maalum na kula akiwa amefungwa kamba huku kwa wiki ama mwezi huoogeshwa mara moja.

Alisema kuwa sababu za kufungwa na kutengwa na familia ni kutokana na tatizo hilo la utindio wa ubongo linalomkabili na kupelekea hali ambayo ndani ya familia yao wamekuwa wakiona kama ni aibu kwa kijana huyo kutembea mitaani na tatizo hilo.

Pia alikili kuwa kijana huyo amekuwa na uwezo mkubwa wa kutambua japo hajapata bahatika kupelekwa shule na kuwa sehemu kubwa hata kutamka baadhi ya maneno ameanza kujifunza baada ya kuanzishwa kwa utaratibu wa kumfunga kamba nje ya nyumba hiyo na hivyo kubahatika kujifunza kuongea kwa kusikika kutoka kwa wananchi ambao wamekuwa wakipita eneo hilo.Hapa ni mwanzo tu zaidi inga hapa .

TUANZE MAPUMZIKO KWA BURUDANI ......Mimi naamini mziki ni moja ya burudani ya sisi binadamu kwa hiyo napenda kuwatakieni mapumziko mema ya mwisho wa juma. Najua wengine tutakuwa tunafanya kazi lakini kutapatikana tu kamuda kiduchu kupumzika basi ndo hapo pa kujiburudisha na mziki. najua pia sisi binadamu huwa tunapumzika/starehe/burudika tafauti lakini sidhani kuna mtu asiyependa mziki kama wengi wanavyosema WAAFRIKA ni watu wenye miziki ndani ya miili yao tangu tuzaliwe....IJUMAA NJEMA NA TUTAONANA WAKATI MWINGINE!!!

Thursday, March 17, 2011

MAISHA: NAZIPENDA SKAFU/SHALI ZANGU!!!

SKAFU ZANGU
Katika maisha sisi binadamu tupo tofauti kwa kila namna. Tukianzia tabia, sura, mwili, kupenda nk. Leo napenda kuzungumzia neno KUPENDA/TAMAA. Lakini si kule kupenda kwa kimapenzi hapana ni kupenda kwa kupenda vitu au kupenda kununua vitu hata kama anavyo vya kutosha:- Yaani utakuta mtu anapenda kikombe chake cha chai kweli kiasi kwamba mwingine akikigusa ni balaa. Mwingine anapenda kweli shati moja tu ambalo anaweza kulivaa kila siku utazani hana lingine. Mwingine akawa anapenda sweta kiasi kwamba hata kulifua anasahau. Halafu kuna hawa wanaonununua viatu, utakuta mtu ana pea za viatu chumba kizima huwa nashangaa sana je atavivaa lini? lakini hii yote ni basi tu yaani tamaa . Kwa hiyoleo nataka kuwaambia mimi ni MDHAIFU SANA wa SKAFU/SHALI. Hapo juu ni zaidi ya ishirini na bado natamani zaidi kwani nataka niwenazo rangi zote. NAPENDA SANA SKAFU.....Swali je wewe ni mpenzi/mkusanyaji wa nini?

Wednesday, March 16, 2011

Monday, March 14, 2011

ULE MRADI WETU SASA UMEIVA………..


Dada Yasinta


Makao makuu ya NGO yetu
Kwako dada yangu mpendwa Yasinta Ngonyani, natumaini wewe na watoto wako pamoja na huyo shemeji yangu anayejifanya kutojibu salaam zangu muwazima wote. Unajua dada simlaumu sana huyo mumeo, maana najua alitishwa wakati anakuchumbia kuwa sisi Watanzania tuna shida sana, kwamba tukiona ndugu yetu kaolewa basi shida zetu zote zitaishia kwake. Naomba umtoe mashaka kwamba ukoo wa Ngonyani hatuka hivyo, yaani hatuko kama ule ukoo wa mzee Makalioni, yule anayependa kusingizia misiba kila uchao ili kujipatia ridhiki.

Mwambie kuwa ukoo wa Ngonyani ni Jiniazi na una watu makini sana na wenye akili za ziada, kwani haoni hao wanae wawili uliomtotolea baada ya kukumimbisha kuwa wana akili sana kama mama zao wadogo na wajomba zao.

Samahani dada ngoja niachane na hayo, unajua leo nimeamua kukuandikia waraka huu asubuhi huku nikinywa chai na mkate wa bofulo nilionunu hapo jirani kwa mpemba kwa sababu waraka huu ni muhimu sana, kwani unahusiana na lile dili nililokudokeza wakati ule ambalo limeanza kutema, kama yale machimbo ya Tanzanite kule Mererani.

Dada mimi sio mbinafsi na ndio maana nikaona nikushirikishe ili wote mimi na wewe na ukoo wote wa Ngonyani tuwe matajiri kama Bill Gate wa Sudani, yule anayetoa tunzo ya Raisi bora wa Afrika. Eti huyu jamaa amegundua kuwa maraisi wa Afrika kwetu wana njaa sana na ndio maana wanakuwa mafisadi na ili kuwatoa wasiwasi akaanzisha tunzo yenye mapesa mengi ili kuwaondolea tamaa ya wizi.

Naamini hata huyo mzungu wako ataamini kuwa ukoo wa ngonyani sio mchezo na una watu makini na mahiri katika kuzitafuta ngawira.

Dada huku nyumbani nimeanzisha mradi wa kuhamasisha ukimwi. Na nimeona nikushirikishe ili wote tuwe matajiri, lakini usidhani nakushirikisha bure, lazima utoe kamchango kako kama kianzio yaani utoe mtaji, kwani usione vinaelea vimeundwa. Sasa ili uwe na wewe ni mmiliki wa NGo yangu…….hapana yetu inabidi utumbukize kama Krona Milioni mia moja ili tuweze kuwavuta wafadhili kuwa NGo yetu sio ya kuganga njaa, dada naamini hizo pesa unazo kwani huyo mzungu wako hawezi kukosa pesa kidogo hivyo, maana hicho kiasi cha pesa ni kama vile anatoa hela ya kununulia Tooth Picks. Naomba hizo pesa uzitumbukize kwenye akaunti ya NGo yetu ambayo ni XXL 000055557788JK/KoeroNGo/Yasinta/Camilla/Eric.com hiyo ndiyo akaunti namba yetu.

Kama nilivyokwambia kuwa nimeanzisha huu mradi wa Ukimwi ambao nimeamua kuuita Intaneshino NGo for fool people of Ruhuwiko die because of ngono zembe. Na kama unavyoona hilo jina linatisha na kuvutia sana.

Dada huku ili uweze kuishi kwa amani na usalama ni lazima uwe mbunifu, ili uweze kuendesha gari linaloitwa Rav 4 au Toyota Haria ni lazima uwe na akili ya ziada ya kuwaona wengine ni wajinga na wewe ndiwe Generali Brigedia mwenye akili nyingi kuwazidi.

Mradi wetu wa ukimwi unaendeshwa kwa njia ambayo ni lazima tutapata fedha za wafadhili kwani tuna watu wanaoweza kubuni na wengine wanaoweza kutusaidia kuthibitishia dunia kwamba Tanzania inayo watu wanaoteketea kwa ukimwi hata kabla bwana hajarudi katika ule ujio uliotabiriwa kwenye kitabu kitakatifu cha biblia.

Kwanza tunajitahidi kuwasiliana na wafadhili na kuwaeleza kwamba huku nchini katika kila watu kumi unaokutana nao, basi kumi na moja wana virusi na kumi na mbili kati yao tayari wanaumwa mahututi. Na ili upate fedha za wafadhili haraka ni lazima takwimu zako ziwe zimechanganyikiwa kidogo kwani takwimu zikiwa sahihi wafadhili lazima wataingia mashaka au watakweri .

Sisi tuna mtaalamu wetu mmoja aitwae Chacha o’Wambura Ng’anambiti ambaye ni mwenyeji wa kule Kyabakari Barracks Musoma, Mara. Huyu kijana tumemuingiza katika mradi wetu kwa kuwa anajua kubuni na kutunga kiasi kwamba anaweza kukushawishi kwamba jina lako sio Yasinta bali unaitwa Jasimini na ukakubali.

Hata hivyo yuko kijana mwingine aitwae Kamala Lutatinisibwa, ambaye amelikimbia jiji la Dar Es Salaam na kwenda kuishi kule Karagwe kutokana na ukata, huyu ndio yuko kwenye mchakato wa usaili akiwania nafasi ya Meneja mahusiano katika NGo yetu. Unajua hii nafasi ya meneja mahusiano inahitaji watu makini na mahiri walio na utaalamu wa utambuzi. Kama atafauli katika usaili atatusaidia sana katika kupiga tiralila za propaganda kwa wafadhili pale watakapotaka kuthibitisha takwimu zetu.

Kwa upande wa huyu kijana Chacha o’Wambura Ng’wanambiti kazi yake ni kuandaa taarifa za kuombea pesa kwa mujibu wa matukio yaliyo katika jamii kwa wakati huo.

Kwa mfano hili tatizo la mafisadi lililoikumba nchi yetu, huyu mwenzetu amewaandikia wafadhili akiwambia kuwa Mafisadi na ukimwi ni ndugu kabisa kwani ukimwi unasambaa sana katika kipindi hiki ambacho mafisadi wameshika hatamu za nchi, kwa sababu mafisadi hao wamekwiba fedha za Richimondi ambazo zingesaidia mradi wa umeme vijijini na kwa kuwa mradi huo umekwama na kusababisha vijiji vyetu kama vile kule Ruhuwiko, Kashasha, Kyabakari, na kwingineko kukosa umeme, watu wanatumia fursa hiyo kuendelea kufanya ule mchezo mtamu gizani yaani ule mchezo ulikataliwa na mungu katika amri ya sita katika zile amri zake kumi.

Ameendelea kuwaeleza kuwa kwa kuwa huko vijijini bado wananchi wako gizani kutokana na kukosa umeme wanaume hawavalishi vilambio vyao vifanyio na inakuwa ni vigumu wanawake kug’amua janja yao kwa kuwa kuna giza totoro na hivyo kuambikizwa ukimwi kirahisi.

Kijana huyo ameendelea kuandika kwamba katika utafiti wetu tumegundua kuwa wakati mwingine hata wale wauza vifanyio huwauzia wateja vifuko vya ashikirimu wakidai ni vifanyio orijino kumbe ni feki, na hivyo vinashindwa kuhimili vishindo na kupasuka kiurahisi.

Kutokana na Write up hiyo Wafadhili wametujibu kwamba utafiti wetu ni wa kiwango cha juu na wameahidi kutupatia kiasi kikubwa cha pesa ili kudhibiti hali hii ya vijana kuendelea kuambukizana ukimwi ambapo unachagizwa na kupenda sana ngono.

Dada namuona Chidakwa, huyu binti wa mzee Makalioni anakuja kwa kasi sijui baba yake kabuni msiba mwingine ili tumpe michango ya rambirambi, hebu ngoja nifiche huu waraka maana akiuona atakwenda kumwambia baba yake ili na yeye aanzishe NGo yake na kujipatia fedha…….unajua dada ukiwa na aidia zilizokwenda shule inabidi ufanye siri maana kuna wezi wa aidia ile mbaya, unaweza kushangaa wenzako wamekupiku……hebu ngoja nimsikilize…..nitakumalizia hii habari wakati mwingine…LOL
Habari hii nimeipenda sana imeandikwa na mdogo wangu Koero Mkundi na nimeona si mbaya kama tukiipitia tena kwani kurudia kitu ndiyo huwa unakumbuka zaidi. Bofya hapa kumsoma zaidi kazi zake.

Sunday, March 13, 2011

JUMAPILI NJEMA KWA WOTE!!


Malaika wapo lakini wakati mwingine hawana mabawa. Na sisi tunawaita wao MARAFIKI. WOTE MNAPENDWA!!! JUMAPILI NJEMA SANA KWA WOTE

Saturday, March 12, 2011

PICHA ZA WIKI HII:- KIDUKU...........

Picha hizi nimetumiwa na kaka yangu wa hiari Shabani Kaluse na katika picha hizo kuna shangazi yangu wa hiari mwanaye Kaka Shabani ni huyu kijana mwenye T-shirt nyekundu. Anaitwa Abraham.
Alianza huyu.....
Kisha huyu.....

Baadaye mweh....

Weweee..toka hapa

Subiri weweeeeeeeeee...

Ngoja tupige picha ya pamoja...
NAWATAKIENI WOTE JUMAMOSI NJEMA NA MAPUMZIKO MEMA PIA TUTAONANA WAKATI MWINGINE!!!!!

Friday, March 11, 2011

MAISHA/MILA,UTAMADUNI NA DESTURI:- SIKU YANGU ILIVYAKUWA LEO....MAZISHI!!!

Sijui nianzia wapi??
Ok ni hivi:- Jana Alhamisi nilikuwa kazini, na baada ya kazi kama kawaida ya watu wote huwa wana hangaika na mihangaiko au kuridi nyumbani na kupumzika. Kwa hiyo nami nilifanya hivyo jana nilikuwa na mihangaiko yangu na baadaye nikarudi nyumbani. Ile kuingia tu ndani nikakumbana na mlio wa simu, kuangalia sioni jina yaani limefichwa, hata hivyo sikusita nikapokea.

Oh! Kumbe wewe Mariana, ndiyo mimi Yasinta, hali yako? Salama tu......tukaendelea maneno mawili matatu...Oh, nilisahau Mariana ni rafiki yangu anatoka Angola. Basi pale tukawa tunapeana habari za hapa na pale na mara akaniambia kuwa rafiki yetu mwingine kutoka Serbien kafiwa na mamamkwe wake na mazishi ni kesho yaani leo.

Hapo nikawa hoi, ingwa huyo mama mkwe wa rafiki yetu Saida sijawahi kumwona hata siku moja. Nikashikwa na uchungu sana. Kwa hiyo nikakata shauri kwenda kwenye mazishi yake ambayo yalikuwa leo. Mamamkwe wa Saida anaitwa Maria amefariki akiwa na miaka 82.

Tulikuwa na misa na baadaye tukaunganika na kumsindikiza mamamkwe Maria kwa safari yake ya mwisho. Kulikuwa na watu 23 na Padre 24. Nasikitika sana kuwa sijaweza kupiga picha nilisahau kamera yangu nyumbani. Mamamkwe Maria na Ustarehe kwa Amani Peponi Amina!!

Thursday, March 10, 2011

TANGAZO:-.PATA KITU AMBACHO ROHO INAPENDA!!!

Kiluvya Pub-Kituo cha starehe kwa watu makini.
Nina marafiki zangu wengi wanaiongelea sana Kiluvya Pub. Nafikiria nikifika Bongo nitajitahidi nifike kujionea mwenyewe. Wanasema walitembelea na wakapenda huduma zao. Ninawashauri muende pia mkajionee wenyewe. Wanasema si Pub zote Bongo kuna huduma nzuri kama Kiluvya pub, kwa muziki na vinywaji.
Kwa waliopo Dar hata nje ya Dar mnakaribishwa ndani ya Kiluvya Pub-Kituo cha starehe kwa watu makini.
Kila kinywaji kinapatikana kwa bei nafuu pia kila aina ya chakula kwa order maalum vinapatikana.
Kwa maelezo zaidi tembelea http://www.kiluvyaspub.blogspot.com/

Wednesday, March 9, 2011

HII NI KAZI YA NANI??

Naona ni siku nyingi hatujasimuliana hadithi na leo nimeona ni wakati mzuri niwasimulia kahadithi haka:-Hadithi, hadithi….


Mmhh! ngoja kwanza nikune kichwa!!


Hii ni hadithi kuhusu watu wanne waitwao Kila mtu, Mtu, Mtu na Hakuna mtu. Kulikuwa na kazi muhimu kufanywa na kila mtu alikuwa na uhakika kila mtu angeweza kufanya kazi hiyo. Kila mtu angefanya kazi hiyo, lakini Hakuna mtu alifanya hivyo. Mtu alipata hasira kuhusu hili, kwasababu ilikuwa ni kazi ya kila mtu. Kila mtu aliwaza kuwa Kila mtu anaweza kufanya hivyo lakini Hakuna mtu aliyetambua kwamba kila mtu asingefanya hivyo. Na mwisho iliishia Kila mtu kumlaumu Mtu wakati Hakuna mtu aliyefanya chochote ambacho Kila mtu angeweza kufanya. ……mwisho wa hadithi!!!!

Tuesday, March 8, 2011

LEO NI SIKU YA WANAWAKE DUNIANI!!!!

Basi ngoja tusikiize ujumbe huu kutoka kwa Mrisho mpoto usemaye KWANI NI YEYE MAMA!!

Monday, March 7, 2011

KUADIMIKA KWANGU NI KWASABABU HII!!

Habari, Hej, Monili, Kamwene, mwaukabwanji, hallo,!hola! nakadhalika. Nilikuwa sipo hewani karibia wiki sasa napenda kuwaomba radhi wasomaji wa Maisha na Mafanikio kwa kuadimika kihivyo. Ni kwamba hapo mkoni petu kulikuwa na likizo ya wiki moja (Sportlov) nami nikaona ni vema nami niwe na familia.
SASA NIMERUDI NIPO NANYI TENA. KUSEMA KWELI NIMEWAMISS SANA NDUGU ZANGUNI:-) OH! MIJA na EDNA AHSANTENI SANA KWA KUULIZA NA SASA NIPOOOOO!!!

Tuesday, March 1, 2011

NIMEJIFUNZA KUTOKA KWA CHRISTINA

Christina akiwa amelazwa KCMC Moshi

Akiwa mjini Arusha akifanya manunuzi baada ya kuruhusiwa kutoka KCMC

Akimsimulia rafiki yaka Laila, walipokutana mjini Arusha


Huwa tunajifunza kupitia kwa wengine hususan kwa yale mambo magumu na yaliyojificha. Naomba nikiri kwamba pamoja na kusoma ushuhuda mbalimbali kupitia magazeti na blogs, lakini sikuwahi kuzipa uzito shuhuda hizo. Naomba nikiri kuwa tukio la hivi karibuni lilipompata rafiki yangu na wifi yangu Christina aishiye Dar es salaam Tanzania nimejifunza kuwa imani ikichangizwa na ibada ina nguvu sana.
Christina Kaluse ni wifi yangu wa hiyari ambaye ni mke wa mwanablog mwenzangu na ambaye ni mwanautambuzi anayetuelimisha kupitia kibaraza chake cha Utambuzi na Kujitambua, huyu si mwingine bali ni mwanablog Shaban Kaluse, ukitaka kusoma habari zake waweza kubofya hapa.
Nimekuwa nikiwasiliana na Christina kwa takriban miaka miwili sasa, na tangu kufahamiana na familia hii ya mwanablog mwenzangu, nimejikuta nikiwa karibu nao tukiwasiliana mara kwa mara kama ilivyo kwa baadhi ya wanablog wengine.
Nisiwachoshe, niwasimulie kisa cha kuandika kile nilichojifunza kwa wifi yangu huyu Christina au mama Abraham.

Nakumbuka ilikuwa ni siku ya jumatatu ya Januari 31, 2011, majira ya mchana, nilipata ujumbe mfupi kupitia simu yangu ya kiganjani kutoka kwa Christina, na ujumbe wenyewe ulisomeka hivi, ‘Yasinta naomba uungane nami kwenye maombi, nimepofuka jicho moja’ .

Ujumbe huo ulinishtua sana, nikaamua kumpigia simu ambapo tuliongea kwa muda mrefu sana.
Kwa kifupi aliniambia kuwa mnamo siku ya jumatano ya Januari 19, 2011, akiwa dukani kwake, (Christina anamiliki duka la vifaa vya ushonaji na ubunifu wa mavazi maeneo ya Tabata jijini Dar es salaam) aliingiwa na vumbi kidogo kwenye jicho lake la mkono wa kushoto, na alijaribu kulisafisha jicho hilo kwa maji safi lakini halikupata nafuu na liliendelea kumuuma.
Alikata shauri kurudi nyumbani kwake ambapo sio mbali na mahali ilipo ofisi yake, alipofika nyumbani aliendelea kulisafisha jicho lake hilo kwa maji safi, lakini halikupata nafuu yoyote.
Usiku kucha hakulala pamoja na kumeza vidonge vya kutuliza maumivu.

Ilipofika asubuhi akiongozana na mumewe walikwenda hospiali maarufu hapo jijini Dar iitwayo Regency ambapo alionana na daktari bingwa wa macho na baada ya vipimo iligundulika kuwa mboni ya jicho imepata kidonda na daktari huyo alidai kuwa huenda lile vumbi liliambatana na mchanga na hivyo wakati alipokuwa analisafisha ule mchanga ukawa umejeruhi mboni ya jicho hilo.

Kumbe huo ukawa ni mwanzo wa safari ya jicho hilo kupofuka, Christina alinieleza kuwa pamoja na kupatiwa matibabu katika hospiali hiyo lakini hakupata nafuu yoyote na usiku kucha alikuwa akikesha kwa maumivu makali ya jicho hata pamoja na kumeza vidonge vya usingizi lakini hakupata lepe la usingizi.

Ilipofika siku ya jumamosi ya January 29, 2011,ikiwa ni siku kumi tangu aanzwe na tatizo hilo, jicho likapoteza uwezo wa kuona na mboni ya jicho ikageuka na kuwa kama ina mtoto wa jicho, kwa maelezo yake Christina alisema kuwa hata yule daktari bingwa wa macho pale Regency alionekana kuchanganyikiwa kutokana na hali ile na alionekana kukata tamaa, lakini hata hivyo alimwandikia dawa nyingine na kumtaka akazitumie kisha arudi siku ya jumanne.
Aliporudi nyumbani walishauriana na mumewe na wakakata shauri kuhamia katika Hospitali ya CCBRT ambayo ndiyo hospitali maarufu hapo nyumbani ambayo inasifika kwa kutibu matatizo mbalimbali ya ulemavu yakiwemo matatizo ya macho.

Siku hiyo ya jumatatu ya Januari 31, 2011 aliyonitumia ujumbe mfupi, ndiyo siku ambayo alikwenda CCBRT. Baada ya vipimo, daktari aliyempima bila kutafuna maneno alimweleza waziwazi kuwa jicho limeshapofuka, na alimlaumu eti amechelewesha jicho huko vichochoroni mpaka limepofuka ndio anakwenda kwao…..

Kauli hiyo ilimshangaza sana Christina, kwani tangu alipopata tatizo hilo alikwenda kupata matibabu kwenye Hospiali ya Regency ambayo inatambulika na inasifika kwa matibabu, sasa iweje alaumiwe na kuambiwa kuwa alikuwa vichochoroni? Christina alionesha kushangazwa kwake na maadili ya Daktari yule.

Yule Daktari ambaye ni Mtanzania mwenzetu (Hospitali hiyo inayo pia wataalamu wa kigeni) alimweleza kuwa tiba pekee iliyobaki ni kuweka uzingativu kwenye kutibu kidonda tu, na hata akipona hataweza kuona kabisa kwani jicho limeshambuliwa na bacteria kiasi kwamba limeharibiwa kabisa. Hata hivyo alikiri kushindwa kubaini aina ya bakeria waliomshambulia, pamoja na kukwangua kidonda hicho na kupima maabara.
Aliandikiwa aende siku ya Jumanne ya Februari 1, 2011, kwa ajili ya operesheni ndogo ya kuliweka dawa na kulifunga.

Wakati naongea naye kwenye simu walikuwa wamekata shauri yeye na mumewe wamgeukie Mungu wakaamua waende kwenye maombi.

Nilimuuliza zaidi ya mara mbili kuwa ana imani akienda kwenye maombi atapona, na alinijibu kwa kujiamini kabisa kuwa daktari pekee aliyebaki ni mungu.
Ingawa tunatofautiana kimadhehebu, Christina yeye ni Msabato na mimi ni Mkatoliki, lakini nilimuahidi kuungana naye katika maombi.

Ni kweli siku iliyofuata alinijulisha kuwa aliombewa na Mwinjilisti mmoja wa kanisa la Wasabato la Chang’ombe SDA aitwae James Ramadhan Rajabu na maumivu yakatoweka na jicho likafunguka na likaanza kuona siku hiyo hiyo….ingawa hata hivyo bado lilikuwa linaonekana kama lina mtoto wa jicho.

Aliniambia kuwa anasafiri kwenda Moshi KCMC kuendelea na matibabu lakini bado imani yake kwa Yesu ni kubwa na anaamini atapona, kwani Mungu ndiye atakayekuwa Daktari mkuu atakayewaongoza Madaktari watakaomtibu huko KCMC.
Tuliendelea kuwasiliana hata alipokuwa huko Moshi KCMC, na alinijulisha kuwa awali madaktari wa KCMC walikanusha kuwa jicho lake limepofuka baada ya vipimo, ingawa hawakuweza kuona aina ya bacteria waliomshambulia.

Walishauri alazwe halafu watajaribu kuwasiliana na daktari mwingine bingwa aliyeko Nairobi ili kuangalia kama anaweza kuja hapo KCMC kushughulikia kesi yake ambayo hata wao iliwachanganya sana, hasa baada ya kuwaeleza kuwa CCBRT wameshindwa kutibu jicho lake.
Siku iliofuata yule daktari kutoka Nairobi alifika na baada ya kulipima jicho lake mara kadhaa hakupata majibu ya kueleweka, aliamua kuchuna sehemu ya kidonda na kuchukua sampuli ambayo ingepelekwa Nairobi kwa ajili ya vipimo katika maabara kasha. Aliamuandikia dawa za matone ambazo zitazuia wale bacteria wasiendelee kushambulia jicho lake wakati akisubiri majibu.

Katika kipindi chote alichokuwa amelazwa hapo KCMC akisubiri majibu ya vipimo vyake kutoka Nairobi, alikuwa akiendelea na maombi kwa kushirikiana na Mwinjilisti James pamoja na Wainjilisti wengine wa dhehebu lake la Kisabato aliowataja kwa majina ya Mwinjilisti Japhet Magoti Matotiwa kanisa la Manzese, na Mwinjilisti Benson Kilango Izoka wa kanisa la Bombo SDA Tanga.
Baada ya siku tatu yule Daktari alirudi na majibu, lakini cha kushangaza alikuta kidonda kimepona kwa asilimia 75. Hali ile haikumshangaza yule daktari peke yake bali pia Madaktari wenzie nao walishangazwa na kule kupona kwake kwa haraka.
Kwa mujibu wa majibu aliyokuja nayo, iligundulika kuwa jicho la Christina lilishambuliwa na Fangasi.

Aliandikiwa dawa na siku iluyofuata ikiwa ni siku ya tano tangu alazwe Hospitalini hapo aliruhusiwa kurudi nyumbani Dar, lakini alitakiwa kurudi klinik baada ya wiki mbili ili kuangaliwa kama anaendeleaje.

Baada ya kurudi Dar, aliendelea na dawa pamoja na maombi, na ilimchukua wiki moja tu kupona kabisa, na jicho kurudi katika hali yake ya kawaida.
Aliporudi Moshi KCMC, Daktari alithibitisha kuwa amepona kabisa, na hakusita kuweka bayana kuwa kupona kwake kumekuwa ni kwa miujiza kwa sababu kutokana na hali ya jicho lake walidhani ingechukua muda mrefu hadi kupona.

Jana nilizungumza naye kwa muda mrefu sana akinisimulia safari hii ndefu ya ugonjwa wake huo na jinsi maombi pamoja na imani ilivyomsaidia kupona kwa haraka.
Kwa kweli nimejifunza jambo moja kubwa sana kutokana na mkasa huu uliompata wifi yangu huyu wa hiyari ya kutokata tamaa pale tupatapo changamoto za kimaisha kama vile ugonjwa na hali zetu kimaisha.

Kama Christina angekata tamaa na kusikiliza ushauri wa Daktari wa CCBRT, ni wazi kuwa leo hii angekuwa amepofuka jicho moja. Lakini yeye mwenyewe alidai kuwa alikataa katu katu kukubaliana na maelezo ya Daktari yule na aliiambia nafsi yake kuwa jicho lake halijapofuka na halitapofuka.

Naamini hata wewe unayesoma hapa kuna jambo utakuwa umejifunza.
Napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza Christina kwa kuwa na ujasiri wa kukabiliana na changamoto hiyo. Namuomba Mungu aendelee kuibariki familia yao, awape ujasiri wa kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha, na asiwape moyo wa kukata tamaa.
Nimejifunza kutoka kwa Christina.

Ebu tumaliza kwa kusikiliza wimbo huu:-