Wananchi wa Kijiji cha Mtua ambacho kinapakana na pori la wanyamapori la Liparamba wilayani Mbinga mkoani Ruvuma wapo katika hatari baada ya ugonjwa wa kifafa kushambulia karibu kijiji kizima.
Uchunguzi umebaini kuwa katika kijiji hicho chenye wakazi zaidi ya 1,600 watu 200 wanadaiwa wanaugua kifafa ambapo kila nyumba kuna mgonjwa mmoja wa kifafa na baadhi ya nyumba zina wagonjwa wawili hadi watatu hali ambayo inasababisha wananchi wa kijiji hicho kuhitaji msaada mkubwa kutoka wizara ya afya na ustawi wa jamii kwa lengo la kukinusuri kijiji hicho.
Kijiji cha Mtua kipo katika kata ya Mpepai ambapo inadaiwa ugonjwa huo ulianza kuwashambulia watu wachache mwaka 1996 ambapo hivi sasa umeenea katika kiwango cha kutisha ukilinganisha na vijiji vingine vya Lipilipili,Kihungu na Changarawe, hivyo kukifanya kijiji hicho kuongoza katika wilaya ya Mbinga na mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.
Samweli Matembo ni mwenyekiti wa kijiji cha Mtua anasema tatizo la kifafa ni kubwa katika kijiji hicho ambapo idadi ya wagonjwa inazidi kuongezeka siku hadi siku na kusisitiza kuwa wananchi wengi wanaamini ugonjwa huo ni wa kurithi na kwamba inadaiwa ugonjwa huo unasababishwa na ulaji wa nyama ya nguruwe ambayo haijaiva vizuri,imani za kishirikina,unywaji wa pombe kupita kiasi na kuoa au kuolewa katika ukoo ambao umeaathirika.
“Tatizo hilo lilianza polepole mwaka 1996 na linazidi kuongezeka kwa kasi ambapo hivi sasa wananchi wanashindwa kufanya kazi zao za kiuchumi na kubakia masikini kutokana na muda mwingi kutumia nyumbani kuwaangalia wagonjwa wa kifafa ambao wanahitaji uangalizi wa hali ya juu hasa kwenye moto na maji,hivi sasa wagonjwa wanatumia dawa za hospitali lakini bado tatizo ni kubwa,tunawaomba watalamu wajitahidi kufika hapa ili watusaidie’’, anasema mwenyekiti mstaafu wa kijiji John Nchimbi.
Kondrad Nyika mzee wa miaka 70 anasema katika nyumba yake wapo wagonjwa wa kifafa watatu akiwemo mke wake ambaye anasema kifafa kilimuanza wakati anapika ugali ambaye hivi sasa anatumina dawa za hospitali na hali yake inaendelea vizuri na kwamba watoto wake wawili bado wanaendelea kuugua kifafa bila kupata nafuu licha ya kutumia dawa za hospitali.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mtua wilayani Mbinga wakimwelezea mwandishi wa habari hizi kuhusu tatizo la ugonjwa wa kifafa lilivyoathiri kijiji kizima kutokana na kila nyumba kuwa na mgonjwa wa kifafa
John Nchimbi anasema idadi kubwa ya wanafunzi wa shule ya msingi Mtua wanadaiwa wanaugua ugonjwa wa kifafa hali ambayo inasababisha wengi kuwa watoro na kuacha shule hata wale ambao wanasoma wameathirika na kushinda kufuatilia masomo kutokana na ugonjwa huo kuathiri ubongo.
Denis Nchimbi mwanafunzi anayeugua kifafa aliungua moto baada ya ugonjwa kumuanza akiwa jirani na moto na wazazi wake walikuwa shambani
Lauriano Komba mkazi wa kijiji cha Mtua anasema wagonjwa wa kifafa 33 hadi sasa wanadaiwa wameungua na moto baada ya kuanguka kifafa wakiwa peke yao na kusisitiza kuwa kifafa kilichopo katika kijiji hicho ni cha ajabu kwa kuwa katika vijiji vingine idadi ya wagonjwa hawazidi wane ambapo katika kijiji hicho karibu kila nyumba kuna mgonjwa.
Wakizungumza kwa niaba ya wenzao Maria Komba, Juliana Hyera na Flora Nchimbi walisema wanashinda kwenda shambani kutokana na muda mwingi kuutumia kuwaangalia watoto wao wanaugua kifafa kuhofia kuangukia kwenye moto au maji endapo ugonjwa huo unawaanza bila kuwa na mwangalizi.
Takwimu za ugonjwa wa kifafa katika mkoa wa Ruvuma zinaonesha kuwa katika kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba 2009 kulikuwa na wagonjwa 1072 kati yao wanaume 639 na wanawake 433 ambapo wilaya ya Mbinga inaongoza kwa wagonjwa 337,Songea manispaa 309,Songea vijijini 217,Namtumbo 62 na Tunduru 147 takwimu hizi ni wale walioripoti kwenye vituo vya afya.
Baadhi ya wanawake katika kijiji cha Mtua baada ya kutoa maoni yao kuhusu tatizo ka kifafa linavyowaandama.
Mratibu wa magonjwa ya akili na kifafa mkoa wa Ruvuma Talumba Gullum anasema wagonjwa wengi wa kifafa hawajitokezi kwenye vituo vya afya na hasa waliopo vijijini ambao kutokana na kukosa elimu sahihi dhidi ya ugonjwa huo wanaamini ugonjwa huo ni ushirikina na wa aibu hali inayowafanya wagonjwa kuwaficha majumbani na tatizo kuongezeka.
Kulingana na watalaamu wa afya kifafa (Epilepsy) kinatokea kunapokuwa na mapungufu katika seli za ubongo na kwamba kunapokuwa na hitilafu katika huu mfumo kifafa kinaweza kutokea ambacho dalili zake ni kuona maluwe luwe (aura), kiasha kupoteza fahamu, kuanguka na kutupa miguu na/au mikono, kukaza mdomo, kutoa povu na wakati mwingine na kutoa haja ndogo au kubwa.Hata hivyo watalamu wa ugonjwa huo wanasisitiza kuwa kifafa sio ugonjwa wa kuambukiza, mara nyingi unakuwa kwenye familia kwa kurithi toka kwa mzazi au wazazi, na kwamba wakati mwingine inaweza tokea baada ya kuumia ubongo kutokana na ajali, kiharusi (stroke), kuumia wakati wa kuzaliwa (birth injuries) na kwamba Kifafa cha aina hiyo ni tofauti na ‘dege dege’ kwa watoto au kifafa cha mimba (Eclampsia).
Kulingana na wataalamu kifafa hakitibiki na mgonjwa kupona kabisa bali kuna dawa za kupunguza au kuzuia kifafa kutokea mara kwa mara na kwamba dawa hizo zinapatikana katika vituo vya afya na hospitali ambapo mgonjwa atakunywa kwa maisha yake yote ambapo dozi inategemea na hali ya mgonjwa anapoonwa mara kwa mara kwenye kliniki zao maalum.
3 comments:
Poleni sana ndugu zetu na msishau kuwa maumivu ni yetu sote!!
nanukuu"Kulingana na wataalamu kifafa hakitibiki na mgonjwa kupona kabisa bali kuna dawa za kupunguza au kuzuia kifafa kutokea mara kwa mara na kwamba dawa hizo zinapatikana katika vituo vya afya na hospitali ambapo mgonjwa atakunywa kwa maisha yake yote ambapo dozi inategemea na hali ya mgonjwa anapoonwa mara kwa mara kwenye kliniki zao maalum."mwisho wa kunukuu:- Ni hivi mimi binafsi nina ndugu ambaye alipata kifafa miaka ya tisini. Akapelekwa kwa mganga wa kienyeji kwanza lakini haikusaidia kitu ndo kwanza homa ilizidi. Na baadaye ushauri ukatolewa kuwa waanze na dawa za hospitali wakaanza matibabu hospitali ya Peramiho na mara akaandikiwa dawa amezitumia zile dawa na amepona kabisa na anaendelea na maisha yake kama kawaida. Nimeshtuka tu hapo juu kwamba haponi mtu atakunywa hizo dawa maisha yote. Nitafanya utafiti zaidi kwa kweli kwani inasikitisha sana kusikia kijiji kizima kinapata homa hii. Ahsante mwandishi kwa habari hii.
Mimi mwenyewe ninae mtoto wangu yalimuanza, akiwa na miaka mitatu .Nanipo Canada nimeagizishia dawa Tanzania , za mitishamba .Mungu amenisaidia . nampaka sasa hivi mtoto wangu amepona anamiaka kumi na tatu
Post a Comment