Monday, February 1, 2010

HAKIKA ALIVUNA ALICHOPANDA!

Ndugu wasomaji leo nina kisa hiki nimetumiwa na mdau wa blog ya MAISHA, ili niiweke hapa tupate kujifunza kutokana na kisa hiki. Naomba muungane nami katika simulizi hii.


Ni binti ambaye amezaliwa katika familia inayosifika kwa uchawi pale kijijini kwetu Matombo Morogoro. Mama yake alikuwa akiogopwa sana na watu kwa kuhofiwa kuwa ni mchawi wa kutisha.

Nakumbuka nilisoma na mmoja wa wadogo wa huyo binti, na kuna siku niliwahi kumpiga mdogo wake baada ya kuniibia kalamu yangu tukiwa darasa la nne nikatishwa kwamba nitalogwa, niliogopa sana.

Niliondoka kijijini mara baada ya kumaliza darasa la saba na kuja jijini Dar Es Salaam, na huo ndio ukawa ni mwisho wangu kuonana na binti huyu. Naambiwa kuwa alikuja mjini na kuishi na dada zake maeneo ya Mwenge, na baadae akawa akijishughulisha na biashara ndogondogo.

Inasemekana alikuwa na kawaida ya kutembea na wanaume za watu kiasi cha kuhararisha ndoa kadhaa hapa jijini. Aliendelea na mchezo huo mpaka alipokuja kukutana na huyu mzee ambaye alikuwa na mkewe na watoto wakubwa tu. Huyo mzee alikuwa na familia yake maeneo ya Kinondoni na alikuwa na kazi nzuri sana, katika taasisi za Kimataifa.

Alikutana na huyo mzee maeneo ya Ubungo ambapo alikuwa na nyumba yake ameipangisha na alikuwa na kawaida ya kwenda kuitembelea nyumba yake kila mwisho wa juma.

Siku ya kukutana, ilikuwa huyu binti amemtembela rafikiye mwenye Grocery maeneo hayo ya Ubungo, na wakati wakiwa wanapiga soga ndipo yule mzee akafika pale kujipatia kinywaji wakati akiwasubiri mafundi wake ambao walikuwa waje kufanya marekebeisho kwenye nyumba yake.

Mzee akamuona mtoto wa Kiluguru ametulia akinywa soda yake baridi, mzee udenda ukamtoka na akaomba kujiunga na meza ile, alikaribishwa na binti huyo, na baada ya kufahamiana na kupata vinywaji kadhaa, na huo ndio ukawa mwanzo wa binti kuanza uhusiano na mzee huyo.

Wakati uhusiano wao ukiwa katika kilele, baada ya kumpagawisha mzee mzima na mapenzi motomoto, na mahaba ya Kiluguru, binti hakulaza damu, alihakikisha anamshika huyo mzee vilivyo, na mzee kutokana na kunogewa na penzi la binti akaamua kumpangishia nyumba na kumfungulia biashara ya Grocery maeneo ya Ubungo External.

Inasemekana mzee alishikwa vilivyo na binti wa Kiluguru na ili kuhakikisha anamshika vizuri akamwambia mzee kama anampenda auze nyumba yake ya Ubungo kisha amjengee nyumba yake mwenyewe ambayo itakuwa na jina lake, na kutokana na mzee kunogewa na penzi la binti akakubali bila kipingamizi, na nyumba ikauzwa na binti akajengewa nyumba yake huko Kinyerezi.

Binti hakuridhika, akamshawishi mzee wafunge ndoa, na ili kuweka mambo sawa akabadili dini kutoka dini yake ya kuzaliwa ya Kiislamu na kuwa mkristo, lakini je dini ya Kikristo inaruhusu ndoa za Mitala, hili likawa ni swali ambalo wapendwa hao liliwasumbua…….any way hiyo haikumsumbua binti. Akajua tu wakati utafika.

Mzee huyo ambaye ni Mhehe wa kule Iringa ambaye alioa mke wa Kimanyema kutoka kule Kigoma, akajikuta akipewa mtihani mwingine na binti wa Kiluguru. Binti akamtaka asiwe na zamu ya kulala kwa mke mkubwa, kwani mzee alishaihalalisha nyumba ndogo kwa mkewe na mkewe hakuwa na la kusema, aseme nini wakati alishaanza kuonja uchungu wa kugawana penzi na nyumba ndogo, kwani mume alikuwa akilala nje mara kwa mara na alikuwa haihudumii familia kama zamani, kwa kifupi mume alishaanza kuitelekeza ndoa yake.

Sasa safari hii binti hakutaka tena kugawana penzi na mke mkubwa,alishaonja asali na sasa alitaka kuchonga mzinga ili arine asali mwenyewe, na ili kujihakikishia kuwa anamshika mzee wa Kihehe alimtaka mzee achague, ama yeye au mkewe wa ndoa, hapo binti alikuwa na sauti maana kajengewa nyumba na mradi wa Grocery kafunguliwa. Mzee hakuwa na ubishi akamkubalia binti, na toka siku hiyo mzee akawa amekata mguu kwenda kwa mkewe Kinondoni akahamia Kinyerezi kwa binti.

Kutokana na kuitelekeza familia yake kule Kinondoni, watoto nao wakasimamishwa shule na kila wakienda kwa baba yao kumweleza kuwa wanatakiwa kulipa ada za shule walikuwa wanafukuzwa na binti kama mbwa.

Binti hakuridhika bado alitaka makuu, mara akamwambia mzee aache kazi ili wasaidiane kuendesha mradi wao wa Grocery, na mzee hakuwa na kipingamizi, akamkubalia binti na hivyo kuacha kazi. Sasa binti akaridhika akawa amemshika mzee vilivo, mzee akawa haruhusiwi kutoka kwenda popote bila ruhusa ya binti, na akawa kazi yake ni kukaa kaunta kutoa vinywaji.

Duh! Mzee alikuwa kama kondoo aliyenyeshewa na mvua, alikuwa akifokewa na binti kama mtoto, binti alikuwa ameshika hatamu. Maisha yaliendelea na binti mambo yake yalikuwa shwari kabisa.

Inasemwa kuwa, usije ukadhani unapomtendea mtu ubaya basi utapotea moja kwa moja, jua kwamba ile nguvu hasi uliyopanda ipo siku itarudi katika njia ambayo huwezi kufahamu hata siku moja na ni lazima itakuumiza na inategemea tu ulitenda nini . Leo hii wapo watu wanaishi katika madhila makubwa kutokana na nguvu hasi walizozipanda hapa duniani. Inasemwa kuwa chozi la mtu haliendi bure, na hiyo ilikuja kudhihirika hivi karibuni.Inaweza kuwa ni nasibu tu, lakini historia inaweza kutuhukumu.Siku moja wakati binti anatoka bafuni kuoga na wakati huo mzee alikwenda kufungua Grocery kama kawaida yake huku akimwacha binti akijiandaa kumpeleka mama yake mzazi hospitali kutibiwa miguu, kwani mama yake alikuwa akisumbuiwa na ugonjwa wa miguu na binti alimfuata huko kijijini ili kumleta mjini atibiwe.

Alipokuwa akitoka kuoga aliteleza kwenye sakafu ya Tiles na kuanguka ambapo alijigonga kichwa kwenya ukuta wa bafuni na kupoteza fahamu.Alikimbizwa hospitali ya Muhimbili akiwa amepoteza fahamu na kulazwa chumba maaluma kwa wagonjwa mahututi maarufu kama ICU.

Alikaa kwa siku tisa bila kupata fahamu na siku ya kumi ndipo akapata fahamu ambapo nilikwenda kumuona, nilipomuangalia sikuona dalili za binti kupona kwani alionekana dhahiri kuyakabili mauti.

Nasikitika kuwa siku ilyofuata binti alifariki majira ya saa kumi na mbili alfajiri. Msiba uliwekwa kwa dada yake mkubwa huko Mwenge, na yule mzee aliambiwa afungashe nguo zake tu na kuondoka katika nyumba ya binti huyo kwa madai eti ni nyumba ya binti aliyoijenga yeye mwenyewe kutokana na biashara zake.

Masikini yule mzee alilia kama mtoto mdogo, sio kwa kufiwa na binti, nyumba ndogo yake bali kwa kunyang’anywa nyumba yake aliyomjengea binti. Alichaoachwa nacho ni biashara ya Grocery peke yake.

Katika msiba huo kulizuka minong’ono kuwa binti kafanyiwa uchawi na mke wa mzee. Lakini hata hivyo mama wa binti pamoja na mabinti zake ambao nao wanasifika kuwa ni Magwiji wa Uchawi walidai kuwa wanamjua aliyemuua mdogo wao, na wakaahidi kuwa wakishamzika watajua cha kufanya.

Kulikuwa na maneno mengi yalisemwa katika msiba huo, kwani kila, mtu alisema lake. Hata baadhi ya marafiki zake walidai kumuonya kuwa mchezo anaoucheza utamletea maumivu, lakini binti alikuwa akijibu kwa kiburi kuwa hakuna atakayemuweza kwa kuwa ameaga kwao. Pia yuko binti mmoja alinukuliwa akisema kuwa hata yeye huchukuwa waume za watu lakini mwenzao alizidi. Kwa maneno yake mwenyewe alisema, “Hata mie nachukua wanaume za watu lakini ikifika jioni, mwenzangu namruhusu arudi kwake, lakini huyu mwenzetu alizidi, yaani alimnyang’anya mwenzie mumme wake hivihivi, hata mie ningemloga”.

Hata hivyo baadhi ya waombolezaji walionekana kupuuza madai hayo na kusimamia dini kuwa ni mapenzi ya mungu kwa binti huyo kufariki, kwani kila nafsi ni lazima itaonya mauti kama ilivyosemwa katika vitabu vya dini.

Binti alisafirishwa kupelekwa kwao Matombo Morogoro na kuzikwa. Mzee wa watu kaachiwa umasikini maana haijulikani kama aliweza kurejea kwa mkewe wa ndoa baada ya binti kufariki au alitafuta nyumba na kupanga kwani alishafukuzwa kwenye nyumba na ndugu wa binti na kazi alishaacha.

Dada Yasinta naamini wengi wanaweza kujifunza kwa kisa hiki ambacho ni kweli kimetokea hivi karibuni.

13 comments:

Bennet said...

Huyu dada na mauchawi yake ndio alimpumbaza mzee wa watu akaiacha familia yake

Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti! said...

Nanukuu: "Inasemekana alikuwa na kawaida ya kutembea na wanaume za watu kiasi cha kuhararisha ndoa kadhaa hapa jijini."

Kwani KUTEMBEA NA MTU barabarani ni VIBAYA? :-( Au kuna maana nyingine hapa? :-(

Haya kazi kwenyu WADADA na VIDUME wenye kufakamia visivo vya kwenyu :-)

Mt. Simon Upo?

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

@bennet inaonekana wewe unalogega!!!!!!!!

@chacha, ingekuwa kiigeleza angesema ku-SEX ila kiswahili eti kutembea siokutiana viungoa au kut***$#, naogopa kusema comment yangu isije ondolewa

ila sio uchawi, ni mapeeenzi, kuna tarafa kule kwetu inaitwa Katerero na kuna mpka shule ya msingi nk, mtu kama Yasinta akipelekwa pale lazima ahame kabisaaaa familia (I hope my new wife wont read this)

ila kudondoka bafuni ni ajali kama nyingine na kufa hakumpi binti funzo lolote lile, sio uchawi jamani, ni ufundi, kuna wengine wanakatika!!!

Koero Mkundi said...

Naamini hii mada kamala na Chaha Wambura watakuwa wamejifunza kitu hasa Kamala maan ndio kawowa juzi tu.
Kwenu wanaume mliioa, inabidi muwapende wake zenu, muwaheshimu na kuwajali, msikodolee wmimacho yenu kwa wanwake wengine kwani sisi akina Koero ambao hatujaolewa tuna kampenni ya kuwapumbaza na kuwachukua kabisaa, msahau ndoa zenu kama kamala alivyosema nje kuna Karufundi ambapo ukionja tu umekwenda na maji.....utahama nyumba yako kutokana na karufundi ka nyumba ndogo.....LOL

Lada tu niseme kuwa tabia hii ipo sana hapa jijijni kwani wenyewe wansema kuwa mume wa mtu mtamu maan hana Dusturbance, akirudi kwakke kimya hata kama una buzi lingine aaaa..unajimwaga tu, na wanadai eti mume wa mtu ni rahisi kumcuuna...
Mie simo naamini ujumbe umefika...LOL

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

KOERO

Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti! said...

@Koero: on the contrary sijajifunza kitu kwa kuwa hayo ni ya kawaida kabisa kwa kuwa kwa Mkurya kuwa na wake wengi na masuria ni SUNNA :-(

Kinachogomba hata hivo ni kwa huyo mbinti ambaye alidhani fedha na kumkalia huyo mume wa mtu ni tija kwake. Ukikula ukaondoka si inatosha?

Kung'ang'ania kuwa amuache mkewe awe naye tu ni sawa na mimi kutaka kuzaa na KOERO ilihali najua mtoto huyo ataishia kuwa na baba mwingine :-(

Lulu said...

ila sio uchawi, ni mapeeenzi, kuna tarafa kule kwetu inaitwa Katerero na kuna mpka shule ya msingi nk, mtu kama Yasinta akipelekwa pale lazima ahame kabisaaaa familia (I hope my new wife wont read this)

Hivi Kamala una mke mpya au una mke??? Kusema your new wife; means you have old wife already.

Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti! said...

@Lulu: habari ndo hiyo :-(

muulize swali hilo KOERO :-)

Yasinta Ngonyani said...

Nanukuu:- "ila sio uchawi, ni mapeeenzi, kuna tarafa kule kwetu inaitwa Katerero na kuna mpka shule ya msingi nk, mtu kama Yasinta akipelekwa pale lazima ahame kabisaaaa familia (I hope my new wife wont read this)" Kamala hivi hapa ulikuwa na maana gani hasaaaaaa????

Kweli tulioolewa na tusioweza kusema kwa mtindo huu hatuna la kusema. Hapa siwezi nikasema kama ni uchawi au ni mapenzi yalikuwa katika hawa watu.Ila niliposoma hapa kweli ndipo niliposhikwa na huruma pia mshangao nanukuu "Kutokana na kuitelekeza familia yake kule Kinondoni, watoto nao wakasimamishwa shule na kila wakienda kwa baba yao kumweleza kuwa wanatakiwa kulipa ada za shule walikuwa wanafukuzwa na binti kama mbwa." mwisho wa kunukuu:- Huyu binti inaonyesha alikotoka hakuwa na maisha ya kawaidi kwani asingeweza kuwatendea watoto wale hivyo. Kwa hiyo kwako hapo kilikuwa ni pesa tu na inaonekana alishatoa taarifa kwako ndio maana mzee wa watu alinyanganywa kila kitu isipokuwa nguo zake tu. Kweli kuna wanawake/binadamu wakatili.

Anonymous said...

Lulu sio kwamba Kamala ana mke bali ana wake wengi, si unamuona jinsi alivyo tu kwenye picha?
Huyo bwana ni kifyagio kweli kweli... mie namjua vizuri tu,,,LOL

Koero Mkundi said...

Asiye na jina, mie simo!!!
Kwa mila na desturi za kiafrika kuwa na wake wengi sio dhambi, ila hizi dini ndio zinawafanya watu wawe wanafiki, mtu kama Chacha ameweka wazi kuwa kwao zsoio dhambi ni suna, bali kama anataka anajifanya kuw ahamnazo....LOL
kaka sema usikike, una wake wangapi?

nyahbingi worrior. said...

Hivi ni kweli?

Mija Shija Sayi said...

@Nyahbingi hivi ni kweli nini sasa na habari yenyewe ndiyo hiyo..

Kweli nimeamini roho mbaya au nzuri hukurudia mwenyewe. Asante mleta mada.