Tuesday, April 5, 2011

NIMEMKUMBUKA KWELI MDOGO WANGU ASIFIWE LEO

Yasinta na Asifiwe 2009 mwezi wa pili
Leo nimeamka nikimuwaza kweli mdogo wangu Asifiwe nusu nichukue simu na kumpigia ili tuchape hadithi zetu kama tulivyozoea. Nikawa nasikia kama vile ananiita dada, dada, nami nikawa namwita jina lake na mara nikakukumbuka shairi hili aliloandika mtani wangu Fadhy ukitaka kusoma mashairi yake zaidi basi ingia Fadhili ya diwani Shairi lenyewe linasema hivi:-
Pumzika kwa amani, Asifiwe Ngonyani

Asifiwe! Asifiwe! sauti zetu sikia,


Asifiwe! Asifiwe! kweli unatusikia?


Asifiwe! Asifiwe! mbona hujaitikia?


Asifiwe umekwenda, dunia 'meikimbia,


Wajua tulikupenda, ila Mungu kazidia,


Mauti yamekutenda, wewe umetangulia,


Pumzika kwa amani, Asifiwe Ngonyani.


Umetwachia majonzi, hakika twakulilia,


Tumejawa na simanzi, hatuwezi elezea,


Mdogo wetu mpenzi, uchungu 'metuachia,


Pumzika kwa amani, Asifiwe Ngonyani.


Ulijawa na adabu, nao ukarimu pia,


Kwa wako utaratibu, ni nuru imepotea,


Umekwenda kama bubu, kwa heri hukutwambia,


Pumzika kwa amani, Asifiwe Ngonyani.


Wewe mtu mwuungwana, kwa njema yako tabia,


Tulikupenda kwa sana, nd'o maana twaumia,


Mfano wako hakuna, kwa pengo kulizibia,


Pumzika kwa amani, Asifiwe Ngonyani.


Kuondoka kwatuliza, kila tukifikiria,


Twatamani tungeweza, kifo tungekizuia,


Mwaka huu kumaliza, nayo inayof'atia,


Pumzika kwa amani, Asifiwe Ngonyani.


Lakini sisi ni nani, Mungu tukamwamulia?


Tukamwuliza kwa nini, wewe amekuchukua?


Mwamuzi ndiye Manani, aloiumba dunia,


Pumzika kwa amani, Asifiwe Ngonyani.


Pengo halitozibika, wewe ulotuachia,


Daima 'takukumbuka, wema'wo kusimulia,


Tukimwomba Rabuka, mwanga kukuangazia,


Pumzika kwa amani, Asifiwe Ngonyani.


Upumzike salama, kwa Mola twakuombea,


Akupe pahala pema, nuru kukuangazia,


Asifiwe mtu mwema, buriani twakwambia,


Pumzika kwa amani, Asifiwe Ngonyani.


Shairi hili nimeliandika maalumu kwa marehemu Asifiwe Ngonyani, mdogo wa kike wa dada yetu, rafiki yetu na mwanablog mwenzetu Yasinta Ngonyani. Asifiwe alipatwa na mauti Jumatano 23.03.2011. Asifiwe umetuacha kimwili tu, kiroho tungali pamoja nawe. Tunakuombea pumziko salama la milele. Amina. AHSANTE SANA MTANI FADHY KWA SHAIRI HILI!!

15 comments:

NAJUA WAJUA said...

Pole sana dada Yasinta, yote ni mapenzi ya mungu!

Mija Shija Sayi said...

Pumzika kwa amani Asifiwe.

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

RIP Asifiwe!

Baraka Chibiriti said...

Naamini Mwenyezi Mungu atakuwa amesikia sala zetu na amempumzisha mpendwa Asifiwe mahali pema peponi.

Pole sana Dada Yasinta kwa pengo kubwa alilo waashia Asifiwe, lakini naamini kabisa yupo pamoja nanyi daima katika mioyo yenu, hata mioyoni mwetu sote ambao tumemfahamu kwa kumwona kwenye picha, huko aliko hata yeye anawamiss/anatumiss sote. Tutazidi kumwombea zaidi na zaidi.

Unknown said...

Pole jamani

EDNA said...

Pole sana dada, na jipe moyo.

Anonymous said...

Yasinta pole sana kumbuka kuwa mungu anampenda na atamlinda .Naamini yuko na malaika wa mungu wakiimba na kutuombea. "TUBUNI NA KUIAMINI INJILI" KUMBUKA U MAVUMBI NA UTARUDI MAVUMBINI"

emu-three said...

Mungu amlaze mahala pema peponi, AMIN

Mwanasosholojia said...

Pole da'Yasinta!Hakika ulimpenda sana mdogo wako,na ndiyo inavyotakiwa.Safari yetu ni moja, nyakati tu ni tofauti, lakini tutakutana paradiso na kuendelea kufurahi pamoja.

Anonymous said...

Pole sana Yasinta - usisikitike sana mwishowe utamkufuru Mungu.

chib said...

Mungu atawapa Nguvu, tukio limekwishapita, kilichobaki ni ile hulka aliyotupa Mwenyezi Mungu ya kusahau, na kutufanya tusipate maumivu ambayo hapo awali yalitusibu.

Mbele said...

Pole tena. Nimeshindwa kuandika mengi, kwa mawazo kuwa mazito juu yako na familia yako. Imebaki kukuombeeni kwa Mungu tu.

Hii picha ya marehemu dada yako imenishtua sana. Anafanana sana na dada yangu ambaye alifariki miaka mingi kidogo iliyopita. Ni ajabu, kufanana huku. Inashtua sana.

Basi, nimalizie tu kwa kusema, yote yako mikononi mwa Mungu. Tuwaombee wenzetu waliotutangulia; wastarehe kwa amani.

John Fisher Kanene said...

Dear Yasinta,

I am a very committed follower of your blog and work and live in Kenya.
I wish to extend my very sincere condolences to you and the entire Ngonyani family for the demise of your sibling sister Asifiwe.
May her soul rest in eternal peace and God give you the C and faith to sustain you through this most diffcult period in your life.
I am praying for you.

Salehe Msanda said...

Pole sana kwa kufiwa na mdogo wako

Ni mapenzi ya mungu,yanatakaiwa kuheshimiwa,yeye ametangulia sisi tuko nyuma yake

Kila la kheri.

Nampangala said...

Mpumzika kwa Amani mdogo wetu Asifiwe. Mungu Baba alikuhitaji zaidi yetu. Pole sana mlongo Dada Yasinta.