Thursday, September 20, 2012

KISA CHA KWELI !!!!


Nimetumiwa kisa hiki na msomaji wa Maisha na Mafanikio. Nikachukua muda na kusoma kwa kweli lazima niseme kisa hiki kimenigusa sana na nikaona kwamba msomaji huyu hajawa mchoyo kwangu kwanini mimi niwe mchoyo nimeona niweke hapa kibarazani ili wengi tujifunze maisha yalilivyo. KARIBUNI MUUNGANE NAMI.
................................................................................................................................................................
Ni siku nyingi kidogo, mwaka 1979, lakini ni tukio ambalo liliniuma sana. Ilikuwa vigumu sana kulisahau na lilinifanya nijiulize, inakuwaje Mungu anakuwa mkatili kiasi kile. Lakini bila shaka ilikuwa ni wakati ule wa ufahamu mdogo. Hivi sasa ninafahamu mengi na hasa baada ya kujifunza maarifa haya ya utambuzi.

Ilikuwa ni mwaka 1979 nikiwa nasafiri kutokea Dar es salaam kwenda Arusha. Sijui ilikuwaje, lakini ilitokea. Tuliondoka Dar es salaam saa 12.30 jioni. Wakati ule mabasi yalikuwa yakisafiri jioni na usiku, sio kama siku hizi.

Nilikuwa ninakwenda Arusha kwenye usaili kwa ajili ya ajira, nikiwa ndio kwanza nimemaliza kidato cha nne. Niliajiriwa moja kwa moja serikalini, kwani siku zile ajira zilikuwa ni za kumwaga. Hata hivyo sikuridhishwa na kazi niliyokuwa nafanya, hivyo niliomba kazi kwenye kampuni moja kule Arusha na niliitwa kwa usaili.

Tulifika mji unaoitwa Korogwe ambao wakati ule ulikuwa ndio mji maarufu kwa hoteli zake katika barabara yote ya Segera hadi Moshi na Arusha. Tulipofika Korogwe basi letu lilisimama kwa ajili ya abiria kupata chakula. Niliingia kwenye hoteli moja ambayo nakumbuka hadi leo kwamba ilikuwa ikiitwa Bamboo. Niliagiza chakula na kula haraka kutokana na muda mfupi wa kula uliotolewa na wenye basi la TTBS ambalo ndilo nililosafiri nalo.

Wakati wa kulipa ndipo niliposhangaa na kuogopa. Niliingiza mkono mifukoni na kukuta kwamba sikuwa na hela. Nilianza kubabaika na mwenye hoteli alisema hawezi kukubali ujinga huo, "Abiria wengine wahuni bwana, anakula na kujifanya kaibiwa, ukikubaliana nao kila siku hasara tu" Mwenye hoteli alisema kwa kudhamiria hasa.

Kulizuka zogo kubwa, huku mwenye hoteli akisema ni lazima anipeleke polisi. Ni kweli alimtuma mmoja wa watumishi wake kwenda kituo cha polisi ili nishughulikiwe……

Hapo Hotelini kulikuwa na bwana mmoja aliyekuwa amekaa pembeni na mkewe na watoto wao wakila. Yule bwana alipoona vile alimtuma mhudumu mmoja aniite. Niliondoka pale kaunta nilipokuwa nabembeleza na kuja kwa yule bwana.

Alikuwa ni kijana mtu mzima kidogo, mwenye miaka kama 50 hivi. Nilimsalimia na aliitikia, nilimsalimia mkewe pia. Yule bwana aliniuliza kisa cha vurugu ile na nilimsimulia. Aliniuliza sasa huko Arusha ningeishi vipi wakati wa usaili wakati nimeibiwa fedha zote na ningerudi vipi Dar. Nilimwambia nilikuwa napanga namna ya kurudi Dar, kama huko polisi ningeaminika.

Kama mzaha vile yule bwana aliniambia kuwa angenipa fedha za kutumia huko Arusha na nikirudi Dar nimrudishie fedha zake. Nakumbuka alinipa shilingi 90 kwa ahadi kwamba nikirudi Dar nimpelekee fedha zake ofisini kwake. Alinielekeza ofisini kwake, mtaa wa Nkuruma na kuniambia kuwa ameamua kunisaidia kwa sababu kila binadamu anahitaji msaada wa mwingine na maisha haya ni mzunguko. Nilimshukuru na kuondoka kukimbilia basini. Basi lilikuwa linanisubiri mimi tu. Nilipanda ndani ya basi na abiria wengine walinipa pole. Tuliondoka Korogwe, lakini haikuchukua muda basi letu lilipata tatizo la pancha ya gurudumu moja la mbele. Ilibidi tuegeshe pembeni ili litengenezwe. Baada ya matengenezo, tuliondoka kuendelea na safari yetu.

Karibu na mji wa Same kwenye saa saba usiku, basi letu lilisimama ghafla. Abiria walisimama ndani ya basi na kulizuka aina ya kusukumana. Huko nje kulikuwa na ajali. Abiria tulishuka haraka na wengine huko chini walishaanza kupiga mayowe, hasa wanawake. Niliposhuka niliona gari ndogo nyeusi ikiwa imebondeka sana na hapo kando kulikuwa na maiti wawili.

Nilijua ni maiti kwa sababu walikuwa wamefunikwa gubigubi. Halafu kulikuwa na katoto kalikokuwa kanalia sana kakiwa kamefungwa kanga kichwani. Tumwahishe huyu mtoto hapo Same hospitali ameumia, ingawa sio sana. Nilikatazama kale katoto ka kiume kenye umri wa miaka kama mitatu. Kalikuwa kameumie kwenye paji la uso, lakini kalikuwa hai. Bila shaka wale walikuwa ni wazazi wake, kalikuwa yatima tayari. Machozi yalinitoka.

Baada ya kupata msaada na askari wa usalama barabarani kuchukua maiti wale tulipanda basini kuendelea na safari yetu. Kale katoto kalichukuliwa na jamaa fulani waliokuwa na Land Rover ya serikali kukimbizwa hospitalini. Ndani ya Basi mazungumzo yalikuwa ni kuhusu ajali ile tu, hadi tunafika Arusha. Tulichelewa sana kufika Arusha kwani tulifika kwenye saa tano asubuhi, badala ya saa mbili .

Nililala kwenye hoteli rahisi na kufanya usaili kesho yake. Ni hiyo kesho, baada ya usaili niliponunua gazeti ambapo nilipata mshtuko mkubwa ajabu. Kumbe wale watu wawili waliokufa kwenye ajali ile ya Same walikuwa ni yule bwana aliyenisaidia hela na mkewe. Yule mtoto wao ndiye aliyeokoka. Niligundua hilo baada ya kusoma jina lake na jina la kampuni aliponiambia nimpelekee fedha zake nikirudi Dar, pamoja na picha yake, mke na mtoto. Nililia sana, kama mtoto.

Nillishindwa kujua ni kwa nini afe. Nilijiuliza ni nani sasa angemlea mtoto yule? Yalikuwa ni maswali yasiyo na majibu na pengine maswali ya kijinga pia.
Nilijua kwamba nilikuwa na deni, deni la shilingi tisini. Kwa wakati ule shilingi tisini zilikuwa ni sawa na shilingi laki moja za sasa.
Kwa mara ya kwanza sasa nilijiuliza ni kwa nini marehemu yule aliniamini nakuamua kunipa fedha zile. Sikupata jibu.

Nilikata kipande kile cha gazeti la kingereza kilichokuwa na habari ile. Nilichukuwa kipande hicho na kukiweka kwenye Diary yangu. Deni, Ningelipa vipi deni la watu? Nilijikuta nikipiga magoti na kuomba mungu anipe uwezo wa kuja kulilipa deni la mtu yule mwema kwa njia yoyote. 'Mungu naomba uje uniwezeshe kulilipa deni la marehemu kwa sura na namna ujuavyo wewe. Nataka kulilipa deni hili ili nami niwe nimemfanyia jambo marehemu,' niliomba. Nilirejea Dar siku hiyo hiyo.Kwa sababu ya mambo mengi na hasa baada ya matokeo ya usaili ule kuwa mbaya kwangu, nilijikuta nikiwa na mambo mengi na kusahau haraka sana kuhusu mtu yule aliyenisaidia mbaye ni marehemu. Nilifanikiwa hata hivyo kupata nafasi ya kusoma Chuo cha Saruji na baadae chuo cha ufundi na hatimaye nilibahatika kwenda nchini Uingereza. Mwaka 1991 nilianza shughuli zangu.

Ilikuwa ni mwaka 1995 nikiwa ofisini kwangu pale lilipokuwa jengo Nasaco ambalo liliungua mwaka 1996, ambapo lilijengwa upya na kubadilishwa jina na kuitwa Water Front. Nikiwa nafanya kazi zangu niliambiwa na sekratari wangu kwamba kulikuwa na kijana aliyekuwa anataka kuniona. Nilimuuliza ni kijana gani, akasema hamjui. Nilimwambia amruhusu aingie. Kijana huyo aliingia ofisini. Alikuwa ni kijana mdogo wa umri miaka kama 17 au 18 hivi, mweupe mrefu kidogo. Alikuwa amevaa bora liende , yaani hovyohovyo huku afya yake ikiwa hairidhishi sana.

Nilimkaribisha ilimradi basi tu, kwani niliona atanipotezea bure muda wangu. Ni lazima niwe mkweli kwamba sikuwa mtu mwenye huruma sana na nilikuwa naamini sana katika watu wenye pesa au majina. Nilimuuliza, “nikusaidie nini kijana na ukifanya haraka nitashukuru maana nina kikao baada ya muda mfupi”. Nilisema na sikuwa na kikao chochote , lakini nilitaka tu aondoke haraka.

“Samahani mzee, nilikuwa na shida…..nimefukuzwa shule na sina tena mtu wakunisaidia kwa sababu …..nime….niko ….kidato cha pili na hivyo tu natafuta tu kama atatokea mtu……..
Nilimkatisha. “Sikiliza kijana. Kama huna jambo lingine la kusema, ni bora ukaniacha nifanye kazi. Hivi unafikiri kama nikiamua kumsaidia kila mtu aliyefukuzwa shule si nitarudi kwetu kwa miguu! Nenda Wizara ya Elimu waambie……Kwanza wazazi wako wanafanya kitu gani, kwa nini washindwe …..Kwa nini walikupeleka shule ya kulipia kama hawana uwezo, wanataka sifa?”

“Hapana wazazi wangu walikufa na ninasoma shule ya serikali. Nimekosa mahitaji ya msingi na nauli ya kwendea shule. Nasoma shule ya Kwiro, Morogoro. Shangazi ndiye anayenisomesha, naye ana kansa na hivi sasa hata kazi hafanyi….,” Alianza kulia. Huruma fulani ilinijia na nilijiambia, kama ni nauli tu na matumizi, kwa nini nisiwe mwema, angalau kwa mara moja tu. “Baba na mama walifariki lini?” Niliuliza nikijua kwamba, watakuwa wamekufa kwa ukimwi, maana kipindi kile ndipo fasheni ya ukimwi ilipoanza, ambapo kila anayekufa huhesabiwa kwamba kafa kwa ukimwi.

“Walikufa kwa ajali nilipokuwa mdogo sana, nilipokuwa na miaka mitatu. Ndio shangazi yangu akanichukua na kunilea hadi sasa anakufa kwa kansa.” Yule kijana alilia zaidi. Naomba nikwambie wewe msomaji unayesoma hapa kwamba, kuna nguvu fulani na sasa naamini kwamba ziko nyingi ambazo huwa zinaongoza maisha yetu bila sisi kujua.

Kitu fulani kilinipiga akilini paaa! Nilijikuta namuuliza yuel kijana. “Kwa nini umeamua kuja kwangu, ni nani alikuelekeza hapa na wazazi wako walikufa mwaka gani na wapi?”
Yule kijana alisema, “Nimeona nijaribu tu kwa mtu yeyote ambaye anaweza kunisaidia, na ndio nimejikuta nikiingia hapa, sijui……..sikutumwa na mtu. Wazazi wangu walikufa mwaka 1979 huko Same na mimi wanasema nilikuwa kwenye ajali, nikaokoka. Niliumia tu hapa.” Alishika kwenye kovu juu ya paji lake la uso.

Nilihisi kitu fulani kikipanda tumboni na kuja kifuani halafi niliona kama vile nimebanwa na kushindwa kupumua. “Baba yako alikuwa anaitwa nani?” “Alikuwa anaitwa Siame….Cosmas Siame….” Niliinuka ghafla hadi yule kijana alishtuka . Nilikwenda kwenye kabati langu mle ofisini na kuchakura kwenye droo moja na kutoka na diary. Mikono ikinitetemeka, nilitoa kipande cha gazeti ndani ya diary hiyo, nilichokuwa nimekihifadhi.

“Ndio alikuwa anaitwa Cosmas Siame. Huyu ni mtoto wake, ni yule mtoto aliyenusurika.” Nilinong’ona. Nilijikuta nikipiga magoti na kusali. “Mungu, wewe ni mweza na hakuna kinachokushinda. Nimeamini baba kwamba kila jema tunalofanya ni akiba yetu ya kesho na kesho hiyo huanzia hapa duniani.” Halafu nillinyamaza na kulia sana. Nililia kwa furaha na ugunduzi wa nguvu zinazomgusa binadamu kwa kila analofanya.

Nilisimama nikiwa nimesawajika kabisa. Nilihisi kuwa mtu mwingine kabisa. Nilimfuata yule kijana na kumkumbatia huku nikiwa bado ninalia. “Mimi ni baba yako mdogo, ndiye nitakyekulea sasa. Ni zamu yangu sasa kukulea hadi mwisho” Naye alilia bila kujua sababu na alikuwa amechanganyikiwa kabisa. Nilirudi kwenye kiti na kumsimulia kilichotokea miaka 17 iliyopita.

Tuliondoka hapo na kwenda kumwona shangazi yake Ubungo, eneo la maziwa ambako alikuwa amepanga chumba. Kutokana na hali yake nilimhamishia kwangu, baada ya kumsimulia kilichotokea. Huyo dada yake Cosmas alifurahi sana hadi akashindwa kuzungumza kwa saa nzima. Alifariki hata hivyo mwaka mmoja baadae, lakini akiwa ameridhika sana.

Kijana Siame alisoma na kumaliza Chuo Kikuu na hivi sasa yuko nchini Australia anakofanya kazi. Ukweli ni kwamba ni mwanangu kabisa sasa. Naamini huko waliko Mbinguni wazazi wake wanafurahia kile walichokipanda miaka mingisana nyuma. Lakini nami najiuliza bado. Ilikuwaje Cosmas akanipa msaada ule? Halafu najiuliza ni kitu gani kilimvuta mwanae Siame hadi ofisini kwangu akizipita ofisi nyingine zote? Nataka nikuambie, usiwe mbishi sana bila sababu, kuna nguvu za ziada zinazoongoza matokeo maishani mwetu…………

*************MWISHO*********

22 comments:

John Mwaipopo said...

ni hadithi nzuri sana. hakika inasisimua na ina mafundisho pia. kingine katika hadithi hii ni matumizi ya kiswahili. mwandishi amekitendea haki kiswahili.

Anonymous said...

kwanza habari ya asubuhi dada Yasinta hiki kisa niliwahi kukisoma kwenye gazeti la Jitambue na wala sio kisa ni kweli ila hapo tukumbuke kwamba wema hauozi na nguvu kweli ni nyingi ukipanda pando jema nikweli utavuna wema na mambo mengine yanatokea ilikusudi sisi wengine tujifunze kutoka hapo ahsante na mchana mwema vile vile pamoja nilishawahi kukisoma nimekisoma leo na bado machozi yamenitoka ya furaha

Anonymous said...

Hii stori imefanya niamini kuwa Mungu wetu yupo pamoja nasi , huwa anajibu maombi yetu pale tuombapo tukimaanisha, Tulilofumbwa ni lini na wakati gani ombi letu litajibiwa ,kumbuka mhusika aliomba mungu amsaidie kulipa lile deni na akamuachia mungu amtafutie jinsi ya kulilipa. Na mungu akatimiza lile aliloombwa kwa muda husika. Ubalikiwe na bwana kwa kumsomesha huyo kijana

Rafikio wa hiari said...

Rafiki yangu hadithi hii imenigusa mpaka nimedondosha machozi. Marehemu baba yangu alikua ananisisitizia daima kutenda mema bila kuchoka na bila kusubiri shukrani na kujaribu kutokuumiza hisia za mwenzako kwa kukusudia huwezi jua jema lako la leo litakuja kumusadidia nani mbeleni. Na hili limejitokeza kwa baba huyu kumuamini kijana huyu wa 1979 bila kusita.
Pia hapa nimejifunza ukiomba kwa Mungu anakupa majibu sawa sawa na mapenzi yake na katika wakati ambao ni muafaka - tumeona jinsi babake mdogo Siame alivyomuomba Mungu kurudisha wema wa mzee yule, asingesikiliza au asingemuamini Mungu angejikuta akikimbilia hospitali kumuuguza yule mtoto halafu baaasi akakung'uta mikono na kusema amemaliza kazi - kumbe la hasha hitaji la mtoto yule Mungu alikwisha jua litakua lini na ndio hata akamuongoza kwa baba mdogo. Nimebarikiwa sana Rafiki yangu Yasinta kwa hadithi hii nashukuru kwa kuileta jamvini kwako. Siku njema, salamu kwa familia.

ray njau said...

@Yasinta;
Hii stori imenikumbusha mambo kadhaa na machozi yanatiririka kutoka moyoni.Kwa mwaka huo Sh.90.00 ilikuwa nauli ya kutoka Dar es salaam hadi Moshi.

ISSACK CHE JIAH said...

UKWELI DADA HII STORI IMENIBURUDISHA NA NIMEISAMBAZA KWA WATU KIBAO ,UKWELI NIMEIPENDA SANA NA KWAKWEIL MAISHA NI NJIA PANDA NA HASA UKIZINGATIA KUWA SISI BINADAMU NI WASAHAULIFU ,TAYARI JAMAA ALISHA MDHARAU YULE KIJANA KUMBE MIMI NAONA NI MALAIKA KAINGIA OFISINI KWAKE ,UKWELI BINADAMU TUBADILIKE TUSIWE KAMA WANYAMATUJUE NINI TUNACHOFANYA KATIKA KUWAPOKEA WAGENI TUSIO WAJUWA NISALIMIE MBOGO NA MWANANGU RECHEL
CHe Jiah

Anonymous said...

hii stori imenifariji sana asnte kwa aliye andika pia imenikumbusha jambo ambalo nataka kulipa fadhila

Baba Mbembe said...

Imenibamba sana hii hadithi hadi natamani kusikia na upande wa kijana anasema nini.
Mungu aliamua kuonesha uwezo kwa huyo baba mdogo wa kuhiari

Anonymous said...

Hii habari inaanza na kusikitisha na mwisho wake unafurahisha kwa kuwa kijana siame ameweza kusoma na kufanikiwa kupata kazi nje. Mungu ni mwema sana hasa kwa wale wamtumainio. Ni fundisho kwetu tunaoishi hapa duniani, je tunawasaidiaje wenye matatizo? je ni ubinafsi tu wa kuwa pesa hizi na mali ni vyangu na wanangu tu? je watu tusiowafahamu kabisa wakiwa kwenye tabu tunawasaidia? haya ni baadhi ya maswali machache ya mimi na wewe kujiuliza. Asante sana Yasinta kuileta hii habari hapa mie ni mara ya kwanza kuisoma, ntaisambaza kwa wengine pia. Ubarikiwe.

Anonymous said...

kijana siame kama unasoma hii blog ya da yasinta, tungependa kukusikia.

Anonymous said...

- Remember then: there is only one time that is important.That time is NOW! It is the most important time because it is the only time when we have any power. The most necessary man is he with whom you are, for no man knows whether he will ever have dealings with anyone else: and the most important affair is, to do him good, because for that purpose alone was man sent into this life !

ISSACK CHE JIAH said...

tunaomba dada Yasinta leo ufunge mjadala huu kwa kusema chochote
CHe Jiah

sam mbogo said...

Pia mimi chozi limenitoka,sijuwi nazeeka vibaya,machozi yako karibu sana sikuhizi. simulizi hii nifundisho maana binaadam tuko tofauti,tunapo patwa nashida hasa inayo husu pesa huwa tunakuwa na mitazamo tofauti na wakati mwingine inakuwa ni ya kikibinafsi sana.hupenda kuhukumu mtu bila kujuwa undani wake.na tukio kama hili kwa miaka ile waungwana walikuwa wengi,miaka ya sasa ni vigumu kumjuwa nani anashida ya kweli. ndugu yangu che mi mzima nafikiri hata binti yako yuko safi,nilikuwa bongo ila sikuweza kuku tafuta,samahani kwa hilo,ipo siku tutaonana tu. kaka s

Yasinta Ngonyani said...

Nawashukuruni wote kwa kuungana nami katika habari hii. Binafsi imenigusa sana. Ni kweli inasisimua na inasikitisha lakini kila mtu aliyesoma hii amejifunza kitu. Pia umewafanya wengi wafikirie ...Ama kweli ukiomba unapata lakini pia inategemea iunaombaje na una imani yaani imani na Mungu.Asante aliyeandika habari hii.Maana wengi tumefaidika

Rachel Siwa said...

Meeeengi yameshasemwa, nami niongezee tuu;Tumrudishie MUNGU UTUKUFU!!!!!!

BABA Yangu CHE JIAH,Nashukuru sana kwa kutukumbuka ujumbe wako nimeupata ndugu yangu, ipo siku tutaonana.

Sam mwana wa Mbogo sisi tunaendelea vyema,Natumai nanyi pia.

Asante KADALA na Wachangiaji wooote tunazidi kujifunza.

gadiel mgonja said...

Hahabari za asubuhi DADA?ahsante sana kwa kuona kua huu ujumbe ni wa mhim na ukaona kua n vzur wafaidike na wengne.waandish wa biblia walivyo andika kua upendo ni msingi wa maisha waliona mbali sana kwani faida yake hamna kinachoipita,tusaidianeni bli kujal huyu na nani,ananini,au anahadhi gani, na nikimsaidia ntapata nn,heri mkono unaotoa kuliko ule ambao cku zote unapokea tu,asante ubarikiwe na bwana.

Anonymous said...

eehh jamani dada Yasintha hii habari inatia huzuni sana na at the end inafurahisha.nimelia jamani as i was reading.Mungu anamaajabu yake.maajabu ya mungu yanatokea kila siku.unaweza ujiulize maswali kama huyu kaka.
Naye ni mtu mzuri tu kurudisha fadhila zile jamani hebu ona jinsi mungu anavyofanya kazi yake.
Mungu ashukuriwe sana.
mlongo.

Anonymous said...

KWA KWELI,WEMA HAUOZI.NA TENDA WEMA WENDE ZAKO USINGOJE SHUKRANI.

jennie said...

kweliwema ni akiba na ubaya pia ni akiba.

Unknown said...

hama kweli mwema hauozi. na pia tumkumbe Allah kwani ana uwezo.mimi nina furaha kubwa sana. kwani milima kwa milima haikutani bali binaadamu hukutana nakytakia maisha mema

Anonymous said...

Hii story ya mda Sana lakini haitakuja kupungua makali siku zote

Anonymous said...

Vizuri sana nimefurahi