Thursday, March 20, 2014

KWA KIFUPI:- HAPA NI HISTORIA YA MASHUJAA NA MAKUMBUSHA YA VITA YA MAJIMAJI SONGEA!!!

Siku ya leo nilikuwa najisomea kitabu changu kiitwacho THE HISTORY OF THE WANGONI KILICHOANDIKWA NA FR ELZEAR EBNER, OSB..Nitawaonyesha siku nyingine. Nachotaka kusema hapa ni kwamba mara nikakumbuka ziara yangu ya nyumbani Songea na hasa hapa katika makumbusho haya. Hakika kama hujafika Songea basi ukifika usikose kufika hapa Makumbushp ya mashujaa wetu. Basi fuatana nami kwa hizi picha chache na maelezo.......KARIBUNI SONGEA
 
 Maandishi yanampa msomaji picha  halisi ya historia ya Makumbusho ya Majimaji yaliyopo katika mji wa Songea kusini mwa Tanzania. Mkoa wa Ruvuma unapakana na nchi ya Msumbiji kwa upande wa kusini, Kaskazini mkoa huu unapakana na mkoa wa Morogoro, Kaskazini Magharibi mkoa wa Ruvuma  unapakana na mkoa wa Iringa, Magharibi mkoa huu unapakana na nchi ya Malawi na kwa upande wa Mashariki kuna mikoa ya Lindi na Mtwara.
Historia ya Makumbusho haya inahusu vita ya Maji Maji ilivyo tokea kati ya mwezi julai 1905 mpaka Agosti 1907. Vita hiii ilianza katika vilima vya Umatumbi kaskazini mwa mji wa Kilwa mnamo mwezi Julai mwaka 1905.
Waanzilishi wa awali wa vita hii walikuwa ni Wamatumbi chini ya uhamasishaji wa Mganga wa jadi /Nabii aliyejulikana kwa jina la Kinjeketile Vita hii ilikuwa kama moto katika nyasi kavu na kusambaa katika makabila ya Wamwera, Wangindo, Wapogoro, Wangoni, Wabena, Wasangu na wengine. Watu hawa walipigana kupinga kukandamizwa na kulazimishwa na wakoloni wa Kijerumani namna ya kuishi, mazao ya kuzalisha na nani wa kumtumikia.
 
 HAPA NI PICHA YA ASKARI WA KIJERUMANI
Jina la vita hii limetokana na imani ya matumizi ya dawa iliyochanganywa na Maji, punje za mahindi na mtama zilizosadikiwa kuwa zitampa mpiganaji kinga ya kutodhurika kwa shambulio la risasi za majeshi ya Wajerumani. Inakadiliwa watu 75,000 walipoteza maisha yao ukanda wa kusini mwa Tanzania baada ya vita. Katika eneo la Ruvuma inakadiliwa kuwa zaidi ya watu 1,000 walipoteza maisha yao.
Baada ya vita viongozi na askari walishiriki katika vita walikamatwa na kuhukumiwa kunyongwa mpaka kufa. Tarehe 27 Februari 1907 ilikuwa siku ya masikitiko makubwa kwa watu wa Ruvuma ambapo kadri ya watu 60 walinyongwa kwa sababu ya kushiriki katika vita. Mashujuaa hawa walinyongwa nyuma ya eneo ambalo leo hii linajulikana kama "Songea Club". Baada ya kunyongwa miili yao ilizikwa katika kaburi la halaiki, lililoandaliwa na wafungwa kwa muda wa miezi miwili. Siku ya tatu baadaye Chifu alinyongwa na kuzikwa katika kaburi lilikoandaliwa na kaburi la halaiki.

 
 Hapa ni kaburi la halaiki walilozikwa mashujaa wa vita ya Maji Maji, ni watu 66 walizikwa hapa.

Eneo walilozikwa mashujaa hawa limekuwa eneo muhimu sana. Tukio hili lilikuwa la kuhuzunisha sana kwa watu wetu hivyo watu hawakulizungumza kwa kitambo kirefu. Baada ya uhuru (1961). Baadhi  ya wazee walianzisha harakati za kuwakumbuka mashujaa hawa. Walianza kufanya maombi yao na maadhimisho katika eneo lililo karibu na eneo walilonyongwa wapiganaji hao. Shughuli hizi zilifanyika katika nyumba ya Padre Chengula.
Wazo la kuwa na maadhimisho ya Kitaifa lilianzishwa na kamati wa wazee wa Kingoni. Walitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa Bw. Martin Haule aliyekuwa ameteuliwa wakati huo. Baadhi ya wazee waliokuwa katika kamati hii ni pamoja na Xavery Zulu, Padre Chengula, Daudi Mbano, Ali Songea Mbano, Agatha Shawa, Alana Mbawa, Mwl. Duwe, Shaibu Mkeso na Daniel Gama.
Baada ya kuwasilishwa wazo hili kwa Mheshimiwa Martin Haule, alichukua hatua za dhati katika kulishughulikia jambo hili. hatua ya kwanza ilikuwa kutambua eneo ambalo Mashujaa hawa walizikwa. eneo hili walipozikwa Mashujaa lilitambuliwa na Bw. Jumbe Darajani ambaye alishuhudia tukio la kunyongwa kwa wahenga hawa (wakati wa utoto wake). Alama iliyotumika kufahamu eneo hili ilikuwa ni mti mmoja uliojulikana kwa jina la CHIKUNGUTI. Baada ya kutambuliwa eneo hilo mheshimiwa Haule alifanya uchimbuzi na kupata baadhi ya mifupa.
Kaburi la Songea Mbano ambaye alizikwa peke yake. Na la Mji wa Songea limetokana na jina lake.
 
Kabla ya Bwana haule kukamilisha kazi hii alihamishiwa Mkoa wa Ruvuma mwaka 1964. Wazo hili  la kuwaenzi Wahenga hawa liliibuka tena mwaka 1979 wakati Bw Laurence Gama alipoteuliwa kuwa Mkuu wa mkoa wa Ruvuma. Aliendelea na jitihada za kutekeleza wazo hili. Alianza kuhamasidha na kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa makumbusho kwa kushirikiana na wazee wa Ruvuma na wananchi wengine, ujenzi wa jengo la makumbusho ulianza na kukamilika mwaka 1980.
Pamoja na kukamilisha kwa ujenzi wa jengo hili pia zilijengwa Sanamu katika eneo la mbele ya jengo. Sanamu hizi zilijumuisha anamu ya Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Mwl. J.K Nyerere na sanamu 12 zamachifu wa kingoni. Lakini kwa sasa sanamu wa hayati Mal. J.K Nyerere imetolewa baada ya kuona haina kiwango cha juu, hivyo inaandaliwa upya ili iweze kuwekwa upya . Kazi ya kutengeneza sanamu hizi ilifanywa na msanii mmoja huko Arusha.
Vifaa vya awali katika makumbusho haya vilitengenezwa na Mheshimiwa Laurence Gama, Padre Chengula na baadhi ya wazee. Vifaa vilivyokusanywa vilijumuisha ni silaha zilizotumika wakati wa vita ya Maji Maji kama vile:- Kwa lugha ya kingoni Chikopa (Ngao), Chibongo(Rungu), Chinjenje (Kishoka), pia baadhi ya viti vilivyotumiwa na Chifu Mputa,vifaa vya ndani na nguo za magome ya miti.
Kwa Hiyo kuanzia mwaka 1980 baraza la wazee lilianza kuadhimisha maombolezo ya mashujaa walionyongwa kila ifikapo tarehe 27/2 ya kila mwaka. Makumbusho haya yalifunguliwa rasmi tarehe 7/7/1980. Kuanzia hapo makumbusho haya yaliendelea kutoa huduma chini ya usimamizi wa Mkoa wa Ruvuma na wazee wanaendelea kufanya maadhimisho ya siku ya Mashujaa katika eneo la Makumbusho haya kila mwaka. Baadhi ya wazee ndio ambao wamekuwa wakitoa maelezo kwa wageni wanaotembelea makumbusho haya. Tarehe 1/9 2005 makumbusho haya yalikabidhiwa kwa Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Miaka 100 ya vita ya Maji Maji iliadhimishwa Kitaifa katika Makumbusho haya tarehe 27/2/2006 na yalizinduliwa rasmi na Rais wa Tanzania Mhe. Jakaya Kikwete.
TUWAKUMBUKE MASHUJAA WETU DAIMA  WALIFANYA KAZI KUBWA SANA..
 

2 comments:

NN Mhango said...

Nikiangalia baadhi yetu walivyogeuka majambazi na mafisadi na mchango uliotolewa na mashujaa wetu nahisi kinyaa kiasi cha kutamani ninywe damu ya mtu. Mashujaa wamesalitiwa. Wananchi wamesalitiwa. Kinachoendelea ni kwamba mashujaa waliishia kuzaa mbwa na fisi wanaowaumiza watu wao kwa kuwauza tena kwa bei ya ugoro kupata vijisenti vya ugoro. Kumbe wakati mwingine samba anaweza kuzaa mbwa siyo?

Yasinta Ngonyani said...

Ni kweli siku hizi kuna majambazi na mafisadi kila kona. Badala ya kuendesha nchi wanaweka katika mifuko yao, hivi ndivyo ilivyo. Hii tumekwisha ona mara nyingi wanapotaka kitu basi wanakuwa wanyenyekevu na wakishapata huwaoni tena ...Hakika tupo mbali sana.
Inawezezekana ni kweli simba anaweza kuzaa mbwa....