Monday, September 5, 2011

NANGOJA ANIUE, NIKIONDOKA WANANGU WATATESEKA!

Kama mnavyojua kuwa hivi karibuni nilikuwa huko nyumbani Tanzania, na nilikuwa pande za huko kwetu Ruhuwiko Songea ambapo nilikaa majuma kadhaa hivi.

Kusema kweli yapo mengi ya kushangaza, ya kutisha na yenye kufurahisha ambayo niliyashuhudia, na kusema kweli kuna mengi nimejifunza.Lakini labda niseme tu kwamba aina ya maisha niliyoyakuta huko kijijini, kwa kweli yalinipa picha kwamba bado kuna safari ndefu sana katika kuufikia ukombozi wa huyu kiumbe mwanamke.

Ninayo mifano mingi lakini tukio nililolishuhudia siku moja nikiwa katika matembezi yangu liliniacha mdomo wazi, na labda niseme kwamba limenikaa hadi leo akilini nikijaribu kuwaza na kuwazua lakini sipati jibu.

Sijui nianze vipi?...Ahh! Kuna siku katika matembezi yangu nikakutana na kundi la akina mama wamekaa wakipiga gumzo, lakini nyuso zao zilikuwa zimegubikwa na huzuni. Nilishikwa na tashwishwi, nikajongea pale walipo ili kujua kama kuna jambo gani limetokea kiasi cha kuwakusanya pale huku wakiwa na nyuso za huzuni.

Si mnanijua tena mie KAPULYA MDADISI. Nikawauliza, ‘jamanindugu zanguni, kulikoni mmekaa na nyuso za huzuni, JE KUNA MSIBA?’
Wote waligeuka kuniangalia, lakini walionekana kusita kunijibu, na ndipo mmoja wao akaniambia kuwa usiku wa jana kulitokea kutoelewana kwa wanandoa wanaoishi hapo mtaani kiasi cha mume kumpiga mkewe mpaka akapoteza fahamu.

Niliuliza sababu ya ugomvi wao, na ndipo nilipoelezwa kwamba, sababu kubwa ni kwamba wanandoa hao wana watoto wanne ambao bado ni wadogo na mume anataka kuongeza mtoto wa tano, lakini mkewe hataki kwa kuwa hali ya uchumi hairuhusu, na pia bado wanalo jukumu la kuwalea hawa watoto wanne ambao kwa kweli ni wadogo. Hata hivyo alimshauri mumewe wavute subira kwanza ili watoto hao wakue.

Mume hakukubali ushuri wa mkewe na ndipo ugomvi ulipoanza.Walibainisha kwamba ugomvi wao ni wa mara kwa mara na sababu kubwa ni hiyo ila ugomvi wa safari hii ulikuwa ni mkubwa na kama sio majirani kuingilia kati basi mume yule angemuua mkewe.

Nikataka kujua kama anapata kipigo cha aina hii kila mara kwa nini aisrudi kwao?
Wakanijibu kuwa, kwanza hana nauli ya kurudi kwao kwani si mtu wa Songea. Pili anaogopa watoto wake watateseka.

Mh! Nilishusha pumzi, ujinga gani huu. Hivi sisi wanawake ni nani ameturoga, yaani unakubali mtu anakutesa na kukunyanyasa kiasi chakutaka kukutoa roho lakini wewe umo tu! Ukiulizwa sababu unadai, eti watoto wangu watateseka!

Bado najiuliza hivi watoto wanne bado hawatoshi? Hili tukio kwa kweli nimekuwa nikijiuliza tangu nirudi huku Sweden, na mpaka leo sijapatajibu kwamba tatizo ni nini? Kutokuelewa haki zetu, ujinga au ni nini?

7 comments:

sam mbogo said...

Napika ,nitarudi baadaye.
kaka S.

o'Wambura Ng'wanambiti! said...

duh!

sam mbogo said...

Haya,Da Yasinta,mapishi yashaiva,japo kwa muda mdogotu,ishaanza ikuungua.kurudi kwenye mada yako.si kweli kama wana wake mmerogwa,hapana. Tatizo, fikrazilizowazunguka wanawake wa vijijini,nabaadhi ya wanawake wa mjini.mazingira yaliyo wazunguka wanawake wa kijijini,ni magumu na yakuwaonea huruma. pia mitazamo juu ya mstakabali mzima wa maisha ya huko waliko. kitu muhimu hapa kubadilisha hali hii, elimu,ya darasani,na pia elimu ya uraia.wewe usinge enda shule,usingekuwa na ufahamu kama huu ulionao sasa.labda kwa nafasi yako unaweza kuwasaidia,kutambua hakizao,ili wawe na uwezo wa kujiamini,kuwa mwanamke ana mchango wake mkubwa katika jamii.kaka s

Goodman Manyanya Phiri said...

Suala hili kulijibu lataka vipengele vingi sana

Je, serikali inamipango gani ya ustawi wa jamii huko vijijini?

Je, haki za wanawake wa vijijini vimehifadhiwa kivipi katika mali yao kama wanandoa? Nyumba ni ya nani? Watoto ni wanani? Wakitalakiana nani anapata nini?


Elimu, kama anavyosema Sam Mbogo, ni ya kiasi gani kwa Mtanzania ki uwastani?


Wanaume majirani (nao pia, wanawake) wanaendesha desturi gani kumwachia jambazi kila mara ampige dada yao....


.... KWANINI SIKU MOJA WASIMVAMIE NAO MPUMBAVU HUYU ILI NAYE WAMPIGE KIASI CHA KUPOTEZA FAHAMU NA AKOME?

sam mbogo said...

Ndugu yangu,Goodman,sheria zipo,zinazo simamiwa na serikali,ugumu unakuja katika kuzitekeleza sheria hizo.mara nyingi huwanufaisha watu waishio mijini.mfano mijini ukimpiga mkeo polisi yaweza kukushughulikia nk. hebu turudi kwenye mada,huyumwanamke anatakiwa kukombolewa kutoka mikono hii ya huyu baba mwanamasumbwi.katika dunia tunayo ishi ,kuna njia mbalimbali za kutoa elimu kupitia sanaa za maonesho.(Theatre for development/community Theatre.sanaa hii nanyinginezo,za weza kufikisha ujumbe huu wa manyanyaso ya wanawake vijijini na nchi nzima kwa ujumla.wapo,na vipo vikundi na wana harakati wengi tu Nyumani Tanzania wanaweza kufanya uhamasishaji huu,wakiwezeshwa.serikali,kama serikari ina suwasuwa sana katika jambo hili,ila kwa NGO,zina nafasi kubwa ya kufanya mabadiliko haya.kaka S

Yasinta Ngonyani said...

Kaka S.! Usiwe na shaka sie twakusubiri!

Chacha! Mbona ume-duh! sana?

Naona kaka S umerudi! Ulichosema ni kweli kwamba inawezekana ni tatizo la kuto kwenda shule...Lakini hapa sasa ni nani anatakiwa kwenda shule? Maana inavyoonekana kwa hapa kama mwanamke anajua kuwa wakiwa na watoto wengi hawataweza kuwalea ipasavyo... Haki zake anajua ila sasa huruma yake ya kwamba watoto watabaki upweke....

Kaka mkubwa Phiri! Maswali yako ni ya msingi sana, hapa nataka kutofautiana nawe kidogo kuhusu ....nanukuu! "KWANINI SIKU MOJA WASIMVAMIE NAO MPUMBAVU HUYU ILI NAYE WAMPIGE KIASI CHA KUPOTEZA FAHAMU NA AKOME?" mwisho wa kunukuu... kama tukifanya hivyo basi wote tutaonekana hatuna akili ni sawa na hizi habari au picha tuonazo watu wanaona mwizi wanamkamata na kumwagia mafuta ya taa na kumchoma moto mzima mzima..Je unafikiri hili ndio shuluhisho?

Kaka S! naona umerudi tena na sasa umerudi na ushauri ambao hata mimi nilikuwa naufikiria lakini ni tafauti kidogo tu nawe ni kwamba kwa nini kusiwe na nyumba fulani ambayo wanawake hawa ambao maisha yao ya ndoa yanakuwa kama haya iwe kama wanakaa ple kutokana na kushindwa kupata nauli kurudi kwao?...Halafu unajua yaani afadhali niache tu kuandika hapa kwani nina hasira siku hii nilifadhaika sana...ila nikakadha moyo na kusema nikifanya kitu hapa ntakuja kujigamba na nitakuwa mjinga kama yeye (mawanaume)...Hilo la kufanya matangazo kupitia SANAA ni wazo zuri sana... Ila sasa tunahitaji mtu shupavu ambaye ataanza kufanya hili....

Anonymous said...

1 Petro 3:1-22

1 Vivyo hivyo, ninyi wake, jitiisheni kwa waume zenu wenyewe, ili, ikiwa wowote si watiifu kwa lile neno, wavutwe bila neno kupitia mwenendo wa wake zao, 2 kwa sababu wamekwisha kushuhudia kwa macho mwenendo wenu ulio safi kiadili pamoja na heshima kubwa. 3 Na kujipamba kwenu kusiwe kule kusuka nywele kwa nje na kule kujivika mapambo ya dhahabu au kuvaa mavazi ya nje, 4 bali kuwe yule mtu wa siri wa moyoni katika vazi lisiloharibika la roho ya utulivu na ya upole, ambayo ni ya thamani kubwa machoni pa Mungu. 5 Kwa maana, pia, ndivyo walivyokuwa wakijipamba wale wanawake watakatifu hapo zamani, waliokuwa wakimtumaini Mungu, wakijitiisha kwa waume zao wenyewe, 6 kama Sara alivyokuwa akimtii Abrahamu, akimwita “bwana.” Nanyi mmekuwa watoto wake, mradi tu mnaendelea kutenda mema na kutokuwa na woga kwa sababu ya kitisho chochote.

7 Enyi waume, endeleeni kukaa nao vivyo hivyo kulingana na ujuzi, mkiwapa heshima kama chombo dhaifu zaidi, yaani, mwanamke, kwa kuwa ninyi pia ni warithi pamoja nao wa pendeleo lisilostahiliwa la uzima, kusudi sala zenu zisizuiwe.

8 Mwishowe, ninyi nyote iweni na akili zinazopatana, mkionyesha hisia-mwenzi, mkiwa na upendo wa kindugu, wenye huruma nyororo, wanyenyekevu katika akili, 9 msilipe ubaya kwa ubaya au matukano kwa matukano, bali, kinyume chake, mkitoa baraka, kwa sababu mliitwa kwenye mwendo huu, ili mrithi baraka.

10 Kwa maana, “yeye ambaye anapenda uzima na kuona siku zilizo njema, na auzuie ulimi wake kutokana na yaliyo mabaya na midomo yake isiseme udanganyifu, 11 bali na ageuke kutoka katika yaliyo mabaya na kufanya yaliyo mema; na atafute amani na kuifuatilia. 12 Kwa maana macho ya Yehova yako juu ya waadilifu, na masikio yake yanaielekea dua yao; bali uso wa Yehova uko dhidi ya wale wanaotenda mambo mabaya.”

13 Kwa kweli, ni nani atakayewadhuru ninyi mkiwa na bidii kwa ajili ya yaliyo mema? 14 Lakini hata mkiteseka kwa ajili ya uadilifu, ninyi ni wenye furaha. Hata hivyo, msikiogope kile kitu wanachokiogopa, wala msifadhaike. 15 Bali mtakaseni Kristo kuwa Bwana katika mioyo yenu, sikuzote mkiwa tayari kujitetea mbele ya kila mtu ambaye hutaka kutoka kwenu sababu ya tumaini lililo ndani yenu, lakini mkifanya hivyo kwa tabia-pole na heshima kubwa.

16 Iweni na dhamiri njema, ili katika lile jambo ambalo wanasema vibaya juu yenu waweze kupata aibu wale wanaosema kwa kuushushia heshima mwenendo wenu mwema kuhusiana na Kristo. 17 Kwa maana ni afadhali kuteseka kwa sababu mnatenda mema, ikiwa mapenzi ya Mungu yanataka hivyo, kuliko kuteseka kwa sababu mnatenda maovu. 18 Ndiyo, hata Kristo alikufa mara moja kwa wakati wote kuzihusu dhambi, mtu mwadilifu kwa ajili ya wasio waadilifu, ili awaongoze ninyi kwa Mungu, yeye aliuawa katika mwili, lakini akafanywa kuwa hai katika roho. 19 Katika hali hiyo pia alienda zake na kuwahubiria roho walio gerezani, 20 ambao wakati fulani hawakuwa watiifu wakati subira ya Mungu ilipokuwa ikingoja katika siku za Noa, safina ilipokuwa ikijengwa, ambayo ndani yake watu wachache, yaani, nafsi nane, walichukuliwa salama kupitia maji.

21 Lile ambalo linalingana na hili linawaokoa ninyi sasa pia, yaani, ubatizo, (si kuondolea mbali uchafu wa mwili, bali ombi linalotolewa kwa Mungu ili kupata dhamiri njema,) kupitia ufufuo wa Yesu Kristo. 22 Yeye yuko mkono wa kuume wa Mungu, kwa maana alienda zake mbinguni; na malaika na mamlaka na nguvu vilitiishwa kwake.
-----------------------
R.Njau