Thursday, May 8, 2014

HADITHI HADITHI....LEO TUSIKILIZE HADITHI HII YA CHINDENDELE...!!!

Natumaini wote tunakumbuka maisha ya zamani kulikuwa hakuna vitabu na kwa kutaka kumbukumbu zote kuhifadhiwa basi mababu na mabibi zetu walikuwa wanatusimulia matukio yaliyotokea. Nilikuwa napenda sana kipindi kile cha mkusanyoko na bibi au babu anaposimulia hadithi...Lakini kuna wengine wamekuwa wavumbuzi na kuzihifhadhi baadhi ya hadithi hebu leo tusikilize hii hapa kutoka katika kitabu kiitwacho HADITHI NA VISA KUTOKA TANZANIA:-

Hii ni hadithi ya mvulana na dada yake. Dada alikuwa mzuri sana, na wavulana wengi walimuonyesha mapenzi yao na hamu yao ya kumuoa. Msichana hakumpenda hata mmoja wao.
Siku moja alitokea mwanamume mmoja ambaye hakuna aliyemtambua alikotokea. Huyu mtu alikuwa na heshima sana, mwenye sura nzuri na mwenye nguvu na afya. Msichana aliwaza: "Huyu ndiye mvulana ambaye nilikuwa nikimsubiri." Kwa hivyo aliamua hapo hapo kuolewa nae. Walikubaliana harusi ifanywe kwenye kijiji cha bwana harusi.
Kaka mtu wakati huo alikuwa akiumwa na pumu pamoja na ugonjwa wa ndui, kwa hivyo alikuwa mchafu sana . Msichana alimkwepa kutokana na hali yake . Mvulana alipoona dada yake ameamua kuolewa na kumfuata mumewe kijijini kwake ambacho hakuna aliyekijua, alimshauri dada yake kuwa yeye angewasindikiza. Lakini alimkatalia na akasema "Aa huwezi kuja kwa hali yako ilivyo. Umchafu na mgonjwa, utaniharibia bahati yangu bora ubaki!" Mvulana alimjibu " Aa, lazima nikufuate. Hujui unakokwenda. Humjui mtu ye yote nchi ngeni hiyo, labda utahitaji msaada."
Lakini msichana alikazania "Mvulana katika hali yako utawezaje kumsaidia mtu. Baki hapa, sitahitaji msaada wako!" "Haya dada safiri tu mie nitabaki". Baadaye dada mtu na mchumba wake waliondoka, kaka mtu aliwafuata. Alifanya bidii wasimuone. Kila walipopita sehemu wazi, alijificha na baadaye alikazana na kuwafikia tena. Aliwafuata huku wakiipita mito na milima  mpaka wakafika kijiji cha bwana harusi. Baada ya muda kidogo kaka mtu alijitokeza. "Habari  dada!  Unaniona nimekufuata njia nzima mpaka hapa!"
Dada alikasirika na akamwambia: " Kwa nini umenifuata? Nilikukataza usinifuate." Watu wa hicho kijiji walisema "Haya, madhali ameshafika hapa muache abakie." Wageni walipewa chakula kizuri ndizi, ugali na nyama pamoja na matunda ya kila aina kama embe, mananasi na mapapai. Walipomaliza kula walijihisi kuchoka sana, na walishikwa na usingizi hapo hapo.
Nchi waliokwenda ilikuwa na watu wengi, watu hao walikuwa wanyonge sana. Wote walikuwa kimya, karibu wote walikuwa hawazungumzi na wenzao. Karibu wote walikuwa watu wa ajabu ajabu. Watu katika sehemu hii walikuwa na tabia mbaya ya kula watu. Huyu msichana aliletwa hapa kwa madhumuni ya kuliwa. Kwanza apewe chakula mpaka anenepe na baadaye aliwe, sio kama mwenyewe alivyofikiri kuwa kaja hapa kuolewa na huyu mvulana! Alipofika tu alipewa chakula kingi sana.
Usiku wakati watu wote wamelala, walaji watu walimnyemelea kwenye kibanda ambacho msichana alilala. Walitaka kumuona jinsi alivyonenepa. Walikuja kila siku usiku kumuangalia. Mvulana alilala pamoja na dada yake kwenye hicho kiband. Hakuweza kulala vizuri kutokana a ugonjwa wake. Siku moja aliwasikia wala watu wakizungumza na kujadiliana kama msichana alikuwa kanenepa vya kutosha. Hawakukubaliana kabisa. Mmoja alisema: " Wacha tumle sasa hivi." Wapili alisema: "Aa  aa, wacha tusubiri kidogo wacha anenepe kidogo!"  Dada mtu hakusikia cho chote kwa sababu alilala usingizi mzuri katika kitanda kizuri.
Siku moja akasema  "Dada, ninakuonya, unawaelewa watu wanaoishi hapa...." Lakini dada mtu akamhamakia " kama nilivyotarajia, ndio maana sijataka kukuchukua. Nilielewa kuwa utawasema vibaya watu wa hapa, sitaki useme cho chote zaidi, unaelewa!" Mvulana alitikisa mabega na kuondoka.
Usiku uliofuata vitendo hivyo hivyo vilirejea. Siku iliyofuata mvulana akaona: " Lazima nimuambie dada yangu" Alimueleza kwa urefu na dada mtu alisikiliza kwa makini. Baada ya kumaliza, dada mtu alikataa kabisa kuamini. Mvulana aliendelea: "Kama  huniamini nitakuhakikishia," na aliendelea; " Nitakufunga uzi mwembamba kwenye kidole chako cha gumba, na leo usiku wakija, nitauvuta huo uzi kwa makini  kwa hivyo utaamka. lakini tahadhari usiamke na kuondoka kitandani! Nataka ufumbe macho tu na usikilize kwa makini halafu ndio utaamini haya ninayokueleza." Usiku ukafka. Msichana alilala vizuri kitandani kwake. kaka mtu alikaa macho na kuwasubiri hao wala watu wafike. Walifika na kuanza kujadiliana kama kawaida yao. Baadhi yao walitaka kumla hapo hapo, lakini wengine walisema "Wacha tusubiri, bado hajanenepa vya kutosha" Mvulana alifanya kama walivyoagana . Alivuta uzi kwa makini. Dada aliamka na kusikia mazungumzo ya wale watu. Baadhi yao walikuwa na majisu makubwa yaliyotiwa kwenye moto na yalikuwa mekunduu kwenye giza. Wengine walikuwa na mashoka, na wengine walikuja na vikapi vya kutilia nyama. Alielewa kuwa walikuwa tayari kumuua na kumkata vipande vipande! Aliogopa sana, walikuwa watu wa kutisha mno. Lakini alibaki kimya kama kaka mtu alivyomueleza. Alipumua baada ya hao watu kutokubaliana na kuondoka.
Walivyoondoka tu, alimuambia kaka yake: "Maneno yako ni kweli, nifanye nini? "Unaniuliza mimi"? Kaka alimjibu, "siku fikiria kuwa ulihitaji msaada wangu mie mwenye pumu na ndui! kwa nini humuulizi mchumba wako yeye atakusaidia!"
"Aa, sifikiri ndugu yangu mpenzi, lazima unisaidie, bila hivyo mie nitapotea!" Mvulana alimtuliza dada yake na klumuahidi kumsaidia. Asubuhi ma nampema wakati wote wamelala, mvulana alielekea shambani, na akaona majani manene ya mahindi. Aliyakata  kata na kutengeneza kizimba na kukileta kijijini. Yeye mwenyewe alijitia ndani ya kizimba hicho na huku akiimba:-
"Chindendele, ndendele, chindendele ndwaleje kumaangwetu ndendele. Ndwaleje kumaangwetu!"
"Kzimba, kizimba, kizimba nipeleke nyumbani kizimba. Nipeleke nyumbani"
Alivyokuwa akiimba kizimba kilianza kutembea na baadaye kuruka juu sana kwenye kijiji. Alivizuka mara nyingi vibanda vilivyokuweko chini na baadaye alishuka katikati ya mji. Alipokuwa akihakikisha kuwa mashini ilikuwa nzuri na wanakijiji walikuja kuangalia kitu gani kinafanyika.
Aliwaeleza uvumbuzi wake, na baadaye aliwaalika waruke nae. Hamna hata mmoja aliyemuamini. "Kijana sikiliza."  Walimueleza: "Upumbavu gani huo unaotueleza!" Kijana alikazania "kama hamniamini, wacha nikuhakikishieni. Kama mnaogopa kujaribu, wacha nijaribu na mbuzi pamoja na ng´ombe wenu. Walikubali na akachukua mbuzi watatu na ngómbe wawili kwenye kizimba. Aliingia mwenyewe ndani na akaanza kuimba.
"Kizimba, kizimba,kizimba. Nipeleke nyumbani, kizimba. Nipeleke nyumbani" Kizimba kikaruka hewani, na wakazi wa kijiji walikiona kizimba kikiruka kwenye vibanda vya kijiji. Kizimba kilipotua, walikubali kuwa kijana aliwaambia ukweli. Baadaye aliuliza kama kuna ye yote anataka kujaribu.Wazee wa kijiji pamoja na mchumba wa dada yake walikubali kujaribu na wakaruka kama alivyoruka mwanzo. Mvulana alikaa kwenye kizimba pamoja na wengine na kuanza kuimba hapo hapa kizimba kiliruka juu na kuzunguka kijiji chote.
Waliposhuka chini, wote waliobaki walitaka kujaribu, na mvulana akawaahidi kuwa kesho wataruka juu zaidi. Alielewa kuwa wale watu walipanga kumla dada yake siku inayofuata, lakini ilitokea kama alivyotarajia, wote walikuwa na hamu ya kuruka, na walisahau mambo yote mengine.
Asubuhi mapema, mvulana alikusanya ng´ombe, mbuzi, na ndege. Alichukua pia ndizi, mahindi na kadhalika na akavitia vyote kwenye kizimba na akawaeleza watu waliohudhuria:- "Leo tutaruka juu zaidi ya jana. Lakini kabla hatujaanza safari nitapendelea kujaribu na dada yangu pamoja na hivi vitu nilivyovitia ndani" Wote walikubaliana nae, na akaingia  ndani ya kizimba pamoja na dada yake na wakaanza wote wawili kuimba "CHINDENDELE"
Kizimba, kizimba, kizimba nipeleke nyumbanii, Kizimba nipeleke nyumbani."
Hapo hapo wakaanza kuruka, na naada ya muda waliiacha ardhi. Walipofika juu kiasi kaka mtu aligeuka, na kupiga makele: "Nyinyi wala watu! Haturejei chini tena. Asanteni kwa herini"
Waliruka na kuruka na baadaye walitua kwenye kijiji chao wenyewe. Hapo mvulana aliamuambia dada yake: "Unaona nilikuambia! Hukutaka kunisikiliza, ati kwa sababu mie mgonjwa. sasa unaona haya. Ningekusaidia, ungeliwa na watu hawa wa ajabu.
Dada aliona haya sana na akafahamu kuwa alivyofanya ilikuwa sio vizuri. Kuanzia siku hiyo alimpenda kaka yake ijapokuwa alikuwa mgonjwa.
Mambo mengi mtu anaweza kusoma kwa hadithi hii.
Kwanza: Wasichana wasiolewe na watu wasiowajua.
La pili: Mtu asichukie wagonjwa, bali awapende na kuwafikiria.
Hadithi hii pia inaeleza vipi watu wa afrika wanaamini aropleni ilivyogunduliwa kutokana na kizimba.

1 comment:

Yasinta Ngonyani said...

HADITHI hii imenigusa mno na hii ni zaidi ya hadithi kwani hii imekwisha tokea mara nyingi tu kwa wengi tu. Ila sio kuliwa lakini mateso ya aina mbalimbali katika ndoa. Wasichana/wanawake tuwe makini tusiwe na hamaki.