Sunday, January 30, 2011

NI JUMAPILI YA TANO NA YA MWISHO YA MWEZI HUU NAWATAKIENI JUMAPILI NJEMA!!!

Katika jumapili hii ya mwisho na ya tano ya mwezi huu basi nimeona tuimalize kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa sala hii :- SALA YA MKE KUMWOMBEA MUMEWE Ee Bwana , ni ajabu, Jinsi fikra zangu zinavyomrudia kila mara Huyu, mume wangu, Mwenzi anayeshiriki maisha yangu kwa namna ya pekee. Ninapofagia nyumba na mazingira yake, Nataka kutengeneza nyumba nzuri kwa ajili yake. Ninapopika chakula vizuri,Napenda kumfurahisha. Ninaponunua nguo mpya na kujaribu kuonekana mrembo, Ni kwa ajili yake tena, Ee Bwana. Na ninaweza kukuambia kwamba Ninamwonea fahari, Anafanya kazi kwa bidii ili kupata riziki yetu; Ni mtu mwenye haki, mwadilifu, Naye hujitahidi kutufurahisha. Kwangu, yeye ni mpole na mwangalifu. Hunijali na kuonyesha kweli kwamba anajali. Hunifanya mimi nijiamini mwenyewe, Anajua jinsi ya kuondoa hofu zangu, Hunipatia usalama na upendo ambao nahitaji sana. Ee Bwana, ninakuomba, Umbariki na umlinde. Katika safari zake, umfikishe salama. Kazini mwake, umpe fanaka Na hapa, nyumbani petu naomba apate amani na heri. Bwana, unisaidie mimi pia Niweze kuwa yule mke anayehitaji. Unifanye niwe mtu anayeweza kumwamini daima, Mwanamke ambaye anaweza kumfurahia, Niweze kumsaidia asahau matatizo yake, Niweze kuondolea mbali hofu zake na kupunguza uchungu wake. Bwana, Wewe ndiwe uliyenipa mume huyu, Na katika yeye,Umenipatia sehemu ya nafsi yako mwenyewe. Ninakusifu kwa ajili yake, Ee Bwana.

Friday, January 28, 2011

TUSISAHAU UTAMADUNI/NGOMA ZETU ZA JADI-NGOMA YA CHIYODA/KIODA!!!


Hapa ni ngoma ya kioda(chioda). Ni ngoma ya WamaTengo na inachezwa na akina mama, hapa ni kijiji cha Mkinga katika bonde la Hagati-Mbinga. IJUMAA NA MWISHO WA JUMA MWEMA KWA BURUDANI HII!!!

Thursday, January 27, 2011

Swali /Tafakari ya leo!!!

Nimekuwa nikijiuliza/nikitafakari jambo hili:- Kwa nini una/tunafumba macho tupigapo chafya? Sijapata jibu kwa nini na ndio nimeona tusaidiana kutafiti kwa pamoja. Tukutane tena wakati mwingine.

Tuesday, January 25, 2011

UNAKUMBUKA MICHEZO KAMA HII?

Nimekumbuka michezo kama hii nilipokuwa mdogo, maana katika familia yetu watoto wa kiume ni wengi zaidi kwa hiyo tulikuwa hawanibagui katika michezo....haya wewe je uliwahi kusafiri na gari kama hili????:-) brrrrrrrrrrrrrrr kanyonyonyooooooo twendeeee....

Monday, January 24, 2011

UKIKUTA MANYOYA, UJUE KESHALIWA!!!

Utotoni kuna michezo mingi ya kukumbukwa
Habari/kisa hii/hiki nadhani wengi mnakikumbuka niliandika mwaka jana katika pitapita zangu nimekutana nacho hapa kibarazani na nimekipenda na nikaona si mbaya kama tukipitia tena kama nilivyozoe kusema kurudia kitu/kusoma ndio kujifunza. Haya karibuni .....
-------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------
Wakati wa utoto wetu yapo mambo mengi ambayo tumeyapitia, ambayo huwa wakati mwingine ukiyakumbuka unatamani sana kurejea utotoni.

Hivi karibuni mdogo wangu Koero aliweka mada yake aliyoipa kichwa cha habari kisemacho, ‘anaposema mwendawazima’.
Katika makala yake hiyo kuna kipengele alizungumzia kuhusu kuteka maji kisimani na jinsi yeye na bibi yake walivyowakuta mabinti wa pale kijijini kwa bibi yake walivyokuwa wakicheza na wavulana pale kisimani badala ya kuchota maji na kupeleka nyumbani.

Pamoja na kukemewa na Bibi Koero, lakini walimdharau ma kuendelea kucheza michezo yao na wavulana wale, bila kujali onyo la Bibi Koero, isipokuwa binti mmoja ambaye alimsikiliza bibi Koero na kuondoka kurejea nyumbani akiwaacha wenzie wakiendelea kucheza pale kisimani. Kama ungependa kujikumbusha makala hiyo unaweza kubofya hapa.

Kipengele hicho kilinikumbusha wakati wa utoto wangu kule kijijini Litumbandyosi/Kingoli wakati ule nikiwa darasa la nne.
Wakati huo tulikuwa tukienda kisimani kuteka maji na huko tulikuwa tukicheza michezo mingi ya kitoto.

Nakumbuka nilipokuwa likizo nyumbani mwaka jana, nilipokuwa naelekea sokoni, njiani nilikutana na kijana mmoja ambaye ningependa kumwita Mpetamanga (Sio Jina lake) kwa kweli nilikuwa nimemsahau, sijui ndio uzee unaninyemelea, maana nilishangaa alinikumbuka vizuri sana tofauti na mimi ambaye nilikuwa nimemsahau.

Mpetamanga nilisoma naye darasa moja na nakumbuka baadae familia yao ilihama pale kijijini na kuhamia kijiji cha jirani na huo ukawa ndio mwisho wa kuonana na kijana huyu.
Kukutana kwetu pale njiani kulitukumbusha mambo mengi sana ya utotoni ikiwemo ile michezo tuliyokuwa tukicheza kule kisimani tulikokuwa tukichota maji.
Mpetamanga alitumia muda huo kunikumbusha mambo mengi ya utotoni ikiwemo hiyo michezo tuliyokuwa tukicheza kule kisimani.

Kwa kuwa nilikuwa na haraka nilimuaga, lakini nilimkaribisha nyumbani, kisha tukaagana na nikaondoka kuelekea sokoni kununua mahitaji yangu.
Siku iliyofuata nikiwa nyumbani na mwanangu Erik, kwani Camilla alikuwa ametoka na baba yake kwenda mjini kununua mahitaji mengine ya pale nyumbani, nilisikia mtu akibisha hodi, nilipokwenda kufungua mlango alikuwa ni Mpetamanga.

Nilimkaribisha ndani kwa bashasha na kisha tukakaa sebuleni kwa mazungumzo.
Nilimwita mwanangu Erik na kumtambulisha kwa mgeni.
Mpetamanga alishtuka sana, na kuniuliza kwa hamaki, ‘Yasinta umeolewa?’
Nilimjibu kuwa nimeolewa na nina watoto wawili. Nilimjulisha kuwa ninaishi nchini Sweden na familia yangu, na pale nyumbani niko likizo tu.

Alishtuka sana na nilimuona dhahiri akiwa amenyong’onyea kabisa. Alinijulisha kuwa alipomaliza shule alikwenda nchini Malawi kundelea na masomo na amekuwa akiishi huko tangu alipoondoka nchini.
Na yeye kama ilivyo mimi aliamua kurudi nchini kuwasalimia ndugu zake na safari hiyo ilimlazimu kufika Ruhuwiko kumuona mjomba wake, lakini pia akiwa na hamu ya kuniona kwani aliambiwa kuwa familia yetu ilihamia Ruhuwiko siku nyingi.

Na pale tulipokutana ndio alikuwa amefika Ruhuwiko.
Aliniambia kuwa, nilipomkaribisha nyumbani alifurahi sana na alijua huo ndio wakati muafaka wa kuzungumza nami kwani ni muda mrefu alikuwa akiniwaza, na lengo lake ilikuwa kama akinikuta sijaolewa basi azungumze nami ili alete posa.

Nilicheka sana na kumwambia kuwa amechelewa kwani mie niliolewa na kuondoka nchini na kuhamia Sweden.
Nilimchekesha pale nilipomwambia, ‘Ukikuta manyoya basi ujue ndio keshaliwa’
Alicheka sana na kuniuliza kama nina maana gani, na ndipo nilipomfafanulia kuwa mpaka amekuta watoto basi ajue kuwa ndio nishaolewa hivyo……..

Lakini kitu kingine kilichomshangaza zaidi ni kuona jinsi ninavyozungumza kingoni na Kiswahili kwa ufasaha pamoja na kuishi nje ya nchi kwa muda mrefu, kwani hata nilipomweleza kuwa nimeolewa na ninaishi nchini Sweden alidhani namtania, hadi nilipomuonesha picha za familia yangu.


Hata hivyo Mpetamanga alikubali matokeo, na kuridhika na maelezo yangu.
Kusema kweli kila niwapo likizo nyumbani nakutana na visa na vituko vingi vya aina hii na haviishii hapo, hata mtandaoni nako kuna visa vyake, hili sitalizungumza kwa undani maana mdogo wangu Koero amelizungumza hili kwa kirefu katika makala yake aliyoipa kichwa cha habari kisemacho, ‘Dalili hizi sio za kweli’ unaweza kubofya hapa kumsoma.

Kuna wanaume wakware ambao hawakubali kushindwa. Hata wakute manyoya lakini bado watapekuwa weeeee! wakiamini kukuta minofu. Jamani mmeshachelewa ndio keshaliwa huyoo…….LOL

Sunday, January 23, 2011

JUMAPILI NJEMA NA WIMBO HUU CHA KUTUMAINI SINA!!!!


Haya jamani ni JUMAPILI nyingine tena na ni ya 4 ya mwaka huu yaani tangu uanze. JUMAPILI NJEMA SANA WANDUGU!!!!

Friday, January 21, 2011

JAMANI MWENZENU YAMENIKUTA LEO TENA NIMETAMANI KWELI HIKI CHAKULA KITAMU CHA NYUMBANI!!!!

Mlo huu sijala muda mrefuuuu!!
Jamani mwenzenu niko katika msimu mbaya sana, UNGA wa ugali umeniishia. Na nimepita kila duka, nimepata unga lakini ni wa njano PALENTA kwa aliyezoea ugali kama mimi haunogi kabisa. Kwa hiyo nilipoiona picha hii mate wacha yanidondoke. Hali hii inanifanya niimbe wimbo huu NARUDI NYUMBANI EEEH, NARUDI PERAMIHO, NARUDI SONGEA NAKWENDA KULA LIKOLO LA NANYUNGU..... Au labda tuusikie mwimbaji mwenyewe akiimba Marehemu Dr. Remmy Ongala


NA JAMANI IJUMAA NA MWISHO WA JUMA MWEMA. TUKUTANE TENA WAKATI MWINGINE!!!

Thursday, January 20, 2011

PICHA YA WIKI: ALA ZETU

Picha hii imenifanya nimkumbeke baba mmoja kule Madaba alikuwa akitoka Madaba mpaka Songea na Zeze yake kwa mguu. Walikuwa wakimwita Perege alikuwa akipita kila kijiji na kupiga zeze yake. Baada ya kukumbuka hivi nikaona si mbaya kama ikiwa picha ya wiki. TUKUTANE TENA WAKATI MWINGINE:-)Tanzanian traditional instruments Zeze from Martin Neil on Vimeo.

Wednesday, January 19, 2011

NAJIVUNIA NA NAIPENDA NCHI YANGU TANZANIA YENYE SIFA ZOTE!!!

Sijui kama wenzangu mmewahi kujisikia hivi, mwenzenu leo nimeamuaka na kujiona ya kwamba:- Ninaringa kwa kuwa mTanzania nchi yangu yenye sifa zote za ustaarabu.

Ninaringia rangi yangu nyeusi, macho meupe, ngozi yangu nyororo, ninapendeza na nywele zangu nyeusi na kiswahili ni lugha yangu.

Ninajivunia nchi yangu ya Tanzania yenye miji ya kuvutia iliyojengeka. Angalia Dar es salaam, Mwanza nayo Dodoma bila kusahau kwenye marashi mji wetu Zanzibar. Halafu ukienda Arusha, Tanga, Kilimanjaro, Mbeya, Iringa na Songea.

Mnajua kuna vivutio vingi ndani ya Tanzania vinavyotufanya sote tujivunie kwa mfano kuna bahari fahari ya Taifa, Ziwa nyasa, viktoria, Tanganyika pia mlima mkubwa barani afrika Kilimanjaro. Bila kusahau mbuga za wanyama Serengeti, Ngorongoro, Tarangire, Mikumi n.k

TAFAKARI YA LEO:- MAISHA

Wakati mwingine tunaweza kuyaona maisha hayana maana/hakuna haja ya kuishi. Lakini hakuna Mungu ambaye kila wakati yupo kwa kubadili hali hiyo. Tusipoteze imani /tumaini yetu/letu, kwa Mungu kwani mwisho atakuja kubadili hiyo hali. Kumbuka hata kama mti uliukata kuna tumaini /imani siku moja utaota tena.

Tuesday, January 18, 2011

JUMANNE YA LEO EBU TUMSIKILIZE DADA HUYU NA STORY YAKE!!


Maisha haya jamani......zaidi bonyeza hapa china kwa pkupata habari yote nzima.
http://www.youtube.com/watch?v=QZ8vRS_FTWM

Monday, January 17, 2011

KWA NINI WATU WANAOANA?

Kama ukimuuliza au ukiwauliza watu wanaooana, kwamba kwa nini wanaoana au ni kwa nini wako kwenye ndoa? Utapata majibu tofauti tofauti kulingana na namna watu hao wanavyotafsiri neno ndoa. Mimi sitajibu swali hilo lakini labda kile ninachokusudia kukiandika hapa huenda kikakusaidia kupata jibu la kwa nini watu wanaoana.

Kuna ukweli kwamba binadamu wamefanya kuoana kama jambo la kimaumbile, na wakilifunganisha na tendo la ndoa. Mtu anajikuta akioa au kuolewa tu. Hana haja ya kujiuliza ni kwa nini anaoa au kuolewa, kwa sababu anaona watu wanoa na kuolewa na akiangalia umri wake anaona kwamba amefikia umri wa kuoa au kuolewa hana haja ya kutaka kujua sababu. Hivi ni nani aliyepanga umri wa kuoa au kuolewa? Na umri wa kuoa au kuolewa umapangwa kwa kuzingatia vigezo gani? Je kupitisha umri huo kuna athari gani?

Ipo sababu nyingine inayotajwa kuwa watu wanoana kwa sababu wamependana, upendo ninaouona hapa ni wa mtu kumtamani mwenzie awe mwanamke au mwanaume, kwani kwetu sisi tunaamini kuwa kutamani ndio kupenda.

Hivi kama watu wanoana kwa sababu ya kupendana kungekuwa na talaka kweli? Naamini kama kungekuwa na talaka basi zingekuwa ni chache sana, na wanaoachana wasingeachana kwa ugomvi na visasi, bali wangeachana kwa upendo na wangeendelea kupendana na kuheshimiana, kwa sababau upendo ni tofauti na kutamani, upendo upo na utaendelea kuwepo na si vinginevyo.

Utakuta wanandoa wanasema “sisi tumeoana kwa sababu tunapendana” lakini baada ya mwaka wanandoa hao hawaelewani na wanakuwa na ugomvi wa mara kwa mara mpaka kufikia mmoja kumuua mwenzie, huu ndio upendo wa aina gani?

Ndoa za namna hii, hazikuwa ni za upendo bali watu kutamaniana au mtu kutamani mwili wa mwenzie, lakini kulikuwa hakuna upendo miongoni mwao.

Wengi wameoana kwa kufuata mnyororo ule ule wa kuoana kwa kufuata dhana iliyowekwa na jamii kuwa ni lazima watu waoana bila kutafuta tafsiri ya kufanya jambo hilo. Na mara waingiapo katika ndoa huona kama wamejitwisha mzigo mzito wasioweza kuubeba. Kuna zile kauli zinazotolewa ambazo wengi huita usia kwa wanandoa kwamba ndoa ni kuvumialiana, lakini watu hawajiulizi ni nini maana ya kuambiwa ndoa ni kuvumiliana, kuvumiliana kwa lipi? Kuna kitu gani katika ndoa kinachohitaji watu kuvumiliana?

Haya maswali inapaswa watu wajiulize kabla hawajaingia katika ndoa maana kuna mambo mengine hayafai kuvumilia, sasa itakuwaje nikishindwa kuvumilia? Na kuvumilia huko ni mpaka wapi?

Kuna watu wengi wanapata shida katika ndoa kwa sababu hawakujua ni kwa nini wanaoa au kuolewa, inawezekana, waliunganishwa na tendo la ndoa zaidi na sio upendo, na hapo ndipo wanpokuja kugundua kuwa walifanya makosa.

Nadhani imefikia wakati sasa ya watu kujiuliza ni kwa nini wanaoa au kuolewa, kwani ni hii itapunguza magomvi na talaka katika ndoa.Inabidi kila mtu awe na sababu yake mwenyewe ya kuamua kufanya hivyo sio kwa kuangalia sababu zilizowekwa na jamii au kusukumwa na matakwa ya jamii bali uwe ni uamuzi wake mwenyewe bila kushurutishwa au kusukumwa na matakwa ya jamii.

Kama hujaoa au kuolewa isikupe shida tulia, na ukitaka kuoa au kuolewa ufanye hivyo ukiwa na sababu yako binafsi

Sunday, January 16, 2011

NAPENDA KUWATAKIENI WOTE JUMAPILI HII YA TATU YA MWAKA HUU KWA SALA HII!!!!

Mungu nakuomba unisaidie niwakumbuke wenye njaa ninapokuwa na chakula, wagonjwa nianpokuwa na afya nzuri, wote wanaoteseka kwa sababu ya vita ninapokuwa na amani, wasio na nyumba ninapokuwa nimelala na pia kuwa ndani ya nyumba yenye joto, pia nakuomba unisaidia niwakumbuke yatima kila ninapokuwa na wazazi wangu.

Na pia nakuomba:

Bikira Maria mama wa msaada na uibariki familia yangu, kaka zangu, dada zangu, wazazi wangu na watu wote dunia hii katika dhambi: AMINA

JUMAPILI/DOMINIKA NJEMA KWA WOTE JAMANI!!!!

Saturday, January 15, 2011

JE UNAJUA HAPA NI WAPI AU HILI JENGO NI NINI?

Nimelipenda jengo hili picha kwa idhini ya kaka Jacob Malihoja.......

Friday, January 14, 2011

MAVAZI YA WANAWAKE

Nimelipenda shairi hili kwani linasema ukweli limeandikwa na Katekista Rafael Mlelwa katika gazeti la Mwenge:-

Natembea natazama, ni hali ya kushangaza,
Mitaani akina mama, mambo wanayoigiza,
Wengine watuwazima, inakuwaje nawaza,
Mavazi mnayovaa, ya aibu kinamama.

Vazi la Mtanzania, tangu kale heshima,
Watu walijivunia, wa lika zote nasema,
Haya nawasimulia, walivaa akina mama,
Mavazi mnayovaa, ya aibu kinamama.

Suruali mwavalia, mfanane na wazungu,
Asili mwaikimbia, mnanitia uchungu,
Watu wote angalia, mnamdharau Mungu,
Mavazi mnayovaa, ya aibu kinamama.

Vimini mwajibalia, mwana kama vikatuni,
Nyingine mnapasua, makusudi mapajani,
Mapaja twaangalia, pia na nguo za ndani,
Mavazi mnayovaa, ya aibu kinamama.

Siketi taiti pia, mitaani mwavalia,
Hiyoni ya kulalia, maungo yaoneshea,
Mitaani mwatembea, watu kwa kuangalia,
Mavazi mnayovaa, ya aibu kinamama.

Kweli mwatia karaha, moyoni nasononeka,
Singerendi mwavalia, maziwa yanaonekana,
Mitaani mnahaha, kutwa nzima mwazunguka,
Mavazi mnayovaa, ya aibu kinamama.

Kwa umbo mmeumbika, kwa uzuri asilia,
Uarabu mwautaka, tena kwa kujichubua,
Kama Mungu angetaka, mngekuwa Saudia,
Mavazi mnayovaa, ya aibu kinamama.

Wengine watu wazima, tena ni wake za watu,
Watoto wenu lazima, watawaigeni tu,
Malazi yao lazima yatakuwa yenye kutu,
Mavazi mnayovaa, ya aibu kinamama.

Hapa mimi nasimama, naomba mnisikie,
Wanamama wenye hekima, hali hii tukemee,
Hakika mimi nasema, tena isiendelee,
Mavazi mnayovaa, ya aibu kinamama.

Thursday, January 13, 2011

TANZANIA:- SANAA NA UTAMADUNI WETU!!!!!

Najuvunia sana sanaa zetu, utamaduni wetu, ebu angalia hapo ni kazi za mikono ya watu hizo. Mti umeguuka na kuwa umbo fulani la kupendeza, matete yamegeuka kiwa vikapu na udongo umegeuka kuwa chungu.....mmmhhh maji ya kwenye chungu,,,oh kuna kitu sina hapo ni kata sijui mnanielewa ile ya knywea maji. Weeee maji yanavyonoga kwenye kata. Tusisahau kwetu, vyetu na kuhusudu vya wengine.

Wednesday, January 12, 2011

MASWALI YA LEO:- UPENDO NI KITU CHA AJABU AU?

Mke,mume na mtoto

Mara nyingi nimekuwa nikifikiri/jiuliza:- Je? ni kitu gani kinachotufanya sisi binadamu tupendane na kisha kuamini kuwa tunastahili kuwa mke na mume?

Kumpenda mtu usiyemfahamu na kisha kuwa mume/mke wako na kisha kuishi naye. Yaani kuwaacha wazazi wako na ndugu zako. Na kuamua kufunga pingu za maisha, na halafu kuishi pamoja na mwisho kupata na watoto. Hapa ndipo ninapokuja kujiuliza ni nini kinachotufanya binadamu sisi tuwe hivyo au ni nini udhaifu wake?

Halafu sasa cha ajabu zaidi hao hao waliopendana sana sana na kuwa mke na mume kwanini baadaye hupeana talaka? Na wengine wanaweza wakawa maadui kabisa ha kuongea tu haiwezekani.

Naomba ndugu wasomaji tusaidiane kupata majibu najua palipo na wengi hapaharibiki neno…..au nisema UMOJA NI NGUVU ……KAPULYA WENU.

Monday, January 10, 2011

KAMA MVI NI KIPIMO CHA BUSARA, NI KWA NINI ZIFICHWE??

Mbona Profesa Mbele anazo mvi lakini hazifichi?

Habari zenu wasomaji/wandugu na wengine wote. Ni Jumatatu nyingine au niseme ni jumatatu ya pili ya mwaka huu na pia ni wiki ya pili .Basi mwenzenu nimeamka nikiwa na wazo hili la MVI au niseme nimeota nina mvi kichwa chote. Ndo nikakumbuka kuwa mwaka hjana niliandika makala na nimeona niiweke tena hapa. Kwani mimi naamini mtu unaporudia kusoma aidha kitabu au habari fulani ndiopo unapozidi kujifunza haya karibu sana......
Mvi ni dalili ya uzee au ni kitu gani? Kwa zamani ingekuwa ni muhali mkubwa mtu kuuliza swali la aina hii, kwa sababu mvi zinahesabiwa kama dalili ya busara, bila shaka zikihusianishwa na kuona mengi ambayo ni wenye umri mkubwa tu waliokuwa na nafasi hiyo.
Lakini leo, mvi ni kisirani na karibu kila mtu anajaribu kuzikimbia, kwani kuendalea kuwa kijana ni sifa kubwa. Kwa sasa uzee unanuka na kila mmoja anajaribu kuukimbia kwa njia mbalimbali ikiwemo ya kukana umri na kujirudisha nyuma kimatendo. Kwa kifupi hii ndiyo historia ya mvi, usiziogope bure!
Karibu rangi zote asilia za nywele zinatoka kwenye kitu kiitwacho melanin, ambacho huzalishwa na mwili kutokana na seli zinazofahamika kama melenocytes. Nywele zinapobadilika na kuwa nyeupe ina maana kwamba, melenocytes haizalishi tena melanin. Mabadiliko haya ya nywele kutoka rangi nyeusi na kukosa rangi (mvi) siyo hatua ya siku moja bali mwaka na miaka, kwani nywele moja hubadilika baada ya muda mrefu na nyingine na nyingine. Siyo hatua ya siku moja tu.
Kwa kadiri mtu anavyozeeka ndivyo ambavyo uwezo wa mwili kuzalisha melanin unavyopungua. Uwezo huu huanza kupungua mtu anapofikia umri wa miaka 35 au 40. Lakini watu wengine huanza kuota mvi wakiwa na umri wa miaka hata 20 tu. Je, hii nayo inatokana na nini?
Hili kusema kwali siyo jambo la ajabu. Ingawa kuna watu ambao huwa wanalishangaa. hata hivyo wana sayansi wanasema kwamba hawajaweza hasa kujua ni kwa sababu zipi uwezo wa mwili kuzalisha melanin huwa unashuka. Lakini wana uhakika kwamba wale wanaoanza kuota mvi kabla hawajafikisha umri wa miaka 35, kwa sehemu kubwa wanaathiriwa na urithi au kizalia.
Kama mtu ataona kwamba anaanza kupata mvi mapema sana ni dhahiri kwamba akiangalia kwenye familia yao atakuta kuna mtu ambaye naye alianza mapema kuwa na mvi. Hii itasaidia kumuonyesha kwamba mvi zake ni matokeo ya kizalia.
Pengine ni jambo la ajabu kwamba kuvuta sigara kunatajwa kama sababu ya kuchochea mtu kupata mvi akiwa na umri mdogo. Ukiwachunguza wavuta wazuri, utagundua kwamba wameanza kuota mvi mapema kuliko umri wa miaka 35 au 40.
Matatizo kwenye kiungo kinachodhibiti ukuaji mwilini, yaani thyroid huweza pia kusababisha mtu kupata mvi kabla ya kufikisha umri wa miaka 35. Pia ukosefu wa vitamin B12 unatajwa kwa sababu nyingine.
Kuna watu ambao hata kama wana umri wa miaka 60 bado hawataki kuona nywele nyeupe vichwani mwao . Watu hawa huangaika huku na kule kutafuta dawa kuondoa mvi na pengine kutumia rangi ya nywele ili kufanya rangi ya nywele nyeupe zisionekane. Huu ni kama mwendawazimu kwa kiasi fulani. Kwanini?
Kwanza kuna ukweli kwamba nyingi kati ya hizo zinazodaiwa kuwa rangi za kuondoa mvi, zina athari katika mwili wa mtumiaji. Lakini wendewazimu mkubwa zaidi ni kitendo chao cha kukataa ukweli ambao inabidi waujivunie.
Mvi bado ni dalili ya busara. Kama umefikia umri wa kuota mvi na hujafanya jambo lolote la maana na hujatoa mchango wowote wa maana kwa familia yako au jamii unamoishi ni lazima utaficha mvi zako. Kwanini?Kwa sababu utaona haya sana kuonekana kwamba umri wako ni mkubwa lakini hujafanya lolote. Tunaposema mchango wa maana hatuna maana ya fedha au mali, bali zaidi tuna maana ya mawazo ya kujenga na pengine kuandaa misingi ya kujenga kwa nia ya kuleta maendeleo baadaye.
Hebu chunguza kwa makini, utagundua kwamba watu wote wanaojaribu kuficha mvi ni wale watu ambao wametawaliwa sana na vionjo na tamaa ya miili yao kuliko maendeleo ya binadamu. Ni wale watu ambao hata kama wana fedha, hawajajua hasa wako hapa duniani kwa sababu gani. Hivi ndivyo ilivyo kwa sababu watu wa aina hii huhofia sana umri, huhofia sana kufa kwa sababu hawajakamilisha walichokuja kukifanya duniani kwasababu hawajajua bado.
Kukosa kujiamini na kujikubali kwamba wewe ni fulani na uko katika hali fulani na kiwango fulani hupelekea watu wengi kubadili majina, kuchukua makabila yasiyo yao, kujiita maarufu au kuongopa kuhusu maisha yao kwa ujumla. Mtu anayejaribu kuficha mvi ili asijulikane kwamba ana umri mkubwa hana tofauti na watu hawa.
Mtu ambaye anajiamini hawezi kuogopa kutaja umri wala kuonyesha kwamba ana umri mkubwa. Na mtu hawezi kujiamini kama hajijui yeye ni nani na kujijua kunataka mtu asiishi kwa kutazama wengine watamuonaje, bali anajionaje.
Kuficha mvi inaweza kuwa ni dalili ya mtu kuvuka kipindi fulani bila kufanya mambo ambayo kisaikolojia alitakiwa kuyafanya wakati huo. Kama mtu alitakiwa kufanya mambo hayo katika umri wa miaka 20 hadi 25 na hakufanya, kuna kawaida ya mtu kama huyo kuja kutaka kuyafanya akiwa na umri wa juu zaidi.
Kwa kuwa wakati huu mvi ni dalili kwamba ameshapita umri wa kufanya mambo hayo, atahakikisha kwamba dalili hii inafunikwa au kufutwa ili isimfedheheshe. Wengi wetu tunawajua wa waficha mvi na vituko vyao huko mitaani kwetu. Habari hii chanzo ni Jitambue.......
Na haya yalikuwa baadhi ya maoni ya wasomaji.....
Mbele said...
Dada Yasinta, shukrani kwa mada yako. Nikiwa ndio mwenye hii sura hapo juu, ngoja nijikongoje niseme moja mawili.

Kwanza naona mada yako imejaa mawazo ya kufikirisha. Ni changamoto nzuri, kwa jinsi ilivyogusia vipengele vya kimaumbile, kiafya, kisaikolojia kijamii, na kitamaduni.

Ili kuanzisha mjadala, napenda tu kusema kuwa mimi nilizaliwa na kukulia kijijini. Pamoja na miaka yote niliyosoma na kufundisha, Tanzania na ughaibuni, katika nafsi yangu najitambua ni mtu wa kijijini. Mila na desturi za kule ndizo zinazogusa roho yangu na kuongoza maisha yangu.

Kuhusu mvi, ni kuwa katika utamaduni wetu wa ki-Matengo, mvi zina maana sana, kama ulvyogusia. Ni ishara ya uzee, na kwa vile uzee unahusishwa na busara zinazotokana na umri mkubwa na kuona mengi, basi unapokuwa na mvi unajikuta ukiwa na wajibu wa kuishi na kufanya mambo kufuatana na mategemeo hayo.

Mvi zinanikumbusha wajibu wa kuishi kwa misingi hii niliyoitaja. Ndio maana mtu mwenye mvi akifanya jambo ambalo haliendani na hadhi hiyo, watu wanalalamika: "Huyu mzee na mvi zote hizi kwa nini amefanya hivi!"

Mvi zinanichunga na kunikumbusha wajibu wangu.

Nafahamu fika kuwa tuna tatizo la watu kuigaiga mambo kikasuku. Kwa mfano, huku Marekani, watu hawathamini uzee. Hamu ya kutaka kuonekana vijana zimetawala maisha ya watu. Sitashangaa iwapo mawazo hayo yataenea katika nchi yetu, kwa jinsi watu wanavyozidi kuwa kasuku wa mambo ya nje, hasa Ulaya na Marekani.

SIMON KITURURU said...
Mie kama mtu mwenye mvi tokea ze utoto kikubwa nilichokuwa nastukia ni watu kushangaa kuwa kwanini namvi.

Na sifichi kuna miaka fulani nilikuwa najaribu kuzing'oa.:-(


Ila siku hizi[aka miaka kibao] umri umekwenda na sichani nywele basi nastukia ZAIDI watu wengi wanashangaa kwanini sichani nywele zaidi ya kustukia nina mvi.

Ila sikubali kuwa kila wenye mvi wazifichao ni kwa sababu ya kukana umri kwa kuwa naamini ukienda UMRI hata ufanyaje unajulisha tu kwa kuwa sio mvi bali mwili mzima kuna namna unageuka na kujulisha tu UMATI kuwa weye MKONGWE ingawa una bonge la kalikiti na na panki lisilo na masihara.


Na kuna watu mvi hazijagawanyika vizuri kichwani .Kwa hiyo utakuta kitita hapa na kitita pale na mvi kadhaa moja moja kule ,...- kitu ambacho kuna niwajuao wenye mvi wenzangu ambao huonekana kama wana nywele chafu kitu ambacho huwafanya kuziweka rangi ili zote ziwe sawa. Kumbuka pia sio mvi zote nyeupe pee kwa baadhi ya watu .

Ukiniuliza miye ntasema kila mtu na staili yake ajisikiavyo kama unajisikia unapendeza zaidi kwa kuwa na nywele za rangi ya kijani na hazikuharibii kazi au kukutafsiria vibaya nini ni maisha yako kuwa utakavyo .

Kwa kuwa maisha yenyewe ya binadamu mafupi na yana fulu matatizo na kama hutaki uonekane unakipara na wigi lenye mvi halipatikani dukani,... vaa tu WIGI lenye rangi nyeusi tii hata kama una miaka themanini ikiwa kwa hivyo angalau siku kadhaa maishani mwako LINAKUFANYA unadunda mtaani umekenua meno kwa furaha.

Na kwa bahati mbaya miye na mvi zangu watu hawakosei sana umri wangu ki hivyo bado !:-(

Kama mvi ni kipimo cha BUSARA ni kwanini zifichwe?

Kumbuka kuna matatizo mengine ya watu ni uke na nawala sio busara ndio matibabu.:-(

Mzee wa Changamoto said...
Tatizo ni kuwa sasa hivi ni vitu vichache saana vijavyo kwa sababu za asili. Hivi sasa hata ukimuona binti huamini kama ni yeye. Kama ni wale wadanganywao kuwa ni "wazuri", basi adhaniaye hivyo bado atajiuliza kama ni "uzuri" wake ama wa maabara. Na pengine kujiuliza kama alizaliwa akiwa mdada ama alibadili jinsia.
Sababu ya kutothaminika kwa mvi ni kwa kuwa zaweza kumpata hata Paulina mwenye miezi sita kwa kuwa yasababishayo mvi sasa ni mengi (kama ambavyo umetaja baadhi).
Pengine ni wakati wa kutoficha kilicho nje na kwa walio nje kutotumia mtazamo wa nje kumjua mtu.
Ni hayo kwa sasa
Tuonane NEXT IJAYO

EDNA said...
Hhahaa Da Yasinta umenikumbusha Mjomba wangu,yeye anamvi na umri umekwenda kidogo, lakini kamwe hawezi kuziachia watu wazione.

Atanyoa nywele zote au atapaka dawa ya kufanya nywele ziwe nyeusi....Baada ya mada hii imeniamsha itabidi siku nikienda TZ nimuulize kisa na mkasa cha yeye kuficha mvi.

Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti! said...
Jamani miye napenda sana MVI lakini ukijitokeza hata u-mvi mmoja tu kuna mtu ananimonita na akiuona tu anasema hataki nionekane MZEE :-(

Sasa naomba walau ziote miguuni ili niwe naziona nikivua suruali...lol!

Tatizo ni kuwa wengi wetu tunaoficha mvi ni kwa sababu ya kutojiamini kama makala inavosema.

Kuna wengine:
1. Wakionekana na MVI wakisema umri wao utasikia mtu anamaka 'mie nilidhani mzee kumbe TOTO DOGO tu?' Hivo wale ambao hawataki kuonekana WATOTO bali wakubwa sasa wanaficha mvi kama ukoma!

2. Wakionekana na mvi hawatai kuwa wazee. Wanataka kuwa vijana na japokuwa umri unawatupa utaona mambo yao wanayofanya ni ya vijana na hata watoto.

Nakubaliana na Mzee Mbele (ktk medani ya elimu nadhani Prof=Mzee....lol) kuwa Mvi zinakumbusha majukumu ya mtu ktegemeana na mazingira (kabila na sehemu).

Tuko pamoja.

Yasinta Ngonyani said...
Kisa cha kuandika mada hii kwanza kabisa niliipenda nilipokuwa nasoma na pia ni kwa sababu mimi mwenyewe pia nimeshaanza kupata mvi miaka mitatu iliyopita. Na leo asubuhi nimeamka na nikaanza kujiangalia kwenye kioo....lol , nikaona uweupe wacha nishtuke nikaanza kuwaza hivi ni kweli nimefikia umri wa kupata MVI? Maana kuna usemi usemao ukiwa na MVI basi ni dalili ya uzee....lol. Ndo sababu nikaona ni lazima niiweke hii mada hapa ili kupata jibu sawasawa ingwa jibu nimelipata lakini inaweza majibu yakatofautiana.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...
sasa unamaanisha huyo pichani anaficha mvi???

hapo zamani ni kweli mvi zilikuwa kipimo cha busara lakini leo hii sio hivyo tena! nikiwatembelea wazee wabgu kama wajomba, dingwadogo, maza, bibi, majirani nk woote husinngizia utu uzima wao na nisipowapa pesa watanilaani

sasa nimewaonya wote wasemao watanilaani kwani mimi naweza kuwalaani kabla wao hawajafanya hivyo nani kasema laana anayo mwenye mvi tu?? \\

harafu sitaki usumbufu eti kwa sababu una mvi,

ila mvi sio kipimo tena cha busara au maarifa kama ilivyokuwa zamani kwani siku hizi maarifa yote na utajiri v imo mikononi mwa vijana na wenye mvi wanategemea huruma ya vijana

ila kuficha mvi ni uchizi, ni ujinga, ni kujikataa nk

PASSION4FASHION.TZ said...
Kuwa na mvi inategemea unaweza kuwa na mvi kuanzia umri mdogo kama alivyosema kaka Simon,pia unaweza kuwa na mvi ukianza kupata umri mkubwa, na pia inategemea na ukoo,kuna ukoo mwingine mvi huanza kuota wakifikisha miaka 20tu,mvi hizo zinaanza sasa hapo huwezi kusema ni uzee.

Pia kuna aina ya nywele ambazo huanza kuota mvi mapema, na kuna ambao hupata mvi kutokana na aina ya mafuta unayotumia.

Kwahiyo kuota mvi au kuwa na mvi sio lazima uwe na umri mkubwa tu,inategemea.

SIMON KITURURU said...
Heri ya Pasaka DADA YASINTA!

Yasinta Ngonyani said...
Napenda kuchukua nafasi hii na kuwashukuru wote kwa maoni yenu mazuri na piakwa kutochoka kutembelea hapa kibarazani kwangu MAISHA NA MAFANIKIO. UPENDO DAIMA!!

Sunday, January 9, 2011

LEO NI JUMAPILI YA PILI YA MWAKA 2011:- JUMAPILI NJEMA NDUGU ZANGU!!!


NAWATAKIENI WOTE JUMAPILI HII YA PILI YA MWAKA HUU IWE NJEMA NA AMANI!!

Saturday, January 8, 2011

TUNAWAEZI VIPI WATANZANIA WALIOTUWEZESHA KUFIKA HAPA TULIPO

Tanzania yetu


Habari ya Jmosi,
Nimeguswa sana na ujumbe wako wa kutakiwa kujivunia makabila yetu,kutokana na ujumbe huu likanijia wazo la kuenzi mambo mema yaliyofanywa na watu mbalimbali katika Nchi yetu ya Tanzania mpaka tukawa wamoja.

Kutokana na hilo nikazikumbuka nyimbo mbili ambazo tulikuwa tunaziimba sana shuleni katika miaka 1970-1980,na nikaona tuna kila sababu ya sisi watanzania popote tulipo kuona kuwa tunachangia kwa namna moja au nyingine katika kuhakikisha nchi yetu inaenedelea kuheshimika na kustawi kiuchumi. Nadhani ni jukumu la kila mtanzania popote alipo kujiuliza yeye ana mchango gani katika kuona kwanza familia yake inastawi kiuchumi na kijamii(maendeleo kwa ujumla) na kwa kufanya hivyo mwishowe tutaifanya Tanzania kustawi. Nimetanguliza kusema kuona jinsi gani familia yako inastawi maana siku hizi kuna msemo unasema Kitu kinachoitwa UZALENDO kimeondoka miongoni mwa Watanzania badala yake kuna kitu kinachoitwa UBINAFSI ambacho kinachukua nafasi ya UZALENDO. Lakini pamoja na ubinfsi kuchukua nafasi naamini kwa kuiwezesha jamii inayokuzunguka,ukoo na familia utakuwa unachangia katika ustawi wa jamii nzima na hatimaye Nchio.
Nabandika na nyimbo mbili tulizokuwa tunaziimba na kutuhamasisha ili ujikumbushe enzi hizo na kuona ni kwa jinsi gani tunawaenzi watunzi wa nyimbio hizi kwa kuifanyia Tanzania kile wao walichokuwa wanakifikiria kupitia katika nyimbo hizo

WIMBO WA HALAIKI WA TANZANIA

1.Tanzania,Tanzania,nakupenda kwa moyo wote;
Nchi yangu Tanzania,Jina lako ni tamu sana;
Nilalapo nakuota wewe,niamkapo ni heri mama we;
Tanzania,Tanzania,nakupenda kwa moyo wote;

2. Tanzania,Tanzania,ninapokuwa safarini;
Kutazama maajabu,biashara nayo makazi;
Sitaweza kusahau mimi,mambo mema ya kwetu kabisa
Tanzania,Tanzania,nakupenda kwa moyo wote.

3. Tanzania,Tanzania,watu wengi wanakusifu;
Siasa yako na destruri,ilituletea uhuru;
Hatuwezi kusahau sisi,mambo mema ya kwetu hakika
Tanzania,Tanzania,nakupenda kwa moyo wote.

Wimbo wa pili unahusu Tanzania nchi nzuri.

1.Tazama ramani,utaona nchi nzuri,
Nchi hiyo mashuhuri inaitwa Tanzania,

2.Nasema kwa kinywa halafu kwa kufikiri;
Nchi hiyo mashuhuri inaitwa Tanzania,

3. Nchi hiyo imejaa mabonde,mito na milima;
Majira yetu haya yangekuwaje sasa,
Utumwa wa nchi Nyerere ameukomesha
Nchi hiyo mashuhuri inaitwa Tanzania.

Nakutakia Jmosi Njema. Na kaka Salehe Msanda Njombe.

Friday, January 7, 2011

SHUKRANI ZANGU KWA DA´MIJA NA WENGINE WOTE!!!

Sijui nianze vipi? Ngoja nianze hivi AHSANTE sana kwa kunipa heshima hii kubwa katika blog yako na kwa vile macho yangu kwa sasa yamejaa machozi ya furaha basi sitasema mengi. AHSANTENI, Ah nimeipenda HESHIMA hii na napenda iwe moja ya kumbukumbu ambazp sitasahau maishani mwangu ndio maana nimeona niiweka hapa MAISHA NA MAFANIKIO ili iwe karibu nami. Kwa mara nyingine tena AHSANTENI SANA!!!!


Ninachomheshimia Da Yasinta..


Wadau jana mwanablogu mwenzetu Yasinta Ngonyani alisherehekea siku yake ya kuzaliwa. Nilifikiria nizawadie nini nikaona ni bora nimpe tuzo ya kuwa mwanamke wa shoka wa wiki hapa bloguni. Haikuishia hapo nikawa nimetoa changamoto kwamba kuna sababu nyingine iliyonifanya nimchague kama mwanamke wa shoka, nashukuru wadau mliochangia kwani hii ni njia bora ya kutiana moyo pia.
Sasa ngoja nami niseme kinachonifanya nimuheshimu huyu dada.

Kwanza kabisa, ni uwezo wake wa kuhakikisha karibu kila siku anabandika kitu bloguni kwake tena chenye ubunifu, Yasinta kwa hilo nakupa hongera sana.
Pili, ni hili ambalo kaka M-3 pia amelisema, ni uwezo wake wa kutembelea blogu nyingi na kutoa maoni, kuna wakati huwa nakutana na blogu mpya kabisa nikizifungua nakuta Yasinta alishapita tena siku nyiiingi. Kubwa zaidi mtu ukipotea bloguni ni lazima akuulizie na akiona kimya Yasinta hurusha e-mail...! Yasinta hii inaonyesha jinsi ulivyo na moyo wa utu kwa wengine...
Kwa kweli kwa hayo na mengine waliyoyasema wachangiaji waliopita, sina budi kusema YASINTA WE SALUTE YOU!!! UNA MOYO WA UPENDO KWELIKWELI UNAOTAKIWA KUIGWA.
UBARIKIWE SANA.


Hapo chini ni wachangiaji walivyomuelezea Yasinta..

mimi nafikiri ume mbandika kwenye blog yako,kutokana namichango yake katika blog mabilimbali.pia nayeye kama mwanamke, mtanzania kwa kiasi fulani ameonyesha nia ya kuwakomboa wanawake wenzie hasa kwa misimamo yake,hisia zake, nahata uwazi kwa upande mwingine.pia ni mdada ambaye anajiwakilisha yeye kama yeye katika blog kwa kuamini kile akiandikacho,ambacho uhodari huo wa kuthubutu ni njia moja wapo ya mwanamke kujitambua, kuwa yeye ninani,nahtimaye kujikomboa, kimawazo,fikra na vitendo.ingawa nikimwangalia Yasinta,alikotoka ni mbali sana nahata kufikia hapo alipo umejitahidi.ombi kwako,unajuwa mchezo wa KOMBOLELA unavyo chezwa,butuua......uwakomowe wenzako. kaka sam

emu-three said...
MIMI NAMHESHIMU SANA HUYU DADA. Nasema namheshimu kwa sababu ya `ucheshi wake' udadisi wake na ni mtu wa watu, kama angekuwa Tanzania ningemshauri agombee ubunge.
Siku moja nilisema ngoje niwe wa kwanza kuwatembelea wenzangu kwenye blog zao, cha ajabu kila nilipopita nilimkuta keshafika...ana upendo na watu na anajali sana kazi za wenzake, ndio maana lazima aache ujumbe kukupa moyo.
Mimi nimshukuru sana kwani alinipa moyo kwenye `kijiwe' changu, nilikuwa nimekata tamaa kabisa, unaandika watu hawafiki hawachangii, lakini akanipa moyo na hata kunisaidia kunitangaza. NAMSHUKURU SANA NDIO MAANA NASEMA NEMHESHIMU KAMA DADA YANGU!
Ahsante na Da mija na wewe ni miongoni mwao!

Swahili na Waswahili said...
Mimi namkubali sana kwa mengi nikiandika hapa unaweza kunistopisha!
kifupi amejaaliwa upendo,utuwema,busara,

Anastahili kuwa mwanamke wa wiki na zaidi!na mengi ya kuigwa kutoka kwake!

Nakupenda dada Mkubwa Yasinta binti wa Ngonyani!!!!!!!!!.

John Mwaipopo said...
naona utufumbulie fumbo wewe mwenyewe

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...
si mwanamke! anasuka harafu ana blogu! mimi kule kwetu naowaona wengi wanaopaswa kuwa wa wiki ila hawana blogu! ila yasinta si anaishi ulaya?
Makala hii imeandikwa na Da mija ukitaka kumsoma daidi gonga hapa

Thursday, January 6, 2011

MAKABILA YETU NCHINI TANZANIA

Ndugu zangu wapendwa leo nataka kusema kitu ambacho kimekuwa kikinikera sana. Ni kuhusu makabila yetu, mnajua ya kwamba nchi yetu Tanzania ni nchi pekee yenye makabila 129-130? Nasikitika sana kuona/kusikia baadhi ya watu huwa wanayakana makabila yao.

Kwa mfano utasikia mtu anasema mimi si mngoni, mimi siwezi kingoni kwanini kukataa uwewe? Uasili wako? KWANINI???

Nawaambia ukweli binafsi najivuna sana kuwa MNGONI na nilipenda kabila langu pia mila zake. Nachukua nafasi hii kumshukuru kaka Matondo kwa utundu wake ingia hapa ufaidi uhundo kwa wale/yule ambaye hajajua na pia wale waliojua si mbaya kujikumbusha. Mimi binafsi nimefaidi na ninaendelea kufaidi kwa mfano gonga hapa yaaani mpaka raha!!!!

Wednesday, January 5, 2011

LEO NI SIKU YANGU YA KUZALIWA

Napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunilinda salama mpaka kufika siku hii ya leo na kuongeza limwaka limoja zaidi. Namshukuru kwa kuniepusha na mambo mabaya, magonjwa na pia vishawishi. Kijana wangu Erik amepata nafasi kuchagua hii picha anasema ameipenda.

kutimiza miaka bila mziki hapana. Haya wote UNGANENI NAMI NA WIMBO WA TUSELEBUKE NI KITOTO/LIZOMBE....


Namshukuru Mungu kwa yote, familia yangu pia ninyi marafiki zangu!!!

Tuesday, January 4, 2011

UJUMBE WA JUMANNE HII!!

Tunahitaji kupendana na kutambua kuwa sote ni ndugu
Sijui ninyi wenzangu mmewahi kufikiria kuwa:- Kuna/ni hisia za pekee kujua kuwa kuna mtu anakupenda, kuwa kuna mtu anakutamani, kuwa kuna mtu anakuhitaji. LAKINI kati ya vyote ni hisia za pekee kujua kuwa kuna mtu KAMWE hatakusahau. Huu ni ujumbe wangu wa leo mnapendwa wote , ahsanteni wote kwa uwepo wenu. UPENDO DAIMA.


Monday, January 3, 2011

HONGERA KWA SIKU YA KUZALIWA KAKA MFALME MROPE


Nakutakia kila la kheri sio leo tu ila kila wakati utakapofanya jambo/mambo yako. Kaka huyu anapatikana hapa. HONGERA SANA KWA SIKU YAKO YA KUZALIWA!!! .

Sunday, January 2, 2011

JUMAPILI YA KWANZA YA MWAKA 2011/JUMAPILI NJEMA WANDUGUNi jumapili ya kwanza ya mwaka. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunilinda mpaka leo hii. JUMAPILI NJEMA JAMANI

Saturday, January 1, 2011

UJUMBE/WOSIA KUTOKA KWA BABA YANGU WA KWA MWAKA MPYA 2011

Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunilinda toka mwaka jana mpaka mwaka huu mpya. Bado ninawaza kama nilivyowaza nilipokuwa mwaka mmoja . Kwa nini hakubadiliki rangi kama ni mwaka mpya?
Nachotaka kusema ni kwamba: Nina ujumbe ambao nimepewa na baba yangu leo katika kuuanza mwaka huu 2011. Kwanza aliniuliza Kama najua Mungu ameiumba kwa kusudi gani?
Nikashindwa kumjibu na yeye akasema atanisaidfia kujubu.na majibu yaka ni haya:-
1. Kujua yeye ni muumba wetu.
2. Tumpende kuliko vitu vyote.
3. Tumtumikie kadiri ya wito wetu.
4. Na mwisho ni kwamba ili tuweze kufuka mbinguni.

Halafu akaendelea kunieleza ni kwamba Mungu anajua kama unamtendea kama unamtendea wema na si lazima uende kanisani ndo kumtendea Mungu mema hapana . Ni kwamba unaweza kumtendea jirani yako kitu na hapa ndipo utakuwa umetenda jema, kumwona mtu kama alivyoo, kumwalika/tembela mtu asiye na uwezo.nk nk. maneno haya yamenipa tafakari sana na nimeona niweka hapa ili mnisaidie kutafakari ujumbe huu.