Wednesday, March 5, 2014

RABIA: MALARIA IMENIFANYA NIWE MWALIMU MLEMAVU WA KUSIKIA...

Katika pitapita zangu nikakutana na habari hii ambayo imenigusa sana na nimeona niwashirikishe kama mlikuwa hamjaisoma basi chukua dakika chache na tujadili kwa pamoja...KARIBUNI...
Mwalimu Rabia Abdallah
“Mwaka 1996 hadi 1998, nikiwa nasoma chuo cha ualimu Korogwe mkoani Tanga, nilidharaulika sana na kuonekana kama kituko kwa baadhi ya walimu na wanafunzi, huku wengine wakishangazwa nami kwa jinsi nilivyoweza kumudu masomo yangu wakati sina uwezo wa kusikia,’’ ndivyo anavyoanza Rabia Abdallah (34) ambaye alikuwa mwalimu wa shule ya viziwi Buguruni akielezea jinsi matatizo ya kusikia yalivyomfanya aonekane kituko wakati alipokuwa akisoma.
Anasema jinsi alivyokuwa akisoma ni Mungu tu ndiye aliyekuwa akimsaidia kwani hakuwa akisikia chochote zaidi ya kusoma vitabu baada ya walimu kumaliza kufundisha na njia hiyo ya kusoma vitabu ndiyo iliyomwezesha kushinda mitihani yake na kufanikiwa kutunukiwa Diploma yake ya Ualimu.
“Wengi hawakuamini na walifikiri naigiza lakini wengine waliamini lakini hawakuweza kunisaidia kwa kuwa hakuna aliyekuwa akiweza kuzungumza kwa ishara kwani hata mimi mwenyewe sikuweza kuwasiliana kwa ishara kwa wakati huo, hivyo maisha ya masomo pale Korogwe yalikuwa magumu mno kwa upande wangu…,’’
anasema Mwalimu huyo ambaye hivi karibuni amepokea barua ya uhamisho ikimtaka kuhamia katika darasa maalumu la wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia (viziwi) katika shule ya msingi Temeke. Rabia kwa sasa ana watoto wawili, anasema alifikiri kuwa kupata Diploma kungekuwa mwisho wa matatizo yake kumbe ndiyo kwanza matatizo yalizidi kuongezeka, kwani baada ya hapo alikumbana na tatizo la kupata kazi kwani kila alikoomba kazi ya kufundisha alikataliwa kwa kutokana na matatizo yake ya kusikia.
“Tatizo liliibuka upya nikaanza kudharaulika tena kila nilipokuwa nikiomba kazi kwani waliniita kiziwi nisiye na uwezo wa kufanya lolote na walishangaa ilikuwaje nimepewa Diploma wakati ninamatatizo hayo, waliamini kuwa mwenye matatizo ya kusikia hawezi kusoma tena maishani mwake,’’ anasema Rabia.
“Hapo nikalazimika kuomba kazi za kawaida ambapo nilipata kazi ya muda katika taasisi ya CCBRT ambapo nilifanya hapo kwa muda wa miaka mitano kuanzia mwaka 2000 hadi 2005, nikaona tangazo la kazi kwenye gazeti, likieleza kuwa manispaa ya Ilala inataka mwalimu wa kufundisha walemavu wa kusikia katika shule ya Buguruni Viziwi, nikaomba na nilipokubaliwa nikaacha kazi CCBRT,’’ anasema Rabia.
Anasema hata hivyo haikuwa rahisi kama alivyodhani hapo alitakiwa kusoma kwanza katika chuo cha walimu wanaofundisha elimu ya watu wenye ulemavu wa kusikia katika chuo cha Patandi kwa ngazi ya Diploma ndipo apate kazi ya kudumu alikubali na kwenda kusoma.
“Nilikwenda huko lakini nilipoomba wanipatie fedha za kunisomesha walisema nitumie zangu kisha baada ya kumaliza manispaa ingelipa lakini tangu 2005 hadi leo sijalipwa chochote na ndiyo kwanza nimepokea barua ya uhamisho wa kutakiwa kwenda Temeke lakini nao hauna fedha za uhamisho, hata sijui kwa nini,’’ anasema Rabia.
Hata hivyo licha ya kusoma katika chuo hicho maalumu kwa walimu wa kufundisha watu wenye ulemavu wa kusikia, Rabia anasema alipomaliza masomo yake hakuwa akijua kutumia ishara jambo lililomlazimu kujiunga na chama cha walemavu wa kusikia ambapo alijifunza na kufahamu vizuri lugha ya ishara.
Akizungumzia jinsi alivyopata ulemavu wa kusikia, Rabia anasema alizaliwa akiwa anasikia kama kawaida lakini alipofika darasa la nne akapatwa na malaria kali ambayo ilimlazimu kutumia dawa kwa muda wa mwezi mzima na baada ya kupona taratibu uwezo wa kusikia ukawa ukipotea na hatimaye hakuweza kusikia tena hadi leo.
Rabia ambaye ni mkazi wa Ilala Sharifu Shamba anasema kipindi hicho alikuwa na miaka nane.
“Taratibu nilijikuta nikipoteza uwezo wa kusikia lakini kipindi hicho nilipata shida sana kwani wazazi na ndugu zangu walidhani nimeanza jeuri hivyo walikuwa wakinipiga makwenzi na kunidhihaki sana bila kujua kuwa nilikuwa sisikii,’’ anasema Rabia kwa kusikitika.
“Unajua hawakuwa wakijua kama nimepoteza uwezo wa kusikia, kwa kuwa mara kwa mara mama alikuwa akiniita lakini sikuwa nikiitika kwa kuwa nilikuwa sisikii hivyo alikuwa akikasirika sana na kunipiga mara kwa mara na ndugu zangu nao pia walikuwa wakinipiga makonzi, iliniuma sana lakini sikuwa na jinsi ya kuwaeleza wasifanye hivyo,’’ anaendelea kueleza Rabia.
Anasema hali hiyo iliendelea kwa muda mrefu lakini baadaye baadhi ya majirani waliingiwa na wasiwasi na hali hiyo na kumweleza mama yake na ndugu zake kuacha kumpiga makonzi kwani huenda mtoto huyo akawa na matatizo ya kusikia hivyo walimtaka mama yake kwenda kumchunguza masikio hospitalini na alipofanya hivyo iligundulika kweli hakuwa na uwezo wa kusikia.
“Matokeo hayo yalimuhuzunisha sana mama, nilimuona akijisikia vibaya kwa kuwa alikuwa akinipiga makwenzi kwa kudhani kuwa nilikuwa jeuri, lakini hakukuwa na la kufanya, kipindi hicho hakukuwa na shule za wenye ulemavu huo hivyo nikalazimika kusoma kwa kuchanganyika na wanafunzi wasio na matatizo kama yangu,’’ anaeleza Rabia.
Kwa masikitiko Rabia anasema kuwa yeye alikuwa katika hali ngumu kwani ilipofika kipindi cha mitihani hasa somo la Imla hakuwa akiambua kitu na wala hakuwa akipata msaada wowote kwa kuwa walimu wenyewe waliokuwa wakisimamia mitihani hawakuwa wakijua kuzungumza kwa ishara.
‘‘Hivyo katika mitihani yangu yote kuanzia darasa la nne nilikuwa nikikosa maswali yote ya Imla na yale ambayo yalikuwa yamekosewa na kubadilishwa kwa kusomwa kwa kuwa sikuwa nikisikia kitu zaidi ya kuhisi baadhi ya mambo, lakini nashukuru Mungu licha ya kushindwa Imla katika kila mtihani wangu, Mungu alinisaidia nikafaulu mtihani wa darasa la saba na kuchaguliwa kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Kisutu,’’ anasema Rabia.
Anasema sekondari nako kulikuwa kugumu zaidi kwani alikuwa hasikii na lugha iliyokuwa ikitumika ni Kiingereza ikawa ngumu kutambua kwa kuangalia mdomo wa mwalimu kwa kuwa maneno hayo hakuwa akiyafahamu, ikawa ngumu kwake kung’amua lolote hata alipojaribu kumuangalia mwalimu wa somo anavyotamka maneno.
Rabia alimaliza sekondari na kupata daraja la nne la pointi 26 hivyo akachaguliwa kujiunga na Ualimu katika chuo cha ualimu Korogwe Tanga.
“Nina ombi kwa serikali, naomba wabadilishe mfumo wa mitihani ya shule za msingi kwa wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia, maswali yasifanane na wasio na matatizo hayo ili kila mtu awe na uwezo wa kujibu na pia wasimamizi wa mitihani hiyo wawe walimu wenye uelewa na watu wa namna hiyo,’’ anasema Rabia.
Makala haya yameandikwa na Festo Polea wa Gazeti la Mwananchi

3 comments:

Anonymous said...

yah! stori nzuri na inafundisha kwamba ujafa hujaumbika na tusikate tamaa katika maisha coz kila kitu kinawezekana asante yasinta kwa kutulea hii habari kwa upande wangu imenigusa!

Steven Bulamu said...

Ina sikitisha Sana!

Yasinta Ngonyani said...

Usiye na jina! ni kweli habari inafundisha, ila hii inatokea mara nyingi sana watu hawana utu kabisa cha mauhimu ni kweli kutokata tamaa. Huyu dada ni mfano mzuri sana.
Kaka Steve! Ni kweli inasikitisha sana kuona watu wengine wapo hivyo sijui kama wana roho?