Monday, May 28, 2012

JE? LAKINI ULIPENDA NINI AWALI?

Hili ni jambo muhimu sana, Tunapomwona mtu kwa mara yakwanza akatuvutia, tunaweza tusijue ni kwa nini ametuvutia, lakini kama tutakuwa wadadisi, tunaweza kubaini kwamba, tumevutiwa na sura, miguu, macho, nywele, mavazai au kingine.  Inaweza kuwa  ni kwa sababu ya kipaji chake, uwezo, umaarufu na vitu vya aina hiyo.
Tunashauriwa kujiuliza kitu au jambo ambalo limetufanya tumpende mtu fulani. Je?, tumevutiwa kwa mguu wake, kwa jicho lake, elimu yake, kipaji chake au kitu kingine tunachokifahamu?

Kama ni kwa kitu tunachokifahamu, tunatakiwa kujiuliza kama kitu hicho ni cha muda au cha kudumu. Kama ni cha muda, kama ilivyo kwa wengi, inabidi tujifunze jambo jipya. Inabidi tujifunze kutafuta kitu cha kudumu ambacho tutakipenda kwa  wapenzi wetu.  Kwa nini?
Kwa sababu, vile vyote vilivyo nje, ambavyo tulivipenda kwa sababu tumeviona,  havidumu sana, ukiwemo mwili kwa ujumla. kwa hali hiyo kama tulimpenda mtu kwa sababu ya mguu, jicho, tabia, fedha, umaarufu. Hivi vyote kuna siku vitachuja au kwisha au kubadilika, na hapo utakuwa ndiyo mwisho wa upendo wetu kwa watu hao.

Lakini kwasababu tulijifunga nao kwa ndoa, tunabaki tukiwa na hasira za kujifunga na watu ambao hatukujua kwamba, hatukuwa tukiwapenda. Tutakorofishana mahali ambapo tulipaswa kufurahi, tutakorofishana mahali ambapo tulipaswa kupendana zaidi.
Kwa sehemu kubwa, unakuta tangu awali tulikuwa hatujapendana. Tangu tulipokutana kwa mara ya kwanza tulitamaniana tu. Tulitamani sifa za muda mfupi, ambazo hatimaye hufutika.

Ni kweli kwamba, kule tunakoita kupendana ambako hutokea tunapokuwa ndani ya ndoa, huanza kwa sisi kukutana kwanza, halafu kwa kila mmoja kuwajibika kwa upande wake, kupendana hutokea. Kupenda kumo ndani mwetu, ni jukumu letu kujua hilo na kukutoa huko kupenda ili kumudu kufurahia maisha na wengine.
Chanzo:- kitabu cha MAPENZI KUCHIPUA NA KUNYAUKA na MUNGA TEHENAN.
MWANZO MWEMA WA JUMA.

3 comments:

ray njau said...

1. Biblia husema kwamba mume ndiye kichwa cha familia yake. (1 Wakorintho 11:3) Ni lazima mume awe na mke mmoja tu. Wao wapaswa kuwa wameoana ifaavyo kisheria.—1 Timotheo 3:2; Tito 3:1.

2. Mume apaswa ampende mke wake kama vile ajipendavyo mwenyewe. Apaswa amtendee kwa njia ambayo Yesu huwatendea wafuasi wake. (Waefeso 5:25, 28, 29) Hapaswi kamwe kumpiga mke wake wala kumtenda vibaya kwa njia yoyote ile. Badala ya hivyo, apaswa amwonyeshe heshima na staha.—Wakolosai 3:19; 1 Petro 3:7.
Mungu huwatazamia wazazi wawafundishe watoto wao na kuwasahihisha

3. Baba apaswa afanye kazi kwa bidii ili kutunza familia yake. Ni lazima baba awaandalie mke na watoto wake chakula, mavazi, na nyumba. Ni lazima baba aandalie pia mahitaji ya kiroho ya familia yake. (1 Timotheo 5:8) Yeye huongoza katika kusaidia familia yake ijifunze kumhusu Mungu na makusudi Yake.—Kumbukumbu la Torati 6:4-9; Waefeso 6:4.

4. Mke apaswa awe msaidizi mwema kwa mume wake. (Mwanzo 2:18) Yeye apaswa kumsaidia mume wake katika kufundisha na kuzoeza watoto wao. (Mithali 1:8) Yehova humtaka mke ashughulikie familia yake kwa upendo. (Mithali 31:10, 15, 26, 27; Tito 2:4, 5) Yeye apaswa awe na staha yenye kina kwa mume wake.—Waefeso 5:22, 23, 33.

5. Mungu hutaka watoto wawatii wazazi wao. (Waefeso 6:1-3) Yeye huwatazamia wazazi wawafundishe na kuwasahihisha watoto wao. Wazazi huhitaji kutumia wakati pamoja na watoto wao na kujifunza Biblia pamoja nao, wakishughulikia mahitaji yao ya kiroho na ya kihisia-moyo. (Kumbukumbu la Torati 11:18, 19; Mithali 22:6, 15) Wazazi hawapaswi kamwe kuwatia nidhamu watoto wao kwa njia yenye ukali bila huruma au iliyo katili.—Wakolosai 3:21.
6. Wenzi wa ndoa wanapokuwa na matatizo ya kupatana, wanapaswa kujaribu kutumia shauri la Biblia. Biblia hutuhimiza tuonyeshe upendo na kuwa wenye kusamehe. (Wakolosai 3:12-14) Neno la Mungu halipendekezi kutengana kuwa njia ya kusuluhisha matatizo madogo. Lakini huenda mke akachagua kumwacha mume wake ikiwa (1) mume akataa kishupavu kutegemeza familia yake, (2) yeye ni mjeuri sana hivi kwamba afya na uhai wa mke umo hatarini, au (3) upinzani wake wa kupita kiasi hufanya isiwezekane kwa mke kumwabudu Yehova.—1 Wakorintho 7:12, 13.

7. Ni lazima wenzi wa ndoa wawe waaminifu kwa mmoja na mwenzake. Uzinzi ni dhambi dhidi ya Mungu na dhidi ya mwenzi wa mtu. (Waebrania 13:4) Mahusiano ya kingono nje ya ndoa ndio msingi pekee wa Kimaandiko kwa talaka inayoruhusu mtu aoe au aolewe tena. (Mathayo 19:6-9; Warumi 7:2, 3) Yehova huchukizwa wakati watu wanapotalikana bila misingi ya Kimaandiko na kuoa au kuolewa na mtu mwingine.—Malaki 2:14-16.

Rachel Siwa said...

Mmmhh ngoja nijifunze kitu hapa,Asante sana Kadala!
Wenu Kachiki!!!!!

Salehe Msanda said...

Ni kweli wengi tunatamana na huwa tunaponzwa na jicho la siku yakwanza. matokeo yake tunaingia katika mhemuko wa kutamani na kujidanganya kuwa tumependa. Kibaya zaidi wengi tuna njaa ya kupendwa wakati hatuna uwezo wa kumfanya mwingine atupende zaidi ya kuanza sisi kuonyesha upendo. Upendo hauji kwa malipo au kwa kuudai. Unatoka ndani mwaka kama alivyosema marehemu munga. Tukiwapenda wengine badala ya kungojea kupendwa maisha yatakuwa mazuri na yenye upendo.

Tafadhali jaribu kuweka pembe tatu ya hicho kitu kinachoitwa kupenda kutoka katika kitabu cha munga ili tubaini tunaunganishwa na upendo upi.

Kila la kheri