Friday, January 14, 2011

MAVAZI YA WANAWAKE

Nimelipenda shairi hili kwani linasema ukweli limeandikwa na Katekista Rafael Mlelwa katika gazeti la Mwenge:-

Natembea natazama, ni hali ya kushangaza,
Mitaani akina mama, mambo wanayoigiza,
Wengine watuwazima, inakuwaje nawaza,
Mavazi mnayovaa, ya aibu kinamama.

Vazi la Mtanzania, tangu kale heshima,
Watu walijivunia, wa lika zote nasema,
Haya nawasimulia, walivaa akina mama,
Mavazi mnayovaa, ya aibu kinamama.

Suruali mwavalia, mfanane na wazungu,
Asili mwaikimbia, mnanitia uchungu,
Watu wote angalia, mnamdharau Mungu,
Mavazi mnayovaa, ya aibu kinamama.

Vimini mwajibalia, mwana kama vikatuni,
Nyingine mnapasua, makusudi mapajani,
Mapaja twaangalia, pia na nguo za ndani,
Mavazi mnayovaa, ya aibu kinamama.

Siketi taiti pia, mitaani mwavalia,
Hiyoni ya kulalia, maungo yaoneshea,
Mitaani mwatembea, watu kwa kuangalia,
Mavazi mnayovaa, ya aibu kinamama.

Kweli mwatia karaha, moyoni nasononeka,
Singerendi mwavalia, maziwa yanaonekana,
Mitaani mnahaha, kutwa nzima mwazunguka,
Mavazi mnayovaa, ya aibu kinamama.

Kwa umbo mmeumbika, kwa uzuri asilia,
Uarabu mwautaka, tena kwa kujichubua,
Kama Mungu angetaka, mngekuwa Saudia,
Mavazi mnayovaa, ya aibu kinamama.

Wengine watu wazima, tena ni wake za watu,
Watoto wenu lazima, watawaigeni tu,
Malazi yao lazima yatakuwa yenye kutu,
Mavazi mnayovaa, ya aibu kinamama.

Hapa mimi nasimama, naomba mnisikie,
Wanamama wenye hekima, hali hii tukemee,
Hakika mimi nasema, tena isiendelee,
Mavazi mnayovaa, ya aibu kinamama.

21 comments:

emu-three said...

Twashukuru kwa shairi, utungo ulotukuka,
Ndani yake kuna ujumbe,wahusika mumesikia,
Kama mnazo hoja, mzitoe kwa malenga

Mija Shija Sayi said...

M-3 kumbe nawe ni mshairi? poa sana.

Haya Da Yasinta nakusubiri nione maoni yako.

Yasinta Ngonyani said...

M-3! hata mimi sikujua kama nawe ni mshairi pia. ni kweli shairi hili lina ujumbe mzuri sana kwa akina mama.

Mija:-)
Haya maoni yangu ni kwamba nakubaliana na mshairi ni kweli akina mama siku hizi wamakuwa kama vichaaau sijui nisemeje hakuna heshima kabisa yaani mtu unatamani mpaka kulia jinsi wanavyovaa kisa kwa asababu ya kuiga. Wanaacha mavazi yetu ya heshima na utamaduni wetu. Kuna kanga nyingiiiii na vitengeeee vingiiii lakini hii wanatupilia mbali na kuvaa mavazi ambayo mtoto wa miaka kumi na mbili angevaa yote hii nini? kwa kweli nasikitika sana na naumia sana nikutanapo na mwanamama aliyevaa hivyo. je nawe Mija unasemaje?

Goodman Manyanya Phiri said...

Sisi wanaume tunaweza kukerwa (na tunakerwa sana barani kote Afrika) na mavazi ya akinamama. Lakini hatunayo haki ya kwambia wavae kivipi. Wao wenyewe waambizane kama kweli tutapata suluhisho la kudumu kuhusu balaa hii.

Simacho yetu wenyewe wanaume ndio wateja wa mitindo hii? Tujikosoe wenyewe kwa kubadili mili za dada zetu kama bidhaa sokoni!

Unknown said...

mimi kigugumizi! Leo ngoja niwe Simon...mmmh!!

Simon Kitururu said...

Mie sikubaliani na Mtunzi kwa sababu za kihistoria ya MAvazi ya WAAFRIKA niijuayo miye ya kuanzia nguo za ngozi na majani za WAAFRIKA kabla ya hata ya vitambaa AFRIKA.:-(


Ukifuatilia historia ya hata vitambaa AFRIKA , unaweza kusita kuhusu vazi la KIAFRIKA LA HESHIMA la aliyeheshimiwa tokea zamani AFRIKA lilikuwa linaficha nini .

Wote tunajua ni ngozi na vibwaya vya majani ndio kiasili mavazi ya Muheshimiwa AFRIKA yalivyokuwa.

Na ambao walikuwa wanaweza kuwa na ngozi za kutengeneza vazi la kujisitiri walikuwa ni wale wafugaji tu zaidi ambao mpaka leo hii hata hapa Tanzania tunawajua, na twajua ni asilimia chache tu ya WATANZANIA .

Na kifichwacho mara nyingi kilikuwa ni sehemu za siri tu na ni kwa sababu(PRACTICAL) -kama kuzuia mchanga , kuchomwana na miba kunako nanihii au tu kuzuia inzi kugeuza SEHEMU ZA SIRI ni sehemu ya kupata KITOWEO kutokana na hali halisi ya sehemu za siri za BINADAMU zilivyo,...
... tukiachilia mbali hedhi kwa wanawake na kwa wanaume kuficha mdindo ashki ya ngono ikiingilia kati RIJALI.

Nachojaribu kusema:

Ni uongo kudai WAAFRIKA walikuwa wanamavazi YA WANAWAKE na hata tu WANAUME yasitiriyo sana kama MTUNZI adaivyo kwenye utunzi.:-(

Na mpaka leo ni makabila kibao vijijini kucheza ngoma matiti wazi ni heshima tu !

Kinachotokea kwa waafrika wa siku hizi ni kuwa WANATAFSIRI mpya tu vichwani mwao vya nini ni HESHIMA,...
.... kitu kifanyacho wakiona paja wanadhani ni kitu cha ajabu wakati kuonyeshwa mpaka chupi yaweza kuwa ni kitu tu cha heshima ikitafsiriwa kuwa ni HESHIMA.

UNAFIKIRIA NINI ukiona kitu ndio chanzo cha TATIZO na mwenye mawazo POTOFU kimjiacho ni POTOFU akiona kitu kama tu MWENYE wazo CHANYA akiona KITU chanya hufikiria mambo CHANYA.


Na haki ya nani VIMINI miaka ya sitini vilikuwepo , MAXI zikaingia na kuwa ndio utundu ,...
kwa kifupi ni TAFSIRI TU za watu hugeuka na hakuna jipya na kwangu binafsi naheshimu sana wanawake wote ikiwa na wale wanikaliao uchi.:-(



Hivi KATEKISTA ndio mtu wa aina gani?
Hivi unafikiri ni kwanini BINADAMU anafikiri kukaa uchi kwa aliyevaa VAZI sio HESHIMA wakati karibu wote waheshimiwa wana uchi kitu ambacho labda kingesaidia kufanya uchi uwe kitu cha kawaida?

NI mtazamo tu HUU!:-(

Mtesuka said...

Ni ujumbe maridhawa. Asante dada kwa kutuletea maoni ya mwl Mlelwa.

MARKUS MPANGALA said...

Nimekumbuka riwaya ya BEN MTOBWA ya MTAMBO WA MAUTI.

anasema, 'wanawake tangu waanze kuvaa kama wanaum'
yaani kuvaa suluwali, nao hujiona vidume' lakini wanasahau kuwa hawatabadili kitu, ila wazingatie nidhamu yao ya kike. usawa ni kwa wote siyo kuwapendelea.
>>>>>>

wanavaa hadi napigwa butwaa,
matiti wayaweka hadharani,
ati mitindo ya kisasa'

wamekuwa wajinga sugu,
huvaa kucha za bandani,
toka mawaziri na wasomi kedekede,
wanasema kuwa nyakati mpya.
wanajichora ati wanja, au lipustiki,
wanaMAGIWI wafanane na wazungu.
hawataki rasta za da' Mija,

wanakwenda dukani kununua urembo ati kujikwatua..... ha ha ha ama kweli Oko pBitek aliandika kitabu chake cha SONG OF LAWINO AND SONG OF OCOL aliona mbali.

au NGUGI WA THIONGO katika A GRAIN OF WHEAT

wanawake wa sasa wakiguswa hata na unyoya.. heeeeeeeeeeeee kesi KISUTU ati nimeipgwa na mume wangu.

haki sawa ati wapendelewe salaaaaleeeeeeee.
LAN MORRIS ametuachia kitabu kipya akisema WHY THE WEST RULES -FOR NOW.

Koero ametuletea msemo MBOMBO JILIPO-kazi ipo

chib said...

Mkuu Kitururu :-)

Anonymous said...

Mjadala mzuri sana.pia mimi napinga kwa nguvu zangu zote,nisiaapo mtu anasema vazi la asili ya kiafrika,au nguo ya kiafrika.pia kuna mchakato wa kutafuta vazi la kitanzania,hapo pia bure kabisa.ukiangalia mavazi waliyo kuwa wakijisitiri maungo babu zetu wa zamani, kwa hali ya sasa tuliyo nayo niaibu,na hii nikutokana na miingiliano ya kijamii.hivyo hakuna haja ya kupoteza muda, kuhusu vazi ,chamsingi hapa ni vaa usitiri maungo yako.kwenye ngoma za kumtoa mwali wa kizaramo, titi njenje,nduguzetu waswazi ndo usiseme kabisa.tunajificha sana maungo mpaka inafika mtu akikaa wazi sehemu ya mwili wake ikaonekana mfano paja mtu hoi nimazoeatu. kaka s

Mija Shija Sayi said...

Kwa kweli mimi nimesimama upande wa Kitururu.

Unknown said...

Mawazo ni mengi, kila mmoja na mtizamo wake. Hakuna asiye na la msingi, tunasema sana lkn ukweli huu ni kwa mke. Jamii haina maana nyingi, ukale ama usasa ni lipi litatufikisha kwake. Mungu alivyoweza kwa wingi, binadamu hana nia njema nafsini mwake. Nauliza, hivi ndivyo mungu alivyokusudia kwetu?

Nawasilisha.

Simon Kitururu said...

@Mkuu Yusuph Mcharia: Mimi nachojua MUNGU aliumba BINADAMU uchi na alimuumba kakamilika asiye na chochote cha kuonea aibu. Ila MUNGU alimpa BINADAMU utashi aka akili na vikorombwezo vingi vimfanyavyo binadamu anatapatapa hutokana tu na matumizi yake ya akili aliopewa na huyohuyo MUNGU. Na moja ya uhangaikaji wa MWANADAMU ulionukuliwa katika vitabu vitakatifu ambao ni wapili baada ya kutafuta MSOSI ilikuwa ni kujisitiri mara tu baada ya mtoto mzuri EVA kumbembeleza ADAMU ale naye tunda.

Na nawasiwasi kuwa hata EVA vazi lake la kwanza baada ya kustukia yuko uchi liliacha paja , TITI na kitovu nje na kilichofichwa kilikuwa ni sehemusehemu tu kwa kibwaya .

Huwa naapata hisia hizi nikisoma ile stori ya NYOKA kamdanganya EVA na eva kamuingiza mkenge ADAMU katika kitabu nguli BIBLIA.


Ila nanukuu``hivi ndivyo mungu alivyokusudia kwetu?´´

Jibu langu ni kwamba MAKUSUDIO YA MUNGU naamini MUNGU mwenyewe ndiye anajua. Ila siye katupa akili na uhuru wa kuchagua na kwa matumizi yetu ya akili tutachagua mpaka hivi tuamini MUNGU YUPO mpaka hivi BIKINI sio aina tu ya chupi .




Kwa wasio amini MUNGU:

-Sijawalenga na jibu hilo hapo juu na samahani!:-(

MARKUS MPANGALA said...

@Kitururu:) hakika wewe ni MWANAZUONI umenikumbusha maswali mengi nijiulizayo, kamba nyoka alimdanganya mlimbwende Eva, lakini wakitetea zaidi wanasema ilikuwa wa uwezo wa mungu.
Ndiyo, nitasema kuwa kama tuliumbwa kwa mfano wao, na inawezekana tukaishi kwa mfano wetu. Kama mkuu Kitururu ulivyosema majibu na sababu zingine anajua huyo MUNGU. na hakuna mtu anayezaliwa akiwa masitiriwa maungo, kila kitu kinakuwa hadharani. Lakini kama tunavyosema, kama watu wazima wameona kuvaa kucha za bandia ni namna ya kuishi, je watakataa kuwa wanaishi kwa mfano wao na siyo MUNGU wao?

na kama suala la kujisetiri ni nyeti ili kuficha kiuno,paja,umbile na kadhalika, ni kwanini tumeamua kuona kujisetiri ni muhimu sana lakini kuishi kwa mfano wa MUNGU ni ngumu?

NAACHA wazo, HEKO kwa Mtakatifu Kitururu kwa aya anuai.

Salehe Msanda said...

Habari ya kazi
Hayo ni matokeo ya kutojipenda na kujikubali na kudhani kuwa kila kinachofanywa na wengine ni bora.

Imefikia mahali wafrika hasa watanzania tumekuwa kama maroboti,inaudhi na kukera lakini bado tuna wajibu wa kukumbushana na kuonyanya kama ilivyo katika shairi hilo

Tunakazi ya ziada kuulinda utamaduni na utu wetu.
Jmos Njema

Simon Kitururu said...

@Mheshimiwa Salehe Matanda:


Kwani UTU ni nini?

Kwani Utamaduni wetu ni upi?

Simon Kitururu said...

Samahani nilikosea jina hapo juu!:-(

Nilikuwa namlenga Mheshimiwa Salehe Msanda na sio Salehe Matanda,...
...ili atuongezee busara sie wengine kwa kuwa nahisi kakatizia ujumbe!:-(

PASSION4FASHION.TZ said...

I salute you Mtakatifu,wewe kweli umegonga point,haya mavazi ya kufunika tumeyaiga kutoka nchi za mashariki ya kati nawala siyo yetu hayo,yetu ni vimin au vibwaya nakuacha kifua wazi..... kama wanavyovaa waschana wa Kiswaziland kwenye chagulaga ya mfalme wao wa Swaziland.

Alivyosema kaka Simon historia ya mavazi yetu halisi ilikuwa ni ngozi,magome ya miti na majani kuficha sehemu nyeti tuu na hata matiti yalitakiwa yaachwe wazi.....sasa siku hizi mtu akiacha wazi anaambiwa ni malaya au anaonekana kachanganyikiwa.

Sasa mtu akisema turudie mavazi yetu ya asili ya kiafrika hivyo ndio vitakuwa vivazi vyetu....na kwa midume ya siku hizi ilivyokuwa na uchu haponi mtu itakuwa ni kubakwa tu.Wanaume wa enzi hizo walikuwa wastarabu sana...lol!

Yasinta Ngonyani said...

napenda kuwashukruni wote kwa maoni yenu. Nakubali na sikubali kuhusu utamaduni wetu kuwa mavazi yetu yalikuwa ngozi, ngome miti nk.nk nk. lakini tukumbuka pia kwamba kila kitu kinabadilika na Mungu alitupa akili ili tuweze kuzitumia. na kikafikia kipindi tukagundua nguo Ninachotaka kusema hapa ni kwamba kuna wakati unaweza kuona mwanamama au mwanadada kavaa kinguo ambacho kinambana sana hapo ndo ninapokuja jiuliza je ameazima kwa binti yake au? Napenda utamaduni, mila na desturi za kiafrika lakini siku hizi kuna mangi mno tunaiga....

Simon Kitururu said...

Nahisi sijakuelewa Mtoto Mzuri Yasinta!

Medson Chengula said...

UJUMBE NIMEUKUBARI. KWAKWELI KINAMAMA ANGALIENI HASA KINADADA WA VYUO VIKUU TENA VYA KIDINI. INAUMA MNAPOTEA NA KUIPOTEZA JAMII YA WATOTO WA KIKE WANAO WAZUNGUKA. JITAHIDINI KUBADILIKA KINADADA. KINADADA MNAOWEZA KUWAELIMISHA WEZENU JITAHIDINI HALI NI MBAYA, MNAPOTEA. BADILIKENI.