Wednesday, September 8, 2010

Upweke, Je wewe umewahi kujisikia mpweke??


Katika maisha haya ya kublog tumekuwa kama vile ndugu, mmoja akiadimika bila taarifa basi twapata wasiwasi. Nimewaza na kuwazua hawa binadamu wamepatwa na nini?. Na mwisho najisikia UPWEKE. Na katika pita pita zangu kama kawaida nikakutana na shairi hili nikaona si mbaya hata kama tumesoma lakini kusoma tena na tena ndio kukumbuka mambo, haya karibu !!. Na shairi hili lina toka kwa mtani wangu Fadhy Mtanga.

Pale unapojikuta u-mpweke, je? ufanyeje?

Upweke jama adhabu, upweke unasumbua,
Upweke ni maghilibu, kukufanya kuugua,
Watamani wa karibu, nenolo taelijua,
Upweke.

Upweke hutesa sana, umpendaye awe mbali,
Utamuwazia sana, hata mara alfu mbili,
Kwa usiku na mchana, maumivu ni makali,
Upweke.

Upweke unakondesha, chakula hukitamani,
Upweke unahenyesha, simanzi tele moyoni,
Homa pia hupandisha, na mwokozi humuoni,
Upweke.

Upweke tele mateso, hata machozi kulia,
Moyoni ni manyanyaso, nao moyo kuumia,
Wala si kimasomaso, kwani huleta udhia,
Upweke.

Upweke ni kama jela, huleta nyingi simanzi,
Huwezi hata kulala, maisha tele majonzi,
Utapiga hata sala, uruke vyote viunzi,
Upweke.

Upweke sawa na shimo, mtu ukatumbukia,
Nako shimoni uwamo, wateswa nayo dunia,
Kwani hauna makamo, kuweza kuvumilia,
Upweke.

5 comments:

Mija Shija Sayi said...

Nimeipenda kauli yako Yasinta, "...kusoma tena na tena ndiyo kukumbuka mambo..."

Laiti kama Watanzania tungelizingatia hili, tungekuwa mbali sana.

Samahani nimetoka nje ya mada.

MARKUS MPANGALA said...

nikiwa na yasinta hakika sina upweke,
bila simu au pepe,
uarfiki kidete,
leo na kesho daima milele,
mani iwe nawe daima mwana wa Gervas,
uwe na wakati poa sana usiowaze upweke,
utaniambukiza upweke,
amani iwe nawe

Koero Mkundi said...

Najua dada mie ndiye niliyeadimika bila taarifa.
Dada yangu mpenzi, kuwa kwangu kimya sio kwamba nimepatwa na jambo baya, bali ni majukumu yamenizidi.

Ninahitaji muda mwingi kujishughulisha na masuala ya kifamilia zaidi, ambayo kwa kweli ndiyo yaliyonileta hapa Arusha.
Nikijichimbia huko Karatu vijijini, mtandao unakuwa adimu na hivyo kutopatikana kirahisi.

mawasiliano yangu na wewe pamoja na wanablog wenzangu ni pale tu ninapokuwa hapa mjini Arusha.

Usiwe na wasiwasi mie ni mzima wa afya tele na wala siumwi typhoid....LOL

Ningependa kuwajulisha wanablog wenzangu na wasomaji wa VUKANI kuwa bado ningalipo.....

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

this tym mimi napitia upweke mgumu, nimezowea kusafiri na kumpigia simu maiwaifu na sasa nakutana na tsunami la upweke, ni wiki ya pili wife na mwanetu wamesafiri yaani kidume niko alone home, wewe I cant xpress what am going thru,

an empty street,
an empty house
a hole inside heart
am all alone,
rooms are getting smaller
........

emu-three said...

Heri mimi sijasema, nikisema nina nongwa.
Upweke ulinisakama, Nikabaki na msigwa.
Niliandika hata zama, labda akaja bingwa
Upweke hutesa roho,usiombe kuukwaa.