Monday, February 8, 2010

Kibanga Ampiga Mkoloni

elimu ni ufungu wa maisha

Katika upekuzi wangu jana nikawa nimekifuma kitabu hiki na mwisho nikakutana na hadithi hii ungana nami kuisoma ina toka katika kitabu cha 6 Tujifunnze Lugha Yetu!

Zamani za ukoloni, palitokea Mzungu mmoja. Mzungu huyo hakuwa mtu mwema. Alikuwa mkali na mkatili sana. Kwa ajili ya ukatili wake watu walimwita mkoloni. Wanancgi wote walimchukia sana popote pale alipokwenda.

Mzungu huyo alikuwa Bwana Shamba. Alikuwa na bakora iliyokuwa imetengenezwa kwa mkwaju. Kila alipokwenda kukagua mashamba, alikuwa na bakora hiyo mkononi. Alipendelea sana kuitwa "Bwana Mkubwa". Mkolono huyo alifurahia sana kupiga watu. Aliwapiga watu waliposhindwa kupalilia mashamba. Aliwapiga pamba yao ilipokuwa chafu. Aliwapa taabu sana.

Katika kijiji cha Kwachaga, Wilaya ya Handeni, alikuwapo mzee mmoja aliyeitwa Kibanga. Mzee huyu alikuwa mwenye nguvu, hodari na shujuaa. alikuwa fundi wa mieleka. Ingawa alikuwa mwenye nguvu, alikuwa mpole. Hivyo watu wa Kwachaga walimpenda na kumtegemea kuwaongoza vitani.

Siku moja yule Mzungu alifika Kwachaga kukagua mashamba ya mihogo. Jumbe pamoja naye wakatembelea mashamba. Kwa bahati mbaya mwaka ule haukuwa na mvua ya kutosha. Kwa hiyo mihogo haikustawi. Kila wakati yule Mzungu alipotazama mashamba alitikisa kichwa na kufoka. Mwisho akamwagiza Jumbe kuitisha mkutano wa watu wote wa kijij. Waliporudi kijijini Jumbe akapiga mbiu. Watu wote wakakusanyika. Walipofika tu, yule Mkoloni akaanza kuwatukana, akawaambia, "Ninyi watu weusi ni wavivu sana. Hamfanyi kazi sawa sawa. Mashamba yenu ni mabaya sana". Jumbe akataka kumjibu ili kumweleza kwa nini mihogo haikustawi. Kabla hajamweleza yule Mzungu alimrukia na kumpiga kofi. Kisha akasema, "Sitaki kijibiwa na wewe, mvivu wa wavivu". Watu wote wakakaa kimya. Hakuna aliyeweza kufanya kitu.

Kibanga akajitokeza, akasimama. Akamtazama yule Mkoloni kwa dharau sana. Kisha akamwuliza, "Kutuita sisi wavivu ndiyo nini? Na kumpiga Jumbe wetu mbele yetu, maana yake nini?"

Kabla ya kumaliza kusema, Mkoloni aliamka kitini kwa hasira , akataka kumpiga Kibanga. Alishika bakora yake mkononi. Akasedma, "Nitakuadhibu vibaya kima we! Unajifanya kuwa shujua? Huwezi kucheza na bwana mkubwa. Nitakupiga, kisha utakwenga jela miezi sita." Lakini Mkoloni hakuwahi kumwadhibu Kibanga. Aliadhibiwa yeye. Kabla ya kumfikia, Kibanga alimpiga chenga. Kisha akamrukia, akamnyangánya bakorta yake. Akaitupa, ikaokotwa na vijana, wakaificha.

Kibanga alimshika yule Mzungu akamwambia. "Wewe umezoea kutoa amri kila siku, lakini leo utashika adabu, mbwe wee!" Papo hapo alimnyanyua juu na kumbwaga chini, puu! Yule Mkolono akaumia sana. Kabla ya kuamka, Kibanga alimwinua tena na kumbwaga chini kama furushi la pamba. Akamkalia.

Hapo yule Mkoloni akawa hana la kufanya. Bila ya bakora alikuwa hana nguvu. Akaomba radhi akilia, "Samahani! Naumia! Nihurumie! Sitafanya tena hivyo." Kibanga alimjibu kwa dharau, "Sikuachi mbwa wee! Leo utakiona cha mtema kuni! Ulijiona una nguvu. Leo nitakutengeneza."

Wazee wakamshika Kibanga na kumwomba asimpiga tena. Akamwacha. Kwa shida yule Mkoloni akajikokota kwenda hemeni. Alikuwa amejaa vumbi huku damu zikimtoka. Wazee wengine wakamfuata nyuma. Walinyamaza kimya, wakimhurumia. lakini vijana walifurahi sana.
Baadaye waliimba wimbo wa kumsifu Kibanga.

Jioni yule Mkoloni aliomba radhi kwa wazee. Mzee mmoja akasimama na kumwambia, "Umefanya vizuri kuomba radhi, nasi tunaipokea. Lakini tangu leo usijivunie ubwana. Jivunie utu. Ninyi wakaoloni mna kiburi. Mnatudharau. Kama ungetuuliza tungekuambia kwa nini migogo haikustawi. Haya yote yamekupata kwa sababu ya kiburi chako. Katika nchi hii tuanaamini kuwa kiburi si maungwana".

Baada ya hapo wazee wakamsamehe, lakini hawakumpa bakora yake. Ikabaki nyumbani kwa Jumbe. Yule Mkoloni akaondoka. Tangu siku hiyo hakufika tena Kwachaga. Kila mara alipokutana na watu aliyakumbuka maneno ya yule mzee, "Kiburi si maungwana".

Siku hizi kijiji cha Kwachaga kina maendele mazuri ya kilimo na mifugo. Maendeleo yote yamepatikana kwa sababu ya uongozi bora wa Serikali ya wananchi.

16 comments:

Markus Mpangala. said...

hapo ndipo penye akili na hekima

Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti! said...

kwa kung'ang'ania bakora mkoloni ana nguvu na jeuri!

Je si kuna wakati tunag'ang'ania mambo hata yasofaa huku tukijiona tuna maguvu na jeuri ya kufanya tutakavo hata kama tunaumiza wengine? :-(

Anonymous said...

Hadithi hii imenikumbusha wakati nilipokuwa mwanafunzi wa darasa la tatu, nakumbuka tulikuwa tunasoma na mwanafunzi mmoja mwenye asili ya kiarabu, sasa siku moja ikatokea tukatofautiana kwa mambo ya kitoto, kama mnavyojua mambo ya watoto, basi nikapania kuwa tukitoka nimpige, na kweli tulipotoka shule jioni nilimfuata na kuanziasha ugomvi na tukaanza kupigana, nilimpiga mpaka nikamkimbiza, na hivyo kuwa mshindi wenzangu wakasema Kibanga amempiga mkoloni wakimaanisha mimi nimempiga mkolni kwa kufananisha lile tukio na hii hadithi na tangu siku hiyo wanafunzi wenzangu wakawa wananiita Kibanga….

Fadhy Mtanga said...

Sista Yasinta Mngoni umenikumbusha mbali na simulizi hiyo. Ahsante kwa kumbukumbu nzuri kama hiyo.

Bennet said...

Hizi hadithi zilikuwa zinasaidia sana kuelimisha juu ya usawa wa binadamu na kuondoa mambo ya ubaguzi wa rangi

Faustine said...

....Umenikumbusha mbali saaaana!

Jacob Malihoja said...

Du! Yasinta we ni noma! umenikumbusha mbali mno. Je Unawakumbuka Wagagagigikoko na mfalme wao Huihui nafikiri ni kule alikoibukia Bulicheka baada ya ajali ile ya majini kama sikosei!.

Mwanasosholojia said...

Dada Yasinta leo umenikumbusha mbali sana!Mafunzo lukuki ambayo ni aghalabu kukutana nayo siku hizi katika kazi za fasihi!Shukrani mno!

Simon Kitururu said...

Nimeipenda sana staili ya ngwala a.k.a kubwengana ya Mheshimiwa mpole Kibanga.

Lakini bado :

``Siku hizi kijiji cha Kwachaga kina maendele mazuri ya kilimo na mifugo. Maendeleo yote yamepatikana kwa sababu ya uongozi bora wa Serikali ya wananchi.´´

- inanitamanisha nitamani kwenda huko KWACHANGA kwa kuwa BADO najiuliza zaidi kuwa;

- hivi huko KWACHANGA ni Tanzania?


Kwa maana nahisi viongozi wao wangeifaa kweli SERIKALI ya Tanzania baada ya Watanzania kumuondoa TANZANIA Mkoloni.:-(

Ngojea niwashangilie washindi,

Kibanga OYEEE! Ukoloni mamboleo OYEE!



Nawaza tu!:-(

Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti! said...

na kwa mtindo wa ushangiliaji wa mt. simon akiwa na glass ya komoni a.k.a ze bia mkoni, nina wasiwasi kama viongozi wetu watazinduka na kuuona ukweli wa kuwa twaweza kujiletea maendeleo wenyewe bila wakoloni:-(

katika dunia ya sasa Kibanga angeweza kuonekana kichaa! je unadhani twahitaji vichaa wengi wa kuwazindua viongozi wetu kama alivozinduliwa waziri mkuu wa Italia?

Samahani jamani, labda naanza kurukwa na akili :-(

Lakini kama ndivo msinambie miye ndo niende kuwazindua hao walolala :-(

Simon Kitururu said...

@Kadinali Chacha Ng'wanambiti: Unauhakika Kibanga alivyompiga Mkoloni ni kweli Mkoloni aliondoka na Ukoloni wake?

Si wajua kuwa jambo kubwa litofautishalo ukoloni na kwenda haja msalani a.k.a CHOONI ni kwamba UKOLONI hauhitaji Mkoloni awepo katika KOLONI kama Haja ihitajivyo ajisaidiaye chooni awe CHOONI?

Lulu said...

Mmmh nahisi harufu ya uji wa bulga maana hadithi hizi za Kibanga zinanikumbusha shule enzi hizo twaziita "vidudu" siku hizi waita chekechea au day care. Haaa haaa ilikuwa uji wa bulga lazima unyweke saa nee. Ahsante Yasinta

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

Yasinta ndo kibanga!

Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti! said...

@Mt. Simon: ni kweli kabisa mkoloni hakuondoka na ukoloni wake kwa kuwa kuna bado vijeba ambavyo ukiviangalia saaaaaana utastukia kuwa ni vikolini katika nguo za rangi ya kijani/njano :-(

na kuhusu choo nadhani silazima mtu aende chooni kwani katika baadhi ya makabila kama la kwangu wawezakuta msitu wa jirani umesheheni uyoga kwa kuwa kuna mbolea-kinyesi cha mtu :-(

na waweza ukakuta karibu na palipo na mzigo wa kinyesi aidha kuna kuna aidha jiwe ama nyasi badala ya ukoloni wa toilet paper :-(

lakini, ni wangapi kati yetu tumefikiria kuhusu ujenzi wa choo au kujisitiri vichakani katika staili ya kumfukuza mkoloni mawazoni?

Una hakika wewe si mkoloni ndani ya Utakatifu? :-(

nyahbingi worrior. said...

mmmm hadithi yenye mafunzo.

Simon Kitururu said...

@Kadinali Ng'wanambiti: Mtu akijisaidia msituni, MSITU ni CHOO.

Kwahiyo
narudia:

Si wajua kuwa jambo kubwa litofautishalo ukoloni na kwenda haja msalani a.k.a MSITUNI ni kwamba UKOLONI hauhitaji Mkoloni awepo katika KOLONI kama Haja ihitajivyo ajisaidiaye msituni awe MSITUNI?

Utakatifu nimejipa mwenyewe HUU kwa kuwa si unajua mie sina ushikaji na PAPA agawiaye Wakatoliki Utakatifu.

Na kwa bahati mbaya utakatifu wangu nahisi hauwanyonyi au kuwakereketa watu wengine kwa hiyo hauna UKOLONI ndani yake.:-(