Monday, August 31, 2009

KUMBE MAISHA NDIO YAPO TOFAUTI HIVI?????

Ngoja leo niwasimulieni kitu ambacho nilipokuwa mdogo nilikuwa nakiwaza. Mimi nilikuwa nawaza hivi kupoje? Nilikuwa na ile picha kuwa maisha yao ni mazuri sana. Yaani wana kila kitu kama vile maisha mazuri, nguo nzuri, nyumba nzuri tena pengine niliwaza hata hawafanyi kazi yaani kazi za mashamba nk.

Nimeshuhudia mwenyewe sasa, watu wanalala njaakila siku, watu wanalala nje na kujifunika mabox (mangumi)na bila kusahau waombaomba .Pia kuna majambazi ambao wanakaa jela miaka na miaka, na kuna wabakaji wengi tu na tena waharifu wa kila aina.

Pia nilikwa nadhani kuna nyumba na tena zote za ghorofa tu. Eti nilifikiri hakuna misitu na wala wanyama wakali. Eee! Bwana, kuna misitu tena leo nilikuwa mstuni kuchuma uyoga na nikakutana na nyoka wacha nikimbie.

Nikakumbuka kuna siku moja nilikuwa nawasimulia ndugu zangu wa Ruhuwiko hali ya huku yaani maisha ya huku si ya kawaida. Nguo unahitaji kuwa na nguo za misimu mitatu:- ni (vinter ), baridi unahitaji nguo nzito sana na maviatu makubwa, makofia, nk…. (Vår) , joto kiasi, (sommar), ”joto” na (höst), ni hali ya hewa ambayo ni mchanganyika wa vyote. Lakini hawakunielewa kabisa. Kwa hiyo kwa mtindo huu hapa kama mpo wengi katika familia kazi kwelikweli. Maana hapo bili, chakula, nk bado hujalipia mmmh sisemi sana kila kitu kinabidi uvumilivu.

Lakini watu wabishi, kuna minongóno watu wanafikiri mimi ni mjanja nawadanganya ile wasije huku ili nifaidi peke yangu. Ya kwamba eti kama kungekuwa kama nisemavuo basi nisingeweza kuishi.

Saturday, August 29, 2009

UGONJWA WA MIGOMBA WAVAMIA AFRIKA

Ugonjwa wa ndizi waikumba Afrika

Wataalam wa masuala ya chakula wameieleza BBC kwamba upatikanaji wa chakula utakuwa hatarini barani Afrika baada ya kuzuka magonjwa yanayoshambulia migomba na kuathiri ndizi.
Mazao hayo yameathirika kuanzia Angola hadi Uganda, ikiwemo maeneo mengi ambapo ndizi ndio chakula kikuu.

Wataalam wamewashauri wakulima kutumia dawa za kuangamiza wadudu au kubadilisha aina ya migomba na kupanda ile inayoweza kukabiliana na magonjwa.
Wanasayansi wamekuwa wakikutana nchini Tanzania kuamua namna ya kupambana na m

Nchi zinazolima ndizi kwa wingi ni Ethiopia, Uganda, Rwanda, Kenya, Tanzania, Gabon, DR Congo, Jamhuri ya Congo , Kaskazini mwa Angola na kati mwa Malawi

Imeandikwa na mwandishi wa BBC.

Friday, August 28, 2009

SIRI INAPOFICHUKA!

Nilipokuwa nyumbani Tanzania hivi karibuni nilikutana na shoga yangu mmoja ambaye katika mazungumzo yetu alinisimulia kisa hiki cha shoga yake mmoja aliyekwenda kwake akimtaka ushauri.

Kisa cha kutaka ushauri ni kutokana na kukuta mumewe amehamia nyumba ambayo inamilikiwa na mpenzi wake wa zamani. Huyo mwanamke alikwenda masomoni nje ya nchi na kumuacha mumewe nchini na huku nyuma mkataba wa nyumba waliyokuwa wakiishi ulipoisha mwenye nyumba akawaamuru wahame ili aifanyie nyumba yake ukarabati, basi yule bwana akamfahamisha mkewe kule ughaibuni alipo kuwa wametakiwa wahame na baada ya kushauriana wakakubaliana watafute nyumba nyingine lakini isiwe ni maeneo yale ya kinondoni walipokuwa wakiishi, wakakubaliana waatafute nyumba maeneo ya Kijitonyama au Mwenge.
Baada ya kuhangaika sana yule bwana alipata nyumba maeneo ya Kijitonyama na kumjulisha mkewe na baada ya kumweleza jinsi nyumba ilivyo mkewe alikubali wahamie kwenye nyumba hiyo.

Ilikuwa ni nyumba kubwa inayojitegemea na mwenye nyumba alikuwa anakaa uani na wao wakikaa nyumba kubwa.

Wakati huo ilibaki miezi sita yule bibie arudi na kuungana na mumewe. Siku, wiki, miezi ilikatika na hatimaye yule bibie akamaliza masomo yake na kurejea nchini. Alipofika nyumbani, kwa jicho la kwanza aliipenda ile nyumba na kuisifia sana, na mumewe alifurahi kusifiwa na mkewe kwa kuchagua nyumba nzuri mpaka mkewe akaridhika nayo.

Kwa bahati mbaya mwenye nyumba hakuwepo alikuwa amesafiri nje ya nchi kwani alikuwa ni mfanyabiashara na mkewe alifariki miaka mitatu iliyopita na watoto wake walikuwa wanasoma nje ya nchi kwa hiyo pale nyumbani alibaki peke yake na mtumishi wake wa ndani.

Baada ya kukaa nyumbani kiasi cha wiki moja aliripoti kazini na kuanza kazi. Siku moja jioni aliporudi nyumbani mumewe alimuomba ampeleke akamtambulishe kwa mwenye nyumba kwa kuwa amerudi, walizunguka hadi uani anapokaa mwenye nyumba na kukaribishwa na mtumishi wake wa ndani {House Boy} akawaomba wamsubiri mwenye nyumba ambaye alikuwa ndani akawaitie.

Mwenye nyumba alipotoka yule bibie alikuwa kama amepigwa na shoti ya umeme na asiamini macho yake, kwani aliyesimama mbele yake hakuwa ni mwingine bali ni mpenzi wake waliyepoteana miaka kumi iliyopita baada ya yule mpenzi wake kwenda nje ya nchi kimasomo na waliachana kwa ahadi ya kuoana akirudi. Hata yule mwenye nyumba alishikwa na butwaa kwa nukta kadhaa, lakini akawa mwepesi kujiweka sawa na kuwakaribisha kwa bashasha huku akimuagiza yule mtumishi wake awaletee wageni vinywaji.

Baada ya kusalimiana na kisha kumtambulisha mkewe kwa mwenye nyumba waliaga na kuondoka kurudi ndani kwao, kuanzia siku ile yule bibie hakuwa na raha na alikuwa akijitahidi kukwepa asionane na yule mwenye nyumba.

Sasa amebaki njia panda. Je amshawishi mumewe kwamba wahame ile nyumba au amwambie ukweli juu ya uhusiano wake na mwenye nyumba miaka kumi iliyopita?
Sijui wewe msomaji unayesoma hapa ungemshauri nini huyu bibie, lakini ninachotaka kusema hapa ni juu ya siri tunazoambiana na waume zetu.

Labda nikuulize wewe msomaji. Je, umewahi kumficha mumeo au mkeo kitu chochote juu ya maisha yako ya zamani au ya sasa? Je mumeo au mkeo aliwahi kukushangaza na siri yoyote ya mambo yake ya zamani?

Naomba niwe mkweli kwa hili kwamba katika mahusiano,zipo siri ambazo unaweza kuzitoa na nyingine hutakiwi kuzitoa. Hata hivyo usijidanganye kuwa unaweza kuficha kila siri, lakini ni vyema ukajua kwamba ukitoa kila siri ndio ndoa yenu itaimarika kwa kuonekana kuwa umkweli, mwadilifu, au mcha mungu, si kweli kwani kuna wakati kusema kila siri kunaweza kuibua migogoro isiyo ya lazima katika ndoa hasa kama upande mmoja unaweza kutumia siri uliyoieleza kama bakora kukuadhibu pindi mkitofautiana katika mambo fulani fulani, ukweli ni kwamba hii itategemea zaidi kuwa mumeo au mkeo ni mtu wa aina gani. Kwani kuficha siri ni kujilinda dhidi ya dhihaka na kukwazana, kusiko na maana.

Kuna siri nyingine ambazo huna budi kuzitoa, kama unahisi kuwa zikibainika zitavunja uhusiano wenu, au zitasababisha uhusiano wenu kuyumba. Mambo kama magonjwa ya kurithi, wapenzi wa zamani au tabia mbaya ulizokuwa nazo kabla ya kuoa au kuolewa, inabidi uziweke wazi kwa mkeo au mumeo ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima pindi akijua, ni vyema ukafahamu kuwa jambo lolote kama likijulikana na zaidi ya mtu mmoja sio siri tena, kwani linaweza kumfikia mwenzio.

Kuna wakati mwanandoa anaweza kuona kama amechelewa kutoa siri yake kwa mwenzie, na hivyo kuamua kukaa kimya, lakini baadae siri hiyo ikifichuka inamuweka mahali pabaya na hivyo kuchanganyikiwa.

Inasemekana kuwa wanaume ndio huwaficha wenzi wao mambo mengi ukilinganisha na wanawake. Kwa nini?
Kwa sababu wanaume wanadhani kuwa, kwa kuficha ukweli, watazuia migogoro ambayo ingeweza kutokea kama mambo hayo yangewekwa wazi. Kwa kawaida wanaume wengi huogopa hasira za wake zao, kwani hawapendi mivutano ndani ya nyumba.

Kuweka wazi juu ya wapenzi wako wa zamani kwa mwenzio ni jambo jema kabisa, hata kama wako 20 we sema tu, ili mwenzio aamue kama yuko tayari kuoana na wewe au la. Kwani hiyo itakuweka huru, hata mwenzio akikutana na washakunaku na kuelezwa, ni rahisi kuwaambia kuwa anafahamu na hivyo kuwaumbua washakunaku hao.

Ukiwa mkweli haitakuwa rahisi kwako kuficha jambo, na hiyo itakusaidia kumfanya mwenzio akuamini zaidi na kuongeze upendo kwako.

Thursday, August 27, 2009

JE, UPWEKE NI UGONJWA?

Kabla na baada ya kuja huku niliko nilikuwa na marafiki wengi kifani. Lakini baada ya kuishi mwaka mmoja hap nililetewa barua toka kwa marafiki zangu na kuniomba niwatafutie wachumba au kazi. Na nilipowajibu kuwa mimi nilikuwa mgeni, pia binafsi sikuwa na kazi wala sikujua lugha walikata mawasiliano nami.
Nikawa nashangaa kwa nini? je? hawa kweli walikuwa marafiki wa kweli yani wale ambao wanasema hufaana kwa penye furaha na taabu. Kwa hiyo nikabaki mpweke bila rafiki wa karibu isipokuwa nilikuwa na rafiki yangu wa karibu sana ambaye ni mume wangu na baadaye wanangu. Na baadaye yaani kama mwaka mmoja uliopita nilianza kublog na hapo nikapata marafiki wengi tena. Na natumaini ninyi rafiki nilowapata hamtanikimbia. Hii ndio sababu nimeuliza je? upweke ni ugonjwa? kwasababu mimi nilikosa sana raha nilipokuwa mpweke.

Tuesday, August 25, 2009

MATESO YA MTOTO FILIMINA

TTTTuwapende mayatima
Nimepata email kutoka kwa msomaji wa blog hii (ameomba nihifadhi jina lake) amenitumia taarifa ifuatayo ambayo imesikitisha sana, nami bila kusita kutokana na kuguswa na habari hiyo nimeona niiweke hapa kibarazani ili kuomba msaada kwa wadau walioko nyumbani Tanzania jijini Dar Es Salaam, wasaidie kumuokoa binti huyu. Naomba kuwasilisha.

Dada Yasinta,

Nimeshawishika kuwasiliana na wewe ili kujaribu kutafuta namna ya kumsaidia mtoto Fina ambaye ni yatima anayeishi katika mazingara ya mateso makubwa kupita kiasi.

Najua hunifahamu na wala sijawahi kuwasiliana na wewe hata siku moja lakini ningependa ufahamu kuwa mimi ni mmojawapo kati ya wasomaji wazuri wa blog yako.
Kwa kuwa nimeona kuwa blog yako inasomwa na wasomaji wengi nimeona nipitishie kilio cha binti huyu kupitia blog yako ili kutafuta namna ya kumsaidia.

Mimi naishi maeneo ya Tabata Kisukulu lakini ninaye girlfrind wangu anayeishi Tabata Kimanga jirani na mama huyo anayemtesa binti huyo yatima asiye na baba wala mama. Nimekuwa nikimtembelea Girlfrind wangu karibu kila siku na nimekuwa nikishuhudia mateso anayofanyiwa huyo binti
Nyumba anayoishi mama huyo iko Tabata Kimanga, unashuka kituo maarufu kiitwacho njia panda, mbele kidogo unafuata njia ya kushoto, utakuta gereji, ukiuliza kwa mama Enok au mama Frank maarufu kwa kuwauzia mafundi gereji maji ya baridi utampata.

Baada ya kuona mateso anayofanyiwa binti huyo, niliijaribu kuwauliza baadhi ya majirani na walikiri kuwa hilo ni jambo la kawaida, kwani binti amekuwa akipigwa kila siku takribani mara tatu kwa siku kwa makosa yasiyo na msingi kabisa.

Naamini wote tunafahamu malezi na namna ya kumuadhibu mtoto, lakini ikiwa mtoto anaadhibiwa hadi kuchomwa moto hiyo ni hatari, na tena kwa jinsi alivyo makini humchoma sehemu za mapajani ili isiwe rahisi kuonekana.
Nimefanya uchunguzi makini katika kipindi hiki cha mwishoni mwa juma na nimepata habari muhimu kadhaa ambazo mtu asipokuwa makini anaweza kudhani kuwa binti huyu haonewi. Huyu mama kwa kutaka kujenga mazingira ya kutoonekana kwamba anamtesa huyu binti, amekuwa akimsingizia mambo mengi kwa majirani na hata shuleni anaposoma ili ionekane kwamba ni mtoto jeuri, malaya na asiyesikia.

Ni mzuri kwa kutengeneza uongo na anaongea sana, ila naamini hata majirani watakuwa ni mashahidi wazuri katika kuthibitisha hili. Ni mateso makubwa sana anayopata binti huyu na hata kama ni mkosaji lakini adhabu anayopewa ni kubwa kuliko kawaida. Inaniuma sana na ninahisi si siku nyingi anaweza hata kumuua. naomba nikiri kwamba katika maisha yangu yote sijawahi kuona mateso ya namna hii, tena yanayofanywa na mwanamke ambaye na yeye anao watoto na anayejua uchungu wa kuzaa............ sasa nimejua ni nini maana ya roho mbaya tena mbaya zaidi naishuhudia kwa mwanamke.........

Nakuomba sana dada Yasinta uiweke habari hii katika blog yako ili jamii ya Watanzania na vyombo vinavyohusika vifahamu. Niliwasiliana na Chama Cha Waandishi Wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), na waliahidi kufuatilia swala hili.
Ukweli ni kwamba dada kila nimuonapo binti huyu roho inaniuma sana na nimeshindwa kuvumilia unyama huu. Naamini labda mungu anayo makusudi yake, kwamba nilione hili ili nichukue hatua, na hatua yenyewe ndio hii ya wewe kunisaidia kumuokoa mtoto huyu. Jamani dhamira inanishitaki na naona kuna kitu kinanisukuma nimsaidie binti huyu kama binadamu mwenzangu....

Nimefanya uchunguzi wa kujua shule anayosoma na jina la mwalimu mkuu na namba yake ya simu, na nimepata taarifa zifuatazo:

Jina la Binti ni Filimina (Jina la baba yake sijalipata bado)na anasoma darasa la Tatu C
Jina la shule ni Tumaini Tabata Kimanga
Jina la mwalimu mkuu ni Mwalimu Mang’enya
Namba ya simu ya mwalimu mkuu ni +255 718 900190

Naomba ushirikiano wako,

Monday, August 24, 2009

NI MALI YA MTOTO AU MUME AU MKE?

Matiti hutoa chakula cha mtoto.

JE? DALILI ZA KUZEEKA NI ZIPI?

Nimeamka na nikaanza kujiangalia kwenye kioo....lol , nikaona uweupe wacha nishtuke nikaanza kuwaza hivi ni kweli nimefikia umri wa kupata MVI? Maana kuna usemi usemao ukiwa na MVI basi ni dalili ya uzee....lol

Nimeona si vibaya kama tukisaidiana kujadili hili swala la uzee. Inasemekana pia watu wengi hawataki kuamkiwa SHIKAMOO kwa vile wanajiona ni wazee. Na wengine hawataki kuwa na makunyanzi. Na hapa ndo wanaanza kutafuta mafuta(lotion) za kuondoa makunyanzi usoni ili kuonekana vijana. Hawakumbuki kuwa siku moja ni LAZIMA watakuwa na makunyazi yaani hatuwezi kuisha maisha yote tukiwa vijana tu. Hapa duniani kuna mambo.

Kuhusu MVI je? inawezekana ni urithi? Nisaidieni sio kwamba naogopa kuwa mzee hapana ila nataka kujua tu.

Hapa nimeona si vibaya kama nikiambatanisha na mada hii hapa ambayo Mzee wa Changamoto aliiandika siku si nyingi. Nayo inaongelea kuhusu kuzeeka:-

Kipi chazeeka kwanza, miili ama akili????

Nikiwa kazini na "rafiki" yangu (ambaye ana umri mkubwa), tulikuwa tukiongelea jinsi watu wanavyoukimbia muonekano wa umri wao. Na yeye alionekana kutetea hilo na kusema kuwa awali alikuwa akionekana ana mvi nyingi kichwani na alijihisi MZEE. Lakini baadae akapata dawa ya kubadili rangi ya nywele zake na hilo likamrejesha katika "ujana" aliokuwa akiutaka. Na baada ya kuonekana kuwa kijana zaidi, akaanza kujihisi kuwa na hata nguvu na uwezo wa kufanya mazoezi. Sasa hivi anakimbia dk 30 za mapumziko ya mchana kazini na amebadili mfumo wake wa chakula, amebadili mfumo wa maisha na kwa hakika sasa anaishi "maisha ya afya" zaidi kuliko ilivyokuwa awali. Hakuna anayebisha kuwa KUJIONA KIJANA kumemsaidia kubadili mfumo mzima wa maisha. Lakini kwangu swali likabaki kuwa alizeeka mwili ama akili? Ni kweli kuwa kabla hajajiona kuwa kijana zaidi mwili wake usingeweza kutenda mazoezi afanyayo sasa? Na je! kama angekuwa amezeeka mwili, angeweza kutenda atendayo hata kama angekuwa anapenda kufanya hayo?
Ninawaona wengi ambao kwa kujiona "wamezeeka" hawajiendelezi na shule, hawawekezi maishani na hata hawafanyi mengi mema ambayo yangewasaidia miaka michache ijayo. Wanaokimbia vivuli vyao kwa kujifanyia upasuaji kutafuta muonekano wa ujana, kutumia makemikali "kijijananisha" na hata kuvaa ki-ujanaujana wakiamini hilo litawapa HISIA nzuri za namna walivyo. Pengine inawasaidia kwani wapo ambao wakishakuwa katika "ujana" wautakao huanza kutenda yale ambayo ni ya manufaa kwa maisha yao na zaidi kwa wale wategemezi wao lakini ambayo wangekuwa wamefanya ama walistahili kuyafanya kabla "hawajajibadilisha."
Haya na mengine mengi hunifanya nijiulize tena na tena.
KIPI CHAZEEKA KWANZA? MIILI AMA AKILI?

Sunday, August 23, 2009

JUMAPILI NJEMA KWA WOTE

Kupenda kazi hurahisisha kazi

Si kwamba tuishi tu mahali, bali tuishi mahali pazuri. Kwa juhudi zetu tunaweza kupendezesha mahali pa kuishi, miji na vijiji vyetu.

Saturday, August 22, 2009

KUANZA KWA MWEZI MTUKUFU WA MFUNGO WA RAMADHANI

Napenda kuwatakia ramadhani njema waislamu wote duniani!!!

Thursday, August 20, 2009

KWA NINI IWE NI WANAUME TU WANAONUNUA MKUYATI?

Kuna wakati wanaume wanaweza kuwa na ugumu wa kujua kwamba wake au wapenzi wao hawaridhiki kimapenzi. Hiyo inatokana na uwelewa mdogo waliokuwa nao wanaume juu ya tofauti kubwa iliyopo kati ya wanawake na wanaume kuhusiana swala zima la hisia za kimapenzi.

Wanawake wana matarajio makubwa sana katika kila eneo linalohusu maisha yao, lakini linapokuja swala la tendo la ndoa mambo ni tofauti sana. Kwa kawaida wanawake wengi ambao hawaridhishwi na tendo la ndoa kwenye uhusiano wao huwa wanafanya siri.

Bila kujali kama tatizo liko kwao au kwa waume zao, wanawake hufanya siri kutoridhika kwao kimapenzi, na huweka siri kwa waume zao na hata kwa madaktari. Na ndio maana sishangai kuona kwamba wateja wa wauza dawa zinazohusiana na kuongeza hamu ya tendo la ndoa yaani Mkuyati ni wanaume.

Nilipokuwa nyumbani Tanzania, jijini Dar Es Salaamu nilishangaa sana kuona katika magazeti maarufu ya Udaku, {Tabloids} matangazo mengi ya biashara yanayotawala katika magazeti hayo ni ya kuuza dawa za kuongeza nguvu za kiume au hamu ya tendo la ndoa kwa wanaume na nyingine zilikuwa ni za kuongeza ukubwa wa maumbile ya kiume, dawa kama Mkuyati, Mzakaru, Super Shaft, Kifaru, Sekwa na nyingine chungu nzima ni maarufu sana jijini Dar Es Salaam.

Sio kwamba wanawake hawana matatizo ya tendo la ndoa, la hasha. Wanawake wanayo matatizo hayo ya tendo la ndoa lakini kwao hiyo siyo agenda, yaani si kitu cha kuwaumiza sana kichwa. Lakini kwa wanaume ni tofauti sana, wanapokuwa na tatizo la kukosa ufanisi katika tendo la ndoa huo utakuwa ni mgogoro mkubwa sana, kwani kwao hili ni jambo linalopewa kipaumbele kuliko mambo yote.

Kwa wanaume kukimbilia hospitalini au kwa mganga wa jadi na kusema “nina tatizo kubwa” ni jambo la kawaida kabisa…. Lakini wanawake hawafanyi hivyo, Badala ya kulifanya tatizo hili ni mgogoro halisi, huwekwa chini kabisa kwenye orodha ya matatizo yao, huwekwa kiporo na litashughulikiwa kwa wakati atakapojisikia kufanya hivyo kwa wakati wake.

Wanawake wanaweza kwenda kuomba ushauri au kuwasimulia mashoga zao, kuhusu matatizo ya ndoa. Lakini ni hadi wachokozwe ndipo wanapoweza kusema kwamba maisha yao ya tendo la ndoa na waume zao hayako sawasawa. Hilo halipewi uzito wa juu au naweza pia kusema hufanywa siri.

Wanawake hawaridhishwi na tendo la ndoa kwa sababu mbali mbali. Lakini bila kujali sababu hizo, kwao ni vigumu sana kusema kuhusu kutoridhishwa kwao. Ukiona mwanamke anatangaza sana kuhusu kutoridhishwa kwake na tendo la ndoa, basi ujue huyo na mumewe wako kwenye uhusiano mbaya sana. Kwani atakuwa anatumia maelezo ya kutoridhika kwake kama adhabu ya kumkomoa mumewe kwa kumuaibisha.

Lakini wale walioko kwenye ndoa imara ni vigumu kuwasikia wakilalamika kwamba hawaridhiki na tendo la ndoa. Inawezekana kutoridhika kwake kunatokana na yeye mwenyewe, yaani labda hana hamu au hafiki kileleni kutokana na matatizo mbali mbali yakiwemo ya kisaikolojia au matumizi ya baadhi ya njia za uzazi wa mpango, lakini bado sehemu kubwa wanaume huchangia. Hata hivyo pamoja na sababu hizo, mwanamke hayuko tayari kusema kuhusu kutoridhika kwake.

Kushindwa huko kunatokana na jinsi jamii ilivyomfunga mwanamke, kutoonesha kuhitaji tendo la ndoa. Akionesha kutoridhika na tendo la ndoa huonekana ni Malaya, kwa hiyo hukaa kimya na kuonesha kutojali.

Lakini bila shaka nadhani umefika muda wa wanawake kuwa huru kuhusu tendo la ndoa na kusema hisia zao wazi wazi bila kuogopa jamii itawaonaje, kwani jamii imekandamiza haki yao ya kuzungumzia tendo la ndoa kwa muda mrefu sasa.

Wanaume nao wanapaswa kujua kwamba wanawake hawapendi au hawawezi kuzungumzia kutoridhishwa kwao na tendo la ndoa, hivyo kutosema kwao kusitafsiriwe kuwa ndio wanawaridhisha, ni vyema kutoa ushirikiano kwa wake au wapenzi wao na kutafuta kujua kama wanawaridhisha. Ni jambo la busara kama mwanaume atadadisi kwa upendo na lugha ya upendo na kuonesha kama yuko tayari kutoa ushirikiano pale ambapo mke au mpenzi ataonesha kutoridhishwa na tendo la ndoa.

MAISHA , MAISHA, MAISHA


NAWATAKIENI WOTE ALHAMIS NJEMA!!!!!

Wednesday, August 19, 2009

KUFA NA KUZIKANA

Sijui nianze vipi?:- Mila na desturi, kweli kila watu wana zao. Nimeishi hapa Sweden sasa miaka mingi kidogo. Lakini bado sielewi pale panapotokea msiba (mtu kufa)

Nina maana hapa Sweden mtu akifa basi wahusika watatangaza kwenye gazeti na pia wanaandika lini mazishi yatakuwa. Sasa hapo ndipo nisipoelewa mimi, yaani hapa sasa sio kwamba kila mtu kuhudhuria msiba huo? la hasha. Ni lazima ualikwe na unapoalikwa ni lazima utoe taarifa kuwa utafika. Sababu kubwa ya kufanya hivyo wanataka wajue kwamba waandae chakula cha watu wangapi.

Sio kama nyumbani TZ mtu ana safari zake au alikuwa shambani, mara akasikia kwa fulani kuna msiba, basi ni kuataacha kila kitu na kwenda huko na kuungana na wafiwa. Kusema kweli mila za huku hasa kuhusiana na misiba inanichanganya sana.
Kuna siku niliwakuta watu wanazika na walikuwa watu watano tu yaani hata ndugu akisikia ndugu yake amekufa haendi kwenye msiba anasubiri kualikwa. Huku mtu hawezi kwenda msibani au kuzika ni mpaka awe rafiki au ndugu na hapo pia mpaka aalikwe. Yaani hata awe jirani hakuna mtu anaenda kila mtu na lwake .

Kitu kingine tena ambacho ni ajabu kidogo kwa mimi sijui wenzangu mnalijua hili. Ni hiki kitendo cha watu wakiwemo ndugu wa karibu wa marehemu kuondoka kanisani na kurejea majumbani mwao baada ya misa na kuuacha mwili wa marehemu hapo, yaani kwao huko ndio kuzika, baada ya hapo shughuli ya mazishi hufanywa na wazikaji wa kukodi ambao hulipwa kwa kazi hiyo, tena hakuna hata kulala matanga, shughuli inakuwa inaishia kanisani. Tofauti na TZ, nadhani wote tunajua nyumbani tunafanya nini. Kwa sababu kama unaenda kuzika ni lazima kuzika kwa maana kuhudhuria mpaka makaburuini na kuhakikisha mwili unafukiwa sio kuuacha mwili kanisana, halafu? Naamini mazishi ni wajibu wa wote waliofika pale kumsindikiza mwenzao katika safari yake ya mwisho yaani katika shamba la Mungu (makaburini) na sio kukabidhi mwili kwa watu wa kulipwa na nyie kuondoka na hamsini zenu.

Pia hapa kuna mtindo wa kuchoma mwili na halafu yale majivu kwenda kuyamwaga sehemu ambayo marehemu alikuwa anaipenda kama vile ziwani au mlimani. Na wengine wanazika au wanaweka kwenye chupa na kuhifadhi kwenye nyumba maalumu (minneslund) sehemu ya makumbusho.

Monday, August 17, 2009

KUMBUKUMBU YA MAMA YETU

Mama Alana Magnus Ngonyani astarehe kwa amani.
Imepita miaka mitano leo tangu mama yetu mpendwa Alana Ngonyani aitwe na Mwenyezi Mungu kwenye makao ya milele, Agosti 17,2004. Mama Alana ameaga dunia akiwa na miaka 52.

Kutokana na pengo kubwa ulilotuachia na lisilozibika sisi watoto wako, mume wako, wajukuu wako, wakamwana na mkwe pia ndugu, marafiki na jamaa bado tupo nawe kwa njia ya sala na maombi. Kwa kuwa tunaamini kuwa Mwenyezi Mungu mwenye huruma amekupokea katika makao yake huko Mbinguni.

Kwa niaba ya familia ya marehemu tunawashukuru wote mliotusaidia na kujiunga nasi kwa hali na mali katika kuokoa uhai wa marehemu.

Aidha, tunawashukuru kwa sala katika kumsindikiza kwenye shamba la Mungu(pale Mkurumo) Mungu awarudishie mara mia wote mliojitolea kutusaidia.
Ee Mwenyezi Mungu umpokee mama yetu katika ufalme wako huko Mbinguni, Astarehe kwa Amani. Amina

Friday, August 14, 2009

UJUMBE WA LEO

Tabasamu la kawaida lina maana nyingi.
Hasa siku ambayo unajisikia vibaya,
Mimi nadhani wengi wanajisikia hivi,
Ndiyo, wote wazee na vijana.

Maneno machache yanaweza kuleta miujiza ,
Hasa katika muda mgumu,
Haya poteza na maneno ya upendo,
Unajua maisha yetu hayarudiwi,
Inabidi tufanye vizuri, kwa kila zuri.

Thursday, August 13, 2009

HONGERA KWA SIKU YA KUZALIWA KAKA, MJOMBA, SHEMEJI PHILOTEO NGONYANI

Huyu ni kaka yangu mdogo na wa mwisho katika kaka zangu watano, jina lake Philoteo. Leo ni siku ile ambayo huyu kijana aliyaanza maisha yake. Ni siku aliyozaliwa. Kwa niaba yake napenda kumshukuru Mungu kwa kumlinda mpaka siku hii ya leo na kuongeza miaka zaidi.

Wednesday, August 12, 2009

SIKUPENDI KIVIPI?

“Unajua siku hizi hunipendi” mwanamke ambaye ameishi na mume wake kwa miaka 6 alimlalamikia mume wake.

"Hivi unaongea kitu gani na wewe, kwa nini unasema hivyo hivyo?"
Mume naye alimjibu mke wake kwa kushangaa kwa nini mke wake anasema hampendi!

"Ni kweli hunipendi na siku zinavyozidi naona hunipendi zaidi" mwanamke aliendelea kulalamika.
Mshauri wa ndoa akaingilia kati na kumuuliza mume "je, huwa unamwambia mke wako Nakupenda?"

Kwa majivuno mwanaume akajibu kwamba
“anajua nampenda kwani kila jioni nawahi nyumbani kuwa naye, nampa pesa anazohitaji anunulie kitu chochote anataka, nimemjengea nyumba nzuri, nimemununulia gari zuri, Pia nimekubali kuja naye kwako mshauri, je unadhani hadi hapo simpendi?

Mshauri akakaza uzi bado kwamba acha hayo yote je, huwa unamwambia “Nakupenda" mke wako?”
Mume akawa anamwangalia mke wake na mke akawa anatikisa kichwa kukubaliana na maneno ya mshauri wao wa ndoa kuonesha ni kweli huwa haambiwi na mume wake “nakupenda mke wangu.
Mume akajibu akasema “hivi kuna ulazima gani kumwambia nampenda wakati vitu ninavyofanya kwa ajili yake vinaonesha nampenda?"

Hapa wanaume wengi tunaweza kuandamana kumtetea mwanaume mwenzetu na kwamba huyu mwanamke ana lake na kweli hana shukuruni kwani wanawake wangapi wamefanyiwa vile yeye amefanyiwa na wapo kimya, huyu mwanamke pamoja na mazagazaga yote mwanaume mwenzetu amejtajidi kumpa bado anaonekana hampendi.
Hata hivyo linapokuja suala kuonesha mwanamke anapendwa tunatofautiana sana na mitazamo tunayo wanaume wengi.

Mwanamke huhitaji kusikia kwa maneno (tamka) over and over mkiwa wawili au hata mbele za watu kwamba unampenda au “nakupenda”.
Pia inaonekana ni jambo au suala la kawaida sana ingawa mwanzo wa kupendana watu huambiana maneno mengi matamu lakini wanavyoendelea na mahusiano huanza kujisahau.

Kuna maneno zaidi ya 16 ambayo wanandoa ni muhimu sana kuyatamka kila mmoja kwa mwenzake ili kuleta affections na msisimko wa kujisikia unapendwa hasa wanawake.

Nakupenda
Ni vizuri kuwambia nakupenda kabla hujaondoka kwenda kazini na wakati ukifika nyumbani baada ya kutoka kazini, mwambie nakupenda kabla hujamaliza kuongea kwenye simu.
Kila ndoa huhitaji dose kila siku na dose mojawapo ya kila siku ni neno nakupenda. Wala usiwe na wasiwasi kusema nakupenda kila si tabia mbaya hata kama mwenzio amekasirika kwa jambo Fulani na kusema nakupenda kunaweza kufungua mlango wa kusamehewa haraka.

Samahani
Uliambiwa unaporudi uwe umenunua maziwa na ile unafika nyumbani kumuona mke wako unakumbuka kwamba maziwa hujanunua, sema nisamehe, wewe ni mke na ulimuahidi mume wako kwamba utafua nguo zake na hana nguo za kuvaa sema unisamehe na maanisha.
Huwa hatumsaidii mtu yeyote tunapojilinda kwa namna yoyote, ila kiburi ndicho hupata faida. Nakuogopa kutumia neno nisamehe lakini, kwani hiyo huua msamaha.

Umependeza
Wakati tunachumbiana huwa tunapeana sifa kila siku hata hivyo baada ya kuendelea sana kwenye ndoa tunajisahau kupeana sifa.
Labda tunadhani mwenzi anajua jinsi tunavyojisikia au tunadhani kwamba haina haja tena kuendelea kutoa sifa.
Mwanamke anahitaji kuendelea kuambiwa anapendeza hata baada ya kuzaa mtoto wa kwanza, wa pili hadi mwisho ingawa kuna wakati anaweza hata mwenyewe asikubali hata hivyo wewe umefanya nafasi yako.
Hata wanaume nao wanahitaji la kuambiwa amependeza au leo yupo handsome na pamba zake alizojipigia.
Kupeana sifa huimarisha intimate kati ya wanandoa, kama mke wako hajioni ni sexy kwa nini awe anataka mahaba kwako? Mhakikishie kwamba yupo sexy na akili yake itafunguka kwamba unamuhitaji.

Nakuhitaji
Wapenzi wetu wanahitaji siyo kufahamu kwamba tuna wa-appreciate tu bali tunawahitaji, tunapaswa kuwaambia kwamba maisha bila wao yangekuwaje? Inakuwaje kila wiki wakijua kwamba tunawahitaji.
Kama kutamka kwa mdomo inakuwa ngumu kumwambia nakuhitaji kila siku basi andika barua, message, email nk.
Mwanamke anahitaji kusikia kwamba anavutia pia wanaume wanapenda kufahamua kwamba mke anamuhitaji pia.

Asante
Hivi inakuwaje watu wa nje ndo wanazipata asante zetu kwa wingi kuliko sisi wanandoa wenyewe.
Ukienda sokoni au kazini asante zinatoka bila wasiwasi na mume na mke inakuwa ngumu?
Mwambie asante mke kwa dinner, asante kwa kusafisha nyumba, kwa kukufulia nguo, mwambie asante mume kwa jinsi anavyoweza kuipa familia kipato, mpe asante kwa kuwahi kurudi nyumba.
Kama unashindwa andika email au ujumbe wa simu au vyovyote unaweza.

“The greatest emotional crime a man commits is to take his wife for granted"

bofya hapa Ukitaka kujua mengine mengi.

Monday, August 10, 2009

SABABU NYINGINE ZA KUZINI ZA AJABU EH!

Leo nimeona tuanze wiki hii kwa kujua sababu hizi haya ebu soma hapa.

Kuna sababu nyingi zinazotajwa zinazosababisha wanandoa kutoka nje ya ndoa, miongoni mwa sababu hizo nyingine ni kichekesho kabisa.
Inasemekana ni rahisi sana kujua kama mwenzako anatoka nje ya ndoa au la, na hiyo inafanyika kwa kuangalia dalili au mabadiliko fulani kutoka kwa mwenzako na kwa kuzingatia tabia yake ya awali uliyoizoea ni rahisi kugundua kuwa kuna jambo ambalo sio la kawaida linaendelea.

Kuna sababu nyingi zinatajwa kusababisha baadhi ya wanandoa kutoka nje ya ndoa.
Inasemekana kwamba sababu mojawapo kubwa ni kutokana na wanandoa kutokuwa karibu kama zamani walipokuwa ndio wameoana, ule moto wa awali unatoweka au kufifia kabisa, kama ni mume au mke anahisi kuchokwa na mwenzake, na hapo kuna uwezekano mkubwa akatafuta faraja kwingine.

Utakuta mume au mke anatoka nje kujaribu kutafuta anayedhani atautuliza mzuka wake wa mapenzi.
Lakini inasemwa pia kuwa kuna wengine hutoka nje ili kuonesha kuwa nao wanaweza, kuna baadhi ya watu kutongoza na kukubaliwa au kutongozwa na kukubali huchukuliwa kama kipimo cha kuonesha kwamba mtu anapendwa au anamudu.

Kuna wengine kutongoza na kukubaliwa huchukuliwa kama mashindano, yaani mwanaume kuwa na idadi ya wanawake wengi aliotembea nao nje ya ndoa huchukuliwa kama jambo la kifahari hakuna mfano.
Kuna wale ambao hawahisi kupendwa ndani ya ndoa zao, nao hulazimika hutoka nje ya ndoa ili kuthibitisha kwamba nao wanapendwa.

Sababu nyingine inayotajwa ni ile ya kisasi, unaweza kukuta mwandoa mwanamke au mwanaume anaamua kutoka nje ili kulipiza kisasi au kumkomoa mwenzake. Tena inawezekana jambo lenyewe likawa ni dogo ajabu lakini ili kuonesha ubabe mwanandoa anaamua kutoka nje ya ndoa ili kumkomoa mwenzake. Kwa mfano mke kuchelewa kutoka kazini mara kwa mara au mume kushindwa kumtimizia mke mahitaji kama vile mavazi au vitu vya urembo, hiyo inaweza ikawa sababu tosha kabisa ya mwanandoa kusaliti ndoa yake kwa kigezo cha kumkomoa mwenzake. Mara nyingi kutoka nje ya ndoa kwa sababu hizi kuna madhara makubwa kwa muhusika

Kuna wale wanaume ambao umri umeenda, hawa nao hudiriki kutembea na vibinti vidogo vya kuwazaa ili kuthibitisha kwamba bado hawajazeeka na wanamudu kufanya tendo, hata wanawake vile vile wenye umri mkubwa pia nao wamo kwenye mkumbo huo wa kutembea na vijana wadogo, wenyewe huwaita Serengeti Boys, wakimaanisha ile timu ya soka ya vijana wa chini ya umri wa miaka 18.

Sababu za wandoa kutoka nje ni nyingi tena nyingine ni za kijinga kabisa, lakini je tunajua madhara tunayopata au tutakayopata kwa ujinga huu?
Ni kitu gani hasa tutakachofaidi kwa kutoka kwetu nje zaidi ya maumivu au hata kuvunjika kwa ndoa?

Siku hizi maradhi ya zinaa ni mengi mno achilia mbali ukimwi unaopigiwa kelele kila uchao katika vyombo vya habari. Takwimu za ugonjwa huo barani afrika zinatisha, lakini mtu yuko radhi kutoka nje ili kumkomoa mwenzake au kuonesha kwamba na yeye anaweza.

Ni vyema kama mwanandoa anahisi kama upendo wa mwenzake umepungua kutafuta suluhu, kwani kujadiliana kwa upendo ili kupata suluhu ni jambo la msingi kabisa ili kurejesha moto wa awali kama unahisi umepungua. Inashauriwa majadiliano hayo yafanyike kwa uwazi na katika njia ya kujenga, na ule upande wenye matatizo, ukubali kurejea katika mstari ili kurejesha amani nyumbani.

Si vizuri kutupiana lawama, hiyo haitasaidia kuleta maelewano, bali inashauriwa kila upande kubeba jukumu lake kwa mustakabali wa ustawi wa ndoa husika.

Saturday, August 8, 2009

TUWE TUNAANGALIA TUKAAPO CHOONI INAWEZEKANA KUKAWA NA MGENI KAMA HUYU



Habari ndio hiyo ndugu zanguni.Haya nawatakienikila ka kheri wote wiki end njema. Kaazi kwelikweli!!!!

Thursday, August 6, 2009

MAISHA YA UGHAIBUNI NA VIJIMAMBO TOKA NYUMBANI

Naomba nikiri kuwa tangu nianze kublog nimetokea kufahamiana na watu wengi sana, si hivyo tu bali pia nimekuwa nikipata email nyingi sana kutoka kwa wasomji wa blog hii ya maisha.

Miongoni mwa email ninazopokea zipo nyingine ambazo kwa kweli huwa zinaniacha na maswali lukuki, hata sijui nisemeje, ngoja leo niwashirikishe wasomaji wa blog hii katika kutafakari jambo hili.

Nakumbuka mwaka juzi 2007 tulikuwa nyumbani Tanzania. Baada ya wiki mbili kupita tulikwenda kumtembelea baba yetu mkubwa. Tulipokuwa pale, baada ya muda akaja mzee mmoja na kuanza kuuliza mama wa watoto yupo wapi? {Akiwa na maana ya mimi}, kisha akaendelea, "Nimesikia binti wa Ngonyani anayeishi Ulaya kaja" Baba mkubwa akamjibu akamwambia "ni huyo hapo" huku akionesha kwa kidole pale nilipokaa. Mzee kusikia hivyo akashtuka na kusema si kweli mbona yupo kama kawaida tu. Hakuamini kwa muda, ila baada ya kuniangalia sana aliona sura inafanana na ya baba yangu, ndio akaamini.

Mwaka huu katikati ya mwezi wa kwanza wakati tulipokuwa nyumbani Tanzania, nakumbuka ulikuwa ni msimu wa kulima. Siku moja tukiwa tunapumzika sebuleni. Mara tukasikia mtu akibisha hodi, tukaitikia karibu na tukafungua mlango, kumbe kulikuwa na watu watatu wanaume ambao hatuwafahamu.
Tukawakaribisha, na wakaingia ndani, wakaanza kueleza kilichowaleta. Walikuja pale kwetu kuomba hela kwa ajili ya kununulia mpira au kama tuna mpira basi tuwape.

Ninachotaka kusema hapa ni kwamba watu wa nyumbani Tanzania au Afrika kwa ujumla wanafikiri mtu kama anaishi Ulaya basi wana ile picha kuwa mtu huyo atakuwa amejiremba kwa kuweka mikorogo na vikorombwezo vingine vya ulimbwende na mavazi yake yatakuwa tofauti na watu wa pale kijijini au mjini, atakuwa anaongea kiingereza au lugha nyingine ya huko aishiko na sio kilugha kama vile kingoni. Pia wanadhani mtu huyo atakuwa anaishi kama yuko peponi na sio mtu wa kawaida kwa maana ya kwamba ana ukwasi uliopindukia, na hana shida kabisa na maisha yamemnyookea.

Ni hivi majuzi tu nimetumiwa ujumbe mfupi kupitia simu yangu ya kiganjani toka kwa mtu nisiyemfahamu akiniomba hela:- nitanukuu ujumbe huo “Mama shikamoo! Za siku nyingi? Nina ombi, ninaomba nisaidie mtaji lengo langu niweke duka la dawa za mifugo tuna shida sana na magonjwa ya mifugo. Nitashukuru sana ukinisaidia, naomba majibu asante” mwisho wa kunukuu ujumbe huo.

Kusema kweli nilishangaa sana kupata ujumbe wa aina hiyo kutoka kwa mtu nisiyemfahamu. Kwa mtazamo wa mtu huyo ambaye sijui kama ni kijana au mzee na hata sijui ni wa jinsia gani akilini mwake anadhani kwamba kwa kuwa ninaishi Ughaibuni ni lazima nitakuwa na pesa, asijue kwamba maisha ya huku ni tofauti sana na tena afadhali hata huko nyumbani Afrika unaweza kwenda kuomba chumvi kwa jirani au hata kula kwa mtu bila hata ya wasiwasi.

Swali:- Je Ungekuwa wewe ndio mimi ungefanya nini?

Wednesday, August 5, 2009

AFRIKA YETU + MUNGU IBARIKI AFRIKA






Mungu ibariki Afrika,
Wabariki Viongozi wake,
Hekima Umoja na Amani,
Hizi ni ngao zetu,
Afrika na Watu wake,
Ibariki Afrika,
Ibariki Afrika
Tubariki Watoto wa Afrika.

Monday, August 3, 2009

WATOTO NA TATIZO LA KUSHINDWA KUSOMA

Wapo baadhi ya watoto ambao hutokea kutokuwa na uwezo wa kusoma kabisa. Hali hii inaweza kutafsiriwa kama kitendo cha mtoto kutokuwa na uwezo wa kiakili, wa kuweka kumbu kumbu na kuta taarifa katika maandishi, kwa maan ya kutokuwa na uwezo wa kusoma na kuandika, na hivyo kuwaweka wazazi katika wakati mgumu wa kutojua mustakabali wa maisha ya mtoto wao.

Inasemekana kuwa watoto wa aina hii huwa wanakuwa na kuiwango cha kawaida, cha chini na hata cha juu cha akili. Tatizo hili kwa kiwango kikubwa huwa linawatokea zaidi watoto wa kiume, ukilinganisha na watoto wa kike, na kitaalamu hujulikana kama Dyslexia.

Watoto wenye tatizo hili hupata ugumu katika kutumia lugha fasaha kwa maana ya kutoweza kusoma neno kama lilivyoandikwa. Kwa mfano anaweza kusoma neno mutaskabali akiwa na maana ya mustakabali au kuandika namba 548 badala ya 584,au wakati mwingine kuandika L akiwa na maana ya namba 7.

Je wazazi watawatambuaje watoto wao wenye tatizo hili?Mara nyingi watoto wenye tatizo hili huwa wanapuuzwa, hivyo kuwa vigumu kuwatambua kwamba wan tatizo hili. Na huw ahawpewi msaada maalum kwa kuonekana kwamba tatizo walilonalo ni la kawaida tu, baadae watajua kusoma na kuandika.

Watoto wenye tatizo hili huwa wanajitanabaisha kwa dalili zifuatazo:

1. Huwa ni vigumu sana kwao kujua kusoma, 2. Wanaposoma wanasoma ovyo ovyo. 3. Wengine hawakumbuki wamesoma nini kwa vile akili yao yote inakuwa maneno sio herufi. 4. Wanakuwa na matatizo ya kuandika/kupanga herufi sawa sawa.

Zipo njia mbalimbali za kuwasaidia watoto wenye tatizo hili. Ni muhimu kwa jamii kutowachukulia kama hawana akili kabisa, kwani kitaalamu watoto wa aina hii wanakuwa na kiwango cha kawaida au kuzidi kawaida. Hivyo kinachotakiwa kwa wazazi na waalimu ni kuwapa msaada wa ziada ukilinganisha na watoto wengine wasiokuwa na tatizo la aina hiyo.

Kwa mfano wazaziwanaweza kutafuta mwalimu ambaye atakuwa anakuja nyumbani kumfundisha mtoto mwenye tatizo hilibaada ya saa za kawaida za masomo. Na mara nyingi zoezi hili linapofanyika linatakiwa lisimjengee mtoto hisia kwamba yuko tofauti na watoto wengine, kwani kwa kufanya hivyo kutamjengea mtoto huyo kutokujiamini na mwishowe kushindwa kabisa kumudu kusoma

Sunday, August 2, 2009

JUMAPILI NJEMA JAMANI


Napenda kuwatakia wote jumapili njema wote. Wuwe na wakati mzuri wa mwisho wa wiki.

Saturday, August 1, 2009

UJUMBE WA LEO

KISWAHILI:- Ulijua ya kwamba.....
......katika maisha ya binadamu nywele zinaota 760 cm?

KISWIDI:- Visste du att......
......håret växer 760 cm under ett människoliv?

KISWAHILI:- Ulijua ya kwamba.....
......kuna aina 2200 za mbu Sweden na 30000 ulimwenguni kwote?

KISWIDI:- Visste du att....
....det finns 2200 olika arter mygg i Sverige och över 30000 i hela värden?


.