Thursday, February 25, 2010

JAMANI HII NI NDOA AU NDOANO?


Je? kuna upendo hapa?

Ndugu wasomaji na wanablog wenzangu, leo nina jambo moja ambalo ningependa tulijadili kwa pamoja.

Kuna msomaji mmoja wa blog hii ambaye ningependa kumuita Mlachaombwani (Sio jina lake halisi) amenitumia email akinitaka ushauri kutokana na kile alichoita jinamizi linaloitafuna furaha ktk ndoa yake.

Kusema kweli, hata mie nimejikuta nikishikwa na kizunguzungu maana mambo ya maunyumba haya yanahitaji umakini pale unapotakiwa ushauri.

Kaka Mlachaombwani anasema kuwa ameishi na mkewe kwa takribani muongo mmoja sasa na wamejaaliwa kupata watoto wawili katika ndoa yao hiyo. Maisha yao kwa ujumla ni mazuri kiasi, kwani ni familia iliyojitosheleza kwa kiasi cha mboga. Awali ndoa yao iloanza kwa bashasha zote ilikuwa na amani na utulivu na kila mmoja alimpenda mwenzake.

Lakini mwaka 2003 mkewe huyo alimbadilikia sana na akawa hawapendi kabisa ndugu zake, yaani ndugu wa mume. Hataki kuwaona wazee wa mumewe wala ndugu zake. Pamoja na ushauri toka kwa viongozi wa dini yao mkewe huyo alishasema kuwa ‘hata kama akija MALAIKA kumshauri hataweza kubadili msimamo wake kwa kuwa akishamchukia mtu basi ni mpaka kiyama’! Kibaya zaidi kafikia hatua anamnyima mumewe huyo unyumba au labda niseme chakula cha usiku, na sasa maisha yao ya ndoa yamekuwa kama vile sio wanandoa, yaani hakuna kupeana lile tendo la ndoa kama ilivyokuwa zamani wakati wanaoana.

Anasema hata kama akiamua kumpa tendo ni pale anapoamua yeye (mwanamke) yaani akipenda yeye na hii inaweza kuwa ni baada ya mwezi au baada ya miezi. Nilipomuuliza kama anapopewa, je wanafanya kwa ile hali ya mapenzi kufurahia tendo la ndoa au vipi? Akasema ni mradi kutimiza tu wajibu lakini hakuna raha yoyote ile. Ni kama vile anabakwa ama anabaka vile.

Nikukumbushe msomaji wangu kuwa ndani ya miaka hiyo kuanzia 2003 ilisababisha huyo kaka Machaombwani kuingia katika ‘mahusiano yasiyofaa’ nje ya ndoa ambayo yalisababisha kupatikana watoto wengine wawili. Nadhani ni baada ya kuona hapati haki yake hapo nyumbani.

Hata hivyo amebainisha kuwa tatizo jingine kubwa linaloitafuna ndoa yake ni wivu usiofaa aliokuwa nao mkewe huyo. Anasema mke wake amekuwa akimlinda sana akijaribu kumpeleleza kama ana wanawake wengine nje ya ndoa (nyumba ndogo?) hata baada ya mume kukiri kilichokwisha kutokea. Kwamba pamoja na kumnyima tendo la ndoa lakini bado anamuonea wivu, na kumlinda. Na cha ajabu pia pamoja na mume kusema kuwa kwa muda wa miaka 2 sasa hamjui mwanamke mwingine nje ya ndoa hataki kusikia chochote ikiwa ni pamoja na kumzuia mumewe kutoa matunzo kwa watoto hao waliozaliwa nje ya ndoa kutokana na ‘ujinga’ wa wanandoa hao.

Tatizo lingine ni matusi, yaani anamtukana hadharani mbele ya watoto bila hata ya aibu. Kuhusu malezi ya watoto, watoto wanalelewa kana kwamba wako ktk kambi ya mateso kwani ni matusi (kama vile mbwa wee, kunguni, mjinga, taahira n.k) na mangumi kwa kwenda mbele. Heshima ndani ya nyumba imepungua na hakuna amani kabisa. Kwamba unaweza kuwakuta wanacheka lakini ni vicheko vya kebehi na ukiwaona leo baada ya saa moja ukiwakuta utadhani ni maadui wa siku nyingi.

Kaka Mlachaombwani anadai kuwa amani yake yeye ni pale anapokuwa kazini, safarini au kwa marafiki zake tu, lakini nyumbani kila siku moto unawaka. Amekiri kuwa sasa wakati wake mwingi anaupotezea katika kompyuta kwa kuwa hapo ndio hupata farijiko huku akijifunza mambo mengi kadha wa kadha ili kupoteza mawazo.

Nimemuuliza kwa nini asimuache huyo mwanamke na kumfukuza kama hali yenyewe ndiyo hiyo naye amenijibu kuwa yupo kwa SABABU ya WANAWE na si vinginevyo. Anasema kuwa muda ukifika ataondoka yeye tu na kumwachia kila kitu huyo mkewe! Yaani pamoja na mahusiano haya mabaya bado yupo tu? Na atakaa kwa muda gani akiyavumilia hayo? Kuna haja ya kuondoka? Kuna haja ya kuoa mke mwingine? Afanye nini?

Wenzangu kwangu mimi huu ni mtihani maana hata sijui nimshauri nini kaka Mlachaombwani.

Swali langu kwa ndugu zangu wasomaji:- Je ndoa ni kupendana kati ya wanandoa au ni tendo la ndoa? Je ni kipi kinachowaunganisha wanandoa, ni upendo au ni tendo la ndoa?
Je kweli kuna upendo kati ya wanandoa hawa na ni namna gani tunaweza kuwasaidia wanandoa hawa?

20 comments:

Shabani Kaluse said...

Japo nimekuwa mtu wa kwanza kutoa maoni, (kama sikosei) lakini nasikitika kusema kuwa sitakuwa na ushauri wa moja kwa moja. Nahitaji muda kutafakari.

Wakati wadau wengine wakikuna vichwa kutafakari, ngoja na mimi niungane nao kutafuta ushauri maridhawa kwa wanandoa hawa

Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti! said...

Kaka Kaluse: mie niliposoma habari hii nilitarajia kusikia toka kwako na Kamala.

Mie natoka lakini ntarejea...ngoja nkabukue kwanza!

Shabani Kaluse said...

Kaka Chacha o'Wambura, mambo ya wanandoa sio ya kukurupuka, yanahitaji mtu atafakari kwanza, kwani unaweza kuja na ushauri wa ajabu hapa kila mtu akakushangaa....

Koero Mkundi said...

Ina maana nyie mnashindwa na jambo dogo namna hii? kaka yangu Shabani mzee wa utambuzi na kaka Chacha Wambura mnashindwa kutoa ushauri kwa jambo dogo hivi.

Mimi nasema hivi, hiyo ndoa haifai kabisa na hasa huyo mwanamke anayebania kidude ambacho kililpiwa mahari huko kwao.

Haiwezekani unamnyima mwenzio hivi hivi....ebo, sasa kiko wapi,,, yeye amemnyima wenzake wamempa na watoto wamemzalia. hivi alidhani wanaume wa siku hizi ni wa kutishiwa nyau?

Nadhani ni vyema hiyo ndoa ivunjwe maana naona dalili za wazi kabisa za wanandoa hao kuleteana UKIMWI.

DADA YASINTA MWAMBIE HUYO KAKA MLACHAOMBWANI AMTIMULIE MBALI HUYO MWANAMKE.......KWANI AMESUSA NA WENZIO TWATAKA HIVOOO.....

Mija Shija Sayi said...

Mlachaombwani, kweli hujawahi mkosea mkeo hadi akaanza ubinafsi alionao sasa? Hebu tumegee kidogo na wewe kwa upande wako ili tujue wapi tuanzie.

Ila una mtihani, tena NATIONAL, NA KAMA NI MSIBA BASI NI WA BABA WA TAIFA.

Kissima said...

Kama alivyodokeza dada Mija, ni vema sana kujua chanzo cha tatizo. Binafsi sijaona chanzo cha tatizo na nadhani aliyosimulia huyu kaka ni yale yaliyosababishwa na chanzo cha tatizo,ambayo mimi nayachukulia kuwa matatizo yatokanayo.


Kwa nini huyu mama awachukie ndugu wa mme wake?
Je, kunyimwa unyumba ni matokeo ya ndugu wa Mume kuchukiwa basi na chuki hiyo hadi kwa Mume?


Ninachomshauri huyu kaka, kama hajui hasa ni kwa nini mke wake anawachukia ndugu zake, na kwa nini manyanyaso mengine, akae chini na mke wake wazungumze(pengine walishazungumza,hajaeleza,na kama walishazungumza,ni yapi waliozungumza, pia hajayaeleza na walifikia wapi). Yawezekana pia huyu kaka ndio chanzo cha yote,kwamba mke kashindwa kuvumilia na akaona yote ayafanyayo ndio suluhisho. Huyu kaka naye ajitathmini kuwa ni wapi anaweza kuwa alikosea kwa kujua au kutokujua.


Ni hayo tu.

Ramson said...

Du Koero! Mie simo, dada umeshindwa hata tafsida...LOL..

Mie ninaomba niongee kwa upole kabisa tena kwa unyenyekevu kuwa msimtafute mchawi maana wachawi ni nyie wenyewe wananandoa. Mkiamua mnaweza kulimaliza hilo tatizo na maisha yenu ya ndoa yakarudi kama awali yaani mkarudia enzi za kula asali na maziwa.

Dada Mija tukisema tumtafute aliyeanza uchokozi tutakesha hapa bila kupata jibu, mie naona swala hapa ni kusameheana na kusahau yaliopita kwani hata mungu hutusamehe sisi wanaadamu pale tunapotenda dhambi seuze sisi wanaadamu ndio tushindwe kusameheana...si itakuwa ni kumkosea mungu dhahiri?

Nawaomba eyni wanandoa wapendwa msameheana na msinyimane tena kwani tendo la ndoa hustawisha ndoa, na hakika ndoa hiyo hujaa baraka za mwenye enzi Mungu.

Dada Yasinta Ndoa ni tendo, kwani pamoja na mambo mengine, lakini tendo ndio kitovu cha ndoa, na pale pasipo na tendo la ndoa basi ndoa hiyo iakuwa legelege, kwani mtatamani vya nje na hivyo kutenda dhambi, na ndio maana biblia ikasema wazi kuwa MSINYIMANE MAANA NI DHAMBI....

Upepo Mwanana said...

Hapo ndoa hakuna wanandugu

Bennet said...

Sio kwamba namshauri bali kama ningekuwa mimi (ingawa hatujasikia kutoka kwa huyo mwanake)hapo hakuna ndoa, maana ndoa inahitaji upendo wa dhati na kuvumiliana
Ndugu zangu hawataki na mimi unyumba kama mvua jangwani, kwa kweli ningeachana naye hata kana dini hairuhusu nisingeweza kuendelea naye maana unakuwa roho juu hata kula chakula chake, anaweza kukudhuru saa yoyote

Koero Mkundi said...

Ngoja nimnukuu kaka Bennet

"Ndugu zangu hawataki na mimi unyumba kama mvua jangwani, kwa kweli ningeachana naye hata kana dini hairuhusu nisingeweza kuendelea naye maana unakuwa roho juu hata kula chakula chake, anaweza kukudhuru saa yoyote"

Mwisho wa kumnukuu.

I LOVE THIS, THANK YOU VERY MUCH BRO........

JUMANNE SANGA said...

Huyo jamaa ajichunguze pahali walipoacha upendo wao.Halafu watafute ushauri wa kimawazo kwa washauri wa mambo ya ndoa.

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

ndoa na ngono jamani,

mimi kama mume wa mtu miaka mingi kiholela na mume wa mtu kisheria muda mfupi uliopita, miezi michache iliyopita nimemonja sumu ya kulala na mkeo harafu kidume kimesimama kama mkuki, harafu mama hataki uchokonoe, wewe!! inauma na kukatisha tamaa japo wewe ni sehemu kubwa ya kwa nini unyimwe!!!!!!!!

harafu, kuna ujinga mwingi juu ya ndoa, kama alivyosema Damija mchaga huyu, sisi huwa tunaona matatizo ya wengine kuliko kucheza nafasi zetu na ndio maana hata ukionana na mwanamke na kuongea naye sirini, utagundua kuwa naye anasema mabaya juu ya mumewe pia. kwa hiyo nguvu hasi a.k.a Shetani, zimekatiza na kuitawala ndoa, kupitia mawazo na matendo. hili dume kwa vyovyote halijasema upande wake, laweza kuwa sehemu ya tatizo pia/

suala la ndugu mimi sitaki kulisikia, ndugu sio sehemu ya familia yenu na sio lazima wawepo

muda unabana naishia hapa ila njoo mpigwe utambuzi muje muone utamu wa ngono..... kama zamani na ndo itasimama kama dume ambalo halijaonjeshwa siku kibao

PASSION4FASHION.TZ said...

Kwakuwa chanzo hatujui,mimi inaniwia vigumu ku comment,nisije mpiga mtu dongo kumbe sio kosa lake.

Anonymous said...

hili suala ni gumu kimtindo, sio kama tunavyofikiria, inabidi kujua na upande wa pili ili kuweza kujua nini chanzo. Bila kujua chanzo ni vigumu sana kutibu. Na kama baada ya kuhoji pande zote mbili ikaonekana kwamba upande wa mwathirika hauna tatizo, basi suluhisho ni kuivunja ndoa, maana hii ni hatari. nikitumia lugha ya Koero, kwamba mtu kutoa kidude chake hataki na wivu anakuwekea, sasa hii manake nini. si awache ili akina Koero wapewe ebo!!!

Mrs Haule said...

Hili swala ni gumu,ila nataka kupingana kidogo na koero mwanaume kutoa mahari isiwe tiketi ya kumnyanyasa mwanamke. Kwanza hapa tumeona upande mmoja wa mwanaume, hatujajua haswa chanzo nini hadi kufikia hapa.


Hadi imefikia hatua mwanamke hataki ndugu hapo nyumbani basi ni tatizo kubwa sana hili na chanzo chake kikubwa pia.

Kwa maisha hayo wanayoishi hii si ndoa bali ni ndoano. Sasa hapo watakuja kuleteana magonjwa.

Kareni Michael said...

Nikiwa kama mimi ushauriwangu nikwamba wamuweke mungu mbele kwa maombi kwa sababu bila maombi ni kazi bure naona shetani amewaingilia kati kama zamani ndoa yao ilikuwa ya amani basi ibiisi ameingilia kati watafute ata wazee wa kanisa watawasaidia hayo ni yangu machache.

Yasinta Ngonyani said...

Napenda kuchukua nafasi hii na kuwashukuru wasomaji wote kwa mchango wengu. Na nimeona wengi wanataka kujua chanzo cha ndoa hii kuwa kama ilivyo. Kwa vile kaka Mlachaombwani anafuatilia mjadala huu ameniahidi kunitumia maelezo ya chanzo cha ndoa yake kuwa hivi. Kwa hiyo nawaombeni mvute subira. Upendo Daima.

Anonymous said...

pouwa Yasi, sie twaivuta hiyo subira kama ulivyonkaomba

peter elisa said...

Duuh! hii ndoa imeshakuwa ndoana, wasemavyo waswahili.Ki ukweli inasikitisha sana kuona wanandoa waliojaaliwa kuisha japo kwa muongo mmoja wanafarakana hadi kufikia walipofikia. Japo mimi si mzuri sana katika Maandiko matakatifu ila sina uhakika kama wanandoa hawa wamekuwa wakifuata baadhi ya mambo yanayopatikana katika maandiko husika,mathalani, wanandoa wanapokosana wanatakiwa kufanya juhudi za kupatana wao kwa wao ila wakiona yanakuwa magumu ni vyema kuwaona wasimaizi wao wa ndoa ili kuwapatanisha,hawa wakishindwa wazazi wa pande zote mbili hushirikishwa ili kurekebisha mambo, mwisho wa yote huwa ni viongozi wa dini.Sina uhakika sana ikiwa ndugu zangu hawa walifanya haya na kwa wakati,kwa kuwa kuna kausemi kanakosema kuwa "UKIMLEALEA KENGE ATAKUWA MAMBA" sasa nahofia kuwa hata kufikia hatua ya kuwa mabondia wa ndoa na si walevi wa upendo basi sasa huenda kenge ameshakuwa mamba,yaani wamefikia "THE POINT OF NO RETURN" inasikitisha sana. Jamaa yangu huyo anadai yuko kwa ajili ya watoto,sawa! lakini ameshawahi kuwaza kuwa huyo Bimkubwa yuko kwa ajili gani kwa sasa?
Mimi kwa mtazamo wangu naamini kuwa katika ndoa kupendana na tendo la ndoa vinaishi kwa pamoja, ndo maana jina lenyewe ni ndoa,naamini tunaanza kupendana kwanza ndio ndoa inakuja baada ya kuona mnaweza kuchukuliana udhaifu wenu ambao naamini kila mtu ana wake. Ila kuna vijimambo flani hivi,kwa mfano, neno "ndoa" liko karibu kabisa na neno "ndoana" wakati huo huo neno "kupendana" na "kupeana " ni majirani. Maana yangu ni kwamba ili wanandoa waonyeshe ni wanandoa lazima wapendane ili wapeane na ili ndoa isiwe ndoana lazima wapendane ili kuepuka undoana huo.
Kwa hawa wanandoa ni wazi kuwa hawana upendo kabisaaa!Nadhani jamaa kama ana mali kidogo huenda huyu mwanamke anapiga hesabu kuhusu hiyo mali na huenda kabla jamaa hajamuachia kila kitu akaondoka anaweza kuondolewa yeye. Kibaya ni kwamba atakuwa hajajiandaa hali ambayo itampotezea mengi na pengine kupoteza kazi na hata uhai,si unajua mambo ya frustration? Hivi ameshawahi kujiuliza kuwa huo ujasiri wa kupiga na kutukana ameupata wapi? vipi kuhusu kuuana?
Kaushauri kwa jamaa yangu ni kwamba jamaa awe makini, na huyo mwanamke,kwani ili kumchinja kobe unahitaji kumlia taimingi! kama ameona kuondoka ni suluhisho afanye haraka huku akichukua tahadhari zote kwa kuamini kwamba sio mwisho wa maisha! Ajiulize tu kwamba kama angemfumania huyo mwanamke siku moja ingekuwaje? au kama huyo mwanamke angefariki ingekuwaje?. Lakini kama hajapeleka suala lake kwa viongozi wa dini ni wakati muafaka kufanya hivyo japo kuwa huyo mwanamke anadai kuwa hata kama angekuja Malaika hakieleweki kitu, siamini, kwani anamtishia tu jamaa ili akate tamaa ya maisha ila ajipe moyo tu kwani hili nalo litapita!Nampa pole sana kwani kila amuzi atakalolifanya liamuathiri kwa pande zote mbili (hasi na chanya)ila kwa kuwa wanadamu tumepewa kusahau, ipo siku furaha yake itarejea.

"We ain't what we oughta be,we ain't what we wanta be,we ain't what we gonna be,but thank God we ain't what we was". MARTIN LUTHER KING.

Anonymous said...

Jamaa alizingua kwanza kumtuma mke kijijini na pia kuanza kuzaa nje!ilibidi asuluhishe first ingeshindikana angeoa mwingine ila hii mambo ya kuvunja uaminifu na kutoka nje kwa kusingizia eti nyumbani sina faraja na mke wangu sio njema!kwanza hao wazazi washamuomba msamaha kwa vitendo vyao vya kumnyanyasa huyo dada?maana kiongozi wa kanisa hana kazi yoyote kama neno la kuomba msamaha halijatoka kwa mkosaji mwenyewe!am a man bt ningekuwa huyo dada ningefanya the same except kwa imani yangu hainiruhusu ndo ingenizuia....ok yalopita si ndwele so the fact is ajaribu kunusuru hiyo ndoa kwa kuita wazaze waapologise.!if it doesnt work basi amkimbie huyo dada ili alee tu watoto aoe mwingine....!japo sipendi tabia ya wanaume kudhani wana haki ya kutembea na kila mwanamke na kuzaa nje sio njema