Sunday, September 11, 2011
Taifa Msibani, Umoja wetu na Utu wetu shakani - Zitto
Ndugu zangu salaam kwenu,naomba mnifikishie ujumbe huu kwa watanzania. Natanguliza shukrani zangu za dhati.
(Nimeandika makala hii nikiwa katika Benchi la Hospitali ya Mnazi Mmoja hapa Zanzibar. Mniwie radhi kama kuna spelling mistakes kwani nilitaka hisia zangu ziwe as raw as possible - Zitto Zitto and not Zitto a Politician).
Jana asubuhi tarehe 10 Septemba 2011 Taifa liligubikwa na habari za kushtusha za maafa. Mwanzoni taarifa zilisambaa kwamba zaidi ya watu 2000 walikuwa kwenye Boti MV Spice Islander lililopinduka na kuzama mbele kidogo ya Nungwi likielekea kisiwani Pemba. Habari hazikuwa za uhakika sana kwani vyombo vyetu vya habari na hasa Televeshini ya Taifa havikuwa vikitoa habari juu ya ajali hii.
Habari zilisambaa kupitia mitandao ya intaneti na kufuatia uchu wa habari nilianzisha #ZanzibarBoatAccident katika mtandao wa twitter ili tuweze kufuatilia kwa karibu habari zote za ajali hii.
Habari zilisambaa kuwa Televisheni ya Taifa ilikuwa inaonyesha muziki wa Taarab na Baadaye vipindi vingine vya kawaida bila kutoa habari kwa Umma kuhusu msiba huu.
Watanzania waliokoa wakiwasiliana kupitia twitter na facebook walikuwa na hasira sana na kituo cha TBC1 kutoonyesha au kupasha habari juu ya ajali hii. Mpaka saa moja jioni kituo hiki cha Televisheni ya Taifa kilikuwa kinaonyesha watu wakicheza muziki wa Kongo, wanawake wakikatika viuno na hata ngoma za asili.
'Hallo, washa TBC1 uone Televisheni yenu inachoonyesha' yalikuwa ni maneno ya Mwakilishi Ismael Jussa Ladhu aliponipigia kuonyesha kusikitishwa kwake na kituo hiki. Mpaka jioni tulikuwa tumepata taarifa kuwa Watanzania wenzetu 198 walikuwa wamepoteza maisha. 570 hivi walikuwa wameokolewa.
Binafsi nilipotembelea Hospitali ya Mnazi Mmoja niliweza kumwona Binti aliyeitwa Leyla, akisoma darasa la Nne huko kisiwani Pemba. Leyla alipona, aliokolewa. Nilimwambia leyla atapona na kurudi Shuleni. Mpaka ninapoandika tumeambiwa kuwa Watanzania 240 wamegundulika kupoteza maisha na zaidi ya 600 wameokolewa.
Napenda kuwapongeza sana waokoaji wetu, wavuvi wa kijiji cha Nungwi na vijiji jirani, wamiliki wa mahoteli waliojitolea vifaa vyao kwenda kuokoa watu na wanajeshi wetu wa majeshi ya ulinzi na usalama kwa kazi hii kubwa ya kuokoa. Kwa kweli tumeokoa watu wengi kuliko ilivyotarajiwa. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imejitahidi sana, ilitulia na kuonyesha uongozi dhabiti katika juhudi za uokoaji.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akafuta ziara yake huko Canada, ziara iliyokuwa imeandaliwa muda mrefu na kwa gharama. Lakini Rais aliona ni vema kupata hasara kuliko kuwa nje ya Nchi kipindi hiki. Hakutaka hata kumtuma Makamu wa Rais au Waziri Mkuu. Alifuta. Akatangaza siku 3 za kuomboleza.
Hata hivyo waandaaji wa Miss Tanzania waliona hasara kubwa kuahirisha shindano la Urembo usiku huo. Wangepata hasara! Hata wafadhili wao Kampuni ya simu za mkononi ya vodacom ambao miongoni mwa waliofariki wamo wateja wa vodacom, waliendelea na shindano hili. Jumatatu, tarehe 12 Septemba 2011 ni siku ya khitma ya kuwaombea marehemu wetu.
Nimeamua kutotumia simu ya ngu ya Voda kwa siku nzima, sina njia ya kuiadhibu Kampuni hii isipokuwa kugoma kutumia simu yao japo kwa siku moja kuonyesha kutoridhishwa kwangu na uamuzi wao wa kutojali msiba huu kwa Taifa.
Misiba huweka jamii pamoja. Msiba huu uliotokea Zanzibar ni jaribio kubwa kwa Umoja wa Taifa letu. Shirika la Utangazaji la Taifa limeshindwa jaribio hili la kudhihirisha Umoja wetu katika kipindi hiki. Nataraji wakubwa wa Shirika hili linaloendeshwa kwa kodi watawajibika au kuwajibishwa!
Jumla ya Majeruhi na marehemu sasa inafikia zaidi ya Abiria 800! Asubuhi ya jana 10 Septemba 2011 tuliambiwa na Serikali kwamba uwezo wa Boti la MV Spice Islander ilikuwa ni abiria 500 na wafanyakazi 12. Pia tumejulishwa kuwa boti hili lilikuwa la Mizigo na sio la Abiria.
Natumai mara baada ya kumaliza maombolezo haya ya siku tatu Wakuu wa Mamlaka zinazohusika na usafiri wa Majini wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar watawajibika au kuwajibishwa. Mkuu wa Bandari ya Zanzibar Mustafa Aboud Jumbe na Waziri wa Miundombinu Hamad Masoud wanapaswa kufukuzwa kazi mara moja kama hawatawajibika wenyewe kwa kujiuzulu.
Kufukuzwa kwao kazi hakutarudisha ndugu zetu duniani bali itakuwa ni somo kuwa hatutarudia tena kufanya makosa yaliyoleteleza ajali kama hii.
Mwenyezimungu atupe subira wakati huu wa msiba mkubwa katika Taifa letu. Alaze roho za marehemu wetu mahala pema peponi na awape unafuu wa haraka majeruhi wetu.
Zitto Kabwe.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
7 comments:
watanzania hatuna tabiya za ajabu au kinyama kitendo walichokifanya vodacom ni chakihuni na uchochezi kwa taifa wanaweza kuwagawa watanzania
Taifa likiwa na majonzi na simanzi kwa kupoteza watu 297 wengi wakiwa wanawake na watoto na vijana waliokuwa wakirudi likizo hii inashangaza sana vodacom kufanya ujinga ushenzi unyama kwa watanzania mimi nimeamua kukatiya huduma zao na kila
Masikitiko ... yaelekea hatujifunzi ... MV Bukoba ilitupa somo gani? Kupoteza watu wengi kiasi hicho ni uchungu mkubwa si kwa wanandugu tu bali kwa Taifa zima. Pengine wakati umefika tusimame kama taifa moja na kutafuta kuleta umoja, kupigana dhidi ya umaskini, kudhibiti yale yanayotutesa na kutunyanyasa ... hatuna budi kuyapiga kumbo.
Hakuna shida kama wameamua hivyo basi sis tuwaombee kwa mungu hiyo ni Biashara.
Gudluck usiwe mjinga kupita kiasi hiyo biashara yao ndio washerekee kufa kwetu,tumeamua wanzanzibar hatutumii tena vodacom abadaa na hatuna iman tena na TBC na huu ndio utakua mwanzo wetu kabisa kupigana vita na makampuni,vitengo na wajinga na wapuuzi kma wewe Gudluck eti tuwaombee dua ile biashara pumbavu mkubwa wewe
Yaani hao kina Goodluck wako wengi, mimi nilipita kwenye blogu ya Mzee mmoja hivi mtu mzima na akili zake ndugu yake Yasinta wa kutoka Peramiho, nikamwambia, kama taifa tuko kwenye maombelezo, umeshindwa kuweka hata mstari mmoja tu wa rambi rambi? Badala yake umekazana na picha za CCM kuwahonga wali wana Igunga. Alichonijibu kuwa blogu ni yake na ana haki na mamlaka ya kuweka akitakacho. Na hata hao walioathirika na hilo janga hawawezi kwenda kusoma kwenye hiyo blogu yake. Pengine huo ndio mtazamo na msimamo wa Vodacom kuwa hao waliokufa na waliotharika hawawezi kuwapa faida yoyote si washakufa watanunua vocha tena kwao? Lakini wamesahau kuwa wako waliopona na hata hao ndugu zao wapo ambao ama wangekuwa wateja wa Vodacom au wangeingia kwenye globu zao na kuongeza traffic. Na huyo bloger anaitwa Profesa Mbele!
Ngoja nione kama Yasinta atatoa hii au ataibania, lakini kiukweli umoja wetu uko mashakani leo hii yakitokea maafa Songea na sisi tukae pembeni tuwaachieni wenyewe?
mara Pumbavu, nyoko fala hayo matusi yote zilipendwa hakuna jipya. Naomba matusi mengine kwani hayo hayatoshi!!!!
maoni: depend on yourself and never beg.
Post a Comment