Thursday, August 14, 2008

AGOSTI 15, 2008 MAISHA YANGU


Kila nikiwaza sipati jibu, kwani maisha yangu ni tofauti sana na ndugu zangu. Mara nyingine naona kama nimetokea hewani (yaani sina ndungu na pia sina mama wala baba) niliondoka nyumbani mapema. Nikiwa na miaka 16, nilianza kujitegemea mapema sana kuliko ndugu zangu. Sijaishi sana na wazazi wangu na sijawategemea sana. Sijafaidi kuwa mtoto wao kama mwenzangu. Na pia sijawategemea sana kwa jambo la uchumi ila kwa namna nyingine. Yaani kama nilivyokuwa shuleni nilipata pesa za matumizi labda kama 200-500Tsh, na hiyo ilikuwa ni matumizi ya mwezi mzima au zaidi. . Wakati nilikuwa mdogo nilikuwa na kanga upande mmoja, vyupi viwili, magauni mawili moja la kuchezea na moja la jumapili. Nilikuwa narithi magauni ya mama, anapunguza na ananishonea mimi. Viatu nilikuwa nasikia jina tu nikipata ndala (za matairi ya gari) nilikuwa najisikia kweli. Fikiria mwenyewe kwenda mstuni kutafuta kuni bila viatu. Unachomwa na miba, unaweza kukanyaga nyoka n,k. Sio kusema wazazi wangu hawakuwa na uwezo hapana. Ila hawakuona kama ni muhimu watoto kuwa na vitu vingi. Pia nilipokuwa mdogo mambo ya kunywa soda, kula pipi hayakuwa kabisa kichwani mwangu. Kwani hatukuzoeshwa Sio kusema maisha yangu yalikuwa mabaya hapana. Mahitaji muhimu nilipata kama kawaida. Lakini sasa watoto wengi hawaridhiki na gauni/shati au suruali moja. Pia wanataka viatu. Na halafu wanataka kila mtu na chumba chake cha kulala. Mimi nilikuwa nanalala chumba kimoja na kitanda kimoja na kaka yangu . Kila mtu alionyesha kichwa upande wake. (mzungu wa nne) Lakini leo mdogo/ndugu zangu wana karibu kila kitu. Kwa jambo hili mara nyingi najisikia nipo peke yangu hapa duniani.

Maisha yangu kwa ujumla hayajawa rahisi. Kipindi kile nasoma kuwa karani nilipata shida sana mimi, asubuhi nilikuwa naamka kuandaa chai na baadaye kwenda shule kwa mguu labda kama saa moja au dakiki 45 hivi. Mchana nilikuwa nabaki shuleni, kwani mwanzoni nilikuwa narudi na sikupata chakula. (Bali ilikuwa kwenda kuchota maji unajua tena foleni kubwa.) Niliporudi na maji kuanza kuandaa chakula, na baadaye muda wa kurudi shuleni umefika. Basi ni kugeuza tena tu bila kula kwani ningekula basi ningechelewa. Nilikuwa naishi kwa "ndugu" lakini nilikuwa kama MFANYAKAZI (mama wa nyumba alikuwa mkatili mno sio mchezo). Jioni baada ya shule kufika tu bila kula kitu amekwishaandaa mahindi kwenda kusaga na niliporudi tu ni kuchukua ndoo kwenda kuchota maji na pia kuandaa mboga. Usidhani hapakuwa na watoto wao, walikuwepo. Lakini walikuwa wanacheza, kufanya homework au walikaa tu. Kila siku hivyohivyo kwa muda wa miaka 2. Labda ndio maana maisha yangu sio kama ndugu zangu, na ndio maana sikuweza kufanikisha masomo yangu vizuri. Kwa namna nyingine namshukuru (mama wa nyumba) amenifundisha jinsi ya kujitegemea, kuishi peke yangu. Ila jamani tembeeni mwoone mmh maisha ni safari ndefu.

6 comments:

Unknown said...

Hongera sana kwa kwa moyo wako wa kupambana bila kukata tamaa naamini imani yako na uvumilivu umekufikisha hapo ulipo.

Ni kweli shida na matatizo ni stepping stones katika mafanikio yetu na mtaji kamili wa baraka za Mungu.
Naamini utazidi kuwa mwanamke wa mafanikio zaidi na kuwa mfano wa wengine.
Nimebarikiwa sana na historia fupi ya maisha yako.

Upendo daima.

Yasinta Ngonyani said...

uhongise kaka MBilinyi. Kwani kuna wakati inabidi kuvulia mvumilivu hula mbivu. Amen

Anonymous said...

dada yasinta utafika mbali kwa uvumilivu wako,historia ya masha yako ni shule kwa wapiganaji wengine kuwa wasikate tamaa.
james.
jingo2020@yahoo.com

EDWIN NDAKI (EDO) said...

Mhh..hakika inapendeza sana mtu kutumia muda wake kushirikisha marafiki kule alikopitia.

Binafsi kuna mengi sana nimejifunza katika historia yako.Na kikubwa zaidi ..ni uwazi na ukweli uliotumia.Amini ni ujasiri wa hali ya juu.

Nakutakia kila jema unaweza kufika mbali zaidi..endelea

Yasinta Ngonyani said...

asanteni sana kaka zangu kwa maoni yenu mazuri

Anonymous said...

Hakuna njia iliyosalama kuelekea katika uhuru wa maisha ya kweli,sote tunapita katika bonde la uvuli/mateso makali. tofauti ni namna ya kukutana nayo. hakika umeshinda wl usilie tone kumbuka simulizi za Tupac alisema 'baby don't cry never give up you was born keep your head up. kila la heri dadangu