Monday, February 20, 2012

KWA NINI WANAUME WANASHINDWA KULING'AMUA HILI?

Kuna wakati niliwahi kueleza juu ya wanaume kudhani kuwa kuwanunulia wake au wapenzi wao kila kitu kwa maana ya nyumba nzuri, magari ya kifahari na mavazi ya thamani, inatosha kupeleka ujumbe kwa mke au mpenzi wake kuwa anapendwa. Nilieleza kwa kirefu sana juu ya dhana hiyo jinsi isivyo sahihi na niliweka bayana kuwa, wanawake ni viumbe wanaohitaji kusikilizwa kuliko kitu kingine, bila shaka mlio wengi mnakumbuka makala hiyo.

Kwa asili wanaume wanapenda sana kuwasikia wake au wapenzi wao wakikiri kuwa wanawapenda na kufurahia tabia zao nzuri wema walio nao, vipaji walivyo navyo na sifa nyingine lukuki. Wanaume wanapopewa sifa za aina hii na wake au wapenzi wao hufurahia na kupata nguvu na kuona kwamba wana thamani kubwa mbele ya wake au wapenzi wao, kinyume na hivyo wanaume hukerwa na kutowajali wake zao.

Pamoja na kuoneshwa upendo lakini hata hivyo hiyo haitoshi kuwafanya wanaume wawapende na kuwajali wake au wapenzi wao. Kuna wakati mwanaume anakuwa na kazi nyingi sana na anatumia muda mwingi kwenye kujisomea au kuangalia Luninga, hata pale mke au mpenzi wake anaponyesha kwamba anahitaji kuwa naye kwa muda fulani. Kuna wakati pia mwanaume anajali zaidi kazi zake kuliko mambo mengine ambayo mkewe anayataka na kuyaona ya maana.

Naamini wengi mtakuwa ni mashahidi wa kauli hizi, “Yaani niache kazi zangu nikae kukusikiliza wewe na upuuzi wako, subiri nikipata muda tutaongea mambo hayo” kauli hizi ni sumu kali sana katika uhusiano, na huchangia kwa kiasi kikubwa ndoa na mahusiano ya wapenzi wengi kuporomoka.

Ni kweli kuwa kuna wakati mwanaume anaweza kuwa bize na shughuli zake,lakini pale mke au mpenzi wake anapohitaji ukaribu na yeye ni wajibu wake kuonesha kujali.Kama mwanamke anahitaji kufanya jambo fulani ambalo inabidi mwanaume amsaidie, lakini inapotokea mwanaume kuonyesha kwamba hajali sana juu ya jambo hilo bila kujali kama yuko bize au hayuko bize, mwanamke huhisi kutothaminiwa na hiyo humuumiza sana kihisia. Lakini kama mwanaume ataonesha kujali hisia za mkewe na kumsikiliza kwa makini hata kama hatatoa ushirikiano hiyo tu inatosha kumridhisha mke au mpenzi kuhisi kuwa anapendwa na anasikilizwa.
Lakini utakuta wanaume wengi hawajali utashi wa kihisia wa wake zao na huamini kwamba wanawake wanachohitaji ni kupewa fedha au mali na kuhakikishiwa maisha ya kifahari basi. Ukweli ni kwamba wanawake wanahitaji sana kusikilizwa hisia zao na kupewa nafasi pekee na mume au mpenzi wake pale anapohitaji nafasi hiyo ya kusikilizwa. Kumuonesha mwanamke kwamba hana thamani na hana nafasi ya kusikilizwa na badala yake kazi na kusoma, au kuangalia luninga kukaonekana ndio kuna thamani kuliko yeye ni kosa kubwa.

Ni jambo la msingi sana kwa wanaume kulifahamu hili kwa ustawi wa ndoa au mahusiano yao na wake au wapenzi wao, kwani wanawake wanahitaji nafasi kutoka kwa wanaume au wapenzi wao zaidi ya kitu kingine, maana hayo mengine yatakuja kujazia tu

3 comments:

Simon Kitururu said...

Mmmmmh!

Yasinta Ngonyani said...

Vipi Simon mbona unaguna?

ray njau said...

Hapa leo mama maisha leo kisu kimegusa mfupa hata la kusema hamna ila tu kwa kweli kwa ustawi wa ndoa na maisha ya familia ni lazima vichwa vya familia [wanaume] tununue wakati.