Monday, February 22, 2010

Siri ya mafanikio Ruhuwiko Sekondari

Wanafunzi wa shule ya Sekondari Ruhuwiko
wakisikiliza hoja kwa umakini

KILA anapotembea shuleni na maeneo mengine mkoani Ruvuma, Mkuu wa shule ya sekondari ya Ruhuwiko, Meja Paul Rugwabuza kifua chake kiko mbele. Kwanza ni kwa vile yeye ni mwanajeshi hivyo lazima awe mkakamavu, lakini pili ni kutokana na matokeo mazuri ya shule anayoiongoza.
Anaonekana mwenye furaha kwa sababu jukumu alilopewa la kusimamia elimu ya watoto katika shule hiyo inayomilikiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) limefanikiwa kwa asilimia kubwa.
"Kitaaluma shule hii imekuwa ikipiga hatua mwaka hadi mwaka hususani kwa kuzingatia matokeo ya kidato cha cha nne na sita viwango vizuri zaidi vya ufaulu ambavyo shule inaweza kujivunia sana ni vya kidato cha sita kwani tangu shule ianze," alisema Meja Rugwabuza katika mahafali ya tano ya kidato cha sita yaliyofanyika hivi karibuni.
"Mfano mzuri wa matokeo ya mock wa kidato cha sita mwaka 2009 katika Mkoa wa Ruvuma kulikuwa na daraja la kwanza 17, daraja la pili 108, daraja la tatu 84 na daraja la nne walikuwa wanne. Hakukuwa na mwanafunzi aliyefeli hivyo tunatarajia kupeleka wanafunzi wengi zaidi kujiunga na elimu ya juu (vyuo vikuu)."
Mbali ya mock, matokeo ya kidato cha sita mwaka 2006 yanaonyesha mmoja alipata daraja la I, daraja la II walikuwa 15, daraja la III walikuwa saba na mmoja daraja la IV.
Mwaka 2007 wanne walipata daraja la I, daraja la II walikuwa 20, daraja la III walikuwa 18, daraja la IV walikuwa sita; na mwaka 2008 mmoja amepata daraja la I, daraja la II walikuwa 30, daraja la III walikuwa 36 na daraja la IV walikuwa 13.
Hata nafasi kitaifa, Ruhuwiko huwa inashika nafasi nzuri. Mathalani mwaka 2006 shule ilishika nafasi ya 16 kati ya shule 57, mwaka 2007 ilishika nafasi ya 38 kati ya shule 230 hivyo iko ndani ya malengo kusudiwa ya maendeleo ya shule.
Takwimu hizo za kitaifa ndizo anajivunia Meja Rugwabuza aliyerithi mikoba ya mtangulizi wake Meja Celestin Mwangasi (amehamia Makongo Sekondari) kuiongoza shule hiyo iliyoko kilomita nne kutoka Songea mjini.
Mbali ya uwezo wa darasani, imeelezwa wana nidhamu nzuri na mitihani yao ya ndani wamekuwa wakifanya vizuri kwa viwango vinavyokubalika.
Matarajio ya baadaye ya Ruhuwiko, Meja Rugwabuza anasema yamo katika mpango wa maendeleo ya shule wa miaka tisa (2006-2015) unaotilia mkazo mambo mengi ambayo ni pamoja na upatikanaji wa maji safi na salama kwa afya za wanafunzi, walimu na wafanyakazi.
Katika kukabiliana na tatizo la utoro wa wanafunzi na kuondoa visingizio vya hapa na pale shule imeendelea mazingira ya shule kwa kuongeza bidhaa kwenye duka la shule, kujenga kibanda cha kutengeneza nywele, kuweka uzio kwenye bweni la wasichana na kumalizia pia bwalo la chakula kwa wanafunzi wa bweni.
Shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1995 inatoa elimu ya sekondari kwa vijana wote kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita na kwa kuzingatia umuhimu wa maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano wameajiri walimu wawili wenye diploma hivyo kuwa na walimu watatu. Matarajio yao ya hivi karibuni ni kuanza kufundisha hata watu wazima muda wa jioni.
"Vijana wengi wanaomaliza kidato cha sita katika shule hii wanajiunga na vyuo vikuu na taasisi nyingine za elimu ya juu.
Pamoja na kujivunia mafanikio hayo shule pia inawawezesha vijana kukabiliana na umasikini kwa kutoa elimu ya ujasiriamali na kompyuta ili mwanafunzi anayehitimu katika shule hii aweze kukabiliana na mazingira yanayomzunguka," anasema Meja Rugwabuza.
Pamoja na mafanikio hayo shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali katika uendeshaji na utekelezaji wa mipango yake ya maendeleo ikiwemo tatizo la kukatika mara kwa mara umeme hivyo kusababisha shule kutumia jenereta. Kutokana na gharama za mafuta kupanda imeongeza gharama za uendeshaji.
Changamoto nyingine ni ujenzi wa ukumbi wa mikutano na mitihani ambao huo uko katika hatua za awali. Nguvu kubwa ya vifaa na fedha inahitajika kwani shule peke yake haiwezi kumudu kwa muda mfupi.
"Tatizo jingine ni kupanda kwa gharama za uendeshaji kutokana na kupanda sana kwa bei ya chakula na vifaa. Hata hivyo, shule imejitahidi kuepuka kupandisha sana gharama za malipo ya ada ili lengo la kuwapatia elimu watoto wengi zaidi liweze kufanikiwa," anaeleza Meja Rugwabuza.
Japo shule hiyo inakabiliwa na changamoto hizo na nyingine kadhaa zinaoendana na uboreshaji wa elimu, Ruhuwiko haijatetereka katika utendaji wake na mfano mzuri ni matokeo yake ya mitihani ya taifa ya kidato cha sita kwa miaka mitatu mfululizo. Matokeo hayo yamechangia kwa kiasi kikubwa kuwafanya watu wengi kuvutiwa na elimu ambayo inatolewa na shule hiyo.
Meja Rugwabuza anasema mafanikio ya shule hiyo kwa kiasi kikubwa yanatokana na ushirikiano mkubwa uliopo baina ya walimu, wafanyakazi, wanafunzi pamoja na wanajumuiya wa shule hiyo akiwemo Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini Dk Emmanuel Nchimbi.
Dk Nchimbi amekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya shule hiyo hususan kwa misaada yake ya mabati na saruji. Aliipatia shule hiyo mabati 240 na saruji mifuko 1000 msaada ambao umefanikisha kukamilika kwa ujenzi wa bweni la wasichana.
"Napenda kukushukuru Mbunge na Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa misaada mbalimbali ambayo umekuwa ukitupatia na mara zote umekuwa mstari wa mbele kwa kutusaidia kila unapopata nafasi ya kufanya hivyo ,"anasema mkuu wa shule mbele ya Dk Nchimbi.
Dk Nchimbi, kwa upande wake aliipongeza shule hiyo kwa kufanikiwa kuongeza ufaulu mwaka hadi mwaka na kuwataka waendelee kuweka mkazo zaidi katika masomo ili kuongeza ufaulu zaidi.
"Nawashauri wanafunzi wa kujenga tabia ya kujiendeleza na kusoma kwa bidii ili waweze kufanya vizuri katika mitihani yao ya mwisho ikiwa ni pamoja na kuchukua tahadhari ili wasiambukizwe virusi vya ukimwi,"anasema.
Amewataka wanafunzi hao wachukue tahadhari mapema na wawe makini na wenye nidhamu kwa kuacha kujiingiza katika vitendo viovu kama uvutaji bangi, uzinzi pamoja na kufanya ngono ili wasiambukizwe ukimwi.
"Nawapongeza kwa mafanikio makubwa mliyopata kwa kuweza kuongeza ufaulu mwaka hadi mwaka, ila nawashauri wanafunzi kuwa makini na msijiingize katika vitendo vitakavyowaingiza katika mtego wa kuambukizwa virusi vya ukimwi kwani taifa na jamii linawahitaji,"anasema.
Naye mwanafunziwa kidato cha sita shuleni hapo Frank Milinga, anasema kutokana na uongozi bora wa shule hiyo wameweza kuonyesha juhudi kubwa katika taaluma, nidhamu, michezo na utawala kwa jumla hivyo kuiwezesha shule hiyo kufanya vizuri katika mitihani ya ndani na nje.
"Bado shule yetu inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ya ukosefu wa vitabu vya kutosha vya kiada na ziada, upungufu wa mabweni, vifaa vya maabara, ukumbi wa mikutano pamoja na gari la shule," anasema mwanafunzi huyo anayetarajiwa kuhitimu mwezi huu.
Wanafunzi hao wamewaomba wadau mbalimbali kuongeza jitihada za kuwasaidia ili kupata ufumbuzi wa tatizo hilo ikiwa ni pamoja na wazazi kuwasilisha michango ya ada kwa wakati
Habari hii imeandikwa na Joyce Joliga katika gazeti la mwanancchi. Nimeona si vibaya kama wasomaji wa blog hii pia wakisoma. Kwani wote tuna nia moja

8 comments:

MARKUS MPANGALA said...

KWANZA; JOYCE JOLIGA ni mmoja ya walimu wangu katika fani ya uandishi wa habari, namkumbuka kwa mengi tangu enzi za kunilazimisha kwenda mikutanoni hasa ile ya wakuu wa kaya hii.
She IS MZURI, CUTE n.k

HAYA KWA PONGEZI ZA RUHUWIKO sina mengi zaid ya kusema popote penye jema kuna jema zaidi. Natumaini mambo yatakuwa mazuri

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

@Mpangala: duh

Hongera Ruhuwiko...au kwa kuwa ni shule ya wajeshi?

Mwanasosholojia said...

Maendeleo huletwa kwa ushirikiano wenye nia moja!Hongera Ruhuwiko!

Majaliwa said...

Hongera sana...elimu kwa kweli ni funguo ya maisha.Tupo pamoja Ruhuwiko!

Anonymous said...

nina mashaka na huo mwaka wa kuanzishwa hiyo shule! hii ni shule kongwe, ilianza na jina la Huduma "service", nakumbuka mimi mwaka 1993 niliomba nafasi ya kwenda kusoma hapo kwa bahati nzuri au mbaya nilipata shule nyingine hivyo sikwenda?

Anonymous said...

Поздравляю вас Старо-Новым годом, желаю вам в новом году успехов и спасибо что вы находите время поддерживать ваш замечательный блог!

Anonymous said...

Растаможка Киев, Одесса
Консультации ВЭД
Дима Литейный
logisticskiev7@yandex.ru
+38 093 318 1567

Anonymous said...

Good post ! Podcherpnul a lot of new and interesting ! Go for a friend in the ladies ICQ :) Your resource for some reason crappy hyped and plohoposeschaem . We advise to promote it by using the XRumer 7 Elite ( Elite Hrumer 7 ) can be obtained here http://x-rumer.ru/ heard a smart program for the promotion of blog sites.