BAADHI ya watahiniwa katika shule ya Msingi, Miburani, Temeke, Dar es Salaam wakishangilia baada ya mtihani wa mwisho wa kuhitimu Elimu ya Msingi. (photo: Bashir Nkoromo).
Vijana hawa wananikumbusha siku tuliyokuwa tukiisubiri kwa hamu kubwa sana, 'kumaliza shule' tukiamini ati baada ya kuondokana na adha ya kudamka alfajiri, kushikana mashati na 'konda', kuwahi 'namba' na 'mstarini'... yaani ndoto za kila aina alimradi kujiaminisha usumbufu utakuwa umekwisha kabisa.
Tulijiona sisi ndiyo 'top' hakuna mwingine duniani kama sisi. Hisia za 'kumaliza shule' na kubaki nyumbani wakati wengine wanaamka asubuhi wakiwa na heka heka za ama kwenda shuleni au kazini, zilitutawala.
Siku hizi, tofauti na zamani nilipomwona 'madha mnoko', huwa najivuna sana kuwa na Mama asiye na longolongo wala 'kukopesha maneno' kwani, aliponisikia nikijitapa eti 'nimemaliza shule' siku moja aliniambia,
"...wewe, umemaliza shule ipi? Subi, hujamaliza shule. Umehitimu Elimu ya Msingi tu. Umeimalizaje shule wakati hujafika hata Sekondari? Umesahau methali mlizofundishwa, Elimu ni bahari; Elimu haina mwisho? au ulidhani ukishakariri na kuandika kwenye daftari ukafunga na ulichofundishwa kimefungwa kwenye mkoba? Yaani mwalimu akishafuta ubao na kwenye akili yako vinafutika? (kichwani mwangu nawaza, 'kwani si ndiyo kazi ya shule? unaandika, mnakusanya madaftari, mwalimu anatia 'pata' kama hesabu umekosea fanya masahihisho tu, basi').
Umevuka madarasa ya shule ya awali, sababu ya kuitwa 'msingi' ni kwa kuwa umeweka msingi wa elimu na maisha yako. Ni sawa na kujenga nyumba. Ili iweze kusimama imara, lazima msingi uwepo, tena uwe ni msingi ulio imara. Msingi ndiyo kigezo cha uimara wa nyumba. Umeweka msingi, bado kuta, madirisha, paa, na fenicha na vifaa vingine vya ndani. Lakini la muhimu ni msingi. Ikiwa uliweka msingi imara, nyumba yako itakuwa imara, utaweza kujenga nyumba kuuuubwa au hata orofa, inategemea na uimara wa msingi wake."
Ni baada ya kwenda kwa Bibi na kuwatembelea ndugu, ninarejelewa kauli ya Mama, 'hujamaliza shule' nhe he, ndipo nilipotia akilini, kumbe tulichokuwa tukifurahia 'standadi seven kumaliza shule' ilikuwa ni furaha ya muda tu, tena ya kitoto, bado ilikuwepo kazi kubwa mbele yetu; Kuna kusaidia kazi za nyumbani sasa zaidi ya wengine na; Kuna kuchukua fomu za shule za "private" tena kujaza zaidi ya moja, na kwa ambaye matokeo ya maendeleo yake shuleni kila mhula hayakuwa mazuri, hali kwake ilikuwa ni mbaya, yaani atazijaza fomu za 'private school' hata tano ili walao abahatishe moja ikiwa atakataliwa kwingineko. Nakumbuka nilizijaza mbili, Majengo Secondary na Uru Seminary. Kisha kuna kufanya tena mtihani wa kuomba kujiunga na shule hizo na, ni lazima ufaulu, la sivyo uaibike kwa kuzurura mtaani na kufanya kazi nyumbani wakati wenzio wanaongozana kwenda na kutoka shuleni! Shabash! Hakuna kumaliza shule!
Naam, huo ndiyo wakati nilipoanza kufahamu kuwa ninayahama maisha ya utoto na kuingia ujanani.
Hongereni vijana mliohitimu elimu ya msingi, shule bado hamjaimaliza. Elimu haina mwisho!
Nimeipenda sana simulizi hii kwani imenikumbusha pia enzi zile namaliza darasa la saba. Ni kweli yaani ile asubuhi kuwahi namba ukichelewa tu viboko hivyo. Halafu kukimbia mchaka mchaka, nakumbuka baada ya mchaka kchaka kulikuwa hakuna tena kuoga maji ni kuaa hivyohivyo darasani na mijasho inakutiririka. Mweeh kwa kweli tunatoka mbali na kweli elimu haina mwiho. Na ukitaka kujua nilipoipata basi unaweza kubonyeza hapa
1 comment:
Nakumbuka nilipomaliza mimi tulikuwa tukijiita LY, manake LAST YEAR, sijui lasy year ilikuwa ikimaanisha nini, kwasababu hata sisi tuliliga hilo neno kwa waliopita.
Ni furaha kwa kweli, na mtu huwa hujui nini maisha ya mbeleni, kwani bado una ule `udekaji kwa wazazi' Baba anacho hiki, mama anafanya kazi...unajiona huna shida, kumbe kuna maisha mbele, hiyo lasy year ilikuwa geresha...!
Post a Comment