Monday, October 3, 2011

TUIANZE JUMATATU HII YA KWANZA YA MWEZI NA HADITHI:- JINSI SUNGURA ALIVYOPATA MAJI


Hapa zamani za kale, kulikuwa na shida Kubwa sana ya maji katika nchi zote. Kwa bahati, likabakia ziwa moja tu. Wanyama wengi wa kila aina walipata maji yao kwenye ziwa hilo. Wanyama wakubwa kama vile Tembo, Simba na Chui; waliwanyanyasa sana wanyama wadogo waliofika kunywa maji kwenye ziwa hilo. Wakawa Hawana raha. Walipata maji kwa shida sana baada ya manyanyaso makali.

Sungura alipoona hivyo, alianza kukuna kichwa akifikiri jinsi ya kuepukana na adha hiyo. Akapata njia. Alitengeneza ngoma na kucheza kwa siri nyumbani kwake. Wanyama wengine waliposikia sauti ya ngoma ile ilivyosikika vizuri, wakavutika nayo. Wa kwanza kuvutika, walikuwa wanyama wakubwa. Wakamwendea Sungura ili wapate kuiona ile ngoma inayotoa sauti nzuri. Sungura akawaambia: “Mimi napiga ngoma hiyo na kucheza pake yangu kwa siri. Ninyi mkitaka kuiona, naomba mje moja moja, nami nitawaonyesha.” Hiyo ilikuwa mbinu yake tu kutaka kujua nani atakuwa wa kwanza na wa mwisho kuja kwake ili apate kuwatenda vibaya.


Tembo alikuwa wa kwanza kwenda kwa Sungura. Akamwambia: “Ingia nyumbani mwangu”. Tambo bila kukawia akaingia ndani. Loo, maskini Tembo! Sungura akafunga mango kwa Nguvu, mara akachoma nyumba yote. Tembo akafa.

Akaja Chui, bila kufahamu kilichotekea kwa Tembo. Yeye akapelekwa kwenye mlima wa mawe wenye mtelemko mkali. Sungura akamwambia: “Hapa wanapatikana wanyama wengi sana. Unisaidie kuwinda ili upate kula karamu kabla ya kucheza ngoma. Wanyama wanapatikana kwa urahisi sana ukifuata taratibu nitakayokuelekeza. Nayo ni hii: Ufumbe macho mpaka mnyama anapoanza kukupita. Kisha, ufumbue macho na umfuate kwa nyuma. Ndipo utakapofaulu kumkamata”.

Chui akakubali. Sungura akapanda mlimani kuporomosha jiwe kubwa. Likaja moja kwa moja kutoka juu na kumponda Chui aliyefumba macho kungoja mnyama. Sungura akamchukua Chui na kumchuna ngozi. Zamu ya Simba ilifika, akamwmbia: “Ngoma hii kila atazamaye, lazima achunwe ngozi kama walivyofanya wenzako. Tazama, ngozi hii ni ya nani? Si ya Chui?” Simba akakubali. Akachunwa kwa tamaa ya kutazama ngoma, akafa. Sungura Akava ngozi hizo kwa zamu ili kwenda ziwani kuwatishia wanyama wadogo. Sungura akatawala maji yale, wakati Wote wa shida, kutokana na werevu wake.

Fundisho
Hadithi hii inawahusu wanyama. Kadiri ya maelezo, unaweza kufikiri kuwa wanyama waliouawa hawakuwa na akili. Hiyo ni hadithi. Na kila hadithi inalo jambo la kujifunza. Kwa mfano:-

Sentensi ya mwisho ya hadithi: “Sungura akatawala maji yale, wakati wote wa shida, kutokana na warevu wake. Werevu wa sungura ulikuwa kuwahujumu wenzake. Hujuma sio kitu kizuri maishani. Ni dhambi. Sisi tusiwe werevu wa kuwahujumu na kuwaonea wenzetu. Mamoja wakiwa wakubwa au wadogo.Katika jambo hilo, Yesu anasema: “Kila kitu mlichomte-ndea mmojawapo wa hawa ndugu zangu wadogo, mlinitendea mimi” (Mt.26:40)
Werevu wetu uwe katika kuwapenda wenzetu na kuwatendea mema.

Hadithi hii imeandikwa na Kat.V:A Ndunguru . Mimi katika pitapita zangu nilikuwa hapa Peramiho basi nikawa nimenunua mkate na nikafungiwa gazeti na baada ya mkate kwisha nikawa naangalia gazeti au kipande cha gazeti na kukutana na hadithi hii nikawasoma wanangu na nimeona niiweka hapa Nayni msome na mcheke kama sisi. Na gazeti lenyewe linaitwa MLEZI.

Halafu hadihi hii imenikumbusha nilipokuwa darasa la kwanza na pili tulikuwa tukiimba sana nyimbo na moja ya nyimbo ni kama hii. Sungura Sungura mjanja wee X2 Ingawa mdogo hushinda wakubwa X2 Akili akili zatoka wapiX2 Ingawa mdogo hushinda wakubwa……

9 comments:

sam mbogo said...

Da Yasinta,kwa wale tulio soma sikunyingi,kulikuwa na kitabu fulani,cha kiswahili ndani yake kulikuwa na hadithi tamu sana ya sungura.'SIZITAKI MBICHI HIZI' nafikiri ndivyo hadithi hiyo iliitwa.mara nyingine tuliiba hadithi hiyo hivi.-hadithi inayokuja niya sungura sikia,alitoka sikumoja njaa aliposikia njaa alipo sikia sungura nakuambia.......sijuwi nininanini pale!!? kama una kumbuka ama mtuyeyote ana kumbuka waweza malizia. hakika sungura ni mjanja.kaka S.

Yasinta Ngonyani said...

hiyo naikukbuka ngoja nitaiweka hapa siku yake ili ifurahi kaka S:-) na wengine pia..duh umenikumbusha

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

SAWA

Anonymous said...

asante dada yasinta kweli hata mimi nilikuwa mpenzi wa kusoma hadithi za sungura lakini kwa sasa sisikumbuki sana majina yake kweli sungura ametumika sana ktk hadithi za ujanja sana napenda sana hadithi zake dada yasinta kama utaweza utuwekee hadithi nyingi za sungura inafurahisha sana

Penina Simon said...

Yasinta umenikumbusha mbali sana, HV hzo hadithi kweli sku hzi zinaendelea kutungwa au ndo zile zile za zamani? Nina wasi wasi zinaweza kupotea, Nakumbuka hata zamani ukienda kwa bibi kumsalimia usiku hamlali anakusimulia hadithi tamu mpakaa, lkn siku hzi sidhani kama hiyo ipo kweli?.na huko vijijini tulikuwa tunangangania kulala kwa bibi na kumsaidia vikazi vidogo vidogo ili afurahi usiku uhadithiwe hadithi

Anonymous said...

sijakumbuka kitu kuhusu hadithi hiyo.

ray njau said...

HADITHI HII INANIKUMBUSHA KANUNI YA KIDHAHABU KATIKA BIBLIA:-
------------------------------------- “Kwa hiyo, mambo yote mnayotaka watu wawatendee ninyi, lazima mwatendee wao pia vivyo hivyo; hii, kwa kweli, ndiyo maana ya Sheria na Manabii._Mathayo 7:12

Anonymous said...

Mimi ni munyarwanda na najifunza kiswahili shuleni lakini nataka niwambieni kwamba hadithi hizi zinanisaidia kuPROGRESS

Alain Dumu said...

duduu yani hadithi tamu mno,,,nimeipenda iasee