Wednesday, February 1, 2012

Ukipenda boga

KATIKA KIPENGELE CHETU CHA MARUDIO JUMATANO HII NIMEONA TURUDIE UJUMBE HUU MAANA KAPULYA NI MDHAIFU SANA WA MASHAIRI.NIMEKUTANA NALO HAPA.
-------------------------------------------------------------------------------------------
Pendo pendo mwapendana, nyie ni nyie wawili,
Pendo pendo mwashibana, lenu la jambo muhali,
Mwanoga mwaambiana, mwingine hatobadili,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

Mapenzi yake matamu, wanogewa na mumeo,
Kamwe haiishi hamu, ana upya kila leo,
Penzi lashika hatamu, huwajali visemeo,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

Mumeo umemkuta, anao na ndugu zake,
Binti unafurukuta, hutaki kwako wafike,
Wataka mume kufyata, lako tu nd’o alishike,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

Siyo vema mwanakwetu, si tabia yenye sudi,
Nao waoneshe utu, upendo kwao si budi,
Mabezo si malikitu, siwoneshe ukaidi,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

Kwa mumeo umekuta, tayari alishazaa,
Kabla hajakupata, akupe wake wasaa,
Mtoto wamkorota, zaidi wamkataa,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

Nawe umepata mke, tayari ana mtoto,
Simfanye ateseke, kuiweka nyumba joto,
Haki yake apendeke, siyo kuleta fukuto,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

Usipende nusu nusu, nani tena wamwachia,
Yake yote yakuhusu, nayo uyapende pia,
Sisite kumruhusu, nduguze kutembelea,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

Mapenzi huleta raha, kwa dhati mkipendana,
Tena huipata siha, kama mwasikilizana,
Siyafanyie mzaha, mkaja kuumizana,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

Cha mwenziyo kyone chako, halafu ukithamini,
Kipende moyoni mwako, sikitenge asilani,
Sikifanyie vituko, kamwe kamwe abadani,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

Ya kusema nimesema, ni vema kuyasikia,
Yatunze yaliyo mema, kazi ukayafanyia,
Pendo lijae hekima, nyote kulifurahia,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

TUKUTANE TENA JUMATANO IJAYO!!!!

4 comments:

sam mbogo said...

Kweli ukipenda, boga penda na ua lake.usemihuu nikiboko,kila mtu anaweza kuutafsiri aujuwavyo.

Baraka Chibiriti said...

Wakati mwingine huwa ni tabu tupu....hasa apatikanapo wa pembeni, hapo panakuwa pachungu kwenye ndoa, utamu unahamia pembeni. Lakini ndivyo tulivyo binadamu toka enzi na enzi...hakuna mshangao sana.

Ila nawaombea sana wanadoa wote, ili ndoa zao ziwe kamilifu kisawasawa. Na mimi siku ya siku yatanikuta haya.
Ila kweli ukipenda boga, lazima upende na ua lake.....ila wakati mwingine ua huwa chungu kweli.....

Simon Kitururu said...

Mmmmh!

Yasinta Ngonyani said...

Kaka Sam! ni kweli kila mtu anatafsiri ajuavyo. Lakini ikiwa ni kweli basi ni safi.

Kaka Baraka! Ni kweli wakati mwingine ni shida.
Kumbe sina wifi mpaka leo...LOL usifikirie kuninyima kadi ya harusi:-)
Mtakatifu vipi mbona mgono ww hufanyi hivyo au? :-(