Wednesday, November 16, 2011

WAMALAWI NA NDOA ZA VIBINTI!

Ni JUMATANO NA NI KILE KIPENGELE CHETU CHA MARUDUI YA MADA/MAKALA NA MTUKIO MBALIMBALI. LEO NIMEPITA KUPEKUA KWA MDOGO WANGU WA HIARI AMBAYE KWA SASA SIJUI YUPO WAPI SI MWINGINE TENA BALI NI KOERO BINTI WA MKUNDI.BONYEZA HAPA.


Mmoja wa wa waathirika wa ndoa hizo



Binti huyu naye ni miongoni mwa waathirika wa ndoa hizi za vibinti


Huyu sio babu na mjukuu wake bali ni mtu na mkewe


“Baba yangu wa kambo aliniamuru niache shule ili niolewe na mzee wa umri wa miaka 77, kwa madai kuwa umri wangu ni mkubwa ukilinganisha na darasa ninalosoma, kwani wakati huo ndio nilikuwa niko darasa la nne. Nilimkatalia na kumweleza wazi kuwa ningependa kuendelea na masomo”. Hivyo ndivyo alivyoanza simulizi yake binti huyu Balita Simpokolwe.



lakini hata hivyo kukataa kwake hakukuweza kumsaidia.



Kwani baba yake alianza kumtuma sokoni kuchukua fedha kwa mtu mmoja mzee hivi, ambaye alikuwa hamfahamu, ambapo alikuwa akipewa kiasi cha kati ya dola 5 mpaka 10, kiasi ambacho alitakiwa anunulie chakula na kiasi kinachobaki alikuwa kumpa baba yake huyo wa kambo.



Balita anakiri kwamba hakuweza kuhisi jambo lolole kuhusiana na zile pesa alizokuwa akipewa na yule mzee kwa kuwa aliamini kuwa yule alikuwa ni rafiki wa karibu wa baba yake wa kambo. Lakini wiki tatu baadae tangu awe anakwenda kuchukua fedha kwa mzee yule, alishangaa kumuona akija nyumbani kwao na jembe dogo la kulimia bustani. ( kwa mila za watu waishio Malawi Kaskazini hususan katika wilaya ya Nsanje jembe dogo la kulimia bustani inatumika kama ishara ya mahari)



“Nilishtuka sana, baada ya baba yangu wa kambo kunitaka nipokee jembe lile la bustani kutoka kwa yule mzee. (Kwa mila zao, binti kupokea jembe kutoka kwa mwanaume ni ishara kuwa amekubali kuolewa na mume huyo). Lakini huku nikiwa imechanganyikiwa, nilikataa kupokea jembe lile.”



Hata hivyo mama yake aliungana naye kupinga binti huyo kuolewa kwa kuwa bado alikuwa ni mdogo, “baba yangu wa kambo alikuja juu akidai kuwa atampa talaka mama yangu iwapo atapinga mimi kuolewa na mzee huyo, na cha kusikitisha zaidi alidai kuwa haiwezekani nisiolewe na mzee huyo kwa kuwa tumeshakula fedha zake.” Alisema binti huyo kwa masikitiko.



Hivyo alilazimishwa kuolewa na mzee huyo, lakini baada ya wiki mbili tangu aolewe kikundi kimoja cha kutetea unyanyasaji wa wanawake na watoto kiitwacho Chitipa Women’s Forum kilimuokoa kutoka katika ndoa hiyo baada ya kuwashwishi wazazi wa binti huyo wamrejeshe shuleni.



Belita Simpokolwe, sasa anaishi na mmoja wa baba zake wadogo, amefurahi sana baada ya kurejea shule kuendelea na masomo yake. Tukio hili ambalo lilimpata Belita Disemba mwaka 2008 lilimuacha akiwa na amesathirika kisaikolojia.



Kwa mujibu wa mwalimu anayemfundisha alikiri kuwa kuna wakati alikuwa anashindwa kuzingatia masomo yake pale kumbukumbu za tukio lile la kutolewa shuleni na kuozeshwa kwa nguvu linapomjia, lakini binti huyo ambaye alikuwa na miaka 13 wakati huo akiozeshwa, amemudu kuendelea na masomo yake ambapo anataka kutimiza ndoto zake za kuwa muuguzi hapo atakapomaliza masomo.



“Kinachoniuma ni kwamba nimekuwa ni muathirika wa ndoa ya utotoni baada ya wale niliowaamini kuwa watanitunza na kunilinda kunitoa kafara kiasi cha kutaka nisitimize ndoto yangu” alisema binti huyo aliyekuwa akisoma shule ya msingi Kawale kaskazini mwa Malawi, akiwa yuko darasa la sita wakati huo.



Belita ni mmoja kati ya mabinti walioathiriwa na mila marufu kama Kupimbira, ambapo mabinti hulazimishwa kuacha shule na kuozeshwa kwa wazee ili kujipatia mahari, na hii hufanyika bila hata ya binti kufahamishwa.



Wakati mwingine wazazi hulazimika kuwaozesha mabinti zao ili kulipa madeni.



Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa hivi karibuni na tasisi ya Chipita Women’s Forum inaonyesha kwamba ,taktibani asilimia 17 ya mabinti huachishwa shule na kuozeshwa kwa wazee, huku wengine wakilazimika kuacha shule wenyewe kutokana na unyanyasaji wa kijinsia unaofanywa na waalimu wa kiume na wanaume wakware wenye uchu wa kufanya mapenzi na vibinti.



Akizungumzia mila zinazotumika kuwakandamiza watoto wa kike na kuwakatisha shule Mwenyekiti wa Chipita Women’s Forum, Bi Ruth Mbale alizitaja mila kama ‘Kupimbira’, ambapo mabinti hulazimishwa kuacha shule na kuozeshwa kwa wazee ili kujipatia mahari, ‘Nhlanzi’ ambapo familia ya mke huozesha binti mwingine kwa mume wa binti yao kama zawadi kutokana na kuitendea wema familia husika, ‘Kulowa kufa’ mwanamke aliyefiwa na mume kuingiliwa kimwili na mwanaume mwingine ili kuondoa mkosi wa vifo kijijini, kwa kawaida shughuli hiyo hufanywa na mwanamume maalum wa kufanya shughuli hiyo. Mila hii pia inasemekana inafanyika hapa nchini hususana wilayani Ukerewe ambapo hujulikana kama ‘Kusomboka’, hii kwa hapa nchini hufanywa na wanaume na wanawake. Bi Mbale pia aliitaja mila ya ‘Fisi’ ambapo mume ambaye hana nguvu za kiume anamkodisha mwanume wa nje ili amuingilie mkewe kwa ajili ya kumpa ujauzito, lengo kuu ni kujipatia watoto.



Bi Mbale alikiri kupata ugumu katika kupiga vita mila hizi kutokana na usiri mkubwa uliokuwepo katika jamii hiyo ya watu waishio Kaskazini mwa Malawi.



Akizungumzia idadi ya mabinti waliiokolewa na taasisi yao tangu walipoanza kampeni ya kuwaokoa wanafunzi walioozwa kabla ya kumaliza masomo, Bi Mbale alisema kuwa wamefanikiwa kuwaokoa mabinti 40 waliokuwa na umri kati ya miaka 7 hadi 16 ambapo walirejeshwa shule na kuendelea na masomo.



Alisema kuwa, ingawa inakuwa ni vigumu kwa mabinti hao kurejea katika hali yao ya kawaida kabla hawajaolewa lakini huwapa ushauri nasaha hadi warejee kwenye hali zao za kawaida na kuendelea na masomo yao.


Habari hii nimeitoa kutoka vyanzo mbalimbali vya habari ukiwemo mtandao wa inteneti.

6 comments:

ray njau said...

Haya ndiyo matokeo ya tamaa mbaya.
Wanaume tumeamua kujidhalilisha wenyenyewe kwa kutamani mabinti zetu badala ya kuwalea katika maadili mema.

"NDOA NI KUFAANA NA SIYO KUFANANA"

Goodman Manyanya Phiri said...

@ Ray Njau

Asante sana Mkuu kwa kulileta jambo hili kama lawama kwa sisi wanaume WOTE!!!


Sasa nikiongelea nje ya shukrani zangu kwa Bw Ray Njau: Stori ya binti huyu ni nzuri sana, tena imekaa vizuri kwa mwelekeo na desturi za maandishi anayeyapenda na kuyaunga mkono Kapulya wetu, mimi ni naye daima.


Hata hivyo ninayo matatizo kidogo leo, labda kwa sababu nimezaliwa nao Wamalawi hasa wa kaskazini, mnisahihishe tafadhali.


1. Tunasikia malalamiko ya upande mmoja tu katika hili. Sasa tutaridhika-je kwamba tunayoyasikia kwa yule binti ndio ukweli?


2. Hata yakiwa ni ukweli, na amini si halali kuwataja Wamalawi, Watanzania, Waswidi au taifa lolote lile katika maovu yoyote ile, kwan dhambi ni ya kila binadamu kote ulimwenguni. Pia, haiji kabisa katika fani ya waandishi kuupeperusha utaifa hata ukabila katika kutaja maovu; na hata ingekuwa ni halali, mimi binafsi ningeonyesha kwamba makabila mengi sana duniani kote anafanya kama ilivyoripotiwa hapo juu (kama vile kila taifa duniani linao majambazi, walawiti, walarushwa na kadhalika wake). Mfano mzuri juu ya mada ya leo, hapa Afrika Kusini ukiwa binti unaibiwa hata unapokwenda kuchota maji kisimani na tayari umeolewa na wale waliyekuiba wazee mara nyingi ni mara tatu au nne ya umri wako! Hata Ulaya, Asia na Amerika utawapata wanaume kama hao kutokana na dhambi ya kugeuza mwili wake Hawa uwe kama mali ya soko tu!


3. La mwisho kwangu ni hili. Lazima sheria za nchi zitumike pia zipewe nafasi yazo ya kushughulikia mambo kama hayo. Na naamini Malawi nayo pia inazo sheria za kupigana dhidhi ya uhalifu kama huo. Bahati mbaya, macho yangu hayakuona hata neno moja kwa mlalamikaji kwamba alivitumiaje vyombo vya dola kujitetea. AIBU KU-PRINT TUHUMA KUHUSU WATU WENGINE BILA KUHUSISHA KWANZA VYOMBO VYA SHERIA KAMA INAVYOSTAHILI! Unaweza pia ukashtakiwa bure!

ray njau said...

@Goodman:-
Ni kwa tukio baya sana mada hii imegusa kwenye chimbuko lako lakini lengo la mtoa habari ni kutimiza wajibu wake wa kuielimisha jamii kupitia blogu yake ya maisha na mafanikio.

Nakusihi urudishe moyo wako na tuungane pamoja tukiwa wadau katika maisha na mafanikio ya jamii yetu na Yasinta akiwa ni mwanamke katika harakati za kuibua changamoto zinazoizuia jamii kufikia maisha na mafanikio.

Dhana ya woga iliojengeka mioyoni mwa wanaume wengi ni kutopenda kabisa kukosolewa na wanawake hasa pale hali ya kukumbatia tamaa mbaya kwa kisingizio cha kudumisha mila chakavu na zilizo nje ya kalenda kupita udhalilishaji wa wanawake na mabinti katika hizi zama za teknohama.

Goodman Manyanya Phiri said...

@ Ray Njau

Kwa heshima yako, Mkuu!

ray njau said...

Hongera sana Goodman kwa kuithibitishia hadhira kuwa wewe ni goodman katika harakati za wanawake na mabinti kufikia maisha na mafanikio.Hongera sana Yasinta kwa kuwekeza katika harakati za wanawake na mabinti kufikia maisha na mafanikio.Hongereni sana wadau wa blogu ya maisha na mafanikio kwa kuendelea kuungana na Yasinta katika harakati za kuibua vikwazo vinavyozuia wanawake na mabinti kufikia maisha na mafanikio ndani ya zama za teknohama.

Yasinta Ngonyani said...

Kaka Ray! Nakubaliana nawe kwanini mabinti? maana kuna wanawake wengi tu. Yaani nimejiuliza hata jibu sipati mjukuu sawa na mke sijui wanajisikiaje hawa watoto wanapoanza kucheza badala ya kuwa mke. Kwasababu hajakamilisha ile hali ya utoto. Mmmmhhh kazi ipo

Kaka mkubwa Phiri! Haikuwa makusudi yangu kugusa huko ulikosema ilikuwa na kuwakilisha ujumbe.
Ahsante wote kwa kuwa nami kwa kuwakilisha ujumbe huu.