Nilipokuwa nyumbani Tanzania hivi karibuni nilikutana na shoga yangu mmoja ambaye katika mazungumzo yetu alinisimulia kisa hiki cha shoga yake mmoja aliyekwenda kwake akimtaka ushauri.
Kisa cha kutaka ushauri ni kutokana na kukuta mumewe amehamia nyumba ambayo inamilikiwa na mpenzi wake wa zamani. Huyo mwanamke alikwenda masomoni nje ya nchi na kumuacha mumewe nchini na huku nyuma mkataba wa nyumba waliyokuwa wakiishi ulipoisha mwenye nyumba akawaamuru wahame ili aifanyie nyumba yake ukarabati, basi yule bwana akamfahamisha mkewe kule ughaibuni alipo kuwa wametakiwa wahame na baada ya kushauriana wakakubaliana watafute nyumba nyingine lakini isiwe ni maeneo yale ya kinondoni walipokuwa wakiishi, wakakubaliana waatafute nyumba maeneo ya Kijitonyama au Mwenge.
Baada ya kuhangaika sana yule bwana alipata nyumba maeneo ya Kijitonyama na kumjulisha mkewe na baada ya kumweleza jinsi nyumba ilivyo mkewe alikubali wahamie kwenye nyumba hiyo.
Ilikuwa ni nyumba kubwa inayojitegemea na mwenye nyumba alikuwa anakaa uani na wao wakikaa nyumba kubwa.
Wakati huo ilibaki miezi sita yule bibie arudi na kuungana na mumewe. Siku, wiki, miezi ilikatika na hatimaye yule bibie akamaliza masomo yake na kurejea nchini. Alipofika nyumbani, kwa jicho la kwanza aliipenda ile nyumba na kuisifia sana, na mumewe alifurahi kusifiwa na mkewe kwa kuchagua nyumba nzuri mpaka mkewe akaridhika nayo.
Kwa bahati mbaya mwenye nyumba hakuwepo alikuwa amesafiri nje ya nchi kwani alikuwa ni mfanyabiashara na mkewe alifariki miaka mitatu iliyopita na watoto wake walikuwa wanasoma nje ya nchi kwa hiyo pale nyumbani alibaki peke yake na mtumishi wake wa ndani.
Baada ya kukaa nyumbani kiasi cha wiki moja aliripoti kazini na kuanza kazi. Siku moja jioni aliporudi nyumbani mumewe alimuomba ampeleke akamtambulishe kwa mwenye nyumba kwa kuwa amerudi, walizunguka hadi uani anapokaa mwenye nyumba na kukaribishwa na mtumishi wake wa ndani {House Boy} akawaomba wamsubiri mwenye nyumba ambaye alikuwa ndani akawaitie.
Mwenye nyumba alipotoka yule bibie alikuwa kama amepigwa na shoti ya umeme na asiamini macho yake, kwani aliyesimama mbele yake hakuwa ni mwingine bali ni mpenzi wake waliyepoteana miaka kumi iliyopita baada ya yule mpenzi wake kwenda nje ya nchi kimasomo na waliachana kwa ahadi ya kuoana akirudi. Hata yule mwenye nyumba alishikwa na butwaa kwa nukta kadhaa, lakini akawa mwepesi kujiweka sawa na kuwakaribisha kwa bashasha huku akimuagiza yule mtumishi wake awaletee wageni vinywaji.
Baada ya kusalimiana na kisha kumtambulisha mkewe kwa mwenye nyumba waliaga na kuondoka kurudi ndani kwao, kuanzia siku ile yule bibie hakuwa na raha na alikuwa akijitahidi kukwepa asionane na yule mwenye nyumba.
Sasa amebaki njia panda. Je amshawishi mumewe kwamba wahame ile nyumba au amwambie ukweli juu ya uhusiano wake na mwenye nyumba miaka kumi iliyopita?
Sijui wewe msomaji unayesoma hapa ungemshauri nini huyu bibie, lakini ninachotaka kusema hapa ni juu ya siri tunazoambiana na waume zetu.
Labda nikuulize wewe msomaji. Je, umewahi kumficha mumeo au mkeo kitu chochote juu ya maisha yako ya zamani au ya sasa? Je mumeo au mkeo aliwahi kukushangaza na siri yoyote ya mambo yake ya zamani?
Naomba niwe mkweli kwa hili kwamba katika mahusiano,zipo siri ambazo unaweza kuzitoa na nyingine hutakiwi kuzitoa. Hata hivyo usijidanganye kuwa unaweza kuficha kila siri, lakini ni vyema ukajua kwamba ukitoa kila siri ndio ndoa yenu itaimarika kwa kuonekana kuwa umkweli, mwadilifu, au mcha mungu, si kweli kwani kuna wakati kusema kila siri kunaweza kuibua migogoro isiyo ya lazima katika ndoa hasa kama upande mmoja unaweza kutumia siri uliyoieleza kama bakora kukuadhibu pindi mkitofautiana katika mambo fulani fulani, ukweli ni kwamba hii itategemea zaidi kuwa mumeo au mkeo ni mtu wa aina gani. Kwani kuficha siri ni kujilinda dhidi ya dhihaka na kukwazana, kusiko na maana.
Kuna siri nyingine ambazo huna budi kuzitoa, kama unahisi kuwa zikibainika zitavunja uhusiano wenu, au zitasababisha uhusiano wenu kuyumba. Mambo kama magonjwa ya kurithi, wapenzi wa zamani au tabia mbaya ulizokuwa nazo kabla ya kuoa au kuolewa, inabidi uziweke wazi kwa mkeo au mumeo ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima pindi akijua, ni vyema ukafahamu kuwa jambo lolote kama likijulikana na zaidi ya mtu mmoja sio siri tena, kwani linaweza kumfikia mwenzio.
Kuna wakati mwanandoa anaweza kuona kama amechelewa kutoa siri yake kwa mwenzie, na hivyo kuamua kukaa kimya, lakini baadae siri hiyo ikifichuka inamuweka mahali pabaya na hivyo kuchanganyikiwa.
Inasemekana kuwa wanaume ndio huwaficha wenzi wao mambo mengi ukilinganisha na wanawake. Kwa nini?
Kwa sababu wanaume wanadhani kuwa, kwa kuficha ukweli, watazuia migogoro ambayo ingeweza kutokea kama mambo hayo yangewekwa wazi. Kwa kawaida wanaume wengi huogopa hasira za wake zao, kwani hawapendi mivutano ndani ya nyumba.
Kuweka wazi juu ya wapenzi wako wa zamani kwa mwenzio ni jambo jema kabisa, hata kama wako 20 we sema tu, ili mwenzio aamue kama yuko tayari kuoana na wewe au la. Kwani hiyo itakuweka huru, hata mwenzio akikutana na washakunaku na kuelezwa, ni rahisi kuwaambia kuwa anafahamu na hivyo kuwaumbua washakunaku hao.
Ukiwa mkweli haitakuwa rahisi kwako kuficha jambo, na hiyo itakusaidia kumfanya mwenzio akuamini zaidi na kuongeze upendo kwako.
8 comments:
Hii imetulia kwakweli, ni kisa ambacho kinaasshiria maisha ya kila siku ya watu. Asante kwa changamoto hii na nadhani kila atakayesoma anapata jambo fulani la kurekebisha katika maisha na mahusiano yake katika familia/ndoa.Hongera kwa stori safi
Lol.... ipo kazi kwali mwavene... mie simo! ha ha ha aise dunia mbovu hakuna usalama wa kutosha kila siku tunararuana, na kusemana na huku tunaharibiana heeee mwenga pana kyani kayni kayani kayani jamani kulikoni???
Dada Yasinta naomba nikunukuu.....
"Naomba niwe mkweli kwa hili kwamba katika mahusiano,zipo siri ambazo unaweza kuzitoa na nyingine hutakiwi kuzitoa. Hata hivyo usijidanganye kuwa unaweza kuficha kila siri, lakini ni vyema ukajua kwamba ukitoa kila siri ndio ndoa yenu itaimarika kwa kuonekana kuwa umkweli, mwadilifu, au mcha mungu, si kweli kwani kuna wakati kusema kila siri kunaweza kuibua migogoro isiyo ya lazima katika ndoa hasa kama upande mmoja unaweza kutumia siri uliyoieleza kama bakora kukuadhibu pindi mkitofautiana katika mambo fulani fulani, ukweli ni kwamba hii itategemea zaidi kuwa mumeo au mkeo ni mtu wa aina gani. Kwani kuficha siri ni kujilinda dhidi ya dhihaka na kukwazana, kusiko na maana."
Mwisho wa kunukuu......
Dada bado unaniacha na maswali, sasa, kwa mujibu wa maelezo yako hayo hapo juu. Je ni busara kusema siri zetu kwa wenzetu au tusiseme, maana umesema siri ikishajulikana kwa mtu zaidi ya mmoja sio siri tena......hivi ni jambo gani unaweza kulijua peke yako tu? yaani peke yako bila ya mtu mwingine?
kama ni mahusiano ya kingono ni lazima yafanywe na watu wawili,kama ni tabia mbaya ni lazima ilionekana na watu wengine na ndio maana ikapewa tafsiri kuwa ni tabia mbaya na kama ni magonjwa ya kurithi ni hivyo hivyo.
sasa ni kitu gani cha kuficha hapo.....!!??
au labda tuseme tusifichane from biggining ili mwenza wako ajue mapema kabisa kuwa ni mbivu au mbichi ili hata kesho asipate sababu ya kukuzodoa, vinginevyo hutaisha kuwa na presha.
Kwa upande wa huyo dada ingawa hukumalizia kuwa huyu shoga yako alimshauri nini, lakini hakuwa na sababu ya ku-panic, kwani hata huyo mumewe ni lazima katika ujana wake alipitapita na wasichana wakati akijifunza mambo ya kikubwa kwa hiyo angemwambia ukweli tu, kwa kumwambia " mwenzangu huyu bwana aliwahi kuwa boyfriend wangu wakati ulee tukiwa vijana miaka kumi iliyopita kwahiyo mimi naona tuhame maana sitakuwa na amani na hii nyumba" kama ni mwanaume muelewa ni wazi hatakuwa na neno anaweza kuridhia ili kulinda ndoa yao.
huo ndio ushauri ningempa, lakini swala la kukaa na kuanza kuhadithiana uchafu miofanya ujanani, hilo nalo sidhani ni jambo la busara...Duh, hivi unaanzaje..........labda niseme tu kwamba kuna wale ambao unaweza kuwazungumzia kulingana na mazingira yaliyopo, na kama kuna umuhimu wa kufanya hivyo, lakini kukurupuka na kuanza kutaja wa kwanza mpaka wa thelathini.....!!! ndio kuna uwezekano mtu akawa amepitia au kupitiwa na watu wengi kutokana na ushapu wake, sasa ndio awe anaandika kwenye diary au........
Kaaaaazi kweli kweli....hii mada dada Yasinta ni ngumu kweli......
Ngoja niwaachie wengine nao waseme halafu labda nitarudi
Jamani, si kila mtu alipitia uchafu mnavyofikiri, mambo ya kusema ni lazima mwanaume alishapitia vijidada fulani.... ebu acheni hizo.
Samaki mmoja kuoza sio wote, huo usemi huwa naupinga. Ninao uthibitisho wa wanaume ambao maisha yao ya awali ni safi kabisa. Nimekamulia hapo tu, nikizidi nita#@* bure...
Kaka Chib, acha Jazba, mwenye mada hakumnyooshea mtu kidole na hata dada Koero hakumnyooshea mtu kidole, mjadala ni mgumu na mtamu na unahitaji kutafakari kwa hiyo usije ukauvuruga.....
Mie mpaka hapo sina la kusema, nangoja kujifunza zaidi kwani hii mada imelenga eneo nyeti la mahusiano na dada yangu Koero kanyumbulisha vizuri.
nangojea wachangiaji wengine nao waseme na mie labda nitapata la kusema........
mmmh! ngoja nikatafakari kwanza nitarudi baadae,Yasinta hii yataka mtu utafakari kwa kina.
Kuwa mkweli ni bomba la jambo ila kumbuka tu mambo mengi ya nahitaji mahali na muda wake maalumu kuongelewa au tu kufanywa!
Kuna siku hata mgumu sio siku anataka kusikia jinsi gani bibie a.k.a kimwana wake anamtamani jamaa fulani na alitakwa na jamaa gani kama tu bado hajaonjwa.
Nishashuhudia hasa wazungu hasa mitaa ya Scandinavia wakiendekeza ukweli mpaka UKWELI UNAZIDI au tu sio MAHALI PAKE mpaka unashuhudia jemadari asimuliwaye ukweli uzalendo unamshinda.
Nisha shuhudia mshikaji kafuatwa kazini na mke wake kisa mke anataka kukiri kaonjwa jana yake na wajanja kwa hiyo anataka ukweli uwe wazi, jamaa bado kidogo azimie.
Na mie mwenyewe nishawahi kustuliwa na kipenda roho mambo zake na sikupaniki tatizo likageuka kuwa labda simpendi kwa dhati bibie kwa kuwa alitegemea nitapaniki na sikupaniki kwahiyo akatafsiri simjali!
Haya mambo kama alivyosema Koero ni magumu!:-(
Ila kuhusu huyo mwanadada nafikiri inategemea na Mr WAKE ni mtu wa aina gani ila kwa kuwa hayuko huru labda ingekuwa afadhali atafute sababu za kuhama bila kutoa kuingilia details za KWANINI hasa kama Mr anawivu.
Najua watu ambao huyo mwanadada akiripoti kuwa mwenye nyumba ambaye sasa yuko single ndio alikuwa mchumba na officially walikuwa hawajaachana, hata wakihama akichelewa kurudi nyumbani inaweza kutafsiriwa kuwa kaenda kutesti zali ili aone bado ananogewa au la na liMr [Baba mwenye nyumba] kama LI Husbandi WAKE linawivu wa kizembe.
Taka usitake kuna watu udhaifu wao ni wivu!
Kaaaaazi kweli kweli, naomba nikiri kuwa hii mada ni ngumu na inahitaji kutafakari.
Naomba nichukue nafasi hii kuwashukuru wote mliotoa maoni katika mada hii lakini pongezi za pekee ziwafikie mdogo wangu Koero na kaka yangu Simon Kitururu.
Nakubaliana na yote mliyosema. Kwa kweli swala la kuambiana siri kati ya wanandoa, ni jambo linalotakiwa kufanywa kwa umakini sana, na itategemea zaidi huyo mpenzi wako ni mtu wa aina gani.
Mdogo wangu Koero, sikueleza kuwa yule dada alishauriwa nini kwa kuwa sikuona umuhimu wa kufanya hivyo, kwa kuwa sio mimi niliyeombwa ushauri, kwani kama ningeeleza kwamba alishauriwa nini na msimulizi, wa stori hiyo ningeibua mjadala mwingine na hilo sikutaka litokee.
Lengo kubwa kabisa la kuweka mada hiyo ilikuwa ni kutaka kupata mitazamo tofauti tofauti kutoka kwa wasomaji wa hiki kibaraza juu ya swala zima la siri tunazoambiana na waume zetu au wake zetu.
Na kusema ukweli nimejifunza mengi. Pamoja na kuweka mtazamo wangu lakini naamini kama ilitokea kutofautiana basi hiyo ni changamoto tunayotakiwa kuifanyia kazi.
Naomba nisihitimishe huu mjadala ili hata wale ambao hawakupata nafasi ya kuchangia waendelee kutoa maoni yao.
Mjadala uendelee……………..
Post a Comment