Kazi hii yaweza kufanywa na wakunga wa jadi wa kiume kama wakifundishwa.
HENRY Teh anasogeza taratibu shuka la rangi ya bluu hospitalini kuonyesha tumbo la mama mjamzito.Wakati akisikiliza mapigo ya kichanga tumboni, mkunga huyo aliyepo kwenye mafunzo anajua anavunja jadi
na kubadili sura ya huduma za uzazi nchini Liberia.
"Katika mazingira yetu, kuna baadhi ya wanawake ambao hawapendi wanaume kuwaangalia... kwa sababu
ya maeneo yao ya siri," anasema, huku akichezea chezea 'stetoskopu' yake.
Mwaka 2009, Teh alikuwa mmoja wa wanaume ambao waliandikishwa katika mpango wa kutoa mafunzo kwa
wakunga wa jadi kusini mashariki mwa Liberia. Shule ya wakunga wa jadi ya kijijini, iliyofungwa miaka 20
iliyopita kutokana na vita, ilifunguliwa upya na shirika la msaada wa dawa la Uingereza la Merlin na Wizara ya
Afya na Ustawi wa Jamii ya Liberia.
Uhaba wa wanafunzi wanaohitimu
Viongozi wa shule wanagundua kwa haraka kuwa kuna uhaba wa wanafunzi wa kike wanaohitimu katika
maeneo ya vijijini. Vijana wachache wa kike nchini Liberia walihitimu kutoka shule za sekondari katika miongo
michache iliyopita kutokana na wazazi kupendelea kupeleka watoto wa kiume shule.
Uamuzi wa kuchukua wanaume ulionekana kuwa na mantiki, alisema mkufunzi wa ukunga Sawah
Shaffa. "Liberia ina madaktari wanaume. Ina manesi wanaume. Hivyo, hata wakunga wa jadi hawapaswi
kuwa wanawake tu."
Katika hospitali ya kutoa mafunzo ya Martha Tubman huko Zwedru, Teh anamkaribisha mwanamke
mwingine kulala juu ya meza na kumfanyia uchunguzi. Kijana huyo anaelezea jinsi gani aliruka na kuingia
katika fursa hiyo na kuwa mkunga kutokana na uzoefu binafsi ambapo dada yake mwenye umri wa miaka 19
alifariki wakati akijifungua msituni.
"Alikuwa akijaribu kutembea kutoka mji wa karibu kwenda Kanweaken, ambako tuna kliniki. Alianza kutokwa
na damu nyingi na kulikuwa hakuna gari."
Wanakijiji walimbeba mwanamke huyo kwenye mkokoteni kwenda mji uliopo karibu, lakini alifariki dunia kabla
ya kufika kwa gari la kubebea wagonjwa.
Huduma bora za uzazi zinahitajika
Ripoti ya mwaka 2009 ya Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (Unicef) inasema kuwa
wanawake wa Liberia wana uwaino wa hatari. Mmoja katika kila 12 ya hufariki dunia wakati wa ujauzito au
kujifungua mara nyingi kutokana na kuziba kwa kizazi, kutokwa damu au maambukizi na kusababisha kuwa
taifa la nane lenye vifo vingi vya uzazi duniani. Unicef inasema asilimia 80 ya vifo vya uzazi vinaweza
kuzuilika kwa kuwa na wafanyakazi wa afya wenye mafunzo.
Liberia ina watu milioni 3.8 lakini ina wakunga wa jadi 400 tu wenye mafunzo. Maofisa wa afya wanasema
wakunga wengine 1,200 wanahitajika.
Kuondokana na vikwazo vya kitamaduni
Mpango wa wakunga wa kiume utakuwa na mafanikio? Hilo ni suala linalohojiwa. Katika chumba cha
kusubiria chenye watu wengi kwenye Hospitali ya Zwedru, mwanamke mdogo mwenye mimba anaugulia
maumivu huku akiminya tumbo lake. Aletha Cherley (22), anaogopa kwa sababu ni ya mimba yake ya
kwanza lakini pamoja na kukamatwa na misuli na kuumwa na mgongo, anasita kuchunguzwa na Teh.
"Kwangu, mwanaume tofauti ambaye siyo rafiki wangu wa kiume anaona sehemu zangu za siri, najisikia aibu
mno ... Ni aibu kubwa kwangu. Hii ndiyo sababu wanawake hapa wanapaswa kufanya kazi hiyo," anasema
Cherley.
"Unajua, ukunga una maana kuwa mtu anapaswa kukaa na mwanamke kwa muda mrefu. Wanawake wengi
watajisikia wenye furaha kwa kuwa na mwanamke mwingine hadi wanajifungua," anasema mkunga kutoka
Kenya, Zeena Abdalla Ramadhan, ambaye ni mratibu wa Merlin.
"Ukunga ni jambo binafsi... ni mwanamke kwa mwanamke."
Abdalla (56), anayejulikana kama "Mama Zeena," ametumia karibu nusu ya maisha yake akiwa anafundisha
wakunga nchini Sudan, Chad na Kambi ya Wakimbizi ya Kakuma, Kenya. Anatambua kuna vikwazo vya
kitamaduni kuanza kutumia wanaume katika fani ya ukunga ambayo kwa jadi ni ya wanawake.
"Katika Sudan Kusini, wanaweza kumwita mwanaume wakati mwanamke anaposhindwa. Wanaume
watakuja na mkuki kumtoa mtoto, mtoto aliyenasa. Hata hivyo bado, mwanamke anapaswa kuwepo."
Je, wanaume waliopatiwa mafunzo wanaweza kujaza pengo?
Mama Zeena alifundishwa kuwa mkunga wa jadi baada ya kupoteza mtoto wake aliyemaliza muda wake
tumboni mwaka 1987. Leo hii, amekuwa mtetezi mkuu wa kutoa mafunzo kwa wakunga wa jadi katika
mataifa masikini yaliyokuwa na vita.
Anaonya kuwa Lengo la Maendeleo la Milenia (MDG) la kupunguza kiwango cha vifo vya mama wajawazito
duniani kwa tatu ya nne ifikapo mwaka 2015 na kutoa huduma ya afya ya umma kwa wote, halitaweza
kufikiwa bila kuwekeza kwa kiasi kikubwa.
Nchini Liberia, amekabiliwa na maswali kama mafunzo ya ukunga kwa wanawake yanafaa kama masuala ya
jinsia yanazuia wanawake wenye mimba kupata ushauri kutoka kwa wanaume. Uamuzi unakuwa mgumu
zaidi kwa sababu wanaume wanapata alama za juu zaidi katika mtihani wa kujiunga na mafunzo.
"Kama tungekwenda na alama, tungeishia na wanaume tu... Lakini (wanajumuiya) walionyesha shaka.
Hatuwezi kutoa mafunzo kwa watu ambao hawatakuwa na maana. Hivyo, tuliamua tusichukue wanaume
zaidi."
Shule ilipunguza idadi ya wanafunzi wakunga wanaume mwaka 2010 hadi wawili tu. Mama Zeena hajui nini
kitatokea mwaka ujao.
Ukirejea katika chumba cha upimaji cha Teh, kijana mdogo anaweka sikio lake kwenye kipimo na
anakibonyeza dhidi ya tumbo la mwanamke mwenye mimba ili kusikiliza mapigo ya mtoto. Teh, ambaye
alikuwa akichaji simu za kiganjani ili kuingiza fedha katika kijiji chao kidogo mwaka jana, anapiga kelele kwa
furaha anapoelezea ni kwa kiasi gani anapenda mafunzo hayo ya kuwa mkunga.
Tofauti na uongozi wa shule, yeye ana imani kuwa wanawake wajawazito wataondokana na aibu yao na
miiko ya kitamaduni kupata huduma za afya kutoka kwake kijijini humo.
"Napenda mno fani hii... na unapaswa kuwakaribia wanawake kwa njia ambayo unadhani watahisi vizuri."
Darasa la kwanza la wakunga 32, ambao watamaliza masomo yao Desemba 2010, limesaini mikataba na
Wizara ya Afya ambayo inawahakikishia ajira kamili kwa miaka mitatu, kwa kuhudumia majimbo sita ya vijijini kusini mashariki mwa Liberia.
kusini mashariki mwa Liberia.
Habari hii nimeipata kutoka gazeti la mwananchi na Bonnie Allen, IPS-Liberia
6 comments:
Najaribu kufikiria wakunga wa jadi wakiume wakianza kazi hasa sehemu kama za umasaini, sijui itakuwaje, ila nafikiri wanawake wengi wataona bora kwenda kujifungulia hospitali....... labda itapunguza masuala ya kukimbia hospitali na kwenda kuzalia nyumbani. Nafikiria kwa mkono wangu tu huku nikidonyoa keyboard
Mie naona wataweza bila kikwazo cha aina yoyote maana hata mahospitalini wapo wanaume ambao ni wakunga wenye msaada mkubwa sana kwa kina mama.
Taifa kuwa na wakunga wa jadi wa kiume inawezekana.
Tatizo sio kuwezekana, inawezekana, lakini wanawake mpo tayari, nasema mpo tayari kwasababu wanaume hawajui uchungu gani mnaoupata, kwahiyo akija kazini ni kazi mtindo mmoja.
Wakunga wa jadi wa kiume inawezekana kabisa kwani nimesikia kwamba, kuna sehemu moja katika kijiji flani yupo mkunga wa jadi wa kiume na ana piga kazi kama kawaida!
Inawezekana kwa kuwa inasemekana kuwa wanawake wanapenda wahudumiwe zaidi na wataalam wa afya!!
sababu ni kuwa gainakolojist wa kiume ni bora mara mia kuliko wa kike....ati wa kike huwa wanawananga wenzao na kuwatukana....mmmh!
sioni tatizo kuwa na mkunga wa jadi ambaye ni mwanaume. kwa sababu gani akina mama wajawazito hawapati mimba peke yao ni "lazima" kuwa na mwanaume. Ndiyo, najua kuwa huyo mkunga hatakuwa alikupa mimba lakini kwa kuhatarisha maisha wakati kuna watu wenye elimu? sababu eti mwanaume sitaki anizalisha nakubali kufa. Wahenga walisema mficha uchi hazai...
Post a Comment