Monday, May 23, 2016

KWA NINI WANAWAKE WANATENDEWA MAMBO YA AJABU NA WANAUME?

Siku ya leo nimeamka na mawazo mengi sana katika kichwa changu....Nimewaza na kuwazoa bila kupata jibu nimeona ni bora tuwaze pamoja.  Mawazo yenyewe  ni haya.....
Hivi ni kwa nini wanawake wanatendewa mambo ya ajabu na wanaume?
Ni kwa nini wanawake wanaonekena wanyonge mbele ya wanaume...?
Ni kwa nini wanawake wanakuwa wategemezi kwa wanaume...?
Kuna tofauti gani kati ya mwanamke na mwanamume kiakili, kihisia, kimwili na kiroho?
Ni nini chanzo cha yote haya:- Ni maumbile? Mfumo dume?  Je? ni uvivu tu wa wanawake?  Au ni kushindwa kujitambua kwa mwanamke?

5 comments:

ray njau said...

Je, Kweli Mungu Anawajali Wanawake?

“Dhambi ilianza na mwanamke, na kwa sababu ya mwanamke lazima sote tufe.”—KITABU CHA KIAPOKRIFA KINACHOITWA ECCLESIASTICUS, KARNE YA PILI K.W.K.

“Wewe ni lango la ibilisi: uliufunua ule mti uliokatazwa: wewe ndiye wa kwanza kuasi sheria za Mungu . . . Uliharibu kwa urahisi mfano wa Mungu, yaani, mwanamume.”—TERTULLIAN, KATIKA KITABU ON THE APPAREL OF WOMEN, KARNE YA PILI W.K.

MANENO hayo yaliyoandikwa kale hayapatikani katika Biblia. Kwa karne nyingi, yametumiwa kutetea ubaguzi dhidi ya wanawake. Hata leo, watu fulani wenye msimamo mkali bado wananukuu maandishi ya kidini ili kutetea ukandamizaji wa wanawake, wakidai kwamba wanawake ndio chanzo cha matatizo yanayowapata wanadamu. Je, Mungu alikusudia wanawake wadharauliwe na kutendewa vibaya na wanaume? Biblia inasema nini? Acheni tuone.

▪ Je, wanawake wamelaaniwa na Mungu?

Hapana. Badala yake “yule nyoka wa zamani, yeye anayeitwa Ibilisi,” ndiye ‘aliyelaaniwa’ na Mungu. (Ufunuo 12:9; Mwanzo 3:14) Mungu aliposema kwamba Adamu ‘angemtawala’ mke wake, Mungu hakuwa akimruhusu mwanamume amkandamize mwanamke. (Mwanzo 3:16) Alikuwa tu akitabiri matokeo mabaya ya dhambi ambayo yangewapata wenzi wawili wa kwanza.

Hivyo, kutendwa vibaya kwa wanawake ni matokeo ya moja kwa moja ya dhambi ambayo wanadamu walirithi, bali si mapenzi ya Mungu. Biblia haiungi mkono wazo la kwamba ni lazima wanaume wawakandamize wanawake ili kulipia ile dhambi ya kwanza.—Waroma 5:12.

▪ Je, Mungu alimuumba mwanamke akiwa duni kuliko mwanamume?

Hapana. Andiko la Mwanzo 1:27 linasema: “Mungu akamuumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimuumba; mwanamume na mwanamke aliwaumba.” Hivyo, tangu mwanzoni, wanadamu wote—wanaume na wanawake—waliumbwa wakiwa na uwezo wa kuonyesha sifa za Mungu. Ingawa Adamu na Hawa waliumbwa kwa njia iliyotofautiana kihisia na kimwili, wote walipokea mgawo uleule na walifurahia mapendeleo yaleyale kutoka kwa Muumba wao.—Mwanzo 1:28-31.

Kabla ya kumuumba Hawa, Mungu alisema hivi: “Nitamfanyia [Adamu] msaidizi, awe kikamilisho chake.” (Mwanzo 2:18) Je, neno “kikamilisho” linamaanisha kwamba mwanamke alikuwa duni kuliko mwanaume? Hapana, kwa sababu neno hilo la Kiebrania linaweza pia kutafsiriwa kuwa “mshirika” au “msaada unaolingana na” mwanamume. Fikiria majukumu ya daktari mpasuaji na ya mtaalamu wa dawa za kupunguza maumivu wakati wa upasuaji. Je, mmoja anaweza kufanya kazi bila mwenzake? Huenda asiweze! Ingawa daktari mpasuaji ndiye hufanya upasuaji, je, yeye ni wa maana zaidi? Hatuwezi kusema hivyo. Vivyo hivyo, Mungu alimuumba mwanamume na mwanamke ili washirikiane kwa ukaribu, bali si kushindana.—Mwanzo 2:24.

▪ Ni nini kinachoonyesha kwamba Mungu anawajali wanawake?

Huku akijua kimbele jinsi ambavyo wanaume wasio wakamilifu wangetenda, tangu zamani Mungu alionyesha kwamba alikusudia kuwalinda wanawake. Akizungumza kuhusu Sheria ya Musa ambayo ilianza kutumika katika karne ya 16 K.W.K., katika kitabu chake La Bible au féminin (Biblia Katika Jinsia ya Kike) mwandishi Laure Aynard, aliandika hivi: “Mara nyingi, agano la Sheria linawatetea wanawake linapozungumza kuwahusu.”

Kwa mfano, Sheria iliagiza Waisraeli wamheshimu baba na pia mama. (Kutoka 20:12; 21:15, 17) Vilevile, Sheria iliagiza kwamba mwanamke mwenye mimba atendewe kwa ufikirio. (Kutoka 21:22) Hata leo, ulinzi uliotolewa na sheria hizo za Mungu ni kinyume kabisa na ukosefu wa haki za kisheria ambao wanawake wengi wanakabiliana nao katika sehemu nyingi ulimwenguni. Lakini kuna mambo mengine yanayoonyesha kwamba Mungu anawajali.(Chanzo:www.jw.org/sw-maktaba)

Yasinta Ngonyani said...

Kaka Ray...Ahsante kwa kupita hapa na kuacha ujumbe mzuri wa kufunza ....

ray njau said...

Asante na nitaendelea kupita na kupitia pia.Uwe na siku njema kifamilia da Kapulya.

Yasinta Ngonyani said...

Ahsante sana. Nawe pia siku yako iwe njema.

NN Mhango said...

Si wanaume wote wanatenda unyama huu; na si wanawake wote wanatendewa unyama huu. Wapo wanawake wanaowadunda wanaume na wapo wanaume wanaowadunda wanawake. Kimsingi, mbali na mila na malezi mabaya, chanzo kikubwa cha ukatili wa kijinsia ni kutojiamini na kujua thamani ya utu. Anayedhalilisha na anayedhalilishwa wote wanahitaji msaada. Ni watumwa wa matendo na hali zao. Mwanaume wa kweli hadhalilishi mwanamke wala mwanamke wa kweli hadhalilishi mwanaume iwe ni kwa limbwata au upuuzi mwingine. Sitaki nitoe lecture ila ukweli ni kwamba unyanyasaji una kila dalili za ujinga, kutojiamini, malezi na mila mbaya ukiachia mbali unyama wa baadhi ya watu waliozaliwa nao.