Hali hii inapotokea, anayependa ambaye tunasema ndiye mtoaji pekee, hufikia mahali huingia kwenye hali ya hisia ambayo hufahamika kama resentment flu (Homa ya masikitiko). Hii ni hali ambayo, yule ambaye anatoa tu, yaani anapenda mwenzake, lakini mwenzake hampendi, huihisi anapokuwa amechoka.
Kwa kawaida tunasema, mtu anapopenda asisubiri naye kupendwa, yaani anapotoa aijali kama mwenzake anatoa au hatui. Lakini hufikia mahali kanuni za maumbile humfanya huyu anayetoa kuhisi kama amebeba mzigo mkubwa sana. Kama tunasema kupenda ni mtu kutoa bila kutarajia kupewa, ina maana kwamba, huyu anayeshindwa kutoa, ameshindwa kupenda.
Kama ameshindwa kutoa ina maana kwamba, ameshindwa kutekeleza jukumu lake na hiyo ina maana kwamba, ameshindwa kupenda. Anaposhindwa kupenda anakuwa amevunja kanuni ya kimaumbile inayosimamia kupendana ambayo inasema ili kupendana kukamilike, pande zote ni lazima zitoe na kupokea.
Kumbuka nasema, kupendana, siyo kupenda. Kwenye kupenda tunatakiwa kutoa tu, kwenye kupendana tunatakiwa kutoa na kupokea. Kama tunampenda mtu na mtu huyo hatupendi, yaani hatimizi majukumu na wajibu Wake kwenye kutupenda sisi, hatimaye tunafika mahali tunaingia kwenye hiyo hali niliyoitaja ya homa ya masikitiko.
Kumbuka ninaposema kutoa sina maana ya kutoa fedha, bali kumtendea na kumtolea kauli za wema mwenzako. Kwenye tatizo hili, wanawake wanaonekana kama wanaathirika zaidi.
Kama mwanamke akihisi kuwa yeye anatumikia upendo na mwenzake hajali tena, huumia kuliko ilivyo kwa mwanamume. Labda ni kwa sababu, wanawake huumia kihisia kirahisi zaidi kuliko wanaume na jambo hili linapotokea huumiza zaidi hisia.
Mwanamke huanza kuingia kwenye hali hii polepole, pale anapobaini kwamba, mwenzake anapokea tu, badala ya kupokea na kutoa. Hii ina maana, mwanamume anaposubiri au kufurahia kutendewa mema na kutolewa kauli njema tu, wakati yeye hafanyi hivyo, hajali kuhusu mpenzi Wake. Mwanamke kwa kawaida huonyesha dalili kwamba, yupo kwenye hali hii kwa kuanza kuacha kufanya vile vitu ambavyo kwa kawaida huitwa au kuonekana vidogovidogo kwenye uhusiano.
Kwana mfano, anaweza akaacha kumtayarishia mumewe chakula anachokipenda sana ambacho alikuwa anamtayarishia kwa nyakati fulanifulani, anaweza asiwe anamchagulia tena nguo za kuvaa, anaweza asiwe anamkagua baada ya kuvaa, anaweza kuchukus hatua mbaya zaidi kama kukataa kushiriki tendo la ndoa. Mwanamume anapoona mke akiwa hivyo, naye huanza kumtendea mkewe kwa njia kama hiyo, yaani kuongea kiwango chake cha kutojali. Anaweza kuanza kuchelewa kurudi nyumbani, anaweza kuacha kukaa pamoja na mkewe hata akiwa nyumbani, anaweza hata kujitoa kabisa kwenye uhusiano, yaani kufanya mambo yake kama vile hana mke.
Inapotokea hali ambapo mwanamke anahisi kuingia kwenye homa hii, inabidi ajiulize haraka ni kwa nini ameingia huko. Ni vizuri kujiuliza kwa sababu, akisubiri zaidi, mume naye ataanza kuwa mkorofi zaidi. Ikifikia hapo, njia ya kusuluhisha tatizo hili ambalo kwa kawaida, linaweza kuondolewa kwa mazungumzo, huwa ngumu zaidi.
Kwa hiyo, hakuna suala la `hitapenda hadi lini,` kwa sababu kupenda hakuumizi. Kunakoumiza ni kushindwa kutoa mapenzi. Ukitoa upendo wako kwa mtu ambaye yeye kazi ni kupokea tu, lakini hajui kutoa upendo, yeye ndiye atakayeumia. Yeye atakufanya uache kuendelea kutoa, hivyo yeye ndiye atakayekosa, sio wewe. Yeye atapata shida kwa sababu, kila mtu akayeamua kuishi naye kama mpenzi, atahisi hali ulioihisi wewe na ataamua kukimbia. Ni hadi ajifunze kutoa, ndipo atakapoanza naye kuingia katika kupendana.
Hebu fikiria kwamba, unamtendea na kumtolea kauli nzuri mkeo au mumeo. Unahakikisha kwamba, unampa kila ambacho nawe ungependa kupewa, bila kujali kama naye anafanya hivyo kwako au hapana. Umemkubali kama alivyo na udhaifu Wake na unazingatia zaidi ubora Wake na siyo udhaifu huo. Hapa tunasema unampenda.
Lakini kwa bahati mbaya, huyo mwenzako ni mkosoaji, asiyejali, mchoyo, mlalamishi na mwenye ghubu. Huyu tunasema, hajui au hataki kupenda. Kwa maana hiyo, anaishi kwenye uhusiano usio na maana kwake. Hauna maana kwake kwa sababu, hana cha kutoa, ameshindwa wajibu wake katika uhusiano ambao ni kupenda. Kwa sababu hiyo, ni wazi hataweza kuendelea na mahusiano, ni lazima atasababisha uvunjike, kama tulivyoona.
Kama nawe hujui kupenda, utamuiga na utakuwa umeshindwa wajibu wako, kama yeye. Kwa hiyo, kwenye hali kama hiyo, hakuna kinachotolewa wala kupokelewa. Ni wazi uhusiano hauwezi kuwepo katika hali ya namna hiyo. Uzuri wa mmoja kuendelea kutoa bila kujali mwenzake anafanya nini ni kwamba, huyu mwenzake anaweza kungámua tatizo au kasoro yake na kubadilika.
CHANZO: MAPENZI KUCHIPUA NA KUNYAUKA/gazeti la Mshauri wako.
2 comments:
Ahsante sana Yasinta kwa makala nzuri ihusuyo upendo na mahusiano. Kwa kweli ni nzuri na nimeipenda kwani inaelezea hali halisi ya upendo wetu katika mahusiano.
Nijuavyo Mimi upendo ni hali ambayo ni ngumu sana kuieleza kwa maneno, ni rahisi zaidi kuieleza kwa vitendo.
Lakini Mara nyingi binadamu huzungumzia zaidi kitu ambacho hana. Akishakipata hawezi kukizungumzia. Kama unaumwa utazungumzia kuwa na afya njema, ukipona huwezi tena kuzungumzia afya njema.
Hapa leo tunazungumzia upendo kwa sababu hatuna upendo, tukiupata hatuwezi tena kuzungumzia upendo, bali tutazungumzia vitu vingine ambavyo hatuna.
Nijuavyo Mimi, upendo ni dhana pana sana. Na inachanganya zaidi pale inapohusishwa na tendo la kujamiiana. Ni kipi huanza..... Upendo au tendo la kujamiiana? Je, tendo la kujamiiana ni upendo? Je, upendo ni tendo la kujamiiana? Je, upendo na tendo la kujamiiana ni kitu kimoja au vitu viwili tofauti? Je, ukimpenda mtu ni lazima uvutiwe naye kimapenzi? Je, ukivutiwa na mtu kimapenzi ni lazima umpende?
Nijuavyo mimi, huwezi kumpenda mtu kama wewe mwenyewe hujipendi. Kujipenda ni nini? Ni kula vizuri ? Ni kuvaa vizuri? Watu wengi wanajua huko ndio kujipenda. Sisemi kwamba kula vizuri ni vibaya, wala sisemi kwamba kuvaa vizuri ni vibaya, ila ninachosema ni kwamba huko siyo kujipenda.
Kujipenda ni ile hali ya kujikubali jinsi wewe ulivyo, ni kujipokea jinsi ulivyo kimwili, kiakili, kihisia, kiroho, bila kutaka kujibadilisha wala kutamani kuwa kama mtu mwingine au kuwa kama fulani. Kujipenda ni kujikubali na kujipokea jinsi ulivyo na mapungufu yako yote, na madhaifu yako yote kwani huyo ndio wewe. Kujipenda maana yake ni kuwa wewe. Ukitamani au kutaka kuwa kama fulani maana yake ni rahisi tu, hujipendi.
Kujipenda ni hatua ya kwanza ya kuelekea kwenye kupenda, ni msingi wa upendo.
Ukiweza kujipenda, ni rahisi sana kumpenda mtu mwingine. Labda niseme hivi, kupenda ni matokeo ya kujipenda. Ni kama ilivyo utajiri ni matokeo ya kufanya kazi kwa bidii, ni kama ilivyo baraka ni matokeo ya kumcha Mungu, ni kama vile kuvuna ni matokeo ya kulima au kupanda.
Shida iliyopo hapa ni kwamba, watu wanataka kupenda kabla ya kujipenda, wanataka kuvuna kabla ya kupanda, wanataka kupata baraka bila kumcha Mwenyezi Mungu, kamwe na katu HAIWEZEKANI.
Kwa kuwa wanataka kufanya hatua ya pili kabla ya hatua ya kwanza ndio maana wanachoka kupenda. Utawasikia wakisema... Kama yeye hanipendi na Mimi siwezi kuendelea kumpenda, huu siyo upendo halisi, ni upendo wa masharti, nipende nikupende. Kwenye upendo halisi kuna kujipenda peke yake, Kupenda ni matokeo yake. Huwezi Kufanya mazoezi ya kupenda, ila unaweza kufanya mazoezi ya kujipenda. Huwezi kuvuna bila kupanda, ila unaweza kuvuna baada ya kupanda.....
Hii ni kanuni ya maumbile, kila kitu ni lazima kianzie kwako. Huwezi kumpa chakula mwenye njaa kama wewe una njaa. Kutoa ni lazima kuanzie kwako, ni lazima uwe na cha kutoa. Upendo wa kweli unajua kutoa tu, hufurahi pale unapotoa na husikitika unaposhindwa kutoa. Upendo wa kweli haujui kupokea. Upendo wa kweli hauchoki kutoa.
Lakini tunachokiona kwenye mahusiano ni kinyume chake. Eti upande unaotoa hufika mahali na wenyewe huchoka kama upande wa pili hautoi, huu siyo upendo wa kweli, huyu mtu hajipendi ila kaamua kupenda kabla ya kujipenda ndio maana amechoka. Kama angekuwa anajipenda asingechoka kutoa.
Kwa hiyo uhusiano wako wewe na watu wengine, hutegemea sana uhusiano wako wewe na wewe mwenyewe. Ninaposema uhusiano wako wewe na wewe mwenyewe nina maana moja tu, nayo ni kujipenda.
Nishauri tu kwamba kama kweli tunataka kuwa na upendo wa kweli, kama kweli tunataka kuwapenda wengine, kama kweli tunataka kutoa, ni lazima kwanza tujipende, tujikubali jinsi tulivyo, tujipokee jinsi tulivyo na mapungufu yetu yote, na madhaifu yetu yote, bila kutaka kujibadilisha, bila kutamani na kuwa kama fulani.
Inatosha kwa leo.
Kaka John...Kwanza nasema karibu sana Maisha na Mafanikio. Ahsante sana kwa maoni yako.
Ngoja niongezee kidogo hapa ina fanana kidogo na aliyosema kaka John:- Kwa hali hiyo, utakuta unaweza kuona jinsi upendo ulivyo kutoa na kupokea au njia mbili-kwenda na kurudi kama tusemavyo. Unapokuwa wa kupoke tu bila kutoa au wa njia moja, hauwezi kuendelea kuwepo
Post a Comment