Wednesday, May 28, 2014

UMOJA NI NGUVU !!!

 Ni raha pale wote mnaposaidiana kazi  sio kumwachia mmoja tu. Hapa akina mama na watoto wanamenya karanga ingawa wengine wanapeleka mdomoni lakini wamejumuika kuifanya kazi...inavyoonekana ni karanga kwa ajili ya mbegu au labda kuunga mboga....Raha sana kushirikiana.....
....na hapa vijana hawapo nyumba wanasaidia kazi za nyumbani hapa wanakoboa mahindi. Wananikumbusha enzi hizi tulivyokuwa tukikoboa mahindi au kutwanga mihogo na kaka zangu. Nani anasema kazi ya kutwanga au kukoboa ni ya akina dada/mama tu?  Nimependa sana hii Je na wewe umependa?:-)

Monday, May 26, 2014

KUULIZA SI UJINGA...NAMI LEO NINA WALI KWENU....KILIMO CHA UFUTA....KAPULYA MDADISI!!!

 Kama mjuavyo na udadisi wangu...nimejaribu kuatika UFUTA na umeota sasa swali niendelee vipi  ili kupata ufuta?
Hili si shamba langu. Ila naota kama lingekuwa langu . Kwa hiyo ndugu zangu naombeni msaada wenu ili nifanikishe ...Kaka Bennet msaaaadaaaaaa...

Sunday, May 25, 2014

LEO NI SIKU YA AKINA MAMA HAPA NAMI NIKIWA NI MMOJAWAPO..HONGERA KWA SIKU HII AKINA MAMA WOTE/GRATTIS PÅ MORSDAG!!!

Napenda kuwapongeza akina mama wote duniani kwani HAKUNA KAMA MAMA. Siku hii ya leo hapa nimepongeza kwa zawadi hizo hapo juu na nimeambiwa nimekuwa mama na mke mwema. Nami nimejibu AHSANTE SANA KWA YOTE NA HAYO YOTE NI KWA AJILI YA MALEZI MEMA YA MAMA YANGU BILA KUMSAHAU BABA YANGU. HONGERA AKINA MAMA/GRATTIS PÅ MORSDAG.

JUMAPILI NJEMA KWA WOTE..NA HILI NDILO NENO LA JUMAPILI HII LILILOCHAGULIWA NA MAISHA NA MAFANIKIO

Mwana  mwenye Hekima humfurahisha Babaye; bali mwana mpumbavu ni mzigo wa mama-Mithali 10:1.
TUMALIZIE JUMAPILI HII NA WIMBO HUU WA JESHI LA MUNGU KUTOKA KWAYA YA MTAKATIFU SECILIA PAROKIA YA IRAMBA NGOREME MUSOMA 

BASI NIWATAKIENI WOTE MTAKAOPITA HAPA  JUMAPILI NJEMA SANA MAANA HUU WIMBO DUH! JASHO LANITOKA HAPA:-)

Friday, May 23, 2014

VYAKULA NILIVYOTAMANI IJUMAA YA LEO.....SAMBUSA NA EMBE!!!


Leo nimetamani kweli SAMBUSA kitu ambacho kinachosha ni kwamba nimewahi kujaribu kutengeneza na sikuweza kama inavyotakiwa na huchukua muda mwiiiingi sana. Sijui kuna njia rahisi zaidi? Halafu......

.....nikajikuta naota ndoto ya hili tunda EMBE...Songea ndo zinakwisha kwisha sasa....Kaaaazi kwelikweli ngoja niache kuota .....IJUMAA NA MWISHO MWEMA WA JUMA!!

Thursday, May 22, 2014

USISAHAU ULIKOZALIWA/TOKA..KWETU NYASA HAPA!!!

Mtazamo/mandhari ya kuvutia ya ziwa nyasa hapa ni Mbamba  Bay Mkoani Ruvuma.

Wednesday, May 21, 2014

MAMBO 6 WASIYOYAPENDA WANAUME KUTOKA KWA WENZA WAO!!!

Ukiwa mpekuzi  utakutana na mengi. Leo katika pita pita kwa majirani zangu nimekutana na hiii kutoka DinaMarios.blogspot.com -- Haya niliyapata kutoka kwa mshauri wa masuala ya mahusiano, ndoa na vijana Frederick Kyara. Hizi ni baadhi tu nakuwekea hapa japo kuna vitu pia wanawake hawavipendi kutoka kwa wenzi wao wanaume.
NAYO NI HAYA HAPA UNGANA NAMI KUJADILI JAMBO HILI ambalo kwangu nimeona ni changamoto au niseme sikujua.

1. Wanaume hawapendi kuambiwa cha kufanya na wenzi waoMwanamke unapotaka mwanaume afanye jambo usimwambie alifanye bali fanya kama una mpa ushauri.Kwamba John hivi kwa nini tusiweke balbu hapa kwenye korido maana kuna giza kweli. Badala ya hivi wewe John huoni hapa kwenye korido kuna giza balbu imeungua mwezi sasa hujabadilisha kwa nini? Weka balbu bwana. Atafanya au asifanye kabisa kwa sababu umemwambia cha kufanya.

2. Wanaume hawapendi mwenzi mwenye makelele, mlalamishi

Yeye ni kulalamika kuanzia Jumatatu hadi Jumapili. Japo wanawake nao wanasema kuna wanaume walalamishii balaaa. Na wenye gubu wanasusa kula mpaka kuongea wanawanunia wake zao mmmmh!

3. Wanaume hawapendi mwenzi mchafu

Mchafu wa mwili wake na hata nyumbani kwenye suala la kutunza nyumba wanayoishi. Uchafu hufanya mwanamke apoteze mvuto.

4. Wanaume hawapendi mwenzi mbishi

Japo na wanawake wanasema wanaume ndio wabishi zaidi. Utampa mwanaume ushauri lakini haufanyii kazi ubishi mwingi.

5. Wanaume hawapendi kuamrishwa na mwenzi wao

Mwenzi mbabe anaetoa amri na kumtawala hawataki.

6. Wanaume hawapendi kuhisiwa hisiwa na kusachiwa sachiwa

Kumpekua kwenye simu, mifuko ya suruali kwamba unamulika mwizi. Hawapendi, tena pengine hawajafanya jambo la kuwafanya wahisiwe vibaya.




Mahojiano ya Maggid Mjengwa na Kwanza Production‏

Maggid Mjengwa
Karibu katika mazungumzo na mwanahabari makini na wa muda mrefu ambaye pia ni mmiliki wa Kwanza Jamii, Maggid Mjengwa kuhusu masuala mbalimbali ya uandishi, siasa, kama mwenendo wa Bunge Maalum la Katiba na mwenendo mzima wa nchi ya Tanzania.
Huu ni mfululizo wa mazungumzo na watu mbalimbali kuhusu masuala mbalimbali muhimu kwa mustakabali wa nchi za Afrika Mashariki
Karibu
Kwa maoni, tafadhali wasiliana nasi kwa barua pepe kwanzaproduction at gmail dot com

Tuesday, May 20, 2014

KUMBUKUMBU YA MAREHEMU BIBI YETU VALERIANA NGONYANI!!!

ILIKUWA MARA YANGU YA MWISHO

KUONANA NA BIBI 2005 MWEZI WA NNE
Leo ni tarehe 20/5 ni miaka tisa imepita tangu bibi yetu mpendwa Valeriana Ngonyani atutoke.  Kwangu ni kama vile jana tu. Alifariki 20/5/2005 katika hospitali ya Liuli. Sisi wajukuu wako wote, watoto wako ndugu na marafiki wote wanakukumbuka daima. Bibi Valeriana ni huyo aliyejifunika kitenge, katikati nadhani mnajua au basi ni mimi na mwishoni ni mama yangu mdogo, mdogo wake mama. TUTAKUKUMBUKA DAIMA KWA NJIA YA SALA ZETU. USTAREHE KWA AMANI AMINA.

Monday, May 19, 2014

JUMATATU YA LEO TUANZE NA CHANGAMOTO HII KUHUSU NCHI ZETU ZA AFRIKA!!!!

SWALI:- Je? ni nchi gani/zipi  haina/hazini  herufi A katika bara la Afrika?
NAWATAKIA KILA LA KHERI. PAMOJA DAIMA!!!

Saturday, May 17, 2014

MHASHAMU BABA ASKOFU MKUU MTEULE DAMIAN DENIS DALLU APOKEWA KWA SHANGWE SONGEA

Mhashamu Baba Askofu mkuu mteule Damian Denis Dallu akiwa kwenye gari la wazi kwa ajili ya kuwasabahi wakazi wa mkoa wa Ruvuma waliojitokeza barabarani ikiwa ni ishara ya upendo baada ya kupokelewa kijiji cha Lukumburu ambacho kipo mpakani kati ya mkoa wa Njombe na Mkoa wa Ruvuma

Thursday, May 15, 2014

PICHA YA WIKI:- SIJUI HAPA WANASUBIRI WATEJA AU....

...labda ni mashindano ya pikipiki..ila huyo mwenye sweta nyekundu sijui vipi na hilo panga?? Watoto bwana wana ubunifu sana..Nimependa sana hii:-) PAMOJA DAIMA!!

Wednesday, May 14, 2014

NI MUDA MREFU SASA UMEPITA :- METHALI ZETU....

Nimeona usipite muda zaidi bila kuzikumbuka METHALI  zetu basi ungana nami  katika hizi chache nilizozikumbuka leo:-

1. Aninyimaye mbaazi, kanipunguzua mashuzi
2. Biashara haigombi.
3. Chanda chema huvikwa pete.
4. Dua la kuku halimpati mwewe.
5. Fimbo ya mbali haiui nyoka.
6. Kikulacho ki nguoni mwako.
7. Kosa moja haliachi mke.
8. Lisilokuwepo moyoni halipo machoni.
9. Mapenzi ni kikohozi hayaweza kufichika.
10. Mficha uchi hazai.
BLOG YA MAISHA NA MAFANIKIO INAWATAKIENI WOTE SIKU NJEMA SANA NA WOTE MNAPENDWA:-)

Tuesday, May 13, 2014

MMMHHH! WAZEE WAMEZUIA NJIA....HAKUNA HARAKA NI ZAMU YETU!!!!!

Hii huwa inatokea sana katika barabara zinazopita katikati ya Mbuga za wanyama. Kwa wale wanaopita katika barabata za kuelekea Mikoani nadhani tunafahamu haya, mara kadha nimekutana na hii pale MIKUMI MBUGANI. Halafu hawana haraka wao kama vile ule msemo usemao HAKUNA HARAKA AFRIKA...Kaaaazi kwelikweli!!!!

Monday, May 12, 2014

HIVI UNADHANI UMELETWA DUNIANI KUFANYA NINI?

Mama Theresa: Alitoa kila alichokuwa nacho kwa ajili ya masikini.

 Nimeakuwa nikiwaza sana kuhusu huyu mama Therese, nikawa najiuliza hivi ile ndoto yangu ya kuwa sista  kama kweli ningefanikiwa je? ningekuwa kama yeye? au je yeye alikuwa hivyi kwa vile alikuwa kama alivyo? au je? kuna mtu mwingine tena kama Yeye? Kama tujuavyo mtu ukipata cheo, au kubahatika kuwa na hali nzuri. Huwa hawawajali kabisa wenzao lakini labda mafanikio yako ni kwababu yao kimalezi na mawazo. Kidogo ulicho nacho gawana na wenzako na Mungu atakujalia..... baadaye nikakumbuka nilisoma sehemu habari ya mama Theresa HAPA...Ebu msoma Mama Theresa.... 
-------------------------------------------------------------------------------------------------------
Maisha. Kila mmoja anaweza kuwa na fasihi yake kuhusu maisha. Wale wanao yafasihi maisha kwa kufuata mafundisho ya imani zao wana fasihi yao wanasayansi wana fasihi yao, na wengine wengi wana fasihi yao, huku pengine kila mmoja pia akiwa na fasihi yake.
Lakini swali hilo nalo je; binadamu amekuja hapa duniani kufanya nini? Huenda hili ndilo ambalo litapata majibu tofauti kupita kiasi. Litapata majibu tofauti kwa sababu kila mtu huamini au kudhani amekuja kuishi hapa duniani ili kutafuta ustawi. Kwa bahati mbaya ustawi wenyewe nao unapimwa kwa kiwango cha fedha na mali mtu alizozipata.

Hebu tujiulize wale wenye fedha kupindukia hawahangaiki hata kuliko wale ambao hawana hata senti ya kula kesho? Bila shaka ni kuwa wanahangaika sana. Hii ina maana kwamba kama binadamu angekuja hapa duniani ili kutafuta ustawi wa fedha na mali watu hawa wasingehangaika kiasi hiko kwani tayari wangekuwa wamepata hicho ambacho kimewaleta.
Kuhangaika kwao kuna maana kwamba binadamu hakuja hapa duniani kutafuta usitawi wa fedha au mali. Kama ni hivyo binadamu amekuja kutafuta kitu gani basi? Ni swali gumu sana na siyo wengi ambao wametafuta jibu wamefanikiwa kulipata.
Ili mtu aweze kujibu swali hili karibu na usahihi inambidi kwanza ajue yeye ni nani. Bila kujua yeye ni nani mtu hawezi kujua kwamba amekuja au kuletwa hapa duniani kufanya nini.
Kwa lugha rahisi na ya kawaida sana binadamu ni mwili na roho yake. Kazi ya mwili ni kuhifadhi roho yake yaani mawazo na uwezo wote unaotokana na kufikiri. Iwe ni kwa imani au sayansi. Binadamu anagawanyika rahisi sana kwa njia au maelezo hayo tu.
Binadamu huzaliwa kukua na badae kufa. Kama kifo ndiyo mwisho wa binadamu basi ni rahisi sana kusema binadamu amekuja hapa duniani kufanya nini lakini kama kifo siyo mwisho wa binadamu kuna ugumu kidogo katika kueleza lengo la binadamu hapa duniani.
Kama kifo ndiyo mwisho wa kuwepo binadamu ina maana kwamba binadamu anapaswa kujitazama kama mwili zaidi kuliko kama kitu kingine. Hii ni kwa sababu kufa kwa mwili wake kutakuwa na maana ya kumalizika kwake. Ukiacha imani inayotokana na mafundisho ya dini zetu wengi wetu huwa tunaamini kwamba binadamu ni mwili na anapokuwa amekufa huwa ndiyo mwisho wake. Imani hii hujitokeza sana kwenye matendo yetu.
Lakini ninavyofahamu mimi ni kwamba maisha ni zaidi ya mwili. Ni katika mkabala huo ambapo tunaamini kwamba binadamu hakuja hapa duniani kukamilisha majukumu ya kimwili na matamanio yake bali amekuja hapa duniani kwa sababu nyingine zaidi.
Wengi wetu tunaamini kwamba tumekuja hapa duniani kwa ajili ya kutafuta fedha pamoja na ‘kutanua’ tunaamini kwamba tumekuja hapa duniani kutafuta vyeo na kuwakanyaga wengine na tunaamini kwamba tumekuja hapa duniani kutafuta umaarufu. Lakini historia haituonyeshi hivyo haikubaliani na imani hiyo ingawa tunajaribu kuikumbatia isituponyoke.
Badala yake ingetakiwa kuanza kujiuliza maswali hayo; baada ya kupata mali na ‘kutanua’, baada ya kupata madaraka na kuwakanyaga wengine na baada ya kupata umaarufu halafu kitafuata kitu gani? Jibu ni rahisi kwamba kutafuata utupu. Ni wengi sana ambao walijidanganya kwamba wamekuja hapa duniani kutafuta vitu hivyo na baada ya kuvipata wakagundua kwamba sivyo walivyovifuata.
Kwa maelezo mafupi na ya moja kwa moja ni kwamba binadamu amekuja duniani kutoa. Kwenye imani ya dini nyingi inaelezwa kwamba binadamu amekuja hapa duniani kumwabudu Mungu. Kuabudu mana yake kufanya ibada na ibada ina maana ya matendo yetu yote mema kuanzia asubuhi tunapoamka hadi tunaporejea tena kitandani.
Binadamu ameletwa duniani kuifanya dunia kuwa mahali pazuri panapofaa mtu kuishi na baadae kuondoka akiwa ameiacha dunia ikiwa salama zaidi kwa wengine. Wale wote walioishi miaka 150 tu iliyopita wameondoka. Wengi wameondoka kama mawe yanavyoondoka kwa kubanduliwa na misukosuko ya jua na mvua, lakini wengine wameondoka na kuiacha dunia mambo ambayo yamefanya maisha yetu kuwa bora zaidi. Hawa ndiyo ambao wangefanya kile ambacho kimemleta binadamu hapa duniani.
Kila mtu anacho kitu cha kutoa. Lakini ni vigumu kwa mtu kuwa na cha kutoa kama mtu huyo hafanyi ibada, yaani hatendi mema. Kama mtu ametawaliwa na mwili ni vigumu kwake kutenda mema, hivyo kuwa vigumu kwake kujua kile ambacho kimemleta binadamu hapa duniani.
Ili kuthibitisha kwamba binadamu ameletwa hapa duniani kwa ajili ya kutoa unaweza kutoa kuanzia leo, hebu jaribu kutoa ili uone matokeo yake, toa kidogo katika ziada uliyonayo kwa wosia nayo, toa upendo kwa wanaoukosa, toa huruma kwa wanaohitaji toa chochote unachoweza kukitoa kwa wanaokihitaji. Bila shaka ukiweza kufanya hivyo, utagundua siri ni kwa nini binadamu aliletwa hapa duniani..

Sunday, May 11, 2014

JUMAPILI NJEMA KWA WOTE!!!

SWALI LA LEO:- Je? unamfahamu mwanadada huyu ?

Saturday, May 10, 2014

TAHADHARI :UGOMVI UNAATHIRI AFYA YAKO!!!


 
Wanaume wasio na ajira wako katika hatari ya kuathirika zaidi kutokana na ugomvi
 
Ugomvi wa mara kwa mara baina ya wapenzi, marafiki ama hata jamii unaongeza hatari ya kufa kwa watu wenye umri wa makamo. Haya ni kwa mujibu wa watafiti nchini Denmark.
Watafiti wamesema kuwa wanaume na wale ambao hawana kazi wako katika hatari Zaidi.
 
Utafiti huo katika jarida la 'Epidemiology and Community Health', unasema kuwa shughuli za kukidhi matakwa na mahitaji ya jamii pia zimehusishwa na idadi kubwa ya vifo vya mapema.
Pia kulingana na utafiti huo utu wa mtu na uwezo wa mtu binafsi kukabiliana na dhiki ilichangia katika matokeo ya utafiti huo.
Ingawa watafiti hao kutoka chuo kikuu cha Copenhagen waliweza kupata uhusiano uliopo kati ya vifo vya mapema na kugombana, na kuwa ugomvi uliongeza hatari ya vifo vya mapema mara tatu, hawakuweza kuelezea kikamilifu sababu haswa ya hali hiyo.
Utafiti wa hapo awali ulionyesha kuwa watu wenye wasiwasi mwingi na mahitaji mengi kutoka kwa wapenzi wao na watoto, pamoja na wale wanao gombana mara kwa mara na jamaa wao, wamo katika hatari kubwa zaidi ya kuugua magonjwa ya moyo na kiharusi.
Tafiti za hapo awali pia zaonyesha kuwa utangamano mwema na watu pamoja na marafiki wengi ina athari chanya katika afya, huku utu kwa kiasi kikubwa ukiamua jinsi mtu hupokea na kuguswa na hali za kijamii pamoja na mahusiano.

Wapendanao hawapaswi kugombana

Kumsumbua mpenzi wako pia kunahatarisha afya
Katika utafiti huu, watafiti walisema kuwa athari za kisaikolojia zinazosababishwa na dhiki, kama vile shinikizo la damu na ongezeko la athari ya magonjwa ya moyo, ndizo hasa zinaweza kueleza athari ya ongezeko la vifo vya mapema.
Utafiti umeonyesha kuwa wanaume wanapokabiliwa na hali za dhiki kwa kuongeza homoni inayokabiliana na hali ya dhiki na wasiwasi, jambo ambalo linazidisha athari ya kiafya.
Utafiti huo ulihusisha watu 9,875 wake kwa waume wenye umri wa kati ya miaka 36 na 52 na ulitumiwa kuchunguza uhusiano uliopo baina ya hali ngumu ya uhusiano wa kijamii na vifo vya mapema.
Wote walikuwa wameshiriki katika Utafiti ‘Denmark Longitudinal’ kuhusu Ajira, ukosefu wa ajira na afya , kuanzia mwaka wa 2000.
Utafiti uligundua kuwa wasiwasi wa mara kwa mara au mahitaji yanayotokana na wapenzi na watoto ulihusishwa na ongezeko la kufikia 50%- 100% la vifo vya mapema.
Ukosefu wa ajira ulionekana kuongeza athari hasi za uhusiano mgumu wa kijamii. Wale ambao hawako kazini wameonekana kuwa katika hatari kubwa zaidi ya kifo kutokana na jambo lolote kinyume na wale walio na kazi.
wanaume pia wako katika hatari zaidi kutokana na mahitaji na wasiwasi unaotokana na wapenzi wao wa kike , huku wakiwa katika hatari kubwa zaidi ya kifo zaidi ya ile ambayo kwa kawaida imehusishwa na kuwa mwanamume.
Dakta Rikke Lund, wa kitengo cha afya ya umma katika chuo kikuu cha Copenhagen amesema kuwa wasiwasi na ugomvi ni sehemu ya maisha. Lakini akaongeza kuwa watu ambao wanakuwa na migogoro mara kwa mara wako katika hatari zaidi lakini wanaweza wakasaidiwa.
CHANZO: BBC.

Thursday, May 8, 2014

WAGONJWA WA DENGUE WAFIKIA 376

Na Hudugu Ng'amilo
Homa ya dengue inaendelea kushika kasi nchini baada ya takwimu za Januari hadi juzi kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kuonyesha kuwa watu 376 wamekwishagundulika kuugua ugonjwa huo.
Mtaalamu wa Ufuatiliaji wa Magonjwa wa wizara hiyo, Dk Janeth Mugamba alisema hadi jana watu wawili walikuwa wamepoteza maisha, idadi ambayo alisema inaweza kuwa kubwa zaidi endapo upimaji utafanyika katika kila wilaya. "Pengine idadi inaweza kuwa kubwa zaidi kwa sababu wengi hawapimwi, Ijumaa (kesho) tutatoa, taarifa zaidi," alisema.
Alisema Wilaya ya Kinondoni ina wagonjwa wengi zaidi, ikifuatiwa na Ilala na Temeke. Hata hivyo, alisema huenda wilaya zenye idadi ndogo ya wagonjwa hazijaweza kupima na kubaini watu wenye maradhi hayo ikilinganishwa na Kinondoni.
Juzi, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid alisema hali ni mbaya na wananchi wanatakiwa kuchukua hadhari wasipate maambukizi ya ugonjwa huo.
Mtafiti wa malaria, tabia za mbu na mazingira, wa Taasisi ya Afya ya Ifakara, Dk Nicholas Govela alisema tayari wameshatuma maombi ya kufanya utafiti wa kina kuwajua mbu wanaoeneza homa ya dengue nchini. "Utafiti huu utasaidia kujua ni mbu kiasi gani wameathirika na virusi hivyo. Tukifanya hivyo tutajua ukubwa wa tatizo, tutajua wanapatikana wapi zaidi na virusi vyao vimetokea wapi," alisema.
Dk Govela alisema ni lazima utafiti huo ufanyike ili kudhibiti maambukizi zaidi ya homa hiyo akisema zipo sababu kadhaa zinazohisiwa kusababisha maradhi hayo, ikiwamo ya wahamiaji kuleta virusi hivyo vinavyosababisha homa hiyo na kuambukizwa kwa njia ya kuumwa na mbu.
"Ugonjwa huu umeenea zaidi nchi za Amerika ya Kusini na Kusini mwa Bara la Asia. Hapa kwetu mbu hawa walikuwapo lakini ugonjwa wa dengue haukuwapo kwa kiasi hiki, ndiyo maana sababu zinazohisiwa zaweza kuwa ni wahamiaji," alisema.
Alisema maambukizi ya homa ya dengue hutokea baada ya mtu mwenye ugonjwa huo kuumwa na mbu hao aina ya Aedes Egyptiae na mbu hao wakichukua virusi, huvisambaza kwa watu wengine. "Inawezekana tatizo ni kubwa zaidi ya hivi inavyofikiriwa kwa sababu wanaokuja hospitali kupimwa na kugundulika ni wachache, wengi wasiofika hawawezi kujulikana," alisema.
Makazi duni hatarini zaidi
Daktari Kiongozi na Mtaalamu wa homa ya dengue, Mrisho Rupinda alisema watu wanaoishi katika makazi duni wapo hatarini kuathiriwa zaidi kwa sababu ya kuwapo kwa taka nyingi na madimbwi.
Alitoa mfano wa wagonjwa wa kwanza wilayani Kinondoni, akisema walitokea maeneo ya Kambangwa, Mwananyamala Komakoma ambako kulikuwa na madimbwi na bwawa la maji.
"Wagonjwa wengi huonekana zaidi kwenye makazi duni kwa sababu ya mpangilio mbovu na kuzagaa kwa taka. Lakini pia maeneo mengine ambayo watu huhifadhi maji kwenye matenki au ndoo kwa muda mrefu bila kuyafunika," alisema.
CHANZO MWANANCHI

HADITHI HADITHI....LEO TUSIKILIZE HADITHI HII YA CHINDENDELE...!!!

Natumaini wote tunakumbuka maisha ya zamani kulikuwa hakuna vitabu na kwa kutaka kumbukumbu zote kuhifadhiwa basi mababu na mabibi zetu walikuwa wanatusimulia matukio yaliyotokea. Nilikuwa napenda sana kipindi kile cha mkusanyoko na bibi au babu anaposimulia hadithi...Lakini kuna wengine wamekuwa wavumbuzi na kuzihifhadhi baadhi ya hadithi hebu leo tusikilize hii hapa kutoka katika kitabu kiitwacho HADITHI NA VISA KUTOKA TANZANIA:-

Hii ni hadithi ya mvulana na dada yake. Dada alikuwa mzuri sana, na wavulana wengi walimuonyesha mapenzi yao na hamu yao ya kumuoa. Msichana hakumpenda hata mmoja wao.
Siku moja alitokea mwanamume mmoja ambaye hakuna aliyemtambua alikotokea. Huyu mtu alikuwa na heshima sana, mwenye sura nzuri na mwenye nguvu na afya. Msichana aliwaza: "Huyu ndiye mvulana ambaye nilikuwa nikimsubiri." Kwa hivyo aliamua hapo hapo kuolewa nae. Walikubaliana harusi ifanywe kwenye kijiji cha bwana harusi.
Kaka mtu wakati huo alikuwa akiumwa na pumu pamoja na ugonjwa wa ndui, kwa hivyo alikuwa mchafu sana . Msichana alimkwepa kutokana na hali yake . Mvulana alipoona dada yake ameamua kuolewa na kumfuata mumewe kijijini kwake ambacho hakuna aliyekijua, alimshauri dada yake kuwa yeye angewasindikiza. Lakini alimkatalia na akasema "Aa huwezi kuja kwa hali yako ilivyo. Umchafu na mgonjwa, utaniharibia bahati yangu bora ubaki!" Mvulana alimjibu " Aa, lazima nikufuate. Hujui unakokwenda. Humjui mtu ye yote nchi ngeni hiyo, labda utahitaji msaada."
Lakini msichana alikazania "Mvulana katika hali yako utawezaje kumsaidia mtu. Baki hapa, sitahitaji msaada wako!" "Haya dada safiri tu mie nitabaki". Baadaye dada mtu na mchumba wake waliondoka, kaka mtu aliwafuata. Alifanya bidii wasimuone. Kila walipopita sehemu wazi, alijificha na baadaye alikazana na kuwafikia tena. Aliwafuata huku wakiipita mito na milima  mpaka wakafika kijiji cha bwana harusi. Baada ya muda kidogo kaka mtu alijitokeza. "Habari  dada!  Unaniona nimekufuata njia nzima mpaka hapa!"
Dada alikasirika na akamwambia: " Kwa nini umenifuata? Nilikukataza usinifuate." Watu wa hicho kijiji walisema "Haya, madhali ameshafika hapa muache abakie." Wageni walipewa chakula kizuri ndizi, ugali na nyama pamoja na matunda ya kila aina kama embe, mananasi na mapapai. Walipomaliza kula walijihisi kuchoka sana, na walishikwa na usingizi hapo hapo.
Nchi waliokwenda ilikuwa na watu wengi, watu hao walikuwa wanyonge sana. Wote walikuwa kimya, karibu wote walikuwa hawazungumzi na wenzao. Karibu wote walikuwa watu wa ajabu ajabu. Watu katika sehemu hii walikuwa na tabia mbaya ya kula watu. Huyu msichana aliletwa hapa kwa madhumuni ya kuliwa. Kwanza apewe chakula mpaka anenepe na baadaye aliwe, sio kama mwenyewe alivyofikiri kuwa kaja hapa kuolewa na huyu mvulana! Alipofika tu alipewa chakula kingi sana.
Usiku wakati watu wote wamelala, walaji watu walimnyemelea kwenye kibanda ambacho msichana alilala. Walitaka kumuona jinsi alivyonenepa. Walikuja kila siku usiku kumuangalia. Mvulana alilala pamoja na dada yake kwenye hicho kiband. Hakuweza kulala vizuri kutokana a ugonjwa wake. Siku moja aliwasikia wala watu wakizungumza na kujadiliana kama msichana alikuwa kanenepa vya kutosha. Hawakukubaliana kabisa. Mmoja alisema: " Wacha tumle sasa hivi." Wapili alisema: "Aa  aa, wacha tusubiri kidogo wacha anenepe kidogo!"  Dada mtu hakusikia cho chote kwa sababu alilala usingizi mzuri katika kitanda kizuri.
Siku moja akasema  "Dada, ninakuonya, unawaelewa watu wanaoishi hapa...." Lakini dada mtu akamhamakia " kama nilivyotarajia, ndio maana sijataka kukuchukua. Nilielewa kuwa utawasema vibaya watu wa hapa, sitaki useme cho chote zaidi, unaelewa!" Mvulana alitikisa mabega na kuondoka.
Usiku uliofuata vitendo hivyo hivyo vilirejea. Siku iliyofuata mvulana akaona: " Lazima nimuambie dada yangu" Alimueleza kwa urefu na dada mtu alisikiliza kwa makini. Baada ya kumaliza, dada mtu alikataa kabisa kuamini. Mvulana aliendelea: "Kama  huniamini nitakuhakikishia," na aliendelea; " Nitakufunga uzi mwembamba kwenye kidole chako cha gumba, na leo usiku wakija, nitauvuta huo uzi kwa makini  kwa hivyo utaamka. lakini tahadhari usiamke na kuondoka kitandani! Nataka ufumbe macho tu na usikilize kwa makini halafu ndio utaamini haya ninayokueleza." Usiku ukafka. Msichana alilala vizuri kitandani kwake. kaka mtu alikaa macho na kuwasubiri hao wala watu wafike. Walifika na kuanza kujadiliana kama kawaida yao. Baadhi yao walitaka kumla hapo hapo, lakini wengine walisema "Wacha tusubiri, bado hajanenepa vya kutosha" Mvulana alifanya kama walivyoagana . Alivuta uzi kwa makini. Dada aliamka na kusikia mazungumzo ya wale watu. Baadhi yao walikuwa na majisu makubwa yaliyotiwa kwenye moto na yalikuwa mekunduu kwenye giza. Wengine walikuwa na mashoka, na wengine walikuja na vikapi vya kutilia nyama. Alielewa kuwa walikuwa tayari kumuua na kumkata vipande vipande! Aliogopa sana, walikuwa watu wa kutisha mno. Lakini alibaki kimya kama kaka mtu alivyomueleza. Alipumua baada ya hao watu kutokubaliana na kuondoka.
Walivyoondoka tu, alimuambia kaka yake: "Maneno yako ni kweli, nifanye nini? "Unaniuliza mimi"? Kaka alimjibu, "siku fikiria kuwa ulihitaji msaada wangu mie mwenye pumu na ndui! kwa nini humuulizi mchumba wako yeye atakusaidia!"
"Aa, sifikiri ndugu yangu mpenzi, lazima unisaidie, bila hivyo mie nitapotea!" Mvulana alimtuliza dada yake na klumuahidi kumsaidia. Asubuhi ma nampema wakati wote wamelala, mvulana alielekea shambani, na akaona majani manene ya mahindi. Aliyakata  kata na kutengeneza kizimba na kukileta kijijini. Yeye mwenyewe alijitia ndani ya kizimba hicho na huku akiimba:-
"Chindendele, ndendele, chindendele ndwaleje kumaangwetu ndendele. Ndwaleje kumaangwetu!"
"Kzimba, kizimba, kizimba nipeleke nyumbani kizimba. Nipeleke nyumbani"
Alivyokuwa akiimba kizimba kilianza kutembea na baadaye kuruka juu sana kwenye kijiji. Alivizuka mara nyingi vibanda vilivyokuweko chini na baadaye alishuka katikati ya mji. Alipokuwa akihakikisha kuwa mashini ilikuwa nzuri na wanakijiji walikuja kuangalia kitu gani kinafanyika.
Aliwaeleza uvumbuzi wake, na baadaye aliwaalika waruke nae. Hamna hata mmoja aliyemuamini. "Kijana sikiliza."  Walimueleza: "Upumbavu gani huo unaotueleza!" Kijana alikazania "kama hamniamini, wacha nikuhakikishieni. Kama mnaogopa kujaribu, wacha nijaribu na mbuzi pamoja na ng´ombe wenu. Walikubali na akachukua mbuzi watatu na ngómbe wawili kwenye kizimba. Aliingia mwenyewe ndani na akaanza kuimba.
"Kizimba, kizimba,kizimba. Nipeleke nyumbani, kizimba. Nipeleke nyumbani" Kizimba kikaruka hewani, na wakazi wa kijiji walikiona kizimba kikiruka kwenye vibanda vya kijiji. Kizimba kilipotua, walikubali kuwa kijana aliwaambia ukweli. Baadaye aliuliza kama kuna ye yote anataka kujaribu.Wazee wa kijiji pamoja na mchumba wa dada yake walikubali kujaribu na wakaruka kama alivyoruka mwanzo. Mvulana alikaa kwenye kizimba pamoja na wengine na kuanza kuimba hapo hapa kizimba kiliruka juu na kuzunguka kijiji chote.
Waliposhuka chini, wote waliobaki walitaka kujaribu, na mvulana akawaahidi kuwa kesho wataruka juu zaidi. Alielewa kuwa wale watu walipanga kumla dada yake siku inayofuata, lakini ilitokea kama alivyotarajia, wote walikuwa na hamu ya kuruka, na walisahau mambo yote mengine.
Asubuhi mapema, mvulana alikusanya ng´ombe, mbuzi, na ndege. Alichukua pia ndizi, mahindi na kadhalika na akavitia vyote kwenye kizimba na akawaeleza watu waliohudhuria:- "Leo tutaruka juu zaidi ya jana. Lakini kabla hatujaanza safari nitapendelea kujaribu na dada yangu pamoja na hivi vitu nilivyovitia ndani" Wote walikubaliana nae, na akaingia  ndani ya kizimba pamoja na dada yake na wakaanza wote wawili kuimba "CHINDENDELE"
Kizimba, kizimba, kizimba nipeleke nyumbanii, Kizimba nipeleke nyumbani."
Hapo hapo wakaanza kuruka, na naada ya muda waliiacha ardhi. Walipofika juu kiasi kaka mtu aligeuka, na kupiga makele: "Nyinyi wala watu! Haturejei chini tena. Asanteni kwa herini"
Waliruka na kuruka na baadaye walitua kwenye kijiji chao wenyewe. Hapo mvulana aliamuambia dada yake: "Unaona nilikuambia! Hukutaka kunisikiliza, ati kwa sababu mie mgonjwa. sasa unaona haya. Ningekusaidia, ungeliwa na watu hawa wa ajabu.
Dada aliona haya sana na akafahamu kuwa alivyofanya ilikuwa sio vizuri. Kuanzia siku hiyo alimpenda kaka yake ijapokuwa alikuwa mgonjwa.
Mambo mengi mtu anaweza kusoma kwa hadithi hii.
Kwanza: Wasichana wasiolewe na watu wasiowajua.
La pili: Mtu asichukie wagonjwa, bali awapende na kuwafikiria.
Hadithi hii pia inaeleza vipi watu wa afrika wanaamini aropleni ilivyogunduliwa kutokana na kizimba.

Wednesday, May 7, 2014

NIMEIPENDA PICHA HII..NA NDIYO BLOG YA MAISHA NA MAFANIKIO IMECHAGUA IWE PICHA YA WIKI!!

Nimependa jinsi walivyojipamba:-Nywele, vidani, na bila kusahau tabasamu/Mapozi na halafu ngozi zao nyororo. PAMOJA DAIMA!!

Tuesday, May 6, 2014

UKOSAPO NENO JEMA, KHERI UJINYAMAZIE.

Nakuasa usikie, usemaji ni karama,
Maneno usirukie, sema mambo kwa kupima,
Utamkapo ujue, neno halirudi nyuma,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Kheri ujinyamazie, ovu huleta khasama,
Majuto yasikujia, “Laiti nisingesema”,
Mtu baa azuae, Motowe utamchoma,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Ni wengi wajiponzao, kwa zao mbovu kalima,
Heshima waitakao, waseme usemi mwema,
Wale waumbukanao, ni kwa ndimi kuparama,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Watazame wakuao, dunia kuwatazama,
Ni wale wapimiao, kabla ya kuyasema,
Na kimya wanyamazao, wakosapo neno jema,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Neno huenda likuwe,lizidi hata vilima,
Mambo mawi liyazue, akili zende mrama,
Au mema yatukie, liwapo neno la wema,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Funzo walitufunzao, wazungupule wa zama
Zama za kale na leo, walokimcha Karima,
Yawe mema tusemao, tusije zusha zahama,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Mola akubarikie, na ambaye akusoma,
Na furaha ututie, uwe ni diwani njema,
Mema utuhadithie, wana kwa watu wazima,
Ukosapo neno jema, kheri ujinyamazie.

Shairi hili limetungwa na Mshairi maarufu Afrika Mashariki Bwana Amri Abedi, nami nimeona sio vibaya kulirejea ili tujifunze pamoja.................

Sunday, May 4, 2014

JUMAPILI YA LEO NIMETAMANI KWELIKWELI DAGAA WA ZIWA NYASA...NYUMBANI LUNDO

LUNDO:- Nimekumbuka sana leo, ugali wa mhogo, dagaa, kisamvu, matembele(mbwaka) bila kusahau samaki wa aina mbalimbali ndicho chakula kilichonikuza. Dagaa hawa ni watamu zaidi pale uwapatapo tu  yaani wabichi ..hasa lile wanaota (lighanda) ikiwa na maana zilizochomshwa na kukaushwa maji yote  usisahau chumvi na kapilipili kwa mbaliiii....Duh! najitesa bure hapa ngoje niache ila nitazile muda si mrefu Mungu akipenda:-)  JUMAPILI NJEMA!

Saturday, May 3, 2014

NGOMA ZA ASILI NDIZO NIZIPENDAZO.....JUMAMOSI NJEMA!!


Yaani hapa hata kama sielewi maneno yote lakin moyo unaridhika kabisa: Kama wehenga walivyosema ya kale ni dhahabu ni kweli kabisa. JUMAMOSI/JIONI NJEMA KWA WOTE. TUPO PAMOJA!!

Friday, May 2, 2014

HAPA NI TANZANIA LAKINI JE?UNAJUA HAPA NI WAP?

NAWATAKIENI WOTE MWISHO MWEMA WA JUMA. UKIPATA MUDA MSALIMIE RAFIKI YAKO MPENDWA AU TU JAMAA. KWANI KUKUMBUKANA NI JAMBO JEMA. IJUMAA YA KWANZA YA MWEZI MEI IWE NJEMA SANA KWA WOTE.......KAPULYA.