Monday, July 6, 2009

YEBOYEBO: USAFIRI WA PIKIPIKI ULIOGEUKA KICHAKA CHA UBAKAJI RUVUMA

Ilitoka katika gazeti la mwanchi
Nimeona si vibaya kama wote tukijua yanayotokea mkoani Ruvuma.

Tatizo la wanawake kubakwa mkoani Ruvuma limekuwa likiongezeka siku hadi siku na kuwafanya wanawake wengi kuishi kwa woga.
Watuhumiwa wakubwa wa vitendo hivi ni madereva wa pikipiki ambao wanafahamika kwa jina la Yeboyebo ingawa pia wamo wanaume wengine katika makala haya Mwandishi Wetu Joyce Joliga anaeleza athari za tatizo hilo.
HUDUMA ya usafiri wa pikipiki ambayo inajulikana kama Yeboyebo mkoani Ruvuma umekuwa na msaada mkubwa kwa wakazi wake. Hawalazimiki tena kutumia fedha nyingi au kutembea kwa miguu mwendo mrefu wala kusongamana katika mabasi ambayo hayakuwa na uhakika.
Si hayo tu, vijana wengi ambao walikuwa wakizurura ovyo na wengine kujiingiza katika vitendo vya uhalifu wamebadilika kwani wamepata ajira na hivi sasa wanaendesha maisha yao kutokana na kazi hiyo ya kuendesha pikipiki.
Hata hivyo, kama wahenga wasemavyo, kila masika yana mbu wake, usafiri huu umesababisha madhara kadhaa. Hayo ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya ajali. Wananchi kadhaa wamepoteza maisha na wengine kupata ulemavu wa maisha kutokana na ajali zilizosababishwa na pikipiki hizi.
Chanzo kikubwa cha ajali hizi ni uendeshaji usiozingatia sheria ikiwa ni pamoja na vijana wengi kutokuwa na ujuzi wa kutosha kwani wengi hawakusomea na badala yake wamekuwa wakijifunza kienyeji tu.
Lakini tatizo kubwa jingine ambalo limesababishwa na kuwepo kwa aina hii mpya ya usafiri mkoani Ruvuma ni kuongezeka kwa matukio ya ubakaji ambayo yamechangia pia ongezeko la maambukizo ya ukimwi, magonjwa ya zinaa, mimba zisizotarajiwa na mauaji.
Waathirika wakubwa wa vitendo hivi ni wanawake hasa wale wanaofanya kazi hadi usiku hivyo kuhitaji usafiri huo kuwarejesha makwao au wanaokwenda katika starehe na harusi.
Pamoja na vitendo hivi kutokea mara kwa mara, vinavyoripotiwa ni vichache mno. Ni wanawake wachache ambao wamekuwa wakithubutu kutoa taarifa katika vituo vya polisi wanapofanyiwa ukatili huo sababu ikiwa ni hofu ya kudharauliwa, kuchekwa au kutengwa na jamii.
Kamanda wa Polisi Mkoa Ruvuma, Michael Kamuhanda anasema kuwa idadi ya wanawake waliobakwa na kuripotiwa mwaka jana ni 298 na Wilaya ya Songea ndiyo iliyoongoza kwa kuwa na idadi ya wanawake wengi waliobakwa ikifuatiwa na Mbinga na Namtumbo.
"Tatizo la ubakaji bado ni kubwa mkoani kwetu. Kwa mfano, Januari mwaka huu wanawake 24 walibakwa. Februari wanawake 25 na Machi walikuwa 37 na hadi kufikia April 3, tayari wanawake watano walikuwa wamebakwa hivyo kufanya jumla ya wanawake waliobakwa mkoani wetu tangu Januari hadi Aprili 3, kufikia 91," anasema Kamuhanda.
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Ruvuma, Baptista Mhelela anasema kuwa mwaka 2008, kesi 39 zilifunguliwa na kati ya hizo, 20 zilisikilizwa na watu nane walihukumiwa vifungo baada ya kupatikana na hatia za kutenda kosa hilo na kesi 19 zinaendelea kusikilizwa.
Anasema mwaka huu kesi 14 zimefunguliwa hivyo kufanya kesi zilizopo katika mahakama hadi sasa kufikia 28.
Mbali ya kubakwa, wanawake wengi wamekuwa wakiporwa mali zao kama fedha, simu za mikononi na vitu mbalimbali vya thamani. Pia wamekuwa wakipigwa na hata kutelekezwa porini au njiani kabla ya kufikishwa waendako.
Kutokana na adha hiyo, wapo wanawake walioamua kuyakimbia maeneo waliyokuwa wakiishi kuepuka aibu lakini wapo walioamua kujiua kutokana na msongo wa mawazo.
Wanawake waliohojiwa wanakiri kufanyiwa vitendo hivyo lakini wamekuwa waoga kutoa taarifa hizo katika vyombo vya dola kwani wengi wao ni wachumba au wake za watu hivyo kuhofia kuachwa.
Halima Rashid (26) anasema alibakwa na mmoja wa madereva wa pikipiki hizo hadi kupata ujauzito. Hamjui baba wa mtoto wake hadi leo na anasimulia kwamba mara baada ya kugundua kwamba amepata ujauzito, alifikiri kutoa mimba hiyo lakini aliogopa baada ya kuelezwa kuwa angepoteza maisha... "Nililazimika kulea mimba hiyo kwa shida huku watu wakinicheka na kuninyanyapaa."
Anasema pamoja na adha hiyo ya kuchekwa hakukata tamaa, aliendelea kufanya vibarua vya kusaidia kuuza chakula kwa mamalishe hadi alipojifungua.
Lakini anasema alilazimika kuondoka eneo alilokuwa anaishi awali la Minazini, Namtumbo baada ya kuchoshwa na kebehi za majirani na baadhi ya ndugu zake na kwenda kuishi Songea ambako anaendesha maisha yake kwa kuuza baa na huku akimlea mwanae wa kiume ambaye sasa ana umri wa mika miwili.
“Sikutoa taarifa popote baada ya kubakwa. Mama yangu alitaka nifanye kuwa ni siri, tulikubaliana nisiende kuripoti polisi kwani mtu aliyenibaka nilikuwa simjui ingawa alinibeba kwenye pikipiki.”
"Nilimlipa Sh2,000 lakini bado alinitupa chini na kuniingilia kwa nguvu, niliumia kwani nilichanika vibaya na baada ya mwezi kupita niligundua kuwa nimenasa ujauzito nikamweleza mama akanitahadharisha nitunze kiumbe hicho kwani ningetoa ningeweza kupoteza maisha. Ingawa niliumia sana moyoni nilikubaliana na ushauri wa mama yangu nikakubali kulea tumbo hadi sasa nimefanikiwa kupata mtoto,' anasema Halima
Mhudumu wa Baa ya Mtini Pub, Oliver Lwambano anasema rafiki yake ambaye hata hivyo, hataki kumtaja jina amewahi kubakwa na dereva wa Yeboyebo baada ya kudaiwa kwamba hakulipa nauli.
Anasema licha ya kufanyiwa unyama huo, mwanamke huyo aliogopa kutoa taarifa polisi na kubaki nyumbani akijiuguza baada ya kuambukizwa ugonjwa wa zinaa.
Kamanda Kamuhanda anawatoa hofu wanawake wanaoogopa kutoa taarifa hizo akisema kwamba ofisi yake imeanzisha kitengo maalumu cha polisi wanawake ambacho kinashughulikia matatizo hayo kwa usiri mkubwa.
Anasema kuna viongozi wanawake ambao kazi yao katika kitengo hicho ni kusikiliza siri za wanawake ambao wamebakwa na kuchukua hatua.
Madereva wa pikipiki hizo wanakiri kuwepo kwa vitendo hivyo, Shaban Kassim (39), anasema amewahi kusikia kwamba kuna wenzake ambao wamekuwa wakiwaingilia wateja wao wa kike kwa nguvu. Hata hivyo, anasema wanaofanya hivyo ni wahuni ambao wanajificha katika biashara ya kusafirisha abiria kwa pikipiki.
"Taarifa hizi zinatuumiza sana moyo hasa sisi ambao tunafanya biashara hii kwa lengo la kujipatia kipato cha kuendesha maisha yetu na familia zetu. Wanatuharibia biashara kwani wateja wengi ni wanawake nao wamekuwa wakituogopa na kutuita wabakaji lakini si wote ambao tunafanya vitendo hivyo," anasema Kassim na kushauri:
"Ilikupunguza tatizo hili ni vyema pikipiki zote ziwe na namba za usajili na za utambulisho, tena ziandikwe ubavuni ili kuzitambulisha kama zinavyoandikwa namba za magari, nafikiri hii itatusaidia kuwajua wabakaji ambao wanajificha katika biashara hii."
Anawashauri wateja kujenga tabia ya kukariri namba za pikipiki ikibidi kwa siri ili wanapofanyiwa ubaya wowote wajue jinsi ya kuwanasa wahalifu wao.
Dereva mwingine Zidadu Seleman (32), anasema baada ya kusikia tuhuma hizo zikielekezwa kwao aliwauliza wenzake ambao walikiri kuwepo kwa vitendo hivyo.
Anasema vitendo hivyo vya ubakaji vinatia doa biashara yao na kuwaweka wahusika katika hatari ya kuambukizwa magonjwa ya zinaa ukiwemo ukimwi.
Mwendesha pikipiki mwingine, Binaya Waliya (29) maarufu kwa jina la Suzuki Buzu anasema wanaofanya vitendo hivyo wanajulikana akiongeza kwamba baadhi yao pia ni wezi, na wanawanyanyasa wateja wao hasa kina mama.
Mkuu wa Wilaya ya Songea, Thomas Sabaya anasema tayari wameanza kudhibithi tatizo hilo na kwa kuanzia polisi inafanya doria usiku na mchana. Ili kuhakikisha kuwa ulinzi unaimarika, kila kata imepangiwa polisi wanne.
Sabaya amepanga kukutana na madereva wote wa Yeboyebo waliopo katika Wilaya ya Songea ili kuzungumza nao na kuwabaini wanaofanya vitendo hivyo ili washugulikiwe na vyombo vya dola.
Anawataka wanawake kuacha kutembea usiku wakiwa peke yao na badala yake watumie vyombo vya usafiri ambavyo ni salama kwa maisha yao.
Kwa upande mwingine, anawataka madereva Yeboyebo kuzingatia sheria ili kurudisha imani kwa wananchi kwa kuwafichua wenzao wanaowabaka wanawake ili kupunguza malalamiko kutoka katika jamii.

5 comments:

Nicky Mwangoka said...

Loh kumbe ni hivyo, poleni sana wanaRuvuma. Ila inabidi kuweka mikakati ya kudhibiti hali hiyo. Asante Da' Yasinta kwa kutushirikisha hilo.

Simon Kitururu said...

Inasikitisha!:-(

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

aisee

Bennet said...

Natoa pole kwa wanawake wote hata wale ambao hawakubakwa, niliwahi kusikia tatizo hili lakini sikufikiria kwamba ni kubwa kiasi hiki (idadi ya wabakwaji)
Hizi pikipiki zimekuwa msaada mkubwa sana kwetu lakini zimekuja na hayo mabalaa mengine hapa lazima kifanyike kitu

Christian Bwaya said...

Du:-(