Wednesday, November 30, 2011

SWALI LILILONIKERA KWA MIAKA MINGI!!!

Nimeshindwa kuvumilia mwenzenu, kwani hili jambo/swali limekuwa likinikera miaka sasa.

Ni hivi:- Hivi kwanini mwanamke mjane anweza kuishi peke yake mudamrefu au hata milele bila kuolewa tena na mwanamume mwingine? Maana ukiangalia asilimia kubwa ya wanaume wajane huwa hawaishi muda mrefu peke yao huwaa wanaoa tena.

Nina mfano mmoja, bibi yangu mzaa mama:- Babu alifariki mwaka 1980 na bibi amekuwa mjane mpaka Mwenyezi Mungu alipomchukua 2005. Na mafano mwingine nilionao ni baba mmoja nimfamuye mkewe alifariki 2004 na yeye 2006 tayari alipata mwanamke mwingine na kufunfa naye ndoa 2008.
Je?Hapa ndo kusema wanawake wanawapenda zaidi waume zao/wana uchungu zaidi kuliko wanaume?
NAOMBA TUJADILI KWA PAMOJA SWALA HILI JAMANI... KAPULYA WENU!!!!!

HISTORIA :-SONGEA MBANO KIONGOZI SHUJAA WA WANGONI ANAYESTAHILI KUENZIWA DAIMA.

Kama kawaida ni JUMATANO YA KILE KIPENGELE CHETU CHA MARUDIO na leo nimeona tubaki SONGEA na kujikumbusha historia hii. Katika mipitopito nimekutana na mada hii hapa. Na nikaipenda na nimeona si mbaya nikiweka hapa Maisha na Mafanikio. Karibuni sana ndugu zanguni.HUWEZI kuilezea na kuikamilisha historia ya vita ya Majimaji na ukombozi wa nchi yetu bila kumtaja shujaa wa kabila la wangoni Nduna Songea Mbano ambaye jina lake lilipewa hadhi ya kuuita mji wa Songea kutoka kwenye jina la Ndonde mwaka 1906.
Kiongozi huyo alikuwa ni miongoni mwa wasaidizi ( Nduna) 12 wa Chifu wa kabila la wangoni (Nkosi) chifu Mputa bin Gwezerapasi Gama.
Ambapo wasaidizi wake wengine walikuwa ni Mgendera Mawaso Gama, Kohongo Magagura, Mputa Mkuzo Gama, Magodi Mbamba Mbano, Mtekateka Muyamuya Tawete, Fratela Fusi Gama.
Manduna wengiwe ni Maji ya kuhanga Komba, Zimanimoto Gama, Mpambalyoto Soko Msalawani, Mtepa Hawaya Gama na Nduna Mkomanile ambaye alikuwa ni mwanamke pekee kuwa nduna.
Nduna Songea Mbano alikuwa ni maarufu kuliko manduna wenzake na hata chifu Mputa Gama alikuwa anamtegemea sana katika kuwaongoza Manduna wenzake na wapiganaji wa vita ya Majimaji kiujumla.
Mhifadhi kiongozi wa Makumbusho ya Taifa Maji maji Songea Philipo Maligissu akizungumzia maisha ya Nduna Songea Mbano katika viwanja vya Makumbusho hayo,alisema kuwa Songea Mbano akiwa miongoni mwa manduna alitokea kuwa maarufu sana ukilinganisha na wenzake 11 ambapo sifa kubwa iliyo mpa umaarufu ili kuwa ni ueledi na ushadi wake wa kuandaa mikakati ya kivita, na maamuzi mazito yasiyoteteleka na kuyasimamia maamuzi hayo kikamilifu.
Kwa umakini mkubwa Nduna Songea Mbano aliweza kufanya kile alichokuwa akikiamini na uthibitisho wa jambo hilo ulianza kujitokeza julai 12, mwaka 1897 katika viwanja vya Bomani kwa mkuu wa Wilaya wa wajerumani luteni Engelhardt.
Maligissu anasema kuwa kwa rekodi zilizopo zinaonyesha kuwa tarehe hiyo Nduna Songea Mbano alionekana kuwa ni mtu wa kipekee katika idadi ya Manduna 11 ambao walikuwa wasaidizi wa chifu Mputa Gama kwa kitendo chake cha kubisha wazi wazi tamko la utawala mpya wa wajerumani la kutaka wangoni wakomeshe biashara ya utumwa.
Siku hiyo ilikuwa ni siku rasmi ambayo utawala wa kikoloni ulikuwa unaanzishwa katika mji wa Songea wakati huo ulikuwa unaitwa Ndonde na Mkoa wa Ruvuma kiujumla chini ya Luteni Engelhardt wa Jeshi la Kijerumani ambaye alikuwa ndiye Mkuu wa Jeshi kwa kanda ya Kusini.
Wajerumani walipofika kuanzisha makoloni yao katika maeneo ya ukanda wa kusini walikutana na msuguano mkubwa kutoka kwenye tawala za kiafrika hususani tawala za wangoni.
Maligissu anasema kuwa wangoni walikuwa na tabia ya kwenda mikoa ya Lindi na Mtwara kuvamia na kuchukua mateka na kuwaleta Songea kuwafanyisha shughuli mbalimbali katika maeneo yao ya utawala.
Tabia hiyo ya wangoni iliwachukiza sana wajerumani kwani wajerumani walikuwa wanaheshimu sana makubaliano yaliyofikiwa kutoka kwenye mkutano wa Berlin wa mwaka 1884 hadi 1885.
Katika mkutano huo moja ya makubaliano yaliyofikiwa ni pamoja na kila nchi yenye koloni barani Afrika ni lazima ikomeshe biashara ya utumwa na kwa kuwa wajerumani walikuwa wamejiimarisha sana katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
Hivyo walipokuja Ruvuma wakatoa tamko kwa wangoni kuwa hairuhusiwi na haitaruhusiwa tena kwenda Lindi,Mtwara na maeneo mengine kuchukua mateka na kwamba mateka wote waliochukuliwa na wangoni waachiwe huru.
Baada ya wajerumani kutoa tamko hilo ndipo Nduna Songea Mbano alipojitokeza waziwazi na kusimama kujibu hoja iliyotolewa na wajerumani kuhusiana na tamko hilo.
Nduna Songea Mbano alisema kuwa utawala wa kabila la wangoni hauwezi kutekeleza tamko hilo na kwamba msimamo wao ni kutoutambua utawala mpya wa kijerumani na tamko lao.
Aliendelea kusema kuwa ujio wa utawala wa wajerumani na kutoa tamko hilo kwa wangoni una lengo la kudhoofisha utawala wa Machifu na Manduna katika maeneo yao kwa kufuata kanuni zao za kimila na kitamaduni.
Kuanzia hapo wajerumani walimuona Nduna Songea Mbano kuwa ni mtu hatari sana katika utawala wao mpya na walimuweka alama maalumu na kuanza kumfuatilia nyendo zake.
Kwa sababu alionekana kuwa kiongozi shupavu na mwenye misimamo mikali na anayezingatia heshima na utu wa kabila lake bila kuyumbishwa.
Alionekana kuwa ni mtu wa pekee mwenye uwezo mkubwa wa kufanya kazi katika mazingira yoyote kwa kushirikiana na wananchi wake ambao walikuwa wana mheshimu sana na kumsikiliza.
Maligissu anaeleza kuwa Nduna Songea Mbano alikuwa na uwezo mkubwa wa kuwaunganisha wananchi wake na kuwa na umoja, upendo na mshikamano na kwamba alikuwa akiwaelekeza jambo wanalifanya kwa umakini na kwa ukamilifu.
Anaendelea kusema kuwa kuanzia hapo Nduna Songea Mbano aliendelea kujizolea umaarufu mkubwa na wajerumani baada ya kuona hivyo na kitendo cha nduna Songea kutamka kuwa yupo tayari kwa lolote lile na hawezi kukubali kuona tawala za kiafrka zinadharauliwa na wakoloni kwa namna yeyote ile.
Waliamua kuwaalika Machifu na Manduna wote Julai 13 mwaka 1897 Bomani kwa mkuu wa Wilaya wa kwanza katika nchi ya ungoni ambaye pia mkuu wa jeshi la wajerumani katika nchi ya ungoni Luteni Engelhardt na kuwaambia kuwa mtu yoyote katika eneo lake atakaye kaidi amri yeyote kutoka kwa uongozi mpya wa wajerumani basi atapigwa risasi, kunyongwa hadi kufa au kufungwa maisha .
Siku hiyohiyo Machifu na Manduna walichukuliwa hadi juu ya mlima wa shabaha wa chandamari uliopo katikati ya mji wa Songea na kuwaonyesha nguvu ya risasi inavyoweza kufanya kazi katika mwili wa binadamu na kwamba silaha za kijadi na kimila za wangoni haziwezi kufua dafu mbele ya silaha hizo.
Licha ya wajerumani kutoa mkwara na vitisho vingi Nduna Songea Mbano aliendelea kushikilia msimamo wake wa awali wa kuchukia utawala wa wajerumani na kuutetea utawala wa kiafrika mpaka vilipo kuja kutokea vita vya Majimaji.
Nduna Songea Mbano alitoa ushindani mkubwa sana katika vita hivyo na alionyesha ustadi mkubwa kwenye mapigano na katika sehemu zote ambazo wajerumani walipigana wameandika kuwa hawakupata ushindi mkubwa kama waliopata katika Mkoa wa Ruvuma zamani nchi ya ungoni.
Ambapo viongozi wao hawa kuwa wanafiki kwani walijitoa kikwe likweli kusaka ukombozi wa kweli na hadhi ya tamaduni zao mpaka dakika ya mwisho, ndio maana idadi ya watu walionyongwa katika historia ya nchi yetu walitoka katika himaya ya Nduna Songea Mbano na ushahidi upo wazi kuwa watu 67 walihukumiwa kunyongwa hadi kufa akiwemo Nduna Songea Mbano.
Katika kuonyesha kuwa Nduna Songea Mbano alikuwa na uwezo wa kufanya mambo kwa uweledi mkubwa bila kusaliti dhamira yake kuanzia mwaka 1897 alianza kuandaa jeshi lake la kupambana na utawala wa wajerumani.
Akaanza kuchukua watu wake na kuwapeleka juu ya mlima wa chandamari, kufanya nao mkutano na kutoa mafunzo ya kivita na kuwaelekeza kwa nini wanawachukia wajerumani.
Katika mlima huo ndipo alipoeleza kwa kina madhara ya kuukubali utawala wa wajerumani na kutoa ahadi kwa wananchi wake ya kuwaondoa wajerumani kwa lazima na kwamba alisema kuwa eneo hilo ni lao na wamekuwa wakiishi siku zote chini ya utawala wao sasa inakuwaje waletewe utawala mpya wakati hawahuitaji.
Chokochoko hizo zilizaa vita vya Majimaji na wakati mapigano yakiendelea wajerumani walianza kumtafuta Nduna Songea Mbano ili wamkamate na kufanya nae mazungumzo ya maridhiano.
Kumbe Songea Mbano alikuwa amejificha kwenye pango kubwa lililopo kwenye mlima wa chandamari na usiku hukutana na askari wake nje ya pango hilo na kuwapa mafunzo zaidi ya kivita.
Maligissu anaeleza kuwa Nduna Songea Mbano alikuwa anaishi na Ndugu zake katika eneo la Mateka lililopo katika eneo la Manispaa ya Songea na wakati wa vita ndipo Songea Mbano alikuwa anajifisha katika pango hilo ili wasimkamate mpaka atakapotimiza malengo yake.
Wajerumani walipoona wanaendelea kupata madhara makubwa kutokana na vita hivyo waliamua kuwakamata ndugu na familia yake, chifu Mputa Gama na Manduna wengine na kuwafunga gerezani kwa lengo la kumdhoofisha Nduna Songea Mbano.
Baada ya wajerumani kumdhoofisha Nduna Songea Mbano alipata taarifa zote na akaamua kutoka kwenye pango hilo na kwenda kwa wajerumani na kutaka watu wake waachiwe ili mapigano yaendelee.
Ndipo naye alipokamatwa na kuwekwa gerezani na kwamba utawala wa wajerumani waliamua kuwa hukumu wafugwa hao kunyogwa hadi kufa akiwemo chifu wa kabila la Wangoni.
Wafungwa hao waliamuliwa kuchimba shimo kubwa bila kujua kuwa shimo hilo ndilo litakalotumika kuwa kaburi lao na ilipofika siku ya kunyongwa walinyongwa kwa zamu siku mbili na maiti zao kwenda kuwekwa kwenye kaburi hilo hadi walipofikia 66 ndipo walizikwa kwa pamoja kwenye kaburi hilo.
Nduna Songea Mbano walimuacha ili aweze kuwasaidia kufikisha malengo yao kwa wananchi kwani waliamini kuwa yeye ni kiongozi jasiri na anayependwa na watu wake na kusikilizwa vizuri.
Toka siku hiyo walipomuacha bila kumnyonga Nduna Songea Mbano aliwasumbua sana wajerumani na kutaka naye anyongwe kama ndugu zake kwani haoni sababu ya yeye kuishi wakati ndugu zake wamekufa na kusema kama hawataki kumnyonga basi hataki kula wala kunywa chochote mpaka afe.
Ndipo wajerumani walipoamua kumnyonga na kumzika katika kaburi la pekee yake wakiamini kuwa ni mtu wa pekee mwenye ushujaa na maamuzi mazito na misimamo isiyoyumba na walimuenzi kwa kubadilisha jina la mji wa Ndonde na kuubatiza jina la Songea ambapo mpaka sasa linatumika kuuita mji huo wenye hazina kubwa ya historia na utalii wa kitamaduni
Kila mmoja wetu hana budi kujiuliza ni mafundisho yepi anaweza kuyapata katika historia ya nchi yetu na mchango mkubwa alioutoa Nduna Songea Mbano na je kizazi kilichopo tunao ule moyo wa ushujaa , uzalendo heshima na usawa kama ilivyo kuwa kwa mababu zetu basi inatupasa tutimize wajibu wetu kikamilifu ili vizazi vijavyo viweze kunufaika na uwepo wetu duniani.
TUKUTANO TENA JUMATANO IJAYO NA NAWATAKIENI MWISHO MWEMA WA MWEZI HUU NA MWANZO MWEMA WA MWEZI WA KUMI NA MBILI.

Monday, November 28, 2011

ULIJUA KAMA SONGEA KUNA HIFADHI /MBUGAYA WANYAMA?


Nimeishi miaka mingi Songea nilikuwa sina habari kama kuna mbuga ya wanyama. Mbuga hii ipo nje kidogo ya Msamala . Kwa hiyo nasi tulipata bahati na kuingia hapa kwa msaada ya mwenyeji wetu ndugu Sunday Hebuka.


Hili ni jengo/au niseme ni ofisi ndipo ambapo unalipa....Na pia unaona magari kwa ajili ya watalii........


Ila sisi tuliona ni vizuri kutembea kama unavyoona tupo katika msululu hapo...kusaka wanyama....

Msafara unaendelea hapa ni kadaraja...
Na hapa ni mto Ruhila kwa ubunifu wao wameweka mawe ni kama daraja vile. Ila inabidi uwe shupavu kwani kulikuwa na utelezi. Hapa ni lazima kuvua viatu pia...Siku hii tulifurahi sana kuwa katika eneo hili ambalo hatukujua kama lipo...Ushauri ukifika Songea usikose kuchungulia hapaa.Sunday, November 27, 2011

NAWATAKIENI JUMAPILI HII YA KWANZA YA MAJILIO PIA YA MWISHO KWA MWEZI HUU PIA NAPENDA KUWASHUKURUNI KWA USHIRIKIANO WENU KWA SALA YA FAMILIA PAMOJA

Milango imefungwa, Ea Bwana.Yule mtoto mchanga amelala, tunajisikia salama.Tuna raha ya ndani, kwani tumeshiba, chakula kilikuwa kizuri, kinatuletea faraja.
Huu nio wakati wa kukugeukia , mwishoni mwa siku hii ya leo, kama familia-familia yako, ambapo Kristu anaishi.
Kwa ajili yetu, kila moja wetu Bwana, tunakushukuru. Kwa ajili ya siku hii ya leo, iliyojaa mambo mengi, mema na yasiyo mema sana. Kwa yote tunakushukuru.
Tunapoangalia nyuma, mara nyingine, ni rahisi kuona kwamba ingaliwezekana kuwa vizuri zaidi. Hapa na pale, tumeshindwa kukupendeza, kwa neno la hasira. Na lile ambalo hatukulitimiza.
Tunasikitika, Bwana tusamehe. Kwani tunahitaji upendo wako. Tunakuhitaji wewe, ukae nasi, ili utulinde, utubariki, kwani wewe ndiwe kuta za kweli na paa za nyumba yetu.
Utubariki tulalapo, utujalie ndoto zetu ziwe za faraha. Na utujalie tuamke kesho tukiwa na uzima mpya tele. Nguvu mpya na starehe mpya. Ili tuweze kuishi tena siku nyingine.

Baada ya hapa napenda kuwashukuruni wote kwa upendo wenu, ushirikiano wenu kwa kushirikiana nami kwa Wiki hii inayokwisha leo kwa maombolezo ya mdogo wetu Asifiwe. AHSANTENI SANA. PIA NAWATAKIENI JUMAPILI HII YA KWANZA YA MAJILIO IWE NJEMA NA MBARIKIWE SANA WOTE MTAKAOPITA KATKA BLOG HII YA MAISHA NA MAFANIKIO. AMINA

Saturday, November 26, 2011

LEO NI 26/11/2011 NDIYO SIKU ALIYOZALIWA ASIFIWE NGONYANI

Tarehe 26/11/1989 ilikuwa siku ya furaha kwa familia ya Ngonyani kupata binti mwingine ambaye ni Asifiwe. Ni hisia za ajabu sana mwaka huu bila kumpigia simu na kumtakia HERI kwa siku yake ya kuzaliwa ambayo ni leo. Na hii ni sababu kubwa nikaona wiki nzima iwe yake kwa vile imekuwa wiki ya matukio matatu kwa mpigo. Kweli Mwenyezi Mungu ndiye muweza ebu jaribu kuangalia Asifiwe alizaliwa 26/11/1989 siku ya jumapili ,na leo na jumamosi 26/11/2011 ange/ametimiza miaka 22 halafu sasa siku aliyozikwa ni 26/3/2011 siku ya jumamosi tena…HONGERA KWA SIKU YA KUZALIWA MDOGO WETU,DADA YETU,MAMA MDOGO WETU, SHEMEJI YETU, PIA RAFIKI YETU. NA USTAREHE KWA AMANI, TUTAKUKUMBUKA DAIMA.
UA HILI NIMETUMIWA NA KAKA ISSACK CHE JIAH AMBAYE PIA NI MSOMAJI WA MAISHA NA MAFANIKIO. AHSANTE SANA.

Thursday, November 24, 2011

MWAMBA ULIOPASUKA...TUMTEGEMEE MUNGU WETU KWA KILA TUTENDALO. PAMOJA DAIMA.

Wednesday, November 23, 2011

TUTAKUKUMBUKA DAIMA ASIFIWE NGONYANI!!!

Kwa vile leo ni JUMATANO NA NI JUMATANO YA KIPENGELE CHA MARUDIO YA mada/makala/matukio mbalimbali. Basi JUMATANO YA LEO imeangukia kuwa tarehe 23/11 ambayo si mara nyingi inakuwa hivi. nasema hivi kwasababu 23/3/2011 siku ya jumatano tuliondokewa na mpendwa wetu Asifiwe na leo imetimia miezi nane na imeangukia siku ya jumatano na tarehe 23/11-11 kusema kweli nimeshikwa na butwaa kidogo maana si mara nyingi inakuwa hivi. Kwa hiyo nimeona si vibaya kama tukimkumbuka Asifiwe wetu.

Hapa ndipo mahali alipopumzika Asifiwe katika safari yake ya mwisho. TUTAKUKUMBUKA DAIMA ASIFIWE.KWANI UPO NASI KIROHO ILA SI KIMWILI. PUMZIKA KWA AMANI MDOGO WANGU/WETU.

Tuesday, November 22, 2011

ASIFIWE NGONYANI (1989- 2011). Kioo kingine cha maisha yetu, kwa maisha yetu na wenzetu

Kama jana jumatatu nilivyosema ni wiki ya kumkumbuka mdogo wangu Asifiwe Kwa hiyo nimeona si mbaya kama tukimkumbuka Asifiwe kwa mada hii iliyoandikwa na Mzee wa changamoto.

"..see you in ZION, holding hands together standing by MY FATHER'S SIDE. Meet you in ZION singing songs together....." LUCIANONi mwaka mmoja na siku 24 tangu ilipobandikwa MAKALA HII YA KUMSHUKURU MUNGU KWA KUFANIKISHA UPAUSAJI WA Dada Mdogo Asifiwe Ngonyani. Leo hii NAMSHUKURU MUNGU kwa maisha na mapumziko ya Dada Asifiwe, ambaye aliaga dunia Machi 23 na kuzikwa Machi 26.Dada wa Asifiwe, ni Da Yasinta Ngonyani. Sio bloga mwenzangu tu, bali ndiye anayewasiliana na familia yangu kuliko bloga yeyote. Twawasiliana kwenye chat, kwenye simu na hata skype ambapo huwa tunaongea mara kwa mara.Mara nyingi tumezungumza kuhusu Asifiwe.Na kila mara alikuwa akitujulisha maendeleo yake. Na kwa kila wakati ambao afya ya Da Asifiwe ilikuwa ikihitaji msaada wa uangalizi wa watabibu, Da Yasinta alikuwa mnyonge. Na nakumbuka siku ambayo alisema hakuweza kuweka bandiko kwenye blogu yake kwa kuwa hakuwa na furaha. Baadae tukawasiliana kuwa ameweza kuongea na Asifiwe na alikuwa na furaha kusika maendeleo yake ni mema.Lakini juma hili, taarifa zimefika kuwa ASIFIWE HATUNAYE. Binafsi niliumia sana. Nilikuwa sijapata kuonana na Asifiwe, lakini mazungumzo juu yake kutoka kwa Dadake na Da Koero yalinifanya kuwa karibu naye kwa namna ya pekee.Lakini kwa wote hawa (Yasinta na Koero), nililogundua ni namna ambavyo FURAHA ZAO ZILIATHIRIWA NA HALI YA ASIFIWE. Kwa maongezi nao, niligundua juu ya maisha yake ambayo ndicho kilikuwa kivutio kikubwa kwa ndugu zangu hawa ambacho ni TABIA. Da Yasinta hakuwa tu akimzungumzia Asifiwe kama ndugu yake ambaye ni wao wawili pekee wa kike katika familia, lakini alikuwa akimzungumzia kama RAFIKI.NA HILI NDILO NILILOJIFUNZA NA NINALOJIFUNA.Ninapomuwaza ASIFIWE, nikimuwaza Dada Yasinta na dugu, jamaa na marafiki wakimlilia, naona AKISI YA MAISHA YA ASIFIWE. Naona jambo ambalo sisi sote twatakiwa kujifunza kutoka kwa Asifiwe, kisha kuona maisha yetu na ya wali walio kwetu yakibadilika.KILIO cha kumlilia Asifiwe ni ishara nyingine kuwa alipendwa, na licha ya kuwa ni KAZI YA MUNGU kumpumzisha baada ya kuyagusa maisha yetu kwa namna alivyoyagusa, bado tungependa kuendelea kuwa naye.Nakumbuka Juni mosi mwaka 2009, NILIBANDIKA MAKALA HAYA KUHUSU KILIO CHANGU KWA MJOMBA WANGU, ambaye nililia kwa kuwa nilimlilia, na katika makala hiyo, niliandika kuhusu kilio cangu kwa mjomba kuwa "nililia kwa kuwa kwa tafsiri yangu, kulia ni kutokubali kuwa wakati wa mjomba kupumzika ulikuwa umefika na hakika alistahili kupumzika baada ya kutenda mema mengi tena kwa mapambano ya hali ya juu. Mjomba alikuwa mtu mwema kwangu na kwa wengi..." Mtu wa kwanza kutoa maoni kwenye bandiko hilo (kama ilivyo kwa mabandiko mengi kwenye blogu nyingi) ni Dada yangu Yasinta ambaye alisema "Mzee wa Changamoto pole sana tena sana. Nalia pamoja nawe kwani nakuelewa kabisa. Na nakushauri lia sana kwani kulia ni moja ya kutoa uchungu wako. Natumanini Mjomba wako yupo nawe kila siku amini. Astarehe kwa amani."Leo hii nami namkumbuka Asifiwe, na licha ya kuwa NAMLILIA, bado nakumbuka kuwa ALISTAHILI KUPUMZIKA na kuwa aligusa maisha ya waliohusiana na kuishi naye na yetu tuliomfahamu kupitia ndugu na marafiki.Lililo kubwa kwetu tuliobaki, ni kuishi maisha sahihi na maisha yaliyo mema. Kama ambavyo aliishi ASIFIWE NGONYANI....Na ndio maana (kama kisemavyo kichwa cha post) namuona "ASIFIWE NGONYANI kama Kioo kingine cha maisha yetu, kwa maisha yetu na wenzetu"Chris Rice anasema....COME THOU FOUNT

AHSANTE MZEE WA CHANGAMOTO/KAKA MUBELWA BANDIO!!!

Monday, November 21, 2011

NI WIKI YA PEKEE KWANGU/KWETU-ITAKUWA NI WIKI YA KUMKUMBUKA ASIFIWE!!!

Natumaini wote mu-wazima wa afya njema, na mwisho wa juma umekuwa safi.
Ni hivi blog ya MAISHA NA MAFANIKIO inapenda kuwaambia kwamba wiki hii haitakuwa kama kawaida. Nitawaambia kwa nini, ila kwa kifupi ni kwamba itakuwa wiki ya kumuenzi mdogo wangu marehemu Asifiwe. Kwa namna nyingine haitakuwa kama kawaida hapa kibarazani. NINA IMANI TUTAKUWA PAMOJA /MTAKUWA PAMOJA NAMI NATANGULIZA SHUKRANI ZANGU ZA DHATI. KAPULYA.

Sunday, November 20, 2011

JUMAPILI NJEMA KWA WOTE...NA TUKUMBUKE KUMSHUKURU MUNGU KWA TULICHONACHO/TULICHOPEWA NA TULICHOPATA!!!

Bwana ndiye mchungaji wangu.Sitapungukiwa na kitu. Katika malisho ya majani mabichi hunilaza. Kando ya maji ya utulivu huniongoza. Hunihuisha nafsi yangu, na kuniongoza. Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake'. Naam, nijapopita katika bonde la uvuli wa mauti. Sitaogopa mabaya. Kwa maana wewe upo pamoja nami. Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. Waandaa meza mbele yangu. Machoni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu. Na kikombe changu kinafurika.Hakika wema na fadhili zitanifuata. Siku zote za maisha yangu. Nami nitakaa nyumbani mwa bwana milele. Amen. ZABURI 23:1-6.
JUMAPILI NJEMA KWA WOTE NA WOTE MNAPENDWA!!!

Saturday, November 19, 2011

JUMAMOSI NJEMA JAMANI!!!

Ila isiwe sanaaaa...Picha hii kutoka kwa Da´Edna tumalizie na kipande hiki cha MBAYUWAYU (NGO, NGO, NGO ") - MALRLAW NYIMBO YAKE MPYA....

NAWATAKIENI WOTE JUMAMOSI NJEMA NA EPUKENI KUNYWA SANA KWANI SI SALAMA KWA AFYA PIA USINYWE KAMA UMEPANGA KUENDESHA!!! MWENYEZI MUNGU AKIPENDA TUTAONANA KESHO....KAPULYA

Friday, November 18, 2011

TUANZE MAPUNZIKO AU MWISHO WA JUMA NA HII TASWIRA MWANANA KATIKA UFUKWE WA MBAMBA BAY!!!

Picha na maelezo toka blogu ya Profesa J. Mbele.
Mbamba Bay ni mji mdogo, kando kando ya Ziwa Nyasa, upande wa Tanzania. Ingawa umaarufu wa mji huu tangu zamani ni bandari, hapo ni mahali pazuri kwa mapumziko.Picha hii ilipigwa mwanzoni mwa Agosti, mwaka huu.Unaweza kusogea hapo ufukweni, ukawa unapunga upepo na kuangalia shughuli za wavuvi, wauzaji wa samaki, akina mama wakifua nguo, na watoto wakicheza majini. Kama unajua kuogelea, mahali hapo utafafurahia. Ukija siku ambapo meli inakuja, utajionea ujio wa meli na kuondoka kwake.


IJUMAA NJEMA KWA WOTE....

Thursday, November 17, 2011

UJUMBE WA LEO NI HUU:- MAISHA NI ZAWADI!!

Leo kabla ya kusema neno baya, mfikiria mtu ambaye hanaweza kusema.
Kabla ya kulalamika kuhusu ladha ya chakula, fikiria mtu ambaye hana kitu cha kula. Kabla ya kulalamika kuhusu mume wako au mke wako, fikiria mtu amnbaye amliliaye Mungu kwa ajili ampe rafiki. Leo kabla ya kulalamika kuhusu maisha. Fikiria mtu ambaye alikwenda mbinguni mapema mnoamekufa mapema mno. Kabla ya kunung'unika kuhusu umbali gani unaendfesha garilako, fikiria mtu ambaye anatembea umbali huo kwa miguu yake. Na wakati wewe ni uchovu na ulalamikapo kuhusu kazi yako, fikiria wale wasio na ajira, walemavu, na wale ambao wanataka wangekuwa na kazi kama yako yako. Na wakati mawazo yanakutawala na kukufanya uwe na huzuni, tabasamu na ufikiri. Wewe ni hai na bado upo.
TUWE NA UHAKIKA NA TUFIKIRI/TUWAZE KWA UHAKIKA!!!! 

Wednesday, November 16, 2011

TWANGA PEPETA OFFICIAL POSTER

salam,
Tafadhali Naomba uturushie poster ya Twanga Pepeta.Natanguliza shukrani.
Urban Pulse

EBU ANGALIENI/TAZAMENI AU SIKILIZENI HIZI HAPA...FUNDISHO KWA WENGITusikilize na hii pia...
JIONI NJEMA KWA WOTE!!!!!

WAMALAWI NA NDOA ZA VIBINTI!

Ni JUMATANO NA NI KILE KIPENGELE CHETU CHA MARUDUI YA MADA/MAKALA NA MTUKIO MBALIMBALI. LEO NIMEPITA KUPEKUA KWA MDOGO WANGU WA HIARI AMBAYE KWA SASA SIJUI YUPO WAPI SI MWINGINE TENA BALI NI KOERO BINTI WA MKUNDI.BONYEZA HAPA.


Mmoja wa wa waathirika wa ndoa hizoBinti huyu naye ni miongoni mwa waathirika wa ndoa hizi za vibinti


Huyu sio babu na mjukuu wake bali ni mtu na mkewe


“Baba yangu wa kambo aliniamuru niache shule ili niolewe na mzee wa umri wa miaka 77, kwa madai kuwa umri wangu ni mkubwa ukilinganisha na darasa ninalosoma, kwani wakati huo ndio nilikuwa niko darasa la nne. Nilimkatalia na kumweleza wazi kuwa ningependa kuendelea na masomo”. Hivyo ndivyo alivyoanza simulizi yake binti huyu Balita Simpokolwe.lakini hata hivyo kukataa kwake hakukuweza kumsaidia.Kwani baba yake alianza kumtuma sokoni kuchukua fedha kwa mtu mmoja mzee hivi, ambaye alikuwa hamfahamu, ambapo alikuwa akipewa kiasi cha kati ya dola 5 mpaka 10, kiasi ambacho alitakiwa anunulie chakula na kiasi kinachobaki alikuwa kumpa baba yake huyo wa kambo.Balita anakiri kwamba hakuweza kuhisi jambo lolole kuhusiana na zile pesa alizokuwa akipewa na yule mzee kwa kuwa aliamini kuwa yule alikuwa ni rafiki wa karibu wa baba yake wa kambo. Lakini wiki tatu baadae tangu awe anakwenda kuchukua fedha kwa mzee yule, alishangaa kumuona akija nyumbani kwao na jembe dogo la kulimia bustani. ( kwa mila za watu waishio Malawi Kaskazini hususan katika wilaya ya Nsanje jembe dogo la kulimia bustani inatumika kama ishara ya mahari)“Nilishtuka sana, baada ya baba yangu wa kambo kunitaka nipokee jembe lile la bustani kutoka kwa yule mzee. (Kwa mila zao, binti kupokea jembe kutoka kwa mwanaume ni ishara kuwa amekubali kuolewa na mume huyo). Lakini huku nikiwa imechanganyikiwa, nilikataa kupokea jembe lile.”Hata hivyo mama yake aliungana naye kupinga binti huyo kuolewa kwa kuwa bado alikuwa ni mdogo, “baba yangu wa kambo alikuja juu akidai kuwa atampa talaka mama yangu iwapo atapinga mimi kuolewa na mzee huyo, na cha kusikitisha zaidi alidai kuwa haiwezekani nisiolewe na mzee huyo kwa kuwa tumeshakula fedha zake.” Alisema binti huyo kwa masikitiko.Hivyo alilazimishwa kuolewa na mzee huyo, lakini baada ya wiki mbili tangu aolewe kikundi kimoja cha kutetea unyanyasaji wa wanawake na watoto kiitwacho Chitipa Women’s Forum kilimuokoa kutoka katika ndoa hiyo baada ya kuwashwishi wazazi wa binti huyo wamrejeshe shuleni.Belita Simpokolwe, sasa anaishi na mmoja wa baba zake wadogo, amefurahi sana baada ya kurejea shule kuendelea na masomo yake. Tukio hili ambalo lilimpata Belita Disemba mwaka 2008 lilimuacha akiwa na amesathirika kisaikolojia.Kwa mujibu wa mwalimu anayemfundisha alikiri kuwa kuna wakati alikuwa anashindwa kuzingatia masomo yake pale kumbukumbu za tukio lile la kutolewa shuleni na kuozeshwa kwa nguvu linapomjia, lakini binti huyo ambaye alikuwa na miaka 13 wakati huo akiozeshwa, amemudu kuendelea na masomo yake ambapo anataka kutimiza ndoto zake za kuwa muuguzi hapo atakapomaliza masomo.“Kinachoniuma ni kwamba nimekuwa ni muathirika wa ndoa ya utotoni baada ya wale niliowaamini kuwa watanitunza na kunilinda kunitoa kafara kiasi cha kutaka nisitimize ndoto yangu” alisema binti huyo aliyekuwa akisoma shule ya msingi Kawale kaskazini mwa Malawi, akiwa yuko darasa la sita wakati huo.Belita ni mmoja kati ya mabinti walioathiriwa na mila marufu kama Kupimbira, ambapo mabinti hulazimishwa kuacha shule na kuozeshwa kwa wazee ili kujipatia mahari, na hii hufanyika bila hata ya binti kufahamishwa.Wakati mwingine wazazi hulazimika kuwaozesha mabinti zao ili kulipa madeni.Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa hivi karibuni na tasisi ya Chipita Women’s Forum inaonyesha kwamba ,taktibani asilimia 17 ya mabinti huachishwa shule na kuozeshwa kwa wazee, huku wengine wakilazimika kuacha shule wenyewe kutokana na unyanyasaji wa kijinsia unaofanywa na waalimu wa kiume na wanaume wakware wenye uchu wa kufanya mapenzi na vibinti.Akizungumzia mila zinazotumika kuwakandamiza watoto wa kike na kuwakatisha shule Mwenyekiti wa Chipita Women’s Forum, Bi Ruth Mbale alizitaja mila kama ‘Kupimbira’, ambapo mabinti hulazimishwa kuacha shule na kuozeshwa kwa wazee ili kujipatia mahari, ‘Nhlanzi’ ambapo familia ya mke huozesha binti mwingine kwa mume wa binti yao kama zawadi kutokana na kuitendea wema familia husika, ‘Kulowa kufa’ mwanamke aliyefiwa na mume kuingiliwa kimwili na mwanaume mwingine ili kuondoa mkosi wa vifo kijijini, kwa kawaida shughuli hiyo hufanywa na mwanamume maalum wa kufanya shughuli hiyo. Mila hii pia inasemekana inafanyika hapa nchini hususana wilayani Ukerewe ambapo hujulikana kama ‘Kusomboka’, hii kwa hapa nchini hufanywa na wanaume na wanawake. Bi Mbale pia aliitaja mila ya ‘Fisi’ ambapo mume ambaye hana nguvu za kiume anamkodisha mwanume wa nje ili amuingilie mkewe kwa ajili ya kumpa ujauzito, lengo kuu ni kujipatia watoto.Bi Mbale alikiri kupata ugumu katika kupiga vita mila hizi kutokana na usiri mkubwa uliokuwepo katika jamii hiyo ya watu waishio Kaskazini mwa Malawi.Akizungumzia idadi ya mabinti waliiokolewa na taasisi yao tangu walipoanza kampeni ya kuwaokoa wanafunzi walioozwa kabla ya kumaliza masomo, Bi Mbale alisema kuwa wamefanikiwa kuwaokoa mabinti 40 waliokuwa na umri kati ya miaka 7 hadi 16 ambapo walirejeshwa shule na kuendelea na masomo.Alisema kuwa, ingawa inakuwa ni vigumu kwa mabinti hao kurejea katika hali yao ya kawaida kabla hawajaolewa lakini huwapa ushauri nasaha hadi warejee kwenye hali zao za kawaida na kuendelea na masomo yao.


Habari hii nimeitoa kutoka vyanzo mbalimbali vya habari ukiwemo mtandao wa inteneti.

Tuesday, November 15, 2011

LEO NIMETAMANI KULA MLO HUU/KULA NJUGU!!!!

Nimetamani kweli kula njugu leo, wengi nadhani mnajua njugu ni nini...ni aina ya karanga na zinalimwa kama karanga. Mimi napenda /pendelea zaidi za kuchemsha. basi leo nimepata HAMU na nimeishi kuangalia tu picha hii...Ni zamani mno nilizila

Hapa zimepikwa na viungo....lakini mimi napenda zaidi zile zilizongólewa tu na kuchemshwa kama vile karanga za kuchemsha ila kwa sasa ningapata hizi hapa ningekula ..mmhhhh. Duh ngoja niache kuota... Haya jamani kila la kheri .......

KUOLEWA NA WANAUME WAWILI!!

Baada ya kusoma habari hii nimekuwa nikijiuliza ya kwamba kwanini kujipa taabu hasa pale asipojua kama uzauzito huu ni wa nani? Kwa sababu inaonekana, hata kama anawawekea zamu hata hivyo imekuwa ngumu kujua nani na baba. Katika jamii yetu "tumezoa" kuona wanaume ndo wanaoa wake 2-4 na anawawekea zamu na hata wakiwa wazawazito inajulikana ni yeye mume/bwana ndiyo baba. Kama mke hajawa mjanja na kutoka nje kwa kushindwa kusubiri zamu yake.. Sasa hii ya kuolewa na wanaume wawili kaaazii kwelikweli. Palipo na wengi haliharibiki nenoo. Naamini mtanisaidia kuelewa jambo hili!!!

Monday, November 14, 2011

HONGERA KWA SIKU YA KUZALIWA MTANI WANGU FADHILI MTANGA!!

Leo ni ni siku huyu kijana alizaliwa na blogg ya Maisha na Mafanikio inapenda kumtakia HONGERA KWA SIKU HII. Kwani ni siku muhimu sana kwake na pia kwetu kwani tumekuwa kama ndugu sasa. Basi ngoja tuselebuka siku hii pamoja na kaka huyu kwa wimbo huu nina imani ni nyimbo azipendazo.....

HONGERA FADHY!!!

TUANZE JUMATATU HII NA UJUMBE HUU:- TAMAA MBAYATuliza moyo wako,kubali mapungufu yako. Rahisisha mahitaji yako, ongeza kipato chako. Chunga tamaaa mbaya…Sifa ya macho kuona yaani kutazama kinachoonekana. Ila sio kila unachokiona ukazani kupata inawezekana. Nyumbani kuna msichana njiani utaona wengi wasichana. Bora kuishia kutazama kuliko kujifanya unaweza sana. Siri ya maisha yako iko kwa muumba, mbuzi ni mbuzi hawezi kuwa simba… hawezi kuonekana eti wala hawezi kuimba bora kutulia ama kupiga malipa utasikia pia .....Chunga tamaa mbaya..... Ni baadhi ya maneno yaliyo tamkwa kwenye wimbo huu....ni ujumbe mzuri sana kwa jamii nami nimeona ni vema nikiwashirikisha wenzangu...

Sunday, November 13, 2011

TAREHE HII 13/11 HAPA LEO NI SIKU YA AKINA BABA/FARS DAG!!

Nami nachukua nafasi hii kwa kuwapongeza akina baba, wa kwanza ni baba yangu mkubwa mzee Lotary Ngonyani, wa katikati ni baba yangu wa kati Efraimu Ngonyani na wa tatu ndiye baba yangu mzazi Mzee Gervas Ngonyani. NAJIVUNA SANA KWA UWEPO WENU. MWENYEZI MUNGU AWABARIKI NA KUWALINDA MUWE NA AFYA NJEMA.

Na hapa ni baba yake Camilla na Erik. Hongera kwa siku ya baba baba yetu pia tunapenda kukuambia ya kwamba wewe ni baba bora hata kama kuna ambaye hatakubaliana nasi lakini huo ndio mtazamo wetu. Kwani pale tunapohitaji msaada wako haupo nyuma kutusaidia kimasoma na pia kwa mambo mengine. BABA SISI WANA TWAKUPENDA SANA NA UWE NA SIKU NJEMA KWA SIKU HII YA AKINA BABA/FARS DAG. Hata hivyo tunapenda pia kuwapa HONGERA AKINA BABA WOTE DUNIANI. Camilla na Erik.

Saturday, November 12, 2011

JUMAMOSI YA LEO NIMEONA NIJIUNGE NA LADY JAY DEE KATIKA MWEZI HUU KWA KUVAA NGUO NYEUPE!!

Hapa ni yeye mwenyewe Lady Jay Dee ndani ya nyeupe....


Na hapa ni kapulya katika nguo nyeupe kwa kuungana na dada Jay Dee kwa kipindi hiki cha maombi ....JJUMAMOSI NJEMA!!!!!!

Basi ngoja tumsikilize pia dada Jay Dee na kipande hiki.........

Friday, November 11, 2011

PICHA ZA VURUGU KUWAFUKUZA WAMACHINGA MWANJELWA LEO!!

Wamachinga wakiwa Tayari kwa ajili ya Kupambana na FFU wakati wa tukio hilo.....
Baadhi ya wananchi wakiwa wameokoka katika eneo hilo.......................................
Wamachinga Mbali mbali wakikimbia katika eneo la tukio wakati wa machafuko hayo yamepamba moto
Polisi wakijaribu Kuzuia Ghasia katika eneo hilo na kufukuza Wamachinga.......
Watu Mbali Mbali wakiwa wanakimbia ili kujiokoa na Hatari katika eneo hilo ......

Picha zote na: http://www.latestnewstz.blogspot.com/. Nimetumiwa Picha na HABARI na:
LATEST NEWS T.

Naona mwisho wa juma hili umeanza vibaya nimejiuliza au hii tarehe 11/11/-11 nini? LOL!!

NAPENDA KUWATAKIENI MWISHO WA JUMA HILI NA WIMBO HUU USEMAO MAISHA NI FORENI NA BONY MWAITEGE!!


IJUMAA NJEMA KWA WOTE na Tuwa na imani katika maisha tusikate tamaan na matokeo yake siku moja yatatokea. Pia nachukua nafasi hii kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunifikisha /tufikisha tarehe hii ya leo ambayo namba zake ni:- 11/11/11 AHSANTE MUNGU KWA KUWA MWEMA KWETU.

Thursday, November 10, 2011

HII NI PICHA YA WIKI /MWANAMTINDO WETU!!!

Picha hii ni zawadi niliyopewa mwaka juzi 2009 na mzee wa Lundu Nyasa
Nimeipenda na nimeona iwe picha ya wiki. Pia huwa napenda kukusanya kila kinachonihusu, nataka kiwe karibu nami. WOTE MNAPENDWA MUWA NA JIONI/USIKU NJEMA/MWEMA. Au pia LABDA MCHANA MWEMA.


AHSANTE MARKUS KWA ZAWADI HII.

UTAPENDA HADI LINI?

Inasemwa siku zote kwamba, upendo ni kubadilishana, yaani mtu anampenda mwingine na huyo mwingine anampenda yeye. Hii ni kweli. Inapotokea kwamba, mpenzi mmoja anasahau wajibu wake, yaani kumpenda mwenzake na anasubiri kupendwa tu, tatizo hutokea.
Hali hii inapotokea, anayependa ambaye tunasema ndiye mtoaji pekee, hufikia mahali huingia kwenye hali ya hisia ambayo hufahamika kama resentment flu (Homa ya masikitiko). Hii ni hali ambayo, yule ambaye anatoa tu yaani anampenda mwenzake, lakini mwenzake hampendi, huihisi anapokuwa amechoka.
Kwa kawaida tunasema, mtu anapopenda asisubiri naye kupendwa, yaani anapotoa asijali kama mwenzake anatoa au hatoi. Lakini hufikia mahali kanuni za maumbile humfanya huyu anayetoa kuhisi kama amebeba mzigo mkubwa sana. Kama tunasema kupenda ni mtu kutoa bila kutarajia kupewa, inamaana kwamba, huyu anayeshindwa kutoa ameshindwa kupenda.
Kama ameshindwa kutoa ina maana kwamba, ameshindwa kutekeleza jukumu lake na hiyo ina maana kwamba, ameshindwa kupenda. Anaposhindwa kupenda anakuwa amevunja kanuni ya kimaumbile inayosimamia kupendana ambayo inasema ili kupendana kukamilike, pande zote ni lazima zitoe na kupokea.
Kumbuka nasema, kupendana, siyo kupenda. Kwenye kupenda tunatakiwa kutoa tu, kwenye kupendana tunatakaiwa kutoa na kupokea. Kama tunampenda mtu na mtu huyo hatupendi, yaani hatimizi majukumu na wajibu wake kwenye kutupenda sisi, hatimaye tunafikia mahali tunaingia kwenye hiyo hali niliyoitaja ya homa ya masikitiko.
Kumbuka ninaposema kutoa sina maana ya kutoa fedha, bali kumtendea na kumtolea kauli za wema mwenzako. Kwenye tatizo hili, wanawake wanaonekana kama wanaathirika zaidi.
Kama mwanamke akihisi kuwa yeye anatumikia upendo na mwenzake hajali tena, huumia kuliko ilivyo kwa mwanamume. Labda ni kwa sababu, wanawake huumia kihisia kirahisi zaidi kuliko wanaume na jambo hili linapotokea kuumiza zaidi hisia.
Mwanamke huanza kuingia kwenye hali hii polepole, pale anapobaini kwamba, mwenzake anapokea tu, badala ya kupokea na kutoa. Hii ina maana , mwanamume anaposubiri au kufurahia kutendewa mema na kutolewa kauli njema tu, wakati yeye hafanyi hivyo. hajali kuhusu mpenzi wake.
Mwanamke kwa kawaida huonyesha dalili kwamba, yuko kwenye hali hii kwa kuanza kuacha kufanya vile vitu ambavyo kwa kawaida huitwa au kuonekana vidogovidogo kwenye uhusiano.
Kwa mfano, anaweza akaacha kumtayarishia mumewe chakula anachokipenda sana ambacho alikuwa anamtayarishia kwa nyakati fulanifulani, anaweza asiwe anamchagulia tena nguo za kuvaa, anaweza asiwe anamkagua baada ya kuvaa, anaweza akaacha kumuuliza angependa kula nini na wakati mwingine anaweza kuchukua hatua mbaya zaidi kama kukataa kushiriki tendo la ndoa.
Mwanamume anapoona mke akiwa hivyo, naye huanza kumtendea mkewe kwa njia kama hiyo, yaani kuongeza kiwango chake cha kutojali. Anaweza kuanza kuchelewa kurudi nyumbani, anaweza hata kuscha Kukaa pamoja na mkewe hata akiwa nyumbani, anaweza hata kujitoa kabisa kwenye uhusiano, yaani kufanya mambo yake kama vile hana mke.
Inapotokea hali ambapo mwanamke anahisi kuingia kwenye homa hii, inabidi ajiulize haraka ni kwanini ameingia huko. Ni vizuri kujiuliza kwa sababu, akisubiri zaidi, mume naye ataanza kuwa mkorofi zaidi. Ikifikia hapo, njia ya kusuluhisha tatizo hili ambalo kwa kawaida, linaweza kuondolewa kwa mazungumzo, huwa ngumu zaidi.
Kwa hiyo, hakuna suala la “nitapenda hadi lini,” kwa sababu kupenda hakuumizi. Kunakoumiza ni kushindwa kutoa mapenzi. Ukitoa upendo wako kwa mtu ambaye yeye kazi yake ni kupokea tu, lakini hajui kutoa upendo, yeye ndiye atakayeumia. Yeye atakufanya uache kuendelea kutoa, hivyo yeye ndiye atakayekosa, siyo wewe.
Yeye atapata shida kwa sababu, kila mtu atakayeamua kuishi naye kama mpenzi, atahisi hali uliyoihisi wewe na ataamua kumkimbia. Ni hadi ajifunze kutoa, ndipo atakapoanza naye kuingia katika kupendana.
Hebu fikiria kwamba, unamtendea na kumtolea kauli nzuri mkeo au mumeo. Unahakikisha kwamba, unampa kila ambacho nawe ungependa kupewa, bila kujali kama naye anafanya hivyo kwako au hapana.Umemkubali kama alivyo na udhaifu wake na unazingatia zaidi ubora wake na siyo udhaifu huo. Hapa tunasema unampenda.
Lakini kwa bahati mbaya, huyo mwenzako ni mkosoaji, asiyejali, mchoyo, mlalamishi na mwenye ghubu. Huyu tunasema, hajui au hataki kupenda. Kwa maana hiyo, anaishi kwenye uhusiano usio na maana kwake. Hauna maana kwake kwa sababu, hana cha kutoa, ameshindwa wajibu wake katika uhusiano ambao ni kupenda. Kwa sababu hiyo, ni wazi hataweza kuendelea na uhusiano, ni lazima atasababisha uvunjike, kama tulivyoona.
Kama nawe hujui kupenda, utamuiga na utakuwa umeshindwa wajibu wako, kama yeye. Kwa hiyo, kwenye hali kama hiyo, hakuna kinachotolewa wala kupokelewa. Ni wazi uhusiano hauwezi kuwepo katika hali ya namna hiyo. Uzuri wa mmoja kuendelea kutoa bila kujali mwenzake anafanya nini ni kwamba, huyu mwenzake anaweza kungámua tatizo au kasoro yake na kubadilika.
Kwa hali hiyo, unaweza kuona jinsi upendo ulivyo kutoa na kupokea au njia mbili-kwenda na kurudi kama wengine wanavyosema. Unapokuwa wa kupokea tu bila kutoa au wa njia moja, hauwezi kuendelea kuwepo.
MAKALA HII NIMEISOMA MARA NGAPI SIJUI NA NIMEIPENDA NA NIMEONA SI VIBAYA NIKIWASHIRIKISHA NA WENZANGU ELIMU KUGAWANA …NIMEISOMA KWENYE KITABU CHA MAPENZI KUCHIPUA NA KUCHANUA KILICHOANDIKWA NA MAREHEMU MUNGA TEHENAN…PIA HABARI HII IMEWAHI KUTOKA KWENYE GAZETI LA MSHAURI WAKO.

Wednesday, November 9, 2011

NIMEKAA HAPA NIKAKUMBUKA HII NGOMA YA CHIYODA/KIHODA!!!Ni siku nyingi sijaweka ngoma zetu za asili hapa leo nimekumbuka shule ya msingi pia maisha ya kitamaduni kwa ujumla nimeona tuselebuke na ngoma hii ya CHIYODA ambayo kwa kawaida inachezwa na watoto wa kike/wasichana na akina mama tu. Nimeicheza enzi zake:-). JIONI NJEMA KWA WOTE!!

TABASAMU!!!

Kama kawaida ni ile JUMATANO YA KIPENGELE CHA MARUDIO na leo Kapulya ameona tuangalia hili neno TABASAMU na nimeikuta hii mada hapa. KARIBUNI.

Tabasamu ni njia rahisi isiyo na gharama ya kubadilisha mwonekano wako.Tabasamu ni kitu gani? Tabasamu ni dirisha linaloonesha nini kilichopo ndani ya moyo wa mtu, ni kitu kinachonyoosha kila kitu kuwa katika mstari ulioonyoka. Ukiwa mtu wa kutabasamu unakuwa na marafiki wengi na ukiwa mtu wa ndita watu huanza kukukwepa.

Kila unapotabasamu kwa mtu yeyote ni ishara ya upendo, ni zawadi kwa yule mtu ni kitu kizuri. Tabasamu ni kusema karibu, tabasamu ni uwezo ambao unaweza kuifanya siku ya giza kuwa siku ya nuru, huweza kufanya pasipo na upendo kuwa na upendo. Inagharimu misuli 17 tu kutabasamu na inakugharimu misuli 43 kuwa na ndita kwa nini ujizeeshe mapema? Amani huanza kwa tabasamu!
Huwezi kuvaa ukapendeza bila kuvaa tabasamu, huwezi kuwa mrembo bila kuvaa tabasamu huwezi kuitwa beautiful one kama hujavaa tabasamu huwezi kuitwa handsome kama hujavaa tabasamu period! Tafiti zinaonesha mtu anayetabasamu huwezi kuongeza miaka mingi katika maisha yake. Hata hivyo watoto hujifunza kutabasamu kutoka kwa wazazi wao.
Umemaliza kusoma hapa, sasa zamu yako kutabasamu halafu kicheko!
AHSANTENI SANA NA TUONANE TENA PANAPO MAJALIWA JUMATANO IJAYO!!

Tuesday, November 8, 2011

HUU NI UJUMBE WA JUMANNE YA LEO!!!

JUMANNE NJEMA NDUGU ZANGUNI!!!Monday, November 7, 2011

TUIANZE JUMATATU HII KWA KUMBUKUMBU HII/JE? WEWE UNAIKUMBUKA HII:-SIZITAKI MBICHI HIZI !!


Hadithi inayokuja, ni ya Sungura sikia,
Hadithi uliyongoja, leo ninakuletea,
Alitoka siku moja, njaa aliposikia,
Njaa aliposikia, Sungura nakuambia


Siku ile akaenda, Porini kutembelea,
Akayaona matunda, mtini yameenea,
Sungura akayapenda, mtini akasogea,
Mtini akasogea, Sungura nakuambia.


Sungura karukaruka, lakini hakufikia,
Matunda hakuyashika, mikononi hakutia,
Hakika alisumbuka, nguvuze zikapungua,
Nguvuze zikapungua Sungura nakuambia.


Mtazame hapo juu Sungura amelegea,
Mtazame na miguu, matunda anarukia,
Atafanya sikukuu, matunda akifikia,
Matunda akifikia, Sungura nakuambia.


Karuka tena karuka, matunda akarukia,
Mwisho Wave akachoka, kachoka hata mk-Ia,
Penye mti akatoka, pembeni akasogea,
Pembeni akasogea, Subgura nakuambia.


“Sizitaki mbichi hizi” Sungura akagumia,
“Naona nafanya kazi, bila faida kujua”,
Yakamtoka machozi matunda akalilia,
Matunda akalilia, Sungura nakuambia.


Sio kama hakutaka, sasa nakupasulia,
Matunda aliyataka, ndiyo kisa akalia
Tunajua hakufika, alichoka kurukia,
Alichoka kurukia, Sungura nakuambia.


Hadithi nimemaliza, nimekwisha simulia,
Jambo moja sikiliza, rafiki yangu sikta,
Usikose kujikaza, mazuri kukazania,
Utamshinda Sungura, utapata mbivu hizi.

Thursday, November 3, 2011

Kijiji cha Lilondo wilayani Songea mkoani Ruvuma kinaoongoza kwa kuwa na ndizi nyingi

Hapa ni aina mbalimbali za ndizi ambazo zinapatikana katika kijiji cha Lilondo wilayani Songea mkoani Ruvuma, ndizi hizo zimetoa ajira kwa wanawake wengi wa kijiji hicho hali ambayo imesababisha kupata maendeleo makubwa kiuchumi.

Leo mwenzenu nimekumbuka kweli enzi zili wakati naishi Matetereka. Kijiji hiki na kijiji jirani cha Lilondo kuna ndizi za aina mbalimbali. Wakati ule bei yake ilikuwa ndizi tatu shilingi tano. Halafu watu wa Matetereka pia Lilondo ni wakarimu sana. Licha ya ndizi, kuna magimbi si mchezo, karanga, mahindi, maharagwe, kahawa bila kusahau kinywaji cha ulanzi pia. Halafu kulikuwa na watu walikuwa wakipisha nyama pori...nimeyatamani sana maisha haya... Mtani Fadhy upoooo maana najua hapa vyakula hivi umekua nanyo:-)

Wednesday, November 2, 2011

WADAU MNAKUMBUKA VITANDA HIVI NA MAGODORO YA SUFI?

Kitanda cha ngozi ya ngómbe au mbuzi wengi huita "teremka tukaze". Kinakukumbusha nini? Mimi nimekumbuka sana leo enzi hizo yaani kitanda kama hiki ........
......na godoro la sufi au Maranda ya mbao. Swali langu ni kwamba je?kuna wangapi nao wamepitia hili?

HOT NEWZ...............UNYAMA UNYAMA MZEE WA MIAKA 60 LUDEWA ACHOMWA MOTO KWA IMANI ZA KISHIRIKINA

Katika kipengele chetu cha JUMATANO YA MARUDIO mbalimbali leo Kapulya amefika mpaka mkoani Njombe na kukutana na habari hii ya kusikitisha ambayo imeniliza na nimeona tulie pamoja. Habari hii nimeikuta kwa kaka Francis. Kweli binadamu tuna roho za namna ya pekee yaani.....

Mwili wa marehemu mzee Laurance Nkwera

Umati wa Wananchi waliofika kushuhudia tukio hilo wakiwa wamemshikilia dada wa marehemu aliyekuwa akilia huku akimlaumu marehemu kaka yake kwa kujihisisha na uchawi na kukataa ushauri wake.

MTU MMOJA aitwaye Laurance Nkwera 60 mkazi wa Kijiji cha Ibani Ludewa katika Mkoa mpya wa Njombe amekufa kwa kuchomwa moto na kuungua vibaya kwa imani za kishirikina, huku nyumba yake ikiteketea, na familia yake kunusulika kifo kwa kutoboa nyumba.

Mwandishi wa mtandao huu kutoka Ludewa Basil Makungu anaripoti kuwa tukio hilo limetokea usiku wa octoba 01 mwaka huu majira ya saa nane alfajili baada ya mlango wa Nyumba yake kufungwa nje na watu wasiojulika kutokana na mvutano uliotokea kati yake na wauaji kabla ya wauaji hao kumzidi nguvu na hatimaye kuchoma nyumba yake.

Akizungumza katika eneo la tukio Cesilia Haule ambaye ni mke wa marehemu Laurance alisema kuwa yeye na mumewe walikuwa wamelala chumbani na watoto wao wawili wakiwa wamelala sebuleni na kwamba ilipofika saa nane za usiku watu wasiojulikana waligonga mlango na kutoa masharti ya kutokutoka nje.

Ester Nkwera ni mtoto wa marehemu na Mwanafunzi wa darasa la nne katika shule ya msingi Kimbila anasema yeye alikuwemo ndani wakati Nyumba ikiunguzwa moto na kwamba yeye na mama yake walifanikiwa kujiokoa kwa kutoboa nyumba yao ya miti lakini Baba yake alibaki pamoja na mdogo wake Laurance.

Laurance ni mtoto wa marehemu mwenye miaka mitano tu, yeye alinusurika kifo kwa kupita katika mikono ya wauaji ambao walikuwa wamezingira nyumba hiyo ya miti huku wakiwa wamesimama pembeni kuhakikisha Nyumba na vyote vilivyomo vinateketea.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Ibani Philipo Haule, Afisa Mtendaji Kata Onesmo Haule wamesema kuwa marehemu pamoja na watu wengine wanne ni muda mrefu walikuwa wakituhumiwa kujihusisha na kuwatesa watu kwa uchawi ikiwemo kubaka wake za watu kiuchawi, kuua watu na kuwafanyisha kazi usiku kwa uchawi.

Wakizungumza kwa masharti ya kutoandika majina kwa kuhofia usalama wao wakazi wa kitongoji cha Ibani Ludewa walisema wamechoshwa na udhalilishwaji unaofanywa na wachawi ikiwemo kuwabaka wake zao kiuchawi,kuwauwa na kuwatumikisha kazi usiku na kwamba watahakikisha wanaikomesha tabia hiyo kwa kila anayehusika kwa kuwa wananfahamika.

Aidha Monica Mchiro Diwani wa Kata ya Ludewa alikiri kufanyika kwa mkutano wa hadhara octoba 11 mwaka huu unaowahusu watu watano wanaotuhumiwa na Wananchi kuwatesa kwa nguvu za uchawi hata hivyo watuhumiwa akiwemo marehemu walikana kuhusika na matukio hayo.

Bi Monica aliwataka wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi na badala yake watoe taarifa polisi na ofisi za vijiji na Kata kuhusu uhalifu wowote uanotokea katika maeneo yao.

Kufuatia tukio hilo,Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Bi Georgina Bundala amemwagiza mkuu wa polisi wilaya kuhakikisha wale wote waliohusika na ukatili huo wanakamatwa haraka na kupelekwa mahakamani ili sheria iweze kufuata mkondo wake.

Aidha Bundala amekemea vikali tabia hiyo na kusema kuwa kwa jamii iliyoelimika haiwezi kufanya mambo kama hayo, na kuongeza kuwa kuna haja ya kutoa elimu kwa wananchi ili kuwajengea uelewa namna ya kukabiliana na matukio kama hayo kwa kufuata sheria.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa Kamishna Msaidizi wa polisi Evarist Mangala alikiri kutokea kwa mauaji hayo na kwamba taarifa kamili atatoa baada ya kupata taarifa kamili ingawa alikiri kuwa chanzo cha mauaji ni imani za kishirikina

Blog ya Maisha na Mafanikio inatoa pole kwa wafiwa wote kwa janga hili. Pia inapenda kutoa ushauri kuwa ingekuwa jambo la busara au ni jambo la busara kutumia vyombo vya sheria. Swali langu ni kwamba hao wanaosema Mzee Nkwera alikuwa na tabia hii wanajuaje kama wao nao wanahusika?
TUONANE TENA JUMATANO IJAYO MPAKA HAPO MUWE NA WAKATI MZURI!!

Tuesday, November 1, 2011

AHSANTE BABA!!!

Hapa Mwenyewe Mzee Ngonyani

Unajua/mnajua kama kumbukumbu nyingine zinakuja wakati ukisikiliza mziki? Basi mimi leo nilikuwa nasikiliza mziki na mara nikakumbuka kisa hiki ambacho kilinipata. Nikiwa nikiishi kijiji cha Kingoli. Nakumbuka nilikuwa darasa la tano. Kwanza nianze na KUMSHUKURU BABA kwa tabia yake aliyokuwa nayo ya kila usiku kupita na kuangalia watoto wamelala? Kwani siku hii aliokoa Maisha yangu. Siku hiyo kama kawaida, nilikuwa na homework , basi baada ya chakula cha jioni nikachukua koroboi yangu na kuanza kusoma. Nilikuwa nimejilaza kitandani na nikaweka karoboi kifuani huku nikisoma. Muda ukapita, nikapitiwa na usingizi. Si mnajua huwezi kulala tu bila kugeuka. Nikawa nimegeuka bila kufikiri ya kwamba koroboi bado inawaka. Halafu mbaya zaidi nilikuwa nimejifunika blanketi. Kama baba angechelewa kidogo tu basi leo nisingekuwa hapa. AHSANTE BABA.

Huu hapa ndio wimbo ambao umenikumbusha kisa hiki.....