Monday, January 30, 2012

WANAUME NA KAULI HIZI: 'HUYO SIO WA KUOA, NI WA KUCHEZEA TU'

Bila shaka wewe msomaji unayesoma hapa utakubaliana na mimi kuwa umeshawahi kuzisikia kauli hizi kutoka kwa wanaume pale anapozungumziwa mwanamke mzuri kwa sura na umbo.

Kwa kawaida vipimo vya uzuri wa mwanamke kwa wanaume vimegawanyika. Wanaume wengi hupima uzuri wa mwanamke kwa sura au umbo, lakini linapokuja swala la kuoa, suala la tabia na mwenendo hupewa nafasi kubwa.
Na ndio maana wakati mwingine unaweza kushangaa kukuta mwanaume ambaye ni hodari wa kuchagua wanawake wazuri, lakini ukija kumuona mke aliyemuoa, utakuta ni mbaya kwa sura na umbo, lakini kwa upande mwingine utakuta mke huyo ni mzuri katika maeneo mengine kama vile, tabia nzuri,upendo, wema, na anayemudu malezi ya watoto katika familia.

Sifa nyingine ni zile za kumkubali mwingine kirahisi, kuwa tayari kusaidia yanapojitokeza matatizo katika familia, mpenda amani na kumfanya mume wake aone kuwa hakukosea kumchagua yeye kuwa mke wake. Kwa kifupi wanawake wa aina hii hata kama wangekuwa ni wabaya kwa sura na umbo bado wako kwenye nafasi ya kuonekana kuwa ni wazuri, na huolewa kirahisi zaidi.

Wanawake wazuri kwa sura na umbo ambao tabia na mienendo yao hairidhishi wako kwenye nafasi kubwa ya kuishi bila kuolewa, na kwa bahati mbaya zaidi wanawake wengi wanaohesabika kuwa ni wazuri, tabia na mienendo yao ni ya kutilia mashaka. Wanaume wengi huvutiwa na wanawake hao kujenga uhusiano nao hasa wa kimwili tu na si vinginevyo, na ndio maana wanawake wazuri kwa sura na umbo wanalo soko kubwa sana kwa wanaume, lakini huishia kuchezewa zaidi kuliko kuolewa.

Wanaume nao kwa upande wao wamejenga dhana kwamba wanawake wazuri sana sio wa kuoa na hivyo kuwaogopa. Wanaamini kwamba wanawake wazuri sana ni wasumbufu, kitu ambacho kina ukweli kwa kiasi fulani. Wanaume wanaamini kwamba wanawake wazuri sana kwa sura na umbo huwasababishia waume zao maradhi ya moyo,shinikizo la damu na wakati mwingine hata kuwafanya kupata matatizo fulani ya kiakili, na hiyo inatokana na waume hao kuwa katika mashaka ya wake zao kuchukuliwa na wanaume wengine wakati wowote kutokana na uzuri wao. Hata hivyo wanawake wazuri nao huwaendesha waume zao wakijua kuwa ni wazuri na soko lao liko juu na waume zao nao huwanyenyekea wakihofia kuachwa.

Na ndio maana usishangae kuona kuwa wale wanawake ambao watu wamekuwa wakiamini kuwa ndio wabaya kwa sura au umbo lakini tabia na mienendo yao ni mizuri ndio wanaoolewa na hata ndoa zao zinadumu, tofauti na za wale wanaoonekana kuwa ni wazuri sana kwa sura na umbo na ambao tabia na mienendo yao si mizuri, ndoa zao hazina umri mrefu

8 comments:

ray njau said...

Wanawake ni viumbe wenye thamani sana na wanahitaji staha na heshima kwa kuwa ni mama zetu waliotunyonyesha na kutulea kwa mikono salama.Ni wake zetu wapendwa na tumewakabidhi dhamana ya maisha yetu kwa viapo vya ndoa na kuahidi mtengano uwe ni kifo tu.Ni dada zetu wema sana katika familia wakiziremba familia zetu kwa khanga,vitenge na cherekochereko.Kwa tunaposema ni wa kuchezea tu tunajitukana sisi wenyewe mioyoni mwetu na ni aibu yetu wenyewe.

EDNA said...

Daah! inauma sana ukisikia mwanaume anasema maneno hayo.

sam mbogo said...

Da ,Edna usisikitike sana, ukisikia mwanaume anasema maneno hayo ujuwe anakasoro/mapungufu/hajiamini pia ni mshamba. kaka s

Swahili na Waswahili said...

Ahsanteni wapendwa kaka Rau tena thamani yajuu,@yaani dada Edna unaweza pata wazimu,@ kaka wa mimi barafu yangu mwana wa Sam leo nimekukubali zaidi!!!!!Mbarikiwe wooote,tena Msiondoke hivihivi mimi nakuna nazi ya kuungia chai mama mwenye nyumba ndiyo kanituma.

ray njau said...

@Rachael asante sana kwa niaba ya mama mwenye nyumba.Chai yako ya tui la nazi ni tamu sana lakini hatuna hakika iwapo baba mwenye nyumba ana taarifa ya wewe kuwahudumia wageni kwa niaba ya mama mwenye nyumba japo hiyo ni sehemu ya ujirani mwema.

Anonymous said...

wanawake wazuri kweli niwakulamba na kuondoka maana ule uzuri wao unawazuzua kila anayeomba anapewa hapo ndo huwa nashangaa

SIMON KITURURU said...

Mmmmh!

Yasinta Ngonyani said...

Kwanza nnapenda kusema nimeyapenda sana maoni yenu.Na ninawapendeni wote.
Hii mada imekuwa si ya kubagua, nimeandika kwa kuangalia pande zote. Kwani mara nyingi wengi wamekuwa wakisema napendelea upande mmoja.

Nawashukuru wote kwa mchango wenu nami nimezidi kujifunza mengi toka kwenu ambayo sikujua. Ni kweli hakuna hapa duniani aliye sawa kabisa, kila mtu ana kasoro yake.
Ni kweli pia ukiwa na sura nzuri na umbo zuri kazi kwelikweli. lakini mimi sioni kama kuna watu WABAYA na WAZURI. Kama nakumbuka vizuri muimbaji Marehemu dr. Remmy Ongala aliimba kama wewe ni mbaya basi oa mke mbaya na kama wewe ni mzuri basi ou mke mbaya. Hapo utakuwa umepunguzi mgogoro wa kusema mimi MZURI na mimi MZURI.Namalizia kwa kusema kweli:- Ndoa ni changamoto, inahitaji kila kukicha utunge mkakati mpya. ruksa kuendelea na mjadala.