Showing posts with label asifiwe. Show all posts
Showing posts with label asifiwe. Show all posts

Sunday, March 23, 2014

KUMBUKUMBU...LEO NI MIAKA MITATU TANGU MPENDWA WETU ASIFIWE NGONYANI ATUTOKE

ASIFIWE WAKATI WA UHAI WAKE
Ni vigumu kuisahau tarehe 23/3/ 2011, siku hii ndiyo tuliyompoteza mpendwa wetu Asifiwe Ngonyani. Na leo imetimia miaka mitatu tangu ndugu yetu mpendwa Asifiwe atutoke. MWENYEZI MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU MAHALI PEMA. AMINA.....TUTAKUKUMBUKA MILELE....

Saturday, March 23, 2013

KUMBUKUMBU...LEO NI MIAKA MIWILI TANGU MPENDWA WETU ASIFIWE NGONYANI ATUTOKE

ASIFIWE KATIKA UHAI WAKE NYUMBANI RUHUWIKO
Ni vigumu kuisahau tarehe 23/3/ 2011.Imetimia  miaka miwili leo tangu ndugu yetu mpendwa Asifiwe atutoke.MWENYEZI MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU MAHALI PEMA. AMINA.....TUTAKUKUMBUKA MILELE....

Saturday, November 26, 2011

LEO NI 26/11/2011 NDIYO SIKU ALIYOZALIWA ASIFIWE NGONYANI

Tarehe 26/11/1989 ilikuwa siku ya furaha kwa familia ya Ngonyani kupata binti mwingine ambaye ni Asifiwe. Ni hisia za ajabu sana mwaka huu bila kumpigia simu na kumtakia HERI kwa siku yake ya kuzaliwa ambayo ni leo. Na hii ni sababu kubwa nikaona wiki nzima iwe yake kwa vile imekuwa wiki ya matukio matatu kwa mpigo. Kweli Mwenyezi Mungu ndiye muweza ebu jaribu kuangalia Asifiwe alizaliwa 26/11/1989 siku ya jumapili ,na leo na jumamosi 26/11/2011 ange/ametimiza miaka 22 halafu sasa siku aliyozikwa ni 26/3/2011 siku ya jumamosi tena…HONGERA KWA SIKU YA KUZALIWA MDOGO WETU,DADA YETU,MAMA MDOGO WETU, SHEMEJI YETU, PIA RAFIKI YETU. NA USTAREHE KWA AMANI, TUTAKUKUMBUKA DAIMA.
UA HILI NIMETUMIWA NA KAKA ISSACK CHE JIAH AMBAYE PIA NI MSOMAJI WA MAISHA NA MAFANIKIO. AHSANTE SANA.

Wednesday, November 23, 2011

TUTAKUKUMBUKA DAIMA ASIFIWE NGONYANI!!!

Kwa vile leo ni JUMATANO NA NI JUMATANO YA KIPENGELE CHA MARUDIO YA mada/makala/matukio mbalimbali. Basi JUMATANO YA LEO imeangukia kuwa tarehe 23/11 ambayo si mara nyingi inakuwa hivi. nasema hivi kwasababu 23/3/2011 siku ya jumatano tuliondokewa na mpendwa wetu Asifiwe na leo imetimia miezi nane na imeangukia siku ya jumatano na tarehe 23/11-11 kusema kweli nimeshikwa na butwaa kidogo maana si mara nyingi inakuwa hivi. Kwa hiyo nimeona si vibaya kama tukimkumbuka Asifiwe wetu.

Hapa ndipo mahali alipopumzika Asifiwe katika safari yake ya mwisho. TUTAKUKUMBUKA DAIMA ASIFIWE.KWANI UPO NASI KIROHO ILA SI KIMWILI. PUMZIKA KWA AMANI MDOGO WANGU/WETU.

Tuesday, November 22, 2011

ASIFIWE NGONYANI (1989- 2011). Kioo kingine cha maisha yetu, kwa maisha yetu na wenzetu

Kama jana jumatatu nilivyosema ni wiki ya kumkumbuka mdogo wangu Asifiwe Kwa hiyo nimeona si mbaya kama tukimkumbuka Asifiwe kwa mada hii iliyoandikwa na Mzee wa changamoto.

"..see you in ZION, holding hands together standing by MY FATHER'S SIDE. Meet you in ZION singing songs together....." LUCIANONi mwaka mmoja na siku 24 tangu ilipobandikwa MAKALA HII YA KUMSHUKURU MUNGU KWA KUFANIKISHA UPAUSAJI WA Dada Mdogo Asifiwe Ngonyani. Leo hii NAMSHUKURU MUNGU kwa maisha na mapumziko ya Dada Asifiwe, ambaye aliaga dunia Machi 23 na kuzikwa Machi 26.Dada wa Asifiwe, ni Da Yasinta Ngonyani. Sio bloga mwenzangu tu, bali ndiye anayewasiliana na familia yangu kuliko bloga yeyote. Twawasiliana kwenye chat, kwenye simu na hata skype ambapo huwa tunaongea mara kwa mara.Mara nyingi tumezungumza kuhusu Asifiwe.Na kila mara alikuwa akitujulisha maendeleo yake. Na kwa kila wakati ambao afya ya Da Asifiwe ilikuwa ikihitaji msaada wa uangalizi wa watabibu, Da Yasinta alikuwa mnyonge. Na nakumbuka siku ambayo alisema hakuweza kuweka bandiko kwenye blogu yake kwa kuwa hakuwa na furaha. Baadae tukawasiliana kuwa ameweza kuongea na Asifiwe na alikuwa na furaha kusika maendeleo yake ni mema.Lakini juma hili, taarifa zimefika kuwa ASIFIWE HATUNAYE. Binafsi niliumia sana. Nilikuwa sijapata kuonana na Asifiwe, lakini mazungumzo juu yake kutoka kwa Dadake na Da Koero yalinifanya kuwa karibu naye kwa namna ya pekee.Lakini kwa wote hawa (Yasinta na Koero), nililogundua ni namna ambavyo FURAHA ZAO ZILIATHIRIWA NA HALI YA ASIFIWE. Kwa maongezi nao, niligundua juu ya maisha yake ambayo ndicho kilikuwa kivutio kikubwa kwa ndugu zangu hawa ambacho ni TABIA. Da Yasinta hakuwa tu akimzungumzia Asifiwe kama ndugu yake ambaye ni wao wawili pekee wa kike katika familia, lakini alikuwa akimzungumzia kama RAFIKI.NA HILI NDILO NILILOJIFUNZA NA NINALOJIFUNA.Ninapomuwaza ASIFIWE, nikimuwaza Dada Yasinta na dugu, jamaa na marafiki wakimlilia, naona AKISI YA MAISHA YA ASIFIWE. Naona jambo ambalo sisi sote twatakiwa kujifunza kutoka kwa Asifiwe, kisha kuona maisha yetu na ya wali walio kwetu yakibadilika.KILIO cha kumlilia Asifiwe ni ishara nyingine kuwa alipendwa, na licha ya kuwa ni KAZI YA MUNGU kumpumzisha baada ya kuyagusa maisha yetu kwa namna alivyoyagusa, bado tungependa kuendelea kuwa naye.Nakumbuka Juni mosi mwaka 2009, NILIBANDIKA MAKALA HAYA KUHUSU KILIO CHANGU KWA MJOMBA WANGU, ambaye nililia kwa kuwa nilimlilia, na katika makala hiyo, niliandika kuhusu kilio cangu kwa mjomba kuwa "nililia kwa kuwa kwa tafsiri yangu, kulia ni kutokubali kuwa wakati wa mjomba kupumzika ulikuwa umefika na hakika alistahili kupumzika baada ya kutenda mema mengi tena kwa mapambano ya hali ya juu. Mjomba alikuwa mtu mwema kwangu na kwa wengi..." Mtu wa kwanza kutoa maoni kwenye bandiko hilo (kama ilivyo kwa mabandiko mengi kwenye blogu nyingi) ni Dada yangu Yasinta ambaye alisema "Mzee wa Changamoto pole sana tena sana. Nalia pamoja nawe kwani nakuelewa kabisa. Na nakushauri lia sana kwani kulia ni moja ya kutoa uchungu wako. Natumanini Mjomba wako yupo nawe kila siku amini. Astarehe kwa amani."Leo hii nami namkumbuka Asifiwe, na licha ya kuwa NAMLILIA, bado nakumbuka kuwa ALISTAHILI KUPUMZIKA na kuwa aligusa maisha ya waliohusiana na kuishi naye na yetu tuliomfahamu kupitia ndugu na marafiki.Lililo kubwa kwetu tuliobaki, ni kuishi maisha sahihi na maisha yaliyo mema. Kama ambavyo aliishi ASIFIWE NGONYANI....Na ndio maana (kama kisemavyo kichwa cha post) namuona "ASIFIWE NGONYANI kama Kioo kingine cha maisha yetu, kwa maisha yetu na wenzetu"Chris Rice anasema....COME THOU FOUNT

AHSANTE MZEE WA CHANGAMOTO/KAKA MUBELWA BANDIO!!!

Monday, November 21, 2011

NI WIKI YA PEKEE KWANGU/KWETU-ITAKUWA NI WIKI YA KUMKUMBUKA ASIFIWE!!!

Natumaini wote mu-wazima wa afya njema, na mwisho wa juma umekuwa safi.
Ni hivi blog ya MAISHA NA MAFANIKIO inapenda kuwaambia kwamba wiki hii haitakuwa kama kawaida. Nitawaambia kwa nini, ila kwa kifupi ni kwamba itakuwa wiki ya kumuenzi mdogo wangu marehemu Asifiwe. Kwa namna nyingine haitakuwa kama kawaida hapa kibarazani. NINA IMANI TUTAKUWA PAMOJA /MTAKUWA PAMOJA NAMI NATANGULIZA SHUKRANI ZANGU ZA DHATI. KAPULYA.

Saturday, April 23, 2011

KUMBUKUMBU:- LEO UMEFIKA MWEZI MMOJA TANGU ASIFIWE WETU ATUTOKE!!

Leo imetimia mwezi mmoja tangu Asifiwe wetu atutoke!


Ilikuwa tarehe 23/3/2011 mpendwa wetu Asifiwe alitutoka ghafla. Leo tarehe 23/4/2011 imetimia mwezi mmoja tangu atutoke. Familia ya Mzee Ngonyani ipo katika harakati za kufanya arobaini(thelathini) ambayo itafanyika Nyumbani Ruhuwiko-Songea 30/4/2011. Mwenyezi Mungu ailaze roho ya mpendwa wetu Asifiwe mahali pema peponi amina.

Hapa china nilitumiwa barua pepa na kaka Raymond Mkandawile ujumbe huu ufuatao. Nami nimeupenda ni ujumbe mzuri na nimeona ni vizuri niuambatanishe hapa. Ahsante sana.Ujumbe wenyewe ni huu :-
Duania tu wapitaji na hakuna ajuaye siku yake ni lini. Hivyo hatuna budi kujiandaa na kuwa tayari kila itwapo leo.Dada yetu Asifiwe pumzika kwa amani na sisi pia tunafuta....bwana alitoa na yeye ametwaa jina lake libarikiwe.
Si vibaya kama tukisikiliza na nyimbo hizi ambazo Asifiwe alikuwa akisikiliza sana....

HALAFU HUU PIA ALIUPENDA PIA....

WOTE TWAJUA UMETUACHA KIMWILI LAKINI KIROHO UPO NASI NA TUTAKUKUMBUKA NA KUKUPENDA DAIMA!!!

Tuesday, April 5, 2011

NIMEMKUMBUKA KWELI MDOGO WANGU ASIFIWE LEO

Yasinta na Asifiwe 2009 mwezi wa pili
Leo nimeamka nikimuwaza kweli mdogo wangu Asifiwe nusu nichukue simu na kumpigia ili tuchape hadithi zetu kama tulivyozoea. Nikawa nasikia kama vile ananiita dada, dada, nami nikawa namwita jina lake na mara nikakukumbuka shairi hili aliloandika mtani wangu Fadhy ukitaka kusoma mashairi yake zaidi basi ingia Fadhili ya diwani Shairi lenyewe linasema hivi:-
Pumzika kwa amani, Asifiwe Ngonyani

Asifiwe! Asifiwe! sauti zetu sikia,


Asifiwe! Asifiwe! kweli unatusikia?


Asifiwe! Asifiwe! mbona hujaitikia?


Asifiwe umekwenda, dunia 'meikimbia,


Wajua tulikupenda, ila Mungu kazidia,


Mauti yamekutenda, wewe umetangulia,


Pumzika kwa amani, Asifiwe Ngonyani.


Umetwachia majonzi, hakika twakulilia,


Tumejawa na simanzi, hatuwezi elezea,


Mdogo wetu mpenzi, uchungu 'metuachia,


Pumzika kwa amani, Asifiwe Ngonyani.


Ulijawa na adabu, nao ukarimu pia,


Kwa wako utaratibu, ni nuru imepotea,


Umekwenda kama bubu, kwa heri hukutwambia,


Pumzika kwa amani, Asifiwe Ngonyani.


Wewe mtu mwuungwana, kwa njema yako tabia,


Tulikupenda kwa sana, nd'o maana twaumia,


Mfano wako hakuna, kwa pengo kulizibia,


Pumzika kwa amani, Asifiwe Ngonyani.


Kuondoka kwatuliza, kila tukifikiria,


Twatamani tungeweza, kifo tungekizuia,


Mwaka huu kumaliza, nayo inayof'atia,


Pumzika kwa amani, Asifiwe Ngonyani.


Lakini sisi ni nani, Mungu tukamwamulia?


Tukamwuliza kwa nini, wewe amekuchukua?


Mwamuzi ndiye Manani, aloiumba dunia,


Pumzika kwa amani, Asifiwe Ngonyani.


Pengo halitozibika, wewe ulotuachia,


Daima 'takukumbuka, wema'wo kusimulia,


Tukimwomba Rabuka, mwanga kukuangazia,


Pumzika kwa amani, Asifiwe Ngonyani.


Upumzike salama, kwa Mola twakuombea,


Akupe pahala pema, nuru kukuangazia,


Asifiwe mtu mwema, buriani twakwambia,


Pumzika kwa amani, Asifiwe Ngonyani.


Shairi hili nimeliandika maalumu kwa marehemu Asifiwe Ngonyani, mdogo wa kike wa dada yetu, rafiki yetu na mwanablog mwenzetu Yasinta Ngonyani. Asifiwe alipatwa na mauti Jumatano 23.03.2011. Asifiwe umetuacha kimwili tu, kiroho tungali pamoja nawe. Tunakuombea pumziko salama la milele. Amina. AHSANTE SANA MTANI FADHY KWA SHAIRI HILI!!