Showing posts with label ulemavu. Show all posts
Showing posts with label ulemavu. Show all posts

Wednesday, March 5, 2014

RABIA: MALARIA IMENIFANYA NIWE MWALIMU MLEMAVU WA KUSIKIA...

Katika pitapita zangu nikakutana na habari hii ambayo imenigusa sana na nimeona niwashirikishe kama mlikuwa hamjaisoma basi chukua dakika chache na tujadili kwa pamoja...KARIBUNI...
Mwalimu Rabia Abdallah
“Mwaka 1996 hadi 1998, nikiwa nasoma chuo cha ualimu Korogwe mkoani Tanga, nilidharaulika sana na kuonekana kama kituko kwa baadhi ya walimu na wanafunzi, huku wengine wakishangazwa nami kwa jinsi nilivyoweza kumudu masomo yangu wakati sina uwezo wa kusikia,’’ ndivyo anavyoanza Rabia Abdallah (34) ambaye alikuwa mwalimu wa shule ya viziwi Buguruni akielezea jinsi matatizo ya kusikia yalivyomfanya aonekane kituko wakati alipokuwa akisoma.
Anasema jinsi alivyokuwa akisoma ni Mungu tu ndiye aliyekuwa akimsaidia kwani hakuwa akisikia chochote zaidi ya kusoma vitabu baada ya walimu kumaliza kufundisha na njia hiyo ya kusoma vitabu ndiyo iliyomwezesha kushinda mitihani yake na kufanikiwa kutunukiwa Diploma yake ya Ualimu.
“Wengi hawakuamini na walifikiri naigiza lakini wengine waliamini lakini hawakuweza kunisaidia kwa kuwa hakuna aliyekuwa akiweza kuzungumza kwa ishara kwani hata mimi mwenyewe sikuweza kuwasiliana kwa ishara kwa wakati huo, hivyo maisha ya masomo pale Korogwe yalikuwa magumu mno kwa upande wangu…,’’
anasema Mwalimu huyo ambaye hivi karibuni amepokea barua ya uhamisho ikimtaka kuhamia katika darasa maalumu la wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia (viziwi) katika shule ya msingi Temeke. Rabia kwa sasa ana watoto wawili, anasema alifikiri kuwa kupata Diploma kungekuwa mwisho wa matatizo yake kumbe ndiyo kwanza matatizo yalizidi kuongezeka, kwani baada ya hapo alikumbana na tatizo la kupata kazi kwani kila alikoomba kazi ya kufundisha alikataliwa kwa kutokana na matatizo yake ya kusikia.
“Tatizo liliibuka upya nikaanza kudharaulika tena kila nilipokuwa nikiomba kazi kwani waliniita kiziwi nisiye na uwezo wa kufanya lolote na walishangaa ilikuwaje nimepewa Diploma wakati ninamatatizo hayo, waliamini kuwa mwenye matatizo ya kusikia hawezi kusoma tena maishani mwake,’’ anasema Rabia.
“Hapo nikalazimika kuomba kazi za kawaida ambapo nilipata kazi ya muda katika taasisi ya CCBRT ambapo nilifanya hapo kwa muda wa miaka mitano kuanzia mwaka 2000 hadi 2005, nikaona tangazo la kazi kwenye gazeti, likieleza kuwa manispaa ya Ilala inataka mwalimu wa kufundisha walemavu wa kusikia katika shule ya Buguruni Viziwi, nikaomba na nilipokubaliwa nikaacha kazi CCBRT,’’ anasema Rabia.
Anasema hata hivyo haikuwa rahisi kama alivyodhani hapo alitakiwa kusoma kwanza katika chuo cha walimu wanaofundisha elimu ya watu wenye ulemavu wa kusikia katika chuo cha Patandi kwa ngazi ya Diploma ndipo apate kazi ya kudumu alikubali na kwenda kusoma.
“Nilikwenda huko lakini nilipoomba wanipatie fedha za kunisomesha walisema nitumie zangu kisha baada ya kumaliza manispaa ingelipa lakini tangu 2005 hadi leo sijalipwa chochote na ndiyo kwanza nimepokea barua ya uhamisho wa kutakiwa kwenda Temeke lakini nao hauna fedha za uhamisho, hata sijui kwa nini,’’ anasema Rabia.
Hata hivyo licha ya kusoma katika chuo hicho maalumu kwa walimu wa kufundisha watu wenye ulemavu wa kusikia, Rabia anasema alipomaliza masomo yake hakuwa akijua kutumia ishara jambo lililomlazimu kujiunga na chama cha walemavu wa kusikia ambapo alijifunza na kufahamu vizuri lugha ya ishara.
Akizungumzia jinsi alivyopata ulemavu wa kusikia, Rabia anasema alizaliwa akiwa anasikia kama kawaida lakini alipofika darasa la nne akapatwa na malaria kali ambayo ilimlazimu kutumia dawa kwa muda wa mwezi mzima na baada ya kupona taratibu uwezo wa kusikia ukawa ukipotea na hatimaye hakuweza kusikia tena hadi leo.
Rabia ambaye ni mkazi wa Ilala Sharifu Shamba anasema kipindi hicho alikuwa na miaka nane.
“Taratibu nilijikuta nikipoteza uwezo wa kusikia lakini kipindi hicho nilipata shida sana kwani wazazi na ndugu zangu walidhani nimeanza jeuri hivyo walikuwa wakinipiga makwenzi na kunidhihaki sana bila kujua kuwa nilikuwa sisikii,’’ anasema Rabia kwa kusikitika.
“Unajua hawakuwa wakijua kama nimepoteza uwezo wa kusikia, kwa kuwa mara kwa mara mama alikuwa akiniita lakini sikuwa nikiitika kwa kuwa nilikuwa sisikii hivyo alikuwa akikasirika sana na kunipiga mara kwa mara na ndugu zangu nao pia walikuwa wakinipiga makonzi, iliniuma sana lakini sikuwa na jinsi ya kuwaeleza wasifanye hivyo,’’ anaendelea kueleza Rabia.
Anasema hali hiyo iliendelea kwa muda mrefu lakini baadaye baadhi ya majirani waliingiwa na wasiwasi na hali hiyo na kumweleza mama yake na ndugu zake kuacha kumpiga makonzi kwani huenda mtoto huyo akawa na matatizo ya kusikia hivyo walimtaka mama yake kwenda kumchunguza masikio hospitalini na alipofanya hivyo iligundulika kweli hakuwa na uwezo wa kusikia.
“Matokeo hayo yalimuhuzunisha sana mama, nilimuona akijisikia vibaya kwa kuwa alikuwa akinipiga makwenzi kwa kudhani kuwa nilikuwa jeuri, lakini hakukuwa na la kufanya, kipindi hicho hakukuwa na shule za wenye ulemavu huo hivyo nikalazimika kusoma kwa kuchanganyika na wanafunzi wasio na matatizo kama yangu,’’ anaeleza Rabia.
Kwa masikitiko Rabia anasema kuwa yeye alikuwa katika hali ngumu kwani ilipofika kipindi cha mitihani hasa somo la Imla hakuwa akiambua kitu na wala hakuwa akipata msaada wowote kwa kuwa walimu wenyewe waliokuwa wakisimamia mitihani hawakuwa wakijua kuzungumza kwa ishara.
‘‘Hivyo katika mitihani yangu yote kuanzia darasa la nne nilikuwa nikikosa maswali yote ya Imla na yale ambayo yalikuwa yamekosewa na kubadilishwa kwa kusomwa kwa kuwa sikuwa nikisikia kitu zaidi ya kuhisi baadhi ya mambo, lakini nashukuru Mungu licha ya kushindwa Imla katika kila mtihani wangu, Mungu alinisaidia nikafaulu mtihani wa darasa la saba na kuchaguliwa kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Kisutu,’’ anasema Rabia.
Anasema sekondari nako kulikuwa kugumu zaidi kwani alikuwa hasikii na lugha iliyokuwa ikitumika ni Kiingereza ikawa ngumu kutambua kwa kuangalia mdomo wa mwalimu kwa kuwa maneno hayo hakuwa akiyafahamu, ikawa ngumu kwake kung’amua lolote hata alipojaribu kumuangalia mwalimu wa somo anavyotamka maneno.
Rabia alimaliza sekondari na kupata daraja la nne la pointi 26 hivyo akachaguliwa kujiunga na Ualimu katika chuo cha ualimu Korogwe Tanga.
“Nina ombi kwa serikali, naomba wabadilishe mfumo wa mitihani ya shule za msingi kwa wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia, maswali yasifanane na wasio na matatizo hayo ili kila mtu awe na uwezo wa kujibu na pia wasimamizi wa mitihani hiyo wawe walimu wenye uelewa na watu wa namna hiyo,’’ anasema Rabia.
Makala haya yameandikwa na Festo Polea wa Gazeti la Mwananchi

Tuesday, May 26, 2009

WATOTO WENYE ULEMAVU NA MARADHI YA KUDUMU.

Ulemavu wa viungo nao sababu zake zinafanana kabisa na zile za mtindio wa ubongo. Kama nilivyoeleza katika makala yangu moja wiki mbili zilizopita .

Kwa mfano, zipo baadhi ya dawa hasa za kutuliza maumivu ambazo zinapotumiwa na akina mama wajawazito, husababisha kuzaliwa kwa watoto wenye upungufu wa viungo au vilema (Deformed Children).

Ipo sababu nyingine ya kibaiolojia inayotokea wakati wa kutunga mimba. Hata hivyo unapotaka kuzungumzia jambo hili inahitaji ushahidi unaojitosheleza.
Ajali pia ni mojawapo ya sababu zinazopelekea ulemavu wa viungo. Kwa mfano, ajali ya gari, kuanguka na kuumia michezoni, zote hizi husababisha ulemavu wa viungo wa kudumu.

Ulemavu huu unaweza kusababisha hali ya kupooza (Paralysis), kukosa uwezo wa kutembea au hata kupoteza nguvu za kiume. Inawezekana umeshawahi kusikia au kuona mtu aliyeumia mpirani au kuanguka juu ya mti na kupata ulemavu wa kudumu.

Leo ningependa kuzungumzia zaidi tatizo la kupooza ambalo huwapata watu wengi.

Kwanza kuna kupooza kunakoanzia katika sehemu ya kiuno kwenda chini miguuni kwa lugha ya kitalamu kunaitwa paralplegic.

Pili kuna kupooza kunakoanzia shingoni kuja mabegani na kwenda chini miguuni kunakofahamika kitaalamu kama Quadriplegic. Watu wenye matatizo haya huhitaji kiti chenye magudumu ili waweze kutembea. Hata hivyo watoto wenye ulemavu unaoambatana na hali ya kupooza huweza kusaidiwa kwa kutumia njia zifuatazo.

Wazazi wenye watoto wanokabiliwa na tatizo hili wantakiwa wazitengeneze nyumba zao kwa kuzingatia hali halisi ya maradhi ya watoto wao. Kwa mfano wanapaswa kutengeneza njia ambayo itatumika katika kupitisha kiti cha magurudumu badala ya ngazi, vitu ama vifaa vya kuchezea vya watoto wa aina hii sharti vihifadhiwe kwenye kabati ambalo litawekwa kwenye sehemu ya wazi ambayo mtoto anaweza kuifikia na kuchukuwa vitu anvyohitaji bila kuomba msaada.

Pia ianshauriwa kuwaeleza watoto wenzake pale nyumbani au hata wale watoto wa majirani kuhusu ulemavu wa mwenzao, kwamba ni kitu ambacho kinaweza kumtokea mtu yeyote ikiwa ni pamoja na wao, ingawa wamezaliwa wakiwa na viungo kamili.

Hii itawajenga kisaikolojia watoto hao wasimtenge au kumdharau mwenzao ambaye ni mlemavu.

Watoto wa aina hii haitakiwi kuwaonesha kwamba hawawezi kufanya kitu chochote. Hivyo inashauriwa kuwajengea tabia ya kujitegemea kwa kuwaruhusu wafanye yale wanaoweza kuyafanya, kwani kwa kufanya hivyo kutawajengea hali ya kujiamini.

Je watoto wenye maradhi ya kudumu wanasaidiwaje?
Watoto wenye maradhi ya kudumu kama vile pumu, kisukari au kifafa ni miongoni mwa watoto wenye kuhitaji msaada maalum, inashauriwa kuwafahamisha watoto hao juu ya maradhi yanayowa sumbua ili wayafahamu na kuyazoea, pia hata wanafunzi wenzao au watoto wa majirani ni vema pia wakafahamishwa kuhusu maradhi yanayowasumbua wenzao kwani itasaidia kupunguza utani na dhihaka dhidi yao. Kwa upande wa waalimu inashauriwa kuwa watoto wa aina hii upendeleo na uangalizi wa karibu pale inapobidi kulingana na tatizo la mtoto husika.

Ukweli ni kwamba kuzaa mototo mwenye matatizo niliyoyaeleza siyo dhambi na wala hatupaswi kuwatenga watoto au watu wa aina hii, kwani wakipatiwa elimu bora na ya kutosha wanaweza kabisa kujitegemea kwa kufanya kazi za aina mbalimbali na kulipa kodi na kuchangia pato la Taifa. Kama nilivyosema katika mada iliyopita kwamba sio lazima wawe na kazi ya maana ila cha msingi ni kuwa na kitu cha kufanya.