Monday, September 27, 2010

LAITI KAMA NINGEKUFAHAMU KABLA.........HADITHI YA KUFIKIRIKA


Miaka mitano iliyopita nilikuwa natafuta mke wa kumuoa ambaye angekuwa na sifa nizitakazo. Nilikuwa natafuta msichana mzuri wa wastani maana sikutaka kuoa mke mzuri kupindukia asije niua bure kwa presha na jakamoyo. Nilikuwa natafuta binti atakanikubali kama nilivyo na mapungufu yangu na mimi niliahidi kumkubali na mapungufu yake ili mradi asiwe ni mwenye tamaa ya kupenda sana pesa na mfujaji.
Awe na staha na anayeweza kukabiliana na hali yoyote, niwe nacho, nisiwe nacho au kwa kifupi tupendane kwa shida na raha.

Pamoja na sifa nyingine ndogo ndogo, lakini muhimu ni upendo na amani vitawale nyumbani kwangu.
Hatimaye nilimpata Binti Yasinaty, na kukutana kwetu kulikuwa ni kama muujiza, nakumbuka siku hiyo nilipanda daladala nikielekea kazini na kwa bahati kiti nilichokalia kilikuwa ni cha mwisho upande wa dirishani. Wakati nakaa nikahisi kukalia kitu kigumu, nilipopapasa ilikuwa ni simu mpya kabisa tena ya bei mbaya kama sikosei wakati huo ilikuwa inauzwa shilingi laki nne kwa wakati huo, kumbuka kwamba hapa nazungumzia habari ya miaka mitano iliyopita.

Kwa bahati mbaya simu ile ilikuwa imezimwa, na nilipojaribu kuiwasha iliwaka na kuzima kuashiria kwamba betri yake iliisha chaji. Niliiweka mfukoni na kujiuliza kuwa ile simu ilikuwa ni ya nani, sikusikia mtu kulalamika kwamba amepoteza simu na niliogopa kuuliza maana nilichelea mtu kujitokeza na kusema kwamba ni yake ilihali sio ya kwake.

Nilifika ofisini na kuanza kazi, baadae nilimuita katibu muhtasi wangu na kumwomba anisaidie kutafuta chaji ya ile simu kwa kuwauliza wafanyakazi pale ofisini, nilikuwa na shauku ya kumfahamu mwenye simu ile ili nimrudishie, kwani nilikuwa namuoana dhahiri akisikitika kwa kupotelewa na simu yake, kwa jinsi ilivyoonekana ilikuwa bado ilikuwa ni mpya kabisa na ilikuwa haijatumika zaidi ya wiki.

Katibu wangu muhtasi hakufanikiwa kuipata ile chaja ya ile simu. Niliweka ile simu kwenye droo ya ofisini kwangu ili jioni nikitoka nipitie nayo kariakoo ninunue chaja yake.
Ilipofika jioni alikuja mchumba wangu ambaye tulitofautiana wiki iliyopita na kuamua kutengana naye. Sikutaka kuonana naye na nilimwambia katibu wangu muhtasi amwambie kuwa niko bize na sitaki afike tena pale ofisini kwangu.

Ukweli ni kwamba nilimpenda sana lakini kitendo chake cha kukuta mwanaume mwingine chumbani kwake tena akiwa amelala kitandani kwake halafu anajidai kunidanganya kuwa eti ni binamu yake hakikunifurahisha kabisa. Nakumbuka nilisafiri kikazi kwenda Mbeya, na ilikuwa nikae kule kwa wiki moja, lakini ilitokea dharura huku Makao makuu Dar ikabidi nirudi baada ya siku mbili tu na nilipofika kwa kuwa ilikuwa ni usiku kama saa mbili niliamua kupitia kwa mchumba wangu ambaye alikuwa akiishi Mwengeili kupata chakula cha jioni kabla sijaenda kwangu Maeneo ya Sinza. Nilipofika nilimkuta akiwa nje akipika, lakini aliponiona alishtuka sana akabaki kinywa wazi, hakunipokea alibaki ameduwaa, nikahisi kuna jambo. Nilimsalimia alijibu kwa wasiwasi nilipotaka kuingia ndani, alinizuia, na huku akiongea kwa sauti yenye kutetemeka aliniambia eti ndani kuna binamu yake kaja na amejipumzisha kitandani kwake, nilishtuka. Niliiingia ndani moja kwa moja na kumkuta kijana amelala kitandani nilipomuhoji kuwa yeye ni nani na anafanya nini pale akaniambia kuwa yuko pale kwa girlfriend wake na alitaka kujua eti mimi ni nani..Sikutaka kuzua ugomvi, nilimwambia kuwa pale ni kwa dada yangu na nilifika kumsalimia, nilimuomba radhi kwa kuingia bila hodi, ila nilimshauri aharakishe kulipa mahari ili tujue kuwa dada yetu anaye mtu, ili wakati mwingine tubishe hodi, niliongea kwa utani, yule kijana alimsifia sana mchumba wangu kuwa ni mzuri hasa na anajua kupenda, alibwabwaja mambo mengi na upuuzi wao wanaofanya nikiwa sipo, niliongea naye kwa utani mwingi na kuaga na kuondoka, lakini moyoni roho ilikuwa ikiniuma kweli. Nilikuwa nampa yule binti karibu kila kitu alichohitaji, lakini kumbe hakuridhika bado akawa na mwanaume mwingine.

Nilitoka na nilimkuta kajiinamia pale nje, sikumuaga nikaondoka zangu. Nilipofika nyumbani nilimtumia ujumbe mfupi wa simu ya kiganjani nikimwambia kuwa kuanzia siku hiyo ilikuwa ni mwisho wa uhusiano wetu. Hakijibu na siku iliyofuata alipiga simu lakini sikupokea, alibadilisha namba na nilipopokea na kugundua kuwa ni yeye nilikata simu, baadae zilifuata ujumbe kadhaa wa simu yake ya kiganjani akitaka tuonane ili tuyamalize. Sikumjibu. Na ndio akaamua kuja ofisini.

Nilimpigia simu katibu muhtasi wangu na kumuamuru amwambie yule binti aondoke pale ofisini. Niliambiwa kuwa amekataa, nilimpigia simu dereva wangu na kumuuliza kama gari limeshatoka gereji, akanijibu kuwa gari litatoka baadae kidogo, nikamwambia akitoka gereji aende nalo nyumbani kisha kesho asubuhi anifuate. Gari langu liliharibika siku mbili zilizopita, hivyo nililazimika kupanda daladala au taxi kama nikiwa na dharura. Niliondoka pale ofisini nikimuacha akiongea na katibu wangu muhtasi na kuondoka zangu. Nilikodi taxi na wakati niko njiani nikakumbuka kuhusu ile simu, lakini niliisahau ofisini, kwa hiyo sikupitia kariakoo tena. Nilikwenda moja kwa moja hadi kwa rafiki yangu anayeishi maeneo ya Kijitonyama na kupoteza muda huko hadi usiku ndio nikarudi nyumbani.

Siku iliyofuata dereva alinifuata na kunipeleka ofisini, nilipofika nilimpa ile simu na kumtuma akanitafutie chaja ya ile simu. Baadae alirudi akiwa na chaja ya simu ile na kunikabidhi. Niliichaji na ilipojaa niliiwasha ziliingia ujumbe kadhaa kutoka kwa watu waliokuwa wakimtafuta mwenye simu ile, nilipozisoma niligundua mwenye simu ile alikuwa anaitwa Yasinaty, nilikata shauri nimpigie mmoja wa watu waliokuwa wametuma ujumbe ambaye alionekana kuwa ni mama yake. Nilipompigia simu na kuuliza kama anamjua mwenye simu kwanza alitaka kujua mimi ni nani na kwa nini simu ya mwanaye ninayo mimi. Nilimsimulia kila kitu na nilimuomba ampe mwanae namba yangu ya simu na kumuomba amwambie awasiliane na mimi ili nimpe simu yake. Yule mama alifurahi sana na kunishukuru sana, kumbe ile simu Yasinaty alitumiwa na kaka yake aishie Ughaibuni.

Mchana nilipigiwa simu na Yasinaty na tuliongea mengi na alionekana ni binti mchangamfu kweli, alinimbia kuwa anafanya kazi kwenye Hoteli moja ya kitalii maarufu iliyoko katikati ya jiji, nilimuahidi kumpitia kazini kwake jioni nikitoka ofisini.
Nilimpitia jioni na kama alivyonielekeza kuwa yuko reception nilimkuta pale akimalizia kazi na aliniomba nimsubiri kweye kijimgahawa kilichopo pale ndani, kwa kuwa mimi sio mnywaji wa pombe niliagiza juisi ili kumsubiri. Baadae alinipitia pale nilipokaa na kunimbia kuwa anatoka hivyo tukutane nje kwani anakwenda kubadili sare za kazini. Alitoka na kunikuta nje nikimsubiri, alipanda kwenye gari na nilimuomba dereva wangu atupeleke Hoteli nyingine ya kitalii maarufu pale hapa jijini ili tupate kahawa na Yasinaty. Tulifika pale tuliagiza vinywaji. Nilitumia wasaa ule kumtazama vizuri Yasinaty, alikuwa ni binti mrembo sana, na mchangamfu hasa, naamini alistahili kufanya kazi reception.

Nilimkabidhi simu yake na yakafuata maongezi mengine ya kujuana na simulizi za hapa na pale. Huo ndio ukawa mwanzo wa kujuana na Yasinaty, ambaye baadae alikuja kuwa mke wangu mpenzi.

Laiti kama ningekufahamu kabla Yasinaty………………….

Habari hii nimetumiwa na msomaji wa blog hii ya MAISHA ambaye anasheherekea ndoa yake kutimiza miaka mitano leo. Na nimeona si vibaya kama nikiweka hapa.

8 comments:

emu-three said...

Nimeipenda sana, kwani mimi ni mpenzi wa visa kama hivi. Na tunamtakia kila-laheri na ndoa yake hiyo.
Wengi wetu tumepitia visa mbalombalihadi kuoana, na sio vibaya, tunaposherehekea mwaka, au miaka fulani ya ndoa tukahadithiana!

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

safi sana!

PASSION4FASHION.TZ said...

Ni hadithi nzuri sana nimeipenda sana, na imenikumbusha mbali sana....lol! watu tunatoka mbali jamani acheni tu.

Matha Malima said...

Kwakweli katika ndoa lazima mwaume awe mwaminifu kuanzia kitu anachokiona au katika mabo mengine ya msingi kwakweli mimi nawatakia maisha mema na kila watakalo fanya katika maisha yao yawe ya amanai daima asante kwa kisa kizuri sana pia ni fundisho kwa familia zingine

ADELA KAVISHE said...

imetulia mpendwa so sweet i like it

Yasinta Ngonyani said...

Ahsanteni wote mliotoa maoni na wale waliopita hapa Maisha na Mafanikio.

Anonymous said...

kwa kweli hii adithi imenikuna aswa sababu yaliwahi kunikuta very interesting Mungu abariki maisha yao yote
shubila

Anonymous said...

Ni moja katika hadithi nzuri nilizopata kuzisoma, kwa mwandishi wa habari hii mungu akupe uwezo wa kuendelea kutuletea visa kama hivi na kwa wale wana ndoa mungu azidi kuwapa upendo wadumu katika ndoa yao . kwa kuongezea tu nataka kukuambia Yasinta Ngonyani kuwa LAITI KAMA NINGEKUFAHAMU KABLA mmmhhh sijui ingekuwaje .
mdau Leicester UK.