Wednesday, September 7, 2011

Moyo wangu!!

Kama kawaida yetu na bila kusahau leo ni ile siku ya KIPENGELE chetu ambayo hutujia kila JUMATANO na leo siku hii inawapelekeni mpaka hapa kwa diwani ya fadhili....karibuni sana..


Usiuache mpweke, maumivu kuufika,
Siufanye uteseke, machozi yakanitoka,
Ufanye ufarijike, upe moyo uhakika,
Moyo wangu.

Upatie unafuu, upunguzie mawazo,
Uweke daima juu, sikalie matatizo,
Siupige kwa miguu, na kuupa mizevezo,
Moyo wangu.

Uondolee karaha, siuweke taabuni,
Ufanye kuwa na raha, sizamishe majonzini,
Utawalwe na furaha, cheko tupu maishani,
Moyo wangu.

Usiutendee hivyo, moyo wangu taumia,
Ukitenda ndivyo sivyo, kitanzi utautia,
Vyovyote vile iwavyo, elewa wakuzimia,
Moyo wangu.

TUKUTANE TENA JUMATANO IJAYO KATIKA KIPENGELE CHETU HIKI.....KILA LA KHERI.

7 comments:

sam mbogo said...

Da,Yasinta,fasihi hiyo mama.moyo wangu,ukipenda hula nyama mbichi......!! wakumbuka kibao hiki.? ujumbe safi.
kaka S.

Simon Kitururu said...

Kwenye shairi hili MOYO hausingiziwi maumivu kweli?

Yasinta Ngonyani said...

Kaka Sam! Mmmmh nakumbuka kakangu.

Mtakatifu...Kwanini MOYO usingiziwe kwani Moyo si upo ndani ya binadamu au?

Rachel Siwa said...

Asante kwa shairi!!

Simon Kitururu said...

@Yasinta: SI matako pia yako ndani ya huyohuyo BINADAMU?
Kwani unafikiri ni UBONGO au MOYO ufanyao ustukie unaumia?
Na wakati unaumia kisa mpenzi kaharibu- unafikiri ni MOYO au UBONGO ndio ushughulikiao umivu?

Unauhakika huwa unapenda kwa kutumia UBONGO?

Sasa turudi palepale:

Kwenye shairi hili MOYO hausingiziwi maumivu kweli?

Yasinta Ngonyani said...

Simon watu tupo tofauti na tunaumia kitofauti nakubaliana nawe ni UBONGO ndio unaokuwa wa kwanza kujua nini kinatendeka....kwa mimi ninavyoelewa mtu anapoumia kutokana na penzi basi anaumia kila kiungo. lakini hii sasa imekuwa kama ni msema watu wanasema "NAUMIA KWELI MOYO KUKUKOSA WEWE"...sijui kama naeleweka labda tungeje mtungaji atajitokeza na kutusaidia.!

Anonymous said...

9 “Moyo ni wenye hila kuliko kitu kingine chochote nao ni hatari. Ni nani anayeweza kuujua? 10 Mimi, Yehova, ninauchunguza moyo, ninazikagua figo, ili kumpa kila mmoja kulingana na njia zake, kulingana na matunda ya matendo yake._Yeremia 17:9,10
----------------------------
R.Njau