Wednesday, January 18, 2012

HUYU NDIYE YASINTA NGONYANI!!!

Kama kawaida ni JUMATANO NYINGINE TENA NA NI KILE KIPENGELE CHA MARUDIO YA MATUKIO MBALIMBALI. Na Makala hii nimeshawahi kuiweka hapa. Lakini nimeshindwa kuvumilia kutoiweka hapa tena. Ni ZAWADI AMBAYO SITAWEZA KUISAHAU MILELE.

Yasinta Ngonyani, Picha kwa hisani ya Maisha Blog
Ni binti halisi wa kitanzania, ingawa anaishi ughaibuni lakini hujivunia asili yake na utaifa wake, ni binti pekee aliyejitolea muda wake kuwaelemisha watu wa rika zote bila kujali rangi, kabila, itikadi, taifa wala jinsia.


Binti huyu si mjivuni na hupenda kubadilishana mawazo na watu mbali mbali, na pia hupenda kufuatilia habari za nyumbani kwao alikotoka na haoni tahayari kuongea lugha ya kwao. Daima hujitambulisha kwa jina la asili ya kwao na huona fahari kutumia jina hilo.


Binti huyu hakuona ajizi kuwajuza wanae asili ya kwao japo wamezaliwa ughaibuni, amekuwa msitari wa mbele katika malezi ya wanae ili kuhakikisha wanae hao hawajitengi na asili ya aliotoka yeye.


Si mchoyo wa ushauri na kupitia makala zake aziwekazo kibarazani kwake amekuwa ni msaada kwa wengi, amekuwa mstari wa mbele katika kuilemisha jamii bila kujali rika. Amejitolea kufundisha kile akijuacho juu ya malezi na matatizo mbali mbali yanayowakabili wanandoa na malezi ya watoto.


Kibaraza chake kimekuwa ni kitovu chenye kukutanisha wadau mbali mbali wenye fikra pevu, na kuibua mijadala yenye kuelimisha, kufundisha, kuburudisha na kuhuzunisha pia.


Binafsi napenda kumuita dada na kwangu mimi ni zaidi ya dada, kwani amekuwa ni mwalimu mzuri kwangu nikijifunza mambo mengi kupitia kibaraza chake nimekuwa nikijifunza mengi, na sisiti kukiri kwamba chimbuko la kibaraza cha VUKANI ni kutokana na kile nilichojifuza kwake.


Ni mkweli na muwazi, na hasiti kusema wazi hisia zake, lakini huwa makini sana ili kuepuka kumuumiza mtu mwingine kihisia, na kama kwa kusema huko kutamkera mtu mwingine, ni mwepesi kuweka sawa maelezo yake ili kuondoa msigishano wa mawazo.


Nakumbuka wakati fulani nlipopata msongo wa mawazo kutokana na tofauti zangu na wazazi wangu, alikuwa ni mtu wa kwanza kunitumia email binafsi akijaribu kuniliwaza na kunitaka nisichukue hatua yoyote kujidhuru, naomba nikiri kwamba email ile ilinisaidia sana kurudi katika hali yangu ya kawaida na nilijisikia fahari kuona kwamba kuna mtu ananipenda na kunijali japo sijawahi kuonana naye uso kwa uso.


Huu kwangu ulikuwa kama muujiza, inakuwaje, mtu kusoma mawazo yangu kupitia blog tu halafu awe karibu nami kiasi hiki, ni kitu gani kimemvuta? Kusema kweli tangu siku hiyo niliamni kuwa maandishi yana nguvu sana na kupitia maandishi yawezekana mtu mwingine kukufahamu vizuri sana.


Nimekuwa karibu sana na binti huyu, na amekuwa ni mwema sana kwangu na mshauri wangu pia, na kupitia vibaraza vyetu, tumekuwa tukibadilishana mawazo na kupeana ushauri mbali mbali ili kuboresha ustawi wetu na wa familia zetu.


Huyu ndiye Yasinta Ngonyani, kwa kumsoma zaidi bofya hapa.


-------------------------------------------------------------------------------------------------Makala hii iliandikwa na mdogo wangu wa hiari Koero Mkundi mwaka 2009/08/14 bado nimevutiwa sana na hii makala na nimeona niiweke hapa kwangu pia kama kumbukumbu na pia kujikumbusha yaliyopita kwani si vibaya. Pia nachukua nafasi hii kwa kumshukuru sana mdogo wangu huyu wa hiari Koero Mkundi kwa kazi nzuri anazozifanya kwa kumsoma zaidi kazi zake ingia hapa. Pia nauthamini sana uwepo wake Mwenyezi Mungu na akulinde na akuongoze na yote utendayo yawe mema. Kwani yeye ndiye mwezeshaji wa yote na yeye ndiye ajua anavyotuwazia maana mawazo atuwaziayo ni mema. Ni hayo tu kwa leo...Halafu sijui upo wapo Koero?
TUKUTANE TENA JUMATANO IJAYO AU WAKATI MWINGINE....


10 comments:

ray njau said...

Kila kuendako hisani hakurudi nuksani bali shukrani na ubaya hauna kwao lakini wema hauozi.

Rafikiyo wa Hiari said...

Napenda kuchukua fursa hii na mimi kutoa yangu machache yafananayo na Koero kuhusu Yasinta. Nitakua mchache wa fadhila na sitautendea haki moyo wangu na kikubwa sitakutendea haki endapo nitakaa kimya kwa hili. Kapulya ni rafiki yangu wa hiari, si kwamba tumeshawahi kuonana uso kwa uso ama tunafahamiana, la hasha, ni kupitia hapa kwenye uwanja wake ndio tukafahamiana na hatimaye mimi kumchukulia kama mtu muhimu sana kwangu, namuona ni zaidi hata ya rafiki ambao ninapishana nao kila siku.
Nilikuja hapa nikiwa nimeelemewa na matatizo mazito, Yasinta alijitolea muda wake mwingi sana kunisaidia mwisho wa siku nikaweza kupata kile nilichokua na kihitaji, yaani mchango wa mawazo ya wadau ambao nao pia kama alivyo mwenyewe ni wastaarabu na mawazo yao kwa kweli yameniweka imara. Sababu kubwa pia iliyonifanya nije kutoa dukuduku langu hapa kwake 1) ukarimu wake kupitia maandishi tu unaweza kujua ni mtu wa namna gain – asiyependa majivuno wala maringo 2) uwakilishaji wa mawazo yake 3) jukwaa la wadau alilonalo ni lile lenye kujiheshimu kama yeye mwenyewe anavyojiheshimu; hayo ni baadhi tu ya mambo yaliyonivutia kwake Yasinta.
Kwa ufupi napenda kutumia wasaa huu kukushukuru sana Rafiki yangu wa Hiari Kapulya. Mungu azidi kukubariki wewe pamoja na familia yako yote kwa ujumla.

ISSACK CHE JIAH said...

Kwakweli nami nitakuwa sijamtendea haki na mimi ni Dada yangu wa hiyari kwakweli huyu dada sijawahi kuonana hata siku moja ila kisa cha mimi na huyu dada anakifahamu sana yeye mwenyewe na mimi ndipo nilpoanza kuipenda BLOG hii ya maisha Kwakweli huyu dada nimefahamiana kwa njia hii na si muda mrefu ila mimi amesha nifahamu kiundani na yeye kwa upande wake nimeufahamu kidogo kwakweli ila ni mcheshi na si mtu wa kukasirika nakumbuka siku alinipigia simu na akawa anaimba ule wimbo ambao ulikuwa unaimba wa haleluya hapo kuna kitu kilipita ila kwakweli nilimwomba radhi naye alinisihi sana kwakweli toka siku hiyo nilipata elimu ya kutoka diploma na kwenda digree nashukuru tulisamehana na mpaka leo nisiposoma maisha lazima nimtumie email na hata wakati mwingi tunapeana ushauri kuhusu familia zetu na huwa ananipa moyo kuhusu kusomesha wototo n.k huyu hana mfano hasa kwa upande wa jinsia yake yaani akina dada ni mdogo wangu mimi napenda nimwite dada binamu kwani kwetu huwa tunataniana sana kaka na dada binamu ukweli nitajaza kurasa bure kwakweli huyu ni kipaji chake leo niishie hapo nugu zangu wasomaji wenzangu kesho kutwa nami ni BESI DAI YANGU TAREHE 21/1/2012 Nnatimiza miaka kadhaa ila nisifiche baada ya hapo besidai itakayo fuata nitatimiza jubilie wataalamu mnajuwa ndugu yangu mfalume MROPE nitumie ile zawadi yetu ya nyumbani hatu ngumbi nitumie au...nuume nk.
kwaheri

Che JIAH

Rachel Siwa said...

Mimi ngoja niseme Haleluyahhhhhhh,Mungu anakila sababu ya kunikutanisha na da'Yasinta,Mungu akubariki sana wewe na familia yako.UBAYA HAUNA CHEO NA WEMA HAUOZI WAPENDWA!!!MBARIKIWE SAAANA WOOOTE.

Simon Kitururu said...

Naona wengine mmenisemea tayari! ubarikiwe Mdada!

Unknown said...

Mimi chichemi neno.. Nikichema mtachema mimi Mmakonde!. Watu tuliokaribu nawe tunajivunia kukufahamu na pia kumshukuru Mungu kwa uwepo wako miongoni mwetu.. Ahsante kwa kuwa wewe ni Yasinta Ngonyani..

PASSION4FASHION.TZ said...

Niliyotaka kusema yote yameshasemwa,na walionitangulia ubarikiwe sana wewe pamoja na Koero.

Said Michael said...

Natamani kusema! Lakini yote yamesemwa, sipendi kuitwa mzee wa kukopi: HONGERA>: Nimepita kukusabahi baada ya kupata salamu zako kwangu

chib said...

:-))

Yasinta Ngonyani said...

Wote nawashukuru sana kwa mchango wenu. Ni furaha kila wakati nisomapo maoni yenu kiasi kwamba natokwa na machozi ya furah. Nafurahi kwa kuona mna tabia ambayo naipenda sana kusema kile mlichonacho moyoni kabla yule anayetaka kukisikia hajaiacha dunia hii. Maana mara nyingi watu huwa waoga kusema kwa yule anayewatendaa kitu akifa ndo wanasema ...Hilo ndilo katika maisha yangu nalipenda sana yaani kuwa muwazi. Koero sijui upo wapi? Mwenyezi Mungu akubari na akujalie maisha mema na yenye furaha na nakutakia siku moja uwe mwandishi kwani kipaji hiki unacho. AHSANTE SANA KWA ZAWADI HII SITAITUPA NA WALA SITAKUSAHAU MILELE.