Thursday, February 28, 2013

TUUMALIZE MWEZI KIHIVI:- NANGOJA ANIUE, NIKIONDOKA WANANGU WATATESEKA!

Kama mnavyojua kuwa hivi karibuni nilikuwa huko nyumbani Tanzania, na nilikuwa pande za huko kwetu Ruhuwiko Songea ambapo nilikaa kama mwezi  hivi.
Kusema kweli yapo mengi ya kushangaza, ya kutisha na yenye kufurahisha ambayo niliyashuhudia, na kusema kweli kuna mengi nimejifunza. Lakini labda niseme tu kwamba aina ya maisha niliyoyakuta huko kijijini, kwa kweli yalinipa picha kwamba bado kuna safari ndefu sana katika kuufikia ukombozi wa huyu kiumbe mwanamke.
Ninayo mifano mingi lakini tukio nililolishuhudia siku moja nikiwa katika matembezi yangu liliniacha mdomo wazi, na labda niseme kwamba limenikaa hadi leo akilini nikijaribu kuwaza na kuwazua lakini sipati jibu.
Sijui nianze vipi?...Ahh! Kuna siku katika matembezi yangu nikakutana na kundi la akina mama wamekaa wakipiga gumzo, lakini nyuso zao zilikuwa zimegubikwa na huzuni. Nilishikwa na tashwishwi, nikajongea pale walipo ili kujua kama kuna jambo gani limetokea kiasi cha kuwakusanya pale huku wakiwa na nyuso za huzuni.
Si mnanijua tena mie KAPULYA MDADISI. Nikawauliza, ‘jamani ndugu zanguni, kulikoni mmekaa na nyuso za huzuni, JE KUNA MSIBA?’
Wote waligeuka kuniangalia, lakini walionekana kusita kunijibu, na ndipo mmoja wao akaniambia kuwa usiku wa jana kulitokea kutoelewana kwa wanandoa wanaoishi hapo mtaani kiasi cha mume kumpiga mkewe mpaka akapoteza fahamu.
Niliuliza sababu ya ugomvi wao, na ndipo nilipoelezwa kwamba, sababu kubwa ni kwamba wanandoa hao wana watoto wanne ambao bado ni wadogo na mume anataka kuongeza mtoto wa tano, lakini mkewe hataki kwa kuwa hali ya uchumi hairuhusu, na pia bado wanalo jukumu la kuwalea hawa watoto wanne ambao kwa kweli ni wadogo. Hata hivyo alimshauri mumewe wavute subira kwanza ili watoto hao wakue.
Mume hakukubali ushuri wa mkewe na ndipo ugomvi ulipoanza.Walibainisha kwamba ugomvi wao ni wa mara kwa mara na sababu kubwa ni hiyo ila ugomvi wa safari hii ulikuwa ni mkubwa na kama sio majirani kuingilia kati basi mume yule angemuua mkewe.
Nikataka kujua kama anapata kipigo cha aina hii kila mara kwa nini asirudi kwao?
Wakanijibu kuwa, kwanza hana nauli ya kurudi kwao kwani si mtu wa Songea. Pili anaogopa watoto wake watateseka.
Mh! Nilishusha pumzi, ujinga gani huu. Hivi sisi wanawake ni nani ameturoga, yaani unakubali mtu anakutesa na kukunyanyasa kiasi chakutaka kukutoa roho lakini wewe umo tu! Ukiulizwa sababu unadai, eti watoto wangu watateseka!
Bado najiuliza hivi watoto wanne bado hawatoshi? Hili tukio kwa kweli nimekuwa nikijiuliza tangu nirudi huku Sweden, na mpaka leo sijapatajibu kwamba tatizo ni nini? Kutokuelewa haki zetu, ujinga au ni nini?
NAWATAKIENI WAOTE MWISHO MWEMA WA MWEZI HUU FEBRUARI (PILI)

Tuesday, February 26, 2013

PALE MNAPOKUTANA NA MLIOFANYA NAO KAZI/MLIOSOMA NAO....

 
 
......Furaha inakuwa ni ya ajabu...hapa ni mwalimu mtaafu Eusebius Mlelwa na mwal. Klaesson walikuwa wanafanya kazi pamoja Wilima Secondary hapa walikutana mwaka huu mjini Songea. Hapa ni stendi kuu ya Songea
Sio wao tu walipata bahati ya kuonana ..la hasha Yasinta/kapulya naye alionana na rafiki yake ambaye walisoma chuo pamoja ni Pendo Mapunda. Nilifurahi sana kuonana na Penda miaka mingi tulipoteana. Hapa ni Lizabon Songea.....Raha eeeehhhh....

Sunday, February 24, 2013

MUWE NA JUMAPILI NJEMA SANA UKIPATA WASAA SIKILIZA WIMBO HUU UTAMU WA YESU NA DADA ROSE MUHANDO!!!


Ni Jumapili nyingine tena na pia ni ya mwisho katika mwezi huu wa pili/februari..bado kama jumapili nne tu na itaqkuwa pasaka...NAWATAKIENI WOTE KWARESMA NJEMA NA WALE WATAKAO/WANAOFUNGU KILA LA KHERI.

Saturday, February 23, 2013

MAISHA NA MAFANIKIO YATIMIZA MIAKA MITANO /5 LEO :- 23/2/2008-23/2/2013!!!!

Kama mchezo nilizanza kublog  Jumamosi tarehe 23/2/2008 na leo ni Jumamosi 23/2/2013 imefika mika mitano..(5) hapa ni siku ya kwanza nilivyoanza ... bonyeza hapa Hakika Maisha na Mafanikio imetoka mbali ..JUMAMOSI NJEMA KWA WOTE...KAPULYA

Friday, February 22, 2013

IJUMAA YA MWISHO YA MWEZI HUU WA PILI TUIMALIZE NA UJUMBE HUU:- KILA BINADAMU ANA MAPUNGUFU YAKE!!!

Sisi binadamu tumeumbwa na mapungufu, Hakuna aliyekamilika kila mmoja ni tofauti na mwingine. Kuanzia kimawazo, kimatendo pia kitabia. Na kwa kuwa kama tulivyo, hii ndio maana tuna hitaji pale jambo linapopinda, tuchukue jukumu na kujaribu kuliweka sawa na pia KUSAMEHEANA. Ila KUMSAMEHE mtu si jambo dogo maana kama kweli unamsamehe mtu basi umsamehe KIDHATI/TOKA ROHONI. Au hata kumpa yule mtu aliyekosea/uliyepishana naye mawazo nafasi ya pili/ajaribu tena. Sababu yeye ni banadamu kama wewe, yule, mimi na wao. NACHOTAKA KUSEMA HAPA:- KAMA UMEHITILAFINA NA MTU JARIBU KUONGEA NAYE ILI KUSHULUHISHA NA UTAOANA MAISHA YANAKWENDA SAFI. KWANI KUKAA NA KITU MOYONI HAISAIDII KITU. Binafsi kama kuna kitu nimemkosea mtu/nimemdanganya mtu basi NASEMA SAMAHANI SANA, SANA, SANA, SANA....kwani hata mie ni binadamu na nina mapungufu.NA NINGEOMBA TUANZE UPYA/SECOND CHANCE. IJUMAA NJEMA!!

Thursday, February 21, 2013

HONGERA KWA KUTIMIZA MIAKA KUMI NA TANO(15) DADA /BINTI CAMILLA!!!

Dada Camilla ndani ya kitenge akiwa nyumbani Ruhuwiko mwaka huu..naenda kusakasaka picha pia...Mdada huyu ni fundi sana wa kupiga picha....
.....Na sio kupiga picha tu binti Camilla anapenda pia kusaidia kazi za jikoni kama mnavyoona . Hapa anatengeneza kachumbali...HONGERA SANA KWA SIKU YAKO YA KUZALIWA CAMILLA. Duh! siku zinakimbia kweli twamshukuru Mungu kwa kututakia kila jema na kumlinda binti yetu mpaka leo anatimiza miaka 15. AHSANTE KWA MEMA YAKO MWENYEZI MUNGU NA TWAKUOMBE UMPE NAFUU KWANI HII SIKU KAAMKA NA HOMA......

Wednesday, February 20, 2013

TANGAZO: MABINGWA WA KILIMO CHA MITI YA MBAO NA NGUZO WAMEREJEA. .....


Habari za jioni wandugu...nimetumiwa habari/tangazo hili na mzee wa Mzee wa LUNDUNYASA karibuni tuwe pamoja-------------------------------------------
Kampuni ya Anesa Co.,Ltd kupitia biashara yake tanzu ya Fresh Farms(T); kwa kushirikiana na kikundi cha “Rudisha Uumbaji wa Mungu kwa Kupanda Miti (RUMM)-Kilolo;” tukiwa mkoani Iringa, tumezindua programu maalumu iliyolenga kuwawezesha watanzania wengi kuwekeza na kumiliki mashamba ya miti ya mbao na nguzo kwa urahisi kabisa.
 1.  Progamu hii inaitwa “GREEN THE WORLD and BECOME RICH” ambapo tunauza mashamba yenye miti (miti pamoja na ardhi) kwa utaratibu wa mtu kulipa kidogo kidogo kwa kadiri ya kipato chake. Kiwango cha chini cha kununua ni ekari tano, ambapo utatakiwa kulipa walau asilimia 50% ya bei yote; kisha fedha inayobaki utaendelea kuilipa kwa awamu kwa kadiri utakavyokubaliana na kampuni
 2.  Tupo Iringa mjini na Kilolo (kijiji cha Mwatasi), na mashamba yapo maeneo mbalimbali katika wilaya za Mufindi na Kilolo. Yapo mashamba yenye miti kuanzia ya mwaka mmoja hadi minne, na bei zake ni kuanzia tsh. 700,000(laki saba) hadi 2,000,000 (milioni mbili) kutegemeana na umri wa miti husika. Bei zote zinajumuisha (miti pamoja na ardhi)
 3.  Miti ya mbao inachukua miaka kati ya 7 hadi 10 tangu kupandwa hadi kuvunwa. Wastani wa faida unayoweza kupata kwa ekari moja ya miti iliyokomaa ni tsh milioni tisa hadi kumi na tano (kama ungekuwa unauza leo). Gharama ya kuhudumia ekari moja kwa mwaka haizidi laki mbili. NOTE KWA WALE WAGENI KUHUSU KILIMO HIKI CHA MITI: Pamoja na taarifa hizi, kampuni inahamasisha watu ambao ni wageni kabisa na taarifa zihusuzo miti; kutafuta taarifa zaidi na zaidi kutoka vyanzo mbalimbali kuhusu kilimo-biashara hiki; ili kujiridhisha kabla ya kufanya maamuzi ya kiuwekezaji.
 4.  Mnunuzi akishafika na kuyatazama mashamba (au kama anayafahamu mazingira yalipo mashamba); akishajiridhisha, atasaini mkataba wa makubaliano ya kimalipo kati yake na kampuni, kisha ataanza malipo mara moja. Baada ya kukamilisha malipo yake, utafanyika utaratibu wa kupata hati za kimila/mikataba ya kiumiliki kutoka mamlaka ya baraza la ardhi la kata/kijiji kwa mujibu wa sheria ya umiliki wa ardhi ya vijiji ya mwaka 1999.
 5.  Fresh Farms(T) tukiwa na falsafa ya “Greening the world and Feeding People”; lengo letu ni kuhakikisha tunawasaidia mamia ya watanzania kutumia fursa ya uboreshaji mazingira; kwa kuwekeza vitega uchumi vya mashamba vinavyowahakikishia kipato kikubwa sasa na siku za usoni.
 6   Kampuni itaendelea kutoa usaidizi wa uangalizi na utunzaji wa mashamba yote yanayonunuliwa kutoka kwetu kwa utaratibu rahisi na nafuu kabisa. Nia yetu ni kuona kuwa kila anayewekeza; avune faida ya uwekezaji wake. Hivyo, hauhitaji kuhofu juu ya usalama wa shamba utakalonunua, popote utakapokuwepo utajihakikishia kuwa “investment” yako inafanyiwa juhudi kubwa kuhakikisha inakua.
 7.  Programu na ofa hii ni ya muda maalumu, imeanza tarehe 15, Februari, 2013 na itamalizika, Aprili, 14, 2013. Programu hii inaweza kukoma kabla ya tarehe ya ukomo, ikiwa ekari zilizotengwa zitaisha mapema. Hivyo kwa yeyote anayehitaji tunashauri kuwasiliana nasi mapema.
 Mawasiliano:
Iringa:Mkurugenzi, Albert Sanga (0719 127 901,  0766 742 414),albertnyaluke@yahoo.com
Dar es Salaam: Meneja Masoko, Markus Mpangala (0764936655),mwanazuoni27@gmail.com

TANZANIA YETU NA ...KARIBU TANZANIA!!!!


Tanzania, mito, bahari, milima, mabonde, watu, ngoma mila,utamaduni ndio asili yake..TUPO PAMOJA

Tuesday, February 19, 2013

MUDA UNAPITA,.....LAKINI......

Bwana wewe nikuambie siri moja ya maisha,…’Mzee mmoja alikuwa kakaa karibu nami kwenye daladala kaniambia, tulikuwa tumekaa wote kwenye daladala na muda huo nilikuwa nimechoka, sikupenda kusumbuliwa, hamu yangu ilikuwa kupata usingizi kidogo, kwasababu najua nina zaidi ya masaa mawili ndani ya daladala hadi kufika kwangu, siunajua tena foleni.


Nikamwangalia yule mzee, alikuwa kaniangalia kuonyesha kuwa ana jambo muhimu nikaona nimsikilize na kumwambia , `Niambie mzee, huenda likanisaidia katika maisha yangu…’

‘Katika mipangilioa yako ya maisha , fanya juhudi pangilia mambo yako, fanya kazi kwa bidii na ipende dunia kama vile utaishi milele..siunaniona mimi hapa nimezeeka nina miaka sitini, lakini najihisi kama nina miaka mingine sitini mbele, sijipweteki, na kusema aah, mimi mzee basi tena, nasubiri cha kupewa, nani atakupa hivihivi dunia hii. Najitosa hivyohivyo kama vile nitaishi milele, ingawaje kwa kweli naukumbuka sana, na kuujutia ujana wangu…’ akaniangalia kwa macho makali. Akaongezea kusema `wakati ni mali, lakini wakati ni ukuta, unahitaji mipangilio…’ akatikisa kichwa na kuendelea kusema;

`Pili muabudu sana mungu wako kama vile utakufa leo, au hata sasa hivi, huwezi jua, hapa gari linaweza likadondoka, tukawa wote marehemu au nikafa mimi peke yangu, au hata bila kudondoka gari unaweza ukakauka ghafla, na ukafa. Sasa ni bora umwabudu aliye na mamlaka na hiyo roho yako kwasababu hujui muda gani ataichukua roho hiyo. Omba, muabudu mola wako kama vile hapo unapoomba ni sekunde au dakika yako ya mwisho…’ akainama chini na nilijua anamuomba mola wake!

Nilijiukuta nimelala na nilipoamuka yule mzee akawa hayupo, ina maana aliteremka kituo nyuma wakati mimi nimelala, nilijuta sana, kwani alionekana ana busara na mengi yakunieleza, lakini nimechelewa keshaondoka.

Mzee huyu namfananisha na mwaka huu, unayoyoma, ni muda mchache umebakia tutauita jina jingine, mwaka jana au sio , na tutaukaribisha mwaka mpya. Mwaka huu tulikuwa nao na tulikuwa na mengi ya kufanya, na sijui mangapi tulifanikiwa kuyafanya na mangapi hatukufanikiwa, sidhani wengi wetu tuna kawaida ya kuweka kumbukumbu hizo, sidhani. Kumbukumbu hizo tunaziona kwenye bajeti za serikali, bajetiza makazini, lakini sio bajeti ya mtu mmoja mmoja.

Mwaka huu tupo nao kwenye kiti una mengi ya kutuambia, lakini tunajifanya tumechoka, tunajifanya tupo busy…labda tungelitulia tukatafakari na kuwa nao bega kwa bega k wa mipango, huenda tungelifanikiw sana. Tumekuwa tukikimbizana na hili na lile na huenda hayo tunayokimbizana nayo haya maana, tunapoteza muda mwingi kwenye vilevi, kucheza bao, kuongea na kufanya mambo ambayo ukiangalia ni ya kupotezea muda, muda uishe ulale, siku ipite. Ndio siku inapita, umri unakwisha na mwaka huo unakwisha, tukiamuka tutaukuta haupo tena!

Tukiangalia katika maisha yapo mambo mengi yanaharibu miili yetu hasa vyakula, vinywaji, vipodozi, hasira zisizo na msingi na mambo kadha wa kadha ambayo unayaona mazuri kwa umri wa miaka hadi telathini ujanani yaani, lakini ukifikia zaidi ya umri huo, hayo hayo uliyokuwa ukiyaona mazuri yanageuka kuwa sumu mwilini mwako. Mfano vyakula vya mafuta, pombe, starehe , madawa, vipodozi na mambo anuai, ni mazuri, yanastarehesha katika umri wa ujanani, lakini ikifikia uzeeni hayo matamu yanageuka kuwa machungu, yanakuwa sumu. Tunajikuta tunaamndamwa na presha, kisukari, ugonjwa wa moyo, vidonda vya tumbo nk, kwasababu ya yale matamu tuliyokuwa tukiyafadi ujanani. Kosa hatukua na mipangilio, hatukuali kusoma na kujifunza uzuri na ubaya wa hilo unalilofanya au kula!

Sasa wakati umefika kabla mwaka haujaisha kaa na huu mwaka kabla haujaisha, kumbuka yale ya muhimu, panga matarajio ukiwa na malengo kuwa utaishi milele. Na mipango hiyo haiwezi kuja kichwani tu, chukua karatasi pata muda, hata ikibidi soma, tafuta , uliza, kaa na mkeo au mumeo, angalieni matarajio, majukumu na mambo mbali mbali ya kimaisha yapangeni vyema na jinsi gani ya kuyatatua matatizo, jinsi gani ya kupata kipato, jinsi gani ya kusaidiana na hata kama huna kitu lakini kwa kujua nini kifanyike na kipi cha muhimu kwanza inasaidia, kuliko kulala, au kunywa pombe, au kusubiri mwisho wa siku ukaanza kupiga mayowe , kurusha mawe kwenye mabati eti unashagilia mwaka umekwisha, lakini umekwishaje? Ulikuwa nawo kweli wewe au ulikuwa umelala…!

Mkumbuke mola wako, kwani imani ni kitu muhimu sana, mola wako ndiye mwenye mamlaka na mwili wako, wangapi ulikuwa nawo siku za karibuni au mwaka huu sasa hawapo, je ina maana wao walikuwa na makosa na wewe uliyebakia huna makosa. Kumbuka wangapi wapo mahospitalini wagonjwa, wengine hawana viungo, wengine wanaomba mola awachukue kwa mateso wanayopata ya kansa au mengineyo, je wao walikuwa wanjua haya, je wao walimkosea Mungu ndio maana wanapata mateso haya, na wewe ni mbora zaidi yao ndio maana leo upo mzima. Hapana, wao hawajakosa, na wala wewe sio mbora sana mbora zaidi ni yule mcha mungu, ni yule anayemuomba mungu kuwa sala yangu hii huenda ikawa ya mwisho kuwa mzima, kuwa hai…nahivyo Sali kama vile hutaiona sekunde inayofuata.

Ujumbe huu nimetumiwa na msomaji wa Maisha na Mafanikio aishiye Arusha. Binafsi umenigusa sana nimeona nisiwe mchoyo niwajumuishe na wenzangu.

Monday, February 18, 2013

KULA MATUNDA NI MUHIMU KWA AFYA ZETU..TUSISAHAU

Matunda ya aina mbalimbali ni muhimu kwa afya zetu...tujaribu kuzingatia kula matunda ,,ikiwezekana kila baada ya mlo JUMATATU NJEMA KWA WOTE...

Friday, February 15, 2013

IJUMAA..TUSISAHAU TULIKOTOKA...UTAMADUNI WETU!!!

Kwa kawaida huwa napenda kusikiliza mziki ambao sielewi wanasema nini kwangu haina shida..kwa mfano hapa sijui wanasema nini ila nimependa sana na hapa nipo hoi ...najua hata wewe utapenda haya twende pamoja ....IJUMAA NA MWISHO WA WIKI UWE MWEMA KWA WOTE!!!!

Thursday, February 14, 2013

NINATISHIWA UHAI WANGU...EVARIST CHAHALI

Evarist Chahali
JUMAMOSI Februari 2 mwaka huu itabaki katika kumbukumbu zangu kwa muda mrefu, pengine katika uhai wangu wote.Majira ya saa 3 asubuhi nilikurupushwa usingizini na kelele za mlango uliokuwa ukigongwa kwa nguvu. Wakati ninajiandaa kwenda kufungua mlango, nikasikia sauti yenye dharura ikisema, “bwana Chahali, polisi hapa, tafadhali fungua mlango.”
Nilichanganyikiwa kwani tangu nifike nchi hii zaidi ya miaka 10 iliyopita sijawahi kufanya kosa lolote au kukwaruzana na vyombo vya dola/sheria. Baada ya kufungua mlango, askari waliovalia kiraia walijitambulisha na kuonyesha vitambulisho vyao. Pia walinisihi kuwa nisiwe na hofu ya kudhani kwamba nimefanya kosa lolote.
Kwa kifupi, walinieleza kuwa wamepewa ujumbe kutoka moja ya taasisi za intelijensia za hapa kuwa kuna tishio la uhakika dhidi ya maisha yangu. Hata hivyo, walieleza kuwa kwa vile wao walipewa tu ujumbe huo na kutakiwa kuuwasilisha kwangu, hawakuwa na maelezo ya ziada. Walisisitiza kuwa nichukue tahadhari muhimu na kunipa maelekezo ya mawasiliano ya dharura.
Kwa vile nilikurupushwa usingizini, awali taarifa hiyo ilionekana kama ndoto iliyokuwa inaendelea hata baada ya kutoka usingizini. Ilinichukua takriban saa tatu kuzinduka kutoka katika mshituko huo, na kutambua uzito wa taarifa niliyopewa na polisi hao.
Nikaamua kwenda kituo kimoja cha polisi kupata ufafanuzi zaidi. Mara baada ya kujitambulisha, mazingira ya namna suala hilo lilivyokuwa likishughulikiwa kituoni hapo lilinipa picha kuwa jambo hilo lina uzito. Kwa kifupi, baada ya kitambo nilipewa ufafanuzi ambao haukutofautiana na maelezo niliyopewa awali na polisi walionitembelea katika makazi yangu.
Kikubwa ni kuwa taarifa hiyo ilionyesha kuwa tishio hilo dhidi ya maisha yangu linatokea huko nyumbani. Swali linaloendelea kunisumbua kichwa ni KWA NINI iwe hivyo.
Wakati si vigumu kwangu kuhisi wahusika wa mpango huo wa kijahili, napata shida kuelewa kwanini wahusika hao watumie fedha za walipakodi kuandaa operesheni ya kutaka kunidhuru ilhali ninaamini kwa asilimia 100 kuwa mimi si tishio kwa usalama wa Taifa letu.
Ndiyo, baadhi ya ninayoandika kwenye makala zangu na tweets zangu huko kwenye mtandao wa kijamii wa twitter yanaweza kuwachukiza baadhi ya watu, lakini kwa hakika kuchukizwa huko si sababu ya kutaka kunidhuru.
Hadi wakati ninaandika makala hii nimekuwa nikiishi kwa tahadhari kubwa. Faraja kubwa kwangu inatokana na sababu tatu za msingi. Kwanza, kwa vile nilizaliwa na kukulia katika familia inayomtanguliza Mungu katika kila jambo, nina imani kubwa kuwa mamlaka pekee kuhusu uhai wangu (yaani kuwa hai au kufa) ni Mungu pekee. Hakuna mwanadamu anayeweza kupora jukumu hilo la Mungu na kufanikiwa kufupisha uhai wa yeyote.
Pili, nina imani kubwa na taasisi za usalama za hapa Uingereza. Kimsingi, wenzetu hawa wanathamini sana usalama na uhai wa binadamu pasi kujali mhusika ni mzaliwa wa hapa au ni ‘mgeni’ kama mimi. Ushauri na sapoti ninayoendelea kupata inanipa matumaini makubwa kuwa nipo kwenye ‘mikono salama.’
Lakini tatu ni ukweli kwamba takriban miaka mitano sasa nimekuwa nikiishi na uelewa kwamba kuna baadhi ya watu huko nyumbani wanaoniona kama kimelea cha maradhi hatari ambacho kikiachwa bila kudhibitiwa kitazua balaa.
Kwa sababu hiyo, tangu wakati huo nimekuwa nikiishi kwa tahadhari japo si kubwa kama hii ninayolazimika kuichukua sasa. Lakini ili uweze kuchukua tahadhari ni lazima uwe na mbinu na ujuzi wa kuchukua tahadhari husika. Kwa bahati nzuri, watu hao wanafahamu fika kuwa nina ujuzi wa kutosha na kuelewa na kumudu fika mbinu za kuishi kwa tahadhari.
Hata hivyo, kumudu mbinu ni suala moja na kuishi kwa kutumia mbinu hizo ni kitu kingine. Si jambo la kupendeza hata kidogo kuishi ukiwa na uelewa kuwa siku moja, mahala fulani unaweza kukumbana na madhara fulani. Lakini kadri unavyolazimika kuishi kwa namna hiyo inakuwa kama sehemu muhimu ya maisha yako, na ndivyo ilivyo kwangu.zaidi soma hapa

Happy Valentines Day/Upendo Daima kwa siku ya wapendanao /Alla Hjärtans Dag

VALENTINES DAY.!!!!
Leo ni Valentineday/siku ya wapendanao/alla hjärtans dag. Sio kama siku zote watu hawapendani HAPANA bali ni kuhamasisha watu wazidi kupendana . Kwangu mimi ina maana kubwa kwani nimekuwa mwanaharakati bora wa Upendo kwa jamii haijalishi nimefika kiwango gani . Nashukuru hata kama sijafika robo. Nakuomba nawe shiriki kutangaza Upendo Duniani. Upendo ulimwenguni kote! na Heri ya siku ya wapendanao kwa wanablog wooooooooooooote! HAPPY VALENTINES DAY.!!!!

Wednesday, February 13, 2013

UJUMBE WA MCHANA/JIONI YA LEO KUTOKA KWA KAPULYA....

Mapendo/upendo hauonyeshwi/hauonekani kwa macho isipokuwa kwa moyo/kutoka moyoni.Kwa roho yote.
KILA LA KHERI, UPENDO DAIMA!!!

CARDIOLOGY CLINIC AT AGA KHAN

The Aga Khan Hospital, Dar es Salaam is now offering Cardiology Clinics.

Monday - Friday, 2:00pm - 4:30pm and FREE consultations on Wednesdays and Thursdays.
For Booking / more information call: +255 22 2115151-53 ext 4702.


Tuesday, February 12, 2013

PAPA BENEDICT WA 16 ATANGAZA KUJIUZULU FEB 28 MWAKA HUU 2013!!!

 Baba Mtakatifu ameelezea kwamba matatizo
ya kiafya yamemfanya kutangaza kujiuzulu

Jana jioni nilipatwa na mshituko niliposikia katika habari, uwamuzi na hatua ya Papa Benedict XVI wa kujiuzulu mwishoni mwa mwezi huu baada ya takriban miaka minane akiongoza Kanisa Katoliki kwa hoja kuwa umri wake wa miaka 85 ni mkubwa kiasi kwamba hawezi kuendelea kuhudumu zaidi ya umri huo.

Makao makuu ya Kanisa Katoliki huko Vatican yanasema yanatarajia Papa mpya atachaguliwa kabla ya mwisho wa mwezi wa tatu, na sherehe za Pasaka.

Wanawake wenye sura hii hawawezi kumuuwa nyoka akafa….!

Sura hiyo hapo ni ya mwanamke. Bila shaka umeshwahi kukutana na sura kama hii katika maisha yako. Kama hujawahi kukutana nayo huenda kuna siku utakutana nayo. Jaribu kuzingatia mdomo, meno, macho na paji la uso. Zingatia baadaye, sura nzima kwa ujumla.
Mwanamke mwenye sura kama hii ana tabia zifuatazo:
Ni mwanamke mcheshi na anayependa kujichakesha. ni mwanamke ambaye ana uwezo na ufahamu mkubwa kiakili. Anajua sana kujiuliza maswali kabla hajafanya jambo lolote kuhusiana na namna anavyohusiana na watu wengine. Ni mwanamke mvumilivu na mwenye subira kubwa kwa wengine, hasa wanaomhusu.
Nikisema ni mvumilivu na mwenye subira, nina maana kwamba, anapokerwa na mpenzi, ndugu au rafiki, huchukua muda kufanya uamuzi, hakurupuki tu. Hujiuliza maswali ya hekima kabla hajafanya jambo. Lakini ni mwanamke ambaye hawezi kuuwa nyoka akafa. Ina maana kwamba, akitendewa ubaya leo, ataendelea kuukumbuka kwa muda mrefu sana. Hatalipa kisasi, lakini itakuwa ngumu kwake kusahau.
Mwanamke mwenye sura kama hiyo, hakawii kubadilika. Anaweza kuonekana amekata tamaa kabisa katika jambo au mambo fulani, lakini akitiwa nguvu kidogo anabadilika kabisa na kujipa nguvu ya kuweza na akaweza hasa. Mwanamke mwenye sura hii ana juhudi ya kujenga maisha yake kwa kiwango chenye kushangaza. Anapoamua kufanya hivyo, hufanya kweli na hana mzaha na kile anachofanya.
Ni rahisi kwa mwanamke mwenye sura hii kuvunjwa nguvu, lakini sifa moja kubwa kwake itakuwa ni ile hali ya kujiambia kwamba, ana maisha yake. Lakini kuna bahati mbaya kwamba, wanawake wenye sura kama hii, huwa wanaingia kwenye uhusiano wenye mashaka kirahisi. Wanatokea kupenda kama vipofu na kushikwa kirahisi na wanaume ambao wameingia nao katika uhusiano. Huwa wanasaidia sana kama wamempenda mtu na kusaidia huku hufikia hatua ya utumwa na siyo upendo.
Wenye sura hii wanavyoonekana sivyo wanavyojibu kwenye ombi la tendo la ndoa. Wanaweza kuonekana kama wako tayari kushiriki tendo la ndoa kwa kuonesha dalili zote muhimu, lakini majibu yakaja tofauti kabisa, hadi mwanaume akashangaa.
Hii inatokana na ucheshi wao, kuwa huru katika kujadili mambo na kuchelea kuwakera wengine. Kwa hali hiyo, huwa wanajenga uadui na wanaume au watu wengine ambao hushindwa kuwaelewa. Uzuri wao mwingine ni kujiamini, kusimama kama wao. Kama nilivyosema, mara nyingi hujihesabu kama wao na sio kama watu wengine. Mara nyingi sana ni watu wasiojali sana wengine wanasema kitu gani juu yao.

Chanzo:- Utambuzi na kujitambua.

Monday, February 11, 2013

JUMATATU HII TUANZA HIVI:-DHULUMA KWA WATOTO YATIMA...


Je huu kweli ni uungwana... tutafakari pamoja..kila la kheri!!

Sunday, February 10, 2013

JUMAPILI NJEMA NDUGU ZANGU:- LEO NA UJUMBE HUU!!!!

Elimu ni ufunguo wa maisha. Tuwaelimishe watoto wetu tangu wangali wadogo ili tuwajengee maisha bora. Wapate kupendwa na kila mmoja wetu na pia Mungu.
UNAJUA UKIAMBIWA KRISTU NAWE UTAJIBU NINI?.............YEYOTE ATAKAYEPITA HAPA LEO AWE NA JUMAPILI NJEMA SANA.

Friday, February 8, 2013

MWANADADA NA MIKANDA YAKE..MWANAMTINDO WA WIKI!!

 Hapa alianza na mkanda wa kipepeo mwaka 1992 hakika zilipendwa haswaaaaaa.................
 .....................akaona ngoja ajaribu na mkanda wa kitaifa  si mbaya au??? 2011
,,,,na leo 2013 yupo na mkanda mwingine, inaonekana anapenda sana mikanda huyo dada...ni kweli:-)
nawatakieni IJUMAA NJEMA NA MWISHO WA WIKI UWE MWENYE FURAHA NA UPENDO KWENU PAMOJA NA MAJIRANI ZENU. TUPO PAMOJA.

Thursday, February 7, 2013

ULIJUA KWAMBA SABABU YA KUWAITA JINA "WAZUNGU" LILITOKANA NA-----

Kuna mzungu aliniuliza maana ya neno mzungu. Nikamwambia haihusiani kabisa na rangi bali inatokana na wale weupe wa kwanza waliofika Afrika na hawakujua wanakwenda wapi, hivyo walikuwa wanazunguka ovyo! Kuna stori nilisimuliwa nikiwa mdogo, kuna kundi la wazungu walifika kijijini. Walikaribishwa vizuri na Chifu wakaondoka. Baada ya wiki mbili wazungu hao hao wakarudi pale kijijini. Chikfu kauliza, "Jamani, hao si ndo tuliwaaga majuzi!" Mzungu kashangaa hakufika popote bali anatembea katika mduara!
Imenukuliwa kutoka kwa Da’Chemi kwenye
blogu yake - “SwahiliTime”.

Tuesday, February 5, 2013

KWA WALE WANYWAJI WA KAHAWA SASA KUNA YA KIKOMBE KIMOJA KIMOJA...MAANA KILA MARA NAONGELEA KUHUSU CHAI KWA VILE MIMI NI MPENZI WA CHAI...

 

 
KAHAWA KUTOKA TANZANIA TANICA CAFE NA AFRICAFE KWA KIKOMBE KIMOJA
Hata hivyo sikuweza kuacha bila kusema kuhusu chai....kwa kikombe kimoja kimoja pia. Haya karibuni mchagua ni ipi ikufaayo..mimi nachagua chai:-)

Monday, February 4, 2013

MKE MWEMA NI UTULIVU NA NEEMA.......

KATIKA PITAPITA MTANDAONA NIMEKUTANA NA SHAIRI HILI NIMELIPENDA NI TAMU NA NIKAONA NISIWE MCHOYO NIWEKE HAPA...KARIBUNI
--------------------------------------------------------------------------------------------------
1.Mke mwema utulivu, hili halina Ubishi
Anakutoa machovu, ya kazini kama moshi
Hana chembe ya uvivu, kila kitu hash hashi
Mke mwema utulivu, ndio raha ya dunia.

2. Ni raha juu raha, nyumbani ukibakia
Wala hamna karaha, bashasha hunawiria
Huna haja ya kuhaha, baridi roho hukaa
Mke mwema utulivu, ndio raha ya dunia

3. Kidogo kwake chatosha, hakuna kudangadanga
Na hakuna mshawasha, hata upande wa kanga
Mahaba hunawirisha, japo kibaba cha unga
Mke mwema ni neema, ndio raha ya dunia

4. Na munapoambizana, hukaa na kusikia
Hafanyi hata kuguna, ishara ya kuchukia
Nyuso zina ng'ara sana, na watu huulizana
Mke mwema ni neema, ni fahari ya dunia

5. Na mume awa hakongi, majirani hushangaa
Kwa nini jamaa dingi, a shine na kung'aa
Siri chini ya mtungi, hataki hata umbea
Mke mwema ni neema, ndio pepo ya dunia

6. Na hapendi vijishoga, mara huku mara kule
Na hana muda wa soga, kila siku yuko mbele
Hapendi kuigaiga, kila kitu kwa sumile
Mke mwema rah a sana, kila mtu alijua

7. Na hata kwenye kibanda, mutaishi kwa murua
Na japo kupanda punda, msimamo hushikia
Hakuna kupinda pinda, na nyuma kufikiria
Mke mwema ni neema, mola akikujalia

8. Utulivu huwa moyo, si mali wala magari
Wangapi waliyonayo, kukicha haweshi shari
Asubuhi wenda myayo, usiku kucha ngangari
Mke mwema ni neema, Muume akiwa nayo

9. Tabia haifundishwi, mtu hujengeka nayo
Na mtu hababishwi, hiyo huwa mwenendoyo
Ni vibaya havipishwi, nafsi huwa na choyo
Mke mwema ni neema, kiumbe ukiwa nayo

10. Kukicha yananawiri, miaka nenda ishapita
Wala husikii kwiri, hutembea na kunyata
Shamsham bila shari, wajukuu washapata
Maisha huwa matamu, mke mwema kuwa nae.

11. Na ukipata mkorofi, atakutoa kipara
Kukicha hwishi makofi, na hakuna masikhara
Hugombana na mawifi, ajae humcharara
Mke mwema ni neema, na ni raha ya dunia.

SARESARE MAUA ASIYEJUA KUCHAGUA KABILA YAKE...au???

 Unaweza kushona shati pia kama kaka Kitururu alivyofanya si unaona kapendeza mwenyewe......
 .....na halafu kama kawaida unaweza kushona gauna kama uonavyo hapa  safi kabisa
aise na hapa pia unaona gauni..kitenge kimoja ila tofauti hasa rangi zake kinapendeza kwa kweli ....Jumatatu njema jamani.

Sunday, February 3, 2013

NAWATAKIENI WOTE JUMAPILI NJEMA NA IWE YA UTULIVU...

Kucheka hakuna majira, chenye majira ni kulimo. Msemo huu hutufundisha kuwa, mtu anaweza kucheka wakati wowote anapoona kuwa pana haja ya kucheka. Lakini, kilimo kina majira yake.Tusiwe wavivu, tufanye kazi. Mungu atatusaidia. JUMAPILI NJEMA SANA NDUGU ZANGU WAPENDWA.

Friday, February 1, 2013

IJUMAA YA LEO NAPENDA KUTOA SHUKRANI KWA WAFANYAKAZI WENZANGU KWA YOTE MEMA NA HASA SIKU HII JINSI WALIVYOIFANYA KUWA SIKU YA FURAHA KWANGU!!!

Leo napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa wafanya kazi wenzangu kwa kuikumbuka siku yangu ya kuzaliwa kwa keki ila haipo kwenye piacha na pia haya maua...ingawa ilikuwa tarehe 5/1.tarehe hii nilikuwa nyumbani TZ.Kwa hiyo ilikuwa ilikuwa mshtuko kwangu kidogo maaana siku zilikuwa zimepita. Ni furaha ilioje kuona kuwa kuna watu wanakuthamini, wanakujali na wanakupenda kihivyo. Ahsanteni sana na mwenyezi Mungu awajalia upendo zaidi..
Na hapa ndio wao wafafanyakazi wenzangu isipokuwa katika picha anakosekama mmoja...hawa ni kama familia yangu ya pili..ahsanteni sana.....