Showing posts with label upweke. Show all posts
Showing posts with label upweke. Show all posts

Wednesday, September 15, 2010

NIMEUPENDA MSEMO HUU!!

"HAKUNA ANAYEJUA UPWEKE UNAOSABABISHWA NA YEYE KUTOKUWEPO MAHALI FULANI"

MTU AKIONDOKA MAHALA HUACHA UPWEKE, NA UPWEKE HUO HAUSIMULIKI. INA MAANA NI LAZIMA UWEPO ILI KUUHISI.
NA UPWEKE HAUWEZI KUWEPO KAMA WEWE UPO

INA MAANA:- NI LAZIMA WEWE USIWEPO ILI UPWEKE UWEPO NA HAKUNA NAMNA YA KUUSIMULIA UPWEKE, HIVYO NI LAZIMA UWEPO ILI KUUJUA
KWA HIYO, HAKUNA AJUAYE UPWEKE USABABISHWAO NA YEYE KUTOKUWA MAHALA FULANI KWANI NI LAZIMA ASIWEPO ILI UPWEKE UWEPO NA HAKUNA NAMNA YA KUUSIMULIA MPAKA UWEPO."
Hii ni nukuu nzuri sana na mimi napenda sana:- Ukitaka kujua nimeipata wapi basi sikiliza kwa kakangu Mubelwa.

Wednesday, September 8, 2010

Upweke, Je wewe umewahi kujisikia mpweke??


Katika maisha haya ya kublog tumekuwa kama vile ndugu, mmoja akiadimika bila taarifa basi twapata wasiwasi. Nimewaza na kuwazua hawa binadamu wamepatwa na nini?. Na mwisho najisikia UPWEKE. Na katika pita pita zangu kama kawaida nikakutana na shairi hili nikaona si mbaya hata kama tumesoma lakini kusoma tena na tena ndio kukumbuka mambo, haya karibu !!. Na shairi hili lina toka kwa mtani wangu Fadhy Mtanga.

Pale unapojikuta u-mpweke, je? ufanyeje?

Upweke jama adhabu, upweke unasumbua,
Upweke ni maghilibu, kukufanya kuugua,
Watamani wa karibu, nenolo taelijua,
Upweke.

Upweke hutesa sana, umpendaye awe mbali,
Utamuwazia sana, hata mara alfu mbili,
Kwa usiku na mchana, maumivu ni makali,
Upweke.

Upweke unakondesha, chakula hukitamani,
Upweke unahenyesha, simanzi tele moyoni,
Homa pia hupandisha, na mwokozi humuoni,
Upweke.

Upweke tele mateso, hata machozi kulia,
Moyoni ni manyanyaso, nao moyo kuumia,
Wala si kimasomaso, kwani huleta udhia,
Upweke.

Upweke ni kama jela, huleta nyingi simanzi,
Huwezi hata kulala, maisha tele majonzi,
Utapiga hata sala, uruke vyote viunzi,
Upweke.

Upweke sawa na shimo, mtu ukatumbukia,
Nako shimoni uwamo, wateswa nayo dunia,
Kwani hauna makamo, kuweza kuvumilia,
Upweke.

Wednesday, November 11, 2009

JE UPWEKE NI UGONJWA?/ UPWEKE

Wapendwa posti iitwayo JE UPWEKE NI UGONJWA hii niliandika 27/8/2009 naomba kama hukusoma basi ipitie ndo utajua kwa nini nimeweka shairi hili la kaka Fadhy Mtanga.

Upweke

Upweke jama adhabu, upweke unasumbua,
Upweke ni maghilibu, kukufanya kuugua,
Watamani wa karibu, nenolo taelijua,
Upweke.

Upweke hutesa sana, umpendaye awe mbali,
Utamuwazia sana, hata mara alfu mbili,
Kwa usiku na mchana, maumivu ni makali,
Upweke.

Upweke unakondesha, chakula hukitamani,
Upweke unahenyesha, simanzi tele moyoni,
Homa pia hupandisha, na mwokozi humuoni,
Upweke.

Upweke tele mateso, hata machozi kulia,
Moyoni ni manyanyaso, nao moyo kuumia,
Wala si kimasomaso, kwani huleta udhia,
Upweke.

Upweke ni kama jela, huleta nyingi simanzi,
Huwezi hata kulala, maisha tele majonzi,
Utapiga hata sala, uruke vyote viunzi,
Upweke.

Upweke sawa na shimo, mtu ukatumbukia,
Nako shimoni uwamo, wateswa nayo dunia,
Kwani hauna makamo, kuweza kuvumilia,
Upweke.

Thursday, August 27, 2009

JE, UPWEKE NI UGONJWA?

Kabla na baada ya kuja huku niliko nilikuwa na marafiki wengi kifani. Lakini baada ya kuishi mwaka mmoja hap nililetewa barua toka kwa marafiki zangu na kuniomba niwatafutie wachumba au kazi. Na nilipowajibu kuwa mimi nilikuwa mgeni, pia binafsi sikuwa na kazi wala sikujua lugha walikata mawasiliano nami.
Nikawa nashangaa kwa nini? je? hawa kweli walikuwa marafiki wa kweli yani wale ambao wanasema hufaana kwa penye furaha na taabu. Kwa hiyo nikabaki mpweke bila rafiki wa karibu isipokuwa nilikuwa na rafiki yangu wa karibu sana ambaye ni mume wangu na baadaye wanangu. Na baadaye yaani kama mwaka mmoja uliopita nilianza kublog na hapo nikapata marafiki wengi tena. Na natumaini ninyi rafiki nilowapata hamtanikimbia. Hii ndio sababu nimeuliza je? upweke ni ugonjwa? kwasababu mimi nilikosa sana raha nilipokuwa mpweke.

Friday, March 6, 2009

SITASAHAU MWAKA 2004­-2005

Sitasahau:- Ghafla 18/8 2004 niletewa habari kuwa sina mama tena. Ilikuwa kama ndoto, kwani sikuletewa habari kuwa anaumwa. Kwa hiyo sikuamini kabisa. Kwa kweli ni pigo kubwa sana kuondokewa na mama. Huku mbali ugenini sikujua nifanye nini, kwenda nyumbani ni mbali. Maisha yangu yanazidi kuwa magumu;- ningebaki nyumbani NINGE. Kwani kuna mambo mengi watu wanahitaji kuongea /kupata ushauri wa mama, sasa nitaenda wapi. Kila nikifikiria hili jambo nakosa raha kabisa. Pole mama yangu hajawafaidi /hajacheza na wajukuu wake. Na pia pole mimi sijamfaidi mama. Namshukuru mume wangu pamoja na marafiki wote kwa kunifariji wakati nilipokuwa na majonzi. Naweza kusema ilikuwa si mbali sana ningechanganyikiwa kabisa. Kwani kidogo nilichanganyikiwa niliacha kula nilikataa kwenda kazini pia shuleni nilichotaka ni kulia tu kwa kweli ilikuwa hatari. Ukizingatia pia sikuweza kuhudhuria mazishi kwa maana hiyo inakuwa vigumu sana kuamini. Mwaka huu mzima ulikuwa mwaka wa majonzi na mateso makubwa sana nilipungua/ kilo 10 hivi. Ila kwa maana nyingine nasi tulihudhuria mazishi yake. Tuliwaombe wapige picha (video) lakini hata hivyo sio sawa na kuwa pale. Kwa hiyo mpaka sasa kichwani/akilini mwangu mnaniambia mama bado yupo. Nimesahau kusema mama alitutoka trehe 17/8-04 saa mbili usiku hii siku ilikuwa si siku nzuri kwani pia binti yangu ilikuwa siku yake ya kwanza kuanza shule. Mama alizikwa 19/8-04

Mapema 2005 mwanzoni tukafunga safari kwenda nyumbani Tanzania. Ilikuwa taabu sana nilibadilika, sikutaka kutoka pale nyumbani kwenda mbali. Kama vile kusalimia marafiki Wino-Matetereka. Nilikuwa naogopa, nilikuwanamsubiri mama. Kwani ilionekena kama tu, ameondoka kidogo. Au yupo safarini. Nadhani maisha yangu hayatakuwa kama yalivyokuwa. Wakati mwingine siwezi kuamini eti mama hayupo. Wengi waliumia sana siku ile, ila kwa kuwa mbinafsi nataka kusema mimi niliumia zaidi. Naletewa habari mama hayupo, lakini siwezi kwenda kwenye mazishi pia wala kumwona mama yangu kwa mara ya mwishoyaani ile (BURIANI). Hii ndio maana siwezi/sitaki kuamini pia kusema hili neno marehemu. Kwa sababu kwa mimi mama yupo nami si marehemu.HILI SITASAHAU.

Monday, September 15, 2008

UNGEKUWA WEWE UNGEFANYEJE?

Umekuwa kijana/msichana wa umri wa kuoa/kuolewa. Umefunga ndoa na matunda yanaonekana. Watoto hao.
Lakini katika historia/ukoo wako wewe ni mtoto pekee kwa baba na mama yako.

Na wewe sasa una mume, watoto na kazi. Watoto wanaenda chekechea, mume ana kazi pia. Na wewe kazi yako mara nyingi mchana na usiku.
Mchana sio kitu watoto watakuwa chekechea au shuleni. Tatizo usiku, umejaribu kumwomba mama yako mzazi msaada awatunze wajukuu. Wajukuu ambao ndio hao tu ambao anao. Lakini kila mara anakataa. Je? ungekuwa wewe ungefanyeje?

Thursday, August 14, 2008

AGOSTI 15, 2008 MAISHA YANGU


Kila nikiwaza sipati jibu, kwani maisha yangu ni tofauti sana na ndugu zangu. Mara nyingine naona kama nimetokea hewani (yaani sina ndungu na pia sina mama wala baba) niliondoka nyumbani mapema. Nikiwa na miaka 16, nilianza kujitegemea mapema sana kuliko ndugu zangu. Sijaishi sana na wazazi wangu na sijawategemea sana. Sijafaidi kuwa mtoto wao kama mwenzangu. Na pia sijawategemea sana kwa jambo la uchumi ila kwa namna nyingine. Yaani kama nilivyokuwa shuleni nilipata pesa za matumizi labda kama 200-500Tsh, na hiyo ilikuwa ni matumizi ya mwezi mzima au zaidi. . Wakati nilikuwa mdogo nilikuwa na kanga upande mmoja, vyupi viwili, magauni mawili moja la kuchezea na moja la jumapili. Nilikuwa narithi magauni ya mama, anapunguza na ananishonea mimi. Viatu nilikuwa nasikia jina tu nikipata ndala (za matairi ya gari) nilikuwa najisikia kweli. Fikiria mwenyewe kwenda mstuni kutafuta kuni bila viatu. Unachomwa na miba, unaweza kukanyaga nyoka n,k. Sio kusema wazazi wangu hawakuwa na uwezo hapana. Ila hawakuona kama ni muhimu watoto kuwa na vitu vingi. Pia nilipokuwa mdogo mambo ya kunywa soda, kula pipi hayakuwa kabisa kichwani mwangu. Kwani hatukuzoeshwa Sio kusema maisha yangu yalikuwa mabaya hapana. Mahitaji muhimu nilipata kama kawaida. Lakini sasa watoto wengi hawaridhiki na gauni/shati au suruali moja. Pia wanataka viatu. Na halafu wanataka kila mtu na chumba chake cha kulala. Mimi nilikuwa nanalala chumba kimoja na kitanda kimoja na kaka yangu . Kila mtu alionyesha kichwa upande wake. (mzungu wa nne) Lakini leo mdogo/ndugu zangu wana karibu kila kitu. Kwa jambo hili mara nyingi najisikia nipo peke yangu hapa duniani.

Maisha yangu kwa ujumla hayajawa rahisi. Kipindi kile nasoma kuwa karani nilipata shida sana mimi, asubuhi nilikuwa naamka kuandaa chai na baadaye kwenda shule kwa mguu labda kama saa moja au dakiki 45 hivi. Mchana nilikuwa nabaki shuleni, kwani mwanzoni nilikuwa narudi na sikupata chakula. (Bali ilikuwa kwenda kuchota maji unajua tena foleni kubwa.) Niliporudi na maji kuanza kuandaa chakula, na baadaye muda wa kurudi shuleni umefika. Basi ni kugeuza tena tu bila kula kwani ningekula basi ningechelewa. Nilikuwa naishi kwa "ndugu" lakini nilikuwa kama MFANYAKAZI (mama wa nyumba alikuwa mkatili mno sio mchezo). Jioni baada ya shule kufika tu bila kula kitu amekwishaandaa mahindi kwenda kusaga na niliporudi tu ni kuchukua ndoo kwenda kuchota maji na pia kuandaa mboga. Usidhani hapakuwa na watoto wao, walikuwepo. Lakini walikuwa wanacheza, kufanya homework au walikaa tu. Kila siku hivyohivyo kwa muda wa miaka 2. Labda ndio maana maisha yangu sio kama ndugu zangu, na ndio maana sikuweza kufanikisha masomo yangu vizuri. Kwa namna nyingine namshukuru (mama wa nyumba) amenifundisha jinsi ya kujitegemea, kuishi peke yangu. Ila jamani tembeeni mwoone mmh maisha ni safari ndefu.