Thursday, September 1, 2011

Baada ya miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika​, je Tanzania inakuhitaj​i?

Mwaka 2011, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasherehekea miaka ya uhuru wa serikali ya Tanganyika, taifa lililomezwa April 26, 1964 baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Kwa hesabu za haraka haraka utaona miaka hamsini ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaadhimishwa April 26, 2014. Muungano wa Tanganyika na Zanzibar una faida na kasoro zake, lakini leo nitajadili mada inayouliza kuwa “baada ya miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika, je Tanzania inakuhitaji?”.

Magwiji na wataalamu wa falsafa ya imani duniani, wanatuaminisha kuwa hakuna nguvu inayozidi upendo, wakidadavua zaidi husema kuwa penye upendo uliopea Mungu yupo. Hata ukitafakari maisha ya mahusiano tunayoishi, huna budi kumpenda mtu kwanza kabla hujaenda mbele zaidi kumpa nafasi ya kuwa mwenzi wako wa ndoa, katika muktadha huo ni kawaida kumwona kijana mwanamke akitoka bara la Amerika kufunga ndoa na kijana mume toka Mwanza, vivyo hivyo haishangazi kuona vijana wakivuka bahari na mito, milima na mabonde kutoka bara moja kwenda bara jingine kutafuta mapenzi yanayojengwa na upendo.

Hakika upendo ni nadharia ambayo hakuna maelezo yanayotosha kuidadavua kwa kilele chake. Bila shaka yoyote upendo miongoni mwa Watanganyika na Wazanzibar ndio uliozaa taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa mtazamo wangu, upendo ule uliozaa muungano hapa Tanzania miaka 47 iliyopita, naona umepoa kama sio kufifia na kuchuja. Makala hii haitojadili nani amefifisha upendo huu hapa Tanzania.

Nakumbuka siku ile, taifa lilipotangaziwa kuhusu afya ya baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, kuwa hali yake sio nzuri, Watanzania tuendelee kumuombea, mwili ulinisisimka kwa hofu. Nikapata baridi na hofu kuu, maswali mengi yalinikaba hasa nikijiuliza, itakuwaje nchi yangu bila “a great man, father of the nation?”. Hakika Mwalimu Nyerere alikuwa “great man”. Hata viongozi waliomzunguka wao pia walikuwa “great people”. Watanganyika hawa “great people” kizazi chao shurti kiwe “great generation”.

Wahenga walipata kusema kuwa “macho ni dirisha la fikra na ujasiri alionao mtu”, ukweli huu nauona kila ninapowatazama machoni Watanganyika nami nawaona kuwa na “great people”. Ujasiri huu tulionao hausemwi sana siku hizi, hivyo ipo haja ya kufanya kampeni ya makusudi miongoni mwa vijana wa Kitanganyika, hivyo upatapo fursa ya kushikana mkono na rafiki yako, vema ukamtazama machoni kwa walau dakika moja, kisha umwambie “you are a great person” kwa vile kila Mtanganyika ni kizazi cha “great people” ambacho ndio kiliasisi taifa la Tanganyika linalotimiza miaka 50 ya Uhuru tarehe 9 Desemba mwaka 2011.

“Great people” wale wakiongozwa na “great man” Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere walifanikisha kujenga misingi ya Taifa la Tanganyika na kufanikisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964, kwa vile upendo baina yao ulipea, vivyo hivyo waliipenda nchi yao na watu wake. Ukweli ni kuwa Watanganyika ni "great people", japo utamaduni wa kuambiana ukweli huu haupo tena nchini Mwetu. Nasisitiza kuwa Watanganyika ni kizazi cha “great people” kwa vile Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliweza kuwakaripia viongozi wa mataifa yenye nguvu za uchumi kama Amerika na Uingereza haya Israel pale alipoona matendo ya mataifa hayo yanaathiri kwa makusudi ustawi wa nchi zenye uchumi mdogo, kwa Mwalimu, kigezo cha ubinadamu hakikuwa uchumi bali ubinadamu wenyewe.

Mwalimu Nyerere hakuishia kukemea mataifa makubwa pekee, bali alikemea pia viongozi wa ndani ya Tanganyika ambao nia zao binafsi zilikuwa zinakinzana na maendeleo ya nchi yetu. Mwalimu hakusita kuanika udhaifu, uchafu na tamaa za viongozi hao na akasisitiza kuwa watu hawa wasipewe uongozi kwa hawana nia thabiti ya kuweza ustawi wa jamii ya Mtanganyika. Bila shaka yoyote, msimamo huu wa Baba wa Taifa ndio ulikuwa msimamo wa serikali yake yote, ndio ulikuwa msimamo wa viongozi wengine wote, Mwalimu Nyerere amekuwa “father figure” kwa viongozi wengi wa Tanganyika kwa kuwa na maneno machache na matendo mengi, nakumbuka tulipata kuwa na wimbo wa kusifia matendo ya Baba wa Taifa kuwa “Raisi wetu hapendi kusema, raisi wetu Nyerere baba, anaonesha mfano kwa vitendo”.

Mwalimu Nyerere alikuwa na shamba lake kule Butiama, shamba la Mwalimu lilikuwa mfano kwa wanakijiji wenzake, ukubwa wa shamba hili la Mwalimu haukuwa nusu ya ardhi ya kijiji, bali alichukua sehemu kidogo ili kila mwanakijiji mwenye nia ya kufanya kilimo naye apate ardhi. Hapa utaona fahari ya Mwalimu Nyerere haikuwa kujilimbikizia mali, ndio maana uwepo wa Tanzania ulimhitaji sana Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Swali linabakia, je baadhi ya viongozi tulionao ambao kujilimbikizia ardhi na mali kwa njia za ufisadi na kuuza mali asili zetu, Tanzania inawahitaji?

Kwa vile utamaduni wa kuambiana kuwa “sisi ni great people”, imekuwa kawaida kuona Watanganyika wa leo tunaishi kama pimajoto -thermometer- ambayo inabadilisha kizio cha joto kadiri unavyoiweka kwenye nyuzi joto tofauti. Ni kawaida kwa pimajoto kusoma nyuzi joto za juu ukiiweka kwenye mazingira yenye joto la juu, pia ni kawaida sana ikiwa pimajoto itatolewa kwenye mazingira ya nyuzi joto la juu na kuwekwa kwenye barafu itasoma nyuzi joto sifuri ama chini ya sifuri. Mfano huu unamaanisha kuwa Pimajoto inaathiriwa na mazingira, hali inayotokea sana kwa Watanganyika wa leo bila kujali elimu zetu, vipato vyetu ama namna yoyote ya uelewa uliokolea, tumekuwa tunaathiriwa sana na mabadiliko ya agenda ama mazingira, kwa mfano bei za bidhaa zinapopandishwa kiholela tunalalamika lakini hatuchukui hatua kukemea na kukomesha hali hiyo, zaidi tumekuwa ni walalamikaji tuliojaa woga wa kuuliza kwa nini hali ipo hivi, nashangaa sana tumekuwa sio “great generation” tuliozaliwa na “great people” chini ya uongozi wa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ambaye agenda yake ilikuwa kukemea uoza huu.

Mwalimu Nyerere na Waasisi wa Taifa letu hawakuishi kama Pimajoto, fikra zao hazikubadilishwa na mazingira kama ilivyo Pimajoto bali wao ndio walipambana kubadilisha mazingira magumu waliyokuwa nayo wakati huo hawakukubali chochote kilichodhalilisha utu wao, kilichobeza ubinadamu wao ama kilichodidimiza ustawi wa Tanganyika ama Watanganyika. Kwa kutunza heshima na utu wa Mtanganyika walisisitiza sana elimu ya ujamaa na kujitegemea. Ukitazama wengi wa viongozi tulionao Tanganyika ya leo wengi wanaishi maisha ya Pimajoto, wanabadilika badilika ili kufanikisha nia zao binafsi zinazokinzana na mahitaji ya mustakabali wa Taifa letu Tanganyika, baada ya miaka 50 ya uhuru wa Tanganyija, Watanganyika tunaoishi maisha ya Pimajoto, Tanzania inatuhitaji?

Miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika imeshuhudia awamu nne za maraisi wa Tanganyika, huku awamu ya kwanza ikiongozwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, awamu ya pili Mzee Ali Hassan Mwinyi, awamu ya tatu iliongozwa na Mzee Benjamini Mkapa na awamu hii ya nne usukani umeshika na Raisi Jakaya Kikwete. Katika awamu zote nne, serikali imepambana na changamoto mbali mbali za maendeleo, pia imetumia fursa nyingi za maendeleo ili kuwezesha maendeleo ya kiuchumi, kisisasa na ustawi wa jamii. Yatokanayo na jitihada hizi na changamoto zake sio muktadha wa makala hii.

Kwa makala hii, miongoni mwa maswali ya kujiuliza ni:- je serikali ikiwa ni mzazi wa kila Mtanganyika, inawapokea Watanganyika na matatizo yao na kuwaongoza kutatua shida zao? Kwa maana jitihada zilizofanywa na awamu zote, miaka 50 baada ya uhuru wa Tanganyika zimefanikiwa kiasi gani kutatua matatizo yanayokabili ustawi wa jamii ya Mtanganyika? Je, miaka 50 inatosha tu inaalika sherehe na karamu ya kujivunia uhuru ama ni fursa kwetu kutafakari wapi tulipojikwaa kama Taifa badala ya kulalamikia wapi tulipoangukia? Maana miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika haijatosha kutatua shida za msingi kama uhaba wa madawati mashuleni, uhaba wa madawa, vitendanishi tiba na watumishi hospitalini, kukosekana kwa nishati ya umeme ya uhakika na mambo mengine mengi.

Kwa bahati mbaya sana miaka 50 baada ya uhuru wa Tanganyika , taifa letu linashuhudia matumishi ya ujuzi na utaalamu wa baadhi ya viongozi wenye tamaa, ulafi na ubinafsi vikitumika kuzidisha umaskini miongoni mwa jamii kubwa ya Watanzania, je, Tanzania itakapofikisha miaka 50, hapo tarehe 26 April 2014 itakuwa bado inahitaji viongozi wa namna hii?

Nihitimishe kwa kusema kuwa, kila tunapotazama tulipotoka, hasa baada ya miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika, vema tukijua kuwa sisi Watanganyika ni “great people” mambo yaliyofanywa na waasisi wa Taifa letu ni mfano hai wa hiki ninachosema. Changamoto tuliyonayo leo hii ni kuishi maisha ya Pimajoto, ambayo ni kinyume na silika ya “great people” maana “great people” wote huwa wanabadilisha mazingara yao na kuyafanya kuwa bora zaidi kwa ustawi wa taifa lao na vizazi vijavyo. Serikali haina budi kusimamia sheria zake ili wajanja wachache wasitumie maarifa waliyoyapata kuihujumu serikali, badala yake wataalamu hawa watumike kusaidia kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya Taifa, tukifuata njia hii ndiposa tutajibu hoja ya Miaka 50 baada ya uhuru wa Tanganyika, je Tanzania inanitaji?
Imeandikwa na,
Barnabas Mbogo.
Nyamagana, Mwanza
.

1 comment:

Beda Msimbe said...

Nilipenda kuunga mkono mawazo ya mwandishi wa makala hasa hitimisho
lake ambalo mimi nililipenda sana. Kuna ukweli usipingika tupo great
klwa sababu watu walioanzisha taifa hili walikuwa great, walifikiria
njia ya kwenda na sina uhakika kama sasa hivi tunafikiria njia ya
kwenda zaidi ya kupiga maktaimu katika matope yasiyoeleweka.Swali la
serikali kama inafanya kinachotakiwa kufanya kama baba. maswali mengi
majibu machache maswali laini majibumagumu.
Mungu atubariki sote
Lukwangule